Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, December 29, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-46




Kiukweli ndoa yangu ilianza kuwa na wakati mgumu, na ikafikia mahali nikaona nianze kufanya yale ambayo sikutaka kabisa kuyafanya katika maisha yangu, na katika ndoa yangu, na hata ikafika mahali sasa nianza kuamini kuwa mume wangu hakuwa mwaminifu kwangu, kifupi kasaliti ndoa yetu, lakini bado nilitaka nisikia kauli yake mwenyewe akikiri ..

‘Nimetoka hospitalini, lakini sina amani..’nikasema

‘Kwanini mke wangu, …upo huru, hiyo kesi isikutia mashaka, haina nguvu, mimi nitaifuatilia na kuhakikisha imekwisha…’akasema

‘Sio kuhusu kesi,…ni kuhusu hayo yaliyosababisha hadi tufike hapa tulipo, sijafahamu ukweli wake bado..’nikasema

‘Kama yapi..eeh, niambie mke wangu nitakuambia kila kitu..’akasema

‘Kwa hili ilivyo yaonyesha wazi, kuwa wewe umenisaliti,..umeenda kinyume cha makubalianio yetu, na nilikuambia tokea mwanzo, kuwa tunaoona, lakini tuchunge milaka ya ndoa yetu, nikakuuliza je kweli unanioa kwa mapenzi au kwa mali, unakumbuka ulisemaje…?’ nikamuuliza
‘Kwa mapenzi…nilikahidi na ni kweli…’akasema
‘Sivyo ilivyo, kidogo kidogo inaanza kudhihiri..naanza kuhisi kuwa huenda nilifanya makosa, naanza kuuona ukweli wa wazazi wangu…’nikasema

‘Lakini sasa mke wangu ulitaka mimi nifanye nini, tuangalia ukweli na uhalisia, mimi sio mume wako…eeh, hebu angalia maisha tuliyokuwa tukiishi je kweli mimi nilionekana kama mume wa familia, swali ni kwanini mpaka ikafikai kubuni hiyo mikataba, wangapi wana hiyo mikataba kaam mume na mke eeh…’akasema

‘Jibu na swali lakini ni kuwa nilitaka kuwe na kitu cha kuhakikisha kauli yako, maana wazazi wangu walisema mengi, kukuhusu wewe, na sio kukusema tu lakini rejea maisa yako ya nyuma yalivyokuwa na zaidi nilitaka kuhakiki kauli yako, na sasa je umetimiza ahadi yako…?’ nikamuuliza

‘Mke wangu ulitaka nifanye nini zaidi ili uonye kuwa mimi nimetimiza ahadi yangu, nimekuwa mwanaume mtiifu kwako, kila utakacho mimi nakifanya, lini nilikukaidi eeh, na wewe je..umetimiza kila nilichokitaka..sema ukweli wako…’akasema

‘Kitu gani ulitaka kutoka kwangu mimi nikakukatalia,…?’ nikamuuliza

‘Mke wangu karibuni hapa, nimekuomba ukubaliane na mikataba , tukianzia na huo ulioubuni wewe mwenyewe, umekataa…huo ni mfano tu, haya maisha ya ndani ya familia, nilikuomba tujitahidi tupata motto mwingine,…mungu angejalai tupate sasa wa kiume, uli…ulileta vipingamizi..sasa ulitaka mimi….’hapo akatulia.

‘Kuhusu mkataba, hilo sitaweza kukubaliana na lo, huo mkataba wa kugushi mimi siutambui,, unasikia,…na hilo ni muhimu katika mustakabali wa maisha yetu, usiporejesha huo mkataba wa zamani, basi ….’nikatulia

‘Mkataba mkataba…unaona mke wangu, huo ndio unaona ni muhimu kuliko ndoa yetu au sio..’akasema

‘Mkataba huo ulikuwa wa hiari, tulikubaliana sote, ukakubali mbele ya wakili, kwanini ulikubali, na kwanini sasa uupinge, na kwanini ugushi ..ina maana kuna jambo umelifanya lipo kinyume na mkataba …na huenda kinyume na ndoa yetu..’nikasema

‘Mkataba ulitusaidia sana tokea awali, maana ndani ya huo mkataba tuliweka yote ambayo yatamlinda kila mtu, na kulinda mali zetu kwa ajili yetu na familia zetu, na hili nilitaka kuwaonyesha wazazi wangu kuwa wewe kweli umebadilika, nilitaka kujithibitishia hilo mimi mwenyewe …ili niishi kwa amani…’nikasema

‘Hebu mke wangu tusilumbane zaidi, mimi nakuuliza hivi kwani kuna tatizo gani.

‘Tatizo ni kuwa wewe hutaki kuniambia ukweli, …’nikasema

‘Ukweli upi mke wangu..?’ akauliza

‘Najua hutaweza kuusema wote, nafahamu kuwa hapo ulipo unajiaminisha kuwa vyovyote itakavyokuwa mkataba wa kugushi utalikulinda, lakini hebu fikiria, je ulichofanya ni sahihi, je sio kweli kuwa umeisaliti ndoa yako, na bado, hukutaka kutubu, ulichofanya wewe ni kutafuta mbinu za kunufaisha matamanio yako,…’nikasema

‘Mke wangu kumbuka, kule hospitalini,nilifanya nini..sikukuomba msamaha mie.. ukasema umenisamehe…’akasema

‘Kwa kosa gani sasa…?’ nikauliza

‘Makosa yote ya kibinadamu, mimi sio malaika, mimi ..ni mwanadamu tu, nateleza, sasa siwezi kusema kila kosa nililolofanya, ..unajua mke wangu, eeh mimi ni mtu mnzima, kuna makosa mengine nilifanya kwasababu maalumu,..japokuwa huenda wewe unaweza kuona sio sahihi, lakini nilikuwa na sababu ya msingi sana…’akasema

‘Makosa kama yap hayo ya msingi kwako,…?’ nikamuuliza

‘Hilo ni moja ya mambo ambayo nahitajia kukaa na wewe , najua utanielewa, vuta subira, lakini nakuhakikishia sio kwa nia mbaya kabisa, ni katika kuhakikisha ndoa na mali zetu zinabakia mikononi mwetu, wewe hulijui hilo kwa vile umefunikwa na …wazazi wako…’akasema

‘Je ni kweli kuwa umenisaliti…?’ nikauliza

‘Kwanini unasema hivyo mke wangu, hapana sijakusaliti kwa maana hiyo unayoitaka wewe, najua kwako wewe utaona ni makosa, lakini mke wangu nilifanya hayo nikiwa na sababu za msingi, sikufanya hayo kwa kupenda kwangu, ..najua labda hutaweza kunielewa, ndio maana nikakuomba msamaha..’akasema.

‘Nikuulize tena je ni kweli kuwa una mtoto nje ndoa..?’ nikaona nimuulize hivyo

‘Mtoto nje ya ndoa una maana gani mke wangu, …unajua nilishakuambia kuna mambo mengine nisingelipeda kuyaongea kwa sasa, kwa sababu yanaweza kuleta picha mbaya, kutokana na ushauri wa wakili wetu, alinishauri marehemu na sasa huyu wakili mwingine hayo yanahitajia , tukae tuyajadili mbele yake, ili kila kitu kiwekwe sawa…’akasema

‘Sizani kama tutakuja kuelewana…mimi nasema hivi, nataka ule mkataba wa awali kama kweli una nia njema, ..na ukiwepo, nitakaa na huyo wakili wako, …vinginevyo, kuanzia sasa sitaki maongezi na wewe…’nikasema na kuondoka kuendelea na shughuli zangu.

***********
Pamoja na hayo aliyoyafanya mume wangu kugushi mkataba, lakini kuna kitu walishindwa..na hapo ikabidi kila mara aje kwangu kuniomba na kila akija kwangu tunaishia kwenye malumbano tu…

Siku moja akaja na kuniomba tukae tuongee, mimi sikuwa na shida, kuongea tu, ..

‘Mke wangu kuna mambo yanakwama, hatuwezi kufanya mambo ya maendeleo..’akasema

‘Mambo gani…?’ nikamuuliza

‘Ya kibenki…’akasema

‘Kwani kwenye huo mkataba wenu wa kugushi, hamuwezi kufanya na hilo…?’ nikamuuliza

‘Mke wangu…’akataka kusema

 ‘Kama unataka tuelewane, rejesha ule mkataba wa awali, hapo tutakaa meza moja kama mke na mume, lakini kama utaendelea na mkataba wenu huo wa kugushi, basi, nitakuacha uendelee na maisha yako na mimi nitaendelea na maisha yangu...’nikasema.

‘Hapana, siwezi kukubali hilo, mimi ni mume wako na mimi ndiye kiongozi wa familia, na natakiwa kuhakikisha familia yangu ipo pamoja, ...nataka watoto wetu watuone tuna upendo na mshikamano,..’akasema.

‘Wewe ndiye uliyesababisha haya yote, kashifa imeingia kwenye familia  , tumeanza kwenye ulevi, ndoa isiyo na masikilizano, ..kuzaa nje, imekwenda hasi kushutumiwa kuua, kugushi, ulaghai, hivi hayo ni maisha geni unayoyataka wewe, mimi sijakulia kwenye maisha ya namna hiyo, familia yangu ni safi....’nikasema

‘Ina maana unaninyanyapaa kuwa familia yangu ni chafu, ndio maana haya yote yanatokea?’ akauliza

‘Usiongelee kuhusu familia yako ongea kuhusu wewe mwenyewe,...kwasababu wewe una uwezo wa kujibadili na kuwa mtu mwema, mwaminifu, mkweli ....unaweza kabisa, lakini kama unataka kuishi kwa ujanja ujanja...hutafika mbali...’nikasema.

‘Mke wangu mimi kama mume wako, naomba kauli hiyo, ya kuiniona mimi mchafu, tapeli mlaghai,..iishie,tafadhali, maana sasa unataka na mimi niwe mkali eeh,  ..’akasema huku akinitolea macho, na mimi nikatabasamu na kusema;

‘Itaisha pale utakapoleta mkataba wetu wa awali, tuliokubalina kwa ridhaa moja,....’nikasema.

‘Mkataba ni mmoja tu, hakuna mkataba mwingine, mkataba ni ule ule,...ila wewe unataka kunipanda kichwani, ili nisiwe na sauti kama mume..hili mimi siliafiki,...na nakuomba mke wangu, jaribu kuniangalia na mimi, unielewe na mimi...kwani nimefanya nini kibaya’akasema kwa sauti ya upole.

‘Wewe sio mkweli, ...’nikasema

‘Kwa vipi, mbona nimekuambia ukweli, kuhusu mkataba wetu, ...sijaukiuka, ..kuna jingine  mke wangu, hakuna, nimejaribu kuwa mume mwema, silewi tena, hilo huliungi mkono, unataka nianze kuelewa tena, unafahamu madhara ya kulewa, eeh, unataka nikafanya nini sasa...’akasema.

‘Usibadili mada, mkataba wetu wa zamani upo wapi,..pili huyo mtoto uliyezaa nje ni nani, na umezaa nani, nijibu hayo maswali, na hayo ukiyaweka wazi, tutakubaliana, ...’nikasema.

‘Mkataba hauna shida, mkataba ndio huo, mimi sijui mkataba mwingine, na ni nani huyo mtoto niliyezaa nje eeh nionyeshe..’akasema

‘Una uhakika na hilo, maana likija kutokea kuwa haya ninayoongea ni kweli, sitarudi nyuma tena...’nikasema.

‘Mke wangu matendo yako ndiyo yaliyonisukuma hadi nikafika huko, sikuwa na raha kama mume, wewe muda wote upo na kazi zako, sikuwa na raha kama mume, sikuwa na sauti kama mume, nilikuwa nipo nipo tu,....nikawa natafuta njia ya kijiliwaza,...nikaona pombe atakuwa mpenzi wangu, kumbe pombe ina mitihani yake..je sasa watana nianze tena hayo maisha.’akasema huku natamani kumzaba kibao, nilimuona kama mtoto mdogo vile.

‘Hivi wewe hujitambui hayo unayoyaongea, unaongea kama mtoto mdogo, ..ulewe kwasababu ya kujiliwaza, ....sikuelewi, ulienda kulewa kwasababu ya starehe zako, mimi muda wote nilikuwa hapa ndani, kwanini hukuniambia unachokitaka wewe...?’ nikamuuliza.

‘Mke wangu mke wangu, ya kale yamekwisha, nakuomba mke wangu tuishi kama mke na mume, tupendane kama zamani, tugange yajayo....’akasema.

‘Hujanijibu huyo mtoto uliyezaa nje, ni nani na ulizaa na nani?’ nikamuliza.

‘Hilo nitakuambia pale utakapokubaliana na mkataba wetu, maana kila kitu kipo wazi, na kama unachosema ni kweli basi tutaambizana....’akasema.

 ‘Unanichefua,...nashindwa hata kukuelewa, sikiliza, mimi ninakupa wiki moja, nataka mkataba wa zamani uje, kama hautapatikana basi, ...tutaita mawakili wetu, tutaangalia haki ilipo, na ikibidi tutafikishana mbali,...nisingelipenda kuwashirikisha wazazi wangu kwa sasa...ila baada ya wiki moja hiyo kwisha, kama utaendelea na ujinga wako huo....hutaamini kuwa ni mimi...’nikasema.

‘Mke wangu, kwanini unakasirika,...kwanini yote hayo, mbona mimi nakupenda, na nafanya haya yote kwa mapenzi ya dhati...jaribu kunielewa na mimi....mbona hutaki angalau kuusoma huo mkataba hakuna kichobadiliak kabisa, na ukweli ni kuwa eeh, mke wangu, mimi nailinda ndoa yangu, mimi sitakubali kamwe ndoa yetu ivunjike, ....nakuhakikishia hilo....’akasema.

‘Kama umekiuka mkataba, ambao tulikubaliana mbele ya wakili, na kauli yako na yangu ilitoka kuwa likifanyika hili au lile ndoa haipo, basi haipo, kaulize mawakili kaulize hata watu wa dini, hukulazimishwa, tulikubaliana…kwa maandishi…’nikasema

‘Ni sawa, si kila kitu kipo kwenye mkataba au sio, mbona unaogopa wewe…’akasema

Mimi sikutaka kuongea naye siku hiyo, nikaondoka kuendelea na shughuli zangu nyingine

***********

Siku zikawa zinakwenda, na mimi nikaendelea na msimamo wangu wa kutokuutambua mkataba huo waliotayarisha wao, sikutaka kulifuatilia kisheria zaidi, hata wakili wangu aliyetaka kulifuatilia kisheria, nilimwambia anipe muda kwanza nijaribu kivyangu, ikishindikana, itabidi tuingie kisheria.

Ikafika mahali mimi na mume wangu hatuongeai, sikutaka hata kuonana naye, mimi niliweka agizo langu kuwa nitakaa meza moja na yeye pale tu huo mkataba wa zamani utakapopatikana. Nikaanza kumwekea shinikizo, kwanza nikakata mawasiliano ya kuongea naye, na kutokushirikiana naye kwenye shughuli zozote alizozifanya kimkataba.

Ikafikia hatua hata hundi za benki ambazo nilihitajia mimi kupitsha nikazizua, kwahiyo akawa hana uwezo wa kipesa zaidi ya kiasi kile alichoruhusiwa kukutoa kwenye kampuni yake, kwani kiasi kikzidi sana ilitakiwa sahihi yangu na yake, kutokana na kumbukumbu za kibenki.

Hali ilivyozid kuwa mbaya, akaona amtumie rafiki yake, ili aonge na mimi na siku hiyo akaja docta rafiki yake…akasema ana maongezi na mimi, akaanzia mbali na baadae akaja kwenye jambo aliloniitia, akasema.

‘Shemeji pamoja na mengine, lakini kuna mambo ya kikazi, ukiwa na msimamo wako huo kazi zitasimama, na kampuni ya mumeo itakufa kabisa...’akasema huyo rafiki wa mume wangu.

‘Kama analiona hilo ni wajibu wake, kuleta huo mkataba wa awali, na kama anajiona kuwa anauwezo wa kufanya anavyotaka basi aendelee, na siku nitakapo kamilisha uchunguzi wangu na kuwa na ushahidi wa kutosha kuwa kweli kavunaj mkataba wa hiari, kuwa yeye alishirikiana na marehemu kufanya hayo yaliyotokea, nitampeleka mahakamani....’nikasema.

‘Lakini mambo ya kampuni msiyaingize kwenye mambo yenu ya kifamilia’akashauri.

‘Sisi tulikuwa na utaratibu wetu mzuri tu, yote hayo ya kikampuni , ya kifamilia, tulikuwa tumekubaliana, ili kulinda mali za familia, ...kama tusingelifanya hivyo, kampuni hizo zisingelikuwepo, angalia sasa anavyofanya yeye, nasikia kuwa ana mtoto nje, na kama ana mtoto nje, ina maana ana kimada nje, ni nini kitaendelea hapo, kama sio kuanza kugawa mali halali za ndani ya ndoa kwa watu wasio na haki hiyo…’nikasema.

‘Sitaki nikukumbushe ..lakini inabidi nikuambie, hayo umeyataka wewe mwenyewe...nilikuambia mwanzoni jaribu kuwa karibu na mume wako, jaribu kuangalia ana shida gani anataka nini, ujue kuwa binadamu wote sio sawa, kuna utofauti wa kuwaza, unavyowaza wewe, sio sawa na anavyowaza mwingine na uvumilivu wako sio sawa na uvumilivu wa matamanio kwa mwingine.’akasema.

‘Nakufahamu sana, huenda hayo mliyapanga pamoja, ili kujionyesha kuwa nyie ni wanaume, mnaweza kufanya mpendavyo, au sio...mlewe , mtembee ovyo na wanawake , mzae ovyo, si ndio,...?’ nikamuuliza.

‘Sina maana hiyo..ila maisha ya ndoa,msipovumiliana, mkaweza kukaa pamoja, mkajaribu kuziangalia zile tofauti zenu za kifikira, mkazitafutia suluhu, siku mambo yakiharibika inaweza ikaleta shida sana kujirudi, kwasababu muda huo kila mmoja atajiona yupo sahihi...kama mngelikaa na kujuana, na kuangalia mwenzangu anataka nini, mgeliweza kulizuia hilo....’akasema.

‘Mwambie rafiki yako, suluhisho la haya ni mkataba wetu wa awali, kwasababu siwezi kukubali huo mkataba wa kugushi, wamekaa na mwenzake, marehemu, wakatunga mambo yao, mimi sikuwepo, na humo wameweka mambo ambayo mume wangu atajifanyia apendavyo, bila hata kibali changu....huoni kuwa ni hatari, kutokana na hilo, nasikia kuna mkataba mwingine, ambao, yeye kama mume, kutokana na mkataba huu, ana hiari ya kuuza hisa kwa mtu mwingine...’nikasema.

‘Mhh, una uhakika na hilo?’ akaniuliza.

‘Ndio maana sitakubali huu mkataba wao, ..kamwe, kwani nikikubali tu, kampuni yake, hatakuwa na hiari nayo, kwani hata marehemu kauziwa hisa, ...ni nani alipitisha hilo, ....hebu niambie, mimi nikubali tu, ‘nikasema

‘Hilo sio kweli…’akasema

‘Wewe si unanichunguza, wewe si ulitumwa kunichunguza mbona hilo hujaligundua,,,,sasa hiyo ni kazi yako, chunguza na utakuja kuniambia..’nikasema

‘Mhh..kama imefikia huko,…unajua mimi nilishaachana na mambo yenu, tuliacha ili mjenge suluhu, lakni kwa hali hiyo, kama ni kweli, mmh, ‘akasema

‘Sasa niambie mimi nifanya nini...ina maana gani kuhangaika, kutokulala, usiku na mchana tulihangaika, leo matunda yamepatikana, yachukuliwe na watu wengine kirahis rahisi tu....na japokuwa hajakubali moja kwa moja, yeye ana mtoto nje, na kwenye huo mkataba wao wa kugushi, motto huyo na mama yake, wana haki, na watachukua sehemu ya mali...’nikasema.

‘Huyo mtoto ni nani na mama yake ni nani…?’ akauliza

‘Hiyo kazi nakuachia wewe..’nikasema

‘Unajua siwezi kulifanya hilo kwa sasa, wewe mwenyewe ulinipiga marufuku kufuatilia mambo ya ndoa yako, nilishakuambia kama unanihitajia ni kusaidie,nipo tayari,ukasema hutaki mim niingilie ndoa yako, kwani lengo langu ni kuvunja ndoa yako, ilinikera kwakweli, je bado una msimamo huo, je bado hutaki nikusaidie…?’ akaniuliza.

‘Kama nilivyokuambia toka awali, wewe endelea na familia yako,mimi hili nitalimazia mimi mwenyewe, yupo wakili wangu, nikishindwa nitamkabidhi, na hapo itakuwa ndio mwisho wa haya yote maana kila kitu kilikuwa wazi kwenye mkataba...’nikasema

‘Upo tayari kuvunja ndoa yako kwasababu ya hilo?’ akaniuliza

‘Wewe unaliona hili ni dogo eeh, ikifikia hapo, hutaamini, kwanza huo mkataba wa zamani ukipatikana tu,...kama tulivyoahidiana, hatua kwa hatua, tutatekeleza, na kuna ahdi yangu kwa huyo mwanamke wake waliyezaa naye, mimi nitamuonyesha kuwa mimi ni nani...huwa nikiahidi kitu sirudi nyuma,....’nikasema.

‘Ndio maana mume wako anaogopa kuuleta huo mkataba wenu wa zamani, anakufahamu ulivyo...’akasema.

‘Huo ni uwoga,...yeye kama ni mwanaume, anatakiwa aingie uwanjani, apambane kiume, na asipofanya hivyo, akaegemea  mawazo ya wenzake, atakosa yote....hajui mimi ninawaza nini, hajui nina mipango gani kichwani, ..hajui...kwani nimetoka naye wapi,...hakumbuki hilo,...’nikasema.

‘Haya mimi sitaki tena kuingilia mambo yenu, nitakuja tu pale mtakaponihitajia, kama ulivyowaambia wazazi wako, kuwa wasiingilie mambo yenu, sisi tunawaangalia lakini kama mkikwama, sisi tupo tayari kuwasaidia..’akasema na kuondoka.


Siku moja wakati nipo nyumbani nimepumzika, nikaambiwa kuna mgeni anataka kuongea na mimi, nilikuwa sitaki kuongea na mtu, lakini nikaona ni vyema kumsikiliza huyo mgeni, kibusara, nikauliza;

‘Ni mgeni gani huyo?’ nikauliza.

‘Ni mtoto wa marehemu Makabrasha..’akasema msaidizi wangu wa ndani.

‘Huyo tena, nilishasema sitaki kuonana na yeye, kama anataka kuongea akaongee na huyo huyo mwenzao, sio mimi…’nikasema

‘Kasema hawezi kuondoka, bila ya kuonana na wewe, kwasababu huenda akasafiri, na hawezi kuondoka bila ya kuhakikisha ameyamaliza mambo yote aliyotakiwa kuyafanya,…kwahiyo yupo nje anasubiria kukaribishwa…’akasema bint msadizi wangu wa nyumbani.

Nikawa kimia nikitafakari,…je dawa ni kukimbia jambo au kukabiliana nalo…nikikataa kuongea naye ina maana nimekimbia..nimeogopa, nikiongea naye je…huenda kuna mitego, kuna jambo wamepanga,na huenda ikawa ni sababu ya kuniumiza zaidi kimawazo.

Nikachukua simu yangu na kumpigia wakili wangu wangu..nikamuelezea, wakili wangu wangu akasema

‘Fanya kama nilivyokuambia…

NB: Jamani hapa nimeazima laptop ya mtu, kuonyesha jinsi gani nawajali


WAZO LA LEO: Siri ya mafanikio, ni kujibidisha kwenye shughuli unayoifanya, na siri ya kushinda vita sio kukimbia, ni kukabiliana na adui yako, na siri ya matatizo sio kulalamika tu, bali ni kujitoa muhanga na kukabiliana na matatizo hayo. Mitihani mingi ipo kwa minajili ya sisi kufunguka akili zetu na kutafuta njia bora zaidi ya kukabiliana na matatizo hayo. Tuifanye mitihani hiyo kama sehemu ya daraja la kuvuka na kusonga mbele..lakinii tujitahidi kupambana na mitihani hiyo kwa njia za heri, huku tukimuomba mola wetu.

Ni mimi: emu-three

No comments :