Jamaa aliposikia nasema ;
‘Afande vipi…’ akajua kweli mimi sitanii, kwani nilimuona
akiangalia muelekeo wa mlangoni, na kwa ile hali ni kama anataka kukimbia, na
mimi nikasogea na kukaa mbele, kama kumkabili hivi, nikamwambia;
‘Rudi ukae tuongee,….’nikasema
‘Siwezi, mimi naondoka….’akasema na kabla hajamaliza mlango
ukagongwa,…alistuka utafikiri alisikia mlio wa risasi, akageuka taratibu
kuangalia tena mlangoni, na mara akaingia jamaa mmoja, kwa umbile huwezi
kukosea ….sura na umbile ulionyesha kuwa huyo ni mtu wa usalama.
Jamaa kwanza akajikuna kichwani, halafu akageuka kuangalia
dirishani akawa anasubiria, sijui sasa atachukua hatua gani,ataondoka au
atasubiria….
***********
Huyu aliyeingia alikuwa mpelelezi wa polisi akiwa kavalia
kiraia, na tukasalimiana naye, wakati huo jamaa alikuwa bado kasimama
akishindwa kuamua kukaa au kuondoka, Yule mpelelezi akajitambulisha na kutoa
kitambulisho chake, akamuonyeshea jamaa…
Na jamaa akageuka kuniangalia akasema
‘Haya yote , yana
maana gani..?’ akaniuliza akimwangalia kwanza huyo mpelelezi na halafu akageuka kuniangalia mimi, akawa
anaashiria kwa mikono kumuonyesha huyo mpelelezi.
‘Mimi sijui…muulize yeye mwenyewe,…’nikasema
‘Mimi nimefika hapa kukufuata wewe, nilifika nyumbani kwako
nikaambiwa haupo, nikaelekezwa kuwa huenda upo hapa….’akasema huyo mpelelezi
akimwangalia huyo jamaa
‘Kuna nini kwani, nimefanya nini, …na ni nani huyo kakuambia nipo hapa?’ akauliza maswali
mengi kwa mfululuzo, kuonyesha jinsi gani hakulitazamia hilo.
‘Ni maswala machache ya kujirizisha, …nilikuwa nataka kuulizia
maswala yanayohusiana na kifo cha kaka yako…’jamaa kusikia hivyo, akashtuka
kidogo…na akamgeukia huyo mpelelezi, na kusema;
‘Kuhusiana na kifo cha kaka yangu!?’ Akauliza kwa mshangao
‘Ndio….’akasema mpelelezi
‘Sielewi, maana kaka kafariki muda, iweje leo ….kwani kuna nini kimetokea mpaka muanze
kufuatilia, au mumegundua nini…?’ akauliza jamaa na sauti yake ilikuwa kama
inatetemeka.
‘Usiogope, ni maswali
ya kawaida tu, ya kujirizisha kabla hatujafunga jalada lake…, hata kamamtu
kafariki zamani, inawezekana kukatokea
kitu cha kutufanya tuchunguze, hata hivyo, jalada la kaka yako lilikuwa
halijafungwa, ….’akasema
‘Ndio nauliza kuna nini cha zaidi, maana mnataka
kutukumbusha ya zamani, na haya mkiongea na mjane, mtazidi kumtonesha…na kwa
hali yake ilivyokuwa, naomba chonde, tusiyaongelee hapa, kama kuna jambo
mumegundua….’akasema
‘Hapana…ni mambo ya kawaida tu,,…ni kweli kaka yako alifariki
kwenye ajali ya gari, hilo halina shaka,..lakini kuna mambo bado tunahitajia
kuyaweka sawa ili kumbukumbu zetu ziweze kuwa kamilifu…na sizani kama hata
shemeji akiyasikia yatamuathiri kitu…yanaweza kumsaidia kutuliza moyo
wake….kwahiyo usijali kwa hilo’akasema huyo mpelelezi.
