‘Ni mtoto wa marehemu Makabrasha anataka kuongea na mimi…’ nikamwambia wakili wangu naye akasema
‘Ongea naye ila fanya kama nilivyokuelekeza…’akasema
wakili.
Nikachukua simu yangu maalumu na kuhakikisha ina chaji ya kutosha.
******
‘Mkaribisheni kule bustanini, nakuja kuongea
naye…’nikamwambia binti wangu wa kazi, sikutaka kuongea naye ndani, kwani
sikuwa na amani naye kabisa, nilihisi kivuli cha baba yake kipo pembeni yake. Huenda mtoto kama baba, hulka hazitengamani
Walimkaribisha bustanini, na mimi nilipohakikisha kila kitu kipo sawa, nikamfuata huko bustanini, nikafika na kusalimiana naye,
sikutaka kumuonyesha jinsi gani nilivyochukia, maana moyoni niliona kuwa wao,
kutokana na baba yao, watakuwa wamepanga jambo la kuifisidi familia yangu, na nilitakiwa niwe makini kwenye kauli zangu kama alivyonishauri wakili.
'Karibu mgeni....'nikasema na alisimama na kusalimia kwa adabu tu, baadae sote tukaa kwenye viti, mimi ndio ni nikaanza kuongea;
‘Haya niambie una shida gani na mimi?’ nikamuuliza huku
nikimwangalia moja kwa moja usoni, maana tulikaa tukiwa tunaangaliana na kati
kati yetu kulikuwa na meza. Nilitaka nimuone usoni, kwani mtu unaweza kumpima
ukweli wake, au ujasiri wake, kwa kumwangalia usoni.
‘Samahani sana kwa usumbufu wangu, wa kutaka kuongea na
wewe...maana nimejaribu mara nyingi bila mafanikio, na leo nilipanga, kama
ikishindikana basi sitaondoka,maana...siku zangu za likizo zimeisha, natakiwa
kurudi kazini...Ulaya...’akasema.
‘Sawa pole sana,na pole sana kwa msiba, kwani sijapata hata
muda wa kukupa pole yangu..ila salamu za rambi rambi nilizifikisha kwa kupitia mume wangu , natumai ulizipata’nikasema
‘Hamna shida, nashukuru sana nilizipata, sina cha kuwalipa ila mola atawalipa zaidi, ….’akasema
‘Kiukweli imebidi iwe hivyo kutokana na hulka
zenu,..kiukweli japokuwa marehemu haongelewi vibaya, alichokifanya baba yako
kimenivunja nguvu, ..namafahamu sana kutokana na tabia yake, lakini sikutarajia
atakwenda kwa kiasi hicho,..sasa kauwawa, sijui ni nani wamefanya
hivyo….imezidi kunivunja nguvu, haya niambie ulikuwa unanitafutia nini, maana kila mara napaat ujumbe kuwa unataka kuongea na mimi..?’ nikauliza.
‘Mimi sina nia mbaya kama unavyofikiria wewe,..huenda
ungelisikiliza toka awali tungelishamalizana mapema tu, na kila mtu akashika hamsini
zake. Hapa nilipo nakwama kuondoka maana mambo mengi bado hayajakaa sawa, na mimi
nimeachiwa majukumu mengi na marehemu baba, na familia yote inanitegemea mimi,
kiukweli sikulipenda hili, lakini nitafanyaje....’akasema.
‘Hayo majukumu uliyoachiwa, yananihusu nini mimi, hayo si
mambo yenu ya kifamilia au sio…?’ nikauliza na yeye bila kujali swali langu
akaendelea kuongea.
‘Mhh..ni hivi, mimi nilipofika hapa Dar kutoka nje kutokana na kifo cha
baba...nilitarajia mengi, maana mimi namfahamu sana baba, yeye na mimi hatukuwa
sambamba kutokana na mitizamo yetu, hata hivyo yeye alinijali kama mtoto wake wa kwanza, na mamambo yake mengi aliyaweka wazi kuwa mimi ndite nitakuwa msimamizi wa kila kitu..’akatulia
kidogo.
‘Kifo chake kimenishtua sana, maana kuna mambo mengi
tulikuwa hatujawekana sana…sikuwa tayari kwa haya majukumu kabisa....lakini ndio hivyo, mapenzi ya mungu hayapingiki…’akashika
leso yake na kufuta machoni, lakini sikuona dalili ya machozi
‘Nilipofika kiukweli kwanza kabisa nilitaka kujua ukweli wa kifo cha baba, na
nilipewa taarifa yote kutokana na uchunguzi wa polisi. Na kwa matizamo wangu wa haraka kutoka na taarifa za watu hata kabla ya taarifa ya polisi,..nilihisi nyie mnaweza
mkahusika, ...na kiukweli kama mngelikuwa nyie mnahusika, ningesimama kidete
kuhakikisha haki inapatikana, bila kujali maagizo ya baba..’akashika kichwa, kama vile kinauma.
‘Sasa uchunguzi wa polisi unaonyesha tofauti, imeonekana
hauhusiki, na kwa kujirizisha, nikafanya uchunguzi wangu binafsi, na kuhakiki
taarifa niliyopewa, nikagundua kuwa mambo ni yale yale, hauhusiki..
'Sawa hausiki
kwa moja kwa moja, lakni bado nikawa na dukuduku, ni kwanini,…baada ya baada ya baba kuwa wazi kwenu, ndio kifo chake kitokee, hapo ulipa maulizo mengi, na sikupendelea sana kuunganisha haya na mambo ya kisiasa japokuwa hilo limebeba uzito wake , lakini kwa vile ushahidi waonyesha kuwa upende wenu haupo, sasa nihangaike nini tena na nyie...bado swali mpaka sasa ni kwanini…tuliache hilo hapo....’akasema.
‘Ngoja nije kwenye hoja...mimi ninamfahamu sana marehemu baba yangu, nafahamu sana
mbinu zake za kupata mali, baba ni mjanja na alichukua kazi hiyo ya uwakili
akijua kuwa itakuwa ni kinga ya ujanja wake…ni sawa kasoma, na kiukweli kaiva,
lakini kwanini asifanye kitaaluma yake zaidi, hilo mimi sijui, na hata tukikutana
naye huwa tunaishia kulumabana juu ya hilo.....’akasema.
‘Kutokana na tabia hizo, niliposikia kuwa baba kafariki cha kwanza nilichouliza kafa kwa kifo cha kawaida au kauwawa, nikaambiwa kapigwa risasi, nikajua tu ni yale yale, na nikauliza ni nani kashukiwa, nikaambiwa ni wewe..nikatamani sana kwanza nije niongee na wewe niujua ukweli.
'Unajua kazi za namna hiyo, tabia ya namna hiyo,..ni lazima ujue kuwa kifo chako kipo pembeni, mimi naishi
nje, na nimeona watu wa aina hiyo wanavyouwawa, bila kufa, watu uliowatendea hivyo hawawezi kuwa na amani, amani yao ni kufa kwako...’akasema
‘Blackmail,ni kazi ya hatari sana,
sio mchezo, kumghilibu mtu, na kupata kile alichokihangaikia kwa jasho lake kwa
shida, wewe uje ukichukue kilaini,sio rahisi kihivyo, sikuwa na ushahidi wa
moja kwa moja wa hilo, ila nishaambiwa na watu naa hata na polisi kuwa alikuwa akishukiwa hivyo…’akatulia
Nilitaka nimkatize lakini alikuwa akiongea kwa haraka sana, na nikaona nimuache tu aendelee..
‘Mimi nilikuwa sielewani na baba tangu niwe na fahamu
naye, japokuwa sikuwahi kuishi naye kikaribu hivi, maisha yangu, nililelewa na babu na bibi,
maana mama alikuwa akiishi huko ,....na hata nilipokuwa nasoma hapa nchini, nilikuwa kwa babu, baadae wakati nipo elimu ya juu, ndio nikapata muda kidogo wa kuishi na baba, hatukuwa tunaelewana, damu zetu hazikuendana kabisa....
‘Baba akataka nisomee uwakili, lakini mimi
siupendi uwakili mambo yangu sayansi, mitandao, komputa, ni hivyo,..ndio ndoto zangu, yeye aliona ni mambo ya tamaa yasiyo na umbele zaidi
'Mimi nikamwambia moja kwa moja baba, mimi sitaki kuja kutegemeamali zake nataka kuja kuishi maisha yanayotokana na juhudi zangu na dua zangu
zikakubaliwa, nikafaulu mitihani yangu, nikaomba kwenda kusomea nje ya nchi, na bahati nikapata nafasi hiyo ..’akatulia
akiangalia saa
‘Na nikuambie ukweli, kwenda kwangu kusoma nje, hakukuwa na
mkono wake, nilihangaika kivyangu, nikafanikiwa kivyangu, na huko nikasoma kwa
shida sana, na aliposikia nasoma kwa shida, ndio akanitumia pesa...nilizikataahizo pesa zake kabisa...nikamrudishia, hakuamini hilo, na akaniuliza kwanini, nikamwamba iweje sasa ndio ananijali, ..kwanini alinitelekeza utotoni mwangu, hayo yana storia yake…’akasema
Hapo nikamuuliza;
‘Kwanini ulifanya hivyo?’ nikamuuliza nikimwangalia
machoni, huyu mtu huwezi kumhisia vyovyote, hajionyeshi tabia yake usoni,..ni
watu wachache wenye tabia hii.
‘Kikubwa ni kuwa nilishamfahamu baba, nilijua pesa zake ni chafu na mimi sitaki pesa
chafu, ndio maisha yangu nilivyoamua yawe hivyo, wewe hujiulizi kwanini baba
alikuwa hakai na mama, mama ni mtu wa dini, na alifahamu tabia ya baba, akaona akae mbali na
yeye, na mimi kiukweli nimerithi tabia ya mama, japokuwa sijasomea mambo ya dini...ila mimi nataka niishi kwa jasho langu, sio kama
alivyokuwa akiishi baba...’akasema.
'Kwahiyo kwa kauli yako mwenyewe unakiri kuwa baba yako hakuwa mwaminifu au sio..?' nikauliza
'Ni kweli, mola amsamehe madhambi yake tu...hilo siwezi kukukatalia...'akasema
'Sawa endelea maana mpaka sasa sijakuelewa mimi nahusikanaje hapo ...'nikasema
‘Kifo cha baba, kikatufanya tukutane kama familia,
nashukuru sana kuwa wanafamilia wote walikuwa wakimfahamu sana baba, hakuna
aliyetaka kuingilia mambo yake, kila mmoja aliona kuwa akigusa huko huenda damu
za watu, dhuluma za watu zitawaandama. Mimi nikapewa jukumu la kusafisha jina
la baba, maana keshafariki sasa tutafanyaje na maisha lazima yaendelee, ..je tutaendelea kukumbatia
hiyo hali, au tutaishije.. ni lazima jambo lifanyika..’akatulia.
'Niliongea na mama, na mama akasema tusaidie japokuwa ...ili roho ya baba iwe na amani, na hilo..likawa jukumu langu la kwanza,...kuisafisha familia yetu na kuhakikisha kuwa hatueleweki vibaya, .....'akasema
'Kwa vipi sasa..?' nikajiukuta nimeuliza hivyo
‘Kazi yangu kubwa, ilikuwa kufuatilia kwa kila aliyeumia
kutokana na baba...wapo wanaojulikana, na tulitangaza kama kuna mtu kwa namna
moja au nyingine alipata athari, kutokana na utendaji wa baba ajitokeze,..watu
waliona kama ni utani,..mimi nikafanya kazi ya zaida ya kuwafuatilia kwa kila
niyekuja kuambiwa, au kuona kwenye kumbukumbu za baba...na ili hayo yafanikiwe,
tulimtafuta mwanasheria ambaye alisaidia kisheria....’akasema.
‘Sasa pamoja na yote...ikabakia wewe, kwa maana ya kisheria, sijui kama kuna baya aliwafanyia, sijui, ...ila kuna mambo ya kisheria, ambayo ni muhimu sana nikae na wewe tuone tutafanyaje, nielewe sana nimechukua muda mrefu wa maelezo ili uelewe dhamira yatu….’ Hapo sasa akaniangalia usoni
moja kwa moja.
'Mambo gani hayo ya kisheria..?' nikauliza
‘Kwanza nianze kwa kuingilia ndoa yako, niligundua kuwa …wewe na mume wako hampo sawa, hilo sihitaji wewe kukubali, ila nilipoongea na baba ...mume wako hata bila kuniambia nikaligundua..lakini kuna mikataba imeachwa, inakuhusu wewe na mume wako, inahusu mali nk...unajua mimi sikutaka hata
kuingilia undani wake, nikawa nimeongea na mume wako kuwa kama kuna lolote baya
ndani yake aniambie tuachane na mikataba hiyo kabisa…’akatulia
‘Mume wako akasema kila kitu kipo sawa, na,yeye
atasimamia kama ilivyo..,..sasa pamoja na huo mkataba, eeh,..unajua nikuambie ukweli mimi
namfahamu sana mume wako mimi namtambua kama baba yangu mdogo, kwa jinsi familia yao
na yetu zilivyokuwa karibu, na baba yangu na mume wako walikuwa marafiki sana
japokuwa baba yangu alikuwa mkubwa kwa mume wako.
‘Kwahiyo nilitarajia msaada mkubwa kutoka kwake, na
kiukweli sikutaka mimi nifanye lolote kwa jinsi mkataba unavyosema bila ya ushauri wake..na sio ushauri wake tu, ila kiukweli mimi sikutaka kabisa..nilimuambia uwanja huo mume wako, afanye anavyoona ni sahihi…’akatulia
‘Kiukweli kwa jinsi mkataba unavyosema kama sisi
tungelikuwa ni watu wa tamaa, basi tungelifaidika sana na vitega uchumi mlivyo
navyo nyie..., maana sisi ni warithi halali wa baba na mkataba unasema wazi warithi wa
mali yake ni nani,…kuna kumiliki hisa zake ndani ya kampuni ya mume wako, na
mume wako anadaiwa pesa nyingi na mkataba unasema hivyo, na ulibaisniha kuwa malipo ya deni hilo ni kupewa hisa zaidi kwenye kampuni ya mume wako, na zaidi pia kuna mkataab mwingine kuwa marehemu anatakiwa kupewa hisia kwenye kampuni yako, kwa kupitia kwa mume wako,....’akasema
‘Matapeli wakubwa nyie....Huo mkataba upo wapi?’ nikamuuliza hapo na nikagundua kuwa nimekiuka ushauri wa wakili, lakini hasira tena
‘Huna haja ya kukasirika, nikuambie tena, sisi hatuna nia mbaya na nyie,..na huo mkataba ninao, kila kitu kipo wazi....’akasema
‘Nautaka huo mkataba niuone kwanza...’nikamwambia.
‘Bado anao mwanasheria wetu, ....’akasema
‘Anao kwa ajili gani sasa?’ nikamuuliza
‘Kuna mambo bado hayajakaa sawa, na hili linatokana na mume
wako, kama mume wako angelikubaliana na sisi, basi tungelishamalizana, na
kuhakikisha kuwa tatizo hili limekwisha kabisa,...’akasema
‘Mambo gani hayo mume wangu hajakubaliana na nyie?’
nikamuuliza
‘Kuna vipengele vingi vipo humo, vikionyesha kuwa mume wako
ndiye anamiliki kampuni yake na yako kwa asilimia fulani za hisa, lakini katika
mkataba aliouacha baba , kuna kipengele walishindwa kukubaliana, kwa idadi ya hisa, kwa maana kuwa wewe kama mshirika, hujaridhika...’akasema
‘Kipengele gani hicho?’ nikauliza
‘Kutokana na deni lilivyo, baba alitaka kumiliki zaidi ya aslimia hamsini ya hiza za
kampuni ya mume wako, na pia kwa vile
baba atakuwa anamiliki zaidi ya asilimia hamsini yeye alitaka hata jina la
kampuni libadilike....na hapo kukatokea sintofahamu, nahisi hata kifo cha baba
kilitokea siku walipokuwa wakibishana kuhusiana na hilo, japokuwa walikuja kukubaliana kuwa jina libakie hilo hilo...’akasema
‘Wewe umejuaje hayo, na wakati hukuwepo....?’ nikamuuliza
‘Baba alikuwa na kawaida ya kuhifadhi kumbukumbu za matukio
yote, ..tulichokuja kuona ni ajabu ni kuwa mle ndani kwenye hicho chumba ofisini
kwa baba kulikuwa na kifaa cha kunasia matukio, lakini sehemu kubwa imefutwa,
kwahiyo haikuweza kuonyesha tukio la kupigwa risasi kwa baba, sehemu hiyo
haipo, ina maana huyo muuaji, alirudi na kufuta sehemu hiyo, na ina maana kuwa
huyo mtu anafahamu siri nyingi za baba.
'Mimi ni mtaalamu sana wa komputa, nikafanya mambo yangu,
nikagundua sehemu ndogo iliyofutwa, inayoonyesha jinsi ya kifo cha baba kilivyokuwa,
lakini kwa bahati mbaya sikuweza kuipata sura ya huyo muuaji, au umbile lake
kwa ujumla zaidi ya kichwa kilichojitokeza na mkono uliokuwa umshika bastola,
ndio nikagundua kuwa aliuwawa na watu wake waliokuwa hawaelewani
naye...’akasema
‘Ni watu gani hao?’ nikauliza
‘Imeshindikana kuwagundua ni akina nani, naomba iendelee kuwa hivyo, na kwa vile huyo muuaji
hakuonekana sura, ...na alitokeza kidogo tu, kiasi cha kuweza kulenga
shabaha..na, kwa vile alikuwa kavaa kitu usoni, na
kuacha macho tu,hata polisi hawajafahamu sehemu hiyo,…’akasema
‘Ina maana polisi hawakupata hiyo video…?’ nikauliza
‘Polisi walipata sehemu hiyo ambayo haionyeshi lolote, ila
mimi kwa vile ni mtaalamu , ndio nikagundua hiyo sehemu iliyokuwa imefutwa,…lakini pia kuna kumbukumbu za baba
nilizokuja kuzigundua zilikielezea watu mbali mbali, lakini hazielezei uhasimu
wowote, ila kuna vitisho vya hapa na pale,..ikiwemo wewe na wengineo, sasa nani ni nani..sikutaka
kuendelea zaidi, hilo niliwaachia polisi.
‘Sasa ulipofanya utundu wako na kuligundua hilo, uliwafahamisha polisi?’ nikamuuliza
‘Hapana, na nina sababu za kutokufanya hivyo…’akasema, na kunifanya
nishangae kidogo,
'Oh, kwanini...?' nikamuuliza
‘Kwasababu kuna sehemu inamuonyesha mume wako...'akasema na kunifanya nishtuke
'Mume wangu, kwa vipi...?' nikauliza
'Ndio mume wako yupo kwenye hiyo kumbukumbu ya video ya matukio, yaliyotokea siku ile,..., na polisi
wangeliona hiyo sehemu mume wako angelikuwa kwenye hatia, mtu mwenyewe mbovu,
halafu ashikwe na kuwekwa ndani itakuwaje...niliona ni heri tu ibakie hivyo
hivyo, kwa vile sio yeye aliyefanya hayo mauaji…’akasema
‘Mimi sikuelewi hapo mume wangu… hapo kuna
makosa, unajua kipindi hicho mume wangu alikuwa kalazwa hospitalini, anaumwa, ataonekanaje kwenye hiyo
video ya matukio, uliyoiona humo ndani, usije ukatumia ujanja wa kimtandao, na
kumweka mume wangu…?’ nikauliza kwa mshangao
‘Siku huyo mume wako alikwenda kumuona baba, marehemu baba,
ndivyo inavyoonyesha, sasa alifikaje na kwanini, hilo kwangu sio muhimu, ila
kwenye hiyo video ya matukio, mume wako alionekana akibishana na baba, ipo wazi
kabisa, na walikuwa wakibishana kuhusu mkataba…’akasema
‘Mkataba gani huo…?’ nikauliza.
‘Kuna mkataba wa hisa za kibiashara, nina Imani umeshalipata
hilo kuwa baba ana hisa kwenye kampuni ya mume wako, na huo mkataba ulikuwa
unaelezea hayo…’akasema
‘Hebu samahani kidogo, kwanini baba yako awe na hisa kwenye
kampuni ya mume wangu, na unafahamu wazi kuwa kampuni ya mume wangu inatokana na
wazazi wangu ndio wao walimpatia mume wangu mtaji…?’ nikauliza
‘Hiyo ni historia ndefu kidogo, ila hapo kwenye matukio, ilisikika marehemu akimuambia mume wako kuwa anadaiwa pesa nyingi tu na baba, …’akasema
‘Pesa nyingi kiasi gani cha kupewa hisa nyingi hivyo, ni
hayo malipo ya uwakili wake, kwani hayo malipo yalikuwa kiasi gani..?’
nikamuuliza.
‘Kama nilivyokuambia awali hiyo ni historia ndefu kidogo
nahisi kuna zaidi ya hilo, na mume wako analijua zaidi,..ila mimi naongea kutokana na
ilivyosikika kwenye video, kuna maongezi kuwa mambo mengi kuhusu kampuni ya
mume wako yalitokana na juhudi za marehemu baba, na tangia awali baba aliwekeza kiasi
cha hisa ndani ya kampuni hiyo kwa siri, sasa alitaka iwe bayana kwenye huo mkataba, sasa mpaka
kufikia kiasi hicho kikubwa cha hisa..hilo utamuuliza mume wako....’akasema.
‘Hapo sizani kama ninaweza kuelewa,..ni udanganyifu mkubwa tu
huo, kampuni hiyo ilianzishwa kwa mkopo
kutoka kwa wazazi wangu,na mpaka leo huo mkopo haujalipwa sasa iweje marehemu
ajiingizie huko,…lakini… anyway, endelea....’nikasema.
‘Siku ile mume wako, alifika kwa baba, alionekana ana
haraka, na mashaka, na alionekana mwenye maumivi nahisi ni kutokana na kujilazimisha kupanda ngazi au kitu kama hicho, sijui labda kuna mtu alimpatia msaada,... ila yaonyesha keshaingia amekaa kwenye kiti wanatoleana
mikataba..’akasema
‘Je mumeshaongea na mume wangu kuhusu hayo uliyoyagundua, kuwa wewe unayafahamu hayo yote..?’
nikauliza
‘Anafahamu kama ilivyo kwenye mikataba, lakini hafahamu kuwa mimi nimegundua kilichotokea siku ile baba alipouwawa..hilo sijamuambia,… ...haya hayafahamu mume wako na mpaka leo nikimuuliza kuwa aliwahi kuonana na baba siku ile ya tukio, ananikatalia,...kwahiyo yeye hayajui kama walivyo polisi, nimeona nisimuambie…’akasema
‘Kwanini…?’ nikauliza
‘Mume wako hana tofauti na baba kwa tabia zao, za tamaa ya mali, bila kujali uhalisia wake, iwe dhuluma au halali kwao ni sawa, nawafahamu sana kwa hilo, na sisi hatutaki kuwa miongoni mwa hilo, na nina amani kama tungelimuambia angetukataza kabisa kuliongelea hilo kwako, sis hatutaki uhasama, sisi tunataka kulimaliza hili kwa njia ya heri…’akasema
na sikumuelewa hapo lakini nikaona nisubiria kwanza, nikasema
‘Ehe ilikuwaje sasa maana hapa unaongea wewe, siwezi
nikakuamini mpaka nione huo ushahidi…’nikasema
‘Nitakuonyesha kila kitu madam, ila mpaka huo muda ukifika…’akasema
‘Muda gani…ukifika..?’ nikauliza sasa kwa mashaka
‘Ngoja kwanza nikuelezee ilivyokuwa, au hutakii kujua zaidi…’akasema
‘Haya elezea…’nikasema
‘Basi mume wako alipofika wakaanza kuongea, na nahisi siku hiyo walipanga iwe
ni kuhitimisha makubaliano yao, nahisi kuna mambo yalikuwa hayajawa sawa kwani
kuna sehemu marehemu alimuulizia je mke wako kakubali, na mume wako akasema
haina shida, yeye tu anatosha, kwa vile mkataba upo wazi, na kukawa na
kubishana kwa hilo na baadae marehemu akasema…’a hapo akautulia kidogo
‘Pamoja na hili kuna mambo ya kibenki, hayo hatuna ujanja
nayo je una uhakika utaweza kumshawishi mke wako..na mume wako akasema, muda utasema kwanza wamalizane na hilo la mikataba,....’ hiyo ilikuwa ni kauli ya
marehemu na mume wako, ipo wazi...
‘Sasa kuna mambo mengi walijadiliana hapo, hayo utakuja
kumuulizia mume wako, lakini nakuomba kwa hili nililokuambia usimuambie kwanza
mume wako, utakuja kuharibu kila kitu…muhimu kwako kufahamu ni kuwa mume wako
baadae waliwekeana sahihi rasmi kuwa hisa za marehemu zitakuwa kiasi gani, na za mume wako kiasi gani, ni unu kwa marehemu na iliyobakia sehemu ni yako na ya mume wako, kama minajili jhiyo baba anakuwa ana hisa kubwa zaidi na anakuwa maamuzi zaidi, hapo sijui ni kwanini..’akasema
‘Mhh,hayo yote yanaonekana kwenye hiyo video…?’ nikauliza
‘Ndio…kila kitu kipo wazi, lakini hayo hayaonekani kwenye
ushahidi walio nao polisi..sijui kama wana utaalamu kama niliufanya mimi hadi
kuligundua hilo na kama wangelikuwa nao basi mume wange angelishakamatwa, au sio…’akasema
‘Hiyo video sio ya kugushi kweli…?’ nikauliza
‘Kuna vitu vya kugushi,…madam,.. lakini sio vitu kama
hivyo, unaweza kwenda kwa wataalamu wakakuthibitishia hilo, lakini naomba hili
liendelee kuwa siri kati yangu mimi na wewe…’akasema
‘Sawa endelea…’nikasema
‘Basi, walipomaliza, na wakati wanapeana mikono ya
kuagana, ndio hapo tukio la mauaji likajitokeza…’hapo akatulia kidogo
‘Mara mlango ulifunguliwa kwa ghafla…lakini mtu hakujitokeza,
marehemu akawa anauliza wewe ni nani… na mtu aliyekuwa kajifunika sehemu zote
za usoni,akajitokeza kichwa tu usingeliweza kuiona sura yake, na hapo
hapo akampiga baba risasi, kifuani kwenye moyo, na baba akaguna na kuwea kichwa mezani, nahisi alifariki hapo hapo..’akatulia kidogo.
‘Kwanini sasa usiwape polisi huo ushahidi ni muhimu sana
kwangu, maana mpaka sasa sijasafisha jina langu kuwa mimi sihusiki na mauaji
hayo…’nikasema
‘Watu hao walitaka kumuua na mume wako…lakini wakati huyo
muuaji anataka kufanya hivyo, ikasikika sauti ya mtu akiita kwa nje, kuwa
waondoke wapo kwenye hatari ya kukamatwa, ndio hapo mlango ukafungika, lakini
kidogo hapo, kabla ya kuondoka, huyo muuaji alirusha hiyo bastola kwa ndani....’akasema
‘Ikawaje maana mume wangu alikuwa humo ndani …?’ nikauliza
‘Ukiangalia hiyo sehemu utaona vyema jinsi gani mume wako
alivyochanganyikiwa, kuonyesha kuwa hakuwa anafahamu hilo tendo, labda kama
alihusika,...maana ungelisema labda ni mtu wake, aliyempanga kuja kufanya
hivyo, lakini utajiuliza kwanini..ili iweje,…na ukiangalia ilivyo, utaona
kabisa mume wako hakuhusika, alicvhanganyikiwa, akawa anahangaika huku na
kule..na kama ni yeye, basi angeliondoka na hiyo mikataba, lakini hakukumbuka
kuichukua wakati anatoka kukimbia…’akasema.
‘Bado hapo …’nikasema
‘Ni hivi huyo jamaa alitokeza kichwa, na mara ikasikika tufu
tufu…risisi zikimpiga marehemu, yeye akainama na kuweka mikono usoni
hivi..yaani kichwa kakilanza mezani huku kaweka mikono kuzuia machoni,…, kama
vile mtu anavyoogopa kupigwa na yeye,
Alikaa hivyo kwa muda hadi hao watu walipoondoka..baadae
ndio mume wako akainua kichwa taratibu, halafu akageuka kuangalia mlangoni, akajihakikishia
kuwa yupo salama, sasa ndio akamtizama marehemu akagundua kuwa marehemu
keshafariki..
‘Utaona jinsi gani alivyochanganyikiwa, akawa anahangaika,
akishindwa afanye nini...baadaye, sijui alijiwa na wazo gani, akafungua mlango,
na kutoka nje, hapo alikuwa akitembea kwa shida sana, ni kama alitojitonesha au
hali..inaonekana hivyo,...huwezi kuona kitu nje ya chumba, sasa sijui
alivyoweza kutembea hadi kutoka eneo hilo…’akasema.
‘Kwahiyo wewe unasema sura ya huyo muuaji haikuonekana, na
huyo mtu alitaka kumuua pia mume wangu, inaonyesha hivyo, na inaonyesha kweli
kuwa mume wangu hahusiki au sio…na huyo mtu hajulikani kuwa ni mwanamke au ni
mwanaume?’ nikauliza
‘Haonekani, huwezi kufahamu...'akasema
‘Bado mimi najiuliza ni kwanini usiwaonyeshe polisi, maana ingewasaidia kujua
zaidi?’ nikamuuliza.
‘Tunafuata maagizo ya marehemu baba, licha ya kuwa sikuwa na
mahusiano mema na yeye, lakini nakumbuka jinsi alivyokuwa akiniambia kuwa kwa
vyovyote itakavyo kuwa awe hai au mzima, mume wako nimuheshimu kama baba yangu
mdogo, kwani amewahi kumsaidia sana katika maisha yake na sisi tumlinde na
kumsaidia..’akasema
‘Ok…’nikasema hivyo
‘Na ..hata mimi alinisaidia sana mume wako nikiwa mdogo..na
alimsaidia sana mama, kipindi mama alikuwa anaumwa sana, hana pesa, yeye
alijitolea kuuza mbuzi wake, aliyekuwa naye, mmoja, kwa ajili ya kumtibia
mama,...mimi nilimwahidi baba kuwa mume wako atakuwa baba yangu mdogo, na
sitaweza kumvunjia heshima. Hili niliahdi na ndio maana nayafanya haya…’akasema
‘Sijakuelewa hapo, ina maana hata kama itaonekana kuwa yeye
ni mhalfu, utamtetea tu, na huenda akahusika na kifo cha baba yako?’
nikamuuliza.
‘Mume wako hahusiki na kifo cha baba yangu, hilo nina
uhakika nalo...usuhuba wao ni wahali ya juu, kifo cha baba kimemuumiza sana
mume wako, ..wewe hujui tu, marehemu baba alikuwa ndiye kichwa cha mume wako,
kila uliloliona mume wako akilitenda lenye tija…, mara nyingi, alikuwa akifuata
ushauri wa baba...’akasema.
‘Hata kuzaa nje ya ndoa?’ nikamuuliza
‘Kuzaa nje ya ndoa…haaah, nani kasema?!’ akauliza kwa mshangao kidogo
‘Unajifanya hulijui hilo…kama kweli yote aliyokuwa
akiyafanya baba yako kuwa anaweka kumbukumbu nina Imani hata hilo lipo, au
sio…?’ nikauliza
‘Kuna mambo mengi nimeyagundua ya baba, lakini hilo,...mmh...lakini nikuambie kitu, nataka haya tuje kuyamaliza...kuna mambo mengine siwezi kukuelezea kwa sasa mpaka hapo tutakapokuja kukubaliana, ndio maana nimekuja na maombi yangu kwako...’akasema
‘Maombi gani?’ nikamuuliza
‘Kwanza na lenye muhimu nakuonmba umsikilize mume
wako...mkubaliane naye..mkisha kubaliana naye , mkawa kitu kimoja,basi sisi
tutajitoa kabisa kwenye huo mkataba ulioandaliwa kuwa baba alikuwa na hisa, hatutaki hizo hisa, lakini huwezi kuziondoa kihivi hivi, ni mambo ya kisheria au sio, ...’akasema
‘Hahaha..nilijua tu…’nikasema
‘Ninasema hivyo kwa moyo safi , nielewe madam..., sina shida na mali
zenu kabisa, hatuna shida na mali za dhuluma…ila mimi nina deni kwenu, maana
kama kuna pesa zilitoka kwenu, zikanisaidia mimi, natakiwa nifanye lolote
kulipa fadhila au sio..sasa furaha yangu ni kuona wewe na mume wako mnaishi vyema.
'Hilo halikuhusu au..kwanini unataka kuingilia ndoa yanu...?' nikamuuliza
‘Kwa kifupi madam, sisi hatutaki kujihusisha na ndoa yako au mali zenu,
hatutaki kupata mali isiyo halali,...lakini tunahitajika kumsaidia mume wako,
kwani ...wema wake kwetu ni mkubwa sana, ndio mume wako ana tabia kama hizo..., lakini ni
mwepesi kujirudi, nampenda sana kwa hilo, sio kama baba, baba alikuwa haambiliki, sasa
tunakuomba umsaidie mume wako, nina Imani atajirudi na mambo yenu yatakuwa
sawa,...hata ukiongea na mama atakuambia hilo…’akasema.
'Mama yako sio...yupo...?' nikauliza
'Yupo ndio, kaja kwa ajili ya huo msiba, wapo wanafamilia karibu wote...'akasema
Mimi hapo kwanza nikatabasamu moyoni nilihisi kupata jambo la kunipa faraja, japokuwa bado nilikuwa sijawa na uhakika, maana hayo ni maongezi tu, ushahidi upo wapi,..nikajaribu kumuangalia huyo jamaa usoni kwa makini
sana, kama nilivyokuambia sio rahisi kumtambua huyu mtu hisia zake kupitia usoni je ni mkweli au
ni muongo, na baadae nikasema;
‘Naweza kuonana na mama yako.....nataka niongee naye ?’
‘Kuonana na mama yangu sio tatizo na mkiongea naye atakuuliza kama umekubaliana na mimi, na mimi ndiye muamuzi..sasa nataka kauli yako kuhusu ombi langu, je upo tayari kushirikiana nasi ili tulimalize hili jambo, ni muhimu sana
kwangu?’ akauliza.
‘Kwanza nataka niongee na mama yako…..’nikasema, na mara
gari la mume wangu likafika, nilimuona yupo na mtu ndani ya gari, nikagundua kuwa ni wakili wake.
NB: Inatosha kwa leo
WAZO LA LEO: Urafiki ni mzuri, unajenga mahusiano
mema, lakini tujaribu kuangalia aina gani ya marafiki zetu,kuna marafiki
wengine wanaweza wakawa ni sumu ya maisha yatu, kutokana na tabia na matendo
yao..utawafahamu kutokana na hulka na matendo yao, hao sio marafiki, hata kama
mumeshibana vipi,…ikiwezekana ni bora utengane nao kabisa, kwani ukiungana nao,
hata kama hutafanya wanachokifanya wao, lakini ubaya wao unaweza kukuleta
matatizo kwani ukikaa na muuza uturi, utanukia uturi....au sio?
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment