Nilipofika
kituoni, nikaanza kuhojiwa tena kwa vitisho, na kuambiwa nitatapelekwa jela,
nisipotaja wapi alipo huyo mdada, wakazidi kusema kuwa nisiposma ukweli, watanifunga, au hata kunitesa, mimi
nikaendelea kusema huo ukweli ninaoujua mimi;
‘Mimi
sijui wapi alipo na hakuwahi kuniambia anakwenda wapi, ni jambo la kushangaza
kwangu kusikia kuwa kaondoka,…?’ nikasema
‘Je
kwa mara ya mwisho mlikutana lini na wapi..?’ nikaulizwa.
‘Tulikutana
sokoni, tukaongea, lakini hakuwahi kuniambia ana mpango wa kutoroka…’nikasema
‘Alikuwambia
ana mpango gani…?’ akaniuliza
‘Aliniambia
ana mpango lakini hawezi kuniambia mimi kwasababu sitauweza….’nikasema
‘Kwahiyo
kumbe alikuambia ana mpango, si ndio hivyo…?’ akaniuliza
‘Ndio….’nikasema
‘Mpango
gani…?’ akaniuliza kwa hasira
‘Hakuwahi
kuniambia…’nikasema
‘Wewe unasema uwongo, na nimesikia ni tabia
yako ya kuficha ukweli, hata kama unaujua huo ukweli, sasa hapa ujue ni wewe mwenyewe
kuamua, kusema ukweli, au ukalale jela, unakufahamu jela kulivyo, huko
utapambana na watu watukutu, watakufunza adabu, na ukitoka huko hata ukiusema
huo ukweli tena hautakusaidia kitu, bora uuseme sasa uwe huru, unajua msema
kweli ni mpenzi wa mungu…’nikaambiwa.
‘Lakini
mimi nimeshawaambia ukweli, mnataka ukweli gani zaidi, niambieni huo ukweli
mnaoutaka nyie ni upi, na mkiniweka jela na hali kama hii, mtakuwa mnanionea bure…’nikasema.
‘Utajua
wewe mwenyewe huko jela, watu wanajifungulia huko, sembuse, wewe, nakuambia
usiposema ukweli, utakuja kujuta,…’akazidi kusema kwa ukali, na mara akaingia
jamaa mmoja, usoni, kakunjamana kwa hasira, kifua ni cha wale wainua vyuma,
akaniangalia, mpaka nikahisi mwili ukinisisimuka kwa uwoga.
‘Unamuona
huyu, huyu ndiye atakuuliza maswali, na ukijibu uwongo, atajua jinsi gani ya
kukufanya, kama hutatoka hapa huwezi kutembea tena, shauri lako, ulishawahi
kuwekewa nyoka mdomoni, um-meze, huyo anayo huyo nyoka, hebu muonyeshe…’akasema
na kunizidishia uwoga, na hapo hapo nikahisi kutapika, kichwa kinaniuma , moyo
unakwenda mbio.
Yule jamaa
akamtoa nyoka kwenye mfuko wake, na kunielekezea mimi, unajua kuogopa, nilitoa
jicho, nikahisi mwili umekufa ganzi,…nilipanua mdomo kupiga yowe, na jamaa
akataka kuingiza yule nyoka mdomoni kwangu…halafu akamrudisha huku kanikazia
macho.
‘Haya
upo tayari kusema ukweli…?’ akaniuliza nikawa kimia, maana siwezi hata kuongea,
na aliponiona nipo kimia, akasema;
‘Haya
inuke unakwenda huko ulipokutaka wewe..atakuuliza maswali, na mtamalizana
huko,..hutanilaumu kwa chaguo lako…’akasema na mimi nikaganda, siwezi kuongea,
siwezi kuinuka.
‘Nimekuambia
simama….’akasema kwa sauti iliyonifanya nishtuke na kwa haraka nikasimama…hapo
nikasema.
‘Lakini
mimi nimesema ukweli wote.., mama yangu alinifundisha nisiseme uwongo, nyie mnataka
niseme kitu gani mnachokitaka..?’ nikauliza.
‘Utuambie
wapi huyo rafiki yako alipokwenda, au huo mpango aliotaka kukuambia, ni mpango
gani…?’ akauliza sasa akiwa kasimama, na mimi nikajibu maneno yale yale kuwa
mimi sijui alipokwenda na wala hajawahi kuniambia huo mpango wake.
Ghafla
nilistukia nimeinuliwa juu juu kama katoto na huyo jamaa akiwa kanishikilia shingoni,
na sikweza hata kuhema, alivyonishikilia shingoni, na kuniinu juu kwa mkono
mmoja tu,..ikawa kama ile ndoto ya majinamisi, nikahisi kichwa kikijaa…masikio
yanataka kupasuka…siwezi kuhema…macho yakanitoka..nikajua sasa nakufa.
Akaniachia
na mimi nikaporomoka chini, na kudondokea sakafuni, nikajaribu sasa kuitafuta
pumzi, na hata nilipoipata, nikaishia kukohoa, na kuanza kutapika.. nahisi hata
mkojo ulipitiliza, na haikupita muda, giza likatanda usoni, na sikuelewa kingine
kilichotokea, kwani nilipoteza fahamu, nilipozindukana nikajikuta nipo
hospitalini.
***************
Nilipozindukana,
sura ya kwanza kuonana nayo, ilikuwa ya yule kijana wa mfadhili wangu wa
kwanza, alikuwa kasimama mbele ya kitanda, huku akiniangalia kwa mashaka, kama
ana wasiwasi, ni kama kajiiba kuja kuniona, akainama kuniangalia, na akukutana
ma macho yangu.
‘Oh,
umeamuka,..vipi, unajisikiaje…?’ akaniuliza
‘Sijambo…’nikasema
nikishangaa kumuona huyo kijana hapo.
‘Pole,
nimesikia yaliyotokea, hivi kweli, hujui wapi huyo mtu alipokwenda, na niambie
walikuuliza nini, na wanataka kujua nini…?’ akaniuliza
‘Mimi
sijui wanasema yule mdada, aliyekuwa akifanyia kazi kwenye katoroka, ..na pesa
na vito vya thamani, sasa mimi sijui kaenda wapi, na sikujua kuwa atakuja
kufanya hivyo…’nikasema
‘Shilingi
ngpi..na vito gani hivyo..?’ akaniuliza.
‘Mimi
sijui shilingi ngapi, na hata hivyo vito sijui ni kitu gani…’nikasema
‘Ssshit…’akasema
hivyo na kugeuka kutaka kuondoka.
‘Mwambie
mama yako aje kunisaidia, maana mimi sitaki kwenda jela wataniua…’nikasema
‘Mama…unasema
nini, mama, aje kukusaidia wewe, hahaha, labda useme aje kukugandamiza, watu
hao hawataki hata kukuona, wewe umekuwa ni chanzo, cha matatizo, wewe na
mwenzako, …hata mimi kuja hapa nimekuja tu, niliposikia umeletwa hapa, nikawa
napita hapo nje, nikaona kwanini nisije kukuona, lakini,….’akasema na kuanza
kuondoka.
‘Sawa,
lakini haya yote sijayataka mimi, na matatizo haya kama ni chanzo, labda ni
huyo mdada, na nyie mkachangia kuniingiza kwenye mambo nisiyoyajua, …’nikasema
hapo akatulia baadae akageuka na kusema;
‘Sikiliza,
jaribu sana kujipigania wewe mwenyewe usiwategemee sana hao akina mama,
usiwaamini sana ukawaambia kila kitu chako..na…, na usikimbilie kumlaumu mtu,
maana kama ni matatizo, unayo, sasa hata ukilalamika, yataondoka hivi hivi kwa
kulalamika,.., na hata ukimtupia mtu lawama, kuwa ndio yeye sababu je huyo mtu
atakusaidia, jiulize sana hayo. Kwasasahivi dunia ilivyo kila mtu anajali tumbo
lake…’akasema
‘Lakini
hata wakijali matumbo yako , kuma mambo mengine mtu akiwa na na uwezo wa
kusaodia, wengine anatakiwa afanye hivyo,..wewe mwambie mama yako, namfahamu
yeye ni mtu mnzuri, ..’nikasema
‘Ni
kweli yeye ni mtu mnzuri, lakini kwa wazuri kwake, wewe hukutaka kuwa mnzuri
kwake, ..na…wote hata hao marafiki zake, sasa hivi wanakunyosheeni vidole kuwa
nyie ndio sababu ya hayo matatizo…’akasema.
‘Lakini
sio kweli, mungu anajua mimi sijahusika kwa yote hayo wanayoyasema, wananisingizia
tu..’nikasema.
‘Mungu
anajua sawa,… sasa…hebu niambie, mungu atakusaidia hivi hivi tu…nimeshakushauri
tu..mimi naondoka, lakini kumbuka , pambana na matatizi yako usitarajia msaada
wa kutoka kwa wengine , hasa hao akina mama, na ukilemaa kwa jinsi nilivyosikia
wewe utaenda kufia jela,…’akasema.
‘Ni
bora nife tu, mama yangu si alishakufa, kwani mimi nina tahamani gani tena…’nikasema.
‘Sawa
kama ndilo unalolitaka, lisubirie tu linakuja hilo, muda si mrefu.., nina imani
wakikupeleka huko jela hutatoka mzima,..na wenzako wataendelea kula nchi,
unakumbuka kuna kipindi nilikubembeleza sana uwe mpenzi wangu uliniambia nini,…sasa
utanikumbuka kwaheri…’akasema .
‘Samahani
kabla hujaondoka, nimesikia na wewe una matatizo, unaumwa, unasumbuliwa na nini…?’
nikamuuliza na akasimama kwa muda bila kunijibu halafu akasema.
‘Matatizo
yangu nayajua mimi mwenyewe, na kama ni mama, kawaambia hilo, …sawa, waache
wasema wanayosema, ila kiukweli matatizo yangu chanzo chake ni wao, wazazi
wangu…’akasema.
‘Kwa
vipi, wazazi wako wamekufanya nini..?’ nikamuuliza.
‘Wao
wakigombana, wakiishi bila kupendana, mimi naumia sana, mimi nawapenda sana
wazazi wangu nataka waishi kwa raha, wapendane kama zamani…’akasema.
‘Kwani
hawapendani, kwanini hawapendani, kama zamani…?’ nikamuuliza.
‘Mimi
sijui, ningelijua ningafanya kila niwezalo warudie hali yao ya zamani, lakini
sijui, na mlipofika nyie mkazidisha matatizo, iliniuma sana, na zaidi nasikia
wamegundua kuwa nyie mumesababisha mataizo haya yanayotokea sasa,..niliapa
nitafanya nifanyalo mpotee kabisa, lakini nawaonea huruma….’akasema.
‘Unaamini
hayo kuwa sisi ndio sababu..?’ nikamuuliza.
‘Niamini
nisiamini, lakini ushahidi upo, niliwahi kumuona yule mdada akifanya mambo ya
kishirikiana uchi, niliwaambia siku ile ya kikao..na nilipomgundua ndio akawa
ananisema umbea kwa wazazi wangu, wakati nilikuwa najitolea kumsaidia, hata
pesa za kujikimu, hana shukurani…’akasema.
‘Lakini
yaonekana wewe na mdada mlikuwa na jambo lenu wawili…?’ nikasema.
‘Kiukweli
ilikuwa hivyo,…kama nilivyotaka iwe kwako, unajua ujana tena..lakini yeye,
alikuwa mjanja sio kama wewe, nampenda sana kwa hilo, ana kichwa cha kutafuta,
kuona mbali sio kama wewe…wewe ni mtu wa mungu mungu tu,…’akasema.
‘Kwahiyo
hicho alichofanya unaona ndio ujanja..?’ nikamuuliza.
‘Hapana
mimi siongelei hayo, wizi …hapana, kama kafanya kafanya yeye, sijamsifia kwa
hilo, na najua akishikwa ataishia kubaya , lakini hakuwa na tabia hiyo ya wizi,
sijui kwanini alifanya hivyo…’akasema.
‘Yeye
aligundua kitu gani akakusema kwa wazazi wako..?’ nikamuuliza na hapo, ikawa
kama nimemfukuza, akasema;
‘Kwaheri,
fikiria yako, usiwazie ya kwangu maana ya kwangu hayakuhusu na hakuna anayeweza
kuyatatua..zaidi yangu na wazazi wangu…’akasema na kutembea kwa haraka kuelekea
mlangoni, lakini kabla hajafika mlangoni, mara akaingia mama yake. Akashtuka na
kushikwa na butwaa…
‘Wewe
umefuata nini huku..?’ mama yake akamuuliza.
‘Nilikuja
hospitalini, kufuatilia kiliniki yangu…’akasema.
‘Kliniki
yako uko huku …?’ akaulizwa.
‘Nilisikia
huyu mdada kalazwa hapa, kwa vile namfahamu ndio nikaona nije kumjulia hali..’akasema
na hapo mama yake akageuka kuniangalia uso ulikuwa umejaa hasira.
‘Achana
na hawa watu mwanangu, unajua ni nini walichotufanyia, ..sasa hamueleweki wewe
na baba yako, unajua chanzo ni nani, ni hawa watu, ..ni watu wabaya sana,
sitaki hata kuwaona, lakini kwa vile nina maswali ya kumuuliza nimeona nije tu,
ubinadamu unaniponza,..haya ondoka hapa …’akasema na huyo kijana wake akatoka
mbio mbio.
***************
‘Haya
mdada, niliwahi kukuambia kuwa kuna siku utanihitajia, nikakuomba uniambie
ukweli ili uwe pamoja na mimi, lakini ukaniona mimi sina maana, unaona dunia
inavyokufunza…’akasema.
Sikusema
kitu, nilikaa kimia tu, nikiwazia ni kitu huyu mama alitaka nimuambie
nikashindwa kumuambia, ni kuhus mume wake, sasa ningesema nini, kuwa alitaka
kunibaka, je ni kweli alitaka kufanya hivyo, mimi sikuwa na uhakika na hilo, na
kama ningelimuambia huenda ingelikuwa mwisho wa ndoa, yao, …hapana nilichosema
ni sahihi kabisa.
‘Sasa
niambie huyo rafiki yako kaenda wapi, unaona mlivyo, mnaaminiwa mnakabidhiwa
dhamana za watu, maana mtu akiondoka kwenda kazini, na wewe ukabakia na nyumba
unakuwa umekabidhiwa dhamana ya kila kitu kilichopo ndani, sasa nyie mnaingiwa
na tamaa mnaiba, …niambie ukweli huyo rafiki yako kakimbilia wapi..?’
akaniuliza.
‘Mama
kiukweli mimi sijui, wewe unanifahamu nilivyo, siwezi kusema uwongo…’nikasema
‘Mimi
ninavyokufahamu ni kuwa unaweza kuficha ukweli kwa kumuonea mtu mwingine huruma
kwa ujinga wako ulio nao, na huyo mtu hawezi hata kukuonea huruma,..ukiogopa
kuusema ukweli, sasa huku ni kwingine, huko kuna mateso, hapatakuwepo wa
kukuonea huruma, nimekuja hapa kukusikiliza kama unahitajia msaada wangu…’akasema.
‘Ndio
mama mimi nakutegemea wewe, nimegundua kuwa wewe ni mama mwema unaweza
ukanitetea kwa hili, maana ukweli mimi sijui, alipokwenda huyo mtu…’nikasema.
‘Lakini
mlionana naye huko sokoni, au sio..?’ akauliza.
‘Ndio…’nikasema
‘Ni
mara ya ngapi kuonana naye, kabla ya hiyo siku..?’ akaniuliza.
‘Mara
nyingi tukija sokoni namuona kwa mbali tu, na hatukuwahi kuongea naye kama siku
hiyo…’nikasema
‘Kwanini
siku hiyo mliongea,..?’ akaniuliza.
‘Yeye
aliponiona aliniita kuwa anataka tuongee…’nikasema.
‘Kwahiyo
yeye ndio alikuita..sio wewe ulimfuata..?’ akaniuliza.
‘Yeye
aliponiona alinionyeshea ishara ya mkono, kuwa nimfuate…’nikasema.
‘Uliwaambia
jamaa zako mliokuwa nao, kuwa umeitwa na mtu ..?’ akaniuliza.
‘Ndio,
nilimuambia mama, akasema nisichelewe…’nikasema.
‘Lakini
hakukuuliza ni nani unataka kuongea naye..?’ akaniuliza.
‘Hakuniuliza,
ila niliporudi baada ya kuongea naye, ndio akaniuliza ni nani niliyekuwa
nikiongea naye…’nikasema.
‘Mlipokuwa
mnaongea naye, mliongea nini na nini..?’ akaniuliza.
‘Tuliongea
mambo mengi, kuhusu maisha yetu yatakuwaje, tutafanya kazi gani ambayo inaweza
kutuingizia, kipato, na baadae ndio akaniambia ana mpango wake, lakini anaogopa
kuniambia mimi …’nikasema.
‘Kwanini
anaogopa kukuambia wewe..?’ akaniuliza.
‘Ananiona
mimi sio mjanja,…akasema mimi kauli
yangu ni mungu anajua, mungu anajua, nikae na kauli yangu hiyo kama itanisaidia…lakini
hakuwahi kuniambia huo mpango wake, akisema haniamini, na kitu kama hicho..’nikasema
‘Mimi
pamoja na mengine nakuamini, lakini hao walioibiwa hawawezi kukuamini,
nimejaribu kuongea nao, wakaona kama na kutetea, mpaka tumeishia kugombana,
hata urafiki umemeguka, kisa ni wewe..sisi kabla yenu tulikuwa marafiki wakubwa
tunasaidiana, sasa mumekuja nyie, mumeharibu urafiki wetu…’akatulia akiangalia
simu yake.
‘Sasa
utanisaidiaje…maana sina mtu wa kunisaidia zaidi yako wewe…?’ nikamuuliza
‘Unajua
nikuambie kitu, unachoniuliza kinaniweka njia panda, nikikusaidia wewe, ina
maana navunja mahusiano yangu na rafiki yangu, huyo mama aliyeibiwa, na ndivyo
alivyoniambia tulipokutana, amesema mtu anayemjali awe upande wake kuhakikisha
kwanza anampata huyo mdada, na pili nyie mnaishia jela, …sasa hebu niambie hapo
mimi nifanye nini, nikusaidie nivunje urafiki wangu, au nibakie kwa rafiki
yangu wewe uende jela…?’ akaniuliza
‘Nitaendaje
jela wakati mimi sikuiba, na wala sijui huyo rafiki yangu kakimbilia wapi na
wala sijui huo mpango wake ulikuwa nini, na kama ningelijua mpango wake ndio
huo, ningemkanya, na kumuambia akiiba nitamuambia madamu wake
‘Je
angelikuambia huo mpango ungalifanya hivyo…?’ akaniuliza
‘Kufanyaje…?’
nikauliza.
‘Ungelimuambia
madamu wake kuwa mwenzako ana mpango wa kuiba..?’ akaniuliza
‘Nikuulize
wewe mama, mtu kaja kukuambia kuwa ana mpango wa kuiba mahali, je unaweza
kwenda kwa hao watu ukawaambia kuwa kuna mtu anataka kuwaibia, je asipoiba, …mimi
ningelijitahidi tu kumkanya kuwa asifanye hivyo, na ningelimtisha kuwa
nitamuambia madamu wake, najua angeliogopa kufanya hivyo,ila mungu alizuia hilo
akijua ungelikuwa ni mtihani kwangu…’nikasema
Mara
simu yake ikalia…akaiangalia, na kusema.
‘Haya
tunakutana mimi na wenzangu, moja ya ajenda ni hiyo, jinsi gani ya kufanya, na
shauri la awali ni kuwa nyie mrejeshwe kijijini, mimi nilijaribu sana kulizuia,
na kulichelewesha nia, tupata sehemu ya kukuweka wewe, lakini imeshindikana
kutokana na matatizo ya mume wangu, sasa hili limetokea, ajenda sasa sio wewe
kupelekwa kijijini tena, bali ni kuhakikisha unapelekwa jela, kama usiposema
wapi huyo rafiki yako amekwenda..’akasema
‘Lakini
mama, ujue mimi nitakwenda jela bila kosa lolote , na hali hii je itakuwaje, na
hali hii imetokea nikiwa kwenu, je kama unawahusu watu wa nyumbani kwako,....?’
nikauliza
‘Hapo
mimi siwezi kusema kitu, na ukizidi kusema kuwa hali hiyo uliyo nayo imetokea
kwangu ndio unazidi kuniti hasira,..lakini nikuambie kitu, hiyo hali umejitakia
wewe mwenyewe, kama ungenishirikisha, ukaniambi aukweli mapema, nikajua ni kitu
gani kinachoendelea isingelifikia hapo…’akasema
‘Kwani
mimi nilikuwa najua…’nikajitetea
‘Ulipojua,
ulipohisi kuna hali kama hiyo, unaota sijui, na hata kama kuna tabia ambayo
ulihisi sio ya kawaida kwa mume wangu ungeliniambia, mimi ningelijua jinsi gani
ya kufanya, na huenda sasa hivi ungelikuwa labda unaishi na huyo bwana, au
kungelikuwa na mpango madhubuti wa kuhakikisha kuwa haki yako inapatikana, sasa
wewe hukutaka kujisaidia, mimi ningeliwezaje kukusaidia..?’ akaniuliza
‘Sawa
mungu mwenyewe atajua ,kwa vile mimi nazungumza ukweli, na hayo niliyosema kwa
polisi ni kwako ndio ukweli ulivyo, kama
nitapelekwa jela na kufungwa, najua ni mipango ya mungu, yeye anajua zaidi, na kwanini
itokee hivyo, lakini sitachoka kuongea
ukweli, na huo niliokuambia ndio ukweli,…kama utanisaidia mungu atakusaidia na
wewe…’nikasema na huyo mama akanigeukia na kuniangalia machoni, niliona namna
ya huzuni usoni mwake.
‘Mhh….huu
sasa ni mtihani…’akasema hivyo tu na kuondoka.
WAZO LA LEO: Ukweli ni silaha kubwa katika maisha
yetu, watu wanafikia kusema uwongo ili wafanikiwe mambo yao, wengine wanafikia
kusingizia wengine uwongo, kujenga fitina, kisa wao waonekane ni wazuri na wengine
ni wabaya, kisa wanataka wafanikiwe kwenye mikakati yao ya maisha, iwe ya
ajira, au uongozi, lakini tunasahau kuwa yupo ambaye anatujua sisi zaidi ya
tunavyojijua.., je ukisema huo uwongo,labda…ndio ukafanikiwa unaijua kesho yako
itakuwaje,..wangapi walipata, lakini hawakuweza kutumia, na wangapi walianza
kutumia lakini hawakuweza kufaidi matunda yake…..Tufanyeni mambo tukijua kuna
leo na kesho.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment