Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, April 28, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-17


‘Unajua huyu mtu kanishangaza kweli, kwanza alipowaona tu nyie alikuwa kama kaona kitu cha kutisha, macho yakamtoka pima kwa woga,..ni kama vile hakutaraji kukutana na nyie, halafu akagundua kuwa ninamuangalia kwa mshangao, akajirudi...lakini kwa jinsi mlivyokuja, akawa hana amani,… akaona hakukaliki, mara huyoo, kaanza kutimua, kuna nini kati yenu na huyo mtu..?’ akauliza

‘Kwani huyo mtu ni nani..?’ nikauliza

‘Huyo ndiye jamaa ambaye kwa hivi sasa ndiye anayeishi kwenye nyumba yangu niliyohama, hahaha, sio kuihama kuikimbia, maana ilifika mahali, na ubishi wangu, tukaamua kuja kuishi huku, sikuwa na jinsi..’akasema.

‘Kwanini mzee, ukaamua kuiacha nyumba yako nzuri , kubwa namna ile, nab ado hupangishi..?’ nikauliza.

‘Mwanangu, tembea uone, unajua mimi nilikuwa siamini haya mambo kabisa, nilikuw ambishi sana, lakini nimeyaona, nimeshuhudia kwa macho yangu, vile viziweza kuonekana,..yaani, usione hata naumwa hivi, vingine vinatisha..’akasema.

‘Mhh, hata mimi siamini, lakini sitaki kukutana na mambo kama hayo, ..ilikuwaje mzee, maana naingiwa na hamu ya kufahamu zaidi..?’ nikauliza.

‘Kiufupi niliondoka kwenye nyumba hiyo baada ya kuanza kuona marue rue, familia usiku hailali,..ikawa ni vurugu mtindo mmoja, sijui wanachokipata , nikiamuka asubuhi nimechoka, hata mke wangu,..kuna wakati tunajikuta tumechafuka kama watu waliokuwa wanalima,..sasa sijui..’akasema.

‘Haiwezekani, ina maana mlikuwa mnalimishwa usiku..?’ nikauliza.

‘Hata sijui..kiukweli mpaka sasa najaribu kujiuliza iwezekane vipi, haya nikasema basi ngoja nihame humo, labda ni wivu, hawataki niishi hapo, nikahama na kuanza kutafuta wapangaji wa hiyo nyumba, ..hakuna aliyetaka kupanga,…kila mtu aliyeletwa hapo alikaa usiku mmoja tu kesho yake anafungasha anaondoka zake, wanadai kuwa nyumba hiyo ina marue rue…’akasema.

‘Lakini mbona huyo mtu hajahama, kwanini..?’ nikauliza, na mzee akawa kama anwaza jambo halafu akasema;

‘Yeye anadai kajikamilisha watu hawamuwezi, anapambana nayo hayo marue rue, …’akasema.

‘Kama ni hivyo, kama yeye anaweza,  kwanini sasa asiwasaidie na nyie, kama anauwezo huo..si mtu mnaelewana naye?’ nikauliza.

‘Aliniambia, kama nataka anaweza kunisaidia, nikamwambia anisaidie, ooh, nikaona anataka kunitumbukiza kule kule nisipokutaka,  mara anadai, sijui tutafute mbuzi mwekundu..., sijui ni nini....hapana mimi nikasema sitaki kujiingiza kwenye shiriki za namna hiyo ninahama,…nikaamua kuhama’akasema.

‘Wewe mzee haikuwahi kukugusa kuwa ni kwanini yeye, akaweza kumudu hiyo hali, ...ni kwanini yeye, ashindwe kukusaidia wewe kwa namna nyingine maana hayo mambo yakija hayakukwazi wewe tu ni pia na yeye..basi angalifanya kwa wote, si alikuwa mpangaji wenu wa siku nyingi au....?’ nikauliza swali hilo.

‘Mimi sijui, muhimu yeye anakuwa mlinzi wa nyumba yangu, ...unajua baadae nikatak kuiuza hiyo nyumba, kwanini iwe shida...nilitaka niipige bei,..lakini hakuna mnunuaji aliyejitokeza, mpaka sasa hakuna,… habari za hapo zimetapakaa kila mahali…sasa hivi wanaiita nyumba ya mashetani nyumba ya marue rue…’akasema.

‘Unahisi ni kwanini..?’ nikauliza.

‘Ni kwanini...ooh,.., mimi hata sikutaka kujua zaidi, unajua haya mambo ukiyachunguza sana yanaweza kukutumbukiza kwenye shiriki, tulipohamia awali hapo tulianza kuishi kwa amani tu,..tatizoo tulipoweka geti, kubwa kuzunguka eneo letu, sijui kwanini,lakini kwa kumbukumbu zangu vioja hivyo vilianzia hapo…’akatulia kama anawaza jambo.

'Au mama yeye hakuwahi kukuambia lolote,..maana wao wanasikia mengi zaidi kutoka kwa majirani nk...?' nikauliza.

‘Nilisikia kupitia kwa wife…eti wanasema tunaringa, tumejitenga,.hatutaki watoto wengine aje kucheza hapo…unajua, mimi sikujali maana nilijua ni nini ninakifanya, tukaziba masikio..sasa ngoma ikaanza, mipaka ya aina yake ikaanza kutujui,..mara sauti..yaani ni vituko vituko..kukawa hakuna amani kabisa..’akasema.

‘Tuliwaita watu wa dini, wakaombea, tukafanya yale dini inataka, ikawa inapungu ainarudi,..lakini amani, haikuwepo tena,..na zaidi sasa ulipotokea msiba wa binti yangu, hapo, ndio ilikuwa kama kuna sherehe ya kutusumbua,naweza kusema, chanzo kilikuwepo lakini zaidi tulipopata huo msiba…’akasema.

‘Lakini mzee, kumbe tatizo, sio baada ya kufariki binti yako,…nyie mlikimbilia mbali sana,na ndivyo wenzenu walitaka ieleweke hivyo,kujenga hisia, na kuwajengea chuki,…wewe hukutaka kuangalia chimbuko la matatizo yako ukakimbilia, matokea yake, na hili ni tatizo, wengi hukimbilia kwenye matokea, hawataki kuangalia chimbuko, ili kesho na kesho kutwa lisitokee tena, ..’akasema docta.

‘Lakini kwa hali kama hiyo ulitaka mimi nifanyeje, nikae kimia wakati binti yangu kauwawa, maana kuna sababu  binti kanywa sumu,..na hiyo ni taarifa ya docta, kutoka hospitalini, na alipopimwa akaonekana alikuwa na uja uzito, ukiunganisha hivyo vitu viwili unapata jibu, kuwa kajiua kwa vile alikuwa na mimba, na  aliyempa mimba kamkataa..ndio sababu ya kujiua..’akasema.

‘Hiyo sababu ya kuwa kajiua kwa vile kakataliwa mliipatia wapi….?’ Akauliza docta.

‘Mdogo wake ndio alituambia kuwa dada yake alikuwa na mimba, na alipokwenda kuonana na huyo mwanaume aliyempa mimba, akamfukuza,…sasa hapo utasemaje..’akasema baba.

‘Mhh…hebu hapo kwanza, kuna ushahidi gani, labda wa maandishi, au wa kauli kuwa nimeamua kujiua kwasababu ya …hiki na hiki…’akauliza docta.

‘Sababu ya moja kwa moja hakuna..ni sababu za kuunganisha tukio, na hali halisi..’akasema mzee.

‘Kwani kwa ujumla binti yako alikuwaje kitabia,…?’ akauliza docta

‘Alikuwa mpole sana...kiukweli hakuwa na mazoea na watu hususani wanaume..., lakini alikuwa ni jasiri, huwezi amini pamoja na vitimbwi vyote hivi, yeye wakati mwingine hutoka nje na kuyapiga mawe hayo mapaka, yanayosuumbua,…haogopi, maana kiukweli hali iligeuka kuwa ni kero..ndio hapo najiuliza ilikuwaje,..aah, hata sielewi, maana hakufanana na mtu wa kunywa sumu, lakini ndio kanywa utasemaje tena hapo..’akasema.

‘Unajua mzee, kuna kitu nataka tukiweke wazi, unaweza ukapatwa na matatizo,kumbe yamepangwa na watu wengine wajanja, wasiopenda maendeleo yako, maadui zako, maana sio wote ni wema kwako,...tuachilie mbali kuwa kifo ni lazima kitokee, na lazima iwepo sababu...'akatulia docta kwani mzee alitaka kusema jambo, lakini hakusema.

'Nina maana kuwa binti yako alipangiwa kifo chake kitokee hivyo, lakini haitoshi sisi kukaa kimia,…kila jambo hutokea ili iwe ibra kwetu, tujifunze, tuelimike na tuchukua tahadhari, mengine, mungu mwenyewe anajua, lakini ziwepo jitihada, akiuwawa mtu tunafanya uchunguzi, akinywa sumu tunafanya uchunguzi..lakini kwanini alikunywa sumu, kwanini alipigwa risasi..hivi pia tuvichunguze...'akatulia docta

'Sawa polisi walifanya hivyo, hawakupata kitu...'akasema

‘Sasa pamoja na hayo, kuna watu siku hizi ni wabaya sana, kila nyakati huja na watu wake kwa mfumo uliopo, sasa hivi ni kipindi cha mitando, digitali wanasema wenyewe..., na hao watu wajanja wajanja,...wanajipanga kihivyo,..wanajua kuwa watu watelekea huko, na wao wanacheza na akili za watu,...

Wao walivyo, wanawekeza mambo yao kihivyo, kusoma akili za watu na kutumia walichojifunza kwa masilahi yao, bila kujali athari kwako, mambo yao yapo hivyo,…na wenzetu huko nje, kwa vile mambo haya yalianza siku nyingi, wana namna yao ya kujilinda, sisi bado..na ni bado sana, maana hatutaki kusoma, hatutaki kufanya utafiti, sisi ni kukopi na kupesti..ni hivyo, na ushabiki, wa nani zaidi…

‘Ujanja wanaotumia, ni kutengeneza jambo lionekane kama kweli, wanajenga sabbu ambazo kwenye uso wa watu zitaonekana ndivyo, na kwa akili zetu ambazo hazitaki kuchunguza, tutakubaliana nahilo, tu..ni mapenzi ya mungu, au sio..lakini mungu katuambia tusome, tusome nini sasa..tuyasome mazingira yetu ili tuweze kuendana nayo, tukibakia tu mungu kapenda, haya mungu kapenda,... hawa jamaa wanazidi kuharibu jamii…’akasema docta.

‘Ukisema hivyo docta, ulitaka tufanyeje labda,…?’ akauliza

‘Hebu kwa kumbukumbu zako rudi nyuma kidogo, …siku hiyo ya tukio ulikuwa wapi..?’ akaulizwa.

‘Siku ile naikumbuka sana, siku ile nilikuwa hapa hapa nyumbani, usiku tulikesha kwa usumbufu wa hayo madude, mara bundi, analia, mara..yaani we acha tu,..kwahiyo siku hiyo mchana nikasema nilipize usingizi wa usiku,..sikuwa na shughuli za kufanya nikaamua nilale tu..

Nikiwa usingizini, ndio mara nasikia ukelele, baba nanihii njoo huku kuna tatizo, nafika namkuta mtoto anatoa mapofu mdomoni,..tukaharakisha kutafuta maziwa, mdomo haufunguki…yaani ..haikuwezekana, ikabidi tukimbize hospitalini, ..oh, tulichelewa..ndio siku ilishafika tena..’akasema

‘Kabla hujalala huyo binti alikuwepo..?’ akauliza

‘Hapana waliaga kuwa wana safari..kidogo, basi nikawaambia mimi nitabakia nyumba wasiwe na wasiwasi..’akasema

‘Ulibakia peke yako..?’ akauliza

‘Ndio..lakini baadae nikasikia mchakariko,..nikachungulia dirishani, nikamuona huyo mpangaji wangu akitokea dukani,au sokoni, alikuwa kashika mfuko wa Rambo, nilipomuona kuwa ni yeye, mimi nikarudi kupumzika..kulala…’akatulia.

‘Halafu baada ya hapo, elezea kila kitu maana nahisi kuna jambo limejificha hapo…’akasema docta.

‘Baadae nikasikia kelele ,nikajua ndio mabinti wamerudi, lakini kukawa kimia, nikajiuliza ni nani hao, ikanipa hamasa nikatoka nje, sikumuona mtu, hata huyo mpangaji hakuwepo, nikajua ni yale yale ya kusumbuliwa, baadae sana, ndio wakarudi wenye nyumba…’akatulia

‘Wenye nyumba ,,?’ nikauliza mimi

‘Ndio wenye nyumba si ndio watoto wangu na mama yao,..lakini wakati huo mama yao alikuwa hajafika, naona mama yao alikwenda kwingine, niliwachungulia dirishani, ..na nikwaona wakiongea, ila huyo mkubwa nilimuona katulia sana , usoni hana raha, nilimchunguza kwa kupitia dirishani wao hawakujua kuwa nawachunguza, ..sikuwa na hamasa ya kutoka .ila baadae nilipowaza sana, niaona nitoke nikaongee nao kidogo…’

‘Vipi mbona huna raha..?’ nikamuuliza binti

‘Hata baba sijisikii vizuri tu…’akasema

‘Tangia jana unasema hivyo hivyo, jiandae twende hospitali..’nikamwambia

‘Hapana baba nimeshakunywa dawa…’akasema basi nikaona hakuna tatizo, mimi nikarudi kulala, baadae mama yao akaja, nikasikia wanaongea, baadae nikashikwa na usingizi, nilizindukana kwa hizo kelele…’akasema

‘Baada ya hilo tukio, ulijaribu kuchunguza chumba cha binti yako uliona nini cha kushuku labda..?’ akaulizwa

‘Mhh, kabla watu wa usalama hawajafika,..nilikagua huku na kule sikuona cha zaidi..hata labda hiyo sumu, hakuna..nilishangaa kusikia kanywa sumu, hakukuwa na kitu chochote humo chumbani,..hata polisi walipokuja na kukagua, hawakukuta kitu kama sumu…unaona…sasa sijui…’akasema

‘Kuna kitu nataka kukuuliza zaidi, turudi nyuma zaidi,..je hicho kiwanja ulichokuwa umejenga nyumba ulikipataje..?’ akauliza

‘Aisee…,unajua ndio maana nilitaka niuze hata hilo eneo, unajua nilinunua eneo hilo, kumbe lilikua na migogoro, lilikuwa ni la kifamilia, wakatapeliana wenyewe kwa wenyewe, na kuuziwa kwangu hakukuwa na makubaliano ya kifamilia, kwahiyo wengine wakawa wamesua..ni mambo yao lakini.., mimi sijui, nakuja kujua baadae sana..lakini nikawalipa hao waliokuwa wakidai, kwahiyo nikawa nimelipa mara mbili, sikujali kipindi hicho maana nilikuwa nazo…na nilishalipenda hillo eneo…’akatulia

‘Ni nani hao, waliokuuzia..?’ akauliza

‘Mh, ni mzee mmoja sasa hivi hayupo duniani, wapo vijana wake…ila yeye kama kaka ndio aliwapunja wengine, kwahiyo kukawa na ugomvi wa kaka na dada zake, baadae kaka ndio akaniuzia,..sasa hao ndugu kaka na dada zake waliyamaliza, waliokuja kuleta shida ni watoto wao..na mmoja wa mtoto wao ndio huyo anayeishi kwenye hiyo nyumba,..ndio maana sikutaka kumuondoa, ni jamaa mnzuri tu, kanisaidia mambo mengi…’akasema.

‘Yeye ni mtoto wa baba au wa hao dada za huyo baba aliyekuuzia,…?’ akaulizwa.

‘Yeye …aah,ni mtoto wa huyo baba, lakini alizaa naye nje ya ndoa, kwahiyo hakuwepo kwenye huo ugomvi, ..kwanini mnashuku ..?’ akauliza.

‘Hapana hatumshuku vibaya bado…ila nikuulize jambo, je ni mganga wa kienyeji, ..?’ akauliza docta.

‘Ndio anajishughulisha na mambo hayo, ...lakini mmh, kwa vile mimi namfahamu sana, sijaweza kumweka kwenye kundi hilo la waganga haswa, ni mjanja mjanja tu...lakini hutaamini, anawateja wake, wanakuja sana, wanamuamini, lakini mimi sina imani hiyo kwahiyo, nachukulia kuwa ni mtu anatafuta tonge kinywani…’akasema.

‘Anatibiaje wagonjwa wake..?’ akaulizwa.

‘Mhh..mimi sijui...maana sijawahi kufika akifanya kazi zake, au kwenda kwake kupata tiba. Huyo jamaa anasema alipatwa na mapepo, na kutokana na hayo mapepo, ndio akajifunzia uganga…wakati mwingine mwanzoni alikuwa anapiga ukelele sana, anakuwa kama ana mashetani,…akipandisha hakukaliki, lakini anayajulia mwenyewe, sikuwa na matatizo naye sana..’akasema.

‘Kasoma soma hivi,..?’ akauliza.

‘Aaah, kasoma wapi huyo, ujanja ujanja wa mjini tu, ndio hao walikuwa wanalipiwa ada wanaishia kwenye miti, ila ni mtaalamu wa kutengeneza redio, tv..na ni mtundu mtundu sana wa ufundi mbali mbali, ana vipaji vingi sana, mimi nilimpendea hivyo maana kikiharibika kitu huhitaji fundi wa nje namtumia huyo huyo..’akasema.

‘Ok…ana mke?’ akaulizwa.

‘Hahaha..huyo jamaa bwana, aliwahi kuoa, akaacha, akaoa, akaacha..sasa sijui kwanini…ila mke wake wa awali, alifariki,..kifo cha ajabu ajabu tu ..yeye alikuwa hayupo kurudi mkewe yupo kitandani anavuja damu puani mdomoni..basi kuchunguzwa wanasema ni shinikizo la damu…alikuwa na mtoto mmoja,..mtoto huyo naye kapotea hadi leo haijulikani wapi alipo, namuonea huruma sana, mpaka sasa hataki hata kuoa alimpenda sana mke wake…’akasema.

‘Kuna tatizo hapo…ana tatizo huyo jamaa.., lakini huenda hajijui, au ndio mambo ya kurithi,au anatumiwa, sasa nilikuwa nataka niongee naye moja kwa moja nijua tatizo ni nini hasa, nahisi kuna watu wako nyuma yake, na wanamtumia, au kweli ni yeye mwenyewe, lakini kama hajasoma, kama yupo hivyo ulivyosema bado kuna mtu yupo nyuma yake…’akasema docta.

‘Kwanin umenihoji sana kuhusiana na hilo,..?’ akauliza mzee.

‘Hapana mzee, mimi ni dakitari wenu, na pamoja na afya zenu nilitaka kuona mazingira yenu, kwani matatizo haya ..yana sababu kubwa, huenda tatizo lilianzia ndani kwenu, na huyo binti yenu akachukuliwa kama kafara, ….sizani kama alijiua..’akasema docta.

‘Acha hiyo docta...anyaway, nisikukatishe kauli..., unajua unachokizungumza hata mimi kiliniumiza kichwa sana niliamini hivyo awali..., nikawachukua watu wa usalama, wapelelezi.. wakachunguza, hakuna kitu walichokigundua, hadi hii leo..nikabakia na kisasi cha huyo aliyemtia mimba binti yangu, kiukweli huyo tutakula naye sahani moja, sitamuachia mpaka nimpate, unajua, hiyo ni ahadi…’akatulia.

Docta akatoa vitu kwenye mkoba wake, halafu akatoa zile picha mbili, na moja akamkabidhi mzee, na kusema;

‘Ndio hivyo mzee, hebu angalia hii picha…’akaitoa ile picha na kumkabidhi mzee.

‘Yah….,hii ni picha ya binti yangu…’akasema akiwa kama hataki kuiangalia zaidi.

‘Uliwahi kuiona hiyo picha kabla..?’ akaulizwa.

‘Hapana,..mabinti zangu wanapiga picha nyingi tu…siwezi kujua ipi ni ipi unajua vijana tena.

‘Hebu iangalie hiyo picha kwa makini, mazingira yake...ichunguze kwa makini..kunaonekana nini na nini..ichunguze vizuri, ni nini kimezunguka hiyo picha…unaona nini zaiidi ya hiyo picha…?’akasema na baba akaikagua, na kusema.

‘Mhh…naona kama walipigia maeneo ya makaburini, ndio unaona huku,..haya ni makaburi..ndio walipigia pale makaburini, sijui kwanini waliamua kupigia huko..’akasema akionyesha mshangao.

‘Hilo namba moja, tunaweza ok, labda waliamua tu, wakati wanapita wakasema tupige picha,..lakini hebu igeuze hiyo picha kwa nyuma...angalia nyuma ya hiyo picha, kuna tarehe hapo japokuwa ni ya hiyo katarasi, au mashine ya kutoa picha, yaonekana picha zao huandika tarehe iliposafishwa, hebu angalia ilikuwa tarehe ngapi…’akasema.

‘Mhh, tarehe..ndio kuna terehe hapa…tarehe…eeh,,mmh, mbona tarehe hii binti yangu alishakufa…akageuza tena kuikagua, akaangalia kwa makini, …halafu akasema,..’halafu, mbona macho yake yapo hivi,…mmh, lakini ni yeye, ila macho,…siwezi kujua zaidi…’akasema akiwa hana hamu tena ya kuikagua hiyo picha.

‘Kuna tatizo limejificha hapo mzee, kuna mtu anawachezea akili..., alishakujulia, alishaijulia familia yako ilivyo, anajua historia ya maisha yako..anajua mengi zaidi yako, kwenye maisha yako…katafuta njia.., na huenda ni sababu ya mali,..sina uhakika.. au kuna jambo jingine zaidi limejificha, ndio maana nataka kuongea na binti yako faragha…’akasema docta.

‘Mimi sikupendelea mambo haya yaendelee zaidi na zaidi, ..na hasa kuja kumchanganya bint yangu maana sioni faida yake,..sitapenda kumhoji huyo binti yangu mambo hayo yaliyopita naona mtarudisha kule kule...'akasema

'Hapana mzee, hii ni moja ya tiba yake, na yeye akilini mwake, dhamira yake ni kuhakikisha kuwa haki imetendeka, sasa itatendekaje..ndio hivi tunataka kutafuta, maana mnaweza mkamnyoshea mtu kidole, mkatuhumu kumbe masikini wa watu hana hatia, ..kwa jaili hiyo, ili kuondoa msononono, ..ni lazima tuutafute ukweli..umeona eeh...'akasema docta.

'Unajua mimi nahisi wana hamu na eneo au nyumba,..sasa kama wanataka hiyo nyumba basi mimi nitaicha waichukue tu..nilikuwa naongea na huyo jamaa, aliyekuwa hapa awali , nikamwambia kama kakosa mnunuzi basi mimi nitaitoa kwa watu wa dini, iwe sadaka yangu..’akasema

‘Alisemaje..?’ akauliza docta.

‘Ndio nyie mkatokea, ila alisema yeye atajitahidi kumpata mnunuzi, …lakini kwanza anataka kuisafisha, kuondoa hayo marue rue.. ..nilikamwambia muhimu ni hilo, hayo mengine anayajua yeye…kuna kitu aliniuliza, kuwa huyo anayemtibia binti yangu ni nani..sijui alijuaje..’akasema.

‘OK….ndio maana alikuja kwako, anataka kukuchota akili tu , ila mzee, uwe makini na marafiki zako, sio wote wanaokuchekea ni marafiki wa kweli, wengine wanakuonyesha meno tu …lakini moyoni ni wanafiki, kuwa makini sana, na muombeni mungu wenu sana..’akasema docta.

‘Sasa hiyo picha mbona ipo hivyo..?’ akauliza huyo mzee alipoitazama tena ile picha.

‘Hii picha ni kiini macho, tu..akkitengeneza, sasa kama anataka kukujua kuchota akili yako, anatumia picha yako au ya mtu unayemfahamu, sasa wewe ukiitizama ile picha kwa makini, unakuwa kama unazama kwenye macho ya ile picha, wenye uamkini huo wataiona hiyo hali, lakini wengu hatupo makini…

‘Sasa unapozama kwenye hisia au kwenye macho ya ile picha, yeye huko alipo, kama alikuwa anakutafuta anaichota akili yako na kujua unachokifikiria..ni darubini zao, ndio maana ukifika kwa mganga anakupigia ramli, anachofanya pale ni kuzama kwenye akili yako, anakuchota akili yako anajua maadui zako, anajua ni nani unamdhania ni mchawi wako,  nani unamchukia, sasa hapo kwa kupitia shetani, anawachanganisha tu, hakuna zaidi…’akatulia.

‘Mhh, docta mbona unatutisha …’ nikasema.

‘Sio kwamba ninawatisha, ni vitu vipo…uchawi sio lazima uwe wa kuwanga, usiku, uchawi upo hata kwenye mitandao,..mtu atahitajia namba yako ya simu, kwa kupitia hiyo namba,…anakuibia, kwa vipi..jiulize hapo…mtu anahitajia picha yako, kwa kupitia picha yako anacheza na akili yako..mtu anataka siku yako ya kuzaliwa, kwa kupitia tarehe yako, jina lako , la wazazi wako, anakuchezea…’akasema.

‘Duuh, docta…’nikasema.

‘Utandawazi…digitali..ndio hivyo , kuweni makini sana mnapoweka kumbukumbu zenu, sio wote wana nia njema na nyie, sio wote marafiki ni marafiki,..ukipata rafiki mchunguze kiukweli, ndio maana wazazi wetu walikuwa wakihimiza mtu uolewe kwenye familia inayotambulikana,…sasa nyie mnatafuta rafiki kwenye mtandao,..mtaumia sana…’akasema.

‘Una maana gani …hii picha..hapana, nikiingalia kweli nakuwa kama nazama kwenye macho ya ….hebu chukua picha yako..’akasema mzee.

‘Mzee, hiyo picha, huyo sio binti yako hasa, ni taswira ya binti yako, iliyotengenezwa kitaalamu, ..viini macho hivi vinatengenezwa kinamna ya kitu wanachotaka kifanane na hilo lengo lao,..kifupi ni shetani…taswira ya kiini macho,..kinatumiwa kughilibu watu…ili watu waone kuwa ni yule mtu, kumbe sio, nia hasa ni hadaa,na ghiliba, kwa kucheza na akili za watu…hujaona mtu anameza misumari, anakula keki anazaa yai..nk. ndivyo watu hawa wanafanya, …’akatulia.

‘Kwahiyo ni uchawi..?’ mimi nikauliza.

‘Kama unatumia utaalamu huo kuwadhuru watu basi wewe ni mchawi, na utaalamu kama huu unaweza ukanunuliwa tu, sio lazima uwe wa asili ya uchawi, sasa kwa huyu sina uhakika kama kaununua au kaurithi, hata hivyo sijajua kwa jinsi gani kaweza kuingia kwenye mtandao, wakati unasema hajasoma, hapo kuna kitu kingine nyuma yake, kama ulivyosema ana mashetani, sijui ;abda ndio anayatumia hayo mashetani..lakini muhimu ni, mpaka tukutane naye kwanza…’akatulia.

‘Kwani wewe docta kwa utaalamu wako, huwezi ukamjua huyo mtu ni nani, wewe pia si unayajua hayo mambo ya kumjua mtu, au..?’ nikamuuliza.

‘Hapana, mimi sio fani yangu hiyo, mimi sio mganga wa kienyeji, mimi ni dakitari lakini pia ni mtafiti najaribu kutafiti undani wa haya mambo,ili nije kuoanisha mambo hayo na hali halisi ya kitaalamu,..muhimu kwa sasa tusubirie tu, huyo jamaa atakuja…’akasema docta.

‘Nani huyoo atakuja…?’ sauti ikatokea kwingine aliyeuliza hivyo alikuwa mama akiwa na binti yake yaonekana walikuwa wametokea kwenye mazoezi. Na walipotuona wakawa na hamasa sana, hasa huyo binti, alionekana kutabsamu, lakini alipotizamana na mimi nikaona kama anakunja uso, nikahsi kuna jambo,


NB: hapa kunahitajia umakini kidogo, ngoja niishie hapa ili nisiwachanganye zaidi.


WAZO LA LEO: Kamari na kupiga ramli, ni dhambi, ni moja ya kazi za shetani..tujiepushe navyo, kwani nia ya vitu hivyo, ni kujenga uadui. Tukumbuke kuwa  Shetani moja ya kazi yake kubwa, ni kuvunja ndoa, kugombanisha ndugu kwa ndungu ,marafiki kwa marafiki, na ndio maana sasa hivi dunia haina amani , kwani mtendo yote ya shetani yapo kwenye nafsi zetu. Tumuombe mola wetu atusaidie kumshinda adui huyu mkubwa wa imani zetu.
Ni mimi: emu-three

No comments :