Ni wakati nafika mlangoni ili nigonge mlinzi anifungulie mara kitu
kikanigonga kwa nyumba kichwani, na giza likatanda,.....nikadondoka, na
kupoteza fahamu….
Tuendelee na kisa chetu…
**********
Nilizindukana na kujikuta nipo hospitalini, akili ilipotulia
nikagundua kuna mtu kakaa pembeni ya kitanda, …ndio nikamgundua kuwa alikuwa ni
mume wangu, wakati huo alikuwa kajiinamia, nikajaribu kujiinua, lakini nikahisi
maumivu ya kichwa, nikashikilia kichwa, na mara ndio mume wangu akagundua kuwa
nimezindukana, kwa akanisogelea na kujaribu kunisaidia, nikainuka na kukaa
vizuri,
‘Pole sana mke wangu unajisikiaje...’akasema kwa unyenyekevu.
‘Kwani kumetokea nini…mbona….oh, kuna kitu kilinigonga kichwani,
ni nani kafanya hivyo…?’ nikauliza
‘Inaonekana kuna watu walitaka kukuumiza huko jela...’akasema
‘Kuniumiza kwasababu gani,…ni akina nani hao?’ nikawa nauliza
maswali kwa mfululizo.
‘Hayo maswali kwasasa hayana msingi, cha muhimu ni kuwa upo
salama, na hilo limesaidia kupatikana kwa dhamana yako haraka, kwani kuna watu
walishaiwekea pingamizi, wakidai kuwa upo mahali salama, ungeliachiwa ungekuwa
kwenye hatari zaidi...’akasema.
‘Oh, kumbe....’nikasema huku nikishika kichwa, sehemu ambayo
nilifungwa bandejii na mume wangu akaniangalia kwa mashaka na kuuliza
‘Kwani unajisikiaje?’ akaniuliza huku akiweka mkono sehemu ile
iliyowekwa bandeji na mimi nikawa najihami asije akanitonesha, na akaondoa
mkono wake, na kuniangalia machoni. Alionekana huruma machoni…
‘Maumivu ya kichwa kwa mbali, lakini sio sana, haya niambie na
wewe unaendeleaje, maana mgonjwa anamuuguza mgonjwa, nani zaidi sasa...?’
nikamuuliza
‘Mimi kwasasa sijambo, sina wasiwasi kabisa, nipo tayari kupambana
na yaliyopo mbele yangu, japokuwa nachechemea, lakini sio kivile…na muhimu kwa
sasa ni mazoezi tu...’akasema huku akijiweka vyema, kama vile anajiandaa
kuongea.
‘Unajiandaa kupambana na yaliyopo mbele yako, yapi hayo mume
wangu, unavyoongea ni kama umemlanga mtu au ni maswala ya kazi na maendeleo...?’
nikamuuliza
‘Dunia hii ilivyo, maisha yetu wanadamu yalivyo, kila siku ni
mapambano, au sio, huwezi kulala tu, ukafanikiwa, ni lazima upambane, na mimi
nimejifunza jambo hapo, ili ufanikiwe hakuna kulala..’akatulia kidogo.
Nilimuangalia kwa makini, na hayo maongezi yake nikahisi kama
hayupo sawa, kwahiyo nikaogopa kuendelea kumuuliza maswali ya kumkwanza, nisije
nikaharibu nikataka kubadili muelekeo wa maongezi kwa kusema;
‘Hivi huyu wakili wangu yupo wapi...maana nataka kujua mambo
yanaendeleaje...aniambie kulitokea nini..nakumbuka nilikuwa mimi nay eye tu mle
ndani, sasa…hapana, lakini sawa…labda…’ nikawa kama nauliza huku nikitafuta
simu yangu, sikujua ipo wapi.
‘Wameondoka muda mfupi uliopita, watarudi, kuna mambo wanafuatulia,
walisema zoezi limekamilika, sikuwaelewa,…kwani ....unatafuta simu yako, nahisi
ipo kwenye mkoba wako, nikuletee?’akaniuliza.
‘Mkoba wenyewe upo wapi, hata sijui…maana akili haipo..’nikasema
‘Mkoba wako huu hapa, walikuchukulia kila kitu chako, haina haja
ya kurejea huko jela, kumbe ni uzembe wa watu tu, hukutakiwa kupelekwa huko…’akasema
‘Nilijua tu, walitaka kunikomoa, kuijengea kashfa, lakini
hawatafanikiwa ukweli utabakia kuwa silaha ya mkweli,…’nikasema
Wakati huo mume wangu aliinuka kuchukua mkoba wangu uliokuwa
umewekwa kwenye meza, alionekana akiinuka kwa shida, yaonyesha bado hajapona
vyema ila anajikakamua tu. Akanipa simu yangu, nikaiwasha kwani ilikuwa
imezimika, nikawa nimeishikilia mkononi.
‘Oh, hamna shida, ..hivi leo tarehe ngapi, ...’nikasema huku
nikiangalia simu, akaniambia tarehe na saa, nikasema;
‘Ahsante sana mume wangu,..nikamtaja kwa jina lake, na yeye
akatabasau na kusema
‘Ahsante mke wangu,…’ na kunitaja jina langu, siku nyingi
sijasikia ukinitaja jina langu na mimi nikatabasamu, halafu nikasema;
‘Kama dhamana imepatikana basi iliyobakia ni kuangalia kesi hiyo
itakwenda vipi, na huyo muuaji ajulikane ni nani, ili niwe huru
kabisa....’nikasema.
‘Mke wangu, kuuwawa kwa Makabrasha kumenishitua sana, sikutegemea
kabisa, ni kama bado namuona vile , yaani jana tu mtu mlikuwa naye, leo hayupo,
keshatoweka duniani, hatutamuona tena,..na zaidi kafaje mpaka afikie adhabu
hiyo.., hapo ndio inatisha zaidi…’akasema
‘Ni kweli pole sana, najua alikuwa wakili wako tegemezi na rafiki
yako mpenzi, lakini yote ni mapenzi ya mungu..’nikasema
‘Mhh ndio hivyo,…kazi ni kazi ukiwa hai, hayupo tena, natakiwa
kupambana mwenyewe…unajua nawaza sana baada ya hilo tukio kuwa sisi wanadamu si
chochote...na wengine wanajiona wana nguvu, kwa vile tu wana mali….’akasema.
‘Mhh…mali,…. ni kweli mali ni mtihani, na usipokuwa na mali ni
mtihani pia, au sio...’nikasema kama namuuliza.
‘Ni kweli,..hilo nimeliona ni mtihani kweli ukiwa huna kitu, na …ukaoa
mke mwenye uwezo, unajikuta mwanaume huna kauli, …sikuongelei vibaya mke wangu, ila nimekuwa nikiliwazia sana hilo…nafahamu
wewe huna shida, mke wangu wewe ni mtu tofauti na wanawake wengine, lakini wewe
utafanyanini, kama wazazi wanataka uwe watakavyo, eeh...’akasema
‘Kwanini unaongea hivyo, kwani kuna kitu gani kibaya umekiona
dhidi yangu, au wazazi wangu, tulishaongea hayo sana tukayamaliza, au…kuna nini
cha zaidi?’ nikamuuliza huku nikimwangalia usoni.
‘Haya yanayoanza kujitokeza, yananipa shida kweli kweli, ndio
maana hata nilipokuwa hospitalini, nilikuwa nikihangaika kujua jinsi gani ya kuyaweka
sawa, na nikawa natafuta njia ya kuyasawazisha, lakini mwili ulikuwa
haukubali,..nilikuwa kwenye mtihani mkubwa sana...lakini sasa naona kila kitu
kitakuwa sawa , ni swala tu la kukubaliana...’akasema.
‘Kukubaliana?? Ukiwa na maana gani hapo, kwani hatukuwa
tumekubaliwana awali, mambo yalikuwa shwari au sio, au kuna tatizo, mume wangu
nakuomba uniambie ukweli, kuna nini kinachoendelea…?’ nikauliza bila kujali
lolote.
‘Kukubalina ni muhimu hasa kwa wote wanaohusika, ili mambo yaishe
tu, kwani tunataka nini zaidi, alikuwepo Makabrasha aliyejiaminisha, msomi,
tena wa nje, mjanja kweli kweli, ..anajua sheria, anajua mbinu za maisha, mbona
kashindwa kujilinda, leo yupo wapi,…mmh,hapo ndio mimi naogopa sana..’akasema
‘Umeliona hilo eeeh, vyovyote utakavyofanya, ukatumia ujanja ujanja
wa maisha, mwisho wake ..sote itakuwa hivyo, hakuna mjanja mbele ya mungu, sasa
kama ulidhulumu , kama ulifany madhambi itakuwaje, inatakiwa mimi na wewe
tuliwazie hilo, au sio mume wangu…’nikaongea , kuuma na kupilizia.
‘Ni kweli mke wangu, sasa tufanyeje ili mambo yawe sawa, ili tuwe
kama zamani, unakumbuka tulivyokuwa tunaishi, …eeh, japokuwa kiundani, nilikuwa
najihisi mnyonge…unanielewa hapo, mume nakuwa hivo hivyo…’akasema
‘Mume wangu tatizo nahisi kuna mtu kakuharibu akili yako, kwani
mimi nilikunyanyapaa, kila kitu tulifanya kwa makubaliano au sio…na nilikubali
kuwa pamoja na yote wewe ndiye mume wangu mwenye mamlaka ya mwanaume,
haijalishi kitu, na kukufanya uwe na nguvu zaidi tukafungua kampuni yako
mwenyewe, ili usiwe mnyonge…’nikasema
‘Ni kweli lakini bado ilikuwa sio kama yangu…nilikuwa sijalifahamu
hilo..lakini nilipogundua kuwa ni mimi tu, nilikuwa sifuatilii mambo, …unajua
hapo ndio namshukuru sana Makabrasha, kanionyesha mambo ambayo sikuwa
nayafahamu, mola ampe makazi mema peponi…’akasema.
‘Mume wangu pamoja na yote hayo, kwanza nakuomba kama upo tayari,
uniambie ukweli, sawa uliniomba msamaha, lakini kwa kosa gani, hujaniambia
hilo, lakini pia haya yanayotokea, …mpaka wewe kutafuta wakili yana ishara
gani, ni kwanini ukafanya hivyo..kama upo tayari nakuomba uniambie…’nikasema
‘Nipo tayari sana mke wangu na ndilo nililojiandaa nalo, sitaki
tena kupoteza muda…’akasema
‘Sawa..msamaha mnzuri ni ule unakiri kosa ulilolifanya au sio…kiukweli
na mungu ni shahidi au sio..sasa mume wangu nataka uniambie ukweli umefanya
kosa gani, mpaka ukafikia kupatwa na ajali, ilikuwa ni tatizo gani…?’
nikamuuliza
‘Mke wangu kweli unataka kuambiwa ukweli..utavumilia huo kweli,
hutanichukia, huta… lakini hata hivyo, mbona ukweli wote upo wazi tu,…mimi
nakumbuka nilishakuambia na kukuomba msamaha au sio…lakini anyway, hilo halina
shida, ila ukweli mara nyingi unauma, naogopa kukuumiza mke wangu ...’akasema
‘Mhh, kwanini ukweli uume, ..labda kama una mashaka, ...lakini
kama una nia thabiti,ya kujua na kukubali kwa nia njema sizani kama utaumiza,...tatizo
ni kuwa watu wengi hawataki kusema ukweli, wakichelea yatakayotokea baada ya
ukweli…’nikasema tukichezeana akili hapo, kwanza nikitaka kumweka sawa nisije
kumuathiri.
‘Hapo ndio kwenye mtihani,lakini kwetu sisi sizani kama kutakuwa
na matatizo au sio mke wangu, sasa hivi hata nikiongea ukweli, najiamini,
hakuna shida mke wangu kwahiyo leo ni siku ya ukweli, ukweli wote kutoka kwangu…’akasema
‘Kwanini sasa ujiamini, kwani zamani kulikuwa na kikwazo gani..?’
nikamuuliza
‘Nilikuwa sijafahamu haki zangu, lakini nashukuru kwa ushauri
wako, na ushauri wa wakili wetu…unajua mke wangu una akili sana, wewe unaona
mambo vyema kabisa, na ushauri wako unakuwa wenye manufaa sana, ingelifaa wewe
uwe mshauri wa watu…’akasema
‘Una maana gani..?’ nikauliza
‘Hata rafiki yako anakusifia sana, …unajua kushauri mambo, bila
kujali ..maana ukimshauri mtu eeh, akifanya inamsaidia na unajua tena …na mengi
uliyomshauri yamemsaidia, na hata ukiangalia mengi uliyoyashauri kwenye familia
yetu, tukayafuata imekuwa ni faraja sana…wewe unaangalia mambo kwa usawa,
ukiwajali wenzako, marafiki zako, familia yako, unaonaeeh, na zaidi hasa
ushahur huo ukiwa kwenye maandishi, ya kudumu ..yaani mimi sikuwa na mawazo
hayo kabisa hata marehemu alisema wewe ni jembe…’akasema
‘Kwahiyo sasa umepona upo tayari kwa haya,…?’ nikamuuliza kwa
mashaka
‘Ndio mke wangu, wala usiogope, kama huamini mpigie simu docta
wangu, nimepona wewe tuongee , maana hili ni la muhimu sana, ili tuyamalize
haya tuwe huru, nina imani baada ya haya, hakutakuwa na tatizo tena, ..kabisa
niamini mke wangu…’akasema
‘ Mume wangu…mimi japokuwa bado nina mashaka na afya yako, lakini
kiukweli nilikuwa nasubiria hatua hii, nilikuwa natamani sana, upone ili
tuyamalize haya matatizo, japokuwa sasa yamezuka haya mambo mengine, ni shida
kwakweli..sijui yataishaje, lakini tukimpata huyo muuaji, basi nina imani mambo
tayakwisha, nina imani..nikitoka hapa tutalimaliza hili...’nikasema
nikimwangalia, na yeye akawa akiangalia pembeni, nikamuuliza
‘Yah, hilo tutalifanyia kazi, kama mume , nina wajibu wa hilo…mke
wangu niamini hilo tutalimaliza,…’akasema akitikisa kichwa.
‘Vipi hali yako kwa ujumla, kweli umepona vyema, maana tusije kanza
kuongea hapa likazuka jingine,..?’ nikamuuliza tena….
‘Hahaha , mke wangu huamini, mimi nimepona, nilifuata masharti
yao,kama walivyotaka, japokuwa ilikuwa kazi nzito, maana nilikuwa kama mfungwa,
lakini kiukweli ilinisaidia sana, na waliponipima kwa mara ya mwisho waliniambia
nimepona kabisa, walisema kila kitu kipo safi, hakuna matatizo tena, usiwe na
wasiwasi na mimi mke wangu....’akasema.
‘Kwahiyo upo tayari kusema yote yaliyotokea, kuanzia yaliyotokea,
ukaja kupata ajali, baadae nakumbuka ukaja hata kuniomba masamaha, nimekuwa
nikijiuliza huo msamaha ulikuwa wa kosa gani, sasa je upo tayari kwa hilo ,
....?’nikamuuliza.
‘Hilo ndilo nataka tuliongelee leo kama na wewe upo sawa,..maana wewe
unaumwa, au tusubiri kwanza hayo mengine ila kuna hili la muhimu kidogo, mimi
kama mume ninawajibu wa kuomba ushauri kwako, au sio, ni la haraka, halihitajii
kusubiria, kama upo tayari, tuyajadili mimi na wewe...’akasema
‘Sawa itakuwa vyema…’nikasema nikiwa sijui anataka tujadili nini,
zaidi nilitaka yeye aniambie ukweli
‘Mke wangu kuna mengi yametokea, na muda umepita, na shughuli
nyingi zimesimama, kiasi kwamba mtu unashindwa uanzie wapi…lakini kuna haya yetu
wenyewe, haya ndio msingi, na nazidi kushukuru kwa mawazo yak o ya kuona
mbali,..sasa ni hivi,…’akatulia kidogo, na mimi nikasubiria.
‘Mimi nataka tuyamalize ikibidi leo, …ila nitakuwa mtomvu wa
shukurani kama nitamsahau Marehemu, na ndio maana naona umuhimu wa kikao chetu,
ili mengina yaishe , Marehemu alikuwa msaada wangu mkubwa, kiushauri, ....kanifungua
macho, hasa kwenye maswala ya maandishi,....’akatulia kidogo.
‘Una maana gani maana naona unatumia maneno hayo ya maandishi,
maandishi…?’ nikamuuliza
‘Hapo namaanisha mikataba...’akasema
‘Mikataba…mmh, tuna mkataba mmoja wangu mimi na wewe, au mingine
ni ya kikazi au?’ nikauliza na kabla hajajibu nikaendelea kuongea
‘Au wewe una maanisha mkataba huo wa hiari ..?’ nikauliza
‘Huo huo, ..yah, hiyo mikataba ya hiari, …’akasema
‘Lakini,..unajua nilishindwa kukuuliza kwa vile ulikuwa unaumwa,
nimeoana ajabu kubwa sana, mbona mkataba ule wa hiari, haupo tena, na sasa upo
mkataba ambao sio ule wa awali…?’ nikauliza
‘Mke wangu, unasema nini…hapana, mkataba ni huo huo, au…?’
akauliza
‘Hahaha, nilijua tu, ni janja yako wewe na Makabrasha, au sio…ule
mkataba wa hiari wa awali, umetoweka, na sasa upo mkataba wa kugushi, sasa
niambie maandishi au mkataba unaozungumzia wewe ni upi, wa kugushi au ule wa
awali…?’ nikauliza.
‘Mkataba wa kugushi!? Mke wangu hakuna mkataba wa kugushi, hilo
neno kugushi limetokea wapi tena …na unasema umetoweka kwa vipi , ni kitu
hakiingii akilini mke wangu, una…aah,..una- taka kusema nini hapo…’ akaniuliza
na maneno ya mwisho akaigiza lafudhi ya kizungu sijui alikuwa na maana gani.
‘Kwahiyo unajifanya hujui kuwa wewe na Makabrsaha ndio mliofanya
hayo!’nikamwambia huku nikimwangalia nikiwa na mashaka nisije nikazua balaa,
lakini sikuona mabadiliko,, yeye kwanza akainamisha kichwa chini, na baadaye
akasema;
‘Mke wangu nakupenda sana, .sitaki kukudanganya, kama nilivyosema
huu ni muda wa kuambizana ukweli, na…kiukweli kuanzia sasa sitaki nikufiche
kitu.,..nitakuambia kila kitu kilichofanyika, na nina imani utanielewa.’akasema
‘Sawa ukifanya hivyo, mbona tutaelewana tu, mimi sina shida,
mwenye shida ni wewe tu ambaye ulihangaika na hadi kubadili mikataba, na ajali
ikaja kukuta, nahisi ni katika kuhangaika huko, sijui ulikuwa unaogopa nini..’nikasema
‘Najua,…hilo sio siri, sasa ni hivi, kiukweli ilibidi nifanye
jambo, maana nisingelikubali mimi na wewe tuje kuachana, kisa mkataba, hapana
mimi nakupenda sana mke wangu,..bila kujali hayo…unasikia, mkataba na nini, ni
katika kujihami tu, au sio… na mimi naahisi kuwa, nitailinda ndoa yangu kwa
kila hali, hilo nakuahidi, mke wangu, ..’akasema
‘Sawa, nimekusikia..’nikasema
‘Na ndoa hapa nina maana ya kila kitu, familia, mali, na..maisha
yetu ya kila siku, kufungwa kwako ilikuwa moja ya pigo kwangu, ..sikuwepo
nyumbani, nilikuwa naumwa, nilitakiwa kama ni kufungwa nifungwe mimi…’akasema
‘Kwani wewe ndio uliua..?’ nikamuuliza
‘Hapana, wewe wanakushuku tu, kama wanakushuku, na mimi nipo,
ningeliwaambia wanifunge mimi,…hadi hapo ukweli utakapopatikana, lakini
nilikuwa sijiwezi, naumwa, nipo hospitalini,ningelifanya nini..ni mtihani..lakini
sasa nipo ngangari, tutapambana na hao watu…’akasema
‘Kwahiyo kwa kifupi ni kweli kuwa uliubadili mkataba wetu kutoka
ule wa asili na kutengeneza mwingine wa kitapeli..’nikasema nikimuangalia,
maana hapo nilitumia lugha ya kumkwanza, lakini hakubadilika, alikuwa vile vile
wa kujiamini.
‘Mke wangu, usitumie lugha hiyo, ‘kubadili’ …maana kiukweli hakuna
kitu kama hicho, kwa lugha yako hiyo ya kubadili, au kugushi hakuna kitu kama
hicho eeh,....mimi kama mume wako niliona ni heri nifanye jambo, kuilinda ndoa
yetu, na nilichofanya ni sahihi kabisa, kwa mujibu wa mkataba unavyosema..
‘akasema
‘Kwahiyo ulibadili mkataba kwa kutaka hayo unayoyataka wewe, na
kujiwekea hayo mamlaka ya kufanya utakavyo.., nataka jibu tu hapo, kweli au si
kweli, je wewe na mkabrasha mlibadili kitu kwenye mkataba, niambie ukweli tu
hapo..?’ nikauliza
‘Mke wangu…’akataka kujitetea
‘Hilo ni muhimu kwangu, kauli yako ni muhimu sana, ni kweli au si
kweli, ukijibu hilo itakuwa ni faraja kwangu, niambie ukweli,..mlibadili huo
mkataba au sio, ni kwanini mlifanya hivyo, nataka jibu la ukweli, kwasababu
umesema leo utaniambia ukweli..sio ndio hivyo..?’ nikamuuliza
‘Ndio..leo nitakuambia kila kiu ..muda ukiruhusu, ni wewe tu..’akasema
‘Haya jibu swali langu…’nikamwambia..
NB: Muda umekwisha, sehemu hii itaendelea…kuna tukio muhimu sana
hapa hutaamini..ngoja niliweke sawa, lakin ngoja nitangulize kipande hiki.
WAZO LA LEO: Mkataba ni kitu cha makubaliano, na
mkataba ulio sahihi ni ule pande mbili zinahusika, na kukubaliana,..mikataba
mingi hasa ya ajira, inakuwa ya pande moja, na muajiriwa anakuwa hana hiyari,
ni kukubali tu, huu sio mkataba sahihi.
Kuna mikataba ya mauziano ya bidhaa, kusiwe na ujanja ujanja wa
kutapeliana, hii ni dhuluma, hata kama ukishinda kumshawishi mwenzako
ukamdhulumu hili ni deni kwako. Lakini pia kuna mikataba ya hiari kati ya pande
mbili, ni lazima kila pande irizike na kila kipengele. Tukumbuke mkiwa wawili
mwenyezimungu yupo kati yanu, au hata mkiwa wengi mwenyezimungu yupo
analithibitisha hilo, hadi kwenye nafsi zetu, kudanganyana ni kujidanganya
wenyewe. Tusipende kudhulumu kwa njia hii dhuluma ni dhuluma na madhara yake ni
makubwa .
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment