Nikiwa
bado hospitalini, akaja mume wa yule mama aliyeibiwa, akanihoji, alinihoji kwa taratibu
tu, na baadae akasema;
‘Mtafuteni
huyo mdada, huyu hawezi kuwasaidia kitu, hamuoni,….huyu atawasaidia nini kumpata
huyo mwizi, muwe mnaelewa,..mnapoteza muda kwa mtu huyu huyu, haya niambieni
mumefikia wapi..?’ akawauliza watu wake wakamuelezea, halafu akasema.
‘Nataka
huyo mdada apatikane, nawapa siku mbili tu..mkishindwa nitaifany amwenyewe…’akasema
na kutoa amri kuwa niachwe huru. Hapo nikawa na amani, na baada ya amri hiyo,
nilipona haraka kuliko ilivyotarajiwa…na siku napewa ruhusa ya kutoka
hospitalini, akaja bint wa kule nilipokuwa nakaa kwa muda huo.
Alikuwa
kabeba begi la nguo, akaja hadi pale nilipokuwa nimesubiria dawa na baada ya
hapo niondoke kurudi nyumbani, huyo mdada sijui alijuaje nitatoka, na hakuwahi
kuja kuniona kabla, wengine walikuwa wakijitahidi kufika, sikumlaumu kwani
nilishamfahamu tabia yake.
Alipofika
na kuniona nasubiria, akaniangalia kwa dharau, ni kawaida yake kuniangalia
hivyo, utafikiri yeye ana kwake, au ana maisha yake ya hali ya juu,…yeye na
wenzake wanaishi kwa wazazi,..sawa ni wazazi wake ana haki ya kuringa, lakini
yeye kazidi, ananichukia sana, na yeye
ni mkubwa tu kuliko mimi , lakini hana mume, nasikia aliolewa akaachika.
Akanisogelea
na kusema;
‘Pole
na kuumwa, najua umeshapona, vinginevyo utakuwa unadeka tu, …ili uendelewe
kuletewa chakula,…’akasemaa
‘Ndio
nimeshapona namshukuru mungu, na nimeruhusiwa nilikuwa nachukua dawa, nitafute
usafiri…’nikasema.
‘Sawa
endelea kumshukuru, na kumuomba sana, haya kabla hujatafuta usafiri, …. hapa kuna barua yako kutoka kwa mama, si
unajua kusoma wewe…eeh…’akasema akinishikisha mkononi, na mimi kwanza nikasita
kuipokea, akanishikiza kwa nguvu, halafu akasema;
‘Isome
mwenyewe,..maana mjumbe hana kosa au sio..haya soma mpendwa…’akasema huku
anacheza mguu chini kwa nyoda na dharau, huku kashika kiuona,…huyu mdada ni
katika mabinti wa pale, wanaonichukia sana, yeye tofauti kama wengine, wengine
kidogo wana afadhali, lakini huyu kazidi kunichukia sijui kwanini;
Nikasoma
ile barua, iliandikwa hivi;
‘Sasa
umepona, nimempigia simu docta wa hapo, sasa ni hivi, muda niliokubaliana na
mume wangu wa kuishi kwangu umeshapita, sasa kwa wema kabisa, ninakushauri
urudi kule ulipotokea, wao ndio walikutoa kijijini na kukuleta hapa mjini, sasa
ni wao wajua jinsi gani utaishi,..kwangu sitaki kukuona tena, usije ukaniibia
kama mwenzako alivyoiba huko, samahani kwa usumbufu, mimi mama …’
‘Sasa
mimi nitaende wapi, jamani, si angenipa muda kidogo, ndio nimetoka hospitalini…oh,
mbona mtihani huu...?’ nikamuuliza huyu mdada, akabenua mdomo kwa dharau na
kuniangalia juu chini, halafu akageuka kuangalia mbele, na kusema;
‘Mimi
isjui ndivyo nilivyoambiwa, unasikia, usije kunitolea machozi hapa, maana kulia
kwako ni wimbo wa taifa, sasa ukalilie huko mbele , sio mbele yangu, ukanitia
uchuro…. na begi lako la nguo hilo hapo…umeliona eeh, mpendwa umesikia, …’akasema akigusa begani,
baada ya kuniona nimeduwaa, na mimi sikusema kitu,
Akatembea
hatua moja mbili kama anazihesabu halafu akageuka na kusema , sasa kwa sauto ya
kawaida, ili watu wamuone kama tunaagana kwa wema; Anajua kuigiza huyu binti,…kuna
muda anaweza kuigiza mtu mwema, utamuona ni katika wema waliofuzu, lakini
unayemfahamu tabia yake, hutatamani kukaa naye dakika mbili, …
‘Kama
kuna kitu kingine kimebakia kule wewe niambie nitakuja kukuletea huko
utakapokwenda kuishi…, sawa, pole sana, eeh, halafu nimesahau…’akarudi na
kufungua pochi yake, akatoa pesa
‘Chukua
hii pesa, itakusaidia kujikimu, hapa nimekata nauli yangu, usije kusema umepewa
pungufu, unasikia, haya tukijaliwa tutaonana, kwaheri eeh mpendwa, usijali,
maisha ndivyo yalivyo, …’akasema na kunikabidhi hizo pesa, na mimi nikawa
nimeduwaa tu, hata sijui niende wapi, nilikaa pale hospitalini kama mgonjwa
tena, na mdada huyo akaita bajaji na kuondoka zake.
