Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, August 22, 2017

DUWA LA KUKU....40


‘Unasema yaonakena kuwa amefariki, ina maana huna uhakika bado…?’ akauliza kwenye simu na kuendelea kusikiliza

Baba mtu aliuliza huku akijaribu kuangalia pembeni ili kijana wake asisikie anachoongea…, baadae akasikiliza kidogo, halafu alipomaliza kuongea na simu akamgeukia mtoto wake na kusema;.

‘Oh….sasa sijui itakuwaje…’akasema

‘Ni nani amefariki..?’ kijana akauliza na baba yake aliposikia hivyo akajua kijana wake kamsikia, hakutaka ayajue hayo kwanza, akasema;

Tuendelee na kisa chetu...


************************


Nilitulia kwanza nikiwa sina nguvu,...unajua kuishiwa na nguvu..nikajikuta nimesema tu...

‘Bado hawana uhakika…, yule mtu ana roho kama ya paka, nasikia kuna kipindi ilitokea hivyo, wakawa wameshajua kafariki, baada ya muda akazindukana..ngoja tusubirie…’akasema akiangalia pembeni, na kijana wake akamsogelea na kuuliza;

‘Lakini ni nani huyo..?’ akauliza kijana, na mara simu ikaita , ilikuwa simu ya kijana, na kijana kwa haraka akataka kuisikiliza....na baba mtu akataka kumzuia kijana asiipokee, lakini kijana alikuwa ameshaiweka hewani, akawa anasikiliza….

‘Ndio unasema, kuwa…taarifa,… taarifa gani hiyo, sijasikia taarifa yoyote..kwani imekuwaje, hakuna nilichosikia bado, sawa nasubiria…kwani…!’ kijana akasema, na kukatiza, yaonekana mpigaji alishakata simu. Kijana akageuka kumuangalia baba yake, baba yake alikuwa karibu akijaribu kusikiliza hayo maongezi.

‘Ni nani huyo…?’ baba akauliza akimuangalia kijana wake,na kijana wake akawa anageuka wasiangaliane na baba yake, akasema;

‘Ni rafiki yangu tu…’akamdanganya baba yake, na baba yake akageuka akiwa anataka  kuondoka, kijana akageuka na kumuona baba yake keshafika mlangoni, akamuuliza;

‘Sasa baba mbona unaondoka, unakwenda wapi..?’ akauliza kijana akitembea kutaka kumzuia baba yake asiondoke , lakini baba yake alishafika mlangoni..
‘Lazima niende huko hospitalini nikaonane na huyo mtu akifariki kabla hajamalizana na sisi unajua itakuwaje,…yaani ni muhimu sana nionane naye vinginevyo, hatutaweza ..oh, ngoja niondoke mwanangu, sijui itakuwaje…’akasema baba mtu, akionyesha kuchanganyikiwa.

‘Kwani ni nani huyo… mbona sikuelewi…baba, niambie..mbona unaondoka…’kijana akasema na baba yake akawa ameshatoka nje, na kwa haraka kijana akachukua simu na kupiga namba na alipopokelewa, akasema;

‘Mzee kaondoka sasa nifanye nini..?’ akauliza na alipojibiwa akasogea kwenye sofa akakaa, na kuinamisha kichwa chini, alibakia pale kwa muda, baadae akasimama, …akatembea huku na kule kwa muda bila kutuilia, baadaye akashikwa kichwa na kujikuna kwa mara nyingi, alikuwa kama anawashwa, akawa anahangaika kwa muda, baadaye huyo akatoka nje

Wakati anatoka simu yake ikawa inaita, yeye hakutaka kuipokea, akawa anatembea kuelekea kituo cha mabasi hadi sehemu wanapokaa vijana na kuongea na mmojawapo, wakasogea pembeni akapewa kitu mkononi, akatoa pesa na baadaye akaondoka pale na kuelekea sehemu nyingine…


****************

‘Umemaliza….’akaulizwa na mkewe na hapo akashika kichwa, na baadae akasema;

‘Hayo ndio maelezo ninayoweza kuwasimulia, kwani baada ya hapo ndio ikaja taarifa kuwa yule mzee mtaalamu amefariki kiukweli, na taarifa hizo nilizipata nikiwa nimeshafika hospitalini, nikiwa nahangaika kuonana naye…

‘Ina maana siku ile ulikuwa upo hospitalini muda, wakati tunakutafuta kwenye simu…?’ akauliza mkewe.

‘Ndio, sikutaka kupokea simu zenu maana ningeliwajibu kitu mshindwe kunielewa,…nilifika hapo hospitalini muda, nia kuonana na huyo mtu, ili nimuwahi aniambie cha kufanya, maana kijana ataponaje, wakati alikuwa hajamaliza hayo mambo yake…’akasema.

‘Sasa ikawaje….?’ Akaulizwa.

‘Yaani pale nilikuwa kama sio mimi….nilitaka hata kwenda kuiona hiyo maiti yake, nilikuwa siamini kuwa huyo mtu ni marehemu..., lakini hao wahusika wa hapo hospitalini walinikatalia kuiona hata hiyo maiti.. , basi nikahangaika pale, baadae wazo likanijia, nimpigie simu huyu adui yake, lakini sikuwa na namba yake ya simu, nikampigia kijana wangu simu;

‘Unaweza kunipatia namba ya huyo mganga wako…?’ nikamuuliza huyo kijana hata bila ya kusema haloo.

‘Mganga wangu, yupi….baba…sipo vizuri kwa sasa, nipigie baadae…’kijana akakata simu, nikahamaki nikampigia tena na tena, baadae nikasikia,

‘Simu unayopiga haipatikani…’hapo nikajua mambo yameharibika.

Nilibakia pale hospitalini kwa muda, na baadae ndio nikapokea simu ya mke wangu akiniarifu kuwa taarifa kamili zimekuja huyo mtu keshafariki, na wao, hawawezi kuondoka hapo, hospitalini  …mimi sikutaka hata kuuliza kwanini hawataki kuondoka hapo hospitalini, nilikata simu.

Kiukweli kuwa muda huo ungeliniona ungelinihurumia, kuna muda, ninalia, kuna muda ninaongea peke yangu , hata sijielewi,.....baadae nikaona watu wanafika, nikamuona mume wa rafiki wa mke wangu ambaye ni askari akifika, mimi nikaona niondoke tu...

‘Kwanini sasa na ulitakiwa uwepo hapo na mkeo ili kujua kinachoendelea…?’ akauliza mama Ntilie.

‘Hapo kichwa hakikuwa changu, na sikuwa nafahamu kinachoendelea kati ya mke wangu na huyo marehemu kuwa walikuwa huko hospitalini kwa dhumuni gani, hilo sikuwa nalifahamu,..na muda huo akili yangu ilikuwa inawaza mengi, nawazia jinsi gani nitaweza kumsaidia kijana, nawazia hatima ya yoe hayo, ina maana baada ya hilo, kijana atamwambia mama yake, na babu yake, kwahiyo itakuwaje, ndoa itavunjika.

Nilitoka hapo nikawa nimepanga sasa niende kwa rafiki yangu mmoja, rafiki yangu huyo ndiye yule aliniunganishia na huyo marehemu, nikijua yeye anaweza kunisaidia kimawazo, nilipofika kwake, hakutaka hata kuniona, kisa nilipofanikiwa sikumjali, ni kweli kipindi hicho, sikutaka hata kumsikiliza matatizo yake, ..

‘Sikiliza kwanza, kipindi kile nilikuwa nimechanganyikiwa…’nikasema kumwambia, hakutaka hata kunikaribisha ndani, mimi nikaingia kama kulazimisha tu..

‘Unachanganyikiwa ukiwa na hali nzuri, hiyo hali nzuri ungeipataje kama sio mimi kukushauri uende kwa huyo jamaa, sasa naona umefirisika, au sio,.sasa  unataka nini kwangu…?’ akaniuliza.

‘Nina shida, umepata taarifa…’nikamwambia

‘Taarifa gani…?’ akaniuliza akiniangalia kwa uso wa kutaka kujua.

‘Yule mtaalamu kafariki…’nikasema na jamaa akashikwa na butwaa kwa muda,….halafu akasema

‘Oh, kumbe ni kweli, usiku nililiona hilo...ooh, sasa eeh...mungu wangu, mambo yameharibika…’akasema.

‘Sasa ndio hivyo nimekuja kwako, unipe ushauri…si unajua...’nikasema

'Najua...najua...oh..hapana, sijui kitu, ondoka, ondoka...'akasema  hivyo, na baadae akakaa kimia, hasemi kitu ni kama ana jambo limemgusa zaidi ya huo msiba..akashika kichwa, akataka kutembea kuingia chumbani, lakini akagundua kuwa kunma mgeni, akasimama.

‘Unasikia, bora uende, maana mambo yameharibika….’akasema

‘Ni kweli yameharibika, kijana wangu nitamfanyaje...'nikasema

'Kijana wako....?' akaniuliza akiniangalia kwa mshangao.

'Ndio, alikuwa hajamalizana naye...ndio nimekuja kwako unipe ushauri, maana yeye ndiye aliyenifanyia mambo mengi, sasa yanamuathiri kijana wangu, nifanyeje sasa…’jamaa akauliza.

‘Wewe unafikiria kijana wako tu, hujui mimi nina majanga kiasi gani,..yeye ndio alikuwa kiongozi wetu, tunakula kwa kupitia mgongo wake, sasa kandoka, kukiwa na mambo mengi hayajakamilika, hata mimi familia yangu ipo hatarini, bora uondoke tu…kila mtu afe kivyake, ...'akasema

'Sijakuelewa ina maana na wewe alikufanyia mambo hayo kama mimi...?' nikamuuliza

'Yaani we acha tu,...lakini mimi sio kama wewe...ila sikiliza, mungu wangu sijui utafanyaje, maana kama mlikuwa hamjamalizana, imekula kwako, jiandae kuwa tahira, vinginevyo, wewe au mkeo, au mtoto wako akatolewe kafara,…’akasema akinisukuma jamaa niondoke.

'Akatolewe kafara la nini na nani...?' nikauliza

'Inabidi ufunge safari...mmh, kamuulize yule binti...'akasema

'Binti gani huyo...?' nikamuuliza

'Yule mfanyakazi wako wa kwanza...atakusaidia..mimi sijui zaidi ya hapo, nina mambo yangu mengi kichwani, sijui. maana kila kitu alikuwa nacho yeye, mambo ya usiku, ...mmh, sasa hili balaa...vitu vyangu vitakuwa wapi...'akasema akishika kichwa.


‘Kwahiyo ina maana gani hapo mbona sikuelewi, au,… wewe  ndio miongoni mwa watu mliokuwa mkishirikiana naye usiku…?' nikamuuliza

'Wewe ondoka bwana usinichanganye..ondoka ondoka....'akasema kwa ukali.

'Wewe ndiye ulinielekeza kwake, wewe ndiye unayemfahamu, na sasa yaonyesha wewe ndiye mlikuwa mkishirikiana naye,...'nikasema

'Sikiliza sasa hivi tupo hatarini,...jamaa kazidiwa na adui yake, na kama ni hivyo wote washirika wake wapo matatani,hapo ni mmoja baada ya mwingine, bila kufanya jambo, tumekwisha...'akasema

'Kufanya jambo gani sasa...?' nikamuuliza

'Mimi sijui...mpaka nihangaike, sijui...wewe ondoka tu, siwezi kukusaidia kwa hilo...'akasema

'Sasa tusaidiane ..maana kama ni hivyo...'nikasema

'Nimekuambia uondoke nyumbani kwangu, usiniongezee matatizo..,..au nikuitie mwizi,..hebu ondoka, jamaa  akazidi kunisukuma niondoke , alikuwa kachanganyikiwa kweli, na mimi nikaona hapo sitasaidiwa kitu ikabidi niondoke

**************

 ‘Ina maana huyo mtaalamu alifariki kutokana na mapigano ya mambo yao na adui yake…?’ akaulizwa baada ya kupita kitambo, kwani alikuwa kama hajisikii vyema, ikabidi atulie kwanza.

‘Yawezekana,…kwani huyo mama ambaye aliongozana na huyo adui wa mpinzani wa mtaalamu wangu, alitumwa kwenda huko hospitalini na huyo mpinzani, sijui alitumwa nini,…maana nilisikia, alipofika tu ndio huyo marehemu akapiga ukelele,…kwahiyo kuna namna ilifanyika hapo…’akasema.

‘Namna ipi hiyo….?’ Akaulizwa.

‘Huyo adui yake alikuwa natafuta mwanya wa kumuingia huyo adui yake,…na akaona njia ni kumtumia huyo mwanamke, ..ni kama vile yeye alijificha nyuma ya huyo mwanamke, na huyo mwanamke alipoingia tu, yeye akarusha hilo kombora lake,..au yeye, alibakia sehemu akiangalia huo mwenendo, au huyo mama alipewa kitu akifanye akifika huko hospitalini…’akasema.

‘Wewe ni nani alikuambia hayo…kuwa huenda ilifanyika hivyo?’ kaulizwa.

‘Nahisi hivyo tu…, maana baada ya hapo sikuweza kuonana na yoyote kati yao, zaidi ya huyo jamaa niliyekwenda kwake akanifukuza..na huyo jamaa akatoweka siku kadhaa alirudi baada ya mazishi, sijui alikwenda wapi, na hata aliporudi na yeye akawa anaumwa sana..’akasema.

‘Sasa ikawaje..?’ akaulizwa.

‘Basi mimi nikarudi nyumbani, nikidhamiria kuonana na kijana wangu , na kijana hakurudi mpaka kesho yake, na aliporudi nikamwambia kuwa huyo mtu kafariki, na kijana hakutaka kusema na mimi akawa kimia tu, ndio nikamwambia naomba namba ya huyo mganga wake, akanipa…’akatulia.

‘Ukampigia huyo mganga wake..?’ akaulizwa.

‘Ndio nilimpigia,…na alipopatikana akasema anaumwa, hataweza kuongea na mimi kwenye simu…hali yake sio nzuri…na nikamuomba anielekeze hapo anapoishi, akasema nimuulize kijana wangu atanielekeza, na nikamuuliza kijana wangu akanielekeza.

Nikajipanaga kwenda kuonana na huyo jamaa nikijua sasa yeye ndiyo wa kutusaidia, kijana akawa haongei zaidi ya kile unachomuuliza, anakujibu kwa mkato tu, akawa hana raha, kama mgonjwa.

 Basi siku iliyofuata nikaamua kwenda kuonana na huyo mtu, nilitoka mapema kabisa, nilipofika nikakuta watu wamejazana, nikauliza kulikoni, nasikia kuna msiba,..msiba wa nani, nikaambiwa ni mzee mmoja alifika hapo, ni mgeni, na nilipodadisi sana, nikagundua kuwa ni huyo niliyemfuata..hapo sikukaa tena nikarudi nyumbani.

Baadae kijana akaja, akiwa anatetemeka, hali yake ni mbaya, nikajaribu kumdadisi ndio akanipa taarifa kuwa huyo mganga wake naye kafariki,…na sasa hajui ataponaje,..basi ikabidi nimliwaze kuwa nitamtafutia mtu mwingine asijali, lakini moyoni nilikuwa sijui ni nani wakutusaidie, nilishakata tamaa.

 ‘Sasa kijana wako ataponaje, au mlifanya juhudi gani …?’ akaulizwa

‘Kiukweli kuanzia hapo, na mimi nikaanza kujisikia vibaya, kichwa kinauma kupitiliza, nikawa kama naanza kuchanganyikiwa, nahisi vitu vingi kichwani,…’akasema

‘Sawa ikawaje..?’ akauliza

‘Sasa ikawaje…hahaha..hapo nikajua sina changu, sina familia, sina ….basi nikaanza kuongea peke yangu kama mtu aliyechanganyikiwa.

****************

Kesho yake nipo nipo tu..mara kijana akaja, na kunikabidhi bahasha, na hakusema kitu akaondoka,…nilipoifungua hiyo bahasha ndio nikakuta kanda ya video,..cd

‘Video ya nini…?’ akaulizwa

‘Sikujua ya nini, maana ilikuwa haijaandikwa kitu juu yake, ila mimi nikaamua kwenda kuitizama ina ujumbe gani ndani yake,..akilini nilishaanza kuingiwa na mashaka, ukumbuke mimi muda huo nipo nipo tu, ila hamasa ya kuiangalia hiyo video, ilinijia tu…nikaenda kuiangalia..mamamama..ni aheri nisingeiangalia…

‘Ilikuwa na nini…?’ akaulizwa

‘Kila kitu kama alichosema kijana..kila kitu, na mwishoni ..ooh, hapo nikaitoa……nilichofanya hapo, ni kuitoa na kuiharibu, nikahakikisha hakuna hata salio limebakia, nikatoka humo ndani na kuanza kukimbia, …

‘Kukimbia…unakimbia kuelekea wapi…?’ akaulizwa

'Kumtafuta mwanagu ,kumuwahi kabla....hapana sikuwa na akili hapo, karibu ngongwe na magari...

‘NB: Haya, jamaa ndio hivyo, je haya yaliendaje…maana baada ya hapa, mke anaanza kuingilia kati..ilikuwaje kuhusu huyu jamaa na je ni nini hatima ya kijana , je kwenye hiyo video kulikuwa na nini hasa….tutaendelea seehmu ijayo


WAZO LA LEO: Chuki ni tabia ya shetani, na yeye kazi yake kupandikiza chuki kwenye nafsi zetu ili tukosane, ili kusiwe na upendo kati yetu, nia ni kufarakanisha ndoa, udugu, na mshikamano. Tunatakiwa tulishinde hili, na kulishinda hili n kujenga upendo, kuhurumiana, kusameheana. Ukijiona wewe unawachukia wenzako, kwasababu mbali mbali ujue unatawaliwa na shetani. Mpende jirani yako, mpende hata adui yako, utaweza kumshinda shetani.
Ni mimi: emu-three

No comments :