Simu ikawa hewani na sauti iliyosikika ilikuwa sauti ya
kukatika katika, yaonyesha huyo mtu yupo kwenye hali mbaya, ….na mawasiliano yalikuwa
sio mazuri…
‘Da -da-lali, ha-ha-halooh,…’ilianza hivyo, na dalilia
akasema
‘Haloo ni mimi kuna nini…mta-alamu?’ akauliza dalali
akimgeukia mpelelezi, na mpelelezi akamuashiria aendelee kuongea.
Sauti ilikuwa ni shida,….mwanzoni nilijua labda huyo
mtaalamu alikuwa mikononi mwa polisi na sasa yupo kwenye mateso…lakini kwa hali
kama hiyo polisi wasingemruhusu kuongea kwenye simu,…labda kama kuwe kuna kitu
wanakihitajia wakipate…, lakini kwa jinsi alivyozidi kuendelea kuongea nikagundua vinginevyo, sauti ikaendelea kusema;
‘Da-dalali wewe mmmmh, ….’akatulia akigugumia,
‘Mtaalamu vipi…kuna nini,….mbona unaongea hivyo?’ akauliza
Dalali akihisi na wasiwasi.
‘Yaani wewe…ndi-ndio unanifanyi-a oooh, hivi…’sauti ikatulia
na mngurumo wa kugugumia ukawa unasikika, halafu sauti ikaendelea kusema;
‘Sasa sikiliza mmmh,….ehuuuh, …mimi nimekwepa kuwaambia polisi
mambo yako….eeeh, oooh,unasikia lakini ujue kuwa ,….sitaweza kuvumilia zaidi,
nilichoongea nimeongea, na ni kweli sikutaka kuwaficha…’akawa anajitahidi
kuongea vyema, na kauli hiyo ilimfanya dalali ageuze jicho kumuangalia
mpelelezi.
‘Hata ….oooh, najiuliza… ni kwanini ni – ni-teseke
hivi,….aaah…., ‘sauti ikatulia, nilimuona Daalli akihangaika nahisi alikuwa
akitafuta njia ya kuizima hiyo simu, lakini mpelelezi alikuwa ndiye kashikilia
ile simu kuhakikisha kuwa dalali haizimi .
‘Na….na….wakati ni mambo yenu…sasa …ooh, nasema..mmmh,….oooh,
utajua mwenye,. ‘akatulia
‘Mtaalamu,….’akataka kusema lakini mwenzake akaendelea
kuongea
‘Nisikilize..sina muda….kwanza ujue… walichonifanya, ooh….watanijua
mimi ni nani….na …si…achilia mbali…..mazindiko,..kazi yako, mimi basi, …., sasa ni juu yako…hayo
nime-ya-ondoa…utajua …we-we- mwenyewe…usinitegemee mimi …ni –wewe ..oooh,
oooh..ooh….mwenyewe…’kukawa na ukimia kidogo, na Dalali alikuwa anataka kukata
simu, lakini mpelelezi akamzuia, na huyo jamaa akasema;
‘Unajua wengi hawanielewi…hahaha….mimi, ….mtaalamu,…hahaha..oooh,
nitawafanyia kitu mbaya sana, hawa watu..oooh, …wanafikiri mimi ni mtu hivi
hivi tu,…achachachacha…..mhhh, mhh, tatizo ni masharti,…haya mambo ya mizimu,
wame-goma, kosa…nimekiuka miiko….kosa, …..yatima…ooh, yatima,…oooh,….haikutakiwa
hivyo….ooh, umeniponza…umeniteketeza…lakini….kabla ya mimi,ni
wewe….naapa,…utajuta…’ akatulia.
‘Vipi mtaalamu ….kwani kuna nini, wanakutesa polisi au?’ Akauliza dalali.
‘Aheri wange…nitesa ,….aaah, mimi wanitese…hahaha…tatizo, ni miiko…
hainiruhusu, lakini, siwezi tena….ngoja, kwasababu kufa nitakufa tu……oooh,
lakini kwanza nitaanzia kwako, sijawahi kufanyiwa hivi …hata siku moja….mmh,
wewe umeniharibia kazi yangu, kwa tamaa zako,….taireeeeh, mizimu
taireee….hapana..hapana…sitaki kufaah…hapana…oooh’akatulia
‘Mtaalamu kuna nini ndugu yangu…?’ akauliza dalali sasa
akionyesha wasiwasi, lakini jamaa alikuwa kama analia..ni kilio cha kweli,
halafu sauti ikasema;
‘Mimi….ndugu yako, ..oooh, wakati nakufa…unaniacha nakufa,
udugu ga-gani -ooh, huo…..yote haya uliyayataka wewe na…na huyo…’hapo akatulia
‘S-sasa kabla sijafa, maana sizani kama nitaishi, naona
wahenga wananiita, oyoyoyoyoyo…oyoyoyo, mhhh, kifo kichungu….oooh, sitaki kufa
…oooh, sifiiiih, oooh…’kukawa na ukimia kidogo.
‘Mtaalamu.upo wapi…?’ akauliza dalali akigeuka kutaka
kuondoka. Na mpelelezi akamuashiria atulie
‘Nipo….karibu kuelekea ahera, …mhhhhhh, sasa sikiliza, hata
nikifa, nataka pesa yangu uifikishe kwa familia yangu..umesikia,….ooooh, ni-ni
ahidi,…dalali niahidi…na nataka wewe, sio huyoo…ni wewe….’akatulia
‘Umesikia,..oyoyoyoyo, oyoyoyo, wahenga wa
jadi,…oyoyoyo…..chachacha….Dalali ,unasikia...usipofikisha hiyo pesa kwa familia yangu kitakachokupata hutaamini,
nitakutokea kama mzimu, na kuyaangamiza maisha yako, umenisikia, …’akatulia
‘Mtaalamu sijakuelewa, pesa ipi…?’ akasema akigeuka
kumuangalia mpelelezi.
‘Pesa ipi….unadiriki kusema hivyo….oooh, utaumia, wewe mtu
utaumia, unamsikiliza huyo…hahaha, eti pesa gani,…..una hatari wewe,…kweli
nimeona, ….niliona, lakini nilifumba macho,..kuna hatari kubwa mbele
yako….umegusa kubaya…mmhh, siwezi kukusaidia tena….kwaheri,…utajuta,….utanikumbuka….uta—ooh,’akatulia,
kulikuwa kama minong’ono ya kuimba, au …sauti ilikuwa ndogo, halafu;
‘Da-la..li….umenisikia…..’akatulia
‘Kwani kuna nini mtaalamu..upo wapi… nimekuelewa, usiwe na
shaka, nitafanya hivyo, utakavyo…usiniangamize mimi ni ndugu yako…upo wapi.?’ Akauliza
Dalali.
‘Usiniulize nipo wapi…mjinga mkubwa wewe…wewe ni mpuuzi tu, …utapata
shida sana..utatamani kifo hutakipata, aheri yangu mimi…oooh, oooh, ooohh…oookokokokoh…umechelewa---koroooooh.’sauti
ikakata, na kukawa kama kukoroma hivi.
‘Mtaalamu, mtaalamu…..mtaala….m’Dalali akawa anaita, lakini
zaidi ya sauti za uvumi wa upepo, hakukuwa na sauti nyingine.
Dalali akashika mikono yake kama kawaida yake, anavishikisha
viganja mbele kama anaomba halafu anavipuliza…, akasimama, akashika
kichwa,…akageuka kuangalia mlangoni, halafu akamgeukia mpelelezi, akamgeukia
shemeji yake….halafu akanigeukia mimi, akanikunjia uso kwa hasira, akataka
kuniambia jambo lakini hakusema, akamgeukia mpelelezi, na kusema;
‘Tafadhali mkuu..nipo chini ya miguu yako, …huyu mtu
anahitajia msaada wangu, ..siwezi kumuacha kwa hali hiyo, …niache niende
nikamuone…’akasema
‘Sasa unajua huyo mtu yupo
wapi…?’ akaulizwa na Mpelelezi
‘Atakuwa polisi, …wanamtesa huyo…nyie polisi kwanini
mnafanya hivyo….’akasema
‘Unahakika na unachokisema…?’ akauliza mpepelezi
‘Uhakika gani?’ akauliza akimtolea macho mpelelezi
‘Kuwa polisi wanamtesa,…polisi wamtese halafu wamuachie simu
aongee na wewe….?’ akaulizwa
‘Kwa mara ya mwisho mlisikia nyie wenyewe akisema kakamatwa,…sasa
alikamatwa na nani , …?’ akauliza na mpelelezi akachukua simu yake kutaka
kupiga lakini kabla hajafanya hivyo simu yake ikaanza kulia, akaangalia
mpigaji,.
Hakuipokea hapo akatembea kuelekea nje huku akiisikiliza, hakuchukua
muda akarudi, na alionekana mwingi wa wasiwasi usoni, akamuangalia Dalali kwa
makini, halafu akasema;
‘Wewe unajua wapi mtaalamu alipo , ..?’ akauliza mpelelezi
‘Sikuelewi afande…’akasema dalali akionyesha uso wa mashaka
na alikuwa anahaha, kachanganyikiwa kabisa,
hapo nilimuona kumbe huyu jamaa naye anachanganyikiwa hivyo!
‘Huyu mtu katoroka polisi, na wakatii anatoroka akapigwa
risasi ya mguu, lakini aliweza kuwakimbia polisi, …alikimbia kama
anapaa….ndivyo walivyoniambia…’akasema mpelelezi
‘Mimi nawaambia huyo mtu si wakawaida, mumeona
wenyewe…..’akasema dalali hapo akawa kama kapaat ahueni.
‘Kama sio wa kawaida mbona hakuweza kuzuia risasi,….na huko
alipo atakuwa kwenye hali mbaya, sasa eleza wapi anaweza kupatikana ili
akaokolewe….’akaambiwa dalali.
‘Akaokolewe au akakamatwe, na mimi siwezi kujua wapi alipo
….’dalali akasema sasa alionekana kama hali imemrejea , aliingiwa na unafuu
fulani.
‘Usipoteze muda, wewe mwenyewe umemsikia hapo, …kwa jinsi
walivyoniambia atakuwa kapoteza damu nyingi sana,…sasa uache ndugu yako afe,….’akaambiwa
‘Hawezi kufa huyo,..i mtaalamu ..nyie hamjamfahamu vyema,
Yule aliwahi kupambana na majamazi akakatwa koromeo, wakajua wamemuua, lakini
akajizuia kwa shingo kuiminya, hadi akafika hospitalini..akapona, iwe hiyo
risasi ya mguuni….’akasema
‘Umemsikia hapo…hiyo ni sauti ya kukata roho…na ufahamu huyo
mtu akifa, makosa yote yatakuwa kwako, ni bora twende tukamuokoe ili adhabu za
makosa yake ayabebe yeye mwenyewe…’akaambiwa
‘Kwani yeye ana makosa gani,…au mimi nina makosa gani…?’
akauliza
‘Unapoteza muda….sema wapi jamaa yako yupo…hapa unacheza na
uhai wa mtu, sema wapi anaweza kupatikana…’akaambiwa kwa sauti ya ukali, na
hapo akanywea na kusema;
‘Hata sina uhakika….’akasema kama anawaza, akapiga simu,
lakini sasa simu inasema haipatikani.
Dalali akakunja uso kama kufikiria halafu akasema;
‘Lakini sina uhakika,…twendeni tukajaribu….’akasema na mara
mpelelezi akawasiliana na watu wake haikuchukua muda jamaa wawili wakafika,
wakamfunga pingu Dalali
‘Sasa kwanini mnanifunga mimi pingu….?’ Akauliza
‘Unaisaidia polisi, usiwe na wasiwasi…’akaambiwa na kitendo
kile kilimfanya Dalali akunje uso aliponiangalia, na shemeji yake alikuwa sasa
kasimama, kama anataka kufanya jambo, lakini hakuweza akabakia kusimama tu.
Sasa mbona mwamfanya hivyo shemeji yangu…’akaweza kusema
hivyo
‘Shemeji, …usijali nitayamaliza…’akasema dalali…na mimi
nikasimama nikianza kuwafuta hao watu, na mpelelezi akaniambia;
‘Na wewe tusubiri hapa hapa, usiondoke….’mpelelezi
akaniambia , nikatulia na kugeuka kumuangalia shemeji na watoto sasa
walishaamuka, lakini bahati nzuri hawakuhai kukiona kile kitendo cha baba yao
mdogo akitoke nje na polisi.
************
Mimi nilibakia pale na Yule mama mjane, tukiwa na tunasubiria
kwa vile nilipewa amari nisondoke pale, nikaona
nitii amri nione mwisho wake utafikia wapi, masaa yakapita, ….
‘Shemeji, eeh, dada
wewe waandalie watoto, naona usiku unaingia,….’nikasema
‘Kila kitu kipo tayari…labda wewe tukuandalie chakula…?’
akaniuliza
‘Hapana….nyie endeleeni, nitaondoka muda sio mfupi…’nikasema
‘Uondoke unieche humu ndani, …siwezi kukaa peke yangu na
watoto,….’akasema
‘Kwanini, mbona mlikuwa mnaishi wenyewe humu ndani…?’
nikamuuliza
‘Mara nyingi alikuwa akija jamaa yao shemeji, au
mlinzi..hata hivyo..bado ukiwa chumbani usiku kuna vitu vya ajabu vinatokea, mara
mipaka inalia…hata hujui wametokea wapi…mara mipanya…kunatisha kweli
kweli…’akasema
‘Nina imani sasa havitatokea…jipe imani , na mungu
atawalinda…’nikasema
‘Kwanini, visitokee, wakati nilipokuwa ndani, nilisikia
sauti ya ajabu ndio maana nikaamua niondoke kwenye hii nyumba, kwanini una
uhakika huo…?’ akauliza
‘Muamiini mungu wako, na kabla ya kulala hakikisheni
mumemuomba mungu …fanyeni ibada, swalini….ombeni, mtayashinda haya yote, kama
haya ulishamkabidhi mungu, ujue sasa ushindi unakuja,…’nikasema na mdada huyu
akaniangalia kwa muda bila kusema neno. Halafu akasema
‘Nakushukuru sana kaka yangu…mungu akuzidishie…’akasema
‘Nendeni…mkapumzike, mimi nipo hapa kwa muda….’nikasema na
kweli.wanafamilia wale wakaingia chumbani kwao kujipumzisha na mimi nikabakia
pale mlangoni nikisubiria, huku nikawasiliana na watu wangu.
***********
Watu wangu walisema kwa hivi sasa wanashindwa kufanya jambo,
kwani polisi wamewazuia,na wanafuatiliwa , kwahiyo wao wameona wasubirie kwanza
wakitegemea wasamaria wetu wanaojitolea kutupatia taaifa ndani ya kundi lao;
‘Au mkuu unasemaje , tuendee, hatushindwi kufanya hivyo ,
lakini inaweza kukuletea athari kisheria…’akasema mmoja wa watu wangu
‘Msiendee…mtanipatia taarifa ..kesho, au…’nikatulia
nikiwanza jambo, halafu nikakata simu, nilichukua ile simu yangu niliyokuwa
nimeweka mezani na kuanza kusikiliza yale yaliyojirekodi mle, …kuna kitu nilikuwa
nakitafuta…
Mara simu yangu nyingine ikalia, alikuwa mmoja wa watu wangu
akasema mtaalamu keshapatikana, lakini
akiwa hana fahamu, kumbe wakati anatoroka alipigwa risasi ya mguuni, na
amepoteza damu nyingi sana, na hali yake
kwasasa ni mbaya sana, inawezekana asipone …
‘Vipi huyu mtu wetu, Dalali, kaweza kuongea lolote na polisi…?’
nikauliza
‘Mpaka sasa kashikiliwa kwa ajili ya kuisaidia polisi, ila kakataa
kusema chochote, anataka wakili wake awepo…, lakini polisi hawajamruhusu kwa
hilo, na pia anataka kuongea na wewe…!’
‘Kuongea na mimi, kuhusu nini…?’ nikauliza kwa mshangao
‘Anasema wewe ndiye umeyasababisha yote hayo, kwahiyo
anataka mkabiliane wewe na yeye ili athibitishe mbele yako kuwa yeye hana
kosa…’nikaambiwa
‘Atathibitishajekwangu, wakati mimi ananiita tapeli…na
polisi wamesemaje…?’ nikauliza
‘Kwa hivi sasa walikuwa wakihangaika na huyo mtaalamu, na walikwenda
kuchunguza nyumbani kwake, wamekuta familia yake haipo…imeshaondoka
kuelekea kijijini kwao, ni kama
walishafahamu kuwa hilo litatokea…’akasema
‘Kijijini kwao ni wapi…?’ nikauliza lakini kabla hajajibu
hilo nikauliza swali jingine kwa haraka;
‘Kwanini polisi hwajaruhusu wakili wa dalali aitwe,na ni
nani huyo?’ nikauliza, na kukawa na ukimia, nikasema
‘Halloh vipi…kuna nini kinaendelea mbona upo kimia, kwani
upo wapi …?’ nikauliza
‘Hebu subiri nitakupigia naona kuna kitu kinaendelea
…’akasema mtu wangu na kukata simu, na mara simu yangu ikaita tena, na
aliyepiga simu kwa sasa alikuwa mpelelezi, akaniambia nipo huru kuondoka ila
kesho nahitajika kituo cha polisi .
‘Nahitajika polisi kwa kosa gani?’ nikauliza
‘Dalali anataka kuongea na wewe..’akasema
‘Kuhusu nini…?’ nikauliza
‘Kasema yote umeyaanzisha wewe na yeye anataka kuthibitisha
kwako kuwa yeye hana makosa,…kwahiyo anataka muendelee na hayo maswali yako, na
mwisho wake itathibitika kuwa kweli hana makosa hahusuki…’akasema
‘Kwahiyo mimi sio tapeli tena…?’ nikauliza
‘Ndio anataka kuthibitisha kuwa wewe ni mwongo, umempakazia
makosa na sisi polisi tumekuamini hivyo….’akasema
‘Kwani nyie polisi mlinifuata mimi, ..au nikutokana na
uchunguzi wenu?’ nikauliza
‘Ni manenoya mfa maji…na sisi hatutaki kumharakisha kwani
kuna mambo bado tunayafuatilia, na mlango wa kuyapata mambo mengine ni kwa kupitia
kwake, …ndio maana tumemkubalia ombi lake,….kesho ufike saa tatu…’akasema
mpelelezi
‘Je wewe umeshamuuliza yale maswali yako uliyoyataka
kumuuliza?’ nikamuuliza
‘Hataki kunijibu, …anasema kwa hivi sasa hataongea lolote
mpaka wakili wake awepo, na mpaka amalaizane na wewe..kwani chanzo cha yote ni
wewe…’akasema
‘Vipi kuhusu mnada wa kesho,
maana ni amri ya mahakama, je huo mnada utakuwepo….?’ Nikauliza
‘Huo mnada wa kesho eeh, ngoja,…bado tunafuatilia taratibu
zake,…japokuwa hakimu hajasema lolote, yote itategeema hiyo kesho…’akasema
mpelelezi.
‘Je ulitaka kumuuliza nini Dalali, mnahisi kaka yake hakufa
kifo cha kawaida, ….na kwanini mnauliza hayo maswali hivi sasa?’ nikauliza
‘Kiukweli awali nilizuiwa kuendelea na hii kesi kipindi cha
nyuma, lakini nilishangaa kuambiwa niendelee nayo hivi sasa….nahisi ni kwa vile
jalada lake lilikuwa halijafungwa, na mimi nimewaambia siwezi kulifunga mpaka
nihakiki baadhi ya mambo…, kiukweli ajali ya huyo jamaa ilionekana ni ajali ya
kawaida, lakini sio kutokana na uchunguzi wangu….hata hivyo, kwa vile
wanafamilia wenyewe walikuja kusema hawahitaji uchunguzi zaidi, ikabidi
tuachane nayo….’akasema
‘Unahisi ni kwanini?’
nikauliza
‘Hata sijui….sababu walizotoa wao ni kuwa ndugu yao ameshakufa, hawataki mambo mengine,
mambo mengine yatakuwa ya kifamilia
zaidi..na hiyo ajali ni ya kawaida tu….na ilitokea hivyo kwani watu wa usalama barabarani walihibitisha kuwa ni ajali ya kawaida, gari
lilishika moto, na dereva akashindwa kutoka kwa mshituko… wao waliangalia kwa
upande wao, kwa upande wangu nilikuwa bado naendelea na uchunguzi….’akasema
‘Unahisi kuna mtu alikuwa nyuma ya hilo, labda…anajuana na
Dalali, labda kuna mgawo, akashinikiza mambo hayo yafukiwe, iishe kihivyo au…?’
nikauliza
‘Hapana…ni kuwa kipindi hicho kulikuwa na kesi nyingi sana,
na hiyo kesi ilionekana haina uzito, kwa vile uchunguzi wa awali wa watu wa
usalama barabarani uliona ni ajali ya kawaida tu…na taarifa ya dakitari
ilionyesha kuwa dereva yaani huyo marehemu alipatwa na mshituko kabla ya ajali….mshituko
huo ndio uliomfanya ashindwe kulidhibiti gari….na moto ulipoanza kuwaka
hakuweza kujiokoa…’akasema
‘Kwahiyo wewe uligundua nini,…?’ nikauliza
‘Nilichogundua , ni kuwa kuna sababu ya hiyo ajali, …na
nilikuwa naitafuta sababu hiyo ni nini, ulipoanza kumuhoji huyo mtu, kuhusu
hilo deni, nimeweza kuunganisha kati ya hilo deni na hiyo ajali…na huo mshutuko
una sababu, yaonekana marehemu alikuwa anaongea na simu…sasa alikuwa anaongea
na nani, je hiyo simu ndiyo ilisababisha hayo…na mabaki ya hiyo simu hatukuweza
kuyaona…kipindi hicho nilitaka kufuatilia kampuni ya simu…lakini nislishindwa,
wangeliweza kutafuta namba yake na kuweza kuyanasua hayo mazungumzo…lakini
sikufanikiwa…..’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema ajali hiyo ilipangwa au….?’
nikauliza
‘Hayo tutayajua hapo kesho, ndio maana hata mimi
nimependelea wewe uendelee kumuhoji huyo mtu na mimi nitakuwepo…’akasema
‘Mhh..lakini mimi , japokuwa hajakubali, kile nilichokitaka
kwa kiasi kikubwa nimekipata,…sikuhitajia kuongea naye zaidi, labda tuje
tukutane niwapatie ushahidi wangu tuliokuwa nao…vinginevyo hata nikimuhoji
itakuwa ni hitimisho tu,…na…’akanikatiza
‘Hilo hitimisho ndilo nalitaka,…..kwani japokuwa vijana wangu na wamelifanyia kazi
hilo , kutakakujua kuhusu hilo deni, lakini bado kuna maulizo mengi, maana
kilakitu kipo sahihi,…hata hivyo kuna mambo wameyagundua,lakini bado kuna
maswali mengi ya kujiuliza….’akasema
‘Wao wamegundua nini….?’ Nikamuuliza
‘Walichogundua…ni hayo hayo,….naona hayo tutayajadili hiyo
kesho,kwanza nataka kusikia kauli yake, nitaweza kuingilia kumuuliza maswali
japokuwa mimi kanikatalia nisimuulize mpaka wakili wake awepo, sitojali sana,
ila nataka kabla uanze na yeye, ili nikiingilia kati iwe rahisi kumnasa….’akasema
‘Kwahiyo vijana wako hwakugundua jambo jipya, mbona
huniambii,…nakuuliza hivyo ili kesho nijue jinsi gani ya kumbana….’akasema
‘Kiukweli, vijana wangu walichogundua ni hayo hayo
yaliyokuwa yametokea kipindi hicho , na tukio hilo japokuwa bado halina
uhakika,linaonekana lilishirikisha watu wengi, na kati ya hao wengi , miongoni
mwao hatujaweza kuwapata, sasa tulijaribu kuangalia kwa upande huo wa benki,
wafanyakazi wengi wa kipindi hicho hawapo, na wengine walikuwa wameshafukuzwa
kazi, ….
‘Kwahiyo kiujumla kulionekana kulikuwa na tatizo, kuna namna
ilifanyika, swali likabakia je kuna uhusiano gani kati ya ajali na hilo deni…..’akasema
‘Je vijana wako waliwahi kuwahoji hao wafanyakazi, ambao
huenda walihusika…?’ nikamuuliza
‘Wachache….wengine wamekataa kutoa ushirikiano, na hata
hivyo, ikibidi nguvu za dola zitatumika, ili muda ukifika wawepo
mhakamani….’akasema
‘Ni kuwa hawapatikani au hawataki kujibu maswali, kuelezea
ukweli….?’ Nikauliza
‘Yote mawili,….maana wengine kuwapata inachukua muda, hata
hivyo hao waliopataikana ni kama wamesahau au wanajifanya wamesahau..….nina imani
hadi kesho tutakuwa tumeshawapata wote muhimu, tutawakumbusha tu ,….ndio maana
nikasema sasa mlango wetu wa kulimaliza
hili ni kwa kupitia huyo huyo dalali, je kuna mahusiano gani kati ya hilo deni
na kifo cha kaka yake…’akasema
‘Je wakili wake keshapatikana?’ nikauliza
‘Kesho atakuwepo, kwahiyo unatakiwa uwe makini katika
kumuuliza hayo maswali yako, ulenge kwenye jambo sio dhana.., si unamfahamu
huyo wakili wao alivyo mkorofi sana, sema na yeye hapendi kuingiliwa kazi
yake…mteja akimuingilia anaweza kukasirika na kuicha hiyo kazi hewani…hata
hivyo , mara nyingi mimi simuamini huyo wakili, natafuta jambo, nihalalishe
hisia zangu,lakini bado sijalipata, ni mjanja sana …’akasema mpelelezi
‘Swali jingine kabla hujakata simu, ni kuhusu huyu mjane na watoto wake, maana walisema
kesho wanaondoka, niwaambieje…?’ nikauliza
‘Hawezi kuondoka kwa hivi sasa, wameshapelekewa
taarifa, ila kama utapitia hapo,…mwambie
aendelee kusubiria,… kwani vipi hali ya mtoto wake ulipoondoka..?’ akauliza
‘Hajambo….sijaona dalili yoyote ya homa, ila mama mjane
anasema humo ndani kuna mambo ya ajabu ajabu yanatokea, ….sijui hilo linatokana
na huyo mtaalamu na mambo yao waliyoyapandikiza humo ndani, au ni kuchanganyikiwa
tu kwa huyo mama…’nikasema
‘Kuna kitu kingine kimejitokeza, …naona utapenda kukifahamu…’akasema
mpelelezi lakini alikuwa kama anasita kuniambia, hata hivyo akasema
‘Dalali ana nyumba ndogo, hii nyumba ndogo tuliona ikatusaidia sana…’akatulia
‘Kwanini….?’ Nikamuuliza nikikumbuka vijana wangu
walivyoniambia kuhusu huyo mdada, na mpelelezi akaongea yale yale niliyoambiwa
na vijana wangu.
‘Huyo mdada…., sasa hivi ni tajiri sana, anamiliki nyumba
nne, za nguvu, uchunguzi wetu unaonyesha ujenzi wa nyumba hizo ulifanyika
kipindi cha nyuma baada ya kufariki marehemu,…au inawezekana ujenzi ulianza nyuma kidogo kabla
hajafariki huyo marehemu,…’akatulia
‘Unahisi huenda huo mkopo ndio ulifanya hiyo kazi….?’
Nikauliza
‘Ndio hapo, ….nakupa hilo kama angalizo,…ukimuhoji vyema huyo jamaa tunaweza kuligundua hilo…’akasema
‘Hilo la huyo mdada, au nyumba ndogo, nalifahamu sana, na
hilo lina ugomvi mkubwa kati ya Dalali na mke wake wa ndoa…vijana wangu walijaribu
kulifuatilia, lakini si unajue tena, hizo ni kazi zenu,tunaogopa kuwaingilia,
ila yaonyesha kuna mgongano kati ya mke na hiyo nyumba ndogo…. je hiyo nyumba
ndogo mumeshaipata….’nikasema na kuuliza
‘Huyo mdada katoweka,….’akasema
‘Katoweka , kwa vipi…?’ nikamuuliza
‘Kiukweli,…kwa hivi sasa haijulikani hasa wapi alipo…na
tumekuja kugundua kuwa nyumba mbili alizokuwa akizimiliki keshaziuza...na
nyingine bado zinatafutiwa soko na madalali….’akasema mpelelezi
‘Haiwezekani..mbona vijana wangu hawajaniambia hilo…na je
Dalali analifahamu hilo…?’nikasema na kuuliza
‘Ni siri kubwa sana, Dalali hajalijua na kama anajua basi
itakuwa ni siri kubwa kwake…nahisi vijana wako hawajakuambia kwenye simu…lakini
kwenye ripoti yao utaliona hilo,…’akasema
‘Sizani kama madalali wenzake wanaweza kuifanya hiyo kazi
bila jamaa kufahamu…..’nikasema
‘Tutaliona hilo kesho, ….unafikiri nyumba hizo zimeuzwa
zamani…ni jana tu , na muda huo dalali alikuwa na wewe huko…na ….’akasema
‘Na kwanini huyo mdada atoroke….unahisi kafanya utapeli,
kumtapeli mwenzake…?’ nikauliza
‘Huyo mdada katoroka usiku…nahisi na gari la kukodi,…asubuhi
vijana walipofika waliambia huyo mdada kaenda site…kuna sehemu walikuwa
wanajenga….wakafika huko, wakaambiwa kaenda kununua vifaa vya ujenzi…huko
kwenye vifaa vya ujenzi wakaambiwa kweli alifika…lakini kaenda kutafuta vifaa
vingine…aliweka alibi ya hali ya juu….’akasema
‘Una maana gani kusema hivyo….?’ Nikauliza
‘Ina maana aliweka ushahidi ambao ulionyesha kuwa yupo…kumbe
yupo njiani anasafiri….na hakuna aliyejua kuwa katoroka hadi ilipofika jioni
hii,….’akasema
‘Sasa atakuwa wapi, na kwanini atoroke…?’ nikauliza
‘Kwa uchunguzi wa haraka,yawezekana atakuwa kavuka mipaka
yupo nchi ya jirani, ambapo ndio asili ya mzazi wake mmoja, yeye mzazi wake mmoja sio asili ya Tanzania,…lakini yote tusubirie
hiyo kesho, Dalali anaweza kulifichua hilo ukimbana vyema…’akasema na
alionekana anataka kukata simu, lakini mimi nikamuwahi kwa swali;
‘Kama nyie mumeshindwa na ndio kazi yenu mimi nitawezaje…?’
nikauliza
‘Sisi hatujashindwa…ila bado wakati wetu, tukitaka ataelezea
kila kitu, kwa hiari yake au kwa nguvu ikibidi,…lakini kwanza tunampa
muda,…tuone lengo lake ni nini…wewe uhakikishe umefika hiyo kesho kituoni…, na
mjane atakuwepo pia…’akasema
‘Kwani na yeye ana umuhimu gani kuwepo, naona kama
tutamsumbua tu, au….?’ Nikauliza
‘Anahitajika kwa matakwa ya Dalali, ni dalali mwenyewe
kahitajia anataka shemeji yake awepo pia,…’akasema.
‘Kwahiyo itakuwa ni siku ya hukumu au..’nikasema na
mpelelezi akaguna na kusema
‘Mhhh..naona ni siku
kabla ya hukumu..’akasema na kukata simu.
NB: Je kulikoni, mara nyumba ndogo…ina nini hii…je dalali
analifahamu hilo….ngoje tuone sehemu ijayo!
WAZO LA LEO: Kuna tabia ya mtu akishafanikisha lengo lake,
hata kama anajua ni la uwongo, lakini ili kuhalalisha pato lake hilo…au kile
alichokifanya, iwe ni madaraka, mali…au jambo lolote, mtu huyo, atatafuta
vipengele, viwe vya kisheria au hata maandiko ya vitavu vitakatifu…kuhalalisha
dhuluma yake…anajipa matumaini…, ili tu ajiweke kwenye uhalali. Kiukweli tunajidanganya,
dhuluma ni dhuluma tu, na tunachofanya ni kujidanganya wenyewe, lakini sio
muumba wetu. Ipo siku tutaumbuka tu!
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment