‘Sikuwahii kumuona kwa sura,…maana kila nikimuota, anakuwa kambeba
mtoto, halafu anageuka kunipa mgongo, usoni…simuoni, najaribu
kumuangalia,..hapo hapo nashtuka kutoka usingizini… lakini kwa maumbile na
wajihi namfahamu…’akasema
‘Kwanini unaficha ukweli mume wangu kwanini uanigiza uwongo…?’
nikamuuliza
‘Ukweli ndio huo ninaokuambia mke wangu, na ilikuwa ni njozi, na
njozi kama hizo ni nyingi za ajabu, na…wakati mwingine nahisi kama ni kweli…’akasema
‘Kwanini unahisi hivyo..?’ nikamuuliza
‘Watu wanaongea….wanayosema ni kama kweli nilifanya…lakini nikija
kwenye akili ya kawaida,…sikumbuki kitu, …nachanganyikiwa mke wangu, niamini,
wewe hujui ni hali gani ninayopitia, najua utafikiria na..na…naigiza, lakini
mungu mwenyewe anajua…’akasema hivyo
‘Sasa hiyo ndoto…iliishaje, na huyo mtoto ulimpataje..?’ akauliza
‘Ndoto!!? Eeh, ..ndoto, inakuwa hivi, ni…sehemu sehemu tu…ila hiyo
ya mtoto kila ikija, haiishi, au ..hata sijui…wakati mwingine nahisi labda ni
kwa vile…labda, nasema labda ni kwa vile.. nilitamani sana kuwa na mtoto wa
kiume…si ndio hivyo…’akasema, hapo ndio akazidi kunipandisha munkari wa hasira.
‘Nasikia kwenye mkataba wenu, mumeandika kuwa mtoto wa kiume
atapewa mamlaka ya kusimamia mali , kama wazazi watakuwa hawapo…na huyo mtoto
umempata nje ya ndoa, ina maana anakuwa na haki zaidi ya watoto wa ndoa ni haki
hiyo…?’ nikamuuliza
‘Mke wangu, hebu kwanza nipe nafasi ya kufikiri…nahisi ..sipo
sawa,..na hayo ya mkataba,..kuna mkataba mwingine upo tena,…ooh , hata
sikumbuki, …basi hilo la mkataba mwingine nitakuja kukuambia ni kwanini, kwanza
tugange hili hapa…’akainua ule mkataba juu.
‘Nilishakuambia huo mkataba wako siutambui, na sitautambua,..na
kwa vile umedhamiria kuung’ang’ania, sawa…mimi nitachukua hatia za kisheria, na
ngoja sheria ichukue mkondo wake…’nikasema
‘Mke wangu mkataba huu ni nani aliubuni, nijibu swali hilo kwanza,
halafu twende sawa…?’ akauliza
‘Huo uliubuni wewe na marehemu..’nikasema
‘Huo unaosema ulikuwepo, sijui ni gani,….aliubuniwa na nani…?’
akaniuliza
‘Huo, ambao ni wahalali, ambao tulikaa mimi na wewe na wakili
wetu, sio huyo marehemu, ilikuwa ni wazo langu…nielewe hapo, usilete ujanja
ujanja wako, mimi nazungumzia mkataba huo…ambao mumeuharibu nyie wawili…’nikasema
hapo akanywea.
‘Sasa mke wangu ni hivi, kama unaona huu mkataba una kasoro,..kiukweli
mimi sifahau,… tufanye jambo moja, ..tukae kikao, tujadili, tupitia vipengele
kimoja baada ya kingine, kama kuna makosa, wakili si wapo, yupo wakwako na wa
kwangu au sio, basi tutarekebisha hayo makosa, unaonaje hilo wazo langu…’akasema
‘Tatizo lako mume wangu, marehemu alikughilibu, unafikiri mimi ni
mtoto wa jana,, huo ni ujanja wako, nia ni kukwepa sheria, unauogopa ule
mkataba wa awali, kwa makosa uliyoyafanya,… kwahiyo unachotaka hapa ni kuvuta
muda, ili uanzishwe mkataba mpya, na utaanza kufanya kazi lini…huo ujanja kawadanganye
watoto sio mimi…’nikasema
‘Mke wangu nisaidie, unajua hali niliyo nayo inanitesa, si
nimekuambia, kuwanahisikama bado kuna tatizo, na tatizo hilo kama walivyosema
madocta, haliwezi kupona,..na toka siku ile waniambie hivyo, mimi nikawa sitaki
hata kuhudhuria kiliniki zao…’akasema.
‘Tatizo gani…?’ nikamuuliza
‘Mimi sitaweza kuzaa tena…’akasema
‘Kwanini…?’ nikauliza
‘Kutokana na athari za ajali, uti wa mgongo umeathirika…’akasema
‘Mbona mimi hilo sijui, sijaambiwa na docta…?’ nikauliza
‘Hilo sikutaka wakuambie wewe …’akasema
‘Kwanini sasa umeamua kuniambia mimi..?’ nikauliza
‘Ni ili uone umuhimu wa watoto…mtoto wa kiume…’akasema
‘Hahaha, mtoto wa kiume ndiye kakufanya ukafanya haya yote, sasa
unaona madhara yake,..umezini, umevunja mkataba wetu, na matokea yake ni nini,
unaona madhara ya zinaa yalivyo, unatusumbua hata sisi tusiohusika, ndio huyo
mtoto wa kiume unayemtaka, au sio…?’ nikauliza
‘Hapana mke wangu,…nielewe hapo, mimi nimekuwa nikiwaza sana, hadi
naota, eeh, kwahiyo hali hiyo ndiyo inaniandama hadi kuja kufanya mambo ambayo
siyakumbuki, mawazo…na docta kaniambia hiyo hali isipodhibitiwa naweza nika…potea,
hata sijui…au kufanya mambo maovu…’akasema
‘Kama yapi…?’ nikauliza
‘Kama kuna kitu …kimeniudhi, au kukasirika, au ..si unajua tena
wanadamu tulivyo, unaweza ukatamani hata kuua, ..mtu ambaye unaona ni kikwazo
kwako…unielewe mke wangu naongea kama alivyosema docta…’akatulia alipoona
namuangalia kwa mashaka na uso umejaa hasira.
‘Siwezi kuamini maneno yako …siku hizi sitakuamini tena, na haya
yote unaongea tu, kujihami, au umeambiwa useme hivyo, uigize hivyo, ili
nikubaliane na matakwa yako, na kwa hilo, usijisumbue kitu…’nikasema
‘Mimi nakuambia ukweli, kama utaamini sawa, kama hutaamini, shauri
lako, ili yasije kutokea ukaja kujutia baadae,…’sasa akasema kwa sauti ya
kawaida sio kama ile ya kudeka.
‘Kwahiyo hayo maovu umeshayafanya au..?’ akaniuliza
‘Maovu gani..?’ akaniuliza kwa mshangao tena
‘Si umesema kuna hali inaweza kukutokea kwasababu ya msongo wa
mawazo, na hali hiyo inaweza kukutuma kufanya maovu…je umeshayafanya hayo
maovu, usisingizie kuzini, maana hilo tendo, ulilifanya kabla ya ajali…’nikasema
‘Kuzini…?’ akauliza sasa akiwa kama anashangaa,
‘Acha ujanja wako bwana…nimeshakuelewa, na tusipoteze muda hapa,
kuna maswali nataka kukuuliza, na ukumbuke kwenye mkataba wetu wa awali,
ulisema tusije kudharauliana, kila mtu aheshimiwe kauli yake,…’nikasema
‘Lakini mimi sijazini…’akasema
‘Huyo mtoto ulimpataje..?’ nikamuuliza
‘Mtoto…!! Wa kiume eeh, nikuulize wewe,…’akasema hapo
nikamuangalia machoni, nikamuona kweli anahangaika, kama kukumbuka jambo,
lakini akilini nikajua anaigiza tu,
‘Mtoto, umesema mtoto,…yawezekana,..ni kweli labda sio
ndoto,..mtoto wa kiume eeh, basi,…mke nisaidia jambo, tumtafute mtoto wetu,
..unaelewa,…’hapo akatulia aliponiona namuangalia kwa uso uliojaa hasira.
‘Wewe umezini, una mtoto nje ya ndoa, ndio maana mlikaa wewe na
marehemu mkaandika maelezo kuhus huyo mtoto wa nje, awe na haki sawa, haya
uliyafanya ukiwa na akili zako timamu, kabla ya ajali…na siku ile ya ajali,
ilitokea kwa vile ulikuwa una haraka ya kubadili mkataba wa awali, na huo wa
kugushi…’nikasema
‘Unasema nini…?’ akaniuliza kwa mshangao
‘Ndio maana nakueleza kuwa kila jambo mimi nalifahamu…’nikasema
‘Mke wangu ...kwanza tuanze moja, hilo la mkataba, au sio,
tumeshamalizana nalo kuwa mkataba uliopo ni huu, kama upo mwingine basi
tutautafuta, tukubaliane hivyo, ili tuyamalize haya…’akasema
‘Na nikikubali, ili iweje…?’ nikauliza
‘Ili maisha yaendelee, tuendee na shughuli zetu za uzalishaji kama
kawaida, kampuni hazifanyi kazi, …madeni yanaongezeka, watu wa kodi wamenijia
juu, wataka kufunga kampuni,..na hali hiyo inaniweka kubaya,..naombe mke wangu
uyamalize ili na mimi nipate nafuu, niondokane na dimbwi hili la mawazo na
mashaka…’akasema
‘Hilo sitachoka kulirudia, hata mbele ya Mahakam, kuwa Mkataba
ninaoufahamu mimi ni ule ule wa mwanzo, ambao haukuwahi kufanyiwa mabadiliko,
hata kama utaumwa,..au… utachanganyikiwa hiyo umejitakia wewe mwenyewe…vinginevyo…’hapo
nikatulia
‘Nakusikiliza mke wangu, vinginevyo,..nini…?’ akaniuliza
‘Uniambie ukweli wote…’nikasema
‘Ukweli gani sasa mke wangu mbona tunarudia kule kule, sasa
sikiliza mke wangu tusipoteze muda, niambie kile unachokitaka…huo ukweli ni
upi, eeh…na mimi nitakujibu, naona
tunapoteza muda bure, na mimi sijisikii vyema…’akasema, nikamtupia jicho,
kiukweli hali aliyokuwa nayo, yaonekana kama kweli hayupo vyema, lakini sikujali
tena moyo nafsi ilishakataa…hapohapo nikasema
‘Kwanza nataka unipe majibu kwa haya maswali nitakayokuuliza..’nikasema
‘Haya uliza…’akasema sasa akiwa kama anakata tamaa.
‘Na..kama usiponijibu tukitoka hapa wewe nenda kwa wakili wako na
mimi kwa wakili wangu tunakwenda kukutana mahakamani, na ndoa hapo haipo tena,
umeshaivunja wewe mwenyewe..na ukumbuke kwenye mkataba wetu wa awali kuna
kipengele hicho, cha kupuuzana, .....’nikatulia kidogo
‘Nakusikiliza mke wangu uliza tu hayo maswali..kabla sijazidiwa
kabisa, mwili hauna nguvu,…ki-ki-ukweli…! Sa-sawa..mimi sitakupuuza kabisa,
hicho kipengere hata mimi nimekiona, .. lakini hilo la kuvunja ndoa sikubaliani
nalo na halipo, na halitakuwepo.....’akasema.
Alipiga miayo, akajinyosha, halafu akaniangalia, na kusema
‘Sasa nipo tayari…’akasema
‘Kwanza kwanini mliamua kubadili huo mkataba bila ya
kunishirikisha?’ nikamuuliza
‘Jibu nimeshakupa ama kwa kumbukumbu jibu ni hivi...mimi sijui
kama kuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa kwenye huu mkataba, naapa…, na ndio
maana naona leo tukae kama yapo basi tukayafanye, mimi sina shida,, mimi
nafahamu kuwa huu ndio mkataba wetu, kama kuna mkataba mwingine zaidi ya huu
nionyeshwe basi, kwanini tupoteze muda...’akasema akionyesha kujiamini.
‘Swali la pili...’nikasema
‘Aaah, umerizika na jibu langu kwanza, sijakupuuza mimi, kwanza
turiziane?’ akaniuliza
‘Hujanijibu swali langu, sijarizika na jibu lako, lakini
tusipoteze muda, hapo kwangu naona kama umenipuuza tuendelee na swali
jingine’nikasema
‘Unataka niseme nini mke wangu sasa, mbona unaniweka kwenye wakati
mgumu, au wewe una majibu unayataka, basi niambie hayo majibu,...’akasema
‘Swali la pili, je una mtoto nje, uliyezaa huko nje ya ndoa....?’
nikamuuliza
‘Jibu la swali hilo,…eeh,… sina uhakika na hilo, nakumbuka ndoto
inasema hivyo, ila kiuhalisia mimi sina uhakika, kama huyo mtoto yupo basi niletewe,
itakuwa heri na kwangu pia, ili nispate shida ya mawazo na mashaka, kiukweli
hilo linanipa shida sana mke wangu,....’akashika kichwa chake kwa mikono yote
miwili.
‘Usijifanye mjanja wa kujizulia ugonjwa wa kuchanganyikiwa,
usinifanye mimi mtoto mdogo, wewe ulishapona, huo ni ujanja ujanja wako
tu, wa kutaka kunighilibu, nijibu swali langu, je wewe una mtoto nje, na ulizaa
nani?’ nikamuuliza.
‘Kama wewe unadai nina mtoto,…mimi sijui..na ndoto huwezi
kuiamini, au sio…sasa kama yupo na umeshamuona niletee ili iwe ushahidi..na
utakuwa umenisaidia na mimi, hilo ndilo jibu langu…’akasema
‘Kwahiyo wewe unataka ushahidi…si ndio…basi utaupata, na je
ukiupata nichukue hatua gani..?’ nikauliza
‘Mkataba huu utahukumu..ndio ulioupendekeza wewe au sio, tutaangalia
sheria inasemaje, au sio…vinginevyo…’akasema na kutulia kama anawaza jambo
‘Vinginevyo nini…?’ nikamuuliza nilimuona akihangaika kama
anasumbuliwa na kitu kichwani, ..lakini kama nilivyosema awali, huruma
ilishaondoka, sikujali tena
‘Mke wangu naomba unipe muda, nikafanyie uchunguzi,…’akasema
‘Uchunguzi wa nini tena…?’ nikauliza
‘Kuhusu hilo la mtoto… sikumbuki hilo kabisa, sina uhakika siwezi
kukudanganya,..ndoto nyingi niliota zinakuwa kama za ukweli…kuna …unasikia mke
wangu, lakini ni siri yetu, hata…siku marehemu anauwawa, ok, tuache tu…’akasema
sasa akinitolea macho.
‘Hayo utayasema mbele ya mahakama,…na mimi nitakuwa shahidi, na
ukumbuke hapo sitasimama upande wako,…kuna mengi nayafahamu dhidi yako, siku
hiyo ndio utayasikia…’nikasema
‘Mke wangu nisaidie, mimi ni mume wako…nahisi kama nimetenda kosa…isije
ikawa ni kweli…labda nimeua kweli…’akasema sasa akinitolea macho
‘Umeua…?’ nikamuuuliza
‘Sijui…mke wangu sijui…ndoto zinaniandama, siwezi kulala….nisaidie
mke wangu….’akasema akiwa kama ananiomba kwa mikono
‘Umemuua nani…?’ niikamuuliza
‘Usirudie hiyo kauli tena, mimi sijaua, au sio, ni ndoto tu mke
wangu,…naogopa mke wangu, usije kusema hivyo tena, unasikia, …’akasema kweli
sasa akionyesha kuhaha
‘Swali la tatu, ni nani mwanamke mliyezaa naye?’ nikamuuliza, sikujali
huko kuhaha kwake, japokuwa kiukweli nilimuona akipata shida.
‘Mwanamke niliyezaa naye!?..mungu wangu, ni nini tena hiki…!’akashika
kichwa
‘Jibu swali acha ujanja…’nikasema
‘Mke gani jamani, mke wangu ni wewe, nimezaa na wewe, nimekumbuka
mwanamke niliyemuona kwenye ndoto ni wewe…wewe ndiye aliyemchukua mtoto,
ukakimbia naye, unasema sio wangu, sio wa halali…ukataka kwenda kumtupa, ni wewe, niambie mtoto wangu yupo wapi,
niambie ....’akasema sasa anasimama kwa
hasira akinielekea mimi.
‘Wewe mwanaume…hebu acha huo mchezo wa kuigiza…’nikasema sasa
akawa ananisogelea katoa macho, anatetemeka, mimi nikasogea, na nilipoona hali
inazidi, nigeuka na kukimbilia mbali na yeye, mara akadondoka sakafuni, na
nikasikia kama akakoroma nikajua nimeua…
***********
Nikarudi pale alipolala
sakafuni…niliona sasa katulia, nikashika mapigo ya moyo, nikaona yanapiga kwa
mbali, lakini inatia mashaka, haraka nikachukua simu, nikitaka kumpigia docta,
mara mtu huyo katikisika
Nikaacha simu, na kumuangalia….akaanza kujiinua, halafu akakaa…akawa
sasa anaangalia huku na kule, mara akasimama,..huku anayumba yumba
‘Kumetokea nini…?’ akauliza
‘Hebu kaa pale maswali yanaendelea…’nikasema
‘Maswali!!, maswali gani…?’ akauliza
`Swali la nne, je ni wewe uliyechukua mikataba kwenye kabati langu,
la hapa na kule ofisini ?’ nikauliza
‘Mimi.!!!...ofisini kwako, lini,..?’ akawa anashangaa , akageuka
akauona ule mkataba, kwa haraka akauchukua na kuishikilia mkononi, halafu
akageuka kuniangalia..halafu, akageuka kuangalia mlango unaolekea maktaba, akaangalia
saa;
‘Mbona umewahi leo kutoka kazini, …?’ akaniuliza
‘Swali jingine…umeniupuuza kunijibu swali la awali, hiyo
inanakiliwa kwenye kumbukumbu, wakili sikia hiyo…’nikasema, akageuka huku na
kule kama anatafuta mtu, nahisi ni hapo niliposema wakili sikia hiyo, hakuelewa
mimi nina maana gani.
Swali la tano…, Je siku makabrasha alipouliwa ulikwenda kwake
kufanya nini?’ swali hili likamfanya ashituke na kugeuka akaniangalia kwa
mashaka, akageuka na kuangalia mlango wa kutoka nje, kama anaogopa vile, baadae
…, akasema;
‘Ma-mamamaah...ina maana ni kweli.....haiwezekani, mke wangu
kumetokea nini, ulirudi ulinikuta nipo wapi, niambie mara moja, maana hii ni
dalili mbaya, mke wangu tafadhali...halafu alishazikwa, ….au..sikumbuki mimi,
hivi kweli eeh…’akasimama sasa..na kuanza kutoka nje
‘Unakwenda wapi, haujamalizana, nimeshakuambia nikitoka hapa mimi
naelekea kwa wakili wetu, nafuata hatua nyingine, tutakutana
mahakamani...’nikasema lakini mwenzangu alikuwa anaondoka, haangalii nyuma
akasema;
‘Nawahi mazishi....’akatoka, mimi nilicheka kidogo na kusema
‘Janja yako...nafikiri wewe hunifahamu eehe...’na mimi
nikamfuatilia huko huko nje, nilitaka hili tatizo nilimalize leo, nimuachie
hiyo kazi wakili, sasa asonge mbele, tulifikishe hili tatizo kwenye vyombo vya
sheria,…
Kwa haraka na mimi nikatoka nje, nikamuona akiingia kwenye gari lake,
na mara simu yangu ikaita, nikaipokea kabla sijaangalia mpigaji ni nani. Huyo
mtu akasema;
‘Mimi ni docta .....’akasema kumbe alikuwa yule docta aliyemtibia
mume wangu, nikashukuru maana nilikuwa na mpango wa kumpigia, kuhakiki haya
anayoyafanya mume wangu kuwa ni ya ukweli au anaigiza tu.
‘Hali yako docta tena nilikuwa nataka kuongea na wewe..’nikasema
‘Ndio ...ndio maana hata mimi nilitaka kujua hali ya mume wako,
anaendeleaje kwani kipindi kile cha matibabu, kulikuwa na docta mwenzangu,
ambaye alikuwa akimwangalia kwa upande wa kumbukumbu, na alitaka kujua kama
kuna hali yoyote inayojitokea kwake..yupo hapa nyumbani ?’ akaniuliza
‘Ndi-ndio…lakini anatoka..’nikasema
‘Sasa Yule docta wake kaja leo ndio karudi toka safari’akasema
‘Kwahiyo anasemaje…?’ nikauliza nikionyesha kushangaa.
‘Sijui kama mliwahi kuongea naye kipindi kile, kuna kitu kwa mume
wako ambacho alikigundua, na kwa muda ule hilo hatukuwa tumelitila maanani sana..lakini
kuna matukio yalitokea…kipindi hicho docta ameshaondoka…’akasema
‘Matukio gani…?’ nikauliza
‘Kusahau..au kujiwa na kitu kama njozi…anaweza akalala, na kuota,
akafanya vitu kwa vitendo, au mchana, akawa kama kalala, akafanya mambo tofauti
na utashi wake, inakuwa kama njozi…’akasema
‘Unasema nini…?’ nikauliza kwa mshangao.
‘Kuna matukio yalitokea akatoweka hapa hosp, na baadae akarudi,
akiulizwa kafanya nini, anakuwa hakumbuki,…au akakumbuka jambo, akafanya kwa
umakini zaidi, au anakuwa na akili ya ajabu unaweza kumuuliza jambo, akakujibu
kwa umakini sana,..na hali hiyo ikiisha, hawezi kufanya hivyo…’akasema
‘Docta …’nikasema sasa nikianza kuingiwa na mashaka.
‘Sasa docta wake kaja, na kaniambia hayo yanaweza kumtokea mgonjwa
wa namna hiyo, inatakiwa kuwa makini naye sana, kwani anaweza kufanya jambo la
hatari....’akasema
‘Unasema nini docta mbona hamkuwahi kuniambia kitu kama
hichoo’nikasema kwa hasira.
‘Baada ya uchunguzi, ...kipindi kile tulipokuwa naye, alionyesha
dalili, kuwa kapona, na mwenzangu akawa keshaondoka, ...tulimwambia yule docta
mnayeishi naye, maana wakati huo wewe ulikuwa na matatizo… ulikuwa jela,..sasa
kwa vile mwenzangu karudi leo na tukawa tunafuatilia jarida la mume wako..’akasema
‘Docta …’nikataka kusema lakini yeye akaendelea kuongea
‘Sasa… kwanini, mume wako hafiki kwenye kliniki yake maana hiyo
ingelisaidia kujua hatua za maendeleo yake, yeye aliandikiwa afike kila mara
hapa hospitali kwa kliniki yake,hajafika kama tulivyomuagiza, ndio maana
tukaamua tukupigie’akasema.
‘Docta mimi ninaweza kuwashitaki, ..hilo ni kosa kubwa sana, maana
sasa hivi nimemuona mume wangu kama kachanganyikiwa, na mimi nilifikiria kuwa
anajifanya..kwasababu nimekuwa nikimuuliza maswali., anajibu kama anaigiza,
kuwa hajui, mara anasema kasahau, mara aliota,..katoka sasa hivi na gari, yupo
kama ...’nikasema.
‘Mfuatilieni haraka,...na mleteni hapa hospitalini hiyo dalili inaweza
kuleta matatizo mengine docta wake yupo, na akiondoka itachukua muda kurudi.
....’akasema docta, na mimi nikakata simu yake na kuingia kwenye gari langu,
nikijaribu kumfuatilia, sikujua kabisa kaelekea wapi.....oh, ina maana mume
wangu akchanganyikiwa kweli....
NB: Kwa leo ndio hivyo,
WAZO LA LEO: Kwa
wandoa mmoja anapoumwa, ni vyema mkajaliana kwanza, hata kama kulikuwa na
sintofahamu, migongano ya kindoa, ya kifamilia, na mitihani mingine ya kimaisha,
hayo yote ya kibinafsi, na masilahi yawekwe kando kwanzao, muangalie swala la
afya, swala la ugonjwa, kwani afya ni bora kuliko mali, kuliko hayo mnayokosana
nayo..na huenda huo ukawa na mtihani katika kutatua matatizo yenu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment