Ilikuwa siku maalumu ya kupokea taarifa kutoka kwa watu wangu, kuna
vijana huwa nawapa kazi zangu, kwa kuwaamini, hasa zinazohusu mambo yangu
binafsi, hata ya kikazi pia…nilifika ofisini na kumwamboa katibu muhutasi kuwa
hao vijana wangu waitwe mmoja mmoja…na wakati nipo tayari, mara mlango
ukagongwa...
‘Unaweza kuingia..’nikasema
Akaingia jamaa mmoja…yeye ni mtu wa masoko, lakini pamoja na kazi
hiyoo yeye nimatumia kwa mambo ya uchunguzi ikibidi..ana utaalamu huo, na
nilishampeleka shule kusomea upelelezi kidogo, inasaidia kwa kazi
zangu…Nilimwambia kuwa nataka asomee upelelezi kidogo, kwa nia ya mashindano ya
kibiashara, lakini pia nataka anisaidie kwenye kazi zangu.Tunaelewana sana.
‘Kutokana na uchunguzi wangu, mtu aliyechukua huo mkataba atakuwa
ni mtu wa humo humo ndani, alitumiwa,…maana hakuna mtu wa nje aliyweza uingia
kwenye ofisi yako, akaonekana…’akasema
‘Huyo mtu wa nje ni nani, uliweza kumtambua …?’ nikauliza
‘Imekuwa ngumu kidogo…’akasema
‘Je ni nani aliwahi kuifika kati ya watu niliokuambia uwachunguze,
?’ nikamuuliza
‘Mtu ambaye aliweza kufika mara kwa mara ni docta Yule unayemuita Rafiki
wa mume wako,…’akasema
‘Ehe…je uliweza kufahamu, kama aliweza kuingia ofisini kwangu au
kuongea labda na mfanyakazi wangu wa usafi…?’ nikamuuliza.?’ nikamuuliza
‘Yeye hata wakati ukiwepo alikuwa akifika kama alivyofika kipindi
hiki…yeye hufika kwa minajili ya kikazi, akifuatilia malipo yake ya matibabu ya
wagonjwa, ya wafanyakazi wako, na mara zote alizofika alikuwa akiishia
mapokezi....’akasema.
‘Una uhakika na hilo…?’ nikamuuliza
‘Kwa uchunguzi wangu naweza kusema hivyo, sizani kama aliweza
kuingia ofisini mwako,…’akasema
‘Mwingine ni nani…?’ nikamuuliza akilini mwangu nikianza kujiuliza
kama docta anaweza kufanya kitu kama hicho, haiwezekani, kwasababu hana faida
yoyote na huo mkataba…labda kumsaidia rafiki yake…hapana haiwezekani.
‘Na mwingine aliyeonekana, ni bosi, nina maana ....rafiki yako, kuna
kupindi alifika kabla hajaondoka kusoma na pia aliporejea,..’akasema
‘Aliporejea..!?...alifuata nini…?’ nikamuuliza
‘Alikuja akikuulizia, lakini hakuweza kuingia ndani ya ofisi yako,
naye aliishia mapokezi, na hakukaa sana, kwani aliambiwa haupo....’akasema
‘Na kabla…?’ nikauliza
‘Kabla ni kipindi ukiwepo, au…kama haupo, anaishia mapokezi
tu…..’akasema
‘Kwahiyo hakuna mtu yoyoye mwingine ambaye tunayemshuku,
aliyeonakana akiongoea na mfanyakazi wangu wa usafi, ambaye ndiye anayetunza
ufunguo za ofisi yangu?’ nikamuuliza
‘Tatizo ni kuwa huyo mfanyakazi wako wa usafi, anaongea na watu
wengi sana, sasa sio rahisi kuhisi yupi ni yupi, hata nilipotumia mbinu za
ziadi kupata taarifa kwake, ilionekana kama tunamshutumu mtu ambaye hajafanya
jambo kama hilo, nina uhakika kama ni mtu aliingia, yeye atakuwa hajui
kabisa..’akasema.
‘Sasa alipaje ufunguo….?’ Nikauliza
‘Hapo hatukuweza kupata ukweli,….’akasema
‘Ina maana kwa uchunguzi wako,…maana nimekupa kazi hiyo ili
nimpate huyo mtu, wewe umegundua nini, angalau kidogo cha kusaidia…au
umeshindwa kumpata…?’ nikamuuliza
‘Mwanzoni nilimuhisi katibu wako muhutasi, kwasababu yeye ana haki
ya kuingia na kutoka ofisi kwako, lakini nilipofuatilia nyendo zake, niliona
hahusiki, maana alikuwa likizo kipindi chote hicho ambapo wewe hukuwepo ofisini.’akasema
‘Kwa kifupi bado hujamgundua ni nani alifanya hivyo..?’ nikauliza
‘Kiukweli bado bosi, tatizo wewe hutaki tufanye tuonavyo sisi,
wewe umeteka tufanye utakavyo wewe sasa inakuwa ni ngumu kidogo, ukitaka
tumgundue kwa njia zetu, tupe hiyo nafasi, tutampata tu,…’akasema
‘Hapana msifanye hivyo, nilitaka kufahamu mambo machache kutoka kwenu
sitaki kuleta utata kwa hili, unanielewa, basi tusipoteze muda, wewe endelea na
kazi zako…’nikasema
‘Sawa bosi….’akasema hivyo na kuondoka.
Wa pili alikuwa mtu ambaye nilimpa kazi ya kuchunguza nyendo za
mume wangu kipindi hicho, kabla hajapata ajali..akasema;
‘Siku mume wako alipopata ajali, alionekana akiwa katokea maeneo
ya rafiki yako,kwahiyo huenda alipita hapo,au alitokea hapo kwa rafiki yako ...’akasema
‘Huna uhakika kuwa alitokea kwa rafiki yangu…?’ nikauliza
‘Uhakika wa moja kwa moja haupo…kwasababu hakuonekana akiingia au
kutokea kwenye nyumba ya rafiki yako,…’akasema
‘Kwahiyo ni kweli kuwa alipita tu…?’ nikauliza
‘Mara nyingi yeye anasafisha gari lake kwa muosha magari karibu na
anapoishi rafiki yako,…cha ajabu muosha magari, japokuwa hayupo, lakini
nilimfuatilia mpaka huko kijijini kwao, nikaweza kuongea naye, hakuataka kabisa
kuongea na mimi, ila baada ya kumpatia chochote, ndio akaongea
‘Anasemaje..na kwanini kaondoka hapa Dar..?’ nikamuuliza
‘Anasema maisha yamemshinda tu, kaona akafanyie shughuli zake
kijijini…’akasema
‘Ehe,siku hiyo ilikuwaje…akiwa kazini kwake,..hakuwahi kuosha gari
la mume wangu..?’ nikamuuliza
‘Anadai hakuwahi kuosha gari la mume wako, hakumbuki
kabisa..anasema yeye anaosha magari ya watu wengi, na sio kazi yake
kukariri..lakini ana uhakika hakuwahi kuosha gari la mume wako, …’akasema
‘Ni kweli au anaogopa tu kusema ukweli..?’ nikauliza
‘Nimetumia kila mbinu hajakubali hilo, nahisi hakuwahi kuosha, au
hakumbuki kweli, sizani kama angetuficha...’akasema
‘Kwahiyo ni kweli kuwa mume wangu alipita tu maeneo hayo na
hakuwahi kufika kwa rafiki yangu..?’ nikauliza
‘Itakuwa hivyo, ila waliomuona akiendesha gari, wanasema alikuwa
katokea maeneo ya huko, na alikuwa akiendesha kwa mwendo kazi sana, nikama vile
alikuwa akiwahi jambo, na.....hakuwa
amelewa kabisa, kwani ofisini kulikuwa na kikao, na alipotoka kwenye kikao
hakupitia kwenye ulevi..’akasema
‘Hakupita kwenye ulevi, aliyekuambia hivyo, amejuaje, …ina maana
alifahamu anapoelekea …alipokwenda mume wangu..?’ nikauliza
‘Wanafahamu wapi anapokunywa mara kwa mara..na hao walimuona
akitoka ofisini, na kuendesha gari…kuelekea upande mwingine, hawakufuatilia,…na
tulijaribu kutafuta mtu mwingine …hakuna aliyemuona akielekea kwa rafiki yako…’akasema
‘Hilo naweza kuamini kuwa hakuwa huko kwa rafiki yangu maana mimi
mwenyewe nilikuwa huko, kama angelifika mimi ningelimuona.’nikasema
‘Sasa ajali yake ilitokea kwa vile alikuwa kwenye mwendo kazi, na
alipokuwa akata kona..ndio akakumbana na hilo gari jingine..akafunga breki
lakini zilikataa, ndio ikapatikana na hiyo ajali...., alikuwa mwepesi kuruka
nje..,na wakati anatoka alionekana, akiwa na mkoba, .....’akasema
‘Aliruka kabla…mmh, hapo, unataka kusema nini, na huo mkoba
wa…komputa au…?’ akauliza
‘Ni mikoba hii ya kawaida, na kwa vile aliumia sana, aliyekuja kumsaidia,
anasema mume wako hakutaka kabisa kuachana na huo mkoba, na kuna mmoja alitaka
kumsaidia, lakini akakataa,...’akasema.
‘Na alipofika mlangoni mwa nyumba yenu, alionekana kupiga
simu,..ndio akaja jirani yenu mmoja…ndiye aliyemsadia hadi kwa nyumbani kwa
docta..na huyo docta ndiye aliyemsaidia kwa huduma ya kwanza...’akasema.
‘Mlipochunguza nyendo zake za huku nyuma , mligundua nini?’
nikamuuliza.
‘Mara nyingi alikuwa akienda kunywa na rafiki yake, yule docta, na
wakati mwingine akiwa peke yake, alionekana mpweke, na hakupenda kukaa na watu
asiowafahamu…’akasema
‘Na zaidi ya huyo docta ni nani wengine alipenda kunywa nao…nikimaanisha
wanawake labda?’ nikauliza
‘Kiukweli hao hawakosekani, wakiwa kwenye makundi, …lakini
haikuonyesha wazi kuwa ana rafiki wa kike wa kupitisha naye muda…’akasema
‘Hakuna mwanamke ambaye alikuwa naye karibu sana..hakuna hata
mmoja..?’ nikauliza
‘Mwanamke ambaye mara nyingi anakuwa naye karibu ni rafiki yako,
huyo anayesoma huko nje, yeye mara kwa mara walikuwa wakionekana naye, najua
hata wewe mwenyewe unalifahamu hilo, ni hata mkiwa wote yeye anakuwepo, au sio,
huwezi kumshuku vibaya..na wengine ni wafanyakazi wake, au wa ofisi
anayoifanyia kazi...’akasema.
‘Je mume wangu hakuwahi kumsindikiza rafiki yangu huyo hadi
kwake,, na hata kuingia kwake, na hata kukaa kwa muda mrefu wa kutilia mashaka,
au japokuwa kwa muda mfupi?’ akaulizwa.
‘Ndio, mara nyingi tu, huwa wanamfikisha kwake, na kuondoka, kuna
muda wanafika na kukaa humo kwa kipindi kirefu tu, kwa vile ni rafiki yako,
hatujaona kama kuna lolote baya, sizani kama wanaweza kuvuka mipaka, ulisema
wewe unamuamini kwahiyo hata sisi tumechukulia hivyo....’akasema
‘Kwa uchunguzi wako, hakuna dalili zozote za mahusiano ya
kimapenzi kati ya rafiki yangu, na mume wangu,..?’ nikauliza
‘Hatukiliona hilo…hawajawahi kulionyesha hilo hadharani…, maana
hata wakiwa kwenye starehe, walionekana wakijali, kuheshimiana, na mume wako
sio mtu wa kufanya mambo ya aibu anajichunga sana, kama alivyo rafiki yako,
hatukuweza kulibaini hilo…’akasema.
‘Na huyo rafiki yangu hakuwa na mahusiano na mdogo wa mume
wangu..?’ nikauliza
‘Kwa uchunguzi wetu, yaonekana rafiki yako hayupo karibu sana na
huyo shemeji yako, na yaonekana kama hawaelewani kina namna fulani, kwahiyo
haiwezekani wakawa wapenzi....’akasema
‘Haiwezekani, ina maana mume wangu hakuwa na rafiki mwingine wa
kike.....sasa huyo mtoto ninayesikia anaye ni kutoka kwa mwanamke gani?’
nikauliza
‘Mtoto…mmh, hapana, ..kwa uchunguzi wetu, ....hilo halikuweza
kuonekana, kwani kama ulivyotaka, ni kuwa tuchunguze bila kuweka tetesi, tuwe
na uhakika na hicho tulichokifanya, na sisi hatukuona au kugundua mwanamke mwenye
mahusiano na mume wako…’akasema
‘Na ni kweli mumegundua kuwa hana mtoto nje…?’ nikauliza
‘Hilo hatujaligundua, hatuwezi kusema kitu ambacho hatuna uhakika
nacho kama ulivyotaka..kama unataka tulifanyie kazi hilo, kuwa kama ana mtoto
nje, tunaweza kulifanyia uchunguzi, lakini kwa mipaka uliyotuwekea sisi
hatujagundua chochote kuhusu mtoto wa nje…’akasema
‘Sawa, ndivyo nilitaka,…sikutaka hayo myafanyie kazi, kama kesi,
hakuna kesi hapa ni kutaka kujirizisha tu,..ila kuna kitu nataka unifanyie,
nenda huko alipojifungulia huyo rafiki yangu uone kama utagundua baba wa huyo
mtoto wake, je alizaa na nani, unaweza kulifanyia kazi hilo…?’ nikamuuliza
‘Naweza bosi…’akasema
‘Unajua …awali sikutaka ulifanye hilo, sasa kalifanyie kazi, na
pili, utafute kama kweli mume wangu ana mtoto nje, mmh, yah, lakini usifanye
kuonyesha mimi nataka kulifahamu hilo, chukua muda, unanielewa…’nikasema
‘Sawa nakuelewa bosi, ila kuna kitu, nilitaka kukuambia,....ila
wewe ulisema tusihangaike sana na rafiki yako na ..na…’akasita kidogo
‘Niambie ni kitu gani…?’ nikauliza
‘Ulisema haina haja ya kumchunguza rafiki yako, na ulisema kuna
mwanaume aliwahi kufika hospitalini,..wa kwanza, kuna kitu kama hicho, ila
ulisema haina haja ya kulichunguza hilo, lakini kwa uchunguizi wetu mwanaume wa
kwanza kumtembea pale hospilaini alikuwa ni mume wako, hakuna mwingine …..’akasema.
‘Unasema kweli,…haiwezekani, mbona rafiki yangu alinificha hilo..,
na hata mume wangu, mmh..hapa kuna kitu,..una uhakika na hilo..!?’ nikauliza
kwa mshangao
‘Ndio…nina uhakika na hilo…’akasema na alitaka kuongea jambo,
lakini mimi nikamtiza kwa swali jingine
‘Je vyanzo vyenu viliwahi kumuona mtoto wa rafiki yangu, kisura,..anafananaje?’
akaulizwa
‘Ni kitu ambacho wengi wetu waliona ni ajabu, kwani mtoto huyo
amekuwa akifichwa sana, hajawahi kuonekana sura yake na mtu yoyote....’akasema
‘Haiwezekani, ina maana na ujanja wenu wote hamkuweza kuiona sura
ya huyo mtoto wake, hajawahi kupiga picha, ?’ nikawauliza
‘Unamfahamu sana rafiki yako huyo, kazi za uchunguzi, ulinzi na
usalama anazifahamu sana, na akiamua kufanya jambo, analifanya kwa makini sana,
nahisi hakupenda kabisa mtu kuiona sura ya mtoto wake…’akasema
‘Mhh..haiwezekani, kwahiyo nyie hamjafahamu yupo je…?’ nikamuuliza
‘Wengine wanasema ana sura ya kihindi, wengine ana sura ya
kizungu,…sasa hatujui kwakweli, nahisi basi atakuwa akimvalisha vitu ambavyo
huwezi kabisa kugundua sura ya mtoto ya asili, nahisi alikuwa akimvalisha
nywela za bandia hata sura za bandia....’akasema.
‘Sura ya kihindi, hahaha..hapana mimi nimemuona ni mwafrika
kabisa…’nikasema
‘Ndivyo watu waliobahatika kumuona wanadai hivyo…’akasema
‘Unahisi ni kwanini amefanya hivyo....?.’nikawauliza
‘Huenda hataki baba wa mtoto huyo ajulikane, au huyo baba amfahamu
huyo mtoto kuwa ni wake...’akasema
‘Kwanini?’ nikamuuliza
‘Huenda ni kuogopa kashifa...
Au yeye mwenyewe rafiki yako hataki baba wa mtoto huyo afahamu kuwa ni mtoto
wake....’akasema.
`Nashukuru, huenda nikakuhitajia tena, endelea na uchunguzi....’
*******
Baadaye alikuja mtu ambaye nilimpa kazi ya kuchunguza kifo cha
Makabrasha, yeye aliwahi kufanyia kazi za upelelezi, lakini kwasababu za kiafya
akaacha kazi, ..na hata alipopona hakutaka tena kuirudia hiyo kazi, akawa
anafanya kazi hiyo binafsi, na yeye akatoa taarifa yake.
‘Kifo cha Makabrasha, kimefunikwa kiaina, nahisi hata polisi
walishachoka na tabia ya huyo mtu, na waliona kufa kwake ni bora tu, japokuwa
walifanya juhudi ya kumtafuta muuaji, lakini hawakufika popote, wakahitimisha
walivyoona wao....’akasema
‘Kwanini unasema hivyo?’
‘Kwasababu ya matendo ya marehemu, kwani alifikia hatua ya
kuwawekea hata hao polisi mitego, akiwanasa kwenye mambo yanayoenda kinyume na maadili
ya kazi zao, anawarekodi, na huja kutumia kumbukumbu hizo kuwatishia, kuwa wakifanya
lolote na yeye atawalipua, kwahiyo hata wao, wakawa hawana jinsi, ila kufuata
anavyotaka yeye....unaona eeh..’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema nini?’ nikamuuliza
‘Ninachotaka kukuambia ni kuwa ukweli wa kifo cha Makabrasha
hautaweza kugundulikana kiraisi unaweza ukaweka shaka shaka kuwa huenda hata
hao watu wa usalama wanajua kitu fulani,lakini hawataki..kiukweli, haipo wazi,
na hata wao hawajachukulia kifo chake kwenye uzito wake...’akasema
‘Haiwezekani, ina maana watu wa usalama wanaweza kuhusika..hiyo
dhana unaiwekaje hapo…?’ nikauliza
‘Sijasema wanaweza kuhusika, ila wanaweza kujua jambo..unielewe
hapo..’akasema
‘Sasa ni nani anaweza kuhusika kwa uchunguzi wako, sizani kama
muuaji anaweza kupotea hivi hivi..?’ nikauliza
‘Huyo muuaji aliyefanya hayo mauaji, ni mtu ambaye alijua ni nini
anakifanya, na inaokena sio mauaji ya kukurupuka, ni mtu alijiandaa kwa muda
mrefu, huenda alikuwa kwenye hilo jengo, siku mbili kabla akimvizia..’akasema
‘Kwa vipi…?’ nikauliza
‘Ni lazima huyo mtu awe anafahamu taratibu zote za marehemu,
ratiba yake, na..anafahamu mfumo mnzima wa mawasiliani, na mfumo wa jengo na
ofisi ya Makabrasha...’akasema.
‘Mapka kufahamu mfumo, ina maana basi anaweza kuwa alihusika na
ujenzi wa hilop jengo au..?’ nikamuuliza
‘Anaweza asiwe ni mjenzi, badi ni mtu aliyelisoma hilo jengo…maana
ukisema ni mjenzi wa hlo jengo, huyo jamaa tunamfahamu, na kwa muda sasa wapo
mikoni kuna ujenzi wanafanya huko, lakini wanaweza kuuza siri za mjengo
huo,..huyo mtu aliyefanya hayo mauaji sio wa kawaida, ni mtaalamu kweli kweli.....kwani
kwa jinsi alivyoingia, na kwajinsi alivyoweza kusoma mfumo wa mawasiliano, na
mtandao uliokuwa umewekwa humo ndani,, ...sio mtu wa kawaida....’akasema
‘Haya niambie kutokana na uchunguzi wenu Makabrasha aliuwawa
kivipi, na kwanini?’ nikamuuliza
‘Huyo mtu inawezekana alikuwepo humo ndani kwa siku mbili kabla,
kama nilivyosema, na silaha aliyoitumia, itakuwa ililetwa usiku wake, na
ikaingizwa kwa kupitia nyuma ya ukuta....’akasema
‘Kwanini unasema hivyo..?’ nikauliza
‘Kwasababu kama ingelipitia kwenye njia ya kawaida, kupitia
mlangoni, ...kungelitokea milio ya kuashiria hivyo.....kuna mfumo mle ndani, wa
kugundua kuwa mtu kabeba kitu cha hatari, kuna mfumo wa kuchukua kumbukumbu za
matukio, ina maana kila anayeingia ataonekana,..lakini cha ajabu siku hiyo ya
tukio, hayo yote hayakuonekana kwenye mtandao uliowekwa humo ndani...’akasema.
‘Ili uingie kwenye jengo hilo kuna njia moja tu, na ukishaingia
kwenye jengo, ili upande juu, kuna njia moja tu, na huko kote waliweka vinasa
matukio na sauti,..hebu fikiri, kote huko hakukuonekana hilo tukio, kumefutwa
kabisa..ina maana huyo mtu hakutaka kabisa kuonekana chochote siku hiyo..
‘Na ina maana basi hata kama huyo mtu aliingia na silaha, ...labda
akamuhonga mlinzi, lakini angelipita wapi na hiyo silaha, kwasababu
mawasiliano ya kudhibiti hiyo hali ipo sehemu ya siri, huko juu, ...inawezekana
basi walinzi wawe wamekula njama,...’akasema
‘Si ndio hapo hata mimi nashindwa kuelewa na kwanini polis
wasimkamate hata Yule mlinzi, wangembana nahisi angeweza kuwafahamisha
jambo..’nikasema
‘Alikamatwa, lakini hawakuweza kupata chochote kutoka
kwake…’akasema
‘Pale mlangoni huwezi kuingia na silaha, pamoja na kukaguliwa na
mlindi lakini pia kuna mtambo,...mtu akipita silaha, kuna kelele za kuashiria
hatari, na hizo kelele, zingelijulikana kwa watu wote, pale huwezi kuingia na
silaha mle ndani kabisa,....’akasema.
‘Sasa hiyo silaha iliingiaje humo ndani…?’ nikauliza
‘Hiyo silaha itakuwa ilipitishwa nyuma ya jengo, na walichofanya
ni kutengeneza kamba ndefu, iliyoshuka hadi chini, na mtu aliyekuwa chini,
akaifunga ile silaha kwenye hiyo kamba, na huyo aliyekuwa juu, akavuta hadi
juu, na kuhakikisha, haipiti sehemu zenye kuhisi au kugundua kitu cha
hatari..na huenda kwa muda huo, huyo mtu alikuwa keshazima viwambo vya hatari
vya ndani....’akasema.
‘Mtu huyo asingeliweza kuzima viwambo hivyo kwa jengo zima,
walinzi wa chini wangeliona hilo, na wangeliweka kwenye taarifa zao, hakuna
taarifa kama hiyo, na hata tulipojaribu kufanya uchunguzi kwa watu hao,
haukukuwa na dalili zozote kama hizo siku hiyo...’akasema
‘Kwahiyo muuaji, atakuwa alikuwa ndani, na muda ulipofika,
akafanya kazi yake kirahisi, akaondoka..na cha ajabu basi hata tukio
lenyewe,hilo la mauaji halipo...polisi wanadai kuwa walioona baadhi ya sehemu
ya tukio hilo, lakini sio kweli..hakuna kitu kama hicho,...kuna mtu
aliyekuja kuondoa kila kitu...cha siku hiyo, na huyo mtu alifahamu ni nini
anakifanya , ...’akasema.
‘Kwahiyo hamkuweza kugundua lolote, kwa njia zenu, kuwa huenda mtu
fulani anaweza kuhusika?’ nikamuuliza.
‘Huyo aliyefanya hivyo ni mtaalamu, kweli..hatukuweza, na kwa vile
polisi wenyewe wamesalimu amri na kuona kuwa ni kifo cha kulipiza kisasi, mimi
naona haina haja ya kuhangaika sana..ila kuna kitu ninachoshangaaa,...’akasema
‘Kitu gani....?’ nikauliza
‘Siku ile ya tukio, kuna watu wanasema kuna mtu, japokuwa
alijibadili, lakini anafanana na mume wako kimaumbile’akasema
‘Unataka kusema nini hapo?’ nikamuuliza
‘Mume wako alikuwepo kwenye hilo jengo, wakati tukio hilo
linafanyika, na polisi hawakuligundua hilo, ..kama wangeligundua hilo, nina
imani kuwa mume wako angelikuwa hatarini, wangemshika....mimi nilijaribu
kufanya uchunguzi wangu, na hata kuongea na mume wako, lakini hakutaka kutoa
ushirikiano...je kuna njia yoyote naweza kuongea naye,...?’ akaniuliza.
‘Hapana, haina haja, inatosha....’nikasema.
‘Lakini nina uhakika sio yeye aliyefanya hayo mauaji, ila nahisi
atakuwa anamfahamu huyo muuaji....’akasema
‘Kwanini unasema hivyo?’ nikamuuliza
‘Mume wako sio mtaalamu sana wa kutumia silaha, huyo muuaji,
anafahamu kutumia silaha, na alifahamu wapi pa kulenga, ...ni mtaalamu kweli
kweli, na alijua akilenga wapi mtu haponi....na kwahiyo huyo mtu atakuwa
kapitia jeshi au kitu kama hicho, sio raia wa kaiwada tu..ni mtu anayefahamu ni
nini anakifanya.’akasema
‘Nashukuru kwa taarifa yako....’ nilisema hivyo, na sikutaka kujua
zaidi,…na hasa niliposikia kuwa mume wangu keshagundulikana kuwa alikuwepo humo
kwenye jengo, na ina maana hata polisi watakuwa wameshagundua, sasa ni kwanini
hajamkamata…
Nilihitajia muda wa kuliwazia hilo, na huyo jamaa akawa anataka
kuondoka, halafu akasema;
‘Yule mdada, rafiki yako…unamuamini sana…?’ akauliza
‘Kwanini…?’ nikauliza
‘Nakuuliz tu…kuna kitu nimekigundua, nitakuja kukuambia, lakini
kwa hivi sasa bado sijamuelewa, ndio ni mtu wako wa karibu, lakini…kuna kitu
simuelewi..mbona walikuwa karibu sana na marehemu…’akasema
‘Kwa vipi…?’ nikamuuliza
‘Kuna matukio mbali mbali wameonakana wakiwa pamoja, wanaongea, na
mara nyingi, rafiki yako anakuwa hayupo wazi kuonekana, ina maana wanaongea kwa
siri, na hataki watu wafahamu kuwa anawasiliana na huyo marehemu…’akasema
‘Kwani siku hiyo ya tukio walionekana na marehemu…?’ nikauliza
‘Ndio..lakini kwa njia hiyo hiyo…’akasema
‘Unahisi yeye anaweza kuwa muuaji…?’ nikauliza
‘Sijasema hivyo, na wala haijagundulikana hivyo,…na hawezi kufanya
kosa hilo.. lakini ngoja nilifanyie kazi, nipe muda,…’akasema
‘Nauliza hivi, kwa hisia zako mpaka hapo anaweza akawa ndiye
muuaji..?’ nikauliza na huyo jamaa akaanza kuondoka, baada ya kutikisa kichwa
tu,.. hakusema neno.
WAZO LA LEO: Dhana mbaya, au tetesi zisizo kuwa na uhakika, zaweza kukushinikiza kufanya
jambo lisilo faa, tuweni makini sana na dhana, au mambo ya kusikia, hasa atika dunia hii ya utandawazi, ukisikia jambo, au kusoma jambo, lihakiki kwanza ukweli wake, kabla hujasema neno, au kabla hujaamini ukweli wake,
fanya uchunguzi kwanza, ili kujiaminisha, usikimbilie kushutumu au kutoa kauli zenye kuumiza, kulaani au kuhukumu watu wengine.
Tukumbukeni ulimi na kalamu(mitandao) inaweza kuwa ni chanzo cha fitina mbaya kwa jamii, tuweni makini sana kwa hili, siku ya hukumu kila kitu tutaulizwa, na kwanini tuwe sababu ya kuumiza wengine,..maandishi tu yaweza kuua, yanaweza kutesa nafasi ya mtu na huwezi kujua ni namna gani mtu huyo ataumia, mauimvu thamani yake ni kubwa sana, utawezaje kuilipa hiyo.
Tumuombe mola wetu atusamehe na atupe hekima ya kuandika membo yenye maana kwa jamii..!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment