Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, January 4, 2018

MKUKI KWA NGURUWE-50



‘Nimekuelewa sana dada yangu, nakushukuru kwa ushauri wako,...lakini. eeh…’nikasita maana niliona kama gari linaingia getini, halafu nikasema

‘Hayo ya mume wangu,..najua mnampenda na kumthamini sana, lakini nawaombeni hayo mniachie mimi mwenyewe…’nikasema na sasa geti likawa linafunguliwa, lilikuwa gari la mume wangu.

‘Oh wamerudi na kunikuta tena hapa, mimi naondoka…’akasema

‘Kwanini haraka hivyo…hatujamalizana …’nikasema

Na kabla hajajibu mume wangu akateremka kwenye gari, na wakili wake,…na walipoteremka, badala ya kuelekea ndani, wakawa wanakuja pale tulipokuwa tumekaa, na ikabidi tukatizie mazungumzo yetu.

Tuendelee na kisa chetu.....

‘Aheri bado mpo..nahisi hili litatufurahisha sote,…maana shemeji yangu upo, na…na mke wangu ..unajua leo kutwa nzima tumekuwa tukilihangaikia hili,…kutafuta haki, ..na haki haiji hivi hivi wakati mwingine au sio..’akasema mume wangu na kumuangalia wakili wake ambaye alitikisa kichwa kukubaliana na yeye.

‘Sasa hivi tumetokea polisi, kumuona Yule mpelelezi anyeshughulikia hii kesi yako ..mke wangu mambo sasa yanakwenda vizuri tu..imebakia maswala machache,..si unajua tena nchi yeu ilivyo…’akasema na kumuangalia wakili wake.

‘Kwanini…maana haya yapo mikononi mwao, na tulikubaliana kuwa hakuna haja ya kuwafuatilia, tuwaachie wao wafanye kazi yao…’nikasema

‘Ndio hivyo mke wangu, lakini ni wajibu wangu, eeh, na wakili hapa kulifuatilia hilo, kuhakikisha kuwa, mke wangu upo na amani, haiwezekani watu wakushuku tu, haiwezekani mtu auwawe tu, na sisi tubakie kimia, ni kwanini …eeh, Yule alikuwa ni rafiki yangu mkubwa..hapana mimi sitakubali kukaa kimia mpaka haki ipatikane…’akasema

‘Ok, kwahiyo…?’ nikauliza, na sasa wakili ndiye akaanza kuongea.

‘Kifupi ni kuwa polisi wanasema bado wanalifanyia kazi, lakini kwa kuhusu wewe kama mshukiwa muhimu, halipo tena,…’akasema

‘Kabisa…kazi nzuri ya wakili wetu…’akasema mume wangu.

‘Lakini hata hivyo kabrasha la kesi halijafungwa, si unajua tena mambo ya kisheria, kuna taratibu zinatakiwa kufutwa, ..na hilo ndilo tulikuwa tunalifuatilia, ili kuhakikisha kuwa gabrasha hilo limefungwa..na wewe utakuwa huru kabisa…’akasema

‘Lakini mimi nina wakili wangu analifanyia kazi hilo…’nikasema

‘Haina shida, yeye afanye kivyake na sisi kivyetu,..lengo letu ni moja, na mwisho wa siku tutakaa pamoja…na kuona kila mmoja kafikia wapi, muhimu ni kuhakikisha kuwa kesi hii haipo tena, ..lakini wkati huo huo, haki imetendeka, na muuaji kapatikana…maana aliyefariki ni jamaa yetu..’akasema wakili.

‘Sawa nashukuru …’nikasema

‘Sasa tatizo mke wangu, kila kitu ni gharama au sio..na unajua hali niliyo nayo, nakwama kabisa, nilikuwa naomba…tukaongee ndani, unipitishie hundi yangu..’akasema

‘Hundi ya malipo gani…?’ nikauliza

‘Ya wakili, na kufuatilia..na mambo mengine ya kikazi..ni pesa nyingi kidogo, na sitaweza kupitisha hundi hiyo kwa sahihi yangu tu..’akasema

‘Naomba hilo tutaliongea baadae..’nikasema

‘Ni muhimu na haraka kuna mambo mengine nayafuatilia,…’akasema

‘Mume wangu tulishaliongea hilo, mimi siwezi kuweka sahihi yangu …kwa kazi yoyote ya ushirika, hasa za makampuni, mpaja swala langu litatuliwe, hilo lipo wazi, kwahiyo kama ni hundi ya namna hayo, samahani sana…’nikasema

‘Mke wangu hili ni la muhimu sana, tunataka tumalizane na kesi yako,..na haki ya marehemu ipatikane,..ina maana wewe huna uchungu na hilo..na hata kama huna uchungu na hilo,na je wewe hutaki uwe huru…?’ akauliza

‘Nitaongea na wakili wangu…’nikasema sasa nikisimama kutaka kupiga simu kwa wakili wangu.

‘Wakili wao wa nini sasa haya ni yetu, hayamuhusu…’akasema

‘Wakili wangu ndiye anasimamia kesi ya mkataba..kila jambo kama ni muhimu yeye ndiye anatakiwa atoe maamuzi ya kisheria, siwezi kulikwepa hilo…’nikasema na wakili wangu akawa hewani.

‘Vipi umefanya kama nilivyokuambia…?’ akatangulia kuniuliza

‘Kabisa…lakini kuna tatizo hapa, mume wangu kaleta hundi ya ushirika anasema anataka niweke sahihi yangu..nishauri…’nikasema na kumsikiliza kwa makini halafu nilipomaliza kuongea naye, nikasema;

‘Kama nilivyosema kila kitu kinachohusu mkataba wangu wa zamani kitapitia kwa wakili wangu,kwahiyo kama ni ya haraka usubiria anakuja…’nikasema na hapo mume wangu akamgeuikia mwenzake na kusema

‘Twende zetu…’akamshika mkono na wakaanza kuondoka.

‘Vipi tena…?’ nikauliza lakini hawakunijibu kitu haoo, wakaingia kwenye gari na kuondoka zao.

*********

 Yule mama akawa kimia, nahisi alijifunza jambo hapo, akasimama sasa akitaka kuondoka.

‘Mimi naondoka maana kijana wangu ana mambo mengi ya kufuatilia…’akasema

‘Umeona mwenyewe mambo yalivyo..’nikasema

‘Lakini yatakwisha tu, ila nahisi mume wako ana jambo…ila anaogopa kukuambia, hebu nikuulize ni nini kikubwa kwenye huo mkataba wenu ..ambacho unahisi kakivunja,…?’ akaniuliza

‘Siwezi kusema lolote kwa hivi sasa, ..’nikasema na hapo akakaa tena kwenye kiti na kwa sauti ya chini akaniliza

‘Nilikuuliza kitu, je mume wako akiamua kukuambia ukweli, utamsamehe?’ akauliza sasa akiangalia saa yake ya mkononi.

‘Hapo mimi sijui, ..kiukweli kachelewa sana kuwa mkweli na zaidi anazidi kuharibu, na kwahiyo kama ataamua kufany ahivyo, najua kabisa itakuwa ni kutokana na kushawishiwa, au kwa vile kaona kakwama…’nikasema

 ‘Nimekuelewa sana dada, ila nauliza hivyo maana ndoa ni mashikamano ya mume na mke, na kila mmoja anawajibika kuitii ndoa yake, lakini ni lazima mfike sehemu myamalize au sio…’akasema.

‘Ni kweli yataisha tu, lakini kuisha kwake ni baada y akuupata huo mkataba wa zamani, tukae tuona unaemaje, na yeye akiri makosa yake, ..mengine yatafuta baada ya hapo…

‘Nakuelewa sana mdogo wangu,...unajua kuna makosa madogo madogo tunayoyafanya sisi wanandoa hasa wa kike, tunaona ni sahihi au ni madogo tu, kwa namna yetu, kumbe kwa wenzetu ni tatizo kwao, na wao kwa uwezo wao wanaweza kufanya jambo, na matokea yake kuna leta matatizo, na ushukuru wewe una uwezo wako…’akasimama sasa akitaka kuondoka

‘Nafahamu hilo,najua hata mimi nina makosa yangu, lakini sio ya kuvunja mkataba ..maana ni mambo ya kuelezana, kama nilikosea, angeniambia,..usitetee hilo…sawa tulikuwa tunahangaika na majukumu ya kazi, na mambo mengine yakawa kama hayana msingi, lakini je hayo ndio yafanye mtu aka…hapana…’nikasema. ‘Ndio awali nikakuambia kuwa sisi wanawake tuna dhima ya kuwalea wanaume wakati mwingine kama watoto wetu,…sina nia mbaya hapa…’akatulia kama anawaza jambo.

‘Mfano nikuulize hivi ukiwa unamlisha mtoto wako vyema, akanisha vyema anaweza kwenda kuomba chakula kwa jirani…?’ akaniuliza

‘Una maana gani…?’ nikamuuliza

‘Nijibu tu…’akasema

‘Hawezi…’nikasema

‘Basi ndio hivyo, wakati mwingine tunaweza kuwanyima watoto wetu, eeh, unanielewa hapo, chakula,..haki yake, ikafikia akazidiwa, sasa akienda kuom,ba chakula kwa jirani, utamlaumu nani…hahaha…’akasema na kucheka.

‘Sijawahi kufanya hivyo…labda …hapana, unajua hayo ni maswala ya kuambiana, kwani mimi si mke wake, kwanini aogope kuniambia…ana njaa…’nikasema

‘Haahaha..tuyaache hayo..ila yakitokea haya ndio tunapata fundisho, mimi nitashukuru sana mkilimaliza hili kwa amani, na sitafurahi kama mtaishia kubaya, haya juhudi yetu itakuwa haina maana…’akasema

'Msimamo wangu upo wazi, …sifanyi kwa nia mbaya, lakini ikifikia huko, nitafanyaje, je kama ndio imeanza hivyo, huko mbele itakuwaje, sasa hivi kaanza kuandikisha watoto wa nje, je mama wa hao watoto ana dhamira gani,…ni lazima niwe makini hapo…’nikasema

‘Ninachoweza kusema kwa msameheane, wewe ulivyo,....hutapoteza kitu hapo au sio, bado una nafasi ya kuendelea na ..na kampuni yako,…nasema hivyo sio kwavile na mtetea shemeji yangu, hapana…’akasema

‘Mhh…unajishuku dada…’nikasema

‘Pamoja na hayo, mimi namfahamu sehemu nyingina ya tabia yake…kila mtu ana hulka lakini kuna hulka hujificha,..yeye ni mwanaume mwema sana, akimpta mtu wa kumjua alivyo, ana huruma sana kwa watu, japokuwa katokea kizazi cha tabia hizo zisizopendeza watu, na mengine ni shida tu..watu hawajapenda wawe hivyo.....’akasema.

‘Nimekuelewa….ngoja tuone ..’nikasema

‘Sasa mimi naondoka tuonane lini sasa…nafahamu kuna maswala hayo ya mawakili, wanafanya kazi zao, naona wanakipizana huku na kule,.. hata hivyo ni lazima maisha yaendelee, naopmba tuje tukae tuongee tuone maisha yanakwendaje, …haya yanayotokea sasa yasitufanye kusimamisha mambo mengine, naomba nije tusaidiane mawazo ya maendeleo…’akasema

‘Sawa kwa hilo tu, hamna shida kabisa, tupo pamoja…’nikasema

‘Na kwa hili je…?’ akauliza sasa akinyosha mkono wa kuagana.

‘Hahaha, dada hujanielewa mpaka hapo…niakuambie kitu, baada ya wiki mimi nitawapatia jibu langu,…kuhusu hili…kwa hivi sasa niacheni nipambane na mume wangu.....’nikasema na kikunja uso wangu kuashiria dhamira ya kweli.

‘Mhh, baada ya wiki sio sawa, basi ngoja waupitie huko mkataba waone wafanyeje, hayo ni mambo ya kisheria, au sio…?’ akauliza

‘Huo mkataba wa kugushi, ..au?’ nikasema kama nauliza

‘Mhh..mimi sijui sasa…naona kwa hili litaleta utata…na hapo ndio tunazidi kuchelewa,…namuonea huruma sana kijana wangu…kwani na yeye anachelewa kuondoka, lakini hawezi kuondoka kabla hili tatizo halijaisha, ya mungu mengi...’akasema.

‘Ninachoweza kukuambia dada, huo mkataba kwangu ni batili, na kama mtaendelea kuutumia basi msije kunilaumu, itabidi mimi niende mbele ya sheria, ili haki itendeke…sasa kwa ushauri wangu wa haraka,  msubirie  baada ya wiki, au hata kabla ya hapo,  kama mume wangu atakuwa tayari kutimiza masharti yangu, nitawaambia, ni nini cha kufanya..’nikasema

‘Sawa nimekuelewa, nashukuru sana,..’sasa akataka kuondoka na ghafla akasimama.

‘Mungu wangu sijui kama mliongea na kijana wangu..kuna jambo limezuka…’akasema sasa akarudi kukaa..

‘Samahani kidogo, ni muhimu kwa kweli…’akasema

‘Jambo gani tena…?’ nikauliza

‘Unajua huku kuzaa ovyo ovyo nje ..mitihani yake ndio hiyo,,..juzi,..kuna msaidizi wa kijana wangu. Msaidizi katika mambo hayo ya mirathi,… Unajua marehemu kila kitu alikiacha kwenye maandishi, utafikiri alijua atakufa…ndio hivyo, usomi nao unasaidia, au sio…si ndio hivyo hata nyie mnakuwa na mikataba ya ndoa nk..kusoma huko…’akasema

‘Mhh..kuna tatizi gani ..?’ nikauliza

‘Huyo msaidizi wake sasa..ni mtoto wa marehemu mwingine, alizaa na mwanamke mwingine..na katika maelezo yake kwenye hayo maandishi aliyoacha,..alitaka huyo kijana atambulikane na awe msaidizi wa kijana wangu, kila kitu kwenye maandishi tena ya kisheria..unaona hapo..’akasema.

‘Sasa huyu msaidizi wake,…ni tatizo, yeye ni mtoto kama baba, unanielewa hapo…’akaniangalia

‘Bado sijakuelewa…’nikasema

‘Ni hivi huyo kijana kamlanda baba yake sio kimatendo tu, bali pia na yeye aliamua kusomea sheria..na ni wakili pia…’akasema

‘Mhh..kwahiyo…’nikasema

‘Na hata tabia za kazi ni kama alivyo baba yake, utafikiri alimfunza hiyo tabia, si unamuelewa marehemu alivyokuwa, basi mtoto ndio zaidi, na kiumri hajapitana sana na kijana wangu…’akasema

‘Sawa kwani kuna tatizo gani hapo, sioni tatizo maana sina jambo na yeye, hayo ni yenu ya kifamilia au sio, au unataka kusema nini hapo…’nikasema

‘Mengi yaliyopitishwa kwenye kikao cha kifamilia yeye alikuwa mpingaji sana, yeye alitaka kila kitu alichosema marehemu kitekelezwe hasa kikiwa kwenye maandishi, mkataba…, unajua nilimuambia kijana wangu mapema awe tayari kwa hili, kwahiyo mambo mengine asiyaweke wazi…’akasema

‘Kwanini sasa na ni haki ya kila mtu au sio, haikuwa na haja y akuficha jambo…’nikasema

‘Wewe ni mungu tu alituongoza, maana huo mkataba wa kuelezea kuwa kuna ..hizo kwenye makampuni yenu, haukuwahi kwenye hicho kikao, kijana wangu alikuja kupewa baadae na kwahiyo hilo halikuzungumzwa siku hiyo..siku hiyo ilikuwa ni madeni, na watoto hao wa nje waliposikia madeni ni mengi kuliko mali za kurithi, wakaondoka mmoja mmoja, maana kijana wangu aliwaambia kila mtu akubali kushika sehemu yake ya deni,…nani akubali hapo, hata huyo msaidizi wake akaondoka akidai ana kesi anafuatilia...’akasema

‘Kwahiyo…unataka kusema kuwa huo mkataba wa kugushi bado haujafika kwa warithi, kama huyo ..na wengineo ..ni vizuri, lakini mimi siutambui…’nikasema

‘Sasa huo mkataba halali upo wapi mdogo wangu…’akawa kama anauliza

‘Utapatikana tu dada….mume wangu atakuwa anafahamu upo wapi…’nikasema

‘Tatizo ni muda..mana sijui kajuaje …huyo mtoto, katupigia simu akidao kuwa tumemficha ukweli…sasa ni hivi kutokana na muda, kama kijana wangu akiondoka, kurudi ulaya kabla hatujamalizana na hilo, mtakuja kupambana na huyo mtoto, ni mkorofi kweli kweli, nina uhakika …hamtaelewana naye, ndio maana tunataka mambo haya yaishe haraka, iwezekanavyo, wewe kaa na mume wako myamalize haya mambo kwa haraka jamani, …’akasema

‘Kuisha haraka ni mume wangu…nimeshakuambia hilo, yeye ndiye anachelewesha haya mambo, kama nyie mnaweza kumshauri fanyeni hivyo, alete mkataba wa zamani, umenielewa hapo dada…’nikasema

‘Nilivyosikia, huu mkataba uliopo sasa nakala zipo kila mahali panahusika, sasa sio rahisi mtu kukubaliana na kauli yako, sijui unanielewa hapo…’akasema

‘Usijali, hilo litafanyiwa kazi..hamna shida …’nikasema

‘Mimi sitaki kubishana kwa hilo, ila ninachotaka kukisema hapa ni hivi…unajua huyo kijana ni mtata kwa sheria,…anapenda sana kesi, nina uhakika atawasumbua sana kwa hilo, na kama siku ile huo mkataba ungelifika mikono mwake, sijui uingekuwaje...’akatulia

‘Dada…’nikataka kusema na yeye akanikatisha, akisema;

‘Sisi kuwa kusaidia hilo, tumesema hatujui, hatuna uhakika, tutalifuatilia tukiupata basi tutamjulisha, lakini hakukubali, kasema huo mkataba tunaufahamu tumemficha…...ndio maana tunataka tulimalize hili haraka…’akasema

‘Kwahiyo mlitaka mimi nifanye nini..?’ nikauliza

‘Sisi lengo letu ni kuhakikisha kuwa huo mkataba unafanyiwa kazi, na kuondolewa kabisa,..mimi kwa ushauri wangu, kubali tu huo mkataba uliopo halafu tunaongea na wakili sisi kama familia tunajitoa, nyie sasa mtajua mnafanyaje na mume wako,..ni ushauri wangu huo…’akasema.

‘Msiwe na shaka na mimi, mimi simuogopi yoyote, ilimradi nipo kwenye haki yangu, wanachotaka kupata sio haki yao, au sio.....kama kweli huyo wakili na anaifahamu sheria, tutaangalia ukweli upo wapi na haki itatendeka, lakini kama ndio hawo wenye tamaa..basi tutapambana hadi mahakamani, hilo usijali kabisa…’nikasema.

‘Lakini muda sasa, na gharama…kijana wangu anaondoka hivyo, lifikirie hilo kwa makini..’akasema.

‘Sawa nimekuelewa...’nikasema na mara simu yangu ikalia, nilipoangalia nikaona ni namba ngeni kwenye simu yangu,, ...sikutaka kuongea na mtu nisiyemfahamu kwa muda huo...tukaagana na mgeni wangu huo, huku simu inaendelea kulia, baada ikakatika, ..baadae kidogo ikaita tena…, nikapokea na kuuliza

‘Nani mwenzangu...?’ nikauliza

‘Mimi ni mtoto wa marehemu Makabrasha....’akasema

‘Yupo huyo..na unasemaje?’ nikuliza

‘Nimesikia tetesi kuwa kuna mkataba unaoonyesha kuwa marehem alikuwa na hisa kwenye kampuni zako, ni kweli si kweli…?’ akauliza

‘Mimi sijui hilo, ni nani kakuambia..?’ nikauliza

‘Wewe si mmoja wa wakurugenzi, kwanini hujui, na ni haki yetu kaam warithi kulifahamu, je ni kweli au si kweli…?’ akauliza

‘Nimeshakuambia mimi sijui…je ndio taratibu za mirathi zipo hivyo, wewe kuuliza hivyo tu kwenye simu,..unajua sheria wewe..?’ nikauliza

‘Naifahamu sana, mimi ni wakili, nimekuuliza hivyo, kwasababu kuna hali inayoendelea kwa kiongozi wetu wa familia, analifahamu hilo na alilificha, sasa natafuta ukweli, ili sheria ichukue mkondo wake…’akasema

‘Kwa kifupi, fuata sheria, ongea na kiongozi wenu, na ikibidi ongeeni na wakili wetu, unanielewa,…’nikasema

‘Nasema hivi kama marehemu alikuwa na hisa kwenye kampuni zako, inatakiwa utuambie, utupe memorandum, na vielelezo vyote vinavyostahiki, ili tuweze kuorodhesha kwenye madai yetu, ndio maana nikakuuliza ili kuupata huo ukweli..’akasema

‘Na mimi ndio nimekupatia hilo jibu…’nikasema

‘Sawa mimi nitafuatilia kuupata huo ukweli, na kama kuna njama zozote za kuuficha ukweli, basi, sitasita kwenda mbele ya sheria…’akasema

‘Na samahani nikuulize tu, ni nani kakuambia mambo hayo?’ nikamuuliza

‘Nimesikia tetesi, hata kwenye kikao walisema kuna mikataba mingine haijapatikana, wanaifuatilia…., niliwaambia mimi ni wakili wanipe mimi nifanye ufuatiliaji wakachelea kunipatia, sema siku ile nilikuwa na kesi nyingine ya haraka siweza kusubiria.., lakini sasa nipo na nafasi, nataka kuuona huo mkataba...’akasema

‘Unasema ulisikia tetesi,..na unadai wewe ni wakili, unajua mambo hayo ya kisheria yanafuatiliwaje au sio..au wewe tetesi tu kwako ni sababu, je ukisikia tetesi kuwa wewe sio mtoto halali wa marehemu utasemaje…?’ nikamuuliza.

‘Unasema nini?’ akauliza kwa hamaki

‘Kuna tetesi kuwa wewe sio mtoto halali wa marehemu, wewe ni mtoto wa kusingiziwa, je unazikubali hizo tetesi?’ nikamuuliza.

‘Sikiliza mimi nakuuliza mambo ya muhimu wewe unaleta mzaha, sikiliza mimi nafahamu sana sheria, kama ni kweli, huo mkataba una haki zetu, nakuhakikishia mimi nitafika hadi mahakamani…sasa kwa vile umejibu ki-huni, nakupatia wiki moja tu, hilo liwe wazi, na ...hizo tetesi zako, hawo waliokuambia waambie, hawana akili kwanini hawakusema hivyo wakati marehemu yupo hai...’akasema.

‘Nilikuwa nataka kukuonyesha kuwa tetesi  sio ukweli wa mambo, kama ulisikia tetesi kuwa kuna mkataba kama huo wa halali wa hivyo unavyosema, ilibidi ufuatilie kwanza sehemu husika..na ni vyema ukamuona wakili wenu, kwani si mna wakili anayefuatilia mambo yenu ya kifamilia..’nikamwambia.

‘Mimi mwenyewe ni wakili, ndiye nimeteuliwa katima mambo ya kisheria, lakini siku ile walinificha hilo jambo, sasa nimeanza kulifuatilia mpaka nione mwisho wake...’akasema

‘Sawa, kama unaona ni haki yako fuatilia, ...ila ni vyema ukawa  na uhakika na hicho unachokidai,..sawa muheshimiwa..’nikamwambia.

‘Sawa …ila nitegemee kukuona, siku yoyote naweza kuja kuongea na wewe kaika kulifuatilia hilo, nataka nionane na wewe uso kwa uso,….jiandae kwa hilo….’akasema na kukata simu.

NB: Tuhitimishe? sehemu hii ilihitajia marekebisho mengi..lkn hatukupata muda,....


WAZO LEO:Kunapotokea mzazi mmoja kufariki hasa wa kiume, kuna watu wanajitokeza kudai, mali wakisema na wao wana haki ya urithi, watu hawa wakati wa uhai wa merehemu, walikuwa hawaonekani, na zaidi inawezekana kabisa marehemu alikuwa akiumwa kwa muda mrefu, lakini hawakuwahi kufika, angalau hata kusaidia kidogo, hata angalau kutoa pole, mpaka mzazi huyo nafariki.

Watu kama hao huja kujitokeza baadae wakati wa mirathi. Je huo urithi, umetokea wapi, ukumbuke hiyo mali ilitafutwa na watu, na ni hawo hao waliohangaika na marehemu, wenye uchungu naye…, wewe unakuja baadaye unadai, mali, hiyo mali kwako itakuwa sio halali ...ni vyema tukajua kuwa, kila penya faida kuna gharama zake pia.

Ni mimi: emu-three

No comments :