Siku kabla ya hukumu!
Dalili za mwanzo…
Siku ya pili nilifika kituoni kama nilivyoagizwa, na nikaambiwa
nisubirie kwanza, kwani Dalali anahitajia wakili wake awepo akiongea, ikabidi
tusubirie kwanza , lakini baadaye mimi nikaruhusiwa kuingia ndani, kwani wakili
wake alichelewa kufika. Niliingia kwenye
chumba maalumu cha maongezi, na humo sikumkuta mtu baadaye kidogo, Dalali akaja
akiwa kaongozana na askari;.
Dalali aliponiona akaanza kucheka ile cheka yake ya dharau, akasema;
‘Ehee wewe tapeli, niambie, umakuja eeh, …wewe mpuuzi kwelikweli…,
yote haya umeyasababisha wewe, yaani mimi nalazwa humu kituoni kama mhalafu,..naumwa
na mbu, kwasababu yako, ….wewe mtu wewe, …tatizo wewe hunifahamu…yaani hili utalilipa,
hutaamini…’akasema
‘Kwani ni mimi ndiye nimekuweka ndani, …wewe si uliona pale,
si mimi ndio nilitakiwa kuweka ndani, na wewe ulikuwa unashabikiwa iwe
hivyo…hukujua kuwa haki ina nguvu sana kuliko dhuluma, umeonaeeh, mungu alivyo, hutoa kila kitu kwa haki…na kwa
ajuavyo yeye, pole sana ndugu yangu, na mimi sikukuombea kabisa uyapate haya…je
hali yako vipi…?’ nikamuuliza
‘Hali yangu vipi….wewe lala humu ndio utaniuliza swali
hilo….’akasema akijikuna, suti ilikuwa imejikunja kunja.
‘Najua sana hali ya hapo, nimeshalala humo mara nyingi tu,
lakini kuwekwa kwangu humo ilikuwa tofauti na wewe…nilikuwa natete wanyonge,
….’nikasema
‘Sawa bwana….endelea kutetea tu,…’akasema akiendelea
kunyosha nyosha suti yake, na kuweka tai yake vyema.
‘Yaonekana unajipenda sana…’nikasema na akatabsamu na kusogeza
kichwa karibu yangu,kama anataka kuniambia jambo la siri au la muhimu akasema
‘Sasa siliza . ile familia ilikuwa ikinitegemea mimi, nibangaize ndio ipate kula,...unanisikia
sana…’akatulia kidogo.
‘Sasa mkuu, kuanzia sasa nakuachia wewe utajua jinsi gani hao
watu wataishi, wewe si umejifanya kidume bwana, wewe ni kaka mtu, au sio..na unajifanya una
huruma zaidi yangu, haya sasa kazi kwako….’akasema kwa sauti ya juu, halafu
kama vile kajitambua akashusha sauti,, kama vile hataki watu wengine wasikie wakati
tulikuwa wawili tu na Yule askari alikuwa katoka alikuwa kwa nje mlangoni.
‘Je kama ulikuwa unaionea huruma hiyo familia mbona unaacha
wanafukuzwa kwenye sehemu yao ya kuishi , wangeenda kuishi wapi, au una nyumba
nyingine ya kuwapatia maana nyie madalali bwana…mnatajirika tu kwa majasho yaw
engine… mhh, mpaka nyumba ndogo mnawajengea nyumba, wewe kiboko,…’nikasema kama utani na yeye akacheka, akitikisa kichwa
‘Wewe mjanja sana wewe, sikuamini, hebu nikuulize wewe anakulipa nani kwa kazi hii,…ya upeku
peku …. hahaha, eti nyumba ndogo, acha hiyo kabisa…najua unaelekea wapi….hahaha
hunipati ng’ooo’akasema akikaa kwenye kiti na kujiegemeza, akawa ananyosha tai
yake vyema, halafu, akageuka huku na kule kama anawatfuta watu wengine.
‘Hawa watu wapo wapi…?’ akauliza huku akiinua mkono kama
anaangalia saa, na mkono haukuwa na saa, na mimi kwa kupoteza muda nikazidi
kumtania.
‘Kwahiyo sasa umekubali ukweli …upo tayari kutubu, au sio….?’
Kwanza akatabasamu, halafu akanikazia macho na kusema;
‘Kutubu nini, kuhusu nini, nitubu kosa gani, …unafikiri kwa
vile wamenishikilia hapa, nina kosa au, au ndio huo upeku upeku wako…’akatulia
kama anasubiria jibu kutoka kwangu, na mimi nikawa nimetulia tu, halafu kwa
sauti ya chini, akaniuliza
‘Hebu niambie mimi nina kosa gani , maana haya yote
umeyaanzisha wewei..?’ akauliza akinikazia macho.
‘Hivi hukusikia kuwa mtaalamu kaongea kila kitu…? ‘
nikamuuliza , akacheka kweli kweli, halafu akatikisa kichwa, akasema
‘Wewe mjanja sana…wewe eeh, ni kiboko…hahahahaha.’akasema na
kuendelea kucheka.
‘Kwani hujaambiwa,…yeye bwana kajitakasa na kusema ukweli wote….’nikasema
‘Ukweli upi bwana,
usifanya mimi mtoto mdogo….nilishakuambia kama unahisi kuna makosa yamefanyika,
…leta ushahidi … upo wapi huo ushahidi
wako, nikuambia ukweli, likiisha hili mimi ninakushitakia rasmi,….hilo ujiandae
nalo..’akasema na kunikunjia uso kuonyesha hatanii.
‘Ushahidi si ndio
huo…shahidi mmojawapo ni Mtalaamu, kaelezea yote kabla hajatoroka, au
hujaambiwa , labda ndio maana umeamua kumuita wakili wako…mimi ningekushauri kitu
kama rafiki yangu, shemeji yangu..useme ukweli tu, maana mwisho wa siku
utabakia wewe mwenyewe…’nikasema kama utani
‘Wewe unajifanya mjanja sana,nimeshakuelewa mbinu zako,
nitabakia mimi mwenyewe kwa kosa gani,,….hebu niambie mimi nina kosa gani,
mbona hutaki kulisema hilo….?’ Akauliza sasa akiwa makini.
‘Unaweza ukashitakiwa kama mshirika mwenza , kama hutakuwa mkosaji, kama atapatikana mtu mwingine aliyetenda
hayo, wewe utakuwa mshirika wake, ndio
maana nakushauri useme ukweli, yaishe, ili haki itendeke, mjane na mayatima
wake wapate haki yao…hilo deni sio haki , huo ndio ukweli,sasa kama deni sio
halali, ni nani aliyafanya hayo, unaona ilivyo….’ akanikatiza na kusema
‘Hebu niambie kwa hilo , maana hapo tu yaonyesha huna
uhakika, mkosaji hajafahamika, au sio….sasa mimi nitashitakiwa hapa kama nani, kama
mshukuwa, haya, kama ni hivyo ushahidi upo wapi,..kwanza tafuteni mkosaji ndio
muanza kumkamata, kama mtampata, mtaniambia,’ akasema
‘Huyo mkosaji alikwenda kwa mtaalamu, akamwambia yote, na
alitaka mtaalamu afanye mambo yake ili kumlinda,….’nikasema nikimuangalia
atakuwaje usoni, lakini hakuonyesha dallili ya kushituka, ila alitanabasamu kwa
dharau tu.
‘Ndio maana nakuambia mwenzako,….mtaalamu, yeye kasema yote, kuwa kazi yake ndio biashara yake, mteja akija
akimuomba amfanyie jambo,kama linawezekana anamfanyia….na ndio akakubali kuwa
alikuja mteja akitaka afanyiwe hayo yaliyofanyika, ili …..’akanikatiza
‘Acha kutunga
hadithi…..wewe ni mtunzi mnzuri wa hadithi, lakini ukumbuke kuwa hii sio
hadithi, hapa unacheza na uhai wa mtu,….unaijua jela ilivyo..hakuna mtu
anayeweza kufanya ujinga kama huo…’akasema kwa hasira sasa.
‘Sasa sikiliza nikuambie ukweli alivyoongea mtaalamu….kuwa kwake
wanakuja wateja wengi wakitaka kufanyiwa ma- jambo, ili hkulindwa…., yeye ni
mtaalamu wa kulinda watu wenye matatizo mbalimbali, kama wana madeni wasidaiwe,
kama wana maadui, maadui washindwe kumfanyia kitu, kama wana matatizo ya mizimu
mashetani…na mambo mengine,
‘Akaulizwa siku kadhaa nyuma alikuja mtu kwa shida hizi na
zile…akataka kufanyiwa hivi na vile…tuambie …akasema hawezi kukumbuka,
akaambiwa afanye utaalamu wake amkumbuke, la sivyo atalazimishwa
akumbuke…akapinga kidogo, akakumbushwa kiaina,….’akamkatiza
‘Kiaina kivipi…?’ akaulizwa
‘Wanajua wenyewe polisi….’nikasema
‘Uwongo…’akasema
‘Alipokumbushwa akasema ndio anamkumbuka mtu kama huyo,
alikuja kwake, lakini kutokana na miiko yake, ilikuwa ni ngumu lakini kwa vile
alihitajia pesa, na pesa alizoahidiwa ni nyingi akakubali….akaubali kufanya
dawa za kinga na dawa za kulinda watu wasifuatilie…..’nikatulia
‘Wewe mjanja…eehe…’akakaa mkao wa kunisikiliza
‘Basi akafanya mambo yake,..akatengeneza mzimu,.shetani
sijui…kwahiyo akaliweka sehemu ambayo litawagusa watu hisia zao ili
wasifuatilie,…’nikatulia nikimuangalia niliona japokuwa alijitahidi lakini
ilimgusa, akasema
‘Ni hadithi nzuri sana…..’akasema
‘Na mwisho wa siku akaambiwa amtaje huyo mtu kwa jina maana
polis wana uhakika kuwa anamfahamu huyo mtu, …. ni nani…, akaanza kusema,eeh….
yeye kutokana na kazi zake huwa anamlinda mteja wake, harushusiwi kumtaja, lakini si unawajua polisi walivyo,
mwisho wa siku alimtaja.. ‘nikasema
‘Hahaha, jamani….., ni huyo huyo mtaalamu ninayemfahamu
mimi,…haya alimtaja nani ,…alimtaja mtu gani , niambie….?’ Akauliza
‘Kwanini hujiulizi ni kwanini polisi baada ya kuongea na
huyo mtaalamu wakaja kukukamata wewe…’nikamwambia na yeye akatikisa kichwa kama
kukataa
‘Hilo sijui,….. wao wamesema wananishikilia ili kuisaidia
polisi , nahisi kama…mshirika wa huyo
mtaalamu, kwa vile anawahadaa watu…eti serikali imetoa amri wataalamu
wanaohadaa watu wakamatwe, na huyo mtaalamu wanahisi anaweza akawa …..wanamshuku
tu kwa vile hawamfahamu vyema, ….. ndivyo nijuavyo mimi, na mimi mpaka sasa
hawajaniambia kosa langu ni nini,…etu natakiwa kuisaidia polisi, sasa nimewashtukia,
….’akasema
‘Mtaalamu anawahadaa watu kwa jambo gani,….nimakuambia
awali, alihojiwa akasema alimjia mtu, huyo mtu alimjia kwa jambo
gani..hujiulizi, hapo, walimtega kuwa anahusiana na mambo ya kukatwa watu
viungo, si unajua polisi walivyo wajanja, kuona kapelekwa huko akasema hapana
yeye hahusiki na hayo, yeye akafanya kadha na kadha,…akabanwa kinamna akaropoka
yote,,…wewe nakupa kama angalizo, mtaalamu keshakutaja baba…’nikasema
‘Kanitaja mimi….kwa vipi!..... Nikuambie kitu, mimi
nimeshajiandaa kwa vyovyote vile, nina uhakika sina kosa,na kwa uwongo wakoo
huo….hunipati ng’ooooo’akasema
‘Sasa kama unajiamini ni kwanini umeamua kumuita wakili….?’
Nikamuuliza, na kabla hajanijibu mara akaingia mtu, alikuwa ni wakili wake, na
Dalali akatabasamu, na kutikisa kichwa kama kukubali …
************
Wakili, akaingia na briefcase
yake mkononi,....na majigambo yake, ni wale wale aina ya Dalali, majigambo kwa
kila hali, mavazi, kutembea, mdomoni,…..Na alipoingia tu…akaniangalia kwa
makini halafu akamgeukia mteja wake, akauliza
‘Huyu ni nani….?’ Akauliza
‘Peku peku…’akasema na wakili akasogeza kitu kukaa karibu na
Dalali, huku akiendelea kuniangalia kwa makini halafu akatikisa kichwa kama
kukubali jambo.
‘Haya niambie…nilitaka tuongee kwanza, kabla hujaanza lolote
lakini foleni bwana, sasa tuanzie wapi..na tutaongeaje na huyu mtu hapa…?’
akauliza
‘Kwanza hakuna muda wa kuongea, …mimi nimekuita kwanza
unisikilize,….utanisikiliza wakati naongea na hawa watu, kuna mambo nataka wewe uyaweke wazi kisheria,
mbele ya hawa watu akiwemo shemeji, ….shemeji naye anatakiwa kuwepo…’ akasema;
‘Mambo gani…?’ akauliza wakili , huku akiniangalia, halafu
akageuka kumuangalia mteja wake,na mara mpelelezi akaingia akiwa na mtu
mwingine ambaye alionekana ni mtu wa kuchukua hayo maongezi kwenye mitambo yao,
kwa ni alikuwa kabeba laptop yenye kamera juu yake…mambo ya kisasa hayo!
Wakili akamgeukia mpelelezi , naona walishaonana huko nje
kwani hawakusalimiana akasema
‘Hebu niambie mteja wangu kashikiliwa hapa kwa kosa gani…?’
akauliza
‘Mteja wako! Ok, hajakuambia eeh,,…yupo hapa kuisaidia
polisi, kuna maswali tunahitajia kumhoji, lakini akang’ang’ania hawezi kuhijiwa mpaka uwepo, kiujumla sisi
tuliona ni maswali ya kawaida tu, sasa huenda anahisi vinginevyo….’akasema
mpelelezi na wakili akamgeukia mtu wake, na Dalali akasema;
‘Usiwe na wasi wasi, wakili wangu, ..ninachotaka ni wewe
usikilize tu, kama utaona ninakosea unaweza kunionyesha ishara mimi nitajua tu,
kuna huyu mtu kanishuku , na shuku hii naona imekwenda mbali hadi polisi
wameingilia kati, lakini kiufupi haina mshiko….sasa wewe sikiliza tu,….’akasema
akitikisa kichwa kujinadi.
‘Kwahiyo…..’akataka kusema wakili wake, lakini Dalali
akamuashiria kwa mkono kuwa anyamaze, na Dalali akanigeukia mimi na kusema;
‘Hasa wewe…ndio nina usongo na wewe….najua wewe ndiye chanzo
cha haya yote, sasa nataka kuuondoa huo uwongo wako wote, ili jamii….hasa
wanafamilia wasiwe na shaka juu yangu,…’akasema
‘Kuna swala nimekuambia muda mchache uliopita, …nikakuomba
kama rafiki unasemaje kwa hilo…?’ nikaanzia hapo
‘Kwanza nikuambie ukweli, mimi sina kosa, siwezi kukubali
kosa ambalo sijalifanya, kama mtaalamu aliongea hayo mbele ya polisi, hayo ni yake yeye…., na kwanza
sio kweli, hayo uliyoniambia, umeyasema ili kunifanya niongee, …
‘Lakini wewe unataka
mimi niongee nini, nidanganye kuwa nimefanya,…..hapana siwezi kufanya hivyo,leo
nitaongea ukweli tu…’akageuka kumuangalia mpelelezi.
‘Mimi namfahamu sana mtaalamu hawezi kusema mambo kama hayo,
eti amekiri kosa, sizani, sijui….na hata
kama kasema alilosema huyu ndugu…, labda, sijui…labda walimtesa, akasema
waliyotaka wao….na kama mumeona ana kosa
basi makosa hayo ni yake yeye mwenyewe…mimi yananihusu nini…’akasema .
‘Yeye kama mtaalamu, kazi yake inatokana na wateja wake….na
nikakuambia alishamtaja huyo mteja wake, ambaye alifika kwake kutaka kinga
yake….’nikasema hivyo, nilimuona
akikunja uso, labda hakutarajia nitaliongea hilo,kwani alijua nilimuambia yale
awali kama utani, sasa anaona naliongelea hapo mbele ya mpelelezi, … akasema.
‘Kwanza…mimi ndiye nimekuita ,.. nataka mnipatie muda wa
kuelezea ’akasema
‘Sawa….nimekuja, na nijuavyo mwito wako ni kuhusu maswali
niliyokuuliza kule nyumbani kwa marehemu au sio..au kuna jingine?’ nikauliza
‘Mhh…..ndio, .lakini mtu mmoja hajafika,….siwezi kuyaongea
niliyokuitia mpaka shemeji yangu awepo, ninataka hili jambo limalizike kabisa,….sitaki
tena kusumbuliwa, hamjui jinsi gani ninavyopata taabu kwa jukumu nililopewa,
naacha kushughulikia familia yangu…na sasa mpaka nalazwa rumande kwa kosa ambalo
sio sahihi…...’akasema na mara mlango ukafunguliwa akaingia yule mama mjane,
akasalimia kwanza kwa kumshika mkono mpelelezi, ambaye alikuwa karibu yake,
halafu akaja kwangu.
Alipofika kwa shemeji yake akasita kuutoa mkono, akawa
anamwangalia shemeji yake machoni, ilichukua muda, akimwangalia hivyo halafu
baadaye, akatikisa kichwa, halafu akainua mkono na kusalimiana na shemeji yake,
kitendo kile naona kiliacha maswali
mengi , nahisi hasa kwa Dalali, je shemeji yake kafanya vile kwa kumuonea
huruma au kuna jambo…hata hivyo kwa mtu kama Dalali mwenye uzoefu wa kazi zake,
hakutaka kuonyesha dalili yoyote machoni mwa watu, akasema
‘Shemu usijali , mimi sina hatia, haya yatakwisha , leo hii
hii, wataumbuka hawa watu….’akasema hivyo .
‘Haya Dalali, tunataka tulione hilo….’akasema mpelelezi
‘Na mtaliona kweli….’akasema
‘Sawa mjue hiki ni
kikao tu cha kuulizana,…sio kikao cha kushitakiana, baada ya hapa, sheria
itachukua mkondoo wake, ….’akasema mpelelezi.
‘Sawa mimi nipo
tayari….’akasema Dalalii kwa kujiamini
kabisa
‘Haya wanandugu, Dalali…ulisema unawahitajia, hawa watu ,
haya hawa hapa wamefika, na ulisema ulihitajia uhojiwe kuhusu hilo deni ili
uondokane na sintofahamu iliyojengeka juu yako,kuwa wewe umelitambua hilo deni
kuwa ni kaka yako, na kwa kulitambau hivyo, wengi wamekudhania vibaya….!
‘akasema mpelelezi
‘Ndio…’akasema hivyo
‘Hayo ni kwa kauli yako, na ulianiambia kuwa wewe huna shaka na hilo
deni kwani wewe una uhakika kuwa kweli
hilo deni ni la kaka yako, na ushahidi unao…, ‘akazidi kusema mpelelezi.
‘Ni sawa, kama kuna mtu ana ushahidi kinyume na huo, wa
kutoka benki ninataka tuuone,…kwa nyongeza hapo….’akasema
‘Na ulianiambia huyu mwenzetu hapa amekuwa akikuhoji kama
vile unahusikana na hilo deni, au sio…anakushuku vibaya kitu ambacho
hukukipendezewa, kwahiyo unahitajia awepo ili uondoe hiyo dhana uliyoiita dhana
potofu, au sio?’ akasema mpelelezi na kuuliza hivyo
‘Ndio…nataka yeye atoe ushahidi, vinginevyo, mimi
sitakubali, nitamchukulia hatua stahiki…sheria zipo, na ikishindikana kwa
sheria…ok…..lakini tuyaache hayo…, ‘akasita kuendelea na sikutaka kusema neno hapo,
nikabakia kimia, akaendelea kusema;
‘Kiukweli inaniuma sana,..nimewaza sana, nikaona ni kwanini,
…..kwahiyo mimi ninachotaka, hili jambo la kunishuku sijui nini…aah, mimi ninataka limalizike hii leo! Na kwa
ujumla mimi naona tulimalize hili jambo
kwa amani, kuliko kupelekana mahakamani,.na zaidi ya hayo ninataka shemeji yangu awe na amani ….’akasema
Alipotamka hivyo akamuangalia shemeji yake, alishangaa
kumuona shemeji yake akimuangalia kwa macho ya mashaka, na walipoangalia na
huyo mjane, yule mama alitikisa kichwa kama
anasikitika na usoni akionyesha huzuni,
akashika shavu, dalali usoni akaonekana akibadilika kama kinyosha, uso wa
kushangaa, halafu uso …akatabasamu. Sijui pale alikuwa akiwaza nini, huenda ni
jinsi alivyomuona shemeji yake, anashindwa kumuelewa kuwa labda shemeji yake
anamuonea huruma au kuna jingine, akaona sasa aulize;
‘Shemeji kuna tatizo huko nyumbani, umesema watoto
hawajambo, lakini mbona naona kama kuna tatizo…?’ akauliza
‘Tatizo!...’akasema shemeji yake kwa mshangao
‘Najua hali za nyumbani, hawa watu wamenishikilia hapa sijui
mna nini cha kula huko nyumbani, inanipa shida sana kuwawazia..sasa muulize
huyu kaka yako nimeshamwambia…nyie mnanitegemea mimi nibnhaize ndio mpate kula,
…..inaniuma sana ’akasema kwa sauti ya huruma, huku akininyoshhea kidole.
‘Kula…ndio unaona ni muhimu kwetu,…kula shemeji sio tatizo, mungu hamnyimi mja wake
riziki, ila hili, nakuonea huruma unavyoteseka huku rumande….na labda huna
kosa,.’akasema shemeji mtu
‘Shemu mimi sina kosa kabisa…hawanielewi tu…’akasema
‘Ndio maana nasema tuyaache tu haya mambo, tumuachie
mungu yeye ndiye anafahamu ukweli….maana
yote haya ya nini, ni sababu gani, sababu ya mali,…mali watu wanaona ni muhimu
kuliko ubinadamu, nikuambie kitu shemeji,….mimi nimeshanyosha mikono yangu juu, na kumuachia yeye mwenye uwezo, kama
kweli mungu anasikia duwa za waja wake waliodhulumiwa, basi ….sina la kusema
zaidi…’akasema huyo mama mjane akinyosha mikono juu.
‘Shemu ndio maana nimekuita hapa, ni muhimu nilithibitishe hili ili moyo wako
uridhike…usiwe na shaka, hawa watu wabaya sana,…wataumbuka wao wenyewe, utaona shemeji nitakavyowaumbua,
na wewe mwenyewe , utahakikisha kuwa mimi sina kosa …, na mimi sijui, kwani
deni hilo limetokea benki,kwanini hawaendi kuwauliza benki,…kwahiyo kwa hivi
sasa nakuomba shemeji yangu uniamini…..unanifahamu vyema, nimeishi kwenye
mikono yako …waache nipambane nao...’akasema na mimi nikasema;
‘Utuelewe Dalali, shemeji yako anataka kauli yenye kumtia
faraja,..kauli itakayoondoa huo uwongo wa kusema mume wake ana deni, kwake yeye
huo ni uwongo, je una kauli gani ya kumsaidia kwa hilo….labda ungelisema
kuwa wewe umegundua kuwa kweli kaka yako
hakuwa ni deni, na hilo deni huenda, …’akanikatisha na kusema
‘Hivi wewe unasema nini..niukatae ukweli,hivi hapo namsaidia
kaka yangu au ninazidi kumuingiza motoni, sikuelewi…’akasema
‘Sasa kwa kauli yako hiyo inazidi kumuuza shemeji yako,
maana yeye ndiye anamfahamu kuliko hata wewe, hakubaliani na hilo,….labda wewe
unajua zaidi, kama unajua zaidi, basi utubu,…’nikasema
‘Nitubu….kwanini nitubu, nitubu nini…?’ akaniuliza kwa
hasira
‘Kuwa ulifanya makosa, na unaungana na sisi kuwa deni hilo
halipo, sio la kaka yako , basi tushirikiane kulitafuta hilo deni ni la nani na
kwanini limeingizwa kwenye akaunti ya kaka yako,…hapo shemeji yako atajisikia vizuri….’nikasema na jamaa
akaniangalia kwa hasira akasema
‘Unajua mimi sikuelewi,….hilo deni ni la kaka, haina haja ya
kumdanganya shemeji, ili iweje, ni kwanini yeye asiukubali huo ukweli , wakati
kila kitu kipo wazi, …hivyo tutamuumiza kaka na kumpendelea shemeji si ndivyo
tunavyotaka, kwa vile yeye hayupo hai kujitetea au sio….’akasema
‘Ndio, kwa vile yeye hayupo hai kusema kweli kuwa hilo deni
sio lake, na walioanya hivyo, wamekusudia hivyo, kuwa yeye ni marehemu hakuna
wa kumtetea, na ndiocho inachomuumiza shemeji yako…’nikasema
‘Shemeji haumii kwa hilo… umemsikia mwenyewe akisema, .nyie
hamjali ubinadamu mnachohangaikia hapa ni mali tu, ugeuze maneno ili deni
libakie, haya likibakia ni nani atalilipa, huoni roho ya marehemu itakuwa
kwenye mateso, je nini kitakuja kutokea kwenye hiyo familia tena, hujiulizi
hilo…sasa nakuambia hivi kama nia yako ni kupata mali, …hupati kitu hapa,’
akasema
‘Mimi na wewe na yoyote yule anapotenda kosa jambo jema ni
kutubu, kuomba msamaha, ukikiri kosa tutakuelewa, huo ndio uungwana, na baada
ya hapo tutaona tufanyeje, hiyo inaleta neema, lakini tukijifanya wajanja wa
kuhadaa, , …sijui kama hiyo mikono iliyoinuliwa juu itarudi chini bure, sijui..’nikasema
na yeye akabenua mdomo kwa dharau
‘Wewe mjanja
sana …na usitake tuharibu hiki kikao, ..unakazania
mimi nitubu, mimi nitubu nini,…..nimeshakuambia mimi sina kosa..na hili
ninataka ulithibitisha hii leo, kama mimi kweli nina kosa toa huo ushahidi
wako ulio nao ,na ikidhirika hivyo mimi nipo tayari kuadhibiwa,….sina
shaka na hilo, hata kaka aliniamini hivyo, nyie tu ndio mumelata fitina zenu,
muulizeni shemeji…’akasema akigeuka kumuangalai shemeji yake.
‘Na..na, mimi nawaambia ukweli kwa hili, …maana mimi
nimejitolea kwa hiyo familia, na pili nataka kuisafisha roho ya kaka itulie
mahali pema,..nyie mnaleta vikwazo, ….mungu atawalipa kwa hilo, mungu ananiona,
mungu atanisaidia nitashinda tu….’akasema na shemeji yake akasema;
‘Aaamini….kama huna kosa shemeji yangu, mungu
atakusaidia,…na huyo anayemsingizia mume wangu , kwa mapenzi ya mungu atabainika
tu, sisi tuna nini,…ni mjane tu, watoto
wangu ni yatima tu, watafanya nini, mungu pekee ndiye anajua hatima yake, …..nyumba , haya na kila kitu wanachotaka
waache wachukue watuachie roho zetu, ….’akatulia kidogo
‘Umeona eeh shemeji…mimi nipo pamoja na nyie msitie
shaka….’akasema
‘Sawa sasa mimi nimeambiwa wewe umeniita, sikutaka kuja hapa,…mimi na watoto wangu tulitaka
twende kwetu, tusubirie lakini ….nimeambiwa nisubirie na kwa hili, nisingetaka
watu wapate shida na huenda hawana hatia, tumuachieni mungu tu, kama tutaishi
kwenye miti, sawa,…ndivyo tulivyokadiriwa, lakini siwezi kusimama mbele ya
mahakama tena kusema kitu…..hapana, nieleweni jamani, ’sauti ilimtoka huyo mama mjane ikiwa ni ya huzuni,
niligeuka kumuangalia Dalali kama imemgusa, lakini nilimuona akishika kidevu
kama anawaza jambo.
‘Ni sawa shemeji, hawa hawajui..angalia mtoto anavyoteseka,
…mimi ninakuahidi shemeji utalala kwenye miti, nitahakikisha unapata nyumba
yako, hata kama haitakuwa sawa na hiyo….haya tulishayamalzia, lakini sababu ya
huyu…..’akaninyoshea kidole!
‘Basi inatosha msinyosheane vidole niambieni mlichoniitia,
kama ni hivyo, basi mimi sina zaidi naomba nindoke….ila nasema hivi,..mume
wangu hawezi …..sijui lakini ya mungu mengi, labda yeye mwenyewe atokeze asema
ukweli,..sijui kwa vipi…lakini nimjuavyo mimi, sio kweli……sio kweli jamani,
msimsingizie uwongo marehemu…’akasema na ilikuwa kama anataka kulia.
Dalali, akataka kusema neno, lakini sauti ikawa kama
imempotea, akageuza kichwaa kuangalia
mbele, ni kama vile aliona kitu,…akawa anatizama mbele tu huku macho yakizidi
ukubwa, ni kama alikuwa anatizama kitu na sote tukageukia huko anapotizama,
lakini hakukuwa na kitu,…..aliyatoa macho yaliyojaa uwoga, huku akisema maneno
haya;
‘Haiwezekani…., bro…haiwezekani…sio yeye, hapana,
msinitishe, wanga wakubwa nyie, sikubali, sio yeye….’ halafu akainamisha kichwa
chini, sijui alikuwa akiwaza nini, kwa hapo hatukujua ni nini alikiona, na
hatukujua maneno hayo ya shemeji yake yalimgusa vipi, na kwa hali ile tukatulia tukimsubiria
atuambie jambo, akawa kimia, kainama hivyo hivyo tu…
Je nini kilitokea….!
NB: Nawaomba muwe na subira, kuna mlolongo wa maswali na
majibu,….Tukio hilo ndivyo lilivyokuwa hadi ukweli ukajulikana, bila hata
kumuhusisha hakimu wa duniani,…tuwe na subira tuone somo na hekima cha tukio
hili, soma katikati ya mistari utanielewa, tupo pamoja
WAZO LA LEO: Mwenyezimungu kwa kutupenda
sisi waja wake,tunapokosea anatupatia muda wa kujirudi, na kutupatia nafasi ya namna kwa namna iwe kwa maono
yaliyodhahiri, au ya ishara , ili tu tuweze kutubu, wengine wanazidishiwa hata mali,
lakini wengine hupata mitihani kama maradhi
nk.., ili tu tumkumbuke mola wetu, tutubu makosa yetu
Lakini kwa kibure chetu, na kujisahau tunatakabari, na
kujiona ni wajanja, tumesoma, tuna mali, tuna nguvu, tuna cheo, warembo nk…na tunajiona
tuna muda, wa kufanya lolote…tunajiona ni sisi ndio tumependwa zaidi,
…walioondoka walikosea…nani kakudanganya!.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
MKUU UPO?
If umekwama twaambie tukukwamue...we need your story very much.
Post a Comment