‘Ok, ulitaka kujua nini, maana huyu naye ana maswali yake hata
simuelewi, nashindwa hata….sasa sijui nianze na nani….?’ Akaniuliza na mimi
nikabakia kimia tu
‘Uanze na nani kwa vipi…kwani….?’ akauliza huyo mpelelezi
akiniangalia halafu akamuangalia huyo jamaa
‘Huyu si mwenzenu, hamjuani, au…?’ akawa kama anauliza na
kuniangalia mimi kwa dharau fulani, na mimi nikawa kimia tu, sikusema kitu…
‘Ok, sawa…sio lazima tujuane, huenda anatokea kitengo
kingine…’akasema huyo mpelelezi
‘Mhhh….naona sasa….’akasema jamaa
‘Kwani kakuuliza nini cha kukufanya uwe na mashaka na yeye..?’
akauliza
‘Unajua yeye nimemkuta hapa akiwa na shemeji yangu, na
katika kuongea akaanza kuniuliza maswali, ambayo yamenifanya nimtilie mashaka,
…’akasema na huyo mpelelezi akaniangalia tena kama anataka kusema neno, lakini
akaghairi, na mimi kwa muda huo nipo kimia tu!
‘Maswali ya namna gani, ….?’ Akamuuliza huyo jamaa,
‘Aaah… muulize yeye mwenyewe, eti haamini kuwa kaka anadaiwa benki , eti
anahisi deni hilo ni la uwongo, sasa mimi sijui kwa vipi….. ‘akasema.
‘Ila wewe unaamini kuwa deni hilo lilikuwa ni kaka yako…?’
akaulizwa
‘Baada ya kujirizisha,….nilifuatilia nikaja kuona vielelezo,
nikaamini, ….’akasema
‘Ok, ok, mimi sioni kwanini uwe na mashaka na yeye , wakati
anachokifanya ni kusaidia jamii,….mimi nimemuelewa, sasa unaogopa kumuambia
ukweli, wewe ukweli si unaujua, kwanini unaogopa kuusema…..?’ akaulizwa
‘Hapana sijaogopa…, lakini hili swala tulishaliongelea na
wenzenu, kipindi cha mwanzo, …..baadaye wakatuelewa, baada ya kuona ushahidi
wote kutoka benki, sasa huyu anakuja na jambo lile lile,…ndio maana simuelewi,
na ananitia mashaka….’akasema
‘Unajua hayo maswala ya benki yana watu wake…mimi sihusiki
huko, kwahiyo siwezi kuliingilia hilo, mimi nimekuja na mambo yangu,…kuhusu
kifo cha kaka yako ambacho kimetokea kwasababu ya ajali, sasa nilitaka
kukuuliza baadhi ya maswali, ambayo yaliachwa bila kupata majawabu…’akasema
‘Maswali gani hayo,…mbona mnataka kuturudisha nyuma,….tulishaanza
kusahau machungu…’akasema kwa sauti ya huzuni.
‘Ni maswala ya kawaida…kwa jinsi ajali ilivyotokea na eneo
lenyewe na gari ….lakini kabla
hatujaenda huko, je mumemalizana na huyu mtu wa jamii…?’ akaulizwa
‘Bado….naona bado, mimi nilitaka kuelewa kabla hatujafika huko,
huyu mtu kwanini asiende kuwauliza watu wa benki, kama ni mtu wenu lakini… , na
kama sio mtu wenu, huoni kuwa anaweza kuwa ni tapeli…’akasita alipoona
namwangalia, halafu akasema
‘Natumia neno hilo…tapeli, kwa maana yake sio kama
namkashifu, unielewe, maana…, amekuja hapa kutaka kumghilibu shemeji, na sasa
amesababisha hata mtoto kupatwa na matatizo na kwa kifupi sijamuelewa…’akasema.
Mpelelezi akaniangalia akitaka kama anataka kuniuliza kitu lakini nikaona anasita akamgeukia jamaa na
kumwambia.
‘Sawa…..unaonaje akiwa anakuuliza hayo maswala,…si maswala
ya deni linahusiana na marehemu, au sio,
hata mimi nitafurahi kuyasikia, ili tuone huo unaosema utapeli, umenielewa?’
akasema na jamaa akaonekana kunywea, na mpelelezi akasema
‘Hayo maswali, naona hata mimi yatanisaidia sana katika
kufunga jalada la kaka yako, na huenda yakanisaidia kuhitimisha kile
nilichokiona, na haki ikaweza kutendeka, kwa manufaa ya familia …sasa nikuulize
wewe, kwani kuna uzito gani, wewe si
unatakiwa kusema ukweli unaoufahamu, au?’ akamuuliza.
‘Sijashindwa kuyajibu hayo maswali unielewe…ila sio kwa kila
mtu…na mimi unielewe hapo…dunia sasa haiaminiki, kuna watu wajanja wajanja….ok,…sawa
kama wewe umemuamini, haina shida,….’akasema
‘Kwahiyo upo tayari kuyajibu maswali yake…?’ akaulizwa
‘Hamna shida…, ndio nilikuwa nataka aniulize hayo maswali, lakini
yaonekana hayo maswali mpaka yatoke mbinguni sijui…maana kila nikimwambia
aniulize, ana….chelewesha, kwa visingizio mbali mbali, …mpaka namtilia mashaka,
…na aheri wewe umetokea, ili umbane,kama ni tapeli awajibike…’akasema na
mpelelezi akageuka mara moja kuniangalia, halafu akasema;
‘Basi mimi nipo tayari kusikiliza hayo mazungumzo yenu..,
yeye aendelee kukuuliza ,mimi nitasikiliza na kama kuna maswali yatanigusa mimi
kwa upande wangu, usiogope nikiingllia, na kukuuliza, au ….?’ Akauliza
‘Sawa,….haya uliza, …lakini wasi wasi wangu huyu ni nani….?’
Akakubali halafu tukashangaa anauliza tena.
‘Wewe usijali,…mimi nimeshamfahamu, kazi zake zinatusaidia
hata sisi, wala sio tapeli….huyu ni mwanajamii…anaweza kukusaidia hata wewe…’akasema
‘Ok….kumbe mna kitengo cha namna hiyo siku hizi, haya…..
lakini sioni kama kuna umhimu wa kuulizwa tena maswala hayo ya benki
tulishamalizana na wenzenu, na benki… halafu,..ni kwanini mimi, unajua imefikia
hatua ,mpaka najiuliza kwanini mniandama mimi hivi…ni kama vile mnanishuku, au
hamuniamini au kuna nini kinaendelea, mimi hata sijui, matokea yake mnafanya
hata mtoto anapata mateso ‘ Akasema
‘Mtoto yupi…?’ akauliza askari huyo na kabla hajajibiwa
akaendelea kusema ‘…..huyo mtoto anapata
mateso gani….na, yeye anahusikanaje na maswala hayo….?’ Akauliza mpelelezi na
jamaa akasema
‘Najua huwezi kuamini, mpaka yakukute, hata mimi sikuwa
nimeamini mambo haya….Kuna mambo ya mizimu ya baba yake,…..aah, eeh, lakini haina
haja kukuambia, tutapoteza muda, na huenda
usielewe, kutokana na kazi zenu,….ila swala ni kwanini mnifuatilie mimi , mnanishuku
nini mimi….?’ Akasema na kuuliza
‘Kwasababu tumeambiwa wewe ndiye uliyeachiwa majukumu yote
ya hii familia, kweli si kweli…na tukajua wewe unajua kila kitu, au….?’ Yule
mpelelezi akasema na kumuuliza halafu akageuka kuniangalia, mimi, na mimi nikatikisa kichwa kukubaliana
naye
‘Haya …niulizeni hayo maswali, mimi sina wasi wasi kwa hilo,
….kwasababu sio mara ya kwanza, kuna
wenzenu walikuwa na mashaka kama hayo, wakaniuliza maswali mengi tu, mpaka
wakaridhika wakaondoka, sasa nyie sijui mnataka nini zaidi, na sijui kwanini
hamshirikiani , wangewaambia huo ukweli,…..lakini sawa …. Haijalishi kitu,
labda kila watu wana maswala yao,…haya uliza maswali yako….’akasema akinigeukia
mimi.
‘Sasa ni hivi,
….nataka nikuulize maswali fulani fulani,..na ni muendelezo wa yale maswali ya awali, kuhusu deni lilopo
benk, nataka unijibu vyema hayo maswali ya msingi….maana wewe ni mkuu wa hii
familia, sasa kama kweli unaijali hii familia, nataka uonyeshe kwa vitendo, …..’nikasema
na yeye akakaa kwenye sofa na kukunja nne, akaweka mikono mdomoni kama
anayeomba, akawa anaipuliza puliza…
Kitendo kile kitufanya tumuangalia kwanza yeye, na mpelelezi
akanitupia jicho kama anataka kujua jamaa anafanya nini, mimi nikasema;
‘Na usiwe na mashaka
na mimi kuwa huenda ni mtu tapeli kama ulivyosema, ….kazi yangu ni ya kuisaidia
jamii, ….na nia kubwa ni kubaini ukweli wa hilo deni ambalo limefikia kuifanya familia iliyokuwa
ikiishi humu mjane na watoto wake,.... isiwe na amani, na imefikia sasa inataka
kufukuzwa kwenye nyumba yao waliyoachiwa na marehemu…’nikasema , na jamaa akawa anaendelea kufanya kile kitendo kwa
muda halafu akasema;
‘Lakini ukweli wa hilo deni lililopo benki utaupatia huko benki, wao wana
vidhibiti vyote… eti afande, mimi nitakuwa na msaada gani zaidi ya watu wa
benki…?’akasema na akamgeukia huyo
mpelelezi, na kabla huyo mpelelezi hajasema neno, mimi nikadakia na kusema;
‘Mbona hujiamini….wewe subiria uone kama hayo maswali
yanaihusu benki au wewe….’nikasema
‘Mimi najiamini bwana, wewe vipi, haya uliza….wewe niulize hayo
maswali yako….’akasema na mara shemeji
akatokea, akiwa kabeba begi la safari na mtoto Yule mdogo kambeba mgongoni, ….na
alipomuona huyo mtu akasita kidogo, ni
kama anamfahamu au anamfananisha, mimi kwa haraka nikasema;
‘Dada usiwe na shaka huyu mtu wa usalama, …kama nilivyosema awali,
swala lako linafuatiliwa kwa karibu…, ujue kuwa serikali ipo na wananchi wake
kuhakikisha kuwa haki inapatikana, usiogope kudai haki yako, hata kuwe na
vistisho gani, haki ina nguvu, na dhuluma kamwe haiwezi kuishinda haki…..mbona
upo hivyo…?’nikasema na kumuuliza na kabla huyo mama hajajibu, huyo jamaa akadakia na kusema;
‘Lakini hayo ya mtoto kupandisha homa, kuumwa,….na…..nilishakuambia
yapo juu ya uwezo wangu, unielewe hapo, msinibebeshe mzigo usio kuwa wa kwangu,
mimi nimetumika tu, na tuseme kosa langu ni kwa vile nilikwenda huko nikaubaini
ukweli……’akasema na shemeji alikuwa kama
anataka kusema kitu, nikaona kama anasita, nikamuuliza;
‘Dada kuna tatizo…mbona waonekana kutaka kuondoka, unakwenda
wapi?’ nikauliza
‘Tatizo!….haya yote ni matatizo kwangu, hapa nilipo moyo hautulii,
nahisi kama lolote baya laweza kutokea kwa mwanangu…Jamani mimi nimeona bora niondoke kabisa kwenye hii nyumba,…nimeamua
niondoke niende kwetu, humu ndani hakuna usalama, hatulali kwa amani, na mtoto
ndio hivyo,kuuumwa magonjwa ya ajabu…..’akasema
‘Kwanin shemeji,ndio hivyo tunataka kulimaliza hili, usikate
tamaa, kwanini ukate tamaa haraka hivyo, eti shemeji…?’nikamuuliza na mpelelezi
akauliza.
‘Huyo mtoto anakuwaje, anaumwa nini, hebu nipeni maelezo
yake kwanza maana sasa naanza kuvutika na hili tuki…?’ akauliza
‘Mimi hata nashindwa kuelezea, huyu mtoto amekuja kushikwa
na ugonjwa wa ajabu hali ikibadilika anaumwa mpaka anapoteza fahamu,tumeenda
hospitali hana tatizo, …fikiria mtoto anachemka homa mpaka anapoteza fahamu
lakini vipimo vinasema hana tatizo, sasa tatizo ni nini….’akatulia
‘Na kwanini hali yake ibadilike kila nikitaka kufuatilia
haki zao, haki ya nyumba, haki…..na …..mimi sijui,ndio maana sitaki tena
kuyafuatilia hayo, na tatizo ni humu ndani nikienda kuishi kwingine watoto
wangu wanakuwa hawana tatizo, sasa naona tatizo ni hii nyumba, ngoja niondoke,
wachukue tu….’akasema huyo mama kwa uchungu.
‘Lakini shemeji si ulishaambiwa ni kwanini hayo yanatokea, tatizo
ni wewe unakiuka …..’ akasema huyo jamaa,na huyo mama akamkatisha na kusema
‘Ndio maana nimeamua niondoke, siwezi kuchezea maisha ya watoto wangu tena, eti kwasababu ya mali, kama ni jasho langu,
kama ni jasho la watoto wangu, mungu mwenyewe atalipa, na yte namuachia mungu,
kwa mapenzi yake najua ipo siku….’akasema kwa huzuni, na shemeji yake akasema;
‘Lakini shemu ukisema hivyo unamlaumu nani, je kweli deni
halipo, sasa ulitakaje, ni nani atalilipa hilo deni, tutalilipaje, kama hili
halitafanyika, ….na sio sisi, ni benki wanataka haki yao,na deni hilo linamtesa
mumeo…hebu niambie ulitaka tufanyeje…?’ akamuuliza
‘Unataka nikujibu…?’ akauliza
‘Sio unijibu, utoe ushauri wako, unavyoona…’akasema jamaa
‘Je mtoto wangu hataumwa…..maana niliyoyataka kufanya ndio
hayo yamefikia hapa , natakiwa nifunge mdomo, …sasa unaniuliza swali, nikuulize
je nikitoa huo ushauri sitakuwa nimevunja hiyo miiko…?’ akauliza na jamaa
akabakia kama kapigwa kibao. Na mimi nikaingilia na kusema;
‘Dada nakuomba usiondoke, …rudisha hiyo mizigo ndani, na
kamlaze mtoto, …haya mambo tunayamaliza leo hii , wewe niamini kabisa, na huyo
mtoto hawezi kupatwa na hayo marue rue tena…huyu mtaalamu yupo hapa.’nikasema na kumuonyeshea huyu jamaa.
‘Hapana,… nyie msisumbuke tena, mimi nipo tayari niache kila
kitu, wafanye watakavyo, kama ni nyumba wanataka waache wachukue…nawaombeni
mnielewe, hamjui kiasi gani ninavyoteseka…’akasema huyo mama, sasa akionyesha wazi anataka kuondoka.Jamaa
akawa kama anakubaliana na mawazo ya shemeji yake lakini hakutamka neno na mimi
nikasema
‘Sawa dada, kama
wataka kwenda utakwenda, lakini mimi nakuomba kidogo tu dada, ..kuna mswali
tunahitajika kumuuliza shemeji yako, tunahitajia na wewe uwepo…’nikasema
‘Maswali gani, ya kuhusu mali ya marehemu au deni,..hapana
hayo ndio yanahatarisha afya ya wanangu…nab ado mnataka kuyarudia, hivi
jiulizeni kama ingelikuwa ndio nyie, mtoto anaumwa hivyo, mngefanya nini….hebu
niambieni, au kwa vile yapo kwa mwingine…hivi,…hapana,mimi ni mama nina uchungu
na wanangu,….siwezi , …mimi nimeamua kumuachia mungu , najua mume wangu kafa,
yote mapenzi ya mungu,…..’akasema na machozi yakimtoka.
‘Mwacheni aende,mimi nitafuatilia kila kitu…’jamaa akasema
na mimi nikasema
‘Dada niamini mimi,..nakuhakikishia hilo, leo hii
tutalimaliza, kuna maswali ya msingi, tukipata majibu yake basi tutakuambia ni
nini cha kufanya, kwa taarifa yako, hatua mbali mbali zimeshaanza kuchukuliwa,
na haki itapatikana, niamini mimi….’nikasema
na jamaa akanitupia jicho, akitaka kusema neno, lakini akasita akatulia, na
mimi nikasema;
‘Dada ujue kuwa haya maswala sio kati yako na ….hao watu,
sasa ni maswala kati ya serikali inayotaka
kulinda raia zake,ndio maana huyu mtu wa usalama yupo hapa…sasa hiyo
mizimu ije …ipambane na serikali…..’nikasema na huyo mpelelezi akaitikisa
kichwa kukubali.
‘Lakini hamjaelewa,…tatizo ni deni…kwanini hamtafuti njia ya
kulilipa, kama mnaijali hii familia, tatizo sio shemeji au mimi, tatizo ni hilo
deni, mnaelewa hapo, sasa mengine yote hayatasaidia kitu , hata kama serikali
ikiingilia, vinginevyo labda iseme itasaidia kulilipa hilo deni…’akasema jamaa.
‘Deni ndio tatizo, lakini je denii hilo ni halali,…je ni
kweli kuwa deni hilo alichukua kaka yako, hayo ndio maswali tunataka kuyauliza
kwa namna yake,…vinginevyo, nahisi kuna namna…’nikasema
‘Kuna namna…hahaha…’ huyo jamaa akijifanya anashangaa, na
kutikisa kichwa na mimi sikumjali nikamwambia huyo dada;
‘Huyu mpelelezi anayechunguza kuhusu kifo cha mumeo, lakini
hakuja kukuuliza wewe chochote, ilitakiwa kuonana na wewe awali, lakini kipindi
hicho kutokana na hali yako hakuweza kuonana na wewe…na kama angebahatika
kuongea na wewe …nahisi mengi yangelijulikana mapema…’nikasema na jamaa
akanitupia jicho.
‘Sasa hakijaharibika kitu…ukweli wote sasa utabainika, …na
haki itatendeka, na wewe mwenyewe moyo wako utakuja kutulia, kwani utakuwa
umetimiza wajibu wako, ….kupigania kile alichokiacha, na ka kufanya hivyo, haya
yote yanayotekea hapa yatakwisha, ….maana mengine ni mitihani tu…’nikasema
Mdada huyo akawa anatikisa kichwa kama kukatakaa….na shemeji
akaonyesha ishara ya kama anasema unaona…haina haja..tunapoteza muda tu..kitu
kama hicho, ..lakini mimi nikampuuza na kusema;
‘Ila kwa sasa mpelelezi huyu anataka kuongea na shemeji
yako, na kwa vile kamkuta hapa,…itakuwa vyema kwetu maana atahakikisha kila kitu kinakwenda sawa, nikimaliza
maswali yangu kwake, ataendelea na mpelelezi , …na nina uhakika, tutamaliza
kazi…’nikasema nikimgeukia huyo
mpelelezi
‘Sawa kabisa, …shemeji usiwe na wasiwasi…..hilo ni jukumu
letu…usiwe na shaka, ….’akasema huyo mpelelezi, na jamaa yetu kwanza
akamuangalia shemeji yake….kwa jicho la aina yake,…, halafu akamgeukia huyo
mpelelezi, …baadaye akaniangalia mimi…na kusema;
‘Haya mimi nipo tayari kwa maswali yako uliza…’akasema, na
shemeji yake akataka kuongea kitu lakini nikaona amesita kutamka neno, akabakia
kimia akiwa bado kasimama na begi lake, na huku kamshikilia mkono Yule mtoto
mkubwa na Yule mwingine yupo mgongoni.
NB: Ni nini kitatokea....mdada kasalimu amri, akiangalia watoto wake, mjamaa, anapambana akiangalia mali( nyumba) iuzwe ili deni lilipwe, je...ni nini kitatokea.
WAZO LA LEO: Tusiogope
kutafuta haki zetu, japokuwa wakati mwingine tunajikuta kwenye mitihani,
mitihani hiyo tuichukulie kama ngazi za kuifikia hiyo haki. Tukumbuke kuwa haki
wakati wote ipo juu ya dhuluma.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Hi, i feel that i noticed you visited my website so i came
to go back the choose?.I'm attempting to find things
to improve my web site!I guess its adequate to use a few of your
ideas!!
Post a Comment