Yule
mzee aliagiza vitu vingi akawa anakula huku kainama, hakutaka kuinua kichwa,
labda hakutaka watu wamuone, na alipomaliza, akaagiza maji ya kunwa, na mimi
nakuchukua maji na gilasi nikafika mezani nikamumiminia na kumpa , akaipokea na
alipotana kunywa akainua uso akaniangalia,..na mimi muda huo nimesimama mbele
yake ili kama anataka maji mengine nimuongezee kwenye gilasi aliyokuwa
kaishika!
Aliponitupia
jicho, na macho yake kukutana na yangu, akashtuka, …na ulikuwa mshtuko kweli,
sio ule mshituko wa kujificha, mpaka gilasi ya maji aliyokuwa kaishikilia,
ikamponyoka, na kudondoka sakafuni ikavunjika, na kila mtu akasikia mlio wa hiyo
gilasi ikivunjika, na mama mwenye mgahawa akasema kwa hasira…
‘Vipi
wewe mzee leo, mbona unavunja vyombo vyangu…’akasema akimuangalia kwa mashaka,
na yule jamaa alikuwa bado kaduwaa, akiniangalia mimi..
Haikutosha
akaanza kulia na kusimama, akatoke kwenye meza na kunisogelea, akapiga magoti
mbele yangu huku akisema
‘Samahani
nisamehe…..’ huku akiwa kashikilia miguu yangu, ili nisiondoke…
Tuendelee
na kisa chetu
***********
Kila
mtu pale alishikwa na butwaa, ni kwanini huyo mbaba mtu mzima, japokuwa kwa
uvaaji wake na jinsi anavyoonekana, alikuwa akionekana kama kachanganyikiwa,,
manywele yamevurugika , madevu kayaachia, ya yenyewe yamevurugika, kwa ujumla
hakuonekana katika hali ya kawaida, hasa kwa umri kama wake,…
Sasa
analia na haitoshi, anakuja kunipigia magoti, kila mtu alihisi sio bure,
yawezekana kukawa jambo kati yangu na huyo mbaba. Lakini kiukweli mimi nilikuwa
simfahamu huyo mbaba, na sikumbuki kabisa kukutana na mtu kama huyo kwangu
alikuwa mgeni kabisa.
Yule mama, maana ndio alishakuwa mlezi wangu
japokuwa,namlipa kodi, ananilipa mshahara wangu wa kila siku, lakini
alishachukua dhamana ya kuwa mimi ni sawa na binti yake, sasa alipoona kile
kitendo cha huyo mbaba, haraka akasimama
na kumkabili huyo mzee, lakini alishachelewa huyo mbaba alishapiga magoti,
mbele yangu na kunishika miguuni…nilikuwa nimevaa dera refu sana,ikizingatia
hali yangu.
Pale nilipo nilikuwa najisikia vibaya, natamani hata kutapika, moyo ukawa unanienda mbio,...nilitamani aniachie nisije kumdondokea, lakini kila nikijaribu kuinua mgu siwezi jamaa kanishikilia bara bara..
'Vipi
wewe mzee unataka nini kwa huyu bint
yangu, si ameshakupa maji ya kunywa, unataka nini zaidi?...’akamuuliza.
Jamaa
ni kama hasikii akawa kanishikilia na kulaza kichwa cheke miguuni mwangu huku
akiinua uso kuniangalia, uso wa huruma huku machozi yakimtoka, mimi nikawa hata
sielewe huyo mbaba ana nini kwangu
Kwa
kitendo kile sikuweza kusogeza mguu, maana kanishikilia, nikisogeza mguu
nitandondoka, na huku nimeshikilia jagi la maji.
‘Wewe
mzee vipi, unataka nini, unajua unamfanya binti yangu ashindwe kuwajibika, hii
sasa unatuletea vurugu kazini, na tutakuitia polisi…’akaambiwa
'Ninataka
anisamehe…..ndio nitamuachia hu-huu mguu…’akasema
‘Akusamehe
kwa lipi kwani umemfanyia nini kibaya…?’ mama akamuuliza
‘Mi-mi..na-na
taka niongee na ye-ye, ili aweze kunisamehe..ta-fa-dhali mama ‘n-ti-ti-lie…’akasema
sasa akijaribu kugeuza kichwa kumuangalia huyo mama.
Huyo
mama kwanza akanitupia jicho, na halafu kuwatupia macho wateja wake, akainua
mkono kuwaashiria wateja kuwa huyo mzee kachanganyikiwa wasimjali.
'Unasema,
akusamehe, kwani ulimkosea nini, muachie awahudumia wateja…unatupotezea muda,
hujui ni hasara kwetu…’akaambiwa
‘Nitawalipia
hiyo hasara lakini ..na-na taka kuongea na –na , na huyu binti,…kwangu ni-ni
muhimu , sa-sa-sana…’akasema
‘Hapana
muachie kwanza,…’yule mama kajaribu kumuondoa huyo jamaa kwenye miguu yangu,
lakini alikuwa kashikilia bara bara, na sasa mama akashikwa na mshangao, akajua
sasa mzee mzima kazamiria
‘Sema
sasa kakukosea nini..mtu atakusameheje wakati hakufahamu, na hafahamu kosa lake
ni nini..?’ kaulizwa
'Yeye mwenyewe anajua,….ndio maana nataka anisamehe,….’akasema
akizidi kunishikilia miguuni.
'Wewe
mzee mimi sikujui, na sijawahi kukuona hata siku moja, niachie nifanye kazi …’nikalalamika,
.
'Nitakuachia
lakini mpaka,ukubali kuwa utanisamehe…..’akasema
'Nikusamehe
nini sasa, kwani ulinikosea nini, mimi sikujui na sijui kosa ulilonifanyia,
haya niachie uniambie kosa langu, …’nikasema.
'Ina maana
umenisahau mimi…, mungu wangu sasa hili ni balaa, ..'akasema sasa akazidi
kunishikilia, huku analia
‘Nisamehe,
nisamehe….’akawa anasema hivyo hivyo tu.
Ikawa sasa ni vurugu, maana wateja wanataka
huduma, mzee hataki kuniachia, kang'ang'ania miguu yangu, ikabidi sasa wateja
waingilie kati na kumuondoa huyo mzee kwa nguvu, na kitendo hicho kilinifanya
mimi niwe kwenye wakati mgumu.
Lakini wateja walikuwa na nguvu, wakatumia
nguvu na kumuondoa miguuni mwangu baada ya kumgonga gonga kidogo mabegani, na
juu kwa juu wakambeba na kumtoa nje…na aliponiachilia nikakimbilia sehemu ya haja na kutapika, na nikasubiria mpaka hali ikawa njema ndio nikarudi ndani.
Nilipofika nikakuta wameshamtoa nje...
Na
hata baada kumtoa nje, bado akawa analia
, kama anavyolia mtoto mdogo…, na kuomba watu wasimfanyie hivyo, maana bila ya
mimi kumsamehe akifa ataenda kuangamia..kauli hiyo ikawashtua wengi, na
ukazudka mjadala ni kwanini huyo mzee akatoa maneno makali kama hayo. Wengine wakazua
visa vya watu kama hao na wakadai maneno mengine ya watu kama hao, yana ukweli
ndani yake.
'Niacheni,
nataka nimuombe msamaha, nimemkosea sana
siwezi kuondoka hapa mpaka nipate nafasi ya kuongea naye ili aweze
kunisamehe….’akazidi kusisitiza.
'Basi sikiliza mzee, muache huyo binti afanye
kazi yake..unajua hapo yupo kazini,..akishamaliza kazi yake ndio mtaongea naye
akujue wewe ni nani na ulimkosea nini, si sawa mzee…’akaambiwa na akazidi
kusema.
'Jaman mnajua ya kesho nyie,…bahati haiji mara
mbili, je nikifa kabla hajanisamehe mnataka mimi nikaangamie…’akasema.
'Mungu
atakujalia hutakufa mzee, je usingelimuona leo, mpaka hapo mwenyezimungu
keshafahamu dhamira yako njema na ukizidi kumsumbua sasa itakuwa sio busara,
utashikwa na kupelekwa milembe, unakufahamu milembe wewe..?’ akauliza
‘Mimi
sio kichaa, kwanini wanipeleke Milembe, hamjui mimi nina matatizo gani, ….hamjui
mimi na huyo binti tuna mahusiano gani, …je kama mimi ni baba yake..’akasema na
watu hapo wakasema.
‘Aaah,
kumbe, ..lakini hata hivyo mzee, subiria kwanza…’akaambiwa.
‘’Huyo
sio baba yangu, baba yangu alishafariki…’nikasema kujitetea, na watu
wakaniambia ninyamaze, kwani nikiongea nitamzidishia ukichaa huyo mzee.
***************
Mzee akakaa hapo nje huku akilia akawa anaimba
kama mtoto mdogo,…
‘Nisamehe
, nisamehe, binti yangu,…nakuomba unisamehe binti yangu…’ basi akalia wewe
mpaka akachoka, akawa kimia, tukajua labda kaondoka, watu wanachungulia nje
wanamkuta kakaa hapo mlangoni, na kila anayetoka anamkagua kwa macho, na akiona
kimia, anatulia huku akiwa kashikilia kichwa ile ya huruma.
Baadae watu wachache waliokuwa wamebakia
wakaanza kumuhoji mama mama mwenye mgahawa
'Huyu
mtu ni nani…mbona hatujawahi kumuona..?’ akaulizwa
'Hata
mimi simfahamu vyema, nimeanza kumfahamu hivi karibuni tu, alianza kuja, kunywa
chai hapa, na awali nikajua hataweza kunilipa, kutokana na jinsi alivyo, yupo
kama kachanganyikiwa, kama mnavyomuona hivyo, aheri leo ni msafi kidogo, siku
nyingine utamkuta varu varu…lakini cha ajabu, akimaliza kula ni lazima alipe,
sijui paesa anazipatia wapi,…’basi akatulia kidogo akikanda chapati zake.
Basi
mimi nikamzoea, na kuanza kumtania kuwa yeye ni mume wangu,…wewe,..hapendi
kutaniwa hivyo….’akasema
'Ukimuita
hivyo anasemaje…?’ akaulizwa
'Hapendi,
hapendi kutaniwa hivyo, yeye anasema ana mke wake mnzur, hahitaji mke mwingine,
mke wake ni mnzuri sana anampenda yeye tu….’akasema
‘Hukumuuliza
huyo mke wake ni nani na yupo wapi..?’ akaulizwa
‘Ukimuuliza
hivyo anasema , nisimuingilie maisha yake, mke wake hataki kusemwa kwa watu,
maana akijua yeye ni mume wake atajisikia vibaya, kwahiyo nisimuulize zaidi
kuhusu mke wake…’akasema huyo mama.
'Hujamuuliza
anaishi wapi, …maana hapo watu wakimuuliza anasema tu, mwambieni
anisemehe,..mwambieni anisamehe, imekuwa kama wimbo….?’ Akaulizwa mama
'Nilimuuliza
hilo swali akasema yeye anaishi duniani, potepote pale hapa duniani ni nyumbani kwake, …’akasema huyo mama.
‘Sasa
hapo ni mtihani, lakini …sio bure…’wakasema wateja.
'Huyo
kachanganyikiwa, watu kama hao, kuchanganyikiwa kwao, inawezekana alikosana na
mke wake, au maswala ya ajira na maisha yakamuwia magumu, akawaza sana mpaka
akachanganyikiwa,..ninachojiuliza pesa anapatia wapi, labda akitoka hapa
anakuwa omba omba…’akasema huyo mama.
'Yawezekana
huyo binti yako anamfahamu, tuambie bintim, usikatae kwa vile yupo hivyo, kama
ni mzazi wako sema, au kama alikufanyia,…maana wengine huwashika wanawake kwa
nguvu..’wateja wakanigeukia mimi kwa maswali.
‘Ukweli
wa mungu, mimi simfahamu huyo mtu, ni mara yangu ya kwanza kuonana naye..huyo
kachanganyikiwa tu, au ananifananisha…’nikajitetea.
'Unajua
leo naona mwezi mpya, maana siku zote anakuja hapa anakunywa chai yake na
kuondoka, harudi tena mpaka kesho yake,…’akasema
‘Sasa
leo mnaye mpaka kieleweke…’akasema mteja mmoja
‘Tutamuitia
polisi…’akasema mama
‘Hapana
msifanye hivyo, hebu msikilizeni kwanza, huenda akawa na jambo muhimu kwenu,
msimzarau tu , kwa vile anaonekana kachanganyikiwa…’wakashauriwa hivyo.
'Au
ndio yeye kampa mimba huyo bint yako, hataki tu kusema ukweli…’mteja mwingine
akaropoka
'Hapana
huyu binti yangu hajapewa ujauzito na huyo mzee, nyie hamuoni huyo mzee na
binti mdogo kaam huyu wapi na wapi…’akasema huyo mama.
'Sasa mtuambie
mama, bint yako kapewa mimba na nani, maana hilo swali kila siku tunaulizana,
tukikuuliza huyo binti kaolewa unasema bado anayetaka alete posa, sasa utaoaje
mke na mimb ya watu…’akasema jamaa mwingine.
'Wewe
kama umpenda lete posa, ukipenda boga penda na majani yake, vyote ni vyakula
tu, mtoto akikua anaweza kukufaa wewe kuliko huyo wa kumzaa wewe mwenyewe..’akasema
huyo mama
‘Haya
mama Ntilia, ngoja tusubiria hatima ya huyo jamaa, ila msimfukuze mpaka atimize
lengo lake, ikibid binti amkubalia tu, kuwa kamsamehe, si inatosha,…’akasema
‘Siwezi
kukubali tu bila kujua kanikosea nini..’nikadakia mimi niliposikia kauli hiyo.
‘Mimi
nitakuambia mwenyewe mimi ni nani na kwanini nakuomba unisamehe..tafadhali naomba nipe nafasi niongee, lakini ningeliomba iwe faragha maana yaliyotokea sio vyema kila mtu akayasikia, tafadhali, msinione nipo hivi, lakini wakati mwingine ninakuwa na akili yangu timamu..nawaombeni sana waungwana mnielewe, sitaki kufanya vurugu….’jamaa akasema sasa akwia kasimama mlangoni.
Mimi pale milipo, kila nikimuangalia mtu huyu nahisi vibaya, sijui ni kwanini, nahisi kama kutapika, moyo unanienda mbio, lakini alipokuja safari hii hiyo hali ikawa imetulia.
NB: Jamaa
anataka kufunguka, ni nani huyu
WAZO LA LEO: Pindi kukitokea uhasama kati ya pande
mbili, lililo jema ni kuwakutanisha wahusika hasimu ili wao waweze kujieleza na
kujitetea wakiwa na msuluhishi kati yao, msuluhisi ambaye hana masilahi na
uhasama huo. Ni vabaya sana nyie watu wa pembeni kuhukumu bila ukweli kuwa
bayana, nyie wapambe mnaweza mkaja kuhukumiwa siku ya mwisho kwa kupandikiza
chuki na fitina, pindi mabaya zaidi yakitokea kati ya wahasimu hao. Kumbukeni
fitina ni mbaya sana zaidi ya uchawi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment