‘Sikiliza nikuambie sasa, eeh,..mimi sikufahamu au kuukariri
mkataba kabla, kwahiyo sikuwa makini kwa
kipengele kwa kipengele…mengi nilikuwa nafanya kuhakikisha nakufurahisha, eeh
kwasababu nakupenda mke wangu.…’akasema
‘Watu wakawa wana..fikia hatua sasa hata ya kuniuliza, umeoa au umeolewa,
unaona eeh vitu kama hivyo, mimi sikujali,..sasa matatizo yakaanza, kuna mambo
mengine, nitakuja kukuelezea baadae, ..’akatulia
‘Marehemu nikakutana naye ndiye akanifungua macho, aliniuliza
tatizo ni nini, awali sikumuambia, baadae kutokana na hayo matatizo …unajua,
ikabidi nimuambie, kuwa kuna mkataba, na mkataba umekuwa ni mnyororo kwangu,..’
hapo akakaa kidogo, baadae akasema
‘Akaomba aupitie,nikampa, samahani kwa hilo…akausoma , akasema,
mbona kila kitu kipo sawa, ni wewe tu hutimizi wajibu wako, unaogopa nini, hiki
kipengele hapa kimekupa mamlaka, ..ilikuwa kama ndio naanza kukiona,…unaonaeeh..’akasema
‘Sasa kama ningelikaa kimia, huo mkataba ukafika kwa wazazi wako, hicho kipengele sikuwa nimekiona
eeh cha mamlaka ya mume, na vingine vingine,lakinikwa leo ni hiki cha mamlaka… mimi
nina uhakika wazazi wako wangelikimbilia kuniwajibisha, na hapo ndoa
ingelivunjika tu,..’akasema
Nilimuangalia tu, na aliponitupia jicho na kuiona hiyo hali
niliyokuwa nayo usoni, haraka akajibaragua na kama anatabasamu hivi, halafu
akasema;
‘Kwahiyo mke wangu, sasa mambo yote yapo shwari, usiwe na wasiwasi
kabisa, sasa nitajitahidi kutimiza wajibu wangu, ..nimeshajielewa, na makosa
yaliyopita ..si ndwele, tugange yajayo, na nachukua fursa hii kukushukuru sana
wewe mke wangu, uliona mbali sana…hata
Marehem alikusifia kwa hilo…’akasema
‘Hahaha, mume wangu usinifanye mimi ni mjinga kiasi hicho, kuwa
mumeweza kubadili mkataba, na mumetengeza mkataba mwingine ambao ndio huo
unakufanya ujiamini saana..’nikasema
‘Kwanini unasema hivyo mke wangu..?’ akauliza
‘Hebu nijibu swali langu , ni kwanini mlibadili huo mkataba…najua mliubadili
na marehemu kwa masilahi fulani…, sasa nataka kauli yako wewe, ni kwanini
ukafanya hivyo, maana unaongea kama vile..hata sikuelewi…’nikasema sasa kwa
ukali.
‘Ninachosema mke wangu ni hivi, kama wazazi wako eeh...wangeliuchukua
ule mkataba, kabla ya mimi sijaupitia vyema, wangeliweza kutoa maamuzi na mimi
nikakubalia tu, maana sikuwa na uelewa …maana wangeliangalia kosa, na adhabu ya
kosa, lakini je vipengele vingine, vya kutulinda, mimi na wewe , je kipengele
cha mamlaka yangu...’akasema.
‘Kwahiyo wewe ulikwenda kwa marehemu ukamwambia umefanya kosa, na
mkataba unasema ukifanya kosa adhabu yake ni hivi, sasa ufanyeje, si ndio
hivyo, ukampa mkataba, yeye akafany alichofanya, akakurejeshea na kusema sasa
kila kitu kipo sawa, ..mume wangu wewe hujui hilo ni kosa mnagushi mkataba
halali..haya ulipofanya hivyo mlikubaliana malipo gani sasa, maana pesa huna, ulimlipa
nini..?’ nikamuuliza
‘Mke wangu sio hivyo, hebu kwanza rejesha akili yako
nyuma…’akatulia kidogo, na mimi nikatulia sikusema kitu.
‘Hili la kupata ushauri kutoka kwa marehemu, ililikuwa ni kama
hitimisho la mambo mengi yaliyokuwa yamejificha, huenda hata mimi sikuwa na
mawazo hayo kabla, na sikuwa na uelewi wa kisheria kivile, unanielewa hapo, na
sitakosea nikisema, matatizo yameanzia kwetu…sikulaumu,…wakati
mwingine..inatokea, na hatuwezi kumkufuru mungu,.. labda nijilaumu mimi
mwenyewe kwa kutokujua majukumu yangu...’akasema
‘Unasema….’nikasema hivyo tu
‘Kiukweli mke wangu Marehemu alikuwa rafiki yangu mkubwa sana, na
mengi alikuwa akinishauri yeye, hata kabla ya hilo, na sikuwa na mtilia maanani
kipindi ch aawali, niliona kama ananionea wivu,..lakini sasa yalipotokea
matatizo…, ikabidi nimkumbuke…’akasema
‘Matatizo gani sasa, niambie..?’ nikamuuliza
‘Matatizo,….yah, ndio
nikafikia kukuomba msamaha, lakini hayo nitakuja kukuambia kwa wakati muafaka,
usiwe na wasiwasi mke wangu, kwanza ni kwanza, hili lililipo mbele yetu....’akasema
‘Kwahiyo sasa hivi unataka tuongelee nini hasa, hiyo kwanza ni
kwanza ni nini..?’ nikamuuliza ilibidi nijishushe tu twende sawa na atakavyo
yeye
‘Kuna mambo kidogo, tunahitajika kukubaliana hapa leo hii, ni
muhimu sana, nataka tuyaongee, ni kuhusu mikataba tu, tukakubaliana basi
kinachofuata ni utekelezaji tu...’akasema, na mimi kwa vile sikujua
anataka kuongelea jambo gani, nikasema;
‘Mhh, haya mambo gani hayo, mimi nakusikiliza wewe sasa...lakini
mimi nitafurahi sana nikiusikia ukweli wote…’nikasema
‘Ukweli,…! Mke wangu usijali,..mimi nipo tayari, nitakuambia kila
kitu hatu akwa hatua, sitaki nikuchanganye, lakini hili kwanza la muhimu,
ambalo ni msingi wa mengine yote, na sio kubwa kihivyo, ni kukubaliana tu, na
ni wajibu wangu kufanya hivyo, na wewe kunishauri, kwa vile wewe ni mke wangu..’akasema
‘Haya ongea ,..’nikasema
‘Kuna mambo kwenye mkataba yalikuwa yamekaa kimtego-tego kwangu,…’akasema
‘Mambo gani sasa…?’ nikauliza kwa sauti mpaka akashtuka na
kuniangalia machoni, halafu akasema
‘Yapo kwenye mkataba tutakuja kuyaona,lakini haina shida saana,…’akasema
‘Unaelewa ni nini maana ya mkataba, mkataba ni makubaliano ya watu
wawili au zaidi au sio…sasa iweje mmoja achukue hatua ya kurekebisha mkataba
uliokubalika bila ya idhini ya mwingine kwa masilahi yake…’nikauliza
‘Sio hivyo mke wangu, naona kama hujanielewa, hakuna kitu
kilichobadilika, mke wangu…’akasema
‘Una uhakika hakuna kitu mumebadilisha, …usiseme uwongo mume wangu
maana nitakuja kulithibitisha hilo,na nikifikia huko sheria itachukua mkondo
wake,…’nikasema
‘Sheria itasimamia kwenye makubaliano yetu..au sio, haiwezi kuvuruga
yale tuliokubaliana, na yapo wazi kwenye huo mkataba au sio..na mimi sijasema
kuwa nitafanya kinyume cha makubaliano yetu, na kama ilitokea tutarudi kwenye kipengele
cha msamaha, nilishalifanya hilo, na wewe ukanisamehe au sio, tena mbele ya
mashahidi…’akasema
‘Kuna kipengele gani kilisema
kuwa wewe kama mume unaweza kubadili mkataba bila ya mimi kuwepo, au cha kukupa
mamlaka ufanye wewe uonavyo ni sahihi, bila ya mimi kuwepo, eeeh hata kama
inanigusa na mimi..?’ nikauliza
‘Mke wangu kuna mambo yakitokea mimi kama mume ni lazima
niwajibike…na hilo sio kwa mujibu wangu, mkataba unasema hivyo, mimi nina
wajibu wa kuhakikisha familia yangu ipo salama, hebu ona mpaka watu wanafikia
kuua,.. ujue watu hao hawana nia njema, sasa kama nisiposimama kiume
itakuwaje…ilibidi mambo yawekwe sawa…’akasema.
‘Unaposema hivyo, mambo yawekwe sawa una maana gani hapo,?’
nikamuuliza
‘Nina maana gani eeh…ina maana mke wangu hulioni hilo, hebu
jiulize ni kwanini Makabrasha akauwawa,…alichofanya yeye ni ushauri tu, na
hatukuwa tumefikia mahali pa …undani zaidi, kabla hatujamalizana, kauwawa,
masikini wa mungu…’akasema kiuonyonge.
‘Mume wangu upo sawa kweli wewe, mbona nakuuliza hivi unapindisha
hivi upo sawa au ulikunywa kidogo leo , ulishaambiwa usinywe pombe …?’
nikamuuliza maana nilimuona anaongea sasa kama kalewa, lakini hana harufu ya
pombe
‘Nipo sawa kabisa mke wangu, nafanya hivi ili unielewe, ili
nikitoka hapa , mimi naenda kufanya kazi, usije kusema aah, nimekiuka mkataba,
hapana…mkataba sasa ufanye kazi yake, mimi najiuliza hapo ni kwanini wakamuua
Makabrasha…?’akasema
‘Kwanini unauliza hivyo, hata mimi sijui…’nikasema
‘Unaona eeh, wewe ni mke wangu , mambo kama hayo mimi ndiye
nilitakiwa niwajibike, …lakini kwa pupa na tamaa za watu, ndio ikafikia hapa,…kuna mambo yanahitajia umakini,
sio jaziba, …’akasema
‘Una maana gani hapo kuwa unanishuku mimi,… eeh mimi nimejikuta katikati ya mambo haya,
na hata kushutumiwa kuwa mimi ndiye niliyemuua, wakati sijui kabisa ni nini
kinachoendelea, lakini ukweli utajulikana tu…’nikasema
‘Umeonaeeh, sasa hiyo ni hatari..ina maanisha watu hao wapo tayari
hata kuua, kisa ni nini, ..kwa vile kagusa kwenyewe, kwenye mali, au…labda walihis
kuwa tumeingilia mambo yao hapana hatukuwa na lengo hilo, basi kama ni hivyo watakumaliza
sote, next ni mimi…’akasema
‘Kwahiyo kumbe wewe kuna watu unawashuku tayari je umeshawaambia polisi..?’
nikauliza
‘Aaah,..hiyo ni kazi yao bwana, sijaongea lolote na polisi, usiwe
na wasiwasi kabisa na hilo…lakini kiuhalisia si inajionyesha, ni kwanini wamuue
huyo wakili, ni kwanini…ina maana kuna sababu, na jiulize ni kwanini itokee
kipindi hiki ambacho anahangaika kuyaweka mambo yetu sawa..’akasema
‘Mambo gani yetu..?’ nikamuuliza
‘Kama huo mkataba..’akasema
‘Ehee..mkataba una nini labda ambacho yeye alitaka kuweka sawa..?’
nikamuuliza
‘Yeye alishajitolea kuusimamia, kwa masilahi ya familia…unaona,
hata kama ni kusimama mahalamani, ilimradi tu masilahi ya familia yetu yalindwe,
na mimi nilikubali kushirikiana naye, na ndio tulikuwa kwenye mipango ya
kukufafanulia hayo hatua kwa hatua, nina imani ingelimuelewa tu…sasa wamemuua..’akasema
sauti kama ya kutaka kulia.
‘Kwahiyo unataka kusema kuwa kauliwa kwa vile alikuwa akihangaika
kuyaweka mambo yenu sawa, kutengeza mkataba wenu wa kugushi, kwahiyo waliomuua
ni hao ambao hawakubaliani na huo mkataba wenu wa kugushi, au sio..?’
nikamuuliza
‘Usiseme mkataba wenu wa kugushi, rekebisha kauli yako, huo ni
mkataba wetu na wewe ndiye uliyebuni hayo, au sio, na kiukweli sio mkataba wa
kugushi kabisa, niule ule mkataba, au umeshakuwa mkuki kwa nani…eeh, hapana
usiwe na wasiwasi mke wangu, …na kiukweli hao wanaoupinga ni kwa mashaka yao
tu, na na..ulikuwa hauwahusu au sio,…’akasema
‘Na ni nani hao…ambao mnawashuku kuwa hawatakubaliana na mkataba wenu
wa kugushi,..ukisema hivyo moja kwa moja unamnyoshea mtu kidole, maana mkataba ule
wa asili ulikuwa kati yangu mimi na wewe…
‘Sio swala la kushuku,..uhalisia unaonyesha..’akasema
‘Sasa ni nani, maana ukiacha wewe , mwingine kwenye mkataba huo ni
wakili wetu, na mimi…kwahiyo unataka kusema nini hapo, kuwa ni mimi nimemuua
Makabrasha si ndio hivyo..?’ nikamuuliza
‘Hapana, sio wewe mke wangu, wewe hauwezi kufanya hivyo, wewe ndio
mimi, wewe ni familia yangu, mimi nawashuku wale wasiotaka mimi na wewe tuishi
kwa furaha na amani….maadui wa ndoa yetu…’akasema
‘Akina nani hao sasa..ni, wazazi wangu au..?’ nikauliza
‘Sijawataja wao, na mimi siwezi kuwashuku wakwe zangu kihivyo, acha
polisi wafanye kazi yao…na ..ni hivi mke wangu, shaka shaka ni lazima ziwepo au
sio, inawezekana kabisa wakawa watu wengine tu, wakitumia mgongo wa watu
tunaowafahamu, na hilo ni lazima tulifanyie kazi, tuwatafute ni akina nani hao,
sisi kwa upande wetu tutakuwa tumenawa mikono au sio…’akasema
‘Sasa niambie ukweli, unataka nini sasa….maana kama hutaki
kuniambia ni kwanini ukachukua maamuzi ya kubadili huo mkataba..sizani kama
tutaelewana, kwa hali kama hiyo sitaweza kukuamini kamwe..?’ nikamuuliza.
*********
‘Hata mimi mume wako huniamini, hahaha, utaniamini tu, wewe ni mke
wangu, huwezi kwenda kinyume na mimi, au sio, na ukweli upi basi, ndio huu
ninaokuambia, tulianzia kwenye hii fitina ya mkataba, hii haikuja hivi hivi
tu…lakini marehemu akaigundua, na kunionya kwa hilo, ahsante marehemu…’akasema.
‘Mume wangu utaniambia ukweli au uondoke zako..?’ nikamuuliza.
‘Mimi ni mume wako, nitakuambia ukweli wote usijali, si ndio
nimeanzia hapo kwenye mkataba, kuwa hauna shaka, mimi nilikuwa sifahamu yaliyomo,
sasa nimeyafahamu na ndio maana nimeanza kuufanyia kazi au..?’ akasema na
kuuliza.
‘Sikiliza mume wangu, usije
ukajidanganya na huo mkataba wa kugushi, ukajiona kuwa upo salama, huo mkataba ni
wa kugushi, ni ukiukwaji wa sheria, na hilo tunaweza kulithibitisha
kisheria, kuwa huo mkataba wa sasa ni wa kugushi...hata kama kila mbinu
zimetumika,… kuubadili na kusambaza nakala kila mahali husika,.. haisaidii kitu
, kwani wakili aliyesimamia hiyo hayupo, ..’nikasema.
‘Hakuna kosa kwenye huo mkataba mke wangu, kila kitu kipo sawa-sawa,
na sijui kwanini unauita mkataba wa kugushi, wakati ni wewe mwenyewe ulikuja na
wazo hilo,iweje leo maneno yako uyapinge, au una ogopa nini, usiogope mke wangu
mimi nipo ...’akasema.
‘Huo mkataba mpya mimi siutambui, maana sikushirikishwa,..kwanza
ni mkataba wa nani na nani, ...nasema hivi ukinielewa nina maana gani, na usinione mimi ni mjinga kihivyo….sasa ni
hivi ili tuelewane mimi na wewe, nauhitajia ule mkataba wa mwanzo kwanza…’nikasema
‘Mkataba wa mwanzo upi tena mke wangu…?’ akauliza
‘Mume wangu usitake tubishane hapa, nikuuliza tu, kama uliona kuwa
kuna marekebisho, ilikuwa ni haja gani kuhangaika hivyo, ungelianiambia tu,
kuwa kuna sehemu hupendezwi nazo, basi mimi na wewe tungelikaa tuone tufanye
nini au, huo ndio uungwana ...’nikasema.
‘Na mimi narudia tena kukuambia mke wangu, mimi sijui kama kuna
mkataba uliogushiwa, upi huo uliogushiwa, kwani kuna mikataba mingapi, mkataba
niujuao ni huo huo, na kama kuna kitu basi tutakaa tutaongea , hilo halina
shaka, ila kwa leo eeh...!’akasema na kunifanya sasa nianza kukasirika,
nilishaona mume wangu kadhamiria.
‘Mume wangu acha hayo maneno...kwa kauli yako ya kuzunguka
zunguka, kuna muda ulisema kama wazazi wetu waneguchukua kama ulivyo, ndoa yetu
ingelivunjika, je hivyo vipengele vya awali vya kuuvunja ndoa, ni vipi na hivyo vya sasa vya kufanya
isivunjike ni vipi, mume wangu nakuona kuwa mkweli tuyamalize haya mambo kwa
amani,....’nikasema.
‘Mke wangu, mimi sijui mambo ya kugushi mkataba,...mimi sio
mwanasheria, nitagushi vipi mkataba, na mkataba huandikwa na wanasheria, baada
ya mimi na wewe kukubaliana, tulikubaliana au sio…na mwanasheria akafanya kazi
yake, na ndio mkataba ninao ufahamu mimi,...’akasema.
‘Una uhakika na hayo unayoyasema…mume wangu usitake tupelekane
kubaya, mimi sipo hivyo, kawaida yangu ni haki na ukweli, kwanini tusiwe hivyo
mume wangu unataka nini lakini, niambie…?’ nikamuuliza na yeye kwanza
akaniangalia, halafu akaangalia chini na kusema;
‘Mke wangu, mimi nina uhakika na hilo ninalolisema, nimeshakuambia
kuwa mimi nakupenda sana kweli si kweli,…, na hayo yaliyofanyika, yalifanyika
kwa nia njema tu, ya kuilinda ndoa yetu, na nakuhakikishia kuwa mkataba
wetu upo vile vile na mambo yake mazuri tu…, na mimi nitakuwa mume mwenye
mamlaka kama mwanaume, sio mwanaume jina tu...’akasema
‘Una maana gani kusema hivyo?’ nikamuuliza.
‘Mkataba ndivyo unavyosema hivyo...kuwa mimi kama mume nitakuwa na
mamlaka ya uongozi wa familia, nitaweza kupitisha maamuzi, kama nionavyo ni
sahihi kwa masilahi ya familia, hilo halihitajii mjadala, au sio…hata bila kuwa
na mkataba hilo lipo wazi, kwanini hunielewi…?’ Akaniuliza
‘Huo mkataba wa kugushi
ndio unasema hivyo, hicho kipengele ni kigeni kwangu ..’nikasema
‘Na...wewe utakuwa msaidizi wangu, na hiyo ndio kawaida ya mume na
mke, mambo mengine ni ya kuiga tu, ..hayana maana kwetu, ndio hata Marehemu
aliyaona, lakini sio kitu kikubwa sana, maana mimi ndio nilitakiwa nilione
hilo, na mimi ndio natakiwa kusema..au sio,…’akauliza na mimi nikaa kimia
‘Mke wangu, kikawaida eeh, mimi ndio natakiwa kuwa kiongozi wa
familia,na ikibidi kurekebisha jambo kwa masilahi ya familia, sihitaji kibali
au sio…ili kuikoa familia, na kila kitu, huo ndio ukweli, zaidi ya hayo, mimi
natakiwa kuilinda familia yangu, ukisaidiwa na wewe mke wako, kwani hapo kuna
makosa, ni maneno yale yale...’akasema.
‘Haya unayoyaongea wewe yapo kwenye huo mkataba wa kugushi au sio
sio kwenye mkataba sahihi tuliainisha wazi kuwa, ili kuondoa utata, kila jambo litafanyika kwa makubaliano,….na
hili uliliongeza wewe siku ile ya majadiliano,…na tulikubaliana kabisa kuwa
asilimia kubwa ya mambo yetu yapo kwenye mkataba, kwahiyo kama kuna kasoro, au
jambo lolote limejitokeza lenye sintofahamu basi, tukae tujadiliane..’nikasema
‘Sawa kabisa,…’akasema
‘Na hii ina maana gani, mkataba hauwezi kubadilika mpaka kuwe na
kikao cha kukubaliana, akiwemo wakili wetu, sasa hayo ya mume kujiamulia
mwenyewe akiona kuna sababu, yanatoka wapi,, na kwanini kuwe na mabadiliko,
kuna nini kilitokea,…?’ nikamuuliza
‘Mkataba ni ule ule mke wangu, hakuna kilichobadilika, hata
ukiuangalia, eeh, ni mambo yale yale, na yote…tulikubaliana mimi na wewe ..na
wakili wetu…wewe ni wasiwasi wako tu’akasema.
‘Tatizo lako, Makabrasha alikuingiza kwenye anga zake za ulaghai,
na umesahau kuwa wewe sio mwanasheria, huyo mtetezi wako sasa hivi hayupo tena
duniani, kuna mambo ya kisheria huyafahamu,...na hayo yatakupeleka
pabaya,...mkataba uliokubalika kisheria ni ule tuliokaa mimi na wewe
tukakubalina sio huo uliokaa wewe na mwanasheria wako, ....’nikasema.
‘Ndio huo huo mke wangu, wewe una nakala yako, na mimi nakala yangu,
nenda unapoziweka ukazichukue,…lakini mimi nina nyingine hapa, na nisisahau
nakala nyingine ipo huko kwenye vyombo vya sheria… hakuna mkataba
mwingine...kila kitu kipo vile vile, hakuna kilichobadilika, na wewe na mimi
tuliweka sahihi zetu na ya mwanasheria wetu, ndio hivyo...’akasema.
‘Mwanasheria gani?’ nikamuuliza.
‘Mwanasheria wetu wa familia, ..ngoja nikuonyeshe mkataba wetu,
ninao nakala yetu hapa..hakuna kitu kilichobadilika, ni mambo madogo madogo tu
ulikuwa huyajui labda, ndio yanakuchanganya, eeh, usijali kabisa, hata kama
wamemuua Makabrasha kuwa labda, nitakosa mtetezi, mimi mwenyewe
nitajitetea,..na haya yote mke angu ni kwa ajili ya masilahi yetu sote...’akasema
huku akiutoa huo mkataba
Na wakati anafanya hivyo macho yangu yakahisi kama kuna mtu
kasimama kwa nje, nahisi alikuwa akisikiliza tunachoongea, akasogea kidogo, …sikuweza
kumtambua ni nani,...nikataka kumpa ishara mume wangu, lakini hakuwa makini na
yeye akawa ananionyesha sehemu zile za sahihi akasema;
‘Huu ndio mkataba wetu,..unaona hii hapa ni sahihi yangu, hii ni
ya kwako, hii ni sahihi ya mwanasheria wetu wa familia, mkataba ni ule ule,
utabadilishwaje na nani afanye hivyo...hakuna kilichobadilika kabisa ,
...unaonaeeh...’akasema huku akifungua fungua huo mkataba, na mimi nikawa
namuangalia tu
‘Mume wangu usitake tufikishane huko..huko unapokwenda ni kubaya,
usikubali hayo mambo aliyokudanganya Makabrasha, ..huyo jamaa anajulikana sana
kwa hadaa na ulaghai, hata watu wa usalama wanalitambua hilo..sasa na wewe
usiwe mshirika wake, tunachotakiwa kwasasa ni kusahihisha yale makosa
yaliyotokea, ili tuanze pale tulipoishia, ..’nikasema
‘Ndio hivyo mke wangu ndio maana hata kama unataka basi hata huu
mkataba tuachane nao au sio, na mimi niwe na mamlaka yangu kama mume wako au
sio, mbona wengine wanaishi tu bila hata
ya mikataba unaona eeh, ni kwanini sisi, sababu ya mali au...’akasema
‘Sikiliza mume wangu,….tusilazimishe migogoro isiyo na msingi, na
tusitake kulazimisha chuki na uhasama, wakati kuna njia nzuri ya haki, yenye
kuleta mariziano na maafikiano,...hebu nikuulize hivi wewe unachotaka hasa ni kitu
gani, niambie ukweli ?’ nikamuuliza mwishoni.
‘Nakupenda sana mke wangu , sitaki mimi na wewe tuachane, mimi
nataka ndoa yetu idumu na tuishi kwa amani na upendo...’akasema
‘Ni nani kasema hatupendana na hiyo hoja ya kuachana inatoka wapi,
eeh, kuna nini kimeileta hiyo hoja ya kuachana?’ nikamuuliza.
‘Mkataba…eeh, …je ikiingia fitina, na wewe ukaridhia nayo, wakaja
wazazi wako ukasema mkataba huu unasema hivyo, itakuwaje, fitina ni mbaya mke
wangu, kuna watu walishajenga majungu, na hata rafiki yako analifahamu hilo,
nina uhakika hadi anaondoka bado mlikuwa hamjawa sawa, kweli si kweli, na wewe
ndiye ulikuwa mshauri wake mkuu, kila jambo anafanya kutokana na ushauri wako,…lakini
hayo yamepita kila kitu kipo sawa sasa, au sio,...’akasema
‘Ndivyo alivyokuambia kuwa kila alichokifanya kinatokana na
ushauri wangu..?’ nikamuuliza
‘Rejea hoja yetu , kuhusu mkataba ni nani alitoa pendekezo hilo, lengo
lake hasa ilikuwa ni nini, sema ukweli wako wote, na je sio kweli kuwa wewe na
rafiki yako, mlikuwa mnashauriana mambo mbali mbali, tatizo lako wewe mke wngu
unasahau, unashauri baadae ikigeuka unakana, usiwe hivyo, mkuki usiwe kwa
nguruwe tu…’akasema
‘Sawa, tuwe wa kweli sote, je kuna vipengele kwenye mkataba
mlivirekebisha wewe na Makabrasha tumalizane na hilo…?’ nikauliza
‘Hapana, hakuna kilichobadilika, …zaidi ni kuhakikisha kuwa mume
ana mamlaka yake, mimi hizo sehemu nilikuwa sijazisomi, nilipozisoma na kuziona
nikajua kumbe nilikuwa siwajibiki..’akasma
‘Haya sawa, sasa nikuulize ni nini lengo la hayo yote , ni ndoa au
ni mali…?’ nikamuuliza na hapo akashituka na kuniangalia machoni.
‘Mke wangu nimesema kuwa nakupenda sana....sipiganii mali hapa.., ninachopigania
ni ndoa yetu,ndoa ni kila kitu humo..ni kwanini niipiganie mali wakati
ipo , mali tunayo au sio, tuna vitega uchumi vingi, ni swala tu la kuviendeleza....huwezi
kupigania kitu chako, eti mke wangu, mbona sikuelewi...’akasema.
‘Kwa hatua mliyofikia, hakuna jinsi, ni lazima ule mkataba wa
asili uwepo, na huo wenu uwepo, tuangalia je ni kweli hakuna kitu
kilichobadilishwa, najua kuna madhambi umeyafanya, na kulikuwa na vipengele vya
kukuwajibisha, ukaogoa, ndio maana ukakimbilia huko kwa Makabrasha.’nikasema
‘Usimsingizie marehemu uwongo, yeye sio kazi yake kuondoa kitu
kwenye mkataba, maana sio yeye aliyeutunga,..kazi yake kubwa ilikuwa ni kunifafanua
na kunishauri, yeye ni kweli, alipitia mkataba wetu, akausoma, na kuniambia upo
safi kabisa, akanionyesha hivyo vipengele muhimu ambayo mimi nilikuwa sivitilii
manani, vya mamlaka yangu...’akasema.
‘Kwahiyo ndio ukafanya ulivyoona kuwa ni sahihi,..hata kama mimi
sijarizia, ?’ nikamuuliza
‘Nimefuata mkataba unavyosema, au sio mke wangu, na .., kama
ilitokea kukosea huko nyuma, ni kwa bahati mbaya, ndio maana nilikuomba msamaha
kipindi kile, unakumbuka,… sisi kama wana ndoa wakati mwingine tunakosea kama
wanadamu, na kama mkataba unavyosema mtu ukikosea unatakiwa kutubu, na kuomba
msamaha, nilitimiza hayo au sio ...’akasema
‘Mume wangu sitaki kusikia hayo tena, tafadhali, nakuomba uondoke,
nataka kupumzika, naona unazidi kunichanganya tu, hayo ni mambo yenu na
marehemu, naomba usiongelee tena kuhusu huo mkataba wenu wa kugushi....’nikasema
‘Lakini mke wangu kuna jambo jingine muhimu kabla sijaondoka,
...kuna mtu anasubiri, maamuzi yangu mimi na wewe’akasema
‘Nani anasubiri hayo maamuzi yangu mimi na wewe, na hapa tulikuwa
tunaongea tu, na wewe mwenyewe ulisema kuwa haya ni mimi na wewe,huyo mtu
mwingine inamuhusu nini hapa …na nikuambie kitu,hakuna maamuzi yoyote yamepita
hapa, ..hatujakubaliana lolote hapa.mimi siutambui huko mkataba wenu, nitakubaliana
na mkataba wetu ule wa awali zaidi ya hapo mimi sipo.’nikasema.
‘Kuna mtu muhimu sana, alikuwa anasubiria haya maamuzi yetu, ni
haki yake lakini, na mimi nilikuja kutimiza wajibu wangu, kuomba ushauri wako…’akasema
‘Mtu gani huyo, na ana haki gani hiyo…?’ nikauliza
‘Ni mtoto wa marehemu, anahitajia maamuzi yetu, ...’akasema, na
hapo nikahisi moyo ukiniruka, ni kama mtu kakushtua ukiwa hujui
‘Nimeshakuambia hakuna maamuzi yoyote yaliyopitishwa hapa, kama
una lako jambo endelea kivyako, na kama umedhamiria hayo uliyokusudia, basi
tutapambana mbele ya sheria, wewe si mjanja, sawa endelea na mpango wako huo,
kila la heri ..’nikasema
‘Mke wangu usifike huko…’akasema
‘Usipoleta mkataba ule wa awali tutafika huko, maana nakuona
hutaki kunielewa, na hutaki kusema
ukweli, usihadaike na tamaa za watu wengine, kumbuka tulipotoka, na kila mara
nilikuwa nakuasa, acha tamaa, tushikamane, tuwe kitu kimoja, sasa haya yote yanatoka
wapi, unataka nini husemi…, au kuna kitu gani kimetokea, hutaki kuniambia
ukweli,…kwa hali hii bora uondoke, hapa sijisikii vyema nataka kupumzika,…’nikasema
‘Sawa kama umechoka hujisikii vyema mimi nitafuata mkataba
unavyosema, au sio, mkataba umenipa mamlaka ya kufanya yale yaliyosahihi kwa
masilahi ya familia, na na nilichokuja kuonana na wewe ni kupata ushauri, …wewe
pumzika, mambo mengine niachie mimi, au sio mke wangu…’akasema.
‘Au sio kuhusu nini…mimi
sijakushauri kitu hapa..’nikasema kwa hasira
‘Mke wangu si umesema niondoke,unataka kupumzika, au?’ akaniuliza
huku akigeuka kuniangalia.
‘Sina cha kuongea na wewe hadi hapo utakapoleta ule mkataba wa
zamani, na kuniambia ukweli wote, vinginevyo hatutaelewana...’nikasema.
‘Hamna shida mke wangu, ..tutaongea tu, wewe pumzika, mimi ni mume wako wa halali, hakuna kibaya
kitakachotokea, yote niachie mimi, mimi nitatimiza kila kitu kama
tulivyoainisha kwenye mkataba wetu..’akasema kwa kujiamini.
Na mara mlango ukafunguliwa,kwa nje, lakin hao watu hawakuingia,
ulionekana mkono tu,..nahisi ni zaidi ya mmoja maana nilisikia wakiongea, walikuwa
wakibishana jambo …mara mlango ukafunguliwa wote sasa, nikaweza kuwaona wapo
watu wawili, kwa upeo wangu.
Huyu mmoja alikuwa karibu
sana na mlango, nilipomchunguza kwa makini nikaona kama anafanana sana na
marehemu nahisi atakuwa ndio huyo mtoto wa marehemu, kwa muda huo alikuwa
akitaka kuingia ndani, na mume wangu akawa kamuwahi na akamzuia,akisema;
‘Mke wangu kachoka, naona mambo yote nitayamaliza mimi mwenyewe,
tunaweza kuongea huko mbele ya safari, au ulikuwa unasemaje…?’ akauliza sasa
wakiwa wamesimama mlangoni kwa nje.
‘Huyu ndiye yule wakili wangu niliyekuambia, atachukua nafasi ya
baba yangu..’sauti yule ambaye nahisi ndio mtoto wa marehemu ikasema. Na hapo
hapo nikachukua simu yangu kwa siri, nikawaweka sawa kwenye kiyoo cha simu na
kuwapiga picha, huku nikimchunguza huyo mtu mwingine ambaye ni wakili kwa kauli
ya huyo mtoto wa marehemu, kwa hisia zangu nilimuona ni kama aina za Marehemu,
kwa hisia zangu tu.
‘Habari yako muheshimiwa, …’ mume wangu akasalimia, na wakati
anasalimia ndio akagundua kuwa mlango bado upo wazi, akasogea na kushika mlango
na kuufunga. Hata hivyo nilikuwa tayari nimeshawapiga picha.
Na mimi nilipohakikisha mlango umefungwa, kwa
haraka nikampigia simu wakili wangu.
‘Sikiliza kama ulivyonishauri haya ni mazungumzo yangu mimi na
mume wangu nimeyarekodi, na picha zao nakutumia sasa hivi, yasikilize na wewe
utajua ni nini cha kufanya , wahi kabla hawajafanya lolote, sawa...’
NB: Doa la tamaa limeshagusa mtima, ibilisi hachezi mbali
hapo,...je itakuwaje, Kwa leo inatosha.
WAZO LA LEO: Imani
ya kweli ya ucha mungu ni pale upomjali mwenzako, na ukawa tayari kutoa hata kile
unachokipenda kumsaidia mwenzako, na ukajali jirani zako, lakini hayo yote kwa ajili ya mwenyezimungu sio kwa ria. Je
ni wangapi wapo tayari kuona mwenzake anapata kabla yake, au zaidi yake, ni wangapi wanayajali matatizi ya wengine, ni wangapi wanaona mali ni kitu tu cha kupita, awe tayari kusaidia wengine, hapa ni mtihani!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment