Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, January 6, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-52



Baada ya kuongea na watu wangu, nakuona hakuna kingine cha maana, nia ilikuwa kama nitapata kitu kingine cha ziada, lakini sikufanikiwa, zaidi ya yale ninayoyafahamu mwenyewe,…baadae, nikaona nitoke ofisini, nia ilikuwa kurudi nyumbani, nikapitia kwa fundi wa gari langu, nikamuachia ili lifanyiewe service, nikachukua bajaji, hadi kukaribia nyumbani kwangu.

‘Kabla sijapita kwangu nikachungulia ndani kwa docta, nikaona gari lake lipo, sijui kwanini leo yupo nyumbani, nikaona kama jirani mwema ngoja nimsalimie tu.

‘Bajaji nisimamishe hapa..chukua pesa yako, inatosha..’nikampa pesa yake na kwaharaka nikatoka kwenye bajaji na kuingia kwa docta, geti lilikuwa wazi, sikuona mtu nje, nahisi hata mfanyakazi wao hayupo…na wakati huo nikakumbuka maneno ya mtu wangu alipokuwa akitoa taaarifa….

Yeye hata wakati ukiwepo alikuwa akifika kama alivyofika kipindi hiki…yeye hufika kwa minajili ya kikazi, akifuatilia malipo yake ya matibabu ya wagonjwa, ya wafanyakazi wako, na mara zote alizofika alikuwa akiishia mapokezi…’

Ngoja niongee naye tu, lakini nina imani hana zaidi cha kunisaidia…’nikasema wakati huo nimeshafika kwenye mlango, nikagonga..

‘Fungua mlango upo wazi…’ilikuwa sauti ya docta

 Ninajua kuwa mke wake hayupo, kwahiyo sikuwa na mashaka ya kuwasumbua, maana muda kaam huo wanakimama wengi wapo na pilika pilika za kuwajibina na familia zao kwa maandalizi ya usiku, ..

Nikaingia ndani, …alikuwa kalala kwenye sofa, akionyesha katingwa na mawazo, na nahisi alikuwa kachoka kutokana na kazi zake za kuwatibu wagonjwa,..alikuwa akiangalia…aliponiona kuwa ni mimi, akashikwa na mshangao, akasimama, tabasamu kwa mbali mdomoni..

‘Niambie hamna tatizo..maana nimechoka kweli..kuna tatizo..?’ akaniuliza akionyesha mashaka na kweli hata kusimama ilikuwa yaonyesha kachoka.

‘Nimekuja kwako mara moja, kuna maswali machache tu nataka unisaidie kunijibia, kama hutojali...’nikasema

‘Ok, afadhali…uliza tu zilipendwa wangu…, lakini ukumbuke tulishakubaliana, kuwa mimi sihitajiki tena kwenye mambo yenu wewe na mume wako au sio, hata mume wako alinijia juu sana, akanisema kuwa mimi nachangia kuivunja ndoa yenu, kwahiyo nimeona bora niwe mbali nanyi kidogo…’akasema akijihami

‘Ninachotaka kusikia kwako ni ukweli, ukiniambia ukweli, aah, mimi sina shida na wewe,...tatizo wewe huwa unanificha mambo ukijidai kuwa unanijali, kunijali gani huko, wakati unaona naharibikiwa katika maisha yangu…’nikasema

‘Ukweli gani unautaka kutoka kwangu shemeji, kuwa mkweli na wewe kwangu, nimejaribu kila niwezevyo, mlitaka mimi nifanye nini, eeh, niambieni..?’ akaniuliza.

‘Nataka kufahamu kuwa je ni kweli kuwa mume wangu ana mtoto mwingine nje..nina uhakika unalo jibu lake…niambie ukweli, ili nikuache upumzike,...?’ nikamuuliza

‘Unarudi kule kule...nakuomba utoke tu, kiukweli hapa nimechoka, kulikuwana kazi kubwa sana,..na akili yangu yahitajia, kitu cha kuniliwaza sio kunitesa…’akasema

‘mpigie simu mkeo aje…kwanini unamuacha anakaa kipindi kirefu huko, utaibiwa…’nikasema

‘Hahaha…nitaibiwa, akitaka siwezi kumzuia,..ndoa ni mwanandoa mwenyewe, hakuna mtu wa kumchunga mwanandoa zaidi ya yeye mwenyewe…’akasema

‘Ni kweli ndio maana nimekuja kwako, kwani unaweza ukawa na nadharia hiyo kichwani lakini mwenzako akakuchezea shere…je ni kweli mume wangu ana mtoto mwingine nje…ya ndoa..?’ nikauliza

‘Shemeji, haya ni matokea ya maisha yenu,…na sina jibu la swali lako, ila nina maelezo ya kukumbusha tu, kuwa hayo unayowaza, hiyo hali inayokusumbua ni matokea ya maisha yenu wenyewe…’akasema

‘Unajichelewesha mwenyewe, hutaki kupumzika…’nikasema

‘Ni lazima nikuambie hili, kuwa..nilishakuambia kuwa mume wako, alifikia kubadilika kutokana na jinsi mlivyokuwa mkiishi..sasa mimi sijui, huenda labda alikuwa na mahusiano na mwanamke mwingine, ila mimi simfahamu…’akasema akinyosha mikono ya kujitoa hivi.

‘Nasubiria jibu…’nikasema
‘Unajua ni hivi, mwanzoni nilihisi huenda mume wako kabadilika na kuanza kujiingiza kwenye mahusiano ya nje,lakini baadaye, nilipochunguza sana, nikaona kama hakuna ukweli ndani yake, huenda, kama waliwahi kufanya hivyo, basi ilikuwa ni bahati mbaya tu...’akasema

‘Ilikuwa bahati mbaya, kwa nani, hiyo kauli inaonyesha kuwa unamfahamu mtu aliyekuwa karibu na mume wangu,…kwahiyo nastahiki kuupata ukweli kutoka kwako, je ni kweli kuwa mume wangu ana mtoto nje ya ndoa, ni nani huyo, ?’ nikamuuliza

‘Nimekuambia kama iliwahi kutokea hivyo, mimi sikuwahi kuona, na kama ilitokea, basi ni siku mimi sikuwepo, kwasababu mimi nisingelikubali hilo litokee, unajua jinsi gani ninavyokujali…’akasema

‘Kwahiyo zile tetesi zako za awali, sio za kweli,…?’ nikamuuliza

‘Tetezi zipi hizo…?’ akauliza

‘Kuwa huenda mume wangu ana mahusiano nje…’akasema

‘Niliwahi kukuambia hivyo!! ? …hapana ulinichukulia vibaya, mimi nakumbuka kuwa nilikuonya tu , kuwa kwa mienendo yenu, kwa tabia zenu, za kuwa hata mkirudi nyumbani mnajifanya mpo bize, hamjali hata ndoa zenu ipo siku mume wako atakwenda kutembea nje ya ndoa, wewe si hujali, unajifanya huna hisia, sasa wanaume wengu kuvumilia ni shida, nilikuambia hivyo, au….’akasema

‘Na kwanini kila ukiwepo,…hasa kule hospitalini, kila nikitaka kumuuliza mume wangu aniambie ukweli, ulikuwa unamzuia, ni kama unafahamu jambo, lakini hukutaka mume wangu aniambie ukweli, ni kitu gani hicho, niambie ukweli, kwani baada ya hapa, naweza tusiwe na urafiki tena mimi na wewe…?’ nikamuuliza

‘Kwa kipindi kama kile, mimi kama dakitari, pia mimi kama rafiki yenu mkubwa, nilijitahidi kuzuia madhara, kwa mumeo na kwako, nakufahmu kama nilivyomfahamu mume wako, haikuwa na haja ya kuongea mambo yanayoweza kuamusha hisia na matokea yake yangelikuwa mabaya, ..’akasema

‘Hahaha..hata sikuamini, …kwanini lakini…’nikasema

‘Na ningekuzuiaje usiongee na mume wako wakati mpo naye siku zote…’akasema

‘Na kwanini ulimshuku rafiki yangu kuna anaweza akawa na mahusiano na mume wangu..bado nahisi wewe una ukweli hutaki kuaniambia,…niambie kama kweli wewe unanijali..?’ nikamuuliza

‘Awali nilikuwa na shaka hiyo...lakini nimekuja kufanya uchunguzi nikaona hilo halipo, na kama lipo,…mimi sijui, labda lilifanyika kwa siri kubwa sana, nimeongea na rafiki yangu, nikamuomba aniambia ukweli...hajataka kuniambia ukwelina tukaishia kukwaruzana, mpaka ananipiga marufuku ya kufika kwako, uelewe hali ilipofikia hapo…’akasema

‘Kwa kukukataa kwa mume wangu kukuambia ukweli ndio umerizika kuwa ni kweli hakuwa na mashusiano ya yeye, au unaogopa kusema kwa vile mumekwaruzana na mume wangu…?’ nikamuuliza

‘Pamoja na hilo, lakini kwa juhudi zangu nyingine nimeona hakuna kitu kama hicho, na mtoto wa rafiki yako, wengine wanasema ana sura ya kizungu, wengine mwarabu, sasa mume wako ni mwarabu, …kwakweli, baada ya yote hayo, nimeona niachane na nyie, mpaka hapo mtakaponihitajia…’akasema

‘Swali langu ni hili, Je ni kweli mume wangu ana mtoto nje..nijibu tu kwa kifupi, ili niondoke zangu?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui, kwasababu hajawahi kuniambia hivyo...’akasema

‘Una uhakika na hilo…?’ nikamuuliza

‘Siwezi nikasema nina uhakika na hilo, je kama anaye, na mimi sijui, ukaja kugundua uaminifu kwangu kwako utakuwaje, nakushauri tu, hujachelewa, kwanini usimuulize kwa staha akuambie ukweli yeye mwenyewe…’akasema.

‘Mara nyingi unamkinga rafiki yako,…sasa unasikia, kama nikija kugundua kuwa ana mtoto nje utasemaje, ..maana kama anaye nina uhakika wewe unalifahamu hilo, ina unamficha siri rafiki yako, lakini kwanini hujiulizi na mimi je..itaniathiri vipi, je inaathiri vipi familia yangu, umejiuliza hilo…’nikasema

‘Kwa hali ile mliyokuwa mkienda nayo, na kwa tabia yake ile ya kulewa, kupitiliza, hilo siwezi kuona ni ajabu....kama nilivyokuambia awali, kwahiyo kama nikujilaumu jilaumu wewe mwenyewe,…....’akasema

‘Kwahiyo wewe huwezi kuona ajabu kuwa yeye ana mtoto nje, ndivyo mlivyo wanaume, je ni sahihi kufanya hivyo, je mimi ningelikuwa hivyo, mgelikubaliana na hilo…?’ nikauliza

‘Kwanini unaniuliza maswali hayo, kuna nini kimetokea shemeji hebu niambie ukweli…?’ akaniuliza

‘Mimi ninachotaka ni ukweli tu…’nikasema

‘Ukweli mimi sina..na zote hizo ni shaka shaka tu, na shaka shaka, zimekujaje kwako, wakati hupendelei tabia hiyo, usiige tabia hiyo utajitwika mzigo kabla haujatua kichwani mwako, utajiumiza mapema, kaeni wawili muongelee matatizo yenu yaishe…’akasema

‘Yataishaje wakati kuna matatizo mengi ambayo, nahitajia maelezo yake, yatakiwshaje wakati kama huu ambapo kuna mambo ya kuharibu kila kitu,.., kuna njama za kuhakikisha kuwa mali za familia zinachukuliwa na watu wengine, mimi sijui, na ni nani kaidhinisha hilo…’nikasema

‘Mhh..kwahiyo tatizo ni wasiwasi wa mali, au sio…?’ akauliza

‘Kutokana na mkataba wa kugushiwa, mali itagawiwa kwa watoto wa nje, kwa wtoto wa marehemu pia, na huyo mtoto wa nje ana haki sawa na watoto wetu…hayo kayaidhinisha nani,…mkataba wa kugishiwa unasema hivyo,…haya sawa, je ni kweli yupo huyo mtoto wa nje, mbona siambiwi ukweli, je kweli sina haki ya kulifahamu hilo….sio kwamba natetea mali, nataka kulifahamu je hiyo sio haki yangu….’nikasema

‘Hapo mimi siwezi kukusaidia kabisa, mkataba mliweka wewe na mume wako na wakili wako, au sio…hao ndio wa kupambana nao, na wala usiwarushie watazamaji mpira ukategemea kuwa watakusaiaid kufunga magali,..huo ni mchezo wako, cheza na mumeo au nimekosea hapo…?’ akauliza

‘Najua sasa utajiweka pembeni, ufurahia ndoa ikisambaratika, si ndio ulichokuwa wewe unakitaka, sawa, nitaucheza huo mpira mwenyewe, ..tatizo ni mkataba wangu upo wapi…’nikasema

‘Kwani ulikuwa haukusajiliwa..?’ akaniuliza

‘Ulisajiliwa na kwa taratibu zote kabisa..lakini sijui kilichotokea, ukaja kubadilisha, kila sehemu husika,..hata nakala yangu ya halali, ikapotea na kuwekewa nakala ya bandia,..’nikasema

‘Hata huko kwa mdhamina …haiwezekani…’akasema

‘Ndio hivyo…’nikasema

‘Kiukweli kutokana na majukumu yangu kuwa mengi, niliacha kabisa kufuatilia mambo yako, na hata wazazi wako wamesema tuachane na familia yako,kwa vile nawe umezidi kiburi, wanakuangalia tu, wameshasema utaweza mwenyewe na uskishindwa utawatafuta…’akasema

‘Sijashindwa bado…ila kuna hayo yaliyozuka kuwa mume wangu ana mtoto nje…hilo linanifanya niwe na wakati mgumu, na hataki kuniambia ukweli,..na kila hatua anazidisha matatizo, je nitaishi na matatizo haya mpaka lini, je nitaweza kuyavumilia…’nikasema

‘Nikuulize tu swali, Je kama ni kweli..unielewe hapo, mimi sijui, ila nauliza tu je kama huyo mtoto yupo utafanyaje…?’ akaniuliza

‘Kwanza nikufahamu ukweli,..hiyo ni haki yangu ya msingi,..kwasababu kama ni kurithi mali, hiyo mali, tumechuma wote..na mali hiyo imetokana na wazazi wangu, je ni haki kuitoa kwa watu baki, bila maelezo…sasa mimi nitafanyaje, hilo tulishawahi kuongea mimi na mume wangu,kutokana na hali ilivyo, ndio tukakubaliana kuwe na mikataba..kwahiyo kwangu haina shida, sheria itafuta mkondo wake…’nikasema

‘Na huo mkataba mpya unasemaje kuhusu hilo…?’ akaniuliza

‘Siutambui,..najua wameweka vipengele vya kujilinda, haina haja ya mimi kuupekenyua sana, haunihusu …’nikasema

‘Lakini mimi bado nina mashaka, maana hilo la mtoto wa nje, mara nyingi halina siri, watu hawawezi kulivumilia hilo, kama kweli angelikuwepo, hiyo taarifa iingeshavuma, ni kwanini iwe siri kihivyo...’akasema.

‘Ndio maana nilitaka kuufahamu ukweli kutoka kwako, maana mpaka inatokea hisia hizo, ina maana kuwa mume wangu alikuwa na mahusiano na mwanamke fulani, sasa kazaa naye au sio yeye, bado haijasaidia kuuficha ukweli kuwa mume wangu alikuwa akitembea nje ya ndoa, au sio...?’ nikamuuliza.

‘Kutokana na ulevi wake, yote yawezekana, ila nasema ukweli kutoka moyoni, kama ilitokea hivyo, basi siku hiyo mimi sikuwepo, kwa ushauri wangu shemeji, kuliko kujiumiza kihivyo, naona hilo achana nalo, litakupotezea muda, na mawazo mengi bure, kama yupo yupo tu....’akasema

‘Sasa hapo unataka kusema nini, kama yupo yupo tu, ina maana mimi nikubali tu hivyo kirahisi..na nikikubali unafahamu madhara yake, leo hii watu baki wameshaanza kugombea mali..wanayodhania ni ya baba yao..unahisi sababu ni nini, ni kwa vile watu mnakumbatia haramu…sasa ngoja niupate huo mataba wangu uone nitakachokifanya...’nikasema.

‘Mimi sijakumbatia haramu , mimi sijaunga mkono hayo, najua ni makosa, lakini ni nini chanzo cha hayo makosa, usije ukawa wewe ndio chanzo…’akasema akiangalia saa yake

‘Nikuulize swali hili, halafu niondoke zangu, awali ulisema kuwa utafany auchunguzi kugundua baba wa mtoto wa rafiki yangu, je uliwahi kuufanya…umegundua baba wa huyo mtoto ni nani..?’ nikamuuliza.

‘Hiyo imekuwa ni siri ya hali ya juu, na hata nilipokwenda kumuuliza dakitari aliyehusika naye siku ile sikuweza kupata lolote, hilo limekuwa siri kubwa sana,..na ni ajabu kutokea hivyo…lakini sikutaka kulifuatilia sana, kutokana na kauli yako wewe mwenyewe, nikajua huenda umeridhika na hilo, huenda wewe unahusika, nikuulize swali wewe si uliwahi kumuona huyo mtoto, je sura yake ipoje,....?’ akaniuliza.

‘Sura yake ipoje,!!!..haiwezi kunipatia uhakika wa swali langu maana sura yake inaweza kufanana nay a watoto wangu, ya watoto wa shemeji, ya….kwahiyo hilo bado halileti jibu sahihi…’nikasema

‘Kama ni hivyo, kwanini uumize kichwa chako, kumbe jibu unalo tayari, muhimu kwa sasa ni kumbana mumeo, au sio….tafuta njia ya kumfanya mumeo aongee, nina imani huwezi kushindwa hilo, au ..unahitajia msaada wangu…?’akasema na kuuliza

‘Kirahisi hivyo, unajua kilichotayarishwa na mume wangu,…tatizo sio hilo tu, ni baada ya kukubali hilo,…na hayo makubaliano ya kuwa haki ziende huko, kwanini mume wangu hakunishirikisha,…huo mkataba mpya ni wa nini…na kwanini hadi familia za marehemu zihusike, huoni kuwa kukubali kwangu kutaharibu mengi…’nikasema

‘Mhh…hapo kuna kazi..lakini..kama ni kweli, utafanyaje sasa, utavunja ndoa yako…?’ akauliza

‘Hayo sio muhimu kwangu kwa hivi sasa… , muhimu kwangu ni kuufahamu ukweli kwanza…na pili muhimu kwangu ni kuwa na huo mkataba wetu wa asili, basi, baada ya hapo kila kitu kitajimaliza chenyewe, na matatizo yataisha..swali ni kwanini ukweli unafichwa, kuna nini kimetayarishwa, mume wangu anaogopa nini…’nikasema

‘Jibu ni tahisi tu…anaogopa huo mkataba wenu wa awali…’akasema

‘Ok…nimekuelewa…’nikasema

‘Mimi nakushauri hivi, kwa vile mume wako kajirudi, ..achana na mambo hayo, ya kumchunguza chunguza sana…kwasababu hilo limeshamuweka kubaya, sasa hivi anatapa tapa..na huwezi kujua zaidi ya hapo ana malengo gani…’akasema

‘Kwahiyo..?’ nikauliza

‘Yavutie subira, kubali kwanza kwa nia ya kuupata ukweli, baada ya hapo, utajua mwenyewe la kufanya…’akasema

‘Huo ni mtego…mimi siwezi kujiingiza kwenye mtego wa tembo..sina uwezo huo…muhimu nitasimamia kwenye ukweli na haki…’nikasema

‘Ni sawa, lakini nilikuambia, je kama hayo yote ni matokea ya wewe mwenyewe utasemaje…?’ akanuliza

‘Hivi, ..mume wangu ni mtoto mdogo, au hao alioshirikiana nao ni watoto wadogo, hawafahamu njia sahihi…unataka kusema mtu akikuambia ule mavi utakula, kwa vile umeshauriwa na rafiki yako mpenzi…hilo sio swali la kuniambia hivyo, kuwa huenda inatokana na mimi..’nikasema

‘Una maana gani..ina maana kuwa kuna mambo yamtokea hapo kutokana na ushauri wako, au…niambie ukweli…’akasema

‘Unanipotezea muda wangu swali jingine kabla sijaondoka je wewe uliwahi kuongea na wazazi wangu hivi karibuni?’ nikamuulzia

‘Jana tu, nilikuwa na wazazi wako…tulikuwa na kikao kirefu tu mimi na wao…’akasema

‘Wanasema nini juu ya hili tukio...?’ nikamuuliza

‘Wao wameamua kukuachia mambo yako, ila wanachoogopa ni kuwa mume wako anaweza kukuingiza kwenye kashifa kubwa, wanahisi hiyo iliyotokea ni ndogo tu…wanaweza kuihimili…, lakini baadaye kunaweza kukazuka mambo ambayo hata wao hawatataka kuyasikia..si unamfahamu baba yako alivyo....’akasema

‘Kwahiyo wao wanashauri nini?’ nikamuuliza

‘Unafahamu msimamo wa wazazi wako toka awali, msimamo wao ni ule ule, hawana imani na mume wako, hilo, sio wao tu, hata wale waliopo karibu na baba yako wanamuonya dhidi ya mume wako,..sasa sijui, ..’akasema na kutikisa kichwa.

‘Mhh..najua tu, hayo ni mambo ya kisiasa, na likitokea wanavyotaka wao, bado italetwa ajenda nyingine, …’nikasema

‘Unajua kuwa wazazi wako wamegundua kuwa mume wako sio mkweli, na ana tamaa, na anaweza akaharibu maisha yako ya baadaye, kuna kipindi waliniomba niingilie kati, ikibidi, ....ooh, sipendi huo ushauri wao’akasema

‘Ikibidi nini..?’ nikauliza

‘Wao, wanazidi kusema kuwa ndoa yako na mume wako haifai,…itakuja kukuumiza sana, na huenda, usiwezi kufaidi matunda ya jasho lenu,..mumeo, ana watu wanaomzunguka, na kumtumia yeye kama daraja, …yeye bila kulifahamu hilo anakubali tu,..mwisho wa siku watamtekeleza, kifupi wao, wanaona ni bora, ndop hiyo ivunjwe, kwa masilahi ya kizazi cha baadae,...’akasema.

‘Hivi nyie mnaona kuwa hilo jambo rahisi sana...?’ nikauliza

‘Ni ushauri wao,..ni ushauri wa marafiki za wazazi wako, ni ushauri wa ….kila mtu mwenye nia njema na nyie… ila hawajataka kukushinikiza kwa vile baba yako yupo kwenye ushindani wa kisiasa…hataki kujiingiza sana kwenye ndoa yako,…’akasema

‘Mimi siwezi kulisikiliza hilo kwa vile yule ni baba wa watoto wangu, ...hamuoni kuwa nikifanya hivyo, nitawaumiza watoto wangu, kwanini hamliangalii hilo pia, sio kwangu tu, je kwa watoto wangu, watoto wangu wanampenda sana baba yao..’nikasma sasa nikitamani hata kulia.

‘Usijiweke mnyonge kihivyo, sitaki ulie kwa hilo, wewe ni shupavu, pambana, mimi nina imani kuwa utashinda…’akasema

‘Hapana inaniumiza sana..nikiona mtu, ambaye niligangaika naye, ili tu atokane na ile hali, nilimpenda nikijua atabadilika, leo hii..hapana..hata hivyo, mimi sitaki watoto wangu waje kuumia, ni kweli hata mimi imefikia hatua natamani nifanye hivyo..lakini kila nikiwaangalia  watoto wangu, nakosa amani...nashindwa kuchukua huo uamuzi...’akasema

‘Hata mimi, nimeliona hilo,..ndio maana nimekuwa nikipingana na ushauri wa wazazi wako, kama ningelikuwa sijaoa, ningelifanya juhudi ya ziada , na ningafanya hivyo,...hata hivyo,  mwisho wa yote ni wewe mwenyewe, kama kosa limetokea, na una uhakika halitajirudia tena basi msamehe mume wako, sio lazima mtu awe kama watu wanavyohisi, yeye kama binadamu anaweza kujirudi na akabadilika....’akasema.

‘Tatizo mume wangu hajakubali kuwa mkweli, na ili kuficha uwongo wake, yeye anazidi kuzua mambo mengine makubwa, na makubwa zaidi, ambayo sitaweza kuyavumilia, na nahisi kutokana na hayo mambo makubwa, yatazuka mengine makubwa, na amani kwenye familia itakuwa haipo tena, je nikae tu  nivumilie, nivumilia mpaka lini..’nikasema.

‘Hayo mambo mengine makubwa ni nini,…ni huo mkataba mpya au…?’ akauliza

‘Kuhusu huo mkataba, kuhusu watoto wa marehemu, kuhusu huyo mtoto wake wa nje…asiyejulikana…hayo yanazidi kuongezeka, bado sijamfahamu mama wa huyo mtoto, je atakuja na ajenda gani..bado watoto wa marehemu hawanipi amani…kwanini hivyo….’nikasema.

‘Hata wazazi wako wanahisi hivyo hivyo’akasema

‘Ina maana wazazi wangu wanafahamu kuwa mume wangu ana mtoto nje?’ nikamuuliza.

‘Huwezi kuwaficha wazazi wako kitu, wazazi wako wana macho ya kuona mbali, wana masikio yakusikia kila kinachotokea kwenye ardhi, kukuhusu wewe, japokuwa hawataki kuthibitisha hilo, lakini nahisi wameshaliona hilo, na hilo ndilo linalowafanya wasimwamini mume wako, ...’akasema

‘Waliwahi kukuambia au kukuulizia hilo…?’ nikauliza

‘Hapana,…hawajasema moja kwa moja, na wao wanakwepa kuliongelea hivyo, najua wana maana yao…ila hilo la watoto wa marehemu kuja kudai hisa,…wamasema wanalisubiria kwa hamu....’akasema.

‘Je wao wanataka mimi nifanye nini?’ nikauliza

‘Wanasema waliwahi kugundua kuwa wewe una mkataba ambao ukiutumia utaweza kumaliza kila kitu, lakini cha ajabu mkataba waliokuja kuuona wao, hauna manufaa kwako, na ndio baadae wakasikia kuwa mkataba huo sio halali, ulikuwepo mwingine. Na ndio maana hawajui ukweli upo wapi…’akasema

‘Ni nani aliwaambia kuhusu kugushiwa kwa huo mkataba je ni wakili wangu nini?’ nikauliza

‘Hapana, ni wakili wao....’akasema

‘Kwahiyo wakili wao anafahamu mengi kuhusu hiyo mikataba?’ nikauliza

‘Sina uhakika na hilo, kwani yule ni mtu wa wazazi wako hawezi kuongea zaidi, yeye anaongea yale wazazi wako wanayotaka aongee, hasa inapofikia maswala ya kifamilia...’akasema.

‘Je nitawezaje kuupata mkataba huo wa awali....?’ nikawa kama namuuliza yeye

‘Je ukiupata huo mkataba wa awali, unaweza kufanya nini?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho ya kunijaribu

‘Mkataba wenyewe utaongea, na kiukweli, sijui…sizani,…nasema hivi, safari hii sirudi nyuma, mkataba wenyewe utasema ni nini cha kufanya, kwakeli nimechoka, ....naona sasa basi....na kama ni kweli kuna mtoto nje, ..nitahakikisha nafanya lile lilipo kwenye huo mkataba, sitavunja ahadi yangu kamwe...’nikasema

‘Uwe makini lakini.., usije ukafanya jambo ukaja kujilaumu baadae...’akasema.

‘Huwezi kubeba mtu asiyebebeka, ...wema wangu usiniponze, ...siwezi kutengeneza maadui kutoka ndani kwa marafiki zangu wenyewe, ni lazima,nijue ukweli, na kama ukweli ndio huo, basi, ni bora nibakie bila marafiki kuliko kuwa na marafiki wanafiki, ambao wananichekea tukiangaliana wakigeuka, wananing’ong’a....’nikasema na kusimama kutaka kuondoka.

‘Una uhakika na hilo…?’ akauliza

‘Lipi sasa..?’ nikauliza

‘Kuwa ukipata mkataba wako wa zamani, hutarudi nyuma, utaacha sheria ichukue mkondo wake..?’ akaniuliza

‘Umenisikia au sio, kama ungelikuwa wewe ungelifanya nini hapo…, baada ya haya yote, jiulize tu…nimevumilia mangapi, wangapi wamenicheka kuwa naona lakini najifanya sioni..sasa imetosha,…lakini muhimu ni ukweli, na ushahidi…sitaki mambo ya kuhisi tu..’nikasema nikianza kuondoka, huku machozi yakinitoka natamani kulia...

‘Sawa ngoja tuone…ili jikaze usiwe dhaifi kihihivyo, hiyo sio damu ya baba yako..thibitisha hilo kwa vitendo…’akasema na mimi nikawa nipo nje, naondoka zangu, sikusubiria anisindikize kama kawaida yake.

********

Nilipofika nyumbani, niliona gari la mume wangu, siku hizi anatumia gari jingine, la kampuni yake, nikajua yupo ndani, nikatembea kwa haraka kwenda ndani, akilini nikitaka kuongea naye niufahamu ukweli wote, hilo la mtoto wan je liliniumiza sana kichwa.

‘Leo ataniambia ukweli wote…’nikasema nikiingia ndani

Nilitaka leo tukae naye kikao, ..sikutaka tena kuzungushana, kama hataki itabidi nichukuea hatua kubwa zaidi, ikibidi niende mahakamani kwa kugushi mkataba, kwa kuvunja kiapo cha ndoa, kwani kwasasa nina ushahidi wa kutosha, na nina mashahidi..

Nikaingia ndani, hadi chumbani, sikumuona nikajua yupo maktaba, nikafungua mlango wa makitaba, hakufunga kwa ndani kwani mara nyingi, kama hutaki kusumbuliwa, huwa unajifungia kwa ndani, nikafungua mlango taratibu na kuingia ndani.

Mume wangu alikuwa kachuchumaa kwenye kabati langu, ...!

Hilo ni kabato langu, na mara nyingi nalitumia mwenyewe, na akitaka kitu huwa nakwenda kukichukua mimi mwenyewe, kwani hana ufunguo wake… na hapo ndipo niliweka ule mkataba

Na nilipotupa macho kwenye kabati ninapoweka bastola, niliona kabati lipo kama limefunguliwa, moyo ukanilipuka, huyu mtu kapatia wapi ufungua, alikuwa hajanigundua kuwa nimeingia, alikuwa kainama akiwa anapekuapekua , ..katoa vitu vingi nje, kuna kitu anatafuta, ...nikavuta subira.

‘Mbo-mbo-na haipo ooh….’akasema akijiuliza na sasa akataka kugeuka, kabla hajageuka nikamuuliza

‘Unatafuta nini kwenye kabati langu, na ufunguo umaupatia wapi...’nikamshitua, oh...alivyoshituka, nikajua nimeua, nimefanya kisichotakiwa kutokana na afya yake!

NB: Mambo yanaanza kujitokeza, wewe unahisi nini hapo…hii ndio ya wikiendi, tujadilikidogo kuhusu hili..je mtoto wa nje ana haki sawa na watoto wa ndani..kama baba akiamua hivyo, je mama hastahiki kufahamu kila kitu, na je akifahamu hatua gani achukue…TUJADILI?


WAZO LA HEKIMA: Mnapo-oana,na mkafikia kwenye msigishano ambao unaweza kuleta madhara ya ndoa, mjaribu kuangalia  hatima ya watoto wenu, je tatizo hilo ni kubwa sana la hata kuvunjika kwa ndoa yenu, inawezekana ikafikia hapo,na hakuna njia nyingine, kama ni hivyo basi ni bora mkapata ushauri wa kitaalamu ni jinsi gani  mnawezaje kuwasaidia watoto wenu, ili wasije kuathirika kisaikolojia....


msiwajengee watoto wenu chuki, kwa mama au baba kwa kuwapandikiza uhasama watoto ili tu eti wamchukie baba au mama, hilo ni kosa kubwa sana kwani wao hawahusiki kwenye matatizo yenu na kuwapandikizia chuki hizo mnawajengea tabia mbaye kwenye maisha yao ya baadae
Ni mimi: emu-three

No comments :