Nilikaa
pale kwa muda mrefu, unajua ni kama mtu kafukuzwa nyumbani kwao, na hajui wapi
kwingine pa kwenda, akili imeduwa, haijui hata ifikirie nini, …nikawa nawaza
hili na lile, nikamuomba mungu kwa imani zangu zote anionyeshe njia, …mpaka
sasa sijui nifanyeje…
Baadae
sana likapita gari, na mara likasimama, alikuwa ni yule mbaba, askari, ambaye
ndio walioibiwa, akaniona bado nimekaa hapo hospitalini ndio akaniuliza mbona
sijaondoka;
‘Mbona
bado upo hapa, si nasikia umesharuhusiwa tatizo ni nini tena…?’ akauliza
‘Wamesema
nisirudi kule tena, wanadai nitawaibia, na mimi sijawahi kuiba maisha
mwangu,…na sasa hata sijui nitakwenda wapi..’nikasema huku machozi yakinilenga
lenga.
‘Oh,
sasa hilo ni tatizo jingine, na wewe huna ndugu yoyote hata mmoja hapa Dar…?’
akaniuliza
‘Sina,
aliyenichukua toka kijijini ni yule mama wa kule, mwenye matatizo na mume
wake,..naye hakutaka nikae kwake tena, hata sijui niende wapi tena ..’nikasema.
‘Sasa
kwanini wanakufanyia hivyo, na hiyo mimba ni ya nani…?’ akaniuliza akinikagua
tumbo langu.
‘Mimi
sijui, ..’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho ya mashaka, halafu akasema;
‘Wewe
hujui,..mbona sikuelewi,…sasa unajua,…hebu ingia ndani ya gari, nikupeleke
nyumbani kwangu, nitaongea na mke wangu, najua sasa hivi yupo na hasira sana,
lakini tutaona tufanyeje, hawawezi kukufanyia hivyo sio utu…’akasema
‘Kwako
tena, si ndio huko walipoiba, naogopa kukutana na mkeo, najua ana hasira za
kuibiwa nay eye anahis labda nimeshirikiana na huyo mdada, kumbe mimi sijui
lolote..’nikasema
‘Wewe twende
tu…tutajua mbele kwa mbele…’akasema na nikaingia kwenye gar hadi nyumbani kwake.
Nilipofika
tu, aliyetufungulia mlango ni huyo mke wake, aaliponiona aliniangalia kwa uso
uliojaa hasira, akageuka na kuingia ndani, hakusema neno. Mimi na begi langu la
nguo, nikaingia na kukaa kwenye kiti, nikisubiria maongezi ya wawili hao,…hawa
nao wana familia, lakini kwa muda huo watoto wapo shuleni, kwahiyo ndani
kulikuwa kimia.
Wawili
hao wakaanza kuongea taratibu, mara sauti zikaanza kuongezeka, mara ikawa sasa
ni mshike mshike mwanamke hakubali, na hasikii chochote anachoambiwa na mume
wake,..
‘Kama
umeamua kumleta huyu, haya ngoja mimi niwapishe, maana hata hiyo mimba mpaka
sasa haijajulikana ni ya nani huenda ni yako….’akasema huyo mama
Baadae
sana, mume mtu akanijia na kusema;
‘Unajua
sitaki matatizo, mke wangu ana shinikizo la damu, naogopa ukiendelea kukaa
hapa, italeta shida nyingine, sasa ngoja kidogo,…akapiga simu kwa mtu, na akawa
anaongea naye;
‘Kile
chumba bado kipo, hakijapata mtu, eeh, safi kabisa, mimi kitanifaa, kuna binti,
..hana mume…eeh, hana matatizo, hilo nakuhakikishia, sawa, anakuja sasa hivi,
hana mizigo yoyote ndio anaanza maisha, hivyo hivyo, ..usijali, tutaongea…’akakata
simu
‘Oh,
afadhali, …kuna chumba, sasa mimi nina rudi kazini,kuna kazi nyingi huko,
lakini siwezi kukuacha hapa, mtaishia kubaya na mke wangu, wewe ingia kwenye
gari twende…’akasema na mimi nikaingia kwenye gari, hao tukaondoka.
Wakati
tupo kwenye gari, akampigia yule mfadhili wangu wa kwanza, kuwa kapata chumba,
na kinafaa mimi nikae huko, wanasema kuhusu kusaidia kulipia kodi, na jinsi
gani ya kuishi…
Mfadhili
wangu wa awali, akasema hawataki hata kuniona kwani hivi sasa wanapambana na
maisha magumu, yeye alifika nikiwa hospitalini akanieleza kila kitu, na hivi
sasa mume wake amekuwa kama kachanganyikiwa, mtoto naye kagundulikana ana
matatizo makubwa, kwa hivi hawezi kubeba
mzigo mwingine, keshachoka.
‘Oh,
mbona inawia ngumu, sawa kwa vile nipo naye nitaona jinsi gani ya kufanya, ila
msisahau kuwa nyie ndio mlimchukua huko kijijini, tukifuatilia sheria mnaweza
kuwa matatani, unielewe,…hamna shida, mimi nitajitahidi kadri niwezavyo,…hamna
shida, sawa shemeji, poleni sana…’akasema na kukata simu
Tukafika
kwenye hiyo nyumba, ilikuwa nyumba ya kawaida tu, ila kuna vyumba vya uwani,
vya kawaida tu, na akaongea na mama mmoja, ..huyu mama ndio mwenye nyumba,
akaniangalia halafu akasema;
‘Sawa
mimi sina shida, wanawake ni wazuri maana sitakwua na shida ya usafi, ila
sitaki mlevi humu au Malaya, tutakosana…’akasema na kutembea kuelekea kwenye
hicho chumba, ..
‘Chumba
ndio hiki,…unakiona kilivyo, hakina tatizo, …ukitumie na ukiache kama kilivyo,
sawa, nimekupa hiki chumba kwasababu ya huyu mtu, kanisaidia sana, …fadhila
zake ndizo zimenifanya nikubali, ila kodi sasa itakuwaje…?’ akauliza
akimuangalia huyo mbaba.
‘Kwanza
nitakulipa kodi ya mwezi huu..shilingi ngapi….’akasema akifungua pochi lake,
akatia pesa, na huyo mama akazipokea na kuanza kuzihesabu, na kusema;
‘Oh,
sasa hii si kodi ya mwezi mmoja tu, sio makubaliano yetu hayo…’akalalamika
‘Wewe
si unanifahamu, nyingine zitakuja, usijali, ngoja nifike kazini, huyu sasa ni
mtu wako, …unanisikia mengine tutaongea…’akasema na kuanza kuondoka, niliogopa
hata kumuuliza nitaishije…
Na mar
akarudi tena, sasa akiwa na mifuko mwili na hisi ni ya kilo tano tano, mmoja
una unga mwingine mchele, na…mafuta kwenye chupa,……halafu akatoa pesa mfukoni
akanikabidhi na kusema;.
‘Sasa
mimi nimejitahidi hadi hapa,…sikulitegemea hili, cha kushuru ni kuwa sasa.umepata
chumba, nimelipia mwezi mmoja, unasikia, utalala vipi, hilo siwezi kuliwazia
kwa sasa, tumetoka kuibiwa, si unalewa hasara tuliyoipta, sasa mimi nakucha,…’akasema
‘Ahsante
nashukuru sana kwa wema wako…’nikasema
‘Muhimu
kwa hivi sasa, kama una jamaa
unaowafahamu basi watakusaidia zaidi…na, kwa miezi mingine..nitaona jinsi gani
ya kufanya, tatizo wewe una mimba,..ok, hilo utajua mwenyewe, sizani kama
unaweza kupewa mimba usijue ni ya nani, kwani ulibakwa…?’ akaniuliza
‘Hapana,
sijabakwa…’nikasema.
‘Ulipenda
mwenyewe…?’ akauliza.
‘Nimekuambia
mimi hata sijui mimba imetoka wapi,…hakuwahi kukuelezea mama…maana wao wanajua…’nikasema.
‘Hapana,
huwa hatoongelei mambo ya watu, mimi na mke wangu, huwa nina sheria zangu,
anyway, hilo utajua wewe mwenyewe…’akasema, na kugeuka kuondoka, halafu
akageuka tena na kuniuliza.
‘Ina
maana wewe kweli huna rafiki yoyote wa kiume…?’ akaniuliza akinikagua tumbo.
‘Mimi
sina tabia hiyo, sina kabisa rafiki wa kiume…’nikasema
‘Haya
tutaona….basi nitaona jinsi gani ya kukusaidia, ila…usije kusema kwa mke wangu
kuwa ni mimi nimekusaidia hadi hapa unasikia,…au kwa yoyote yule, sawa…nitakuja
nikipata muda, ila sikuahidi unielewe,…zaidi nitakuwa nawasiliana na huyo mama
mwenye nyumba wako, huyo mama ni mtu mwema sana, ananifahamu sana…’akasema na
kunitupia jicho….nilihisi namna ya mashaka, wanaume hawaaminiki, lakini
nikamuomba mungu apitishie mbali.
Basi
nikachukua vile vitu na kuingie kwenye chumba hakina kitu chochote …zaidi naona
kulikuwa na jiko la mchina, na sufuria moja, sijui ni vya nani, nikasema
moyoni, hivyo ndio vya kuanzia maisha.
Huyu
mbaba akaondoka na gari lake, nikabakia humo kwenye chumba, kitupu, nikahesabu
pesa nilizopewa na huyo mbaba na zile za yule mdada aliyekuja hospitalini,
nikaona nitaweza kuishi siku mbili tatu, lakini sasa humo nitalalaje, hakuna
godoro,..ila shuka ninayo,…nikafungua lile begi, nikakuta shuka, na khanga
zangu, …sio haba, nitaishi.
Hapo, nikakaa chini kwanza, nikiwaza….na mara
moja nikayakumbukia maisha yangu na mama, yalikuwa ya dhiki hivi hivi, lakini
tulikuwa na kitanda, hapo machozi yakaanza kunitoka na haikupita muda
nikashikwa na usingizi, na mara mama akanitokea
‘Mwanagu,
usikate tamaa, unakumbuka usia wangu,…usiogope kusema ukweli hata kama utakuumiza wewe au huyo unayemuambia huo ukweli..ukweli uwe ndio silaha yako..na pia usimuamini kila mtu, sio kila akuchekeaye ana nia njema na wewe, cheka naye, lakini akili kichwani mwako, jingine nilikuambia, uwe mbali na wanaume, na usipende kupokea misaada yao, kwani kila wakitoacho kina namna ya ghiliba,..
Muhimu mwanangu, ishi ukimtegemea mungu wako, kwani kila alilokujalia nalo lina maana yake, usijione upo mpweke, mungu wako yupo nawe kila mahali,usichoke kumuomba...na kumbuka jambo moja,sasa ndio maisha yako yameanza,..subira yako ndiyo
itakufikisha kwenye mafanikio,…kamwe usikate tamaa..
‘Sasa mama na hizi pesa za huyu mbaba, na vile vitu alivyoninunulia nivirudishe kwake..?’ nikauliza na
mara nikazindukana.
Nikasikia mtu anagonga mlango, nikaitikia karibu,
‘Kuna
mgeni wako huko nje…’nikasikia yule mama akiniambia, lakini sauti ya mashaka
‘Haya
nakuja…’nikasema hata sijui ni nani kaja kunitembelea ambaye anajua nimehamia
hapo..,
*****************
Alikuwa ni yule mama aliyeibiwa,
sikumkaribisha ndani, na yeye hakuonekana kutaka kukaa, akasema
‘Ndio
sehemu mume wangu kakuleta huku, eeh...mume wangu ni wajabu sana, ..hahaha....kwahiyo kakuleta huku muwe mnakutania mara kwa mara nilijua tu kuna kitu kati yako wewe na mume wangu, au sio..?’ akaniuliza.
‘Mama
, mbona unanishutumu kitu ambacho mimi sikijui, yeye, kanileta huku, wala sijui…’nikasema
na yeye akanionyeshea mkono wa kuwa hataki kunisiliza.
‘Ila
mimi nakuonya tu, nitakuwa nakufuatilia hatua kwa hatua siku nikimkuta mume
wangu hapa, mpo naye…utanitambua mimi ni nani…umenisikia, labda mtafute sehemu
nyingine, nisiwagundue, lakini nitawafikia tu, siku hiyo ndio hasira zangu zote zitaishia kwako…’akasema na kugeuka kuondoka.
Na
alipoondoka yule mama mwenye nyumba akaja na kuniuliza
‘Huyu
kajuaje kuwa upo hapa, maana mume wake hakutaka kabisa mkewe ajua kuwa upo
hapa, ooh, sasa naona nyie watu mnataka kuniletea balaa kwenye nyumba yangu, kama ni hivyo
tutashindwana..’akasema.
‘Lakini
mama mimi sijui chochote, hata huyo mume wake kanichukua hospitalini na
kunileta hapa, sikujua kama ana lengo lolote baya…’akasema.
'Lengo lolote baya, kwani hujui kwanini kakuleta hapa...hahaha wajifanya huelewi eeh,,,,'akasema
'Mimi ninachojua ni usamaria wake mwema tu ...'nikasema
‘Kwahiyo wewe na yeye, hamjaelewana chochote kuwa ukae hapa kwa vipi ...?' akaniuliza.
‘Kuelewana kwa vipi mama, ..?’ nikauliza.
‘Kwani
hiyo mimba sio yakwake..?’ akaniuliza
‘Hapana..’nikasema
bila kuongeza maneno na huyo mama akanikagua kwa macho halafu akasema;
‘Ya
nani sasa, binti,..hala hala… usije ukawa na matatizo, sitaki matatizo kwenye
nyumba yangu, namuheshimu tu huyo askari, kwasababu kanisaidia mambo mengi,
vinginevyo nisingelikukubalia wewe, kwasababu huna kazi, je utanilipaje,
nikajua huyo askari ni mwenza wako, kumbe tena, huna mahusiano naye,..oh, ngoja
nitaongea naye…’akasema
‘Mama
, kwangu usiwe na wasiwasi sina matatizo na mtu yoyote…, sina tabia mbaya kamwe
haya yaliyonikuta ni mitihani tu ya mungu, na wala sijui hata hii mimba
imeiingiaje,...’nikasema
‘Imeingiaje,
kwani mimba zinaiingiaje, usinichekeshe binti, mimi ni mtu mnzima usinifanye
mtoto mdogo, ina maana labda ulibakwa au..?’ akaniuliza
‘Yaani
mama mimi sijui...hata sijui nikueleze vipi unielewe…’nikasema.
‘Sawa
mimi sina tatizo, ila masharti yangu ni hayo, kukitokea tatizo lolote, wanaume
kuja kugombana huku au wake zao kuja kuleta zogo humu, unaondoka,…sawa…’akasema
na kuondoka.
****************
Kumbe
huyo mama alikuwa na biashara zake , alikuwa anatengeza chapati na kuuza chai,
na mara nyingine mama ntilie, na sijui ni kwanini anasema huyo askari alimuokoa
hadi biashara zake bado zipo…sikupata muda wa kumdadisi saa maana muda mwingi,
alikuwa kwenye shughuli zake na wateja wake.
Siku
iliyofuata nilifika kwa huyi mama anapofanyia shughuli zake nikamuomba
nimsaidie atanilipa chochote, atakachoweza na nikashangaa, akanikubalia tu.
Halafu
siku hiyo ikawa ni kama bahati, kukawa na wateja wengi, kiasi kwamba hata huyo
mama alishangaa, ikabidi aagize vitu vingine vya kupika na kupika mara mbili,
isivyo kawaida yake.
'Haijawahi
kutokea, yaonekana wewe umekuja na bahati, kesho uje tena…wewe naona unanifaa…’akasema
na mimi nikamkubalia kwa furaha nikijua sasa nimepata sehemu ya kujishikiza.
Basi ikawa hivyo, namfanyia kazi zake, ikifika
usiku ananilipa ujira wangu, wiki ikapita, na kila nikienda dukani kununua
vitu, naomba maboksi, na mifuko fuko, na hiyo nikatengeneza kitanda, siku zikaenda,
maisha yakasonga mbele…
Kila siku ilikuja na neema zake, nikaja kupata
kitanda kilikuwa kinatupwa, nikakiomba, nikampelekea fundi, akanitengenezea
vizur tu, huku naendelea kusaidiana na yule mama katika shughuli zake za
biashara, akanipenda sana, wateja wakawa wanamiminika…
Pamoja
na hayo yote, tumbo lilikuwa linanisumbua sana, ilikuwa mtoto tumboni hatulii,
na zile dalili za kukanguliwa zikawa ndio zinazidi, lakini mimi sikujali vile
vitisho kuwa ni dalili za kuwa mtoto huyo atakayezaliwa atakuwa si mtoto wa
kawaida, atakuwa na dalili za shetani.
'Kama
nitazaa mtoto mwenye sijui tabia za shetani, basi hata yeye ni kiumbe cha
mungu, yeye aliyekiumba atajua jinsi gani ataishi,..ila nakuomba ewe mola
wangu, mimi nikiumbe chako dhaifu, nakuomba sana ewe mola wangu nisaidie niyashinde
haya majaribu maana mimi sikuomba hili linitokee…’nikawa kila nikiwaza au kutokea
na maumivu hayo namuomba mungu wangu hivyo.
Siku moja nikawa naumwa sana tumbo, yule mama
akaniambia nipumzike tu, yeye ataendelea na malipo yatakuwa kama kawaida, basi
ikawa hakuna jinsi,lakini sikutaka kwenda kulala kule ndani kwangu, nikatafuta
sehemu hapo hapo huyo mama anapofanyia kazi, nikajiliza, sio mbali na hapo, na
sehemu huyo mama anapofanyia shughuli
zake. Nilitaka nikijisikia vizuri nimsaidia hata kusoha vyombo.
Wakati nipo hapo, hali ikazidi kuwa mbaya
sana, na wakati napambana na maumivu mara nikasikia huyo mama akiongea na mteja
mmoja, cha ajabu niliweza kusikia kwa mbali wanvyoongea, lakini sikuweza hata
kujiinua, mwili wote ulikuwa umeishiwa nguvu, mwili umelegea kabisa siwezi hata kuinua mkono
au kutoa sauti, nikawa nasikia maongezi yao, kama ndoto vile, kwa mbali kweli…
'Mimi
nimetokea huko kijijin kwetu nilikuja kutafuta wafadhili, wa ujenzi wa nyumba
ya ibada…..’nikasikia hivyo, lakini mengine sikuyasikia,…baadae nikasikia, huyo
mama akimuuliza huyo mteja..
'Ina
maana hakuwahi kuwa na mtoto….’sauti ikakatika, na nikajihisi sasa kama
napoteza fahamu kabisa, natamani nipige ukelele lakini sikuweza hata kufunua
mdomo.
'Alikuwa
naye…., tumemtafuta hapatikani, nasikia, alikuja…. Tujenge…ibada, na kama…..’nikawa nasikia
vipande vipande wanavyoongea, mengine sikuyasikia, na sikuweza hata kutafakari,
walikuwa wakiongea nini…ila mwishoni nikasikia, hivi;
'Je
akitokea na ikawa yeye hataki hilo jengo, anataka kujenga nyumba yake ya kuishi
mtafanya nini…?’ ilikuwa sauti ya huyo mama, hapo nikasikia vyema, na sauti ya kiume
ikasema;
'Tutamtafutia…….’hapo
sauti ikakata,…sasa hapo ndio hali ikawa mbaya kabisa, na nikahisi kupoteza
kumbukumbu masikio yakawa hayasikii tena, nikazama kwenye giza na kupoteza
fahamu.
Kumbe kwa bahati nzuri, walivyoniambia baadae,
alipita mmoja wa wateja eneo hilo, sijui alikuwa anatafuta nini, ndio,
akaniona, akatoa taarifa kwa huyo mama, na walichofanya hapo siwezi kujua, ila
walikuja kuniambia walinibeba na kunitoa nje ili nipate hewa, lakini
haikusaidia, wakahisi nimekufa,..ila wakajadiliana kuwa nipelekwe hopsitalini.
Kwa tukio hilo nililazwa karibu wiki, na
baadae nikatoka na nilipotoka, nikarudi kwenye chumba changu, na yule mama
akawa sasa ndiye ndugu yangu wa karibu…., na tukaanza kuzoeana kiukweli, hata
ikafikia hatua nikaanza kumuhadithia baadhi ya maisha yangu, alisikitika sana,
mengi ya huko nilipofikia na yaliyotokea kwa hao akina mama, sikumuhadithi,
nilimuhadithia, ya nyumbani nilipotokea na kupata taarifa ya kuwa mama kafariki
kwa kuchomewa nyumba moto..
'Wewe,
unajua kuna mzee mmoja,..tena siku ile ulipozidiwa ndio alikuja akawa
ananihadithia,…umesema kijiji gani, ..ndio huko huko, ..yeye alikuja hapa na
karatasi anachangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya ibada, nimemzoea
tu, kila akifika safari zake za kutoka kijijini anapitia hapa sio mara ya
kwanza kuoana naye, lakini hatuna udugu naye kabisa….
'Sasa
nitampataje huyo mzee…?’ nikamuuliza nikiwa na hamasa fulani, japokuwa
sikupenda kabisa kurudi huko, lakini kwa vile wametaja eneo, nikawa nimekumbuka
eneo la mama, hata hivyo sikuwa na tamaa nalo maana hata kuchomewa nyumba na
visasi vinawezekana ni kutokana na eneo hilo.
'Aliacha
karatasi ya kuchangisha watu kwa ajili ya ujenzi wa hiyo nyumba ya ibada, mimi
sikutilia maanani, sikjui kama ipo ngoja tukimaliza kazi nitaitafuta, kama ipo
au nimefungua wateja vitafunio,…’akasema na tukaendelea na shughuli zetu,
tukasahau, siku pili, hata hatukukubuka kuliongelea, ila siku ya tatu, akaja na
hiyo karatasi.
Kweli
kwenye ile karatasi kulikuwa na namba ya simu, anasema alimpigia na akamwambia na
yeye alikuwa na mipango ya kuja huku dar, wiki ijayo, basi tukasema tusubirie….
Nikawa namsaidia huyo mama napata ujira wangu,
japo kidogo sio haba, na humo humo, nikaanzisha mradi mwingine wa uji, kidogo
kidogo nikaanza kuwekeza, nikanunua godoro la bei ndogo, ili nikifungua nipate pa
kulala na huyo mtoto nitakayejifungua mungu akipenda.
Siku moja akaja mbaba mmoja kafuga madevu, alionekana
kama kachanganyikiwa vile, akaagiza chain a vitafunioa, na uji,…vitu
alivyoagiza, tuliingiwa na wasiwasi huenda asilipe, lakini cha ajabu akaomba
apigiwe mahesabu yake, na alipotajiwa ni kiasi gani akalipa, na kuanza kula,
taratibu hana haraka.
Na
muda wote alikuwa kainamia vitu vya kula, hakuwa akimuangalia mtu…sasa
alipomaliza, akajifuta mdomo na midevu yake, akasimama akitaka kuondoka, ndio
akaweza kuniangalia mimi,..muda alikuwa kashika gilasi ya maji, aliomba maji ya
kunywa na mimi ndiye nilimpelekea, aliponiona akashtuka, na kudondosha ile gilasi
ya maji ikavunjika…
‘Vipi mzee mbona wanivunjia vyombo vyangu…’mama akamuuliza na jamaa akasema.
'Samahani mama Ntilie, na..na...nataka kuongea na huyu binti....tafadhali...' akasema
'Wa nini...kuongea naye nini...?' akaulizwa na kabla hajajibiwa akaanza kulia, kulia kweli kweli, na alipotulia akanisogelea na kunipigia magoti....watu kimia, kila mmoja anajiuliza hili na lile kichwani, kunani kwa huyu mzee ambaye anaonekana kama kachanganyikiwa!
NB: Je
ni nani huyu.
WAZO LA LEO; Sio kila baya lina ubaya, mabaya
mengine yanatokea kwa minajili ya kuleta neema fulani ambayo sisi kama wanadamu
hatuwezi kuifahamu kwa hapo hapo, na sio kile jema lina wema wote, wema
mwingine unaweza ukawa mtego wa kukupeleka kubya, kwahiyo, kila jambo
likitokea, shukuru na mkabidhi mola wako, kwani yeye ndiye anajua zaidi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment