Labda nielezee vizuri,... jinsi chumba chetu maalumu,
tulichokiita ,maktaba kilivyokuwa,…
Kwa vile kila mmoja alikuwa na kampuni yake, na mara nyingi
kulikuwa na kazi nyingine ilibidi tuzifanyie nyumbani,kila mtu kwa wakati wake,
au siku nyingine tunakutana na kuwemo humo, …
Kutokana na hali hiyo, tukapanga kuwa maktaba hiyo
ibororeshwe zaidi iwe kama ofisi ndogo ya nyumbani..na kwa vile kila mmoja ana
ofisi yake, tukakubaliana kugawanywe sehemu mbili, lakini sio kuwa kuweka uzio
kabisa, ni kwa mtindo wa makabati na meza, kutenga huku na kule,..kiukweli
tulipatengeneza vizuri sana.
Hakuna aliyekuwa akihangaika na sehemu ya mwenzake,
labda uamue tu kumtuma mwenzako, kuwa nisaidie kunichukulia kitu fulani kwenye
sehemu ya vitu vyangu..sasa kila mmoja akawa anapaboresha sehemu yake kwa jinsi
aonavyo yeye.
Kwangu nikaongeza kabati moja imara, ukiliona utasema
ni meza au kabato la vipodozi na vitu vya kike lakini kwa ndani, nikaongeza
sehemu maalumu ya kuweka vitu vyangu vya siri,..ambavyo sitaki mtu
aviguse..hata mume wangu sehemu hiyo alikuwa haijui..Anaweza akawa anaifahamu,
maana sikuwa namficha sana, lakini hakuwa na habari kabisa na vitu vya kabati
hilo.
‘Hilo kabati lako la kike kike, sitaki hata
kulisogelea,…’kuna siku aliwahi kuniambia hivyo
Sasa humo ndio niliweka nakala ya mkataba wangu,
kwangu mkataba huo ulikua ni moja ya vitu muhimu sana ..nikimaliza kusoma kama
kuna kitu nataka kukifuatilia, naurudisha hapo…
Kulikuwa na kabati la vitu vya kuchangiana, lakini pia
ni maalumu kwa kumbukumbu zetu za nyumbani, hapo kila mtu angeliweza kuweka au
kuchukua vitu,lakini mara nyingi,nimekuwa nikilitumia mimi mwenyewe tu na mume
wngu hana habari nalo.
Lenyewe lina sehemu ya nje na ya ndani, unaweza
ukachukua vitu vya nje, bila kujua kuwa kuna sehemu nyingine ya ndani,..sasa
sehemu hiyo ya ndani, ndio kuna vikabati maalumu,..humo kuna nyaraka za
nyumbani za kuchangia…na kuna sehemu maalumu, ndio kuna sehemu tunaifadhia
silaha….
Kupotea kwa mkataba wangu, kwenye kabati langu, na mimi mwenyewe ndiye
mwenye ufungua, kuliniweka kwenye njia panda, sikutaka hata siku moja kumshuku
mume wangu kwa baya lolote lile, yeye ni mimi, na mimi ni yeye, nilimuamini
sana kutoka moyoni mwangu, ....sasa mkataba wangu umepotea, na mtu ambaye
anayeweza kuuchukua ni mume wangu, swali lilikuja kwa kutumia ufungua gani, na
mimi ufungua za kabati langu ninao mimi mwenyewe, na hakuna nakala ya akiba
ambayo niliwahi kuiweka sehemu, na ufunguo zangu mara nyingi natembea nazo.
Leo hii ninafika nyumbani ninamkuta mume wangu akiwa
kwenye kabati langu,..na kabati limefunguliwa, na ufungua zipo zimening’inia
kwenye sehemu yake..na kulihakikisha hilo nilisogea taratibu hadi pale
alipochuchumaa
Kwa muda huo hakuwa na habari kabisa kuwa nimeingia,
na alionekana kuna kitu muhimu anakitafuta hasa pale aliposema
‘Mbo-mbo-na haipo ooh….’
Na kilichoniuzi zaidi
ni kuona nyaraka muhimu za ofisi nyaraka ambazo kwangu ni muhimu sana, alikuwa
kazisambaza chini, bila mpangilio maalumu, mimi napenda vitu vyangu viwe kwenye
mpangilio maalmu,..hapo subira, ilinishinda ndio nikasema...
‘Unafanya nini kwenye kabati langu...’nikamshitua...
Tuendelee na kisa chetu..............
Mume wangu aliposikia sauti yangu, alishituka, hadi ile karatasi
aliyokuwa kaishikilia mkononi kwa muda huo, ili ilimdondoka,… kwanza alitulia,
kama anatafakari jambo, na baadaye
akajifanya kama hajali..na kwa haraka, akaikota ile karatasi, halafu . akageuza
kichwa kidogo na kuniangalia usoni, halafu akasema;
‘Afadhali mke wangu umekuja, maana hapa akili yote imevurugika,..kauli
zako za hivi karibuni zimenifanya nichanganyikiwe kabisa…’akasema na sasa akawa
anaendeela kama kutafuta kitu.
‘Unajua, ..sijui ndio huku kuumwa,..hii ajali imenifanya niwe mtu
wa ajabu kabisa,..uliposema kuhusu mkataba mwingine wa zamani,…nimekuwa
nikihangaika kujiuliza ni upi huo…lakini kuna kitu,,…unasikia..’ sasa akaacha
kutafuta na kukaa vyema sakafuni.
‘Nakumbuka hata wewe ulikuwa nayo, nakala yako au sio..na mimi ya
kwangu, hii niliyo nayo mimi, ni ambayo niliitoa nakala , kutoka kwenye ila
nakala ya mwanzo, nahisi ndio hiyo unayoiita nakala ya mkataba wa zamani, kweli
si kweli..’akatulia
‘Sasa akili ikanijia,…kama wewe ulikuwa na nakala yako, kwanini
usema kuwa imebadilishwa,…sasa nikawa natafuta ukweli..tatizo ni hili nakala
yangu, ya zamani…eeh, siioni, nia nione kama kweli ipo tofauti na hii ambayo
nilikwenda kuitoa nakala..unielewe hapo, nakala ni ile ile,, ila nilikwenda
kuitoa nakala nyingine kwa ajili ya wakili..ni ile ile..
‘Cha ajabu, kwenye kabati langu haipo…ni ile ya zamani, unanielewa
hapo, ambayo niliichukua na kuitoa nakala,…hapo kabisa..ipo hii ambayo ni
nakala kutoka kwenye nakala hiyo…hii ya sasa unaiona imefifia kidogo,…kama imefutika
futika vile lakin ikila kitu ni kile kile...sasa nikawa nahangaika weeeh,
mwishowe nikasema, aah..’akasema na mimi nikamkatisha kwa kuuliza
‘Kwahiyo unatafuta nini hapa kwenye kabati langu, ndio mkataba
au..?’ nikauliza
‘Kiukweli, nikuombe samahani kwa hilo..lakini sio kosa,..si
ndio…niambie mke wangu hapo nimekosea nini…sawa, kiutu , ilitakiwa nifanye
hivyo,..lakini nikuulize kwani..kuna kosa mtu akitafuta kitu kwenye sehemu za
mke wake..mhh, kosa labda ni kwa vile sikukufahamisha mapema kwa vile…kuna vitu
vyako vya kiofisi, lakini ofisi zi zetu wote au…ama kwa hilo, basi nikuombe samaha
mke wangu…’akasema.
Aliinua macho na kunitizama..nilishikwa na kitu kama mshangao…hayo
macho…sio yale ya mume wang ninayemfahamu…lakini sikujali hilo
‘Mume wangu, toka lini tukawa tunachangiana makabati, kila mmoja
ana kabati lake na kila mmoja ana vitu vyake na humu naweka vitu vyagu vya
kikazi, angalia jinsi gani ulivyoviweka ovyo vitu vyangu sakafuni, …kwanini
jamani…’nikawa naviangalia vile vitu, sakafuni.
Hapo akatikisa kichwa, ni kama vile haamini, na akaehema kwa
nguvu, halafu akaendelea na shughuli yake kama hajali, na mimi nikasema kwa
hasira.
‘Mume wangu unafanya nini…unajua utaratibu wangu wa kikazi
ulivyo,..kwa jinsi ulivyovuruga hivi…hata ule utaratibu wangu wa kumbukumbu za
kwenye kabrsaha umeuharibu, itachukua muda tena kuutengeza vizuri,...huoni kuwa
unataka kuniweka mimi mahala pabaya..vikiharibika hivi au vikipotea..unaniweka
mimi kubaya....’nikasema.
‘Usijali kabisa mke wangu hakitaharibika kitu hapa, niamini mimi,
mimi ni mume wako, nitahakikisha hakiharbiki kitu hapa, hata hivyo…kama
nilivyokuambia, siku hizi akili yangu imekuwa ya ajabu kabisa, inanasa kila
kitu ninachokifanya, yaani siku hizi mke wangu naona nipo mtu wa ajabu sana, nina
akili mbili tofauti, hii ya ajabu, inakuja na kuondoka, ..wewe mwenyewe utaona,
nitakirudisha kila kitu kwa mahali pake, bila hata kukosea wewe mwenyewe utaona...’akasema.
‘Kwahiyo umesema ulikuwa unatafuta nini humu,… mkataba wako kwenye
kabati langu, kwanza ni mkataba upi huo, unajifanya nini hapa..?’ nikamuuliza
kwa hasira.
‘Nakala ya zamani, ya mkataba...mwenyewe ulisema unahitaji ile
nakala yangu ya zamani, si ndio hivyo…umesema bila hiyo huwezi kukaa kiti
kimoja na mimi na wakili au sio..’akasema
‘Kwahiyo ipo kwenye kabati langu, uliiweka wewe..?’ nikamuuliza
‘Ni hivi… pale nilipokuwa nimeiweka nakala yangu, kule
kwenye kabati langu, siioni, siku hizi akili yangu inanituma mambo mengi,
na nikiweka kitu sisahau pale nilipokiweka, sasa ni ajabu kabisa kuwa siuoni, imekuwaje tena, hapana lazima kuna
tatizo...’akatulia sasa akianza kupanga karatasi zangu zilizokuwa sakafuni.
‘Mume wangu…tafadhali…’nikasema kabla sijamaliza akasema
‘’Najua utanifikiria vibaya, lakini sivyo hivyo…mimi nilijua labda
wewe umeamua kuichukua il nakala yangu ya zamani,…na kwa bahati mbaya ukaja
kuiweka hapa kwako, kiusalama zaidi, hapa kwako kuna usalama sana au sio…’ akasema,
huku akiendelea kupekua kwenye mafaili yangu.
‘Sikiliza mume wangu, ..sijapendezewa kabisa na hiki kitendo ulichokifanya,
..na sio tabia yako, imekuwaje siku hizi, mume wangu, ...kuna nini unanitafuta
wewe mume, kuna tatizo gani limekutokea ili niweze kukusaidia..kwanini
unahangaika hivi mpaka unaniletea matatizo makubwa kwenye maisha yangu..?’ nikamuuliza
huku nikiendelea kumwangalia.
‘Hujapendezewa na mimi, kwanini…..hapana mke wangu usinifikirie
vibaya kabisa,…na mke wangu, nikuulize, wewe si mke wangu, nimekuoa kwa
taratibu zote za ndoa, au sio…je nikifanya hivi kuna kosa gani…?’ akauliza
‘Kuja kupekua kwenye kabati langu, tena kuna mambo ya kofisi, je
mimi nikifike kwenye kabati lako nikafany ahivyo utafurahia,…kila siku unazidi kunichefua, kuna kitu gani kinakusumbua hivyo…’nikasema
na kumuuliza
‘Hakuna kitu kinanisumbua, ila kwanza nijibu swali langu halafu
nitakuambia tatizo ni nini….swali langu ni hivi…, wewe si mke wangu..?’
akauliza na mimi nilikaa kimia, akauliza tena
‘Mke wangu nauliza tena, samahani nijibu tu, wewe si mke wangu…?’
akauliza na mimi nikaona isiwe shida nikajibu
‘Ndio..’nikasema hivyo tu.
‘Sasa kama ni hivyo, nina makosa gani kumkagua mke wangu…’akasema
‘Mume wangu acha maneno yako ya mitaani, kunikagua kwa vipi..?’
nikauliza
‘Kama mimi ni mume wako, kila chako ni change au sio…na pia changu
ni chako au sio..tuseme kiukweli kutoka haki za kindoa, achilia mbali mambo ya
mikataba, achilia mbali sheria za kidunia,...na hata ukirudi kwenye mkataba
kama umeusome vyema inasema hivyo hivyo,… na wewe mwenyewe ni mmoja wa
waanzilishi wa huo mkataba wetu na sahihi yako ipo, usikate ukweli mke wangu,
ach ubinafsi…’akasema
‘Mimi siutambui huo mkataba wenu wa kugushi..’nikasema kwa
hasira,…mume wangu kwanza akatabsamu, halafu taratibu akanigeukia, na
kuniangalia…
Kama kuna mtu kampanga mume wangu, basi huyu kafanya kazi kubwa
sana, anavyofanya sio kuigiza, utafikiri ni kweli kabisa, yaani utafirikia
naongea na mto tofuati sio kama yule mume ninayemfahamu ukimuambia kitu hewala,
hewala..tu.
‘Hapana…sio wa kugushi mke wangu, kwanini unasema hivyo,…ni ule
ule tulioutengeza pamoja…,tuwe wakweli hata mkataba wa halali wa ndoa,
unasemaje, mimi ni mume wako, na wewe ni mke wangu, kwanini sasa isiwe halali
kwangu kufanya ya halali…hili ni halali kwangu au sio…nakagua vitu vya mke
wangu, ambaye ni mke wangu, au sio,…?’ akauliza.
‘Usipoteze lengo…tafadhali…’nikasema
***************
‘Mke wangu nikuulize tu, kwanini huniamini,..eeh, na …na ..kimkataba…,
mimi kama mume wako nina haki ya kuangalia chochote kwenye mali zetu, ...au
nimekosea..kasome mkataba vyema…?’ akaniuliza na safari hii alianza kurudisha
vitu kwenye kabati, nikawa namwangalia tu.
Hutaamini baada ya dakika moja, alikuwa karudisha kila kitu kama
kilivyokuwa awali, halafu akaniangalia, kama vile anataka mimi nikague kama
kila kitu kipo sawa, baadae akainama na kufunga, ufunguo ulikuwa umening’inia
pale pale…alipogakikisha kafunga, akauchomoa ufungu…, nikagundua kuwa ufunguo ule
ni kuchongesha, aaaah, kumbe, ...
‘Huo ufungua uliupatia wapi?’ nikamuuliza, sasa nikijaribu
kuukagua huo ufungua, na yeye kwa haraka akauweka mfukoni mwake.
‘Mbona ninao siku nyingi mke wangu...niliamua kuwa na nakala ya
ufungua zote, maana sisi sote ni binadamu tu, tunaweza kupoteza ufunguo,
kwahiyo kuna haja ya kila mmoja awe na nakala za mwenzake, ni vibaya kufanya
hivyo, au…’akasema kama ananiuliza
‘Hilo ulilifanya lini bila ya mimi kufahamu..?’ nikamuuliza
‘Hilo la kuchongesha ufunguo…?!! Mmh, mke wangu umesahau jambo
kuwa mimi ni mume wako, natakiwa kuwa mbele kwa ajili ya familia yetu,..ni
lazima niwe makini kwa kila kitu, na usalama wetu, na mali zetu pia, kwahiyo
hilo sio la kuniuliza, nilifanya muda tu,..na hivi sasa nina uhakika kila kitu
kipo salama au kufanya hivyo,..ni-ni..nimekosea mke wangu…’akasema
Alisema hivyo sasa akiwa
kamaliza kupanga kila kitu, akawa kama akumbuka kitu, kwa haraka sana akageuza kichwa kule kwenye kabati la pamoja,
lipo wazi…kwa haraka ya ajabu, akaliendea, akahakiki kama kila kitu kipo sawa,
huyoo, akalifunga.
‘Umeona eeh…kila kitu kipo sawa..kama
kilivyokuwa..umeonaeeh,…’akapitisha macho huku na kule, baada y akurizika
akaniangalia mimi.
‘Twende…’akasema
‘Mume wangu usijifanye mjanja sana, unajua mimi nafahamu kila
kitu, hizo zote ni mbinu zenu, kwanza mumefanya njama za kubadili mkataba, ili
kutengeneza mkataba utakaokidhi matakwa yako, na mkafanya mbinu ya kuhakikisha
nakala zote za mkataba huo wa kugushi zipo kile idara, lakini mumesahau kitu
kimoja…’nikasema
‘Kitu gani mke wangu…’hapo akasema kama kashtuka, halafu
akajifanya yupo sawa.
‘Nina uhakika, mliamua kuchongesha hizo ufunguo, ili wewe uje kuiba
mkataba wangu, ili mkabadili na kuhakikisha nakala za awali, mumeziharibu, na
pia ukaja ukachukua bastola yangu, nakumbuka wewe ulikuwa hutaki hata kuishika
hiyo bastola,....imekuwaje sasa…?’ nikamuuliza
‘Bastola!!!…mke wangu, toka lini nikagusa silaha yako, mimi
naogopa sana siliha hiyo, aah, hapo umezidi, bastola, mimi na bastola wapi na
wapi…’akasema
‘Na kwa taarifa yako, silaha iliyotumika kwenye hayo mauaji ya
wakili wako,..ni hiyo bastola, na wewe ndiye mwingine mwenye nakala ya kabati
hilo, mimi wamegundua kuwa sihusiki, sasa wao wanamtafuta huyo mtu mwingine
mwenye nakala ya hilo kabati, kumbe ni wewe, ole wako polisi wakifahamu hilo...’nikasema
‘Unasema nini mke wangu, sijakuelewa hapo bado, kwanini mimi
nilichongesha ili nije kuiba, hahaha, hapo mke wangu unakosea sana,.... kwa
nini niibe, kuna mtu anaiba kitu chake, mbona mke wangu
unaniangusha,...usisahau kuwa mimi ni mume wako, sio mtu mwingine
yoyote,...’akasema,
Moyoni, akilini, nilikwua nimejawa na hasira, lakini nilikumbuka
jinsi alivyokuwa akinishauri docta, kuwa nisije kulogwa na kusema mume wangu
kapona, kwani hapo alipo ikitokea tena,… mshtuko,… akapatwa na kiharusi
(stroke) basi, sitaweza kumponya tena!
Hapo mimi.., nikabakia kukunja uso, na aliponiangalia usoni
jinsi nilivyobadilika, aligeuka kwa haraka akatoka nje ya hiyo makitaba…alikuwa
anatembea kwa mwendo wa haraka …kama haumwi, kikawaida yeye anatembea kwa
shida, kwa kuchechemea..!
**********
Nilichukua mkoba wangu na kuutafuta ufunguo wangu, ulikuwepo
kwenye moja ya fungua zangu ninazotembea nazo, nikafungua lile kabati na kila
kitu kilikuwa kwenye nafasi yake, na ule mkataba wa kugushi upo hapo hapo..
Sikutaka hata kuukagua kama ni ule ule wa kugushi au ni ule wa
awali nikafunga lile kabati vyema, na akilini mwangu nikapanga nikitoka hapo
nabadili ufunguo zote na naweka taratibu mpya za kufungua hilo kabati kwa namba
za siri.
Nilitoka mle makitaba na kuingia kwenye chumba chetu cha kulala,
kuna mlango wa kuingilia huko,..nilitarajia nitamkuta mume wangu kalala
huko,..lakini hakuwepo, mimi kwa haraka, nikabadili nguo, na kuelekea sebuleni,
chumba cha maongezi.
Chumba cha maongezi, nilimkuta mume wangu akiwa kakaa huku
kashikilia mkataba, ..mwanzoni nilifikiria ni ule mkataba wa zamani, lakini
ulikuwa ule ule waliougushi wao, niliugundua kwa jinsi ulivyo juu, ..jalada
lake limefifia kidogo.
Nilimsogelea na kumwangalia, alikuwa katulia, hana wasiwasi, na alionekana
alikuwa akisoma sehemu fulani kwenye huo mkataba, kwa makini, na alipohisi
nimesimama karibu yake, akauweka pembeni huo mkataba, na kuinua uso kuniangalia,
akatabasamu na kabla hajasema neno, nikasema;
‘Haya hebu niambie ukweli, ni kitu gani kinachoendelea hapa kwenye
nyumba yetu?’ nikamuuliza..yeye akasogea kidogo, kama kunipa nafasi nikae
karibu yake, sikufanya hivyo.
‘Mke wangu hebu kwanza kaa, njoo ukae karibu yangu,…mimi ni mume
wako wala usiniogope, kuwa labda kwa vile naumwa, ninaweza kukudhuru, hapana,
hilo halitaweza kutokea abadani, ninakupenda sana mke wangu…’akasema
Na mimi nikakaa, lakini sio karibu yake kihivyo, akasema
‘Mhh, mke wangu, kwani kuna nini kibaya umeiona kimetokea ambacho
kinakufanya useme hivyo,…, mimi sioni kama kuna kitu kibaya kimetokea, hiyo
ajali isiwe ni sababu ya kuharibu maisha yetu, ajali ni ajali tu, na ajali
haina kinga, na mengine yanatokea ni…maisha tu…’akasema na mimi hapo nikabakia
kimia kwanza.
‘Mke wangu haya yanaweza kumtokea yoyote, hasa sisi tunaotumia
vifaa vya moto..kilichotokea kwangu sio uzembe, sio…au kama watu
wanavyosema,..ilitokea tu..na hali ninayokwenda nayo itakwisha tu, nisaidie
nipone kabisa…’akasema
Hapo nilitaka kumuambia kumbe kweli hajapona, maana wakati
mwingine ukimuuliza anasema kapona lakini hapo anajifanya hajapona kabisa.
‘Ni haki yako kunisaidia..nikikosea,…nikifanya kinyuma na kawaida,
ujue ni madhara hayo ya ajali..na hapa nilipo, sio kwamba nakumbuka kila kitu
kihivyo, inatokea …nika-ka-sahau,..yawezekana, wakati mwingine nahis kama nipo
kwenye njozi, lakini kiukweli nimepona, au sio…’akasema, na mimi sikumjibu
kitu.
‘Au mke wangu niambie …, labda mimi sijui, maana muda mrefu
nimekuwa hopsitalini, je kuna tatizo lolote…nipo tofauti, nimechanganyikiwa
labda..niambie ukweli au…? ‘akauliza
‘Mume wangu, leo ni siku ya mwisho, sitakaa tuongee hivi tena,
labda kuwe na kuelawana, na kuelewana kwetu, nimeshakuambia,kutakuja pale tu,
wewe utakapokubali kuniambia ukweli, wote na pili ule mkataba wa asili uweppo
mezani…’nikasema
‘Eheee,…wewe unautaka ukweli, lakini,…ukweli upi.. hamna shida,
mimi nitakuambia kila kitu, ila sasa nikuulize unataka mimi nikuambia ukweli
gani labda, nisaidie hapo mke wangu…’akasema
‘Leo ni siku ambayo…kama hutaniambia ukweli, sijui…maana tukimaliza
hapa ni utekelezaji,…hata kama utauficha huo mkataba,…na
vinginevyo,..tutafikishana mahakamani, au….’hapo nikatulia, alipogeuka
kuniangalia
‘Mahakamani, kuna nini cha kwenda huko, hapana mahakamani hapafai,
yetu tutayamaliza hapa hapa nyumbani au sio....?’ akauliza
‘Vitendo vyako vimenichosha, kwanza umekiuka makubaliano yetu,
umevunja mkataba wa ndoa, na hata sikuelewi,…. na hutaki kuniambia ukweli,
...ni kwanini lakini, kwanini unanitesa hivyo, una lengo gani na mimi…?’
nikamuuliza na yeye akanitupia jicho, halafu akafungua ule mkataba wake, akawa
kama anasoma jambo, mimi sikutaka hata kumsogelea na kuangalia anasoma kitu
gani.
‘Kwanini unasema ….eeeh,maana
tukimaliza hapa na utekelezaji, ama twende mahakamani,…hapana usiseme hivyo, tupo wote, na kila
siku tutaongea tu huo ndio utaratibu wa mke na mume au sio..hata bila mikataba,
hilo la kuongea ni jambo la kawaida kwa mke na mume, sasa niambie nimekufanya
nini kibaya, mpaka useme hivyo…?’ akasema na kuuliza, na aliponiona nipo kimiya
akasema;
‘Kwani mke wangu situlishaelewana, na ndio maana nilikuwa nataka
niutafute ile nakala yangu ya zamani,…ili tukae tulianganishe kama kuna maneno
yameongezeka au kupungua,…sijaiona kabisa..na ya kwako ipo pale pale au sio…kwanini
tuandikie mate,..nenda kaulete, ..tulinganishe tuone kama kuna utofauti wowote,
utakuta kitu ni kile kile neno kwa neno....’akasema.
‘Mume wangu…’nikataka kusema, yeye akanisogelea akiwa kafungua
mkataba wake na kusema…
‘Hebu angalia, mwenyewe, ....maneno ni yale yale..hebu soma uone…’akasema
huku akinipa ule mkataba, na mimi sikuugusa na wala sikuinua mkono wangu,
nikawa namwangalai usoni nikasema.
‘Mume wangu kwanini upo hivyo, upo sawa kweli wewe, ni kwanini hutaki
ku-usema ukweli, ni kwanini mlichukua hatua ya kuubadili huo mkataba bila
makaubaliano na mimi…niambie tu ukweli, ili twende sawa….?’ nikamuuliza
‘Mke wangu, mimi nakumbuka , hilo swali nilishakujibu, hakuna
aliyebadili huo mkataba,mbona huniamini mke wangu, mimi nipo sawa kabisa,
kifahamu, au..?, tuache kuhusu mimi, eeh,...hebu niambie ni wapi huo mkataba
umebadilishwa, na kama ulibadilishwa kwanini sahihi yako iendelee kuwepo hapo,
huoni unakosea kabisa kisheria….eeh, niambie sahihi zote za wahusika sizipo,
angalia hapa, hii sio sahihi yako…hata ukienda mahakamani watahakiki hilo…’akasema.
‘Kwahiyo kumbe bado upo na msimamo wako ule ule,....hutaki kusema
ukweli, hutaki kuniambia ni nini kinachoendelea, na ni ni kusudio lako,au
kusudio lenu, na washirika wako....eeh, na sasa watoto wanadai wanachohisi ni haki yao
, si ndio unataka hivyo…’nikasema huku nimemkazia macho, yeye akaniangalia mara
moja halafu akatabsamu, na kusema;
‘Haki ni haki tu…tusiibeze haki, au sio, na…hayo niachie mimi, na
nikuulize tena mke wangu, labda kuna kitu wewe unakihis hakipo sawa, ni kitu
gani, niambie ukweli, kama ni mkataba upo vile vile..na kwanini mtu afanye
ufoji huo, agushi, kwanini,...hebu niambie wewe…?’ akaniuliza
Mimi hapo nikakaa kimia.
‘Mke wangu , tusaidiane, huenda mimi nipo dunia nyingine, huenda
kuna kitu umekigundua kwangu na unaogopa kuniambia, au nimebadilika, baada ya
kuumwa, nimekuwa tofauti, ...’akasema
Hapo nikasimama,..nilitaka kuondoka kabisa kwa hasira…, lakini
nikajiuliza nitakuwa nimefanya nini sasa,
leo ni lazima nimbane mpaka asema ukweli wote hawezi kujifanya mjanja hivyo
hapo ndio..nikageuka kumuangalia,
Yeye akawa anausoma ule mkataba, hajali kabisa, hana wasiwasi….
Nilimuangalia mume wangu, kiukweli nilimuona kama sio Yule mume
ninayemfahamu kabisa,…maana mume niliyemzoea alikuwa nikimuuliza jambo,
tunakubaliana, tunaongea yanakwisha, lakini huyu wa sasa, wala hanijali, na
pili amekuwa kama yupo mbali, kama alivyosema, ni kama yupo dunia nyingine
tofauti ya ukweli….
‘Mume wangu , pengine, hujanifahamu , pengine unafikiria kuwa
nakutania, pengine, nahitajika kuchukua hatua nyingine ndio utanielewa,....’nikasema
na kutulia kidogo.
‘Nakusikiliza endelea…’akasema hivyo akiendelea kuusoma huo
mkataba.
‘Hivi unajidanganya nini, hivi wewe hufahamu kuwa hilo
unalolifanya linaweza likakufunga, na hata kukuvunjia ndoa yako, unayoringia
nayo wakati wewe mwenyewe umeshaivunja…ukweli ndio huo, umeshaivunja ndoa
yako,..hebu niambie imebakia nini…sasa...’nikamwambia na yeye hapo akashituka,
na kuinua uso kuniangalia...
‘Unasema nini..kuvunja ndoa yetu, hapana mke wangu, hilo halipo,
na hali-hali-tatokea abadani, labda mimi
niwe nimekufa....kwanza kwanini unasema hivyo?’ akaniuliza na safari hii akawa
ananiangalia moja kwa moja usoni,akionyesha wasiwasi. Kikweli kuna kitu kwenye
macho yake nakiona sio cha kawaida….lhata hivyo, hali ya kujali haikuwepo tena.
'Kutokana na makubaliano yetu ya awali, hata kama mumeugushi huo
mkataba halali, na kupandikiza huo wa kwenu, na kuweka mambo yenu ya kujihami…lakini
ukumbuke, kugushi ni dhambi, kugushi nyaraka za kiheria ni kosa kubwa sana…sasa
jiulize unataka kufanya hivyo kwa ajili ya nani…’nikasema
‘Hapo jiulize wewe mwenyewe…’akasema kwa kujiamini kabisa
‘Sawa nikuambie kitu.., hata kama unajifanya mjanja sana,lakini
ukumbuke kuwa makubaliano yetu ya awali yapo pale pale, na moja ya makubaliano
yetu ni kuwa mmoja akivunja miiko ya ndoa..unaifahamu hiyo miiko, ile mikubwa…’nikasema
‘Kama upi huo…?’ akauliza
‘Kuzini…kutembea nje ya ndoa…’nikasema
‘Nini, …wewe mke wangu ni nani anaweza kufanya dhambi hiyo, hapana…mimi
nakubali hilo ni kosa, ..na kwenye mkataba wetu inasemaje..hebu kidogo…’akasma
na sasa akifungua mkataba wake, na akawa kama ansoma
‘Yah, hapa kupo wazi…ni kosa, ila sasa unajua kiubinadamu, eeh..si
semi hivyo kwa vile, labda..hapana mimi sijafanya, ikitokea wewe ukafanya
hivyo, kwanza kuwepo na ushahidi…wa bayana, lakini pia…sisi ni wanandoa,
tumzee, tuna watoto…mmoja akaghafilika, kutokana na sababu…maana huwezi kufanya
dhambi kama hiyo bila sababu…’akasema
‘Sababu gani,…hakuna sababu hapo, kuzini ni kuzini tu…’nikasema
kwa hasira.
‘Je kama imetokana na wewe..’akasema
‘Kwa vipi..?’ nikauliza
‘Tuache hayo, ila hapa kwenye mkataba inasema hivi, kama …itatokea
hivyo, kwasababu za kujitetea, kuna sababu japo kidogo, ya kujitetea,
inayoingia akilini, japokuwa..ushahidi upo, na mmoja akaomba msamaha, ukakubalika,
basi,..ni kusameheana ya kale yaishe watu wagenge yajayo,…hiki ni kipengere cha
nyongeza..’akasema
‘Hivi wewe mume wangu kweli hilo lilikuwepo…?’ nikamuuliza.
‘Si ndio nimesoma hapa…hebu soma wewe mwenyewe…lakini pia kuna
vipengele vingine hakuna haja ya kivisoma,…kama vile mume wakiona kuna haja, ya
kufanya jambo lenye tija kwa familia,..yeye kama kiongozi wa familia anaweza…ni
vipengele vye kujitetea,..vinasaidia kisheria,..lakini muhimu ni kusameheana …’akasema
‘Kwahiyo uliongeza hivyo, ulipobaini kuwa umezini….?’ Nikamuuliza
‘Nani kazini,…mimi,…mke wangu unanifahamu nilivyo, mimi….hapana
sijaweza kufanya hivyo, kwanza ni nini kuzini….mmh…hivi kuna kipengele hapa…’akawa
anafunua kutafuta.
‘Hapana achana na huo mkataba wa kugushi, nijibu swali langu,…’nikasema
kwa ukali,
‘Kabla sijakujibu swali, twende pole pole, kwani huo mkataba
unaojua wewe ulisemaje…?’ akauliza
‘Unajifanya hujui..ni hivyo…kama umezini, ina maana umetembea nje
ya ndoa,… kukawa na ushahidi wa kutosha, basi ndoa haipo..na huna haki tena
kwenye mali zilizochumwa kwenye ndoa…’nikasema
‘Wauuuh…hiyo mpya kwangu…’akasema
‘Na kwenye kile kikao, wewe mwenyewe ulilisitiza sana hilo kwa
kujiamini,..na ukasema ushahidi ni lazima uwepo, nikakuuliza ushahidi gani na
watu wanafanya kwa siri, ulisema wewe mwenyewe, mtu kama huyo ataumbuka,
anaweza akapata mtoto , huo ni ushaidi tosha,..ikipimwa ikahakikiwa kwa DNA,
basi huo ni ushahidi wa kisheria, unabisha…’nikasema
‘Kikao gani hicho..?’ akauliza akionyesha mshangao
‘Utabisha lakini mbele ya sheria, utanaswa tu…na kwa vile hutaki
kukiri kosa, ukasema ukweli, basi mimi kuanzia leo, najiandaa kwenda mahakamani…’nikasema
‘Mke wangu unakwenda mahakamani kwa kosa gani, mimi nimefanya kosa
gani…?’ akaniuliza
‘La kuvunja mkataba wa ndoa, na kugushi mkataba halali wa ndoa…’nikasema
‘Nimevunja mkataba wa ndoa…!! ?’ akauliza kwa mshangao
‘Ndio umezini…’nikasema
‘Kuzini….’akasema hivyo, sasa akawa anatoa macho kama kuogopa
‘Mimi,…hapana, sijawahi kufanya hivyo, hata kama ulitoa kibali
hicho, lakini mimi sijafanya…’akasema hivyo akiongea kwa haraka haraka kiasi kwamba sikumsikia vyema.
Akatulia kama anasubiria mimi niongee, kiukweli, ukimuangalia mume alivyo, ni kama mtu aliyechanganyikiwa, hajui kabisa
anachokisema, lakini hakuweza kunishawishi kwa hali hiyo, kangu mimi , nilimuona kama anaigiza tu.
‘Ndio wewe umezini, usijitete hapa, kubali tuyamalize, hapa hapa…maana
tukifika huko mbele mimi ninao ushahidi…’nikasema na nilitaka aulize ushahidi
gani lakini hakuuliza hivyo, yeye akasema
‘Mke wangu unasema nini,....sijawahi kufanya hivyo,.....ni nani kakuambia
nimezini, ....na na...mbona sikuelewi..nimezini na nani , umedanganywa mke
wangu, temea mate chini, sijawahi, ..kamwe…’akawa sasa kama anahangaika hivi.
‘Usijifanye mjanja,..leo imefika mwisho wako, ..leteni mkataba ule
wa zamani tuyamalize kwa amani, mimi nitakusamehe, lakini kama haupo huo
mkataba wa zamani, basi kitakachofuatia hapo ni mimi kwenda
mahakamani..’nikasema
‘Mke wangu…’akasema hivyo na mimi nikaa kimia, na akarudia tena...
, ‘mke wangu kwanini unalirudia hilo, mimi nakupenda sana mke wangu, kweli
kabisa....hilo la mkataba wa zamani, silijui mimi, sikumbuki kama kuna mkataba
mwingine zaidi wa huu, kama ungelikuwepo,ningeuleta, tuyamalize mimi na wewe
mbona tumekuwa wa kuridhiana mambo,ulishawahi kuniambia jambo nikakataa..eeh…sasa
huo mkataba ..upo wapi huo…’akasema
‘Sikiliza,… usijifanye
kuigiza mambo hapa,..najua yote hayo, mumepanga uigize hivyo..ujifanye
umechanganyikiwa, ujifanye hukumbuki kitu….na ujanja wako umeshafika
mwisho,..sasa ni muda wa wewe kuniambia ukweli ili tuyamalize kwa amani,..kwani
unataka nini, niambie…sasa nakuulize tena kwa amani, ..je sio kweli kuwa wewe una
mtoto nje ya ndoa?’ nikamuuliza
Kwanza ilikuwa kama kapatwa na kitu kimemfinya hivi, akashtuka, na
alitulia kidogo, halafu akainua uso, na kuniangalia…kiukweli hayo macho yake sijayaona
kabla…akaniangalia, ..mpaka mimi sasa niangalia pembeni..
‘Mtoto nje wa ndoa…!!!’akasema hivyo halafu akatulia, …hakusema
neno, mpaka nilipouliza tena..
‘Nimekuuliza hivi, sio kweli kuwa wewe una mtoto nje wa ndoa,
ambaye hata kwenye mkataba wenu mwingine wewe umemuandikishia urithi, na kwenye
huu mkataba wangu mimi na wewe wa kugushi, kuna maneno mumeyaongezea kuwepo
kwake, ili na yeye atambulikane na apewe haki sawa na wengine, sio kweli ..na hapo
hapo nakuuliza ni kwanini kipengele hicho mkakiongezea maneno kama hayo, kama
sio kweli….?’ Nikamuuliza
‘Mkataba unasema hivyo au sio..huu mkataba, niliona sio, mkataba
wetu mimi na wewe au sio…sasa ngoja nikuonyeshe hapo…unaona hapa, na huu ndio
mkataba wetu au sio…, umeukubali mwenyewe..kwahiyo hiyo sehemu inasemaje,
nikumbushe kidogo mke wangu, mimi nashahau sahau wakati mwingine…’akasema
‘Hapo hukumbuki vyema, lakini kwenye kurudisha vitu kwenye kabati,
hukusahau kitu..hapa kwa hivi sasa huna akili za ajabu,..huoni kuwa unajifunga wewe
mwenyewe…’nikasema
‘Hahaha, hapana mke wangu, sijifungi bwana…ila wewe wanipambikia
mambo, huyo mtoto eeh,....mke wangu kiukweli mimi sikumbuki hilo, ila kuna kitu
nataka nikuambie ukweli, ..hebu kaa kwanza, nitakuambia kila kitu…’akasema na
mimi sikukaa, akainaimisha kichwa chini kwanza kama anawaza jambo…
‘Mke wangu nimekuwa nikiota ndoto ya ajabu sana, kuwa kweli mimi
nina mtoto, tena mtoto huyo ni wa kiume….’akasema
‘Hahaha, umeshaanza kukubali, …haya sema ukweli wote mimi sasa
nitakusikiliza…’nikasema sasa nikikaa.
‘Sasa tulia basi nikuambie..hiyo ni ndoto jamani…’akasema
‘Haya wewe singizia vyovyote vile, ..una mtoto wa kiume au sio, na
huyo ndiye kakufanya ubadili hadi huo mkataba…’nikasema
‘Sikiliza kwanza, nikuhadithis hiyo ndoto, sio kweli, ni ndoto,..ndoto,..kuota
usiku, na kwa bahati mbaya,…nimekuwa nikiota hiyo ndoto sana baada ya
ajali,…wakati nilipoanza kupata kumbukumbu zangu…kuwa nina mtoto wa kiume,’ akasema
‘Una mtoto wa kiume au sio, sasa swali ulizaa na nani huyo mtoto…?’
nikauliza
‘Kwanza nikuulize wewe huyo
mtoto yupo au hayupo…?’ akaniuliza mimi sasa.
‘Unaniuliza mimi tena…’nikasema
‘Mke wangu nisaidie kujibu hilo swali, maana nateseka sana,
kumuwaza, kama yupo, ni heri sana kwangu na kwetu kama familia…’akasema
‘Mume wangu…nimechoka, na maneno yako,…nakuuliza tena hili swali,
kama ni ndoto au ni kweli, je una mtoto nje ya ndoa, kauli yako ndiyo
itathibitisha hili, kama hayupo, basi hatakuwepo,…ilo uweke akilini, kimkataba
na kila hali, sasa kama yupo, ni vyema hilo uliweke wazi,…’nikasema
‘Kama hayupo..hatakuwepo, au sio…’akasema sasa akitabasamu.
‘Ndio hivyo, ukitoa kauli yako sasa hivi, kuwa hakuna mtoto wa
nje..ndio hatakuwepo hivyo…, akitokea…huyo shetani, au sio….’nikasema, nikijua
kama yupo hawezi kumkana.
‘Usiseme hivyo, damu ni nzito kuliko maji…’akasema
‘Hahaha, umeona eeh, hebu rudia tena…?’ nikauliza kama sikusikia
‘Nasema hivi, usiite watoto wa nje mashetani, kwani wao wana kosa
gani,…’ akauliza
‘Kwahiyo wewe unaye, ili tusimuite ni shetani, sema ukweli wako
usimkane mtoto wako…?’ nikamuuliza
‘Mimi sijui….’hapo akasema hivyo
‘Haya niambie uliota nini…?’ nikamuuliza
‘Ehee hapo sasa tuendelee na ndoto yangu, na tusaidiane kwa hili,
ninaota mara nyingi tu, kuwa tuna mtoto wakiume, tatizo sasa ni huyo mama
yake,..hataki ..’akasema
‘Hataki nini..?’ nikauliza
‘Hataki huyo mtoto atambulikane kwa jamii…’akasema
‘Kwanini, ni kashfa au..?’ nikamuuliza
‘Sijui,…ni ndoto, inanitesa sana, sasa nataka wewe unisaidie kwa
hilo, akili yangu inawaza sana hilo, na zaidi ni kauli ya
madocta,..hawajaniambia wazi wazi, lakini nayo ilikuwa kama ndoto…’akasema
‘Wamesemaje…hao madocta..?’ nikamuuliza
‘Mimi sitaweza kuzaa tena…’akasema kwa sauti ya unyonge..
‘Hayo ni ya kwako, nikuulize tena, ni nani mama wa huyo mtoto..?’
nikamuuliza
‘Huyo mwanamke…cha ajabu kabisa, alikimbia na huyo mtoto na ghafla,
sasa wakati nahangaika, eeh…puuh, ajali..na ghafla, nikashtuka kutoka usingizi…’akasema
‘Mume wangu acha ujanja…’nikasema
‘Sasa nikuambie kingine mke wangu, huyo mtoto wetu anafanana kabisa
na watoto wetu utafikiri mapacha..sasa najiuliza ni kwanini huyo mwanamke akimbie
na mtoto wetu,…’akawa kama anataka kulia.
‘Nakuuliza hivi,…huyo mama aliyekimbia na huyo mtoto si unamfahamu…?’
nikamuuliza
‘Ndio namfahamu, kwanini nisimfahamu…’akasema
‘Ni nani sasa…?’ nikamuuliza na hapo akainua uso, akanitizama na sasa
niliona dalili za machoni machoni kwake…anataka kama kulia, moyoni sikuwa na
huruma naye tena, kila kitu cha huruma kilikuwa kimefungwa, nikamkazia macho
yaliyojaa hasira nikisubiria jibu lake.
NB: MBONA NDEFU HIVI
WAZO LA LEO: Huwezi ukahalalisha dhambi kwa
kutengeneza dhambi nyingine juu yake…, usifanye dhambi ili kuficha dhambi
uliyowahi kuifanya, dawa ya dhambi ni kutubu, na kutubu kupo kwa namna nyingi, …moja
wapo ni kukiri kosa, kwa Yule uliyemtendea ukamuomba msamaha, akikubali kutoka
moyoni kuwa kakusamehe, basi hapo huna shaka…lakini kutumia ujanja wa kuhadaa
ili kosa lisionekane kosa na ili Yule uliyemkosea aseme tu kakusamehe,…bila ya
ridhaa yake kutoka moyoni, bado utakuwa kwenye deni ya dhambi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment