Mara mpelelezi akaingia… cha ajabu sasa alipoingia alikuwa
kashikilia pingu mkononi, ….akawa
anatembea mwendo wa hatua za kuhesabu, akinijia mimi, pale nilipokuwa
nimekaa, akilini nikawa najiuliza kuna nini, nikakumbuka yale maneno ya jamaa wakati
akiongea na shemeji yake alisema;…
‘Nilijua tu…hawa ni matapeli, sasa ngoja
waionje joto ya jiwe….shemu usiwe na wasiwasi, hawa sasa hivi wanakamatwa, wewe
utaona tu…
Yule mpelelezi akawa sasa kanifikia pale nilipokuwa …., na
akawa ananiangalia kwa jicho la kujiuliza, yaonyesha , kwa jinsi nilivyomuona
alikuwa akishindana na dhamira, inawezekana kitendo hicho anachotaka kukifanya
kilikuwa hakimpendezi au hana uhakika nacho, au…, lakini hana budi,… akawa sasa
keshanifikia lakini alikuwa hajatamka neno,nikajua sasa kuna tatizo…
Tuendelee na kisa chetu
************
‘Vipi afande mbona unanijia na pingu mkononi…?’ ikabidi
nimuulize mimi kwanza kwani niliona kusubiria kunanitesa zaidi.
‘Nilijua tu…’sauti ikatoka kwa jamaa yetu dalali, akiwa na tabasamu tele mdomoni.
Mpelelezi likuwa keshanifikia akawa kasimama akiniangalia; Yule mama mjane
akawa naye kainua kichwa anamuangalia huyo mpelelezi kwa macho ya mshangao!
‘Kwanza nikuulize hii kazi unayoifanya una kibali nayo…?’
akaniuliza yule mpelelezi.
‘Afande si unajua kazi yangu, kazi kama hizi ni za kujitolea
tu, …mara nyingine hazihitaji kibali, mimi nikiona jambo linaigusa jamii, huwa
nalifanyia kazi na nikipata ushahidi wa kutosha naukabidhi kwa polisi, na mara nyingi imekuwa hivyo, na nia yetu ni
kuhakikisha tunasaidia jamii , na haki itendeka…na
sisi tumegundua kuwa hapa kuna tatizo, kuna dhuluma inataka kutendeka, ….’nikasema
‘Dhuluma gani wewe, hakuna dhuluma yoyote hapa, …muongo huyo
afande…ni tapeli huyu.’akadakia jamaa akinionyeshea mkono.
‘Kwanza afande nikuulize kuna nini cha ajabu…?’ nikamuuliza
‘Kwa amri ya wakubwa zangu, wewe umeingilia amri halali ya
mahakama, na umejaribu kuvuruga ukweli, na kuleta mtaharuki ….umejenga fitina
kwenye jamii, na nimeamuriwa ni nikukamate, na mengine utaambiwa huko kituoni,…kazi
yangu ni hiyo kwasasa,…kuna watu wanahusika na hilo,… kwahiyo upo chini ya
ulinzi…’akasema akiwa kashikilia pingu yake.
‘Nimeingiliaje amri ya mahakama!….hebu lifikirie hilo, mimi
nimefanya kosa gani kwa hivi sasa la kuingilia amri ya mahakama?,..Sisi tumeliona
hili jambo lina utata, na tunahisi kuna tatizo, ndio tukawa tunautafuta
ushahidi, tena kwa njia halali, ya kuulizana maswali….hatujatumia nguvu yoyote
kuzuia amri ya mahakama, na kuja kwangu hapa sikuwa nimepanga,sikuwa nimelifahamu
hili, imetokea tu…..je kuwasaidia wajane na mayatima ili wapate haki zao ni
kosa?’ nikauliza
‘Afande huyo mwongo, tangia afike hapa imekuwa ni
balaa….mtoto anateseka kwa ajili yake, …maana hilo tulishaliweka sawa, ikawa
haitokei tena, mtoto akawa hana tatizo tena, sasa huyu kaja, kaanzisha balaa,mtoto anaumwa, muulize
mama yake….’akasema akimuonyeshea shemeji yake.
‘Muulize, … kisa eti anatafuta ukweli, ukweli gani ambao
nyiewatu wa usalama mumeshindwa kuupata, anainglia kazi zenu, …huoni huyu ni
tapeli, mwongo…ana lake jambo…’akasema jamaa na mpelelezi akawa hamuangalii
yeye, alikuwa akiniangalia mimi tu,na kwa upande nilimuona Yule mama mjane
akiwa kaduwaa, japokuwa alikuwa na machozi machoni.
‘Ilivyo ni kuwa umekiuka amri halali ya mahakama, kwasababu ilishahukumu kuwa nyumba
hii ipo kwenye taratibu za mnada baada ya mahakama kurizika na ushahidi, kuwa kweli hilo deni lipo, na mwenye deni
aliweka nyumba hii kama dhamana,…na wenyewe wamekubaliana na hilo,..na huenda
ulishaambiwa yote, sihitaji kukufanulia, …na hukumu ikapitishwa kuwa nyumba hii
ipigwe mnada kwani mkopaji hana uwezo tena wa kulipa hilo deni…’akasema
‘Hebu nikuulize afande, huyo mkopaji ni nani na ni nani
alikubaliana na hilo kuwa nyumba ipigwe mnada?’ nikauliza
‘Kutokana na mahakama ni mwenye nyumba hii…’akasema
‘Ni nani…na huyo aliyekubaliana kuwa mnada uwepo ni nani?’
nikauliza
‘Hilo swali sio muhimu kwangu kujibu…ila kwa maelekezo niliyopewa
ni mwenye nyumba hii…’akasema
‘Ambaye ni marehemu au sio…sasa yeye alikubalije kuwa mnada
upigwe wakati ni marehemu?’nikasema kwa kuuliza
‘Awe ni marehemu, haijalishi, kwani wapo watu wanaoendelea
kumiliki hizi mali, sio kwamba mtu akifa basi kila kitu chake kimekufa, madeni
ni lazima yalipwe, hata kidini wanasema hivyo kama kuna mtu anamdai marehemu
ajitokeze, si ndio hivyo ?..........
‘Na jingine marehemu aliweka dhamana, na ujuavyo dhamana
inawekwa kwa mali zisizohamishika…unanielewa hilo…na taratibu zote za kisheria
zimefuatwa , sio kwamba ni maamuzi tu..na kosa lako ni kuwa, wewe umeanza
kuzikiuka, kutaka kuzuia…ni kosa au sio…’akasema
‘Sawa kabisa afande, nakubaliana nawe,maana …kutokana na
deni hilo kaka anatusumbua…mzimu wa kaka unatujia…., anatutokea kwa kupitia kwa
mtoto…na kama ulivyosema hata dini anasema deni ni lazima lilipwe sasa huyu
tapeli anajifanya anajua zaidi, ana lengo lake…..hebu muulize lengo lake ni
nini….ili upewe nini, na wakuruhusu apate kitu ni mimi, sasa nakuambia hapati
kitu hapa….’akasema huyo jamaa na mimi sikumjali nikaendelea kuongea na huyo
mpelelezi
‘Afande nikuambie kitu,…tuna ushahidi kuwa deni hilo sio la
marehemu, na kama marehemu angelikuwepo
hai, …hili deni lisingelikuwa lake huenda angelibambikiwa mtu mwingine hilo
tutalithibitisha, na ndicho nilitaka kukithibitisha hapa kwa kumuhoji huyu
mwenye mamlaka sasa hivi….’nikasema nikimuangalia huyo jamaa halafu nikamgeukia
mpelelezi na kuendelea kusema;
‘Hili deni lilikuwepo bila marehemu kufahamu na ilitakiwa
lijitokeze baada ya kifo cha huyo marehemu, aliyekuwa mume wa huyu mama, huyu
mama ana uhakika kabisa hilo deni sio la mumewe, kwani anamfahamu vyema,…, na
sijui… huenda hata hicho kifo kimepangwa, lakini hilo tutakuja kulijua baadaye
…’nikasema na jamaa akacheka kweli.
‘Hahahaha…..Unaona huyu mtu alivyomshirikina…ina maana kuna
mtu alijua kaka atakufa liini, …hivi kweli kuna mtu anaweza kujua mwenzake
atakufa lini, ….tena akiwa mnzima hana ugonjwa….?
‘Hahaha…hapo sasa unadhihiri uwongo wako, wewe kweli
umeshindwa hoja, utapeli wako hauna hata maana,…nilijua wewe ni mjanja, kumbe
ovyooo, haaaa, eti kifo kilipangwa, na
nani, nani ana mamlaka na mungu hahaha, unalo hilo…’akasema
‘Afande tulichogundua sisi kwa muda mfupi tu, hilo deni
limewekwa kwa marehemu kinamna, …hilo deni sio la marehemu,…nina ushahidi….unataka
nikuonyeshe….’nikasema na jamaa alishtuka kidogo halafu akacheka tena kicheko
cha dharau, na kusema;
‘Ni deni la nani, hizo hati aliweka nani sahihi , unasema
eti una ushahidi, hana lolote huyo, asikudanganye,…mwongohuyu…unajua wewe
unaongea tu bila kufikiria, ….ujue hilo deni lipo benki, ni nani anaweza
kuwadanganya benki…eti afande, hebu muulize huyu mtu, …. anafahamu taratibu za
benki zilivyo, hivi kweli hilo linawezekana….huyu ni tapeli, mpeleke
kunakohusika….’akasema.
‘Kwanini unaogopa nisiuonyeshe huo ushahidi…?’ nikauliza
‘Nionyeshe…kama utanionyesha mimi nipo tayari
kufungwa…’akasema kwa kujiamini
‘Nikuonyeshe ushaidi sio, ushahidi wa kwanza….’nikaanza
kusema na mpelelezi akanikatiza na kusema;
‘Sasa hivi hayo mimi siyajui, na hili la kukukamata wewe sio
kesi yangu…unajua tuna taratibu zetu, na moja ya taratibu zetu ni kutii amri ya
mkubwa wangu, na hili ni lazima lifanyike hayo mengine utayaongelea huko mbele
yao kwa muhusika, ….natumai unanielewa….’akasema mpelelezi sasa akinikabili.
‘Nakuelewa sana….lakini kwanza nina ombi kwako, mimi sikatai
kwenda huko polisi tutakwenda tu, lakini kwanza nina ombi….maana hilo linagusa
keso unayoishughulikia wewe…’nikasema
‘Afande usimsikilize huyo ni tapeli, anataka kutumia ujanja
wa kukulaghai, deni hilo lipo kweli….na
ni kutokana na nyaraka zilizopo benki,…hebu fikiria mimi ni ndugu yake,
nimelikubali…yeye huyu mtu baki ana
uchungu gani zaidi yangu mimi,..huyu , yeye anajifanya anajua sana, na nia yake
ni kuleta fitina na matatizo kwenye hii familia yetu,…kamwe
usimsikilize..’akasema jamaa na yulempelelezi hakumuangalia, alikuwa
akiniangalia mimi,akasema;
‘Una ombi gani….na ushahidi gani ulio nao amabo unaigusa
kesi yangu ninayoifuatilia?’ Akauliza
‘Nataka kwanza uniruhusu nimuhoji huyu mtu, kuna maswali
nilitaka kumuuliza kuhusu uhalali wa hilo deni, na yeye anaweza kunisaidia kwa
hilo,na hilo deni ndicho kisa cha hiyo kesi yako utakuja kugundua mbeleni.,
maswali yangu ni kutaka kujua ukweli,..akinijibu hayo maswali, basi tutaondoka,…’nikasema
‘Ni ushahidi gani ulio nao ….’akauliza mpelelezi
‘Mwongo huyo , hana lolote….’akasema jamaa
‘Nionyeshe au niambie huo ushahidi…’akasema mpelelezi
‘Ushahidi wa kwanza ni yeye mwenyewe….’nikasema na mpelelezi
kwanza akatulia akiwaza jambo halafu akauliza
‘Kwa vipi….?’ Akauliza huku jamaa anacheka kweli .
‘Haiwezekani mtu awe na uchungu na familia, awe na uchungu
na kaka yake, atokee mtu mwingine kutaka kusaidia kuupata ukweli, halafu yeye
awe mstari wa mbele kumpinga huyo mtu, huo ni ushahidi namba moja, tumie hekima
utaugundua…..’nikasema na huyo mpelelezi akaangalia saa yake, halafu akageuka
kumuangalia jamaa na jamaa alikuwa bado anacheka kwa dharau, na alipoona
mpelelezi anamtizama akatulia
‘Sawa….muulize hayo maswali…’akasema mpelelezi
‘Afande…huyu anasema nini,…eti mimi japokuwa ni ndugu lakini
sionyeshi uchungu…hata kama angekuwa ni mtoto wangu wa kuzaa kakiuka sheria
siwezi kuipuuza sheria, mimi tabia yangu ni kufuata sheria, na jingine ni muito
wa marehemu anataka deni lilipwe,…’akatulia
‘Afande…sasa kwanza amri ya mahakama, nitawezaje kuipinga,
pili muito wa kaka,….yote hayo yana uzito, ndio maana nikawa mstari wa mbele
kuhakikisha deni hilolinalipwa sasa kwa njia gani,…mimi sina pesa, shemeji hana
pesa, ulitaka tukaibe….huo ushahidi wako hauna mshiko….hahahaha.’jamaa akasema
.
‘Kama ni hivyo kwanini unaogopa kuulizwa maswali, ….?’ Akauliza mpelelezi
‘Sijaogopa kuulizwa maswali…unasikia afande, … lakini kwa
utaratibu gani, na kwa nani….huyu tapeli ndiye aniulize maswali,….mtu
anayekiuka sheria za mahakama… akama anataka kuniuliza aulize kwa utaratibu
unaotakiwa mimi nitamjibu kila kitu, sina cha kuficha, sina cha kuogopa….’akasema
‘Kwahiyo upo tayari kuulizwa hayo maswali na yeye…?’ Akauliza
afande,
‘Mimi nimesema hivi, kama ni kwa utaratibu unaokubalika,
mimi siogopi hayo maswali
yake..nimeshajua ni nini anakilenga, mimi ni mjanja, naona mbali, najua ana
duku duku gani siwezi kumlaumu, lakini wenzake walikuwa hivyo hivyo,
nikawaridhisha, benki wana kila kielelezo,sasa tatizo lipo wapi…., ila huyu mtu
anaonekana ni mjanja sana, ni tapeli aliyekubuhu…’akasema.
Yule mpelelezi akaenda kukaa kwenye sofa, na kusema ;
‘Haya kama huna kikwazo, na upo tayari kuulizwa hayo
maswali, ngoja tuyasikie, anza kumuuliza…’akasema mpelelezi, na jamaa kwanza
alionyesha uso wa kushangaa, na baadaye akajirekebisha. Huyu jamaa anajua kweli
kujiigiza…anabadilika kama kinyonga!
‘Afande…!’ akasema kwa kushangaa, na mpelelezi akawa kimia.
Sasa akaniangalia
akiwa na tabasamu la dharau mdomoni….akakunja nne, na mguu mmoja ukawa
unatikisa tikisa akinisubiria nimuulize maswali. Mimi nikagueza uso kumuangalia
shemeji, nilimuona bado analia, akilini nilijiuliza ni kitu gani aliongea huyu
jamaa kwa shemeji yake ambacho bado kina mliza mpaka sasa…huo unaweza
ukawa ushahidi mwingine.
Niligeuka kumuangalia jamaa yetu, alikuwa akiendelea
kuutikisa mguu wake akijifanya kama vile hana wasiwasi,…lakini kiukweli
hakuweza kunidanganya mimi. Hapo alipo
ana wasiwasi kibao ….
Mara simu yake ikaanza kuita, na kwa haraka bila kutazama
mpigaji akaipokea, yaonyesha kuna kitu alikuwa akikisubiria kwa hamu,
…akasikiliza, niliona uso wake ukibadilika, akamtizama mpelelezi kabla hajasema
neno, halafu akasema;
‘Una uhakika,…ndio nakuuliza una uhakika hayupo kwake, kaenda
wapi, ….?’ Akauliza na akawa anasikiliza halafu akasema;
‘Ndio….nimemtumia ujumbe wa maneno hajibu, nikampigia simu
yake, hipatikani,…..kuna nini kwani..?’ akasikilza baadaye akakata simu,kwa hasira …usoni akawa
kakunja ndita, makunjazi,kuashiria kukasirika... akageuka kuniangalia mimi , akajaribu
kukunjua hizo ndita, akasema;
‘Uliza maswali yako haraka nataka kuwahi sehemu, na wewe
ukapambane na nguvu ya dola…hahaha, unafikiri utapeli una tija, sasa utajua
kuwa mimi ni nani, afande anakusubiria, uliza haraka, au ni mbinu za
kujichelewesha, mhhh...’akasema, akitabasamu sasa kwa dharau, na mimi nikasema;
‘Haya,…Tuanzie pale tulipoachia,….’nikasema na kabla
hajasema neno nikasema;
‘Kawaida za mwizi ni arobaini..na mungu ana namna yake ya
kumnasa mnafiki..hata ufanyeje, itafika muda ukweli utajulikana…na haki ipo
juu, …ngoja tuone’nikasema na yeye akijifanya kutabsamu bila wasiwasi,
akatikisa kichwa kama wafanyavyo wahindi kukubali ,….. akasema;
‘Wewe uliza hayo maswali yako ndugu…na sijui utaanzia wapi,
wewe mwenywe unajua wapi pa kuanzia,
mimi sikumbuki uliachia wapi…’akasemaakizungusha shingo kama kunyosha.
‘Mimi nataka tuende sawa, sio kwa ugomvi, na kwa
kuelimishana …tulishaanza kuulizana awali, au sio…sasa tuanze mwanzo au
tuendeleze pale pale, unaonaje afande…?’ nikamuuliza mpelelezi.
‘Nyie endeleeni tu….’akasema
‘Afande huyu anataka kukupotezea muda wako, kwa uwongo wake wa kitapeli, kwanini haanzi
kuuliza maswali yake, mimi nitakujibu na
mwisho wa siku utaumbuka wewe mwenyewe…., mimi sio mnafiki, mnafiki ni wewe
unayeingilia maswala yasiyokuhusu….’akasema akajifanya kutabasamu, lakini nahisi
kuna kitu kaambiwa huko kwa watu wake na kimemgusa.
‘Hebu nikuulize tena, …kuhakikisha tu, je wewe ulijua lini
kuwa kaka yako anadaiwa benki?’ nikamuuliza
‘Nilijua kipindi kidogo, nilishakuambia hilo, unakumbuka
kuwa nilikuambia kuwa, nilijua hilo deni
pale nilipokwenda kuchukua pesa benki, unakumbuka…?.... au unauliza kwa faida
ya afande, haya hilo ndio jibu lake,au hutasheka na jibu hilo, …?’ akauliza
akiigiza kama muungwana fulani.
‘Nikumbushe vyema, kwa kutoa ufafanuzi…’nikasema
‘Ok,… ni hivi, nilikuambia kuwa mimi ndiye niliyachaguliwa na wanafamilia wote
kuwa niwe msimamizi wa hii familia ya kaka,…ni taratibu za mirati hizo zipo
waazi, pande mbili zinakutana sawa unahitaji nielezee inavyo kuwa au… ?’ akauliza
na mimi nikabakia kimia yeye akaendelea kusema.
‘Kama unaelewa ndio hivyo, mimi nikachaguliwa kuwa ndiye
msimamizi….na kwahiyo kila jukumu, ikiwemo matumizi,…nakadhalika yalikuwa
mikononi mwangu, na ukumbuke shemeji alikuwa hajiwezi, mgonjwa, yupo kitandani
hata kugeuka hawezi. Kwahiyo mimi ndiye niliyekuwa msimamizi wa kila kitu, huku
nikimsaidia, japokuwa awali kulikuwepo na watu wanamsaidia kibinadamu lakini
sio kimatumizi, unajua…yupo hapo muulizeni..’akatulia akimuonyeshea shemeji
yake.
‘Na ujue kuwa matumizi yanahitajia pesa, kwahiyo kile
tulichokuwa nacho kilifikia mahali kikaisha,….sasa tufanyeje, ndio ikabidi niende benki kuchukua pesa , huko
kulikuwa na akiba ya kaka, eeh,… sikujua ni kiasi gani, na kama shemeji
angelikuwa anaweza angeniambia labda kuna salio kiaisi gani….’akatulia
akimgeukia shemeji yake.
‘Kwa maana kuwa kwa muda huo, hata kuongea ilikuwa shida,….angelisema
kuna kiasi gani, lakini mimi nikajua tu, huko benki kuna kitu,….hizi kadi za siku hizi
, huwezi kujua mpaka uende benki au sio..au kwenye mashine zao..na
nisingeliweza kwenda kwenye mashine, lazima nifuate taratibu za kujitambulisha
kuwa mimi sasa ndiye msimamizi wa mirathi…’akatulia kidogo
‘Sasa siku hiyo…nikadamkia benki…nafika nikajaza fomu zao,
nikiimbatisha na barua kuwa mimi sasa ndiye msimamizi…’akatulia
‘Na mara nikaambiwa subiri…baadaye ndio nikaambiwa kuwa
siwezi kuchukua pesa kwasababu kuna deni….’akatulia.
‘Alikuambia nani…?’ nikamuuliza na yeye akacheka kwa dharau
kama vile nimemuuliza swali lisilo na maana
‘Na mtu wa benki, …ok, nani kwa jina sio ndio unataka hivyo,
unataka …..eeh labda uwasiliane naye kuhakikisha, …kiukweli mimi siwezi
kumkumbuka jina….na ukumbuke kuwa ni siku nyingi, huenda hata sura
nimeshamsahau…’akajibu akibenua mdomo wa
dharau
‘Ulipoambiwa hivvyo ulichukua hatua gani?’ nikamuuliza
‘Kama umeshapewa jukumu la kulea familia, utafanya nini
hapo…unahitaji pesa, nisingelirudi nyumbani na kusema hakuna pesa, au sio…?’ akaniuliza na
mimi nikabakia kimia, alipoona simjibu akaendelea kutoa maelezo.
‘Mimi sasa kama mkuu wa familia ikabidi akili ya ziada
ifanye kazi…ukumbuke na mimi nina familia yangu nayo inahitajia kula na kila
kitu, huu ni mzigo mwingine wa ziada…, lakini sikujali kwa vile hawa pia ni
watoto wangu, watoto wa kaka ni wangu pia, au sio…kiujumla, ilibidi nianze
kutafuta njia, ili watu hawa waweze kuishi, mgonjwa aweze kuendelea na
matibabu…’akasema akimuonyeshea shemeji yake kwa mkono.
‘Je ulipopata taarifa hizo uliwahi kumwambia shemeji yako…maana
licha ya kuwa hajiwezi lakini najua kuna mambo ulikuwa unafika umamwambia au
sio, je kuhusu hilo deni uliwahi kumwambia shemeji yako?’ nikamuuliza
‘Hapana mimi sio mjinga kiasi hicho ….sikumwambia shemeji….nilikwepa
kabisa kumwambia hilo…maana lingemchanganya akili, mtu keshachanganyikiwa
unamzidishia dozi, ulitaka nimuue shemeji yangu..hapana mimi sikumwambia
kabisa…’akatulia
‘Hukuamwambia mpaka lini…?’ nikamuuliza
‘Ilifikia hatua niliona nisimuambie nipambane
mwenyewe…lakini maswala hayo hayana siri, wakaja kutuma barua ya kukumbushia
ndio shemeji akaja kujua, ….lakini mimi bado nilikuwa na mashaka, , ndio maana
hadi inafikia hatua mbaya, nilikuwa bado nasita kumwambia ...’akatulia.
‘Kwahiyo wewe ulikwenda benki kwa vile ulichaguliwa kuwa msimamizi ,hebu tufafanulie ulivyofanya pale
benki, kiutaratibu wa mirathi,…ulipofika pale ulifanya nini?’ nikamuuliza
‘Wewe mwenyewe unazijua taratibu za benki,….kuna haja ya
kulijibu hilo swali?’ akaniuliza
‘Ipo haja, na muhimu sana kwangu….’nikasema
‘Haya ndugu, nilifika pale nikajaza fomu za kuchukkulia
pesa, ile fomu nikaambatisha na ile barua ya kuwa mimi ndiye msimamizi wa
mirathi….ok, sasa wataka nikuambia kila kitu nilichokifanya, hata kama nilenda
chooni, au sio…, nilimkuta nani, nikakaa foleni..ikafika zamu yangu…hivyo au…?’akaniuliza.
‘Ina maana ilivyo wewe ulipewa barua na kikao cha
wanafamilia, upeleke benki, au sio…kwenye hiyo barua ukatambulishwa wewe na
picha yako,..na sahihi yako au sio…,na
benki wana taratibu zao, huwezi kuchukua pesa mpaka uwe umeidhinishwa kama signatory, unanielewa nikitumia hilo,…?’
nikamuuliza
‘Nakuelewa bwana, mimi nimeenda shule, endelea…’akasema
‘Kwahiyo ili hilo
lipite kulikuwa na taratibu zao, si ndio hivyo…?’ nikamuuliza
‘Ndio hivyo,….hahaha, kumbe unajua, sasa kwanini unaniuliza,
ndio hivyo…ni mambo ya kawaida hayana kuremba…benki hawana jinsi unafuata
wanavyotaka wao, na sio wanavyotaka wao ni utaratibu dunia nzima au sio...’akasema
kama ananiuliza.
‘Labda swali la kujikumbusha, nyie mpo ndugu wengi, na kuna
wakubwa zaidi yako au sio, ni kwanini walikuchagua wewe uwe ndiye msimamizi wa
familia?’ nikamuuliza akatabasamu kidogo, lakini akilini alihisi kuna mtego,
akawa makini kulijibu, akasema;
‘Nimeshakuambia kwenye kikao hicho walikuwepo ndugu wa pande
zote, hakukuwa na swala la kampeni hapo, ni wao wanavyokuona,…upande wa shemeji
…walimtegemea ndugu yao, lakini alikuwa hajiwezi kwahiyo kwa kiasi kikubwa
walitegemea upande wetu…sasa kwa upande wetu..’akatulia akikohoa kidogo.
‘Kwa upande wetu…, nahisi ni kwa vile mimi nilikuwa karibu
sana na marehemu,labda ndio sababu kubwa ya msingi ya kunichagua mimi…na labda
ni kwa vile mimi najulikana sana kutokana na shughuli zangu za hapa na
pale,kwahiyo kukihitajika kitu haitakuwa
vigumu kwangu kukifuatilia, na wananifahamu kuwa mimi nakutana na watu wengi,
na nakumbuka wateja wangu, hasa wale ninaoingia nao mkataba, siwezi kuwasahau, …ndio
wakanipendekeza mimi, nikapita ’akasema.
‘Hebu sasa turudi huko benki, wewe ukafika pale wakakuambia
kuwa kuna deni …ilikuwaje kwanza?’ nikamuuliza
‘Ilikuwaje kwa vipi… ni pale nilipotaka kuchukua pesa, …
ndio nikaambiwa kuna deni kubwa, nikashituka kuna deni, wakasema ndio tena deni
kubwa na kutokana na mkataba, hilo deni lilitakiwa kulipwa kila baada ya muda
fulani, lakini halikuwahi kulipwa,…’akatulia
kidogo.
‘Ndugu yangu kiukweli mimi mwenyewe nilishangaa, kaka achukue
mkopo mkubwa hivyo bila ya mimi kujua, na, sijui alichukua kwa minajili gani,
sijui, na nisingeliweza kwenda kumuuliza shemeji kama anafahamu hilo, unajua
sio… ‘akatulia kidogo akitaka nisema neno lakini mimi nikabakia kimia ndio
akaendelea kusema;
‘Pale pale nikawaambia watu wa benki ,… mimi sijui kuhusu
hilo deni,…nikaja juu kweli, …namfahamu kaka yangu vyema , asingelikopa bila
kuniambia, mimi,…yawezekana alimwambia mkewe..lakini kwa ufahamu wangu kitu
kama hicho angeniambia, tulikuwa karibu sana na yeye, ….nimjuavyo kaka
asingelinificha, ….lakini kila kitu kilionyesha, utasema nini...’akatulia
‘Kila kitu kwa vipi…?’ nikamuuliza
‘Nilitakaa kuthibitisha hilo deni kama kweli ni la
kwake…nikaambiwa nisubiri, baadaye nikaambiwa niingie nikaonane na
mhasibu,…..nikaingia na huko nikaonyeshwa vielelezo vyote,….ujue mimi kutokana
na kazi zangu nimezoea sana kukumbana na makaratasi,…na macho yangu huwa mapesi
sana …niliyapitia yale makaratasi kwa macho kwa haraka nikaona kila kitu kipo sahihi….kwahiyo hata alipoanza
kunionyesha kwa hatua, nilisharizika..lakini hata hivyo, nilikubali tu…’akatulia
‘Baadaye nikaomba huo mkataba….maana pale mtu wa benk
alikuwa akinionyesha nyaraka nyingine, mimi kitu muhimu kilikuwa ni mkataba,
ndio…akanionyesha huo mkataba,…deni hilo lilitakiwa kulipwa kila mwezi,…kuna
kiasi kilitajwa, na chini ndio kuna hilo rungu, usipolipa ni nini kifanyike na
ndio huyo mhasibu akasema mimi kama msimamizi natakiwa kulisimamia hilo ili
lilipwe kwa wakati na ni muda mrefu hakuna malipo yaliyofanyika…’akatulia.
‘Hebu hapo….kwahiyo walikuambia hivyo, siku ile ile
ulipowenda kuchukua pesa au sio….huku nyuma hukuwahi kuchukua pesa, au?’
nikamuuliza.
‘Ndio ni siku ile ile ya kwanza ….’akatulia kama anawaza
jambo.
‘Ni siku ile.., nilipotaka kuchukua pesa, ndio yote hayo
yakajulikana, wakasema siwezi kuchukua
pesa, kwani kuna deni, na deni hilo ni kubwa,…’akasema
‘Ikawaje sasa….?’ Nikamuuliza
‘Ndio hapo nikawaomba waniruhusu nichukue kiasi kwa ajili ya
kusaidia familia,wakakataa, ..nikaomba na kuomba, nikaona hawa hawanifahamu,
nikawaambia nataka nionane na meneja wao wa benki….’akatulia
‘Mnafahamiana na huyo
meneja, au…?’ nikamuuliza akasema
‘Sio swala la kufahamiana , hata angelikuwa nani mimi
ningemuingilia tu,…ili familia iweze kwenda choo…’akasema
‘Sawa ikawaje?’ nikamuuliza
‘Mimi kutokana na kazi zangu, najua nifanye
kipi…hawakunifahamu, nikaenda kuonana na meneja, nikamuelewesha, …unajua tena,
ukiwa muongeaji, kuna raha zake, meneja akakubali kuwa sasa nichukue pesa
lakini iwe bado ni deni, kwani pesa yote iliyokuwa nayo kaka kwenye dhamana yake,….kwenye akiba
yake, imelipia sehemu ya hilo denii,
kwahiyo ndio maana ukiangalia kwenye statement
utaona deni liliongezeka…’akasema
‘Ngoja kwanza hapo…umesema uliambiwa hivyo siku ya kwanza,
si ndio hapo kuwa huwezi kuchukua pesa kwa vile kuna deni..?’ nikamuuliza
‘Ndio…kwani kuna tatizo gani hapo…?’akasema na kuniangalia
kwa mashaka.
‘Na tangia marehemu afariki, hukuwahi kuchukua pesa..?’
nikamuuliza hapo akasita na akawa kama anawaza
‘Jibu swali….hilo halihitajiki kufikiria je tangia kaka yako afariki hukuwahi kuchukua pesa
kablaya kuja kuambiwa kuna deni…?’ nikamuuliza
‘Sikumbuki…’akasema
‘Hukumbuki, ….lakini wewe uliagiza statements, ambayo
inaoinyesha kila kitu…na wewe ndiye peke yako ulikuwa na mamlaka ya kuchukua
pesa ndio au sio…?’ nikamuuliza
‘Yawezekana, lakini ….’akageuka kumuangalia shemeji yake.
‘Shemeji yako alikuwa mgonjwa, asingeliweza kuchukua pesa,…ndio
maana nimekuuliza hilo deni uliambiwa siku ipi, ….umesema siku ya kwanza tu
ulipopewa hilo jukumu..haya turudi kwenye statement, hakuna maingizo
yaliyotokea kabla ya kuongeza hilo deni…?’ nikamuuliza
‘Nimekuambia hilo sikumbuki mpaka tuangalie hiyo statements,
nikiangalia hiyo, nitakumbuka….’akasema
‘Hiyo ni ushahidi mwingine…’nikasema nikimgeukia mpelelezi..Mpelelezi
akawa kimia tu
‘Unasema nini….ushahidi gani huo….wewe tapeli kweli, hilo
lina maelezo, ngoja nikiangalia hiyo statement nitakuambia kama ni mimi nitakumbuka maelezo
yake,…..hebu shemeji samahani , tunaomba
hiyo statement ya benki, nikiona hiyo pesa na tarehe nitakumbuka maelezo yake, …’nikasema
‘Pesa ipi…?’ nikamuuliza na yeye akashtuka, akajiona
keshaingia kwenye mtego, lakini keshachelewa
‘Nakumbuka umesema kuna pesa ilichukuliwa kabla,….ndio maana
nataka nione hiyo statement kama ipo ipo itakuwa na sababu…’akasema
‘Hiyo nyaraka ya benki haina haja kwasasa hivi….’akasema
mpelelezi
‘Umeona afande huyu ni mjanja tu…hana lolote, yawezekana kweli
ipo au haipo, mimi sikumbukI na kama ipo ina sababu..na huenda benki kwa wakati huo walikuwa hawajaweka mambo yao
sawa,…kuhusu madeni, ndio maana nasema, mpaka nione hiyo statement…lakini kama
ni ushahidi wake, sawa tutapambana mbele kwa mbele, mimi siogopi, maana
sijafanya kosa…’akasema
‘Huyo mhasibu wa benki uliyekutana naye unamtambua kwa
jina.. unaweza ukamkumbuka?’ nikamuuliza
‘Nimekuambia siwezi kuwakumbuka, kwanza ni siku nyingi…simkumbuki
kabisa, ni siku nyingi jaman, hivi kweli unaweza kukumbuka kila kitu, kila mtu
wa mwaka wangapi huu, na huenda keshakufa,..maana sikumbuki, na binadamu ni
mpita njia tu….’akasema
‘Nakumbuka ulisema kutokana na kazi zako wewe huwaga husahau
hasa watu, sura za watu hasa wale mnaoingia nao kwenye mikataba huwezi
kuzisahau au sio…., sasa ilikuwaje huyo muhasibu ukamsahau…?’ nikamuuliza, na
yeye akajifanya kutabasamu kabla hajajibu na mara simu yake ikaita,
alipoangalia mpigaji, akasimama, na kusema;
‘Nahitaji kuujibu hii simu nje ni wateja wangu, sawa afande….’akasema
na afande akasema
‘Unaweza kuijibu hiyo simu hapa hapa, kama huwezi mwambie
utampigia baadaye, au sogea pale , sisi
hatuwezi kusikia mtakachoongea ,…kwani
tukisikia kuna ubaya, ni mambo halali au sio?’ Akauliza mpelelezi, na
jama akaizima ile simu kwa haraka. Mpelelezi akawa kama anataka kusimama,nikajua
anataka kufanya nini…ushahidi mwingine!
NB: Kibano kingine, Maswali yanaendelea muwe wavumilivu hapa,
kwani ukweli uligundulika humo humo kwenye maswali…ndivyo ilivyokuwa, na hapa utaona dua ya mwenye kudhulumiwa ilivyo na
nguvu. Huyu mama mjane aliinua mikono yake juu, akasema yote anamuachia mungu…ogopa
sana dua hii!
WAZO LA LEO : Moja ya
dalili za mnafiki ni uwongo, akiongea hupenda kudanganya, uwongo kwake ni jambo
la kawaida, na hujiona mjanja kudanganya, na hajali kupata kipato kwa njia hii
ya urongo, kwake uwongo ni fani.…lakini tabia hii haishii hapa, mtu huyu hata
uaminifu wake utakuwa na walakini, na huwezi kumwamini kwasabbau haaminiki,,
hawezi kutunza siri…maana hulka ya uwongo imeshajijenga. Tumuombe mungu atunusuru na tabia ya uwongo,
na kama tunayo tuiache, kwani tabia hii inakuwa mama wa dalili nyingine za
mnafiki, na athari yake ni kubwa.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Wanasema anaesema uwongo basi asiwe msahaulifu na mwisho wake ni aibu tupo pamoja m3
Post a Comment