Mtoto wa marehemu alionekana mtu mwema
kwangu…, na alikuwa tayari kuniambia mengi ambayo huenda yangelifanikisha
malengo yangu, ya kutaka kujua ni kitu gani kinachoendelea, kitu gani
kilichoweza kumbadilisha mume kiasi hicho..na je ni kweli ana mtoto nje ya ndoa..huo kwangu ungelikuwa ni ushahidi mkubwa sana...tatizo huyu mtoto wa marehemu akatoa sharti ambalo
lilinipa wakati mgumu kulikubali,
Sio kwamba simpendi mume wangu, sio
kwamba…simuamini, lakini kama ni kweli kayaafanya hayo ninayoyasikia, na kavunja
mkataba, je haiwezi ikawa ndio njia, na sababu ya kutenda mengine makubwa zaidi ya hayo.....na je
nikikubaliana naye si ndio sababu ya kupoteza mali na juhudi zangu zote, je wazazi watanielewa kweli….
‘Nataka umsikilize mume wako..mkubaliane
naye..mkisha kubaliana naye , mkawa kitu kimoja,basi sisi tutajitoa kabisa
kwenye huo mkataba ulioandaliwa, mkataba huo ulionyesha kuwa baba ana hisa
kwenye kampuni zako, ...’
‘Naweza kuonana na mama yako.....?’ nilimuomba hivyo..akili ikiwa imechanganywa na sharti hilo....
Endelea na kisa chetu.......
Mara mume wangu
akaja na gari lake, na ndani ya hilo gari alikuwepo mtu mwingine alikuwa ni
wakili wake, walifika na hawakutaka hata kutusalimia, wakaingia ndani,..na mimi
sikutaka kuwafuata, japokuwa ni adabu mgeni alifika umkaribishe, lakini kwa
hali ilivyokuwa, ..sikujali tena….
‘Mume wako anaonekana hayupo vizuri…’akasema
‘Ni kawaida ..nahisi ni majukumu ya kazini kwake, ila sijui
kwanini kamleta huyo wakili hapa nyumbani, ..kama watanihitajia
wataniita..’nikasema
‘Yah….basi…kama haupo tayari, mama anaweza kuja wakati
mwingine..’akasema
‘Kwanini, …nipo tayari,..hao wana mazungumzo yao, hayawezi
kuzuia hili, kama wangenihitajia wangeniambia..si umeona..hawakutaka hata kusalimia,
ina maana wana mazungumzo yao binafsi…’nikasema
‘Sawa…kiukweli mama, atashukuru sana kuongea na wewe, kwani
hata yeye alikuwa na hamu sana ya kuonana na wewe, lakini kweney haya, yeye
hana zaidi ya kuamua, zaidi ya yote ananitegemea mimi, yeye ni muwekezaji tu wa
huko kijijini ...’akasema.
‘Kwanini alitaka kuonana na mimi, ni kuhusu mambo hayo
hayo…?’ nikamuuliza
‘Pamoja na hayo yaliyotokea, yeye alishasikia sifa zako, za
uchapa kazi wako, na kwa vile yeye ni mjasiriamali, alikuwa na hamu sana ya kuonana
na mtu kama wewe, ajifunze mengi kutoka kwako, na ni muongeaji, atakusimulia
mengi ambayo hata hukuyaka kuyafahamu, uwe mvumilivu tu...’akasema.
‘Kwani mama yako huko kijijini anafanya kazi gani hasa?’
nikamuuliza
‘Amejiajiri, ana miradi yake, ni mmoja wa viongozi wa akina
mama, na hamu yake kubwa ni kuja kuwekeza hapa Dar kama itawezekana, lakini sio
rahisi kama ujuavyo, gharama, masomo …, lakini hiyo ni mipango ya
baadaye...’akasema.
‘Nahisi kwa mtizamo wangu, mumepanga kufanya hivyo kwa
urithi wa baba yako, au sio..na baba yako ana vitega uchumi vingi, nasikia ana
nyumba zaidi ya tano, .....?’nikauliza.
‘Nyumba zote tumepiga mnada, kwa ajili ya kulipa watu,
waliopata madhara kutokana na mambo yake, ...sisi kama sisi, hatutaki chochote
kutoka kwake,mali zake na miradi yake, kwetu sio muhimu, muhimu ni kulisafisha
jina lake ili mungu amsamehe makosa yake,..’akasema.
‘Mnaonekana hamtaki ubaya wa baba yenu uwangilie na nyie au
ni mbinu tu za kuataka kunihadaa, kiukweli mimi siwaamini, nikuambie ukweli
kutoka moyoni mwangu, yaliyonikuta…yamenipa fundisho?’ nikauliza
‘Ndivyo tunavyotaka, lakini watu wengine wanaonekana
kutokutuamini, sioni ajabu na wewe ukisema hivyo, lakini dhamira yetu ipo pale
pale, hata kama hamtatuamini sisi tutafanya yale tunayoona ni sahihi,
tukimaliza hayo, basi wale wenye nia njema na sisi watatuamini tu...’akasema
‘Mimi sina ubaya na nyie, kama kweli mna nia hiyo njema,
ila sitaki mtu kuniingilia kwenye mambo yangu, ....baba yenu alianza hivyo,
akajitahidi, na nilimkanya sana, bado hakuchoka, akatafuta mbinu mpaka akaweza
kuingia kwenye mambo yangu hata bila ya mimi kufahamu..kama kweli mna nia njema
mumeliona hilo, lakini nina iamni kuwa sio yeye, kuna mtu anamtumia…’nikamwambia.
‘Hayo mimi siyaamini sana, kuwa kuna mwanasiasa anamtumia,
hapana,..mimi namfahamu baba, ni hulka yake, sawa anaweza kuwa anatumiwa,
lakini yeye si ana akili….sijui lakini, maana huko mimi sija..paangalia
sana..’akasema
‘Sawa pamoja na sharti lako hilo, ambalo mimi kwangu ni
gumu, na mimi nina sharti langu, kama tutakubaliana, basi nitajua na nyie mpo
na nia njema,…’nikasema
‘Sharti gani,…niambie tu , maana nia yetu ni
kujenga…’akasema
‘Ili kweli niwaone kuwa hampo nyuma yake, na hamna nia
njema, nawataka kwanza, nipate mkataba wangu, upo mkataba wangu wa asili kati
yangu na mume wangu, baba yako aliuchukua, akaugushi na kutengeneza mkataba huo
ambao mnao sasa…yeye aliyeubadili, na najua kabisa anao, ule wa asili, sasa
nipeni huo, ....’nikasema na yeye akanikatiza kwa kusema;
‘Sisi hatujui lolote kuhusu mkataba wenu wa asili, na
hatuna haja nao, sisi mkataba tulioupata
ambao hata wakili wetu anaufanyia kazo ndio huo, unaoonyesha kuwepo kwa
hisa za baba kwenye kampuni zenu, na ndio maana kwanza tulitaka kulithibitisha
hilo, …’akasema
‘Mtathibitishaje, kwasababu kulithibitisha hilo ni kuwaona
wahusika, je mumelifanya hilo…?’ nikamuuliza
‘Ndio…tumeongea na mume wako, amelithibitisha hilo...ila
alisema kuwa hiyo ya umiliki wa hisa zaidi ya nusu, ya hisa, haikuwa ni hiari
yake, ..kulikuwa na shinikizo fulani kwake, juu ya uwezo wake,, ila yeye alikubali
tu ili mambo yaishe..na tukamuuliza ni shinikizo gani..’akasema.
‘Je yeye aliweza kuwaambia ni kutokana na shinikizo gani?’ nikamuuliza
‘Hakutaka kusema ni shinikizo gani, lakini kwa vile
tunamfahamu baba, kuwa akiwa anatafuta kitu, hasa mali, hajali aliyepo mbele
yake, hatukutegemea kuwa watafikia hatua ya kushinikizana kiasi hicho, kwani
haiingii akilini, mume wako akubali kumpa nusu ya hisa baba, kwa sababu ya
deni, na ni kweli madeni yapo..kuna hati hizo,..lakini kwanini kuwe na
shinikio..madeni ni madeni au sio…sasa ni nini, sisi hatukutaka kumlazimisha
mume wake atuambie...’akasema.
‘Wewe hukugundua ni kitu gani, si ulisema ulifanya
uchunguzi wako au sio…?’ nikamuuliza.
‘Hapana, sisi hatukutaka kuingilia huko kwa undani zaidi,
ili iweje, kwani tunataak nini, …mmh, mimi naona yale niliyotaka kukuambia kwa
sasa yanatosha, na kwa vile unataka kuongea na mama, ngoja nikamuite, muongee
naye, nitamsubiria kwenye gari...na mume wako naona anaongea na wakili wake,
sijui watanihitajia au la..nisingelipenda kuongea naye kwa leo…’akasema
‘Ina maana mumekuja na mama yako kumbe mbona hukuingia
naye..yupo wapi…!?’ nikamuuliza kwa mshangao.
‘Tulikuwa naye, alikuwa na mambo yake, nikamwambia napitia
kwako kwanza kujaribu kama utakubali kuongea na mimi, na yeye akawa
anawasiliana na wateja wake kwenye simu, nikamuacha nje kwenye gari, yeye muda
wote ni kuongea an simu, si unajua ujasiriamali ulivyo...’akasema
‘Sawa nitafurahi nikiongea naye, na samahani sana, kama
sitaweza kukubaliana na ombi lenu, nalisema hili mapema, uelewe msimamo wangu,
muhimu ni mkataba wangu wa awali, huo ndio utakuwa ufunguo wa makubaliano
mengine bila huo, sizani kama tutaweza kukaa meza moja na mume wangu...’nikasema.
‘Hamna shada, ..nimefurahi sana kuongea na wewe nahii iwe
ni mwanzo tu wa mazunguzmo yetu, na nina imani tutashirikiana kulimaliza hili
jambo…na kama upo huo mkataba mwingine, kwanini usitolewe..usijali
tutalimaliza hilo…haya ngoja mimi nikamuite mama aje muongee naye..’akasema na kusimama, tukashikana
mkono, na akaondoka na kuniacha nikiwa nimesimama nikimwangalia anavyoondoka.
**********
Mke wa marehemu alikuwa wale akina mama wahangaikaji, wake
wa shoka, hata jinsi alivyokuwa akitembea kuja pale nilipokaa alionekana ,mama
mchapakazi kweli,...mwendo wake sio ule wa kike kike wa kutembea kimikogo,
anatembea kama mwanajeshi
Alipofika pale nilipokaa mimi nikasimama kwa adabu na
kwanza , akasimama hatua chache kutoka pale niliposimama, kwanza akaniangalia
kama ananikagua, halafu akanisogelea tukakumbatiana, na kusalimiana.
‘Siamini kama ni wewe..’akasema
‘Kwa vipi dada...?’ nikamuuliza
‘Unafahamu, nimeziona picha zako kwenye magazeti tu,
kwenye majirida mbali mbali yakitangaza biashara zako, ..lakini unavyoonekana
kwenye picha, sio sawa na nilivyokuona leo, leo upo kihalisia zaidi...’akasema
‘Kwani leo nipo vipi na huko kwenye magazeti naonekana
vipi?’ nikamuuliza kwa mshangao kidogo
‘Tuyaache hayo, maana sisi akina mama tukikutana mengi
tutakayoanza kuzungumzia,ni mavazi, muonekano , sura, hata tutasahau
jambo muhimu, na majukumu ya kila siku, mimi siku hizi sitaki kupoteza muda
tena, na tangu nije hapa Dar, naona napoteza muda wangu bure tu na mambo
yasiyonisaidia kitu...’akasema huku akikaa kwenye kiti.
Akaletewa kinywaji, na matunda…akapiga mafundo mawili,
halafu akainua uso na kuniangalia, akasema;
‘Haya niambie kulikoni, hivi Samahani kidogo, hivi wewe na
mume wako mna matatizo gani?’ akakimbilia kuniuliza hilo swali. Na kunifanya niingiwe
ni tahayari kidogo
‘Mhh, kwanini…oh, kwanza nikupe pole za msiba wa mumeo,maana
hatujaweza kukutana kwa sababu ya haya mambo yanayoendelea kwa sasa, pili sio
kweli kama watu wanavyodai kuwa eti mimi ndiye nimemuua mume wako…, kwanini
mimi nimuue mume wako..’nikasema.
‘Ni kweli kibinadamu, hisia hizo zipo, japokuwa mimi na
mume wangu tulikuwa mbali sana, huwezi amini hilo, nimeishi kama sina
mume, lakini ki ndoa yeye ni mume wangu
eeh…,siwezi kumkataa hadi kesho, japokuwa sasa ni marehemu..ila hutaamini yeye,
kwa kauli yake, alishanifanya mimi sio mke wake....inasikitisha…’hapo akatulia
kidogo.
‘Kwahiyo mlishatalikiana au..?’ nikamuuliza
‘Hamna talaka,..mimi sikukubaliana na hilo, …, kwahiyo bado
alikuwa ni mume wangu, ndio maana sasa nimepewa cheo cha mjane, na hata kwenye
mirathi yake sikuamini,kuona na mimi nipo kwenye orodha ya warithi,…ni ajabu
kabisa, alikumbuka kuniweka nahisi hili kalifanya baade sana, sijui ni nani
kamshawishi kufanya hivyo..hata hivyo kinafsi yangu, sikutaka chochote kutoka
kwake,…mengine tuseme yote ni mapenzi ya mungu..’akasema akionyesha huzuni.
‘Je wewe ulikuwa ukimpenda mume wako?’ nikajikuta nikimuuliza
hivyo.
‘Sana tu...huwezi amini, mimi nilikuwa nampenda sana mume
wangu, na nikuambie ukweli,..hili watu hawalifahamu na hata mume wangu akitoa
kauli zake hizo za kuwa hanitambui kama mke wake..alikuwa akisema hivyo akiwa
kalewa tu…kuwa mimi ndiye niliyemtaka
yeye…awe mume wangu...’akasema na kunifanya niingiwe na hamu ya kuyafahamu
maisha yao.
‘Hebu niambie ina maana wewe ndiye uliyemtongoza mume wako…au
kwanini alikuwa akisema hivyo…, nisamehe kwa kuuliza haya, maana imenipa hamasa
tu ya kufahamu…?’nikamuuliza
‘Hahaha, ndio hivyo, siwezi kulipinga hivyo..lakini sio
kwamba alikuwa hanipendi, kihivyo, hapana, kipindi hicho tulikuwa kwenye
ushindani wa kumpata yeye, unajua tena kijijini, na sisi tulijiona wasomi
fulani..hivi, tukiwa darasa la sita, mwili na sura vilitudanganya…’akatabasamu.
‘Kulikuwa na kundi la mabint warembo wa hapo shuleni na kijini,
nikiwemo mimi..unasikia…sasa, unajua tena, naongea haya..aah....tulikuwa
mabinti watatu, warembo…kila mmoja anataka yeye ndiye ampate huyo mwanaume,
kipindi hicho yeye ni kijana mtanashari eeh, na ana majigambo fulani,
kiingereza mdomoni hakimtoki, ..’akatulia.
‘Mrembo..?’ nikauliza na yeye akacheka, halafu akasema
‘Kijijini bwana,..mwanaume akionekana msomi, kiingereza
kingi…si unajua tena, huyu jamaa alikuwa msomo, kiukweli…na …ndio hivyo..basi
bwana, sisi ni mabinti wadogo warembo wa hapo kijijini...ilikuwa hapatoshi, kushindana
ni nani atachukuliwa na huyo msomo,..hahaha, ..lakini ndio hivyo, mwisho wa
siku nikasimama mimi kidedea, ..tukawa wapenzi, japokuwa ni upenzi wa kijijini...’akasema.
‘Hongera, ...’nikasema
‘Unafahamu, mimi tangu nikiwa mtoto, nililelewa kwa shida,
sikuwahi kupata raha, ...wazazi wangu hawakunidekeza, hawakuwa na kitu, kwahiyo
ilikuwa ni maisha ya suluba, ..kula na kulala kwa shida, ..unajua maisha tena
ya kijijini..basi ikatokea nikamfahamu huyo mwanaume…, kiajabu ajabu tu..’akasema
huku akitabasamu.
‘Yeye nakumbuka tangu nimfahamu, alikuwa ni mtu wa kusoma
vitabu tu...hata alipokuja huku mjini, na baaadaye akawa anafika fika, alikuwa
muda mwingi ukimuona kashikilia kitabu, hivi vitabu vya hadithi, alikuwa
anapenda sana kusoma vitabu vya kizungu, nakumbuka kuna vitabu vyake, aliwahi
kunionyesha, hata mimi baadaye nilipojiendeleza nimekuwa nikivisoma, hivi
vinaitwa, eeh, Jemsi Hadley Chase, na Peri Masoni, nahisi ndio maana
akajikita kwenye uanasheria...’akasema.
‘Siku ya kwanza kukutana kwetu, ilikuwa kama vile
wanavyoonyesha kwenye sinema, maana ilikuwa ni kwenye shughuli, mimi nilikuwa
kasichana, na bahati mbaya mwili wangu ulikuwa haraka, ni baadhi ya wasichana
kijijini kwetu tuliokuwa kimwili haraka, ...ilikuwa siku hiyo nafanya usafi
kuwaandalia wageni, mara wakati nawapelekea watu maji ya kunywa, nikagongana
naye, ..akadondosha kitabu chake, kikalowana maji...maana kulikuwa na maji maji
sakafuni, mimi nikakiokota na kukifuta kwa kitambaa changu cha mtandio. Picha ndio
ilianzia hapo…
Nilipomaliza nikamkabidhi kitabu chake, kumbe mwenzangu
wakati wote huo nahangaika kukifuta kile kitabu, alikuwa akinitizama, na hata
namkabidhi hicho kitabu, bado alikuwa akinitizama tu machoni....hapo mimi bado
mbichi nasoma, vititi saa sita..’akasema.
Nilishamuona kabla, na tulikuwa tukimuongelea shuleni,
wasichana na tama zetu…lakini hilo la kukutana kihivyo, ilikuwa siku hiyo, na
ndio nikaweza kujuana naye, na kuanza kujenga urafiki, na urafiki ukatibua nyongo…’akatulia
‘Kwa vipi…?’ nikauliza
‘Alinibebesha mimba..na kunifanya nifukuzwe nyumbani kwa
wazazi wangu..’akasema
‘Mungu wangu…’nikasema hivyo
‘Nilikwenda kuishi kwa bibi, mpaka nikajifungua...hebu
fikiria, darasa la sita enzi hizo, unabebeshwa mimba,hata darasa la saba
sikumaliza, ingawaje baadaye nikijisomesha, kujiendeleza,…usinione hivi , nilijisomesha
hadi sekondari, kiaina aina.
‘Basi aliponipa mimba, wazazi wangu wakafahamu, palikuwa
hapatoshi jamaa huyo akakimbilia mjini, sio kweli kuwa alikuja huku mjini kwa
ajili ya masomo, hapana,..ni lugha ya kudanganya , kuficha ukweli, yeye
alikimbia kuogopa balaa la wazazi wangu....’akasema
‘Lakini umesema yeye anasema ni wewe ndiye uliyemtongoza,
naona hapo inaonyesha yeye alikupenda pendo la awali,...au sio, lile pendo watu
mnaonana hapo hapo, kunajengeka hisia za kupendana au sio...’nikasema.
‘Baada ya pale,…kwenye shughuli… siunajau tena mambo ya
shule, nikawahadithia wenzangu, basi, marafiki zangu kila mmoja akataka ampate
yeye, na kila mmoja akawa anajibaragua kwake, kijinsi ajuavyo yeye, mimi
ikaniuma sana, wivu tena… ina maana kuwaelezea wenzangu ndio imekuwa
nongwa..basi nikaona nisilaze damu, ...’akasema.
‘Nilipoona wenzangu wanambana sana huyo kijana, kila mara
wapo naye, nikaamua kumwambia ukweli, ilikuwa ni kazi nzito kujielezea si
unajua tena wasichana…, lakini mwisho wa siku alikubali kuwa hata yeye
ananipenda sana tangu siku ile kwenye shughuli, ya kudondosha kitabu,...mambo
yakakolea sasa kuanzia hapo, ikawa mimi na yeye, nikawa nachapwa nyumbani kwa
ajili yake, sikusikia,...haniambii mtu...na asiyesikia la mkuu
huvunjika mguu...ikatokea kama mchezo tu, mimba hiyo...’akatulia.
‘Kiukweli mimba ilikuwa ni bahati mbaya, maana pamoja na
urafiki wetu huo, hatukuwa na mambo ya kisasa, haya ya kimjini mjini,
hapana...ilikuwa ni kukaa pamoja kuongea, kutaniana, kukimbizana,...ila siku
hiyo sikumbuki ni kitu gani kilitokea, na tukajikuta tumefanya jambo ambalo
ndilo lilimleta huyu mtoto wangu duniani, mliyetoka kuongea naye....’akatulia
kidogo.
‘Nilitenda hilo mara moja, na ikawa ndio tiketi ya shida,
...shida kweli...na nikuambie ukweli, mtoto huyo alinitesa kweli kweli…ilikuwa
ni mimba ya fundisho, na sikutaka kuzaa tena..licha ya mimba yake, na hata
malezi yake…, nilimlea kwa shida sana, huwezi amini. Siwezi hata kukusimulia,
....hata hivyo.. mungu hakunitupa mja wake, mateso hayo yalinijenga..nikawa
mke-dume, aliyejengeka kijasiri, unaniona nilivyo hata kutembea kwangu..na
nilitaka mtoto wangu awe hivyo hivyo, sikupenda awe mtoto wa ovyo ovyo,
nilijitahidi kumlea kihali niliyoona ni njema kwake..’akasema.
‘Ina maana ulipomzaa huyo mtoto, hukupata msaada kutoka kwa
mume wako?’ nikamuuliza.
‘Msaada gani, angelipata wapi pesa za kunisaidia wakati
huo, wakati huo wa awali, yeye mwenyewe alikuwa kula kulala..hana mbele wala
nyuma, na aliponipa mimba akakimbilia mjini kujificha, hakuonekana, hadi
nilipojifungua na alifika kwa mara ya kwanza mtoto anatembea,hamjui ,.....na
sikutaka hata kuongea naye..’akasema.
‘Ikawaje sasa mpaka mkafunga ndoa?’ nikamuuliza
‘Wazazi wangu waliweka shinikizo..kuwa ni lazima
anioe...huoni , hata nikiwa naye naonekana mimi ni mkubwa kuliko yeye, lakini
ni kwasababu ya maisha, na mwanamke mara nyingi anaonekana mkubwa, kama mkiwa
umri karibu sawa..sisi wanawake tunakuwa haraka haraka, na ukizaa ndio basi
tena...’akasema.
‘Basi ikabidi kweli anioe, kuepusha shari, japokuwa hakutaka, alishaniona sifai
tena..japokuwa mimi nilikuwa nampenda kweli kweli,...hata tulipoona hatukuweza
kuishi kwa upendo, ilionekana kama ndoa ya lazima, akawa ananinyanyasa,
...yaani sikuwa na raha na yeye, na hakutaka hata kutembea na mimi, yaani kutembee
mitaani kama mke na mume, haikuwahi kutokea....aliniona simfai, mwanamke wa
kijijini, mshamba, asiyejua kujiremba...na yeye keshakulia mjini,
anawafahamu warembo wa mjini, eeh..’akasema akibenua mdomo kwa dharau.
‘Basi bwana, ..mimi nikawa mama wa kijijini, sikujali, bado
nilimtambua yeye kama mume wangu, yeye akawa anishi mjini , mimi kijijini,
sikujali, nikawa napigika kijijini, maisha ya shida, anakuja mara moja au mbili
kwa mwaka, ..hanitumii pesa, akibahatisha ni mara moja kwa miezi mitatu, ni
pesa yenyewe pesa basi, nikawa nahangaika kivyangu kumlea mwanangu, sikujali na
wala sikukata tamaa...’akasema.
‘Nikawa naletewa taarifa za ajabu ajabu kutoka huko mjini,
kuwa mume wangu ana wanawake, sio mwanamke, ana wanawake, anawabadili kama
nguo...ikafika mahali nikamuuliza, na kumshitaki kwa wazee, nilivyosikia,
hutaamini kibao kiligeukia kwangu, kuwa mimi nasikiliza majungu, ni wapi
nilimuona na hawo wanawake,...iliniuma sana, kwani mmoja wa wanawake zake, namfahamu,
alikuja kuniambia yeye mwenyewe, kuwa mimi nitabakia huko kijijini yeye atakuwa
akistarehe na huyo mume wangu, eti sababu mimi nilimuibia yeye...’akasema.
‘Mwanzoni nilipata shida sana, na ikafikia hatua nikaamua
kumwendea huko mjini, ili nikapate huo ushahidi wanaoutaka wazee, najuta
kwanini nilifanya hivyo, maana nilizalilika,....sitasahau, kwani siku hiyo
nikiwa nimevalia zile nguo zetu, kwetu kijijini niliziona za maana , gauni
refu...mikono mirefu, kitambaa kichwani,...nikaingia dar, ilikuwa ni mara ya
tatu, nilishawahi kufika kabla.
‘Nilikuwa nafahamu wapi mume wangu huyo anaishi, nikafika
bila hata ya yeye kufahamu, ilikuwa saa kumi kumi hivi, nikafika nyumbani
kwake, ...kulikuwa na mvua mvua inaanza kunyesha, nikafike eneo alikopanga
chumba, alikuwa na chumba kimoja, maisha muda huo hayajamnyookea,…anasoma na
kufanya kazi, nikagonga mlango , mara akatokea mwanamke na khanga moja kiunoni,
akafungua mlango, huku akisema kwa nyodo.
‘Hivi nani hawa wanaharibuu starehe za wenzao, ni Malaya
gani wewe...’akasema huku akinifungulia mlango, na kuniona mimi, akashikwa na
butwaa, maana ananifahamu, ndio huyo aliyeniambia, kuwa mimi ndiye nilimuibia
mchumba wake..kiukweli, yeye alionekana mrembo kwa maisha aliyokuwa akiishi ya
mjini, mimi nimeshachakaa na maisha magumu ya kijijini, na kuzaa .
‘Ni wewe....?’ akauliza kwanza kwa aibu lakini baadaye
akabadilika na kugeuka kuangalia ndani, na kusema kwa sauti iliyojaa dharau;
‘Haya wewe bwana, kuna mgeni wako nje..’akasema na kuingia
ndani, na mimi nikaingia na kumkuta mume wangu akiwa na taulo kiunoni, kakaa
kwenye sofa, akageuka na kuniona, hakuonyesha ile dalili ya kushituka akasema;
‘Wewe mwanamke ni nani kakuambia uje bila taarifa, bila ya
kibali changu, nataka nikiinuka hapa haupo ..rudi huko, huko
ulipotoka..’akasema huku haniangalii usoni...’
‘Mume wangu niende wapi, ..wakati nimekuja kwako,
..nitapata wapi basi muda kama huu?’ nikamuuliza kwa adabu zile za kijijini,
huku moyo unaniuma kweli.
‘Utajua mwenyewe....kwani ni nani alikuambia uje,
nilishakuambia kuwa mimi sikutaki...unang’ang’ania tu kuwa wewe ni mke wangu,
hebu jiangalie wewe ulivyo, una hadhi gani, na shepu gani ya kuwa mke wangu,
...huoni aibu, eti kusema `mume wangu’, sikiliza rudi huko huko
ulipotoka,unasikia...’akasema na kusimama,
Mimi sikusogea nikasimama pale pale, na yeye bila kujali
kuwa kavaa taulo, akaanza kunisukumia nje huku yule mwanamke wake, akiniangalia
kwa nyodo kashikilia kiuno...sikuona taabu, awali nikapambana naye , lakini
mwanaume ni mwanaume,…akanitoa nje..nilikaa pale nje, kibarazani hadi
walipomaliza mambo yao, ...’akasema huku akitabasamu tu.
‘Ina maana hawakujali, na bado walikuwa wakiendelea na
starehe zao?’ nikamuuliza.
‘Yaani tena kwa karaha, maana walijua nipo hapo nje, na
mvua inanyesha..lakini kila kilichokuwa kikifanyika huko ndani, nilikuwa
nakisikia, kwa dharau..ili kunionyesha kuwa mimi sina maana..’nililowana, maana
kibaraza kilikuwa hakina sehemu nzuri ya kujificha, na walipomaliza starehe
zako, wakatoka wakaenda bafuni kuoga, wakavalia, wakaondoka, sijui
walipokwenda, nikabakia hapo hapo..nje,sijui niende wapi…nalia…nifanyeje sasa,
na kuja mjini nilipanga nije kupambana na hao wanawake wanaoniibia.
‘Bahati nzuri jirani yao, akanikaribisha ndani, akanipa
nguo nikabadili, akanipikia tukala, japokuwa chakula hakikushuka vyema, na huyo
huyo jirani yake ndiye aliyenisaidia nauli, kesho yake asubuhi nikaondoka
nikarudi nilikotoka,...hebu ona huo unyama, hata nauli hakunipa...nimesaidiwa
na majirani ambao waliniambia mume wangu kila siku anakuja ni mke mwingine...na
sijui kwa vipi hakupata ukimwi...’akasema huku akikunja uso.
‘Niliporudi kijijini, nikamsimulia mama yangu hayo
nailiyoyaona, akasema, hayo ndio yo niliyoyataka, waliniambia sikusikia, ni
kweli , walinisema sana, kipindi hicho, nilipoanza mahusiano na marehemu,
wazazi wangu walichapa sana, lakini sikuwasikia, na hayo yaliyokuja kutokea
nilikiri kuwa ilikuwa ni dhambi zangu ndizo ziliandama ngoja nipatilizwe, ...nilitubu
sana, nililia sana, lakini itasaidia nini…’akasema.
‘Niliishi kijijini kwa shida, hadi nilipokutana na huyo
mume wako....’akasema
‘Na mume wangu..!! ?’ nikauliza nikianza kuwa na hamasa
zaidi kwani huko ndipo nilipataka kufahamu ukweli zaidi wa mume wangu.
‘Ndio na …mume wako,…’akasema
‘Mkawa….eeh..’nikasema hivyo
‘Hahaha…mume wako kwangu namuona kama mdogo wangu, lakini
alinionea huruma sana, kwani alikuwa akiniona ninavyoteseka, yeye alikuwa
akihangaika na shughuli zake anapita kwetu ananiachia chochote,, huwa alikuwa
akiniita shemeji....basi ndivyo tulivyozoeana. Hakuwahi kupita hapo bila
kuniacha kitu.
‘Kuna kipindi niliumwa sana...karibu ya kufa, hatukuwa na
hata senti nyumbani, sina pesa ya kununua dawa, kwani nikwenda hospitalini na
kuandikiwa dawa za kununua, ...hatuna pesa, na tatizo hilo lilikuwa kubwa, hadi
nikaambiwa nikafanyiwe upasuaji, ..nipelekwe mjini, sina pesa, wazazi hawana
pesa , na mume wangu alipoambiwa hakujali..alitaka nife tu...’akatulia.
‘Namshukuru sana mume wako, nafahamu kipindi hicho, alikuwa
hajaku-oa...kama sikosei, akauza mbuzi wake, akapata pesa, na kuzileta
nyumbani, hatukuamini, akasema amekuja kunisaidia ili nikatibiwe...na kweli
nikapelekwa mjini nikafanyiwa upasuaji, nikatibiwa nikapona..sitamsahau mume
wako...’akasema.
‘Je alifanya hivyo kwa sababu gani hasa?’ nikamuuliza
‘Yeye, alisema alifanya hivyo, kwa vile mume wangu ni
rafiki yake ,mume wangu alikuwa akimfundisha fundisha ufundi wa magari,
..udereva,..unafahamu mambo ya kijijini, basi wakaivana, sijui zaidi ya hapo
ilitokeaje wakaivana kiasi hicho, kwahiyo yeye alinitambua kama shemeji , mke
wa rafiki yake, akanijali kihivyo.....na ujirani mwema tu...’akasema.
‘Kwahiyo kwetu sisi , kama familia, tunamthamini sana mume
wako, ni mtu mwema sana, mume wako ana roho nzuri , uliza huko kijijini, alipenda
kuwasaidia sana watu,..sio mimi tu, ..yeye alikuwa na tabia yake ya kupenda
kusaidia watu, .. japokuwa familia yao ina tabia ambayo wengi wanaiona sio
nzuri, baba yale ni mlevi kupindukia, na mama yake akawa hivyo hivyo....basi ni
familia ya shida, lakini yeye akawa anajibidisha na maisha yake, kuhangaika
kivyake..hadi hapo mlipokutana naye...’akasema.
‘Mhh, kweli umenifungua masikio, hayo yaliyokukuta ni
makubwa, mimi niliona nipo kwenye mitihani, lakini kumbe wapo wengine
wanakutana na mitihani zaidi ya unavyowazia, wewe ya kwako ilikuwa zaidi, sasa
ikawaje, maana muda umekwenda, kuna mambo ulitaka kuongea na mimi na mimi
nataka kujua…eeh..?’ nikamuuliza. Na sote tukageuka kuangalia kule mlango mwa
nyumba yangu, kulikuwa na jambo…
‘Sasa ikawaje…oh, namuona mume wako anatoka, nilionana naye
hapo nje wakati anaingia, tukaongea kidogo…ana haraka zake…?’ akasema,na ni
wakati huo mume wangu alikuwa akitoka na wakili wake, na aligeuka akatuona ni
kama vile ndio anatuona kwa mara ya kwanza, ikabidi sasa aje pale tulipokaa…..
....NB: Nimejitolea leo kuleta sehemu hii…Ni kisa mkasa,
lakini kwa huyu mama kuna mengi ya kujifunza, tutakuja kuona ilikuwaje kati ya
mama huyu na mume wake, na kwanini alifika huku mjini, je inaweza ikawa njia ya
kumfanya mdada abadili nia yake na kumsamehe mume wake..tuzidi kuwemo..?
WAZO LA LEO: Maisha yana mitihani yake, ukiona
kwako ni kugumu, ujue kuwa kuna wenzako kwao ni kugumu mara mbili zaidi yako,
ukipatwa na mitihani, ujue kuna wengine mitihani hiyo ni mazoezi tu ya
nyumbani(homework), kwahiyo ili uone uhalisia waangalie hawa waliopo chini yako,
ambao wanataabika zaidi yako.
Na ili uvuke huo mtihani waangalia walipo juu yako, jifunze
kutoka kwao,uwe na wivu wa maendeleo...usikate tamaa, pambana, lakini kwenye
njia iliyo sahihi, ukijua kuwa wewe sio wa kwanza kupata mitihani kama hiyo,
wapo waliopata mitihani hiyo na wakaishinda, kwanini wewe usiweze...kumbuka
jambo moja, kila kitu kila jambo lina ugumu wake, lakini baada ya dhiki, mara nyingi huwa ni faraja,
hasa kwa wale wenye kuvumilia na kujibidisha kwenye shughuli zao.., huku
wakimtegemea mola wao.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment