Dalali alipopigiwa
simu aliomba akaisikilizie hiyo simu nje, lakini mpelelezi akamuagiza aisikilizie
humo homo ndani au amwambie huyo aliyempigia wataongea baadae , dalali akaizima simu yake, na kitendo hiki kilimfanya
mpelelezi ashuku, ahisi kuna jambo….na mpelelezi huyu akasimama na akawa kama
anamuendea huyo dalali….
Tuendelee na kisa
chetu…
**********
Mpelelezi aliposimama , dalali akahisi huyo mpelelezi
anataka kuja kwake, …alichofanya ni kuweika ile simu yake kwenya mfuko wake wa
suruali, akawa anamuangalia mpelelezi anataka kufanya nini, akatabasamu, na
kusema;
‘Huyu ni mmoja wa wateja wangu…nitaongea naye baadaye, naona
tuendelee tu…’akasema
‘Tafadhali naomba hiyo simu yako….’akasema mpelelezi
akimkazia macho
‘Unaomba simu yangu ! Aaah, mkuu, ya nini, na kwanini, …si
unayo simu yako, huna salio au…?’ akauliza.
‘Ninaomba kikazi, sio swala la salio…ninataka kuhakiki jambo linahusiana na kesi yangu, …’akasema
‘Afande hapana, humu kuna wateja wangu , na sio vizuri
kuwatangaza kwa watu, si unajua masharti na mikataba, ….unielewe afande…’akasema
akitikisa kichwa kukataa.
‘Nakuelewa sana, na mimi sina nia hiyo ya kuwatangaza hao
wateja wako wau siri zako…, kuna kitu nahakiki mara moja halafu nitakurejeshea,
usiwe na wasiwasi…’akaambiwa
‘Hapana afande, haiwezekani,…siruhusiwi, sio haki, hapana,
siwezi….’akasema
‘Kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa, nina haki ya kuchunguza kila ninachoona
kinahusikana na kesi ninayoifuatilia…,ili
tusipotezeani muda, nipe hiyo simu yako….’akaambiwa, na Dalali akaona sasa hali
sio shwari,kwanza akajifanya anataka kuitoa, halafu akageuka kuniangalia mimi.
‘Uliuliza swali gani vile..’akasema akijipapasa mfukoni.
‘Nipe hiyo simu yako…’ilikuwa sauti nzito ya mpelelezi, sasa
akiwa kabadilika.
‘Afande nitakupatia, usiwe na shaka,…unafikiri, mimi sina
shaka ila sizani kama ni sahihi…’akasema Dalali, na sasa akawa anaitoa
mfukoni,.
‘Mimi nafanya kazi yangu, …’akasema mpelelezi
‘Unajua afande sikuelewi, badala ya kufanya kazi yako kazi
uliyoagizwa ya kumfikisha huyu tapeli kituoni, unaingilia mambo mengine, wewe
unamsikiliza huyu tapeli, nilikuambia awali kuwa huyu ni mjanja, naona …keshakuhadaa
..’akasema
‘Kama unajiamini kuwa huna makosa, nipe hiyo simu, kuna kitu
naangalia, kama hakuna kitu
nitakurudishia, na unavyozidi kuchelewesha kunipatia hiyo simu ndivyo
unavyonipa mashaka…..nipe hiyo simu….’akaambiwa na sasa alikuwa keshaitoa na
vidole vikawa vinahangaika kutka kuzima, lakini mpelelezi akaiwahi kuichukua
mkononi mwake.
‘Usiwe na shaka…’akasema mpelelezi,na ile simu sasa ilikuwa
mkononi mwake, na mara ikaanza kuita tena…, na mpelelezi akaitupia jicho na
kuona jina la huyo anayepiga simu, akaminya kitufe cha sauti ya spika ya nje kwa
haraka, halafu akabonyeza sehemu ya kupokea na kunyosha mkono kumkabidhi
Dalali.
‘Pokea hiyo simu yako…’akaambiwa,
‘Haina haja ,…’akasema na mara sauti kubwa ikaanza kusikika,
huyo mpigaji akaanza kuongea kwa sauti kubwa na kwa hasira.
‘Wewe Dalali...kwanini hupokei simu yangu, unajua nipo wapi
mimi…natafutwa na polisi, kwa ajili ya taama zako,sasa sikiliza…unisikilize kwa
makini…usinihusishe na mambo yako tena, na ole wako unitaje, umenielewa,…nitakupigia
tena baadaye…’akatulia
‘Umenisikia…?’ sauti ikauliza na mara simu ikakatika
Mpelelezi akamuangalia Dalali,..Dalali, kwanza alitulia tuli
kama aliyemwagiwa maji, akajikuna kichwa, halafu akawa kama anataka kupiga simu,
halafu akasita na kusema ;
‘Huyu mtu mpuuzi tu…naona labda kaharibu mambo yake, unajua
hawa wataalamu wakati mwingine wanaweza kuchanganya wateja wake, sizani kama
alikuwa anataka kuongea na mimi, ngoja nitaongea naye, …unajua mimi
sijamuelewa, …nitaongea naye…’akasema
‘Lakini kakutaka Dalali,ina maana alikuwa anauhakika
anaongea na wewe…’akasema mpelelezi
‘Nitaongea naye, nitajua anataka nini...ila kuna kitu naona
ni muhimu kwasasa, unajua ili mnielewe na ili mambo haya yawe kisheria, mimi naona wakili wangu awepo, maana nyie watu
siwaelewi, haya maswali yenu yaannitia mashaka….’akasema
‘Wakili wako wa nini…kwani unahisi una kosa?’ akauliza mpelelezi
‘Maana maswali yenu yananipa mashaka, mnakuwa kama
mnanishuku jambo, na mimi sina makosa, na mnaweza kunitega jambo nikaongea bila
kujielewa….’akasema
‘Mimi ninahitajia kuhakiki kesi ya kaka yako ili nifunge
jalada lake, hilo linakupa mashaka, mashaka gani?’ akaulizwa
‘Ni maswali ya huyu mtu tapeli, mimi nilitarajia ungemuhoji
yeye, au uondoke naye, sasa naona unazidi kumchelewesha au kuna kitu….’akasema
akiniangalia mimi
‘Sawa endelea naye malizana na maswali yake, ili tuendee na mimi,…’akaambiwa.
Mara simu yake ikawa inaita tena,…akabakia kimia, na
mpelelezi akasema
‘Pokea simu yako, sogea pale uipokee, ukumbuke nilikuja hapa
kuja kukuhoji wewe, na sio kuhusu huyu mtu wa mitandao…., tatizo la huyu ni
jambo jingine kabisa…’akasema na jamaa akaichukua simu kutaka kuipokea na sasa
akasogea pembeni, akaanza kuongea kwa sauti ya chini, alishasahau kuwa
mpelelezi alikuwa kabonyesha kitufe cha sauti kubwa.
‘Mtaalamu kakamatwa na polisi sasa hivi, na anavyoonekana
keshakutaja kwahiyo sisi tunahitaji malipo yetu sasa hivi, maana naona dili
yako umenuka…’sauti ikasema
‘Unasemaje, kakamatwa, poa nimekuelewa….nipo kwenye kikao
nitakupigia…nini…unasema nini malipo, malipo gani, nitaupigia baadaye….’akakata
simu, na kubakia amesimama, kawa kuduwaa kama anawaza jambo, na mpelelezi
akamuendea, na kunyosha mkono.
‘Hebu nipe hiyo simu yako…nitakaa nayo,….’akaambiwa
‘Itakusumbua bure, huoni watu wanapiga simu mara kwa mara,
kwanza simu yangu ina nini afande …’akasema
‘Sikiliza mimi nipo
kazini, na tendo lolote utakalolifanya kuanzia sasa litachukuliwa kama kitendo
cha kunizua nisifanye kazi yangu. Sogea ukae pale ,umalizie maswali yako na
ndugu hapo,…ukimalizana naye nitakuuliza maswali yanayohusiana na kifo cha kaka
yako …’akaambiwa
‘Afande, kaka yangu alifariki kwa ajali hilo lipo wazi, lakini
anyway, mimi siogopi maswali yako,
hawa watu nia yao ni kuniharibia, sijui
wana mashaka gani na mimi na hili nitalimaliza tu, ….’akasema
Na mara simu yake ikaita tena,….mpelelezi akaangalia
mpigaji, akaoa jina limeandikwa,….’mtaalamu’ akanyosha mkono kumkabidhi dalali huku
akibonyeza kitufe cha kuweika hewani, na sauti ikasemai;
‘Haloooh, dalali…’sauti ikasema mpelelezi akamsogezea Dalali
mdomoni, na kumuashiria aongee
‘Unataka kusema nini…tutaongea baadaye sasa nipo kwenye
kikao, unasikia nipigie baadaye ….’akasema dalali na sauti ikasema
‘Ni hivi , nimeshakamatwa na polisi, sasa sikiliza….unasikia,
niipate pesa yangu kama ulivyoniahidi, na kesho, sijui kama itawezekana kuhusu
huo mnada ulioniambia, uhakikishe sehemu ya mshiko wangu naipata, vinginevyo,….
na mbona sauti ya simu yako ipo hivyo,nasikia sauti mbili mbili…unajifanya
mjanja eeh, unanirekodi, mpuuzi mkubwa wewe….’akakata simu.
Mimi nilibakia kimia, nikiangalia hayo yanavyoendelea,
nikageuka kumuangalia mama mjane,ambaye alikuwa akimuangalia shemeji yake anavyohangaika
na simu naona sijui kama alikuwa akimuonea huruma shemeji yake au alikuwa naye
akimuhisi vibaya, na alionekana kutaka kusema neno lakini sauti ilikuwa
haitoki, akabakia kaduwaa tu.
‘Haya maswali yaendelee…’akasema mpelelezi
********
‘Dalali, tuendee na
maswali yetu,..’nikasema
‘Maswali gani ,mimi nimechoka na maswali yako ya kujirudia
rudia,… naona wewe ni kama unanishuku jambo, na mamabo ya shakashaka kwangu
sitaki, sasa mimi naona twende kisheria, nahitajia wakili wangu awepo…’akasema
‘Haya ni maswali ya kuhakiki, …uhalali wa hilo deni, hayajakushuku
jambo, kwanini unaanza kujihami, nia yanu, ni kutaka kuhakiki kama kweli hilo deni llilikuwa deni la kaka yako au la….vinginevyo
useme ukweli tu tumalizane…’nikasema
‘Nisema ukweli upi,….nimeshakuambia hilo deni ni la kaka
kama huamini nenda huko benki ukawaulize….’akasema
‘Nilikuuliza hilo
deni la pili, ulilichuukua kwa makubaliano gani,…tuangalie taratibu za benki
zilivyo…wewe ulifika ukaonyesha barua kuwa wewe ni msimamizi….na wakaja kusema
huwezi kuchukua pesa kwasababu kuna deni..si ndio hivyo kutokana na kauli yako ya kwanza au sio…?’
nikamuuliza
‘Sasa kuna tatizo gani hapo…ndio unataka kusema nini ?’
akauliza
‘Kiutaratibu wewe bado ulikuwa hujawa signatory..ulitakiwa kwanza ujaze fomu ya kuwa signatory, na taratibu hizo zinachukua muda, sio kitu cha siku
moja,…ilikuwaje wewe wakakubalai kwa siku moja tu..’nikasema na kumwangalia
mpelelezi kama amenielewa hapo.
‘Na pili ni kwanini kwanza wakimbilie kukuambai kuwa hakuna
pesa, kabla hawajakuambia kuwa mbona wewe sio mwenye akaunti umenilewa mashaka
yangu hapo, iweje siku ya kwanza tu
uanze kuchukua pesa.. ukimbilie kuchukua pesa, na benki wakimbilie kukuambia
kuwa hakuna pesa kuna deni, hebu tuambie hapo..?’ nikamuuliza na hapo akawa
kama kashituka, akacheka kidogo na kusema;
‘Nimeshakuambia, tulikuwa na shida ya pesa, kwahiyo mimi
nilipofika tu na kuwaonyesha zile nyaraka, kuwa mimi ndiye msimamizi wa malipo,
nikawa nimeshajaza tayari karatasi ya kuomba kulipwa kiasi fulani cha pesa
nilijua hili laweza kufanyika tu, huku wanaendelea na mambo yao mengine…sijui hayo mambo yako ya signatory… …’akatulia
‘Kwahiyo kwanza kabisa ulijaza fomu za kuchukua pesa…hata
kabla hujakubaliwa kuwa wewe ni signatory….si
ndio hivyo?’ Nikamuuliza
‘Ndio kuna ubaya gani hapo, usitake na wewe kunichanganya,
nilijaza vitu vyote kurahisisha kazi…’akasema kwa hasira
‘Ulipojaza hiyo fomu ya kuchukua pesa ….uliweka sahihi yako
au sio…?’ nikamuuliza
‘Hahaha…sasa ningeliweka saini ya nani, mimi ndiye nachukua
pesa ningeweka saini ya nani, kwa vipi kwanza, hebu hebu fafanua swali lako
unataka nini hapo….’akasema sasa akitoa
simu nyingine akitaka kumpigia mtu.
‘Wewe uliweka saini yako, na unajua kabisa kuwa kabla ya
kuchukuliwa pesa mlipaji hulinganisha sahihi yao na ile ya kwenye karatasi ya
maombi…ndio maana nakuuliza wewe uliweka sahihi yako…?’ nikamuuliza
‘Ndio niliweka sahihi yangu yangu na nikiwa na kila kitu tayari, na ukumbuke
nilikuambia nilishaongea na meneja,…sasa hayo mengine ni juu yao
kunifahamisha….’akasema
‘Benki walikuwa bado hawajakukubalia wewe kuwa ni signatory…
huwezi kuchukua pesa..?’ nikamuuliza
‘Waliniambia siwezi kuchukua pesa kwasababu kuna deni, hiyo
ni kauli yao ya awali….’akasema
Na wakati huo ulikuwa umeshajaza fomu, ukawaomba, na unasema
wao wakasema hawawezi kukuruhusu pesa kwa
vile kuna deni …lakini hawakukuambia mbona sahihi yako na ile ya mwenye akaunti
hazifanani,….na bado wakakukubalia kuchukua deni jingine,…na bado hujawa signatory… hebu elezea hapo tukuelewe.?’
Nikamuuliza
‘Sasa hapo kuna tatizo gani, ..wakati nina kumbukumbu za
kuniidhinisha kuwa mimi ndiye nitakayesimamia kila kitu cha marehemu, na kwenye
kumbukumbu hizi kuna sahihi yangu, hayo mengine ni juu yao, sio mimi…mimi sioni
mantiki ya swali lako…kabisa kabisa wewe unataka kunitega tu hapo….’akasema kwa
hasira.
‘Nakuuliza hayo maswali nikiwa na maana …tunachotaka ni
kuona jinsi gani huyo mtu aliweza kuchukua pesa kwa jina la kaka yako….unielewe
hapo, ili nijue hilo ni lazima nianze na wewe…kwani wewe kwanza ulikuwa mtu wa
karibu kwa kaka yako….sasa…iweje...’akanikatiza kwa kusema
‘Sikiliza, hakuna mtu mwingine alichukau hizo pesa, hilo
ondoa akilini mwako, hakuna…usitake kutunga kitu ambacho hakipo…kama hawa
wapuuzi wengine wanafikiri watanifanya nibabaike, ….sina wasiwasi, maana sina
kosa…’akatulia kidogo halafu akaendelea kusema.
‘Wapuuzi gani…?’ nikamuuliza
‘Wewe uliza maswali yako….mimi nashughulika na mambo mengi,
na akili yangu inafanya kazi ..huwezi ukanichanganya…nina uzoefu wa kudili na
watu zaidi ya kumi, sibabaiki…endelea ,,’akasema akijifanya anajiamini.
‘Shaka yangu ni jinsi ulivyoweza kukubaliwa kwa siku moja,
wakati hujawa signatory…na ni kwa vipi wakimbilie kukuambia hakuna salio, ni
kipi kilitangulia, unasema walianza kukuambia hakuna salio…lakini hawakusema
mbona sahihi hazifanani…na mwenye akaunti…’nikasema
‘Sasa labda niseme ukweli, maana mambo mengine unataka wewe
mwenyewe uelewe tu…tulikuwa tumekwana sana, mimi sina kitu muda huo,…unajua
kazi zangu sio za moja kwa moja kupata pesa, kuna muda unakuwa kwenye hali
mbaya kweli, …ni muda huo nilikwama kweli…kwahiyo mimi Ilibidi nipige
magoti,…sasa ningefanyaje, shemeji anaumwa, na anaumwa kweli,sina pesa
ningefanya nini,…’akawa kama ananiuliza
‘Kwahiyo kupiga magoti kwako kukawafanya watu wa benki
wakiuke misingi yao…?’ nikamuuliza
‘Hapana sio hivyo…’akasema
‘Ni vipi….?’ nikauliza
‘Kupiga magoti ni kweli nilifanya hivyo, mbele ya meneja,
kwanza nilianzia kwa muhasibu….acha wee….ukitaka cha mvunguni sharti uiname….Kwahiyo
nilikwenda mpaka kwa meneja,…katika kuomba sana ndio wakanikubalia kuchukua
deni…na siri moja nikuambie, mimi
nikitaka kitu nitakipata tu, kwa njia yoyote…,si unajua bongo hii, siwezi
kusema yote, natumai umenielewa….’akasema kwa majigambo.
‘Yaonkena hivyo ukitaka kitu ni lazima ukipate,…..lakini mimi
bado hapo nina mashaka…bebu nikuulize tena hizo famu za kuchukua pesa uliweka
sahihi gani….?’ Nikamuuliza
‘Sahihi gani, kwa vipi, mbona unarudia rudia hilo swali,… si
nimeshakuambia ni ya kwangu..sahihi ina nini sikuelewi.?’ Akauliza kwa hasira
kidogo, halafu akawa kama kushituka kidogo.
‘Benki ili uchukue pesa sahihi ni kitu muhimu sana, sura
yako na kaka yako mnafanana sana…lakini sahihi sizani kama zinaweza kufanana au
sio…na benk wanalinganisha sahihi yako na ile iliyopo kwenye kumbu kumbu zao,
wewe ulikuwa hujakubaliwa kuwa signatory iweje wakukubalie, iweje wasikuulize kwanza
kuhusu maswala ya sahihi….?’ Nikamuuliza
‘Unajua maswali yako sikuelewi…kama meneja wa benki
keshakubali, hawa wa chini wa naini, waliniruhusu, kwasababu kumbukumbu za hizo
fomu zilikuwa mikononi mwake, keshaona sahihi yangu mle, yeye ni kutoa maagizo
tu, kinafanyika, sasa tatizo lipo wapi hapo…’akasema
Ok,…kwenye huo mkopo,…si umesema ulikubaliwa sasa uchukua
kama mkopo, na mkopo unahitajia mlolongo wake, huo mkopo uliuandikaje, kama wewe au kama familia husika?’ nikamuuliza
‘Kama familia husika,mimi ningechukuaje kama mimi, ….ila kwa
vile mimi sasa ndiye mwenye dhamana, ndiye nimepewa mamlaka ya usimamizi wa hii
familia, kila kitu kiliandikwa kwa jina
langu, …’akasema
‘Kwenye hiyo fomu,…kwa ajili ya huo mkopo, je, ulijaza kuwa wewe peke yako ndiye unawajibika
na huo mkopo kwa vile wewe ni signatory,au pamoja na mtu mwingine?’
nikamuuliza
‘Hapana,we-we-we…mhh,hilo ni deni bwana, ….niliweka na mtu
mwingine, nilimweka na shemeji…’akasema na shemeji yake akainua kichwa
kutuangalia lakini hakusema neno
‘Lakini shemeji alikuwa anaumwa au sio….?’ Nikamuuliza
‘Ilibiidi nimuweke tu, ukumbuke tangu mwanzoni yeye alikuwa
kawekwa na mumewe kwenye hiyo akaunti yao, na mimi nilifuata hivyo hivyo…
lakini katika maelezo ni kuwa yoyote kati yetu anaweza kuchukua pesa, ila …kuwe
na barua ya makubaliano kama kuna tatizo, kwahiyo kilichogomba kwa muda ule
ilikuwa ni sahihi ya shemeji…’akasema
‘Ndio maana nauliza je kwa muda huo shemeji alikuwa anaumwa, angewezaje kuweka sahihi yake..?’
nikamuuliza, akasita kidogo, halafu akasema;
‘Kulikuwa na muda shemeji
hali yake ilikuwa inajirudi, anaweza….kujitambua, unajua alikuwa ..akili
inafanya kazi,ila viungo, kwa sehemu kubwa ilikuwa haifanyi kazi,mwili ulikuwa
hauwezi kujiinua, lakini muda mwingine alikuwa
akiongea kwa shida,…kwahiyo hapo
ndio aliweza kuweka sahihi yake,…, …’akasema
‘Hapo sijakuelewa, kuna muda alikuwa anaweza kujitambua, ina
maana ulipochukua hizo fomu, ulisubiria mpaka huo muda ufike au sio, ndio ukamwambia shemeji akusainie..si
ndio hivyo au?’ nikamuuliza. Akahema kwa muda kama kuchoka na maswali yangu, kama
nampotezea muda wake, akasema;
‘Hivi kwanza….hebu nikuulize
na wewe ni kwanini unaniuliza maswali yote hayo, unataka kuhakikisha nini…kuwa huniamini, ukumbuke mimi mdogo wake marehemu,
…mimi ni mzazi wa hii familia nina uchungu zaidi ya huyu shemeji…’akatulia
akinikodolea macho.
‘Kwani una wasiwasi
gani…ni maswali tu ya kuhakiki , inawezekana ulifanya makosa bila kujua ?’
nikamuuliza
‘Mimi nimechoka na maswali yako, ya kujirudia rudia, na
yananilenga mimi kama mkosaji vile, badala ya kuulizia benki kama unakuja
kuniuliza mimi, kwangu utakuwa unapoteza muda wako, mimi najua ni nini ninachokifanya,
sio zezeta mimi, ….’akaangalia saa yake, halafu akamuangalia mpelelezi, akasema
‘Sasa mimi nataka
kuondoka, mukitaka zaidi utaniita huko jela,…au kituo cha polisi, unampeleka
wapi huyu tapeli, maana hana jipya,…’akasema akimuangalia mpelelezi.
‘Kwani amemaliza kuuliza…?’ akauliza mpelelezi na kumfanya
jamaa atoe jicho la kushangaa, halafu akageuka kuniangalia mimi, na mimi
nikamuuliza
‘Mimi nazungumizia hili deni jipya, na wewe ndiye
uliyechukua hizo pesa au sio, …sasa kwanini nikawaulize benki,….tuendelee , umesema
ulipofika benki kuchukua pesa ndio ukagundua hilo deni, sawa si sawa..?’
nikamuuliza
‘Nimeshakujibu hilo swali, siwezi kukujibu tena..’akasema
‘Na akaunti iliyotumika ni ya mume na mke, ya kuwa mume
hawezi kuchukua pesa mpaka mke aweke sahihi yake, sasa wewe ukapewa majukumu ya
kuchukua pesa, ina maana mlifanya utaratibu na benk mkapeleka nakala za mirathi
kuwa wewe ndiye utakuwa unachukua pesa, je katika makubaliano hayo na
benki …’nikatulia nilipomuona akishika
shika simu yake,
‘Unajua wasi wasi wangu , ni jinsi gani shemeji yako
alivyoweza kuweka sahihi yake na wakati yeye alikuwa mgonjwa, je sehemu hiyo ya
mke ilikuwaje,….ulisubiriaje mpaka aweze kuweka sahihi na wewe ulisema ulikuwa
unahitajia pesa kwa haraka,walitoaje pesa wakati sahihi ya shemeji yako ilikuwa bado…?’
nikauliza
‘Nimekuwambia japokuwa alikuwa anaume kuna muda alikuwa na
hali nzuri ya kuweza kuweka sahihi sasa mengine sijui , nenda kaangalia kama
hakuweka sahihi yake,… na au muulize…’akasema na kumgeukia shemeji yake.
‘Na je wewe ulimwambia
hiyo sahihi ni ya nini ?’ nikamuuliza
‘Kiukweli….unajua mambo mengine niliyaacha tu, sikutaka
kumwambia shemeji, ….na pesa tunahitajia, kwahiyo,sikumwambia shemeji kuwa hizo
fomu ni kwa ajili ya deni, niliogopa
kumshitua, nilimwambia ni ili tuweze kuchukua pesa ya matumizi…’akasema
‘Kwahiyo yeye hakuweza kuuona huo mkataba wa kuchukua mkopo,
yeye hakuweza kusoma kilichoandikwa na wala hukumsomea, wewe ulimuonyesha tu
sehemu ya kuweka sahihi,….?’ Nikamuuliza
‘Ndio nilifanya hivyo, kuogopa kumshtua…’akasema
‘Na kwenye huo mkopo mpya, nyumba pia iliwekwa kama dhamana…?’ nikamuuliza na
ilikuwa kama nimemzaba kibao usoni, akabadilika usoni, akasema.
‘Unajua unielewe….huomkopo ni muendelezo tu, kwahiyo mambo
mengine yalikuwa yale yale..’akasema na simu yake ikaita tena, alikuwa nayo
mpelelezi, mpelelezi akaiangalia na kufanya kama awali, na Dalali akaipokea na
kuangalia mpigaji, akasema;
‘Huyu mtu ana nini na mimi, oh, sio yeye ni….’akasema akiwa
anasita kupokea
‘Pokea…’akaambiwa na
kwanza akataka kuminya sehemu ya kuzuia sauti na mpelelezi akasema
‘Pokea kama ilivyo…’akaambiwa, na mpelelezi akasogea na
kubonyeza sehemu ya kupokea.
‘Mpenzi, wangu, vipi, mtaalamu kapiga simu, anasema atakachokufanya
hutamsahau, unamfahamu huyo mtu alivyo, kwanini humalizani naye, unajua bila
yeye usingafanikiwa, mpe pesa yake, au
na huo mnada ni keso au sio, …?’ akauliza mkewe
‘Achana naye, nitakupigia nina maswala mengine muhimu,
unasikia nitakupigia….’akasema na sauti ikauliza tena
‘Huo mnada upo au haupo….?’ Akauliza
‘Nitakupigia,…..’akasema akitaka kukata simu
‘Ukitoka huko uje, kwani
kuna wapelelezi wamefika wamenihoji kuhusu nyumba na …..’dalali akakata
simu simu akitamka neno
‘Wapelelezi…mhh’akasema na kuguna
‘Kwanini unakata simu, huoni kuwa angekupatia jibu ya swali
unalojiuliza mwenyewe …?’ akauliza mpelelezi na jamaa akawa kaduwaa, naona sasa
alihisi mambo yanamwendea kombo, akatikisa kichwa kama kuondoa kitu.
‘Swali, swali gani…huyo mwanamke anatupotezea muda ,
tuendelee naomba tufanye haraka naona nina mambo mengi ya kufanya….’akasema
‘Huyo ni nani, nyumba ndogo…?’ akauliza mpelelezi
akitabasamu. Na jamaa aliposikia hivyo na yeye akajilazimisha kutabasamu na
kusema;
‘Ndio maana nimekuambia hiyo ni simu yangu ina mambo yangu
binafasi, halafu afande, wewe unataja nyumba ndogo wakati shemeji yangu yupo hapa
anasikia,..’akasema kiutani huku akitabasamu akimwangalia shemeji yake ,
shemeji yake alikuwa kama hayupo, alionekana kazama kwenye mawazo huku sasa akiwa kaangalia nje.
‘Hiyo nyumba anayoishi huyo mpenzi wako, umemjengea wewe…?’
akauliza mpelelezi na jamaa akajibu kama anashtuka akasema;
‘Nani kasema hivyo…?’ akauliza akikunja uso kuonyesha
halitaki hilo swali, akageuka kumwangalia shemeji yake na shemeji yake sasa
alikuwa akimtizama kwa haraka akakwepa kumuangalia na akaweka mikono yake mbele
kama anaomba akaipuliza na akageuka kumuangalia mpelelezi, lakini hakusema kitu
na mpelelezi akasema;
‘Jibu swali….’akaambiwa na simu ikaita tena, akaangalia
mpigaji ni nani, akaona jina
‘Mtaalamu…’ akataka kuminya sehemu ya kukata, lakini
mpelelezi akamzuia na mpelelezi akaminya sehemu ya kupokea,…..sauti ikaanza
kusema;
NB: Mambo yanazidi kujileta, je simu ya pili inasemaje
WAZO LA LEO: Hata
tujifanye wajanja wa kuongea, wajanja wa kudanganya, wajanja wa kupata vitu
visivyo halali, tusisahau kuwa waliodhulumua wanalalamika, na wengine
wameshashitaki kwa hakimu wa mahakimu, ambaye anajua kila kitu, na kwahiyo hata kama tumepata kipato hicho sumu, ambayo
itakutafuna kidogo kidogo na muda ukifika, ni majuto. Ewe mja tubu dhambi zako,
acha hiyo tabia, dhuluma ni mbaya sana.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment