Mhh, kweli umenifungua masikio, hayo
yaliyokukuta ni makubwa, mimi niliona nipo kwenye mitihani, lakini wewe ilikuwa
zaidi, sasa ikawaje?’ nikamuuliza.nikitaka kufahamu mengi kuhusu maisha ya huyo
mama, ambaye nilimuita dada...
Aliendelea kunisimulia maisha yake na mume wake ambaye sasa
ni marehemu...
*******
`Mimi sikukata tamaa na mume wangu, niliendelea kumsubiria,
nilimuomba mungu, kuwa ipo siku,atajirudi, na kunikumbuka , lakini haikiutokea,
mimi nikaendele kuishi kijijini, nikijitegemea, na hata ikafikia wazee wao
wenyewe wakaamua kuliingilia kati. Ikabidi mume wangu aitwe kwenye kikao cha
wazee, na yeye mbele yako akaja kukubalia kuwa kakosea, na akakubali kuwa mimi
ni mke wake wa halali, na yeye anawajibika kwa hilo.
‘Sasa kwanini unamfanyia hivyo mwenzako?’ akaulizwa
‘Nilipitiwa tu na mihangaiko ya kutafuta riziki’akasema.
‘Hizo riziki unamtafutia nani sasa?’ akaulizwa
‘Mimi na familia yangu..’akasema
‘Mbona hukimbuki familia yako, au familia yako ni akina
nani?’akaulizwa
‘Ni mke na watoto wangu, lakini pesa haitoshi...mambo ni mengi
sana huko mjini, kuna kodi za nyumba kuna gharaam nyingi tu, lakini najitahidi
au sio ...’akajitetea
‘Sasa unasemaje, ?’ wakamuuliza
‘Wazee wangu, mimi najitahidi na kiukweli nimeanza kujiweka
sawa, kwani nina ndoto ya kusoma sana, na kuwa wakili…kwahiyo mambo yatakuwa
sawa na nina uhakika familia yangu nitaihudumia vyema…’akasema
Kiukweli hata mimi kwenye kikao hicho niliona kama mume
wangu kabadilika, sikusikia kauli zake zile..sijui kwa vile ni wazee, au ..lakini
moyoni nikaamini kuwa huenda kweli mume wangu kabadilika
Ikafikia muda akaniomba msamaha mbele ya wazazi kuwa kakosa
na hatarudia tena, uone wanaume walivyo…, lakini aliporudi mjini hali ikawa ile
ile...hata wazee hawakuamini kuwa ndio Yule mtu aliyekiri na kuomba
msamaha..basi ikabidi tukachoka, tukaamua kumuacha aendelee na maisha yake, na
mimi nikajibadili sasa ..maana mitihani ni shule…ndio mwanzo wa kuanza
kujiajiri...
Bahati nzuri, walikuja wawekezaji wanasaidi wanawake
waliokatiza masomo kwa uja uzito na mimi nikajiandikisha, ufadhili ukanisaidia
nikaanza kusoma, masomo ya watu wazima sasa, japokuwa mimi bado nilikuwa sio
mkubwa kihivyo,.. nikafanya mtihani wa darasa la saba nikafaulu kwenda
Nikaanza elimu ya sekondari ya miaka miwili…nilikuwa na
akili darasani kwahiyo niliweza kufaulu vyema…hadi nikafika elimu ya juu,...hutaamini,
nilifaulu kwa njia hiyo nikasomea…diploma, nikaishia hapo...nikaanza mapambano
ya kujiajiri…nilikuwa nasoma huku nafanya vibiashara…nalea..hivyo hivyo..
‘Ukiniona hivi huwezi amini, lakini nia na lengo langu
ilikuwa kufika chuo kikuu, watu hawajui, hata huyo mume wangu alikuwa
hajui..hamna aliyemwambia,maana haulizi hana habari na mimi, ..ni kama hana
mke, ..mimi niliamua na nikafanikiwa, lakini sikuwahi kumkataa kuwa yeye sio
mume wangu.
‘Alishangaa siku moja nipo Dar, nahutubia akina mama mpango
wa kuwezeshana akina mama, waliokatisha masomo kwa ajili ya uja uzito, sijui
ilitokeaje na yeye siku hiyo alikuwepo kwenye huo mkutano, nilipomaliza
kuhutubia akanifuata na kuniuliza
‘Wewe mwanamke, umewezaje kufikia hatua hiyo, na kwanini
unasimulia maisha yangu mimi na wewe…, ina maana mimi nilikutesa kiasi
hicho…kwani nilikulazimisha, unakumbuka, nilikuambia sikutaka kukuoa, ni wazazi
wako walinilazimisha, unakumbuka, sasa unakuja kunilaumu mbele ya vikao kama
hivi, ujinga mtupu…akanilaumu sana…?’ akaniuliza na mimi nikamjibu
‘Ni kutokana na hayo uliyonitendea, hata hivyo mimi nashukuru
sana...’nikamwambia, na ghafla huyo …akaniomba msamaha, mimi nikamwambia mimi
sina kinyongo na yeye na bado mimi ni mke wake, lakini siwezi kwenda kwake,
maana bado nipo kwenye hiyo adhabu aliyonipa...
Kuna kipindi aliniambia amenipa adhabu, ya yeye kulazimisha
kunio mimi wakati alikuwa hanipendi, ...na ndio maana nikamwambia hivyo, kuwa mimi
bado nipo kwenye adhabu yake...nikaondoka kesho yake, kiukweli mimi sikufika
nyumbani kwake, japokuwa aliniomba nifanye hivyo,.. nilimwambia naogopa yasije
yakanikuta yale yaliyonikuta kipindi cha nyuma.
Basi kuanzia siku hiyo, sasa ikawa yeye anakuja huko
nyumbani kijijini, na akafika kwa wazee wangu, akawaomba msamaha,…na mimi pia, na mimi niliendelea kumwambia kuwa mimi ni mke
wake, asiwe na wasiwasi, sina kinyongo na yeye, lakini bado nipo kwenye adhabu
yake...
‘Ina maana alipokuwa akifika, alikuwa anakuja kwako, au
kwao…kwani wewe ulikuwa unaishi wapi hadi muda huo , ?’ nikamuuliza
‘Alikuwa anakuja kwao, mimi nilikuwa naishi na babu na
bibi, ...kwa wazazi wake, au nyumbani kwao, sikuweza kuishi nao, kulikuwa na
manyanyaso, ikabidi niwe naishi na wazee wangu hao, na walikuwa wakinihitajia
sana…ilikubalika iwe hivyuo, sio kwa kulazimisha…’akasema
‘Sasa alipokuwa kija kama hivyo, mimi sikumkubalia kuja
kulala kwangu, nikimwanbia bado nipo kwenye adhabu aliyonipa...hali hiyo
ilimtesa sana,...akahangaika, sijui kwanini aliamua kufanya hivyo...kiukweli
mimi sikugeuka nyuma,...’akasema.
‘Vipi mtoto…alikuwa akiishi wapi..?’ nikamuuliza
‘Mtoto naye akawa anakuwa akawa an juhudi sana darasani…akafaulu
hadi sekondari, na hatukutaka msaada wa baba yake sio kwamba tulimkataza hivyo,
hapana ni yeye mwenyewe tu....ila aliendelea kumtambua kama baba yake,
nilimwambia huyo ni baba yako,asije hata siku moja kumkana, au kumsema lolote
baya, na alinitii, ila hatukutaka msaada wake, akiwa na shida ni mimi
nawajibika.
Sasa baada ya kuniona huko Dar, akawa sasa anatuma pesa za
matumizi, tulipokea na kiukweli sikupendelea kuzitumia, hata hivyo, kwa vile ni
wajibu wake, ikabidi tuwe tunazitumia tu, ila sikuwa na ile hali ya kumtegemea
yeye kabisa.....’
‘Ikatokea wazazi wakaingilia kati, hadi
tukasuluhishwa...nikaona haina haja, na kwa vile mimi nampenda mume wangu,
nikakubali yaishe, tukaanza maisha mapya,..lakini kwa masharti kuwa mimi
nitaendelea kuishi huko huko kijijini, yeye aendelee kuishi mjini na wanawake
zake, siku akijiskia anakuja huko kijijini namkaribisha kama mume wangu, anakaa
siku mbili anaondoka zake, nimezoea, sina shida naye, mpaka umauti ulipomkuta.
‘Oh…kweli wewe.., una moyo kweli…’nikasema
‘Nilikuja kuajiriwa na kampuni isiyo ya kiserikali kwa
ajili ya kusaidia akina mama waliokatiza masomo kwa ajili ya uja uzito, kwahiyo
sikuwa na shida, ya kumtegemea mume tena,...sikuwa namfuatilia maisha yake, na
mengi nilikuwa naambiwa na watu tu...mtoto wangu ndiye aliyejitahidi
kumfuatilia na kujaribu kumkanya, lakini hakumsikiliza mtu, alidai kuwa hayo
ndio maisha yake, mtu asimuingilie.
‘Sasa kwanini nije kuchukua urithi wake, .kwanini nije,
kuchukua mambo yake, ambayo hatujui yametoka wapi...sisi tuliamua kila kitu
chake tukiuze, tulipe watu, na kama hakuna watu tutatoa sadaka…’akasema
‘Mhh…lakini..’nikataka kusema neno lakini hakunipa nafasi
akaendelea kuongea.
‘Na katika huu msiba ndio tukaja kugundua kuwa kumbe ana
watoto wengi wa nje, ana madeni mengi ya watu,...na hawo waliofanyiwa ubaya, ni
wengi, japokuwa awali hawakutaka kujitokeza…ndio tukajaribu kuwalipa lipa na
kuwaomba msamaha, na hili zoezi ndilo tunaendelea nalo mpaka sasa nia ni
kumsaidia marehemu,....’akasema.
‘Kwahiyo ndio maana mlikuwa mnanitafuta mimi, lakini mimi
simdai, ila nasikia anamdai mume wangu, mimi sijui..?’ nikamuuliza
‘Ni pamoja na hayo, ila cha muhimu kwa hivi sasa ni huo
mkataba, madeni hayana nguvu sana…sasa sisi tunachotaka kwako ni kujua ukweli,
na kama tulivyohisi, tumegundua kuwa ni yale yale ...kwahiyo, tunaomba,
mtuambie tufanye nini, kwani sisi hatutaki kitu chochote kutoka kwake, ila tunachotaka
ni kuyaweka mambo yawe sawa, kusiwe na kudaiana , na tunafanya haya kwa vile
mtoto wangu ndiye kapewa hilo jukumu....’akasema
‘Je unafahamu lolote kuwa mkataba huo mlio nao…umetokana na
kugushi mkataba mwingine uliokuwa halali?’ nikamuuliza
‘Nimesikia hilo kwa wakili wetu, na yeye alisikia kutoka
kwa wakili wako,sasa ukweli upo wapi, ndio tukaona kuna umuhimu wa kuonana na
wewe ...’akasema.
‘Je mna amini hilo, kuwa mume wenu alikuwa na hisa kwetu?’
nikamuuliza
‘Sisi hatuna haja ya kupekenyua ukweli, ukweli mnaufahamu
nyie..sisi hatuna haja na hizo hisa, hata kama kulikuwa na ukweli, hatuna haja
nao....tulishaanza maisha yetu, hatukuwa tunamtegemea yeye, kwanini sasa
kafariki tuanze kugombea mali yake, kama walivyokuja watoto wake wa nje kuja
kugombea mali yake....sisi tuliwaambia kuwa kama wanahitaji mali ya marehemu,
basi wakubali na madeni yake, na alipopigwa mahesabu ikaonekana madeni na
mengi, kuliko, wenyewe wakakimbia.
‘Hayo ni ya mume wako, sasa tuongee kuhusu mume
wangu,...kwanini mnamtetea yeye mnajuaje kuwa yeye sio mkosaji kama alivyokuwa
mume wako ?’ nikamuuliza
‘Sisi hatumtetei, ila tunatimiza wajibu wetu, yeye kama
wengine, ni miongoni mwa watu walioathirika kutokana na tabia ya mume
wangu....anahitajia kupata haki yake,...alihadaiwa, na akajikuta anatoa hisa
kwa mume wangu, tunahisi hivyo, …japokuwa bado hatujaupata ukweli, ukipataikana
ukweli tutafanya inavyostahiki...’akasema
‘Kwa vipi mtaweza kuupata huo ukweli?’ nikamuuliza
‘Kutokana na mikataba,.wakili wetu katushauri hivyo..hatuna
jinsi nyingine, sisi , na mtoto wangu,..tunajitoa kwenye huo mkataba, na nio
bora uvunjwe kabisa, lakini kama miktaba hilo ilitengezwa kisheria, basi sheria
ifanye kazi yake kuivunja, au sio, ndio utaratibu muafaka, tusaidiane kwa hilo…’akasema
‘Ndio lakini huo mkataba mliona nao, sio sahihi, ni wa
kugushi…’nikasema
‘Ndio maana mwanasheria wetu anaufanyia kazi, ila
tunahitajia msaada wenu, ..mume wako kasema wewe unaweza ukawa ni kikwazo, ndio
maana tokea awali tumekuwa tuklitaka kuonana na wewe..hukushangaa
nilivyokuuliza awali, je mna matatizo gani wewe na mume wako…nashukuru kuwa tumekuona na iliyobakia ni wewe kushirikiana
na sisi, tulimalize hili jambo..’akasema.
‘Nakushukuru sana kwa kuwa mkweli kwangu na kunielezea
sehemu ya maisha yako, na mimi sina kinyongo na nyie tena, ...ama kuhusu
maswala ya mume wangu, hayo hayawahusu, nawaombeni msijaribu kuyaingilia,...kama
mnataka kumsaidia kwa hilo, nyie mshaurini yeye aulete ule mkataba wetu wa
awali, ambao tuliandikishana mimi na yeye,kuhusu mambo yote,yeye akaghilibiwa
na mume wako akakubali ubadilishwe, ...hilo tu, ...’nikasema.
‘Sisi hatuujui kama kuna mkataba mwingine tumaliskia hili
hivi karibuni kutoka kwa hao mawakili, .sasa..hata sijui huo mktaba mwingine
upo wapi..na je uhalali wa hiyo mikataba itakuwaje…’akasema huyo mama
‘Hata mimi siujui huo mkataba wenu mnao-uongelea, na
wala siutambui, maana ulitengenezwa kimbinu kutokana na kuvunja mkataba watu wa
awali bila mimi kujua, umegishiwa na sahihi na kila kitu, sijui walifanyaje...kwahiyo
huo mkataba mlio nao ni batili,..’nikasema.
‘Kwahiyo nyie au wewe unataka sisi tufanye nini?’
akaniuliza.
‘Kwa hivi sasa niseme tu, kuwa nyie mumeshatimiza wajibu
wenu, ..nawashukuru sana kwa hilo, sisi au mimi sina kinyongo na nyie na kwa
vile mume wako, ...hayupo tena hapa duniani, huwezi kumuhukumu maiti au sio…,
anayehukumiwa kwa hivi sasa ni swahiba wake..naye ni ni mume wangu...nafikiri
umenielewa hapo….’nikasema.
‘Mdogo wangu, mimi nataka kukupa ushauri tu, ni ushauri wa
bure, kama utauona una maana haya, kama ndio wa kupitwa na wakati haya, ukitaka
kuufuata ufuate kama hutaki basi, ni hivi, hakuna mkataba wa ndoa zaidi ya ndoa
yenyewe, mkataba wa ndoa ni kiapo chenu cha ndoa, pale mliposimama wewe na mume
wako, ukakubali kuolewa na yeye na yeye kukubali kukuoa,..au sio’akatulia
kidogo huku akionyeshea kwa mikono.
‘Hilo ni sawa, lakini matendo ya wanandoa yanaweza kuuvunja
huo mkataba…amini hilo, …kuna matendo yanaharibu kabisa ndoa…lakini watu
hatufuatilii..je ni nani wa kulaumiwa hapo…’nikasema
‘Ni sawa, lakini kusameheana kupo, au sio…nakubali hilo..lakini
ninachotaka kusema kuhusu ndoa,…msije kuvunja ndoa kwa sababu ya vitu vingine
kama mali..na watoto..’akasema
‘Watoto kwa vipi…?’ nikamuuliza
‘Ndugu yangu tusiongee sana, huo ndio ushauri wangu, unajua
kwenye hii kazi nimejifunza mengi, nakubali ukweli, kuwa wanandoa, tupo kwenye
mitihani mikubwa sana, hasa mmoja wapo anapokuwa sio mkweli,.....’akasema
‘Sasa hapo utafanya nini..hebu niambie kama mmoja wapo
anavunja mkataba, na hakuna kitu mlichoandikiana naye….’nikasema
‘Nikuambie ukweli, sisi wanadamu , nikiwa na maana sisi
wanandoa, hata kama tutajaribu kuwekeana mikataba mingine, tunayoona sisi ni
kisheria zaidi, tukajenga ukuta wa kulindana, tukaweka na walinzi wa kutulinda,
ndani na nje, ...tukafanya kila iwezekanavyo, ili mmoja asivunje miiko ya ndoa,
…hatatuweza..’akasema
‘Kwanini..?’ nikamuuliza
‘Mikataba halisi ya ndoa ipo kwetu sisi wenyewe…kama mioyo
yetu, kama sisi wenyewe hatukujibidisha hivyo, tukakubali mioyoni mwetu kuwa
ndoa ni kati ya muma na mke, kuwa ina masharti yake, ambayo kila mmoja
anatakiwa kuyatimiza kidhahiri na kificho,...kama hatutajua hayo sisi wenyewe,
tukayakubali sisi wenyewe ndani ya nafsi zetu, haiwezi kusadia kitu,...kamwe,
hatutaweza kufanikiwa....’akasema.
‘Kwahiyo unataka mimi nifanye nini…?’ nikamuuliza
‘Mimi nakushauri kama mkubwa kwako, maana kiukweli wewe ni
mdogo wangu mbali tu, nimkuzidi kiumri, na huenda hata kiuzoefu, mimi nimepitia
kwenye mitihani mingi migumu, niliyokusimulia hapa ni cha mtoto, nikushauri
jambo, hakuna haja ya kuhangaika sana kwa hili…, cha muhimu kwa sasa ni
kumsameheana tu…’akasema
‘Kusamehe sio tatizo tatizo unasamehe nini sasa…’nikasema
‘Sio lazima kila la kusamehe liwe wazi kwako mengine ni
bira uyasamehe bila kuyafahamu maana ukiyafahamu huenda ukashindwa kuyasamehe,
yaache yabakia na muhusika mwenyewe atajuana na mola wake, nina uhakika mumeo
kakukosea, hata kama hajakutamkia, maana madume, wanaweza kujifanya
hawajakosea, lakini kiukweli kwenye nafsi zao, wanajua kabisa wamekosea...na
wengi hujijutia..’akatulia kidogo.
‘Ni rahisi kumsema mwenzako au sio…’nikasema
‘Unajua nikuambie jambo sisi wanawake, kwa waume zetu ni
kama mama zao, tunabeba yote kama mzazi anavyobeba makosa ya mtoto wake,
..mtoto, anaweza kukosea sana, lakini mwisho wake kama mzazi, unamsamehe,
unaona mtoto ni mtoto tu…’akasema
‘Lakini mume sio mtoto, ana akili zake na pia kapewa
wadhiaf wa kiongozi wa familia, au sio…’nikasema
‘Ndio…lakini kuna mambo sisi tumetukuzwa nayo,…uvumilivu,
malezi, kunyenyekea,…mapenzi haya ni tunu kwetu, tusiyabeze, wapo waliojaliwa ni
heri kwao, lakini..nasema tena lakini wapo,...wengine wanaweza kuleweshwa na tama
ndogo tu, ya kiwiliwili cha mwanamke, akaghilibika, na akajikuta kafanya
lisifanyika, kama walivyo watoto...ukimuuliza anajifanya hajui, au hata
kukataa, anakataa…, sasa sisi tujitahidi tu kuwasamehe....’akasema na mimi
nikawa natikisa kichwa kutokukubaliana na maneno yake.
‘Nikuambie tena,....wengine wanaweza hata kukubali makosa
yao, lakini anakubali mdomoni tu, mwingine anaweza asikubali, lakini moyoni
kakubali makosa, ila anaogopa kuonekana kakosea,sasa mimi namfahamu sana mume
wako,... kama kakubali kujirudi, kama yupo tayari kuishi na wewe, na kuwa
hatafanya tena hayo makosa yaliyotokea,...basi msamehe tu,….mengine muachie
mola wako…’akasema
‘Hapana, mimi nataka mkaaba ufanye kazi yake ili watu
wajifunze…tusiendekeze mambo…’nikasema
‘Mkataba,..mkataba…mama nanihii…kwani huo mkataba ndio
ndoa,..huo mkataba hauna maana yoyote kama hutaweza kuishinda nafsi yako..
..unaweza ukawepo na bado kwa siri watu
wakawa wanauvunja tu, utajuaje…, sasa inasaidia nini hapo..mkataba mnzuri upo
ndani ya mioyo yenu....’akasema.
‘Mhh..mimi naona nyie mnamtetea sana jamaa yenu, kwa vile
lakini kama mngelitendewa kama mimi najua mngelichukua hatua……’nikasema
‘Sio kumtetea, nakushauri tu, …mangapi yametokea kwangu,
nimekuhadithia ili ujifunze kidogo kutoka kwangu, nakushauri tena, achana na
kuhangaika na huo mkataba, ...wao wanajua wenyewe kwanini waliubadilisha, wewe
shikilia mkataba wao ambao mungu anautambua, kiapo cha ndoa, na timiza wajibu
wako kwenye hilo, sasa kwa ushauri wangu, kaeni tena pamoja, jadilianeni, muone
chanzo cha kosa ni nini, huenda chanzo ni wewe mwenyewe lakini
hujatambua hilo,…’akasema
‘Kama chanzo ni mimi, kwanini hajaniambia, nikajijua na
kujirekebisha, yeye si mume wa familia, ilitakiwa yeye aniambie, ..kama alikaa
kimia, mimi nilijionea ni sawa tu,…sasa mimi natimiza wajibu wangu siwezi kukaa
kimia, …tuje kuangalia sote…’nikasema
‘Jingine si nyie mna watoto, sasa mnataka watoto wenu waje
kujifunza nini kutoka kwenu,...wakiona
baba na mama wapo kitu kimoja, wanakaa wanashauriana kila mara wanafikia
muafaka, na wao wanajiwekea nadhiri mioyoni mwao kuwa nikiwa mkubwa, nikaoa,
nitaishi kama walivyokuwa wakiishi baba na mama...’akasema na mimi hapo nikakaa
kimia.
‘Sasa kama nyie wawili, kila mara mazozano, au
mumanuniana,..au kila mtu na hamsini zake…na baadae mnaishia
kutengana,..kuachana,..wao watamfuata nani, au wao watajifunza nini, wataona kumbe
kuishi kila mtu maisha yake, inawezekana, ndio mtindo wa maisha, lifikirieni
hilo kwa ajili ya kizazi chenu, na huo ndio mzigo tunaoubeba sisi wanawake...’akasema.
‘Nakushukuru sana kwa ushauri wako dada yangu, lakini
nilikuwa na swali moja nataka nikuulize, ili nione kama kweli wewe unatetea
pande zote mbili, ili kuona suluhu ya kweli, .. je mume wangu aliwahi
kukuambia kuwa ana mtoto nje ya ndoa?’ nikamuuliza. Alikunja uso kidogo, halafu
akatabasamu, na kusema…
‘Mhh, kwa jibu la moja kwa moja, kiukweli kwangu hajawahi
kunitamkia hivyo, huwa naongea naye, kama mtu na dada yake, kama shemeji yake,
tunataniana hapa na pale, lakini kwa hilo hajawahi kuniambia, siwezi kukuficha…’akasema
na akawa kama anawaza jambo, halau akasema
‘Unajua watoto wa nje..kwangu wapo..na siwezi kuona ajabu
kwako pia…lakini hayo sio kosa lako, au sio..na sio kosa la hao watoto au sio….na
wao wana haki yao,..sio kwamba natetea hilo, hapana, lakini kama limetokea
..ufanyeje sasa…ndio iwe kigezo cha kuvunja ndoa…’akasema
‘Sio kigezo kwa mimi, ni kigezo cha yeye, kuwa kavunja
ndoa,…je hilo ni sahihi kwenye ndoa..kwenye ndoa, ilisemwa kuwa anaweza kuzaa
nje bila ndoa..niambie ukweli hapo…je kuzini sio dhambi, ni nini adhabu ya
mzinifu ndani ya ndoa..tusije kutetea dhambi tukaja kupata dhambi…’nikasema
‘Hahahaha…ukisema hivyo, nahisi wengi watavunaj ndoa zao,
na wengi watapigwa mawe mpaka kufa…sasa sijui…lakini msamaha ni bora zaidi au
sio..ukimsamehe abada ya kukiri kosa basi,…tufanyeje sasa…’akasema
‘Unaona..udhaifu wetu huo..wewe awali umesema sisi wanawake
ni wazazi ni walezi, na kila mmoja ni mchungi kwa mwenzake, je tutachungana
hivyo kwa kuyakubali makosa, yafanyike tu..tusamehe tu..wengine wataona ni
mchezo, acha adhabu ifanye kazi yake uone watu kama hawataogopa….’nikasema
‘Ni sawa, lakini wewe hujafanya makosa yanayofanana na hilo…usiangalie
upande mmoja tu…unaweza ukawa umezini kwa namna nyingine..samahani usiona
natetea hayo, maana hata mimi yananiuma sana..lakini tuangalia jinsi gani ya
kuokoa, kuliko kubomoa…nakubali kama kafanya hivyo kakosea, lakini
tufanyeje..naangalia upande wa watoto…’akasema
‘Watoto, watakua watajifunza, ukweli utakuwa bayana, …mimi
bado nipo pale pale…ukweli, na ukweli wetu ulisimamiwa na mkataba, ni kwanini
wakaja kuuharibu mkataba , kama kweli alitaka haki, …kama kweli alikosea, basi
angelikuja akaniambia, ndio ningeumia..lakini ningelijua kuwa kweli mwenzangu
kateleza, lakini kwa hatua waliyofikia, hapana..’nikasema
‘Unajau kiukweli mimi sina uhakika na hilo, ila…,
ninachokumbuka, ni kuwa, kuna siku nimemuuliza, hivi yeye kwa sasa ana watoto
wangapi, aliniambia kuwa tu ana watoto wengi, lakini.., hakusema idadi,....’akasema.
‘Hakukuambia kuwa ana watoto wangapi..na hujui kuwa mimi
nina watoto wangapi?’ nikamuuliza…’ nikasema.
‘Hakusema idadi kiukweli, ila nakumbuka kauli yake aliyotoa
ni kuwa, yeye atahakikisha watoto wake, wote, bila kujali ni mke au ni mume,
atawaandikishia haki zao, na ni vyema kufanya hivyo kimaandishi....’akasema
‘Ehee…kama ni wakike au wa kiume…unakumbuka ni lini..?’
nikauliza
‘Sio muda mrefu,…na alisema, kitu kama hicho kuwa hataki
watoto wake waje kubaguana, awe wa kiume au wa kike….nakumbuka kitu kama hicho,
na kwa kauli hiyo, nilifahamu kuwa nyie mna watoto wa kike na wa kiume’
akasema.
‘Hapo kuna kitu, …lakini kwa kauli yako tu, sasa naanza
kuhisi kuna yawezekana kweli kuwa akawa na mtoto nje, huyo mtoto wa kiume
katoka wapi...?.’nikamuuliza huku nikionyesha kushangaa, na yeye akaonyesha
kushangaa jinsi nilivyomuuliza, akaniuliza swali;
‘Kwani nyie mna watoto wangapi?’ akauliza huku akiangali
huku na kule, kama anawatafuta watoto.
‘Mhh, usijali dada yangu, naona tuishia hapo, au kuna
jingine ulitaka kuniuliza maana nyie mumesema mlikuwa mkinitafuta sana…maana
haya mambo mengine ni mambo yangu na mume wangu, tutaelewana tu...’nikasema.
‘Aaah, uliniuliza swali, nikakujibu, na wewe naomba unijibu
swali langu...ili kama nina cha kukushauri, nitakushauri, sina nia ya umbea,au
nimekosea jamani...’akasema.
‘Kiukweli, sisi tuna watoto wawili tu, tena wakike wote...’nikasema.
‘Basi labda mimi nilisikia vibaya, lakini nina uhakika,
kutokana na kauli yake, ni kama vile mna watoto wa kike an wa kiume...hata
kwenye huo mkataba niliouona, mimi sikuusoma sana,..maana sikuona umuhimu wake,
kuna kitu kama hicho,...sikumbuki vizuri, na kwahiyo hapo siwezi kusema
kitu,...nisije nikawa mbeya,, ila lisemwalo lipo, kama halipo
laja....’akaniangalia kwa macho ya udadisi.
‘Nitaligundua tu, nina uhakika kabla ya wiki nitakuwa
nimeshagundua ukweli...na hapo ..sijui, maana huo ni ushahidi wangu wa kutosha,
na kuanzia hapo nitajua nichukua maamuzi
gani..na ka hatua hii,.....’nikasema.
‘Kwahiyo huenda hilo ndilo linafanya msielewane nyie wawili
au sio, ....na hilo huenda ni moja ya jambo ambalo wewe unaliona linalovunja
mkataba wenu au sio..ni sawa kwa hilo hata mimi silipingi, unapotoka nje ya
ndoa umeshavunja mkataba wa ndoa..lakini kusameheana ni bora zaidi, au
sio…’akasema
‘Sio rahisi kihivyo….mimi ni mvumilivu sana, na wengi mpaka
huniona ni mjinga, sielewi, sikubali ukweli…lakini nina subira ya namna hiyo,
ila sasa ikizidi kama hivi, basi moyo wangu ukikengeuka, siwezi tena…’nikasema
‘Yeye si kakubali kuwa kakosa au sio, na wewe ukubali
kumsamehe....kama kuna mtoto nje, ambaye humjui, basi jadilianeni muone jinsi
gani mtamtambua huyo mtoto...wewe waonaje kwa hilo…?’ akasema na kuuliza.
‘Mkataba wetu ulikataa hilo, na hadi hii leo yeye
hajakubali hilo, sasa wewe unanishaurije hivyo,kwanza kazini, kuzini si kuvunja
mkataba, halafu kama ana mtoto, sio ndio ushahidi wenyewe…tatu anavinja
mkataba, anaugushi..kwanini afanye hivyo,…anamdanganya nani hapo.., aah, mimi
hilo sitavumilia kabisa…’nikasema
‘Kama nilivyokushauri, labda mimi ni tofauti na wengine, unielewe
vizuri hapo, maana kiukweli mimi sijui...kama limeshafanyika, na mtoto yupo, na
yeye anawajibika kwake, na sijui labda huenda anawajibika na kwa mama wa mtoto
pia, na kama bado mtoto ni mchanga,kiukweli ni lazima awajibike, hana
ujanja hapo, na ni vyema, akuambie ukweli....muulize, kwa wakati muafaka,
atakuambia...’akatulia.
‘Nimeshamuuliza sana, lakini hataki kuwa mkweli…’nikasema
‘Kwahiyo kumbe mna mabinti wawili, hamjajaliwa kupata
mvulana....ndio maana niliwahi kusikia zamani kidogo, kuwa akizaa mtoto wakiume
atakuwa katimiza ndoto yake...lakini ni zamani kidogo,...’akasema
‘Zamani ya vipi…?’ nikauliza
‘Aaah, zamani, sikumbuki, ila muhimu kaeni mliongelee kama
wanandoa,....ili mambo yaishe, mgange yajayo..msisubiri mpaka kutokea msiba,
mmoja wenu hayupo duniani ndio hawo watoto wa nje, wanaanza kujitokeza,
na kuleta mfarakano, kama ilivyotokea kwetu, japokuwa tumeshayamaliza kiaina,
..’akasema.
‘Nimekuelewa dada yangu, nakushukuru kwa ushauri
wako,...lakini hayo ya mume wangu, yaacheni kama yalivyo, ninafahamu jinsi gani
ya kufanya, nilitaka kuwa na uhakika tu,…’nikasema.
‘Sasa nikuulize kitu, je akija kwa hivi sasa akakuambia
ukweli, utamsamehe?’ akaniuliza. Na kabla sijamjibu macho yetu yakaona jambo….
Kule mlangoni nikawaona mume wangu na Yule wakili wake
wakitoka, wakawa wanashikana mikono kama kuagana, na mume wangu akageuka na
kutuona ..akamshika bega wakili akaongea naye jambo, na wote wawili wakawa
wanakuja kuelekea pale tulipo…
NB: Ni nini kitaajiri hapo
WAZO LA LEO: ushauri mnzuri ni ule
unaoangalia usawa, kuwa ninachomshauri mwenzangu hata mimi ningalifurahia
kufanyiwa hivyo. Mshauri mwenzako kwa wema, mshauri kwenye mambo ambayo
yatamjenga,..na hata yeye akifanya au wewe ukifanyiwa hatupata madhara yoyote.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment