Ni wakati ule mjane, ambaye namuita shemeji anataka
kunipatia vielelezo vinavyohusikana na mkopo uliosababisha nyumba hiyo kupigwa
mnada, …ndio wakati ule mtoto alipoanza kuumwa, hali ilimbadilikia ghafla,
mtoto akaanza kutetemeka, kumchunguza joto lipo juu ….
Cha ajabu kabisa mtoto mwanzoni alikuwa mzima, hana dalili
yoyote ya kuumwa, sasa anachemka homa, anahema kwa shida na ghafla mtoto
akalegea, …akawa kama kapoteza fahamu…na muda wote huo tunahaha, mama anakwenda
huku anarudi kashika kichwa, huku akisema ;
‘Mungu wangu…nimefanya nini,….. mungu wangu…..nisaidie…..’
‘Kwani tokea asubuhi alikuwaje…?’ nikauliza
‘Alikuwa mzima,..ndio hayo niliyokuwa nikikuambia, unaona
sasa…sitaki haya mambo tena, sitaki jamani mtoto wangu jamani…..’akasema huku
anapiga miguu chini..
‘Lakini hii ni homa…tena homa kali, sijawahi kuona hivi,..
tunatakiwa tumpeke haraka hospitalini….’nikasema
‘Wewe hujui tu…..nilikuambia, inakuwaga hivyo,…jamani sasa
nitafanya nini…na shemeji ndio hayupo, yeye ndiye anajua la kufanya ikitokea
hivi, …..ngoja kuna dawa huwa anampakaga, lakini sijui anafanyaje….kuna jinsi
anamuombea mimi sijui…halafu…’akasema huku akitaka kwenda huko ndani, mara
anarudi, alikuwa kachanganyikiwa kabisa.
‘Hiyo dawa iko wapi sasa….?’ nikamuuliza
Kwa hali ya huyo mtoto sikuona umuhimu wa kuendelea kukaaa
hapo, mimi nilataka tumpeleke hospitalini, ….maana sasa lawama natupiwa mimi,….
Nikaona nipambane sasa kama mzazi, kwanza nikamfanyia huduma
ya kwanza, kujaribu kumzindua, nikawa nakanda kanda yule mtoto na maji,…na kwa muda
huo mtoto alikuwa kalegea kabisa, ni
kama vile kapoteza fahamu, hahemi kabisa, joto lilikuwa juu, sasa nashika
miguuni ….nilishituka miguu imeanza kuwa ya baridi, ubaridi usio wa kawaida…
mtoto kimia, hapo na mimi nikaanza kuogopa.
Kwa mashaka nikajaribu kuangalia mapigo ya moyo, ….hakuna
kitu, mapiga ya moyo hayasikiki…mhh….sasa nimesababisha makubwa, moyoni
nikasema sasa ukiona mtu anafungwa ndio
hapo, maana huyo mama kweli alinikanya, sikusikia,….nikasema;
‘Unajua shemu, ….huyu tumpeleke hospitalini…’nikasema
‘Nilikuambia,…nilikuambia..ndio haya yametokea sasa,
unaona….jamani nitampoteza mtoto sasa…’...mimi sasa nikaanza kumuomba mungu, kwa
duwa zote nizijuazo, mtoto yupo kimia,
ni kitendo cha muda mfupi, lakini jasho lilinitoka….
Hali ya mtoto ikawa haionyeshi dalilii yoyote, ya matumaini,
….lakilini akilini wazo jemanililoliona
ni kumpele lakini kwa vipi, ….
Na kabla sijasema lolote zaidi ndio mara mlango ukagongwa, …
*********
Mgongaji aligonga tu…kuashiria kuwa kuna mgeni, lakini mlango ulikuwa wazi, huyo mgongaji
akaingia, alikuwa jamaa mmoja kavalia suti safi yaonyesha ni bosi fulani au
sijui…na, mkononi kashika briefcase,
ni kama ofisa katokea safari kutoka
Ulaya, ….mimi kwanza sikujua ni nani, ila huyo mama ndiye aliyeanza kusema;
‘Oh ahsante mungu, Shemeji karibu, ….aheri umekuja, mtoto
kazidiwa tena….’huyo mama akasema akionyesha matumaini, mimi nilikuwa
nimeganda,nikiwa sasa napoteza matumaini kwa mtoto…. lakini akilini nilitaka
mtoto apelekwe hospitalini, nikijipapasa mfukoni sina kitu!. Patamu hapo…
Yule jamaa kwanza aliniangalia, halafu akasogea hadi pale
nilipokaa na huyo mtoto, akamshika huyo mtoto shavuni kupima joto….alivyokuwa
akifanya utafikiri docta, akatikisa kichwa kama kukubali kitu,…akamshika
miguuni, akamuachia kwa haraka, …akaguna tu `oooh,…’
‘Imepita muda gani…?’ akauliza
‘Hata robo saa haijapita…’akasema shemeji yake.
Akashikanisha viganja vya mikono baada ya kuvipuliza, halafu
akaviwekea viganja vyake kichwani kwa huyo mtoto, akawa awewesa maneno, sikuweza kuyasikia vyema,
mdomo ulikuwa ukicheza cheza tu, alifanya hivyo kwa muda, mtoto kimia,
akamwangalia mama yake, akatikisa kichwa, akasema;
‘Mumefanya nini tena shemeji…mnataka kuua mtoto nyie…..Nipe
ile dawa ya unga…..’akamwambia shemeji yake. Mimi simu ikawa inaiita lakini
sikutaka hata kuipokea, ….
‘Pokea simu yako….’akaniambia, na mimi nikaitoa simu yangu
kutoka mfukoni, na kuiminya kupokea,
ilikuwa ni maelezo ya vijana wangu kwa kazi niliyowapa kufuatilia maswala ya
huyo mama, nikawa nasikiliza kwa muda, …nilichosikia kilinifanya nianze kuwa
mashaka, nikamuangalia huyo jamaa akiwa anachezesha chezesha viganja vyake vya
mkono, akivisugua sugua huku na badaye
kuvipuliza, akawa anafanya hivyo kwa muda
Mimi nikawa naendelea kusikiliza maelezo ya vijana wangu
mmoja baada ya mwingine, halafu nikasema;
‘Nyie endeleeni…tutaongea baadaye,…nipo site…’nikasema na kukata simu,
Nilitaka kuurudidhs ile simu mfukoni , lakini nikakumbuka
kitu, … sasa akili ilishaanza kufanya kazi, nikajua sasa nipo kwenye mapambano,
sitakiwi kupoteza kitu, nikaiminya simu sehemu
ya kurekodia matukio, bila jamaa kufahamu, nikaiweka ile simu kwenye meza.
‘Hizi simu kwa sasa nazona hazina maana, nimechanganyikiwa
kuhusu huyu mtoto….’nikasema huku nikiiweka ile simu pale mezani.
‘Hiyo simu ya bei mbaya, unaweka hapo unaweza ukasaishau, na
watu leo wanaingia humu ndani na kutoka…’akasema huyo jamaa akiitizama pale
nilipoiweka.
‘Ni za kawaida tu…sitaweza kuisahau…nikisahau wewe si
utanikumbusha au..’nikasema kama nauliza
Mara shemeji akaja na karatasi imekunjwa, kuonyesha kuwa
kuna dawa ndani yake au kitu kimefungwa humo, akampa huyo shemeji yake, shemeji
yake akaifunua na kutoa kitu kama unga unga hivi, kwenye vidole na kuweka puani
mwa huyo mtoto, na mara huyo mtoto akapiga chafya, mara tatu…..
‘Tayari, keshaondoka huyo….’akasema
Baadaye akawa anasema maneno fulani huwezi kuyasikia
vyema,…., akampaka Yule mtoto usoni ile dawa, halafu taratibu bila wasi wasi
akasogea hadi kwenye sofa, akakaa, na
kukunja nne, yaani utafikiri docta anayejua anachokifanya, inaonekana huyu jamaa ana majigambo fulani
hivi.
Mimi nilikuwa bado nimempakata huyo mtoto, na Yule mtoto
sasa akaanza kujitikisa na baadaye akawa anajiinua kutaka kusimama, lakini
akawa bado hana nguvu, nikamsaidia kuinuka, akasimama…hapo nikapumua, eehuuuuh,
…..
Mtoto akasimama akitaka kuinua mguu, akawa anayumbayumba, nikajiinua kidogo na kumshikilia,
bado nilikuwa sina imani, moyoni nataka tumpeleke huyo mtoto hospitalini.
Nikasema;
‘Jamani huyu mtoto tumpeleke hospitalini…hii hali sio ya
kukaa nyumbani’nikasema
‘Haina haja,…’akasema huyo jamaa, sasa nikainua uso na
kumuangalia vyema huyo jamaa usoni, nahisi niliwahi kumuona mahali,…sikumbuki
wapi, hata hivyo,kwa muda ule akili yangu ilikuwa bado kwa mtoto..
‘Huyu mtoto kwa hali hiyo inabidi tumpeleke kwa docta bingwa
wa watoto, msiseme tu haina haja, mlishawahi kumpeleka huko kwa docta bingwa wa watoto, kama tatizo kama
hili huwa linajirudiarudia ujue kuna kitu anatakiwa kuchunguzwa….?.’nikauliza.
‘Hayo sio maradhi ya kupelekwa hospitalini, hata hivyo,…ni
kweli mtu akiumwa, hasa mtoto inatakiwa kufanya hivyo, na sisi mwanzoni tulifanya
hivyo, kwa vile tulikuwa hatujui na haikusaidia,…..’akasema
‘Kwahiyo….’nikasema na yeye akapiganisha viganja kama
anajifuta kitu akasema
‘Kwahiyo….?, kwahiyo nini, haina haja kumpeleka hospitali,…,
kwa hivi sasa yupo safi kabisa….’akasema huyo jamaa akiangalia dirishani, hana
wasiwasi, ….
Na kweli Yule mtoto
sasa akawa kachangamka, akamwendea mama yake, na mama yake akamwinua na kumpakata
miguuni mwake…., mama alimuangalia mtoto wake kwa macho yenye huzuni, …na mara
machozi yakaanza kumtoka huyo mama, pale nilipo nilihisi hasira, sijui ni
hasira za nini…nikageuka kumuangalia huyo jamaa. Alikuwa sasa kashika simu,
anachat, au …huku akisema haya maneno;
‘Hawa watu bwana….wanataka kuja kesho, duuh, sasa ninani ,
hapa ni mwenye kisu kikali, …..hawa watu wana haraka….ngoja tuone.’akainua uso
na kumwangalia shemeji yake, akamuona shemeji yake machozi yakimtoka, alipoona hivyo akasimama na kumsogelea shemeji
yake, huku akisema;
‘Shemeji lakini si nilikuambia, … usivunje miiko, unaona
sasa, unamtesa huyo mtoto bure,…kuna kitu ulitaka kukifanya, kweli si kweli….,
ulitaka kufanya nini, au umefanya nini,?’ akamuuliza shemeji yake lakini
shemeji akawa anatoa machozi tu.
‘Shemeji, wewe unajua kabisa,…. baba yake hataki mambo hayo,
…si unakumbuka maagizo tuliyopewa…sasa haya ni matokeo yake, kwahiyo ukilia,
haisaidii kitu kama hutatimiza hayo uliyoambiwa,….kutokutii hayo maagizo…itakuwa
hivi, na sasa ni kubaya zaidi.’akasema jamaa
‘Samahan kidogo, umesema baba yake hataki, baba yake yupi
hataki mambo hayo, baba yake si….., marehemu au ?’ nikauliza na kabla
sijajibiwa nikauliza swali jingine…
‘Na hataki mambo gani?’ sasa nikawa nimemkazia macho huyo
jamaa na huyo jamaa akaniangalia na kusema;
‘Shemeji anajua,…’akasema akionyesha dalili za kunishangaa,
alinitizama kwa muda halafu akageuka kumuangalia shemeji yake.
‘Na mimi nataka kujua pia, maana hii sio hali ya kawaida…mtoto
anakuwa hivyo, halafu ….hapana, niambieni tatizo ni nini…’nikasema kama mtu
mwenye mamlaka
‘Kwanza wewe ni nani unayetaka kujua mambo ya nyumba hii?’
akaniuliza akigeuka kuniangalia, ilikuwa sauti ya msisitizo kama mwenye nyumba.
‘Mimi kama uncle wa huyo mtoto,….nataka kujua kwanini
imekuwa hivi, mtoto alikuwa mzima ghafla akaanza kuumwa, na wewe umekuja,
umemshika kichwani akapona,….na hutaki tumpele hospitalini, kuna nini kinaendelea kwenye nyumba hii,… ,
hebu dada niambie..’sasa nikajifanya ni kaka wa huyo mama, ili niweze kufanya
mambo yangu.
‘Ndio hivyo, kama ulivyoona, inaniuma kwa kweli,lakini
nitafanya nini, ni hivyo kama ulivyoona akianza kuumwa hapo ni …aah, inakatisha
tamaa, sasa sijui, kama ni hiyo mizimu sijui, kwanini iwafuate watoto wangu…,
hawa watoto masikini ya mungu wana makosa gani, …wangenifuata mimi basi, si
mimi mkosaji, basi iniandame mimi, sasa..sasa…kwanini wananitesea watoto
wangu….’akasema huyo mama kwa uchungu.
‘Anayewatesa watoto ni wewe usiyetaka kuelewa shemeji, mimi
nilishakuambia hilo, hiyo ni mizimu, huyo ni baba yake, hataki maswala hayo
unayoyataka kuyafanya wewe….., nilikuambia kabisa achana nayo, naona kama
ulitaka kufanya kitu, unataka kufanya nini wakati kesho hawa watu wanakuja
kumalizia tatizo,…hivi nikuulize wewe unaona nyumba hii ina maana sana kwako,…’akasema
akionyeshea kidole kuzungusha akielekezea juu.
‘Shemeji, hawa watoto wakipata shida watakuja kukulaumu wewe
kwa kuangalia mali zaidi,..muhimu ni afya yao, muhimu ni uhai wao,…hivi huyo
mtoto akifa, hatuombei mabaya, lakini kwa jinsi tulivyoambiwa, ukichelewa
tu,….ukiendelea kufanya hivyo mara tatu, ikamtokea mara zaidi ya tatu, mtoto
utamkosa, sasa utakuwa na furaha gani, hata ukiipata hii nyumba na mtoto keshakufa….hutakuwa
na raha yoyote…’akasema huyo jamaa.
‘Samahani kidogo
hapo…, ni nani atamuua huyo mtoto ndio hiyo mizimu, au….mimi nijuavyo mtu akifa
anakufa kwa mapenzi ya mungu au sio,…’nikasema na huyo jamaa akanitupia jicho
la dharau, halafu akasema;
‘Lakini ….eeh, wewe
mwenyewe si-umeshuhudia hapa, huyo mtoto
alikuwa na hali gani, , ….jinsi mtoto alivyobadilika, si uliona, sasa nikuambie
kitu, sisi hayo, tulihangaika nayo, mpaka basi, hebu jiulize, ….je sasa nisingelitoka
kwa muda muafaka ingekuwaje, hebu niambie unafikiri kingetokea nini hapo, walisema
ikitokea hivyo, mtoto akaachwa saa moja,…basi…tunakwenda kuzika’akatikisa kicha
kusikitika
‘Kweli…..?’ nikasema
‘Ndio, akiwa katika hiyo hali, damu imesimama,…akaachwa
zaidi ya saa moja akiwa kapoteza fahamu, ndio basi tena, ….na hii ya kupoteza
fahamu ni dalili mbaya, mwanzoni alikuwa hapotezi fahamu , ni joto tu kuwa
kali, sasa hii,…ya kupoteza fahamu kutokana huyo mtaalamu alivyosema hiyo ni
dalili mbaya shemeji …achana na hiyo tamaa, nyumba, nyumba ….nyumba kitu gani
mbele ya uhai wa mtoto ,….’akasema akimuonyeshea kidole shemeji yake.
‘Lakini sijafanya kitu shemeji….huyu ….huyu , she-, eeh,
kaka yangu, alikuwa akiniulizie jinsi gani tulivyofuatilia, nikataka
kumuonyesha jinsi tulivyohangaika, sasa…..’shemeji akamkatiza kwa kusema.
‘Shemeji hao jamaa hawadanganyiki,..unajidanganya
mwenyewe…’akasema , halafu akanigeukia na kusema.
‘Jamaa gani hawadanganyiki..?’ nikauliza
‘Mizimu….’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine
akasema;
‘Unajua ndugu, Sisi tumemuhangaikia sana na huyu mtoto na ndio tukaambiwa ni baba yake
hataki maswala ya kesi, …na baya ni kuwa kaondoka duniani akiwa kaacha deni,
hilo deni linamtesa, kwahiyo anataka hilo deni lilipwe kwa gharama yoyote
ile,….ili yeye aweze kupumzika huko alipo, kauli ya marehemu ni muhimu sana,
maana hatujui huko anapata shida gani….., sasa huyu shemeji yangu sijui haelewi…’akasema
‘Ohooo kwahiyo kumbe, nilikuwa sijaelewa, ….kwahiyo kumbe
mtoto alipoanza kuumwa ndio mkaenda kwa mganga,au sio? Si ndio hivyo au? Na huko
mkaambiwa kuwa tatizo lake sio la
hospitalini, ni maswala ya kimila, au sio…?’ nikauliza na kujifanya nipo pamoja
na yeye
‘Haswa,…..lakini hatukuanzia kwa mganga, hapana…..wewe,
usininakili vibaya,…sisi sio watu wa namna hiyo…kwanza tulihangaika na mambo ya
hospitalini, kila akipimwa hana tatizo, mtoto anazidi kuteseka, homa haishuki….mtoto
anaweweseka, wengine wakasema ni degedege, wengine UTI, naimonia na nini sijui
..lakini kwenye vipimo hakuna kitu kama hicho….wakatibia aah wapi, …..’akaonyesha
kwa kidole mdomo akitamka hiyo `aa wapi…’
‘Ni kama ulivyoona leo, ….je nikuulize wewe , ulipokuja hapa
ulikuta huyu mtoto anaumwa….?’ Akaniuliza
‘Hapana alikuwa mzima kabisa…sikumuona na dalili yoyote ya
kuumwa…..’nikasema
‘Sasa umeona, kuna mambo yakifanyika mambo amabyo yanakwenda
kinyume na matakwa, maagizo tuliyopewa, miiko….mtoto huyo huanza kuumwa,…’akawa
anachezesha mkono kama anaongea jambo, lakini sasa akawa hatamki neno baadaye akasema;
‘Ujue na sisi awali tulikuwa
hatujui hilo….tunahangaika huku na kule, hospitalini ,dawa hizi na zile…wakati tunafuatilia, maswala ya mkopo, maswala ya
deni, kumbe hayo ndio tatizo,hatujui masikini,, twauliza huyu mtoto ana nini,
mbona hivi, mtoto anaumwa haponi….homa inageuka sasa kama anapandisha mashetani,
mtoto mdogo apandishe mashetani, wapi na wapi, ….tuliona ajabu
sana….hospitalini akipimwa, hana ugonjwa,…’akatulia
‘Mara kwa bahati akatokea mzee mmoja, akasema nyie huyu
mtoto mpelekeni kwa mtaalamu,…kwa mtaalamu!, ….’akasema akitamka neno hilo la
mwisho kwa mshangao.
‘Ndio….tukabakia kuulizana ni nani huyo mtaalamu…. Unajua
tena sisi wa siku hizi mambo ya waganga
wapi na wapi….lakini sasa tufanyeje, na mimi ndiye baba yao, nikamwambia shemeji
hilo…shemeji naye ndio mambo hayo hayajui kabisa, …nikaona na yeye anasita
sita, Mimi nikaona hakuna jinsi, mimi ni baba yake…nikaanza kazi ya
kuulizia,maana hao watu wapo wengi, na wengine hawaaminiki…nikampata
anayestahiki….’akaonyesha mkono wa kishujaa akiwa kakunja ngumi.
‘Na kwa bahati nzuri kipindi hicho hapa nyumbani kulikuwa na
ndugu yake shemeji, yeye alikuwepo hapa kumsaidia dada yake…yeye ni mkubwa kwa
shemeji, ana akili za utu uzima akajitolea kwenda na mimi, ….tukaondoka naye…kama
angelikuwepo mungemuuliza vyema yeye, ….maana mimi nikisema mtaona labda
aah...lakini ujue mimi ni baba yake mdogo, mimi ni mzazi wa mtoto pia, nina
uchungu zaidi….’akatulia
‘Ni sawa nakuelewa, ikawaje….’nikasema
‘Sasa tulipofika huko…ubosi ukanitoka, si unajua tena mambo
ya huko, yalivyo, kuna msharti sharti, ukifika utajionea mwenyewe, … ikanibidi
…nikakalishwa chini, kuna vitu vya ajabu ajabu unatapakwa mimi hapo ni mzazi wa
mtoto…. utafanya nini tena hapo, huko ndio tukaambiwa tatizo ni hilo….’akatulia
‘Mliambiwa tatizo ni nini….?” Nikauliza na yeye akatikisa
kichwa na akawa kama anacheka
‘Kama nilivyokuambia awali, kuwa marehemu kaacha deni,…na
marehemu anataka deni hilo lilipwe, na kingine
yeye hataki mambo ya kesi kesi,hapendi kesi na kweli toka kaka akiwa hai huwa
hapendi maswala ya kesi kesi….lakini cha muhimu ni kuwa…hilo deni lilipwe kwanza,
sasa kama kutakuwa na jingine la kutuhusu sisi wa duniani, haya, lakini kwanza
deni..’akatulia
‘Ni nani anasema hivyo…?’ nikauliza
‘Wakati huo anayeongea ni huyo mtaalamu, lakini akiwa kapandisha
na sauti tunayosikia kwa muda huo ni sauti ya marehemu kaka, ….’ooh, waungwana, nawaambia nimeondoka duniani
nikaacha deni, hilo deni linamtesa huku nilipo…fanyeni kila mbinu lilipwe
haraka….’ Akawa anaigiza sauti nyingine.
‘Mimi pale sikujivunga, maana nitadanganya, nitapatia wapi
hizo pesa zote…nikasema hatuna hizopesa
tufanyeje, …deni hilo ni kubwa sana, …sauti ikasema ‘hata kama ni nyumba iliyokuwa
yangu, na iuzwe ili deni lilipwe haraka,….vinginevyo,…’hapo akasita halafu
akasema
‘Sauti ikasema , ikatoa onyo kuwa hilo deni lisipolipwa
haraka, … mmoja baada ya mmoja ataondoka….’akatulia akimuangalia shemeji yake.
‘Hiyo ilikuwa lini,…?’ nikauliza huku naangalia saa maana
nilitakiwa kukutana na watu wangu, kuna jambo walitakiwa waniambie.
‘Lini kwa vipi….?’ Akaniuliza na yeye akiangalia saa yake
‘Yaani ni muda gani
tangia hilo tatizo la mtoto lianze?’ nikauliza
‘Mhh, eti shemeji, nisaidie hapo…hivi, mtoto alianza hayo
matatizo lini,maana sikumbuki, mambo yamekuwa mengi, mara yeye ….unajua hata
kuumwa kwa shemeji, kumbe mambo ni hayohayo, hatukujua, yalianzia kwake…..shemeji
hali yake ilikuwa mbaya sana,..sasa kidogo unamuona hivyo , tena sio kidogo,
unaona anatembea sema ….yupo imara kiimani, …..muulize mwenyewe ilikuwaje…’akasema
‘Ok,…sasa mimi nauliza kuhusu huyu mtoto kuanza kuumwa
ilianza lini,…..?’ nikauliza huku naangalia simu pale mezani niliona kama
imezima..lakini mara nikaona ishara kuwa bado inafanya kazi.
‘Tuseme eeeh…mimi nafikiri, hata mwaka haujaisha, ni
karibuni tu, yalipoibuka haya maswala ya kesi kesi au sio shemeji.. ….’akasema
akimuangalia shemeji yake.
‘Yalipoibuka hayo maswala ya benki au sio,shemeji yako
alipojua kuwa kuna deni na nyumba inatakiwa kupigwa mnada au sio.. na hasa
alipoanza kufuatilia, au sio…na alipokwenda polisi wakachunguza wakagundua kuna
jambo nyuma ya pazia, kuhusu hilo deni,….sasa hapo mizimu ikaibuka, wameona dili inataka kufichuliwa, au sio…?’
nikauliza
‘Unataka kusema nini hapo, sijakuelewa….?’ Akauliza
akiniangalia usoni, niliona hali ya mashaka i machoni mwake.
‘Unasema huko kwa mganga ulikwenda na ndugu yake shemeji, ni nani huyo.?’ nikauliza
kama vile nawafahamu hao ndugu zake shemeji yake wakati hakuna hata mmoja
ninayemfahamu lengo nikimuweka huyu jamaa sawa asinishutukie mapema.
‘Kuna ndugu yake mmoja, …nimekuambia ni mkubwa wake shemeji,…shemeji,
hebu mwambie ni nani,…maana sasa naona nimechoka kuongea, tatizo unauliza
maswali kama polisi, hao polisi wenyewe walinisumbua wee mwishowe wakasalimu
amri….’akatulia
‘Polisi waliniuliza maswali.., utafikiri mimini mhalifu,
hawajui kuwa mimi ni mzazi wa hawa watoto, nina uchungu zaidi ya wanavyofikiria
wao, na. unauliza kuhusu huyo ndugu yake shemeji, …huyo ndugu yake shemeji
tulikwenda naye…akaona hivyo vitu vya huyo mtaalamu,…na tulipofuatilia
wanavyotaka wao hali ikawa nzuri, muulize mwenyewe shemeji , mtoto akawa na
afya yake nzuri tu, sasa nahisi kaanza tena, keshasahau…’akasema
‘Ninachojiuliza ni kwanini hayo yatokee kipindi hicho, kipindi hiki yaani… kwanini hayakutokea huko
nyuma, kwasababu ….mume wa dada alifariki
muda, au sio..sikubahatika kufika hapa…, lakini ni muda sasa, kwanini hayo
matatizo yakudai kuwa ana deni, hayakutokea kipindi cha nyuma baada ya mume wa dada kuondoka, yaje
kutokea wakati shemu anatafuta ukweli…si kumepita muda, eti…hapo ndio nauliza?’ nikauliza
‘Sasa hayo mimi sijui….kamuulize huyo shetani anayemtokea huyo
mtoto, ukiniuliza mimi…nitakuambia nini, … nitajuaje hayo ni kwanini, marehemu
huko anajua ni kwanini,huenda katika kuhojiwa ndio ilikuwa imefikia muda
muafaka wa hilo swali, …’akasema
‘Kwahiyo huyo anayemtokea huyo mtoto ni shetani..?’
nikauliza
‘Sasa utamuitaje,….eeh, hebu niambie wewe,….’akasema
akiniangalia, halafu akasema;
‘Na ujue , haya mambo ni ya ajabu sana, unajua marehemu anaweza kujitokeza kwa njia yoyote
ile ili kuleta ujumbe wake…unaweza ukamuota kwenye ndoto, hiyo ni ahueni…na hawezi kujitokeza mwenyewe, si unajua hilo, maana akijitokea mwenyewe…ooh,
si tutakimba, kwahiyo yeye kaamua
kujitokeza kwa kupita kwa mtoto wake...’akasema
‘Huyo Shetani sio,….?’ Nikauliza
‘Eeeh bwana, ….hunielewi…na sauti tuliyoisikia ni ile ile ya
kaka, mimi naijua vyema …’akasema.
‘Lakini si umesema ni shetani, au nimekosea, kinachomtokea
mtoto ni kama mashetani, ulisema hivyo,..na nijuavyo mimi, shetani huwa hashauri
mambo mema au sio, anaweza kushauri
mambo mkayaona mema kumbe yana mtego, yana ajenda ya siri..?’ nikamuuliza na
kuelezea hivyo.
‘Inategemea na aina ya shetani kuna….kuna, hayo madudu
yanakuwa mazuri, yanakuja kwa nia njema,…mizimu, hapo tunazungumizia tuseme
mizimu, naona nikitumia neno shetani, unakuwa huelewi,….ni mizimu,kuna yenye
nia njema na mbaya na pia wengine wanaweza kufanya yote mawili, wao si wana
uwezo huo, ..’akasema
‘Nikuulize kitu kwanza ili tuwekane sawa, naona unabadili
maelezo yako ya awali kuhusu shetani, ni wapi wamesema hivyo,maana kwa vyovyote
utakavyowaita ni hao hao, mizimi, vibwengo, hao wote ni mashetani,…mimi
nijuavyo kwenye vitabu vya dini shetani ni muasi,shetani aliasi , alikataa amri
ya mungu ndio akaamua kutupoteza na sisi wanadamu, au sio….sasa iweje tukubali
maagizo yake, na yeye alivyo ana mbinu nyingi, anaweza kutumia mbinu kadha wa
kadhaa…?’ nikamuuliza na maelezo juu.
‘Sasa huko unapokwenda, aah,…. mimi sio mtaalamu nako, sina
ufahamu huo ….mimi nafuatilia aliyosema huyo mtaalamu…yeye anajua yote,….yeye hiyo
ni fani yake, na kuhusu kasoma sana, dini anajua, alituchambulia maandiko wenyewe tukaduwaa, kwahiyo sio kwamba hajui
dini, anaijua vyema na hata wewe ukienda ukamsikiliza utajua kuwa kweli
anafahamu yote, …au nikupeleke kwake, ukamsikie mwenyewe, kama hutaamini…….’akasema
‘Huyo mtaalamu unamuamini vipi…maana mtu na biashara zake
bwana, ni lazima atajua jinsi gani ya kumteka mteja wake akili, si anataka
kuvutia wateja wako…., sasa wewe ulimuaminije, unamfahamu vipi,…najua wewe ni
dalali, unajua hayo au sio?’ nikamuuliza na nilipotaja neno udalali, nikaona
anashtuka! Nilishamkumbuka huyu jamaa pamoja na kazi nyingine pia anafanya kazi
ya udalali.
‘Hayo maswali gani sasa,….sisi tulichotaka ni mtoto kupona…unaona
ndugu, hayo ya udalali yanakujaje hapa…sisi tulihangaikia mtoto, na katika
kuulizia tukaambiwa kuhusu huyo mtaalamu, ndio tukaenda kwake,…ndio hapo na
mimi nikamfahamu, ina maana mimi nilifanya vibaya , kwa vile mimi ni dalali, au
una lako jingine, na kwanini unachunguza chunguza, ili iweje,…hebu niambie
unataka nini…unanishuku….?’akasema sasa akionyesha kubadilika.
‘Hapana, …sina nia mbaya na wewe …najua wewe ni mzazi wa
huyu mtoto na ulitakiwa kuhangaika sana, nashukuru kwa hilo, maana hata kwa
jinsi ulivyoweza kumtibia huyu mtoto hapa, ooh, nimekuaminia…sasa mimi nataka unielewe,….hili
tukio kwakweli limenigusa sana, ndio maana nataka kujua hatua kwa hatua, ili
nisije kuhangaika na mimi, wakati wewe ulishafanya jitihada….’nikasema kumweka
sawa.
‘Ndugu ..unajua nyie watu mnaojifanya wazungu , au nisema wa
kileo, nikiwemo mimi, ….mnasahau mambo ya kimila, wazee wetu hawakuwahi kwenda shule
kipindi hicho, walikuwa wanajitibiaje…?’ akawa kama ananiuliza hakusubiria
nijibu akasema
‘Wazee wetu, walikuwa wanajuaje matatizo yao, ni kwa njia
hizo, tunazozipuuza ….kulikuwa hakuna hospitali, hospitali ni kwa wazee wetu
ilikuwa kwa hao wataalamu, waganga wa kienyeji,…na wao dawa zao zaidi ni miti
shamba, na kufuata masharti fulani fulani….na zaidi walikuwa wakifuata mizimu
na mambo yao yalikwenda vyema , hebu angalia hivi sasa na usasa wetu…., mambo ni magumu,maisha ni
magumu….sababu ni haya maswala ya kupuuza
mambo ya mila..’akasema sasa akiongea kwa utaratibu.
‘Kwahiyo wewe kwa hivi sasa unafuata mambo ya mila, unaabudu
mizimu, na naona umekuwa mtaalamu na wewe au sio?’ nikamuuliza
‘Sijasema mimi nafuata mambo hayo, wala siabudu mizimu,
lakini mambo yakizidi inabidi …na katika kufuatilia haya ndio nikajifunza kuwa
kumbe haya mambo yapo, maana huyu sio wa
kwanza kwenye familai yetu kuna ndugu wanapandisha hayo mapepo, ….tulihangaika
sana, tulipofuatilia tukaambiwa tulikiuka miiko,…mila fulani fulani… tukafanya
walivyotaka hao mizimu…’akatulia
‘Kwa huyo huyo mtaalamu…?’ nikamuuliza
‘Hapana alikuwa mwingine…huko kijijinu kwetu…’akasema na
kabla sijamuuliza swali jingine akaendelea kuongea
‘Na mizimu ni mababu na mababu zetu uelewe hilo….ndiyo haya
yanamsumbua mtoto, lakini hilo la deni lipo wazi, ni kweli kuna deni, kaliacha
kaka, na deni hata kidini latakiwa kulipwa hata kabla marehemu hajazikwa, sasa
sisi hatukuljua hilo deni ndio maana hata mimi niliposikia hivyo nikaamua
kufuatilia..’akasema
‘Wewe ulipojaribu kufuatilia kulitokea nini kwa watoto
wako…au ….maana si hivyo, ulikiuka miiko,au sio… kwa muda huo…ni kitambo etu..,
sawa si sawa, kwanini kusitokee kitu kama hicho muda huo, hapo ndio najiuliza,
unaweza kunijibu hilo…?’ nikauliza na yeye akatikisa kichwa kama kusikitika.
‘Unajua wewe hunielewi….na nimekumbia maswali mengine yapo
juu ya uwezo wangu, ni kwanini, hayakutokea muda huo eeh, sijui nini…, mimi
siwezi kujua….mimi sina ujuzi huo, labda turudi kwa huyo mtaalamu
tukamuulize…’akasema
‘Ok,ok…naona muda unakwenda, …kwahiyo wewe unajua jinsi
gani ya kumfanya huyu mtoto apone… hiyo
hali ikitokea, kama ulivyofanya hapa kwa mtoto, kwanini hukumfundisha shemeji
ili ikitokea na yeye afanye hivyo..?’ nikamuuliza
‘Ndio mimi najua na ni mimi tu naweza kufanya hivyo, yeye
hawezi, maana …kuna miiko hapo, sasa siwezi kukuambia zaidi hayo ukitaka
utaambiwa na huyo mtaalamu , nafuata alichoniambia, ….’akasema
‘Miiko…kwenye kutibia,….sasa ukifa je…?’ nikauliza
‘Huyu mtaalamu alinielekeza, kuwa hali hiyo ikitokea,
na….haitokei mpaka mtu akifanya yale yasiyotakiwa, akikiuka miiko,..na
nikuambie ukweli, pindi hilo deni likilipwa, hakutatokea tena kitu kama hicho,
tatizo hapa ni hilo deni, ndivyo alivyosema huyo mtaalamu…kwahiyo mimi silali,
nahangaika huku na kule kuhakikisha hilo deni limelipwa…na hakuna njia nyingine
maana hiyo pesa ni nyingi sana…’akasema
‘Kwahiyo hilo deni, una uhakika aliliacha marehemu au sio?’
nikamuuliza
‘Ndio, hajakuambia dada yako…si umesema huyo ni dada yako,
hajakuambia…hata yeye hakulijua, lakini tulifuatilia tukawa na uhakika huo..’
akasema
‘Mimi kiukweli bado nina
mashaka na hilo deni,..’nikasema
‘Una mashaka …!?’ akanikazia macho, mimi nikatulia kwanza
sikusema kitu, na ndio akaendelea kuongea
‘Una mashaka gani, ni sawa hata sisi tulikuwa na mashaka
hayo, siwezi kushangaa, lakini ili kuyaondoa hayo mashaka, nenda kafuatilie
benki, sisi…mimi mwenyewe nilihangaika kufuatilia hilo, nikachemsha, maana
hatujua , na hata shemeji naye akajaribu
akachemsha,…’akatulia kidogo
‘Tatizo kaka alichukua mkopo huo bila kumwambia mtu, na
matokea yake ndio haya, na mbaya zaidi ukifuatilia unamuumiza mtoto, unaona
jinsi ilivyokaa vibaya…muhimu hapo kwasasa ni kulilipa hilo deni…’akasema
‘Kwahiyo kwa msimamo wako, kwa hekima zako, wewe umeona ni
vyema tuache, nyumba ipigwe mnada, ili
lilipwe hilo deni….huoni kuwa tutakuwa hatujawatendea haki hawa wanafamilia,
mama na watoto wake?’ nikauliza
‘Hii ilikuwa nyumba ya marehemu na yeye ana mamlaka ya
kufanya apendavyo,…si ilikuwa nyumba yake, na maswala ya watoto wana riziki yao, haikupangwa
iwe yao, mungu atawajalia watapata ya kwao, hata mimi sio kuwa napenda iwe
hivyo, hiyo ni amri ya benki, kama kuna namna nyingine tusaidie wewe, au
niambie sisi tutapatia wapi hiyo pesa…?’ akasema
‘Mimi sijakataa ..maana kama imefikia hapo ina maana
ulijitahidi kutafuta njia nyingine ukashindwa,…na kama mkopo ulichukuliwa ina
maana kulikuwa na namna, mtu alijua
ataurudisha kivipi,, au sio…na kwa vile hamkuwa na taarifa ya huo mkopo,
mtakuwa vile vile hamjui jinsi gani ya kuurejesha au sio…l?’
‘Ndio…’akasema akitikisa kichwa kukubali
‘Ndio hapo mimi ninakuwa na mashaka na huo mkopo, yawezekana
huyo kaka yako hakuchukua huo mkopo…kama aliuchukua mkewe angejua, wewe
ungejua, na kungekuwa na mradi…kitu cha kuzalisha, je miradi ya marehemu ipo
wapi…?’’nikauliza.
‘Hakuna mradi kama mradi alioacha,…nijuavyo mimi, miradi
yake ilikuwa ya kuchukua mizigo anauza, mzigo ukiisha anakwenda kuchukua
mwingine ni hivyo tu…na akiba akawa anaweka benki…na ni pesa ndogo tu
tuliyoikuta benki, ina maana alipoondoka alitoa pesa karibu yote, kwenda
kuchukua mzigo, akijua akirudi, atapata fadia kubwa….’akasema
‘Hapo sasa ndio naona kweli yeye hajachukua huo mkopo…kuna
namna, kuna mtu kachukua huo mkopo kwa ujanja, …..’nikasema
‘Kwanini unasema hivyo, ….hahaha, eti hakuchukua huo mkopo …’akacheka
kwa dharau,
‘Wewe unasema alichukua pesa iliyokuwa benki karibu yote
kuchukulia mzigo, huo mkopo mkubwa hivyo ulikuwa ni wa nini…?’ nikamuuliza hapo
akasita kidogo.
‘Huenda alichukua kwa shughuli nyingine,
hatujui….’akasema ‘ unasema labda kuna
mtu mwingine alichukua, hebu niambie, huyo mtu mwingine angelichukuaje,…unakuwa
kama hujasoma bwana, mkopo uchukuliwe benki na mtu mwingine uwekwe kwa mtu
mwingine, kwa vipi…wewe kweli sikuelewi,…nakutilia mashaka na elimu yako….au huwaamini
watu wa benki au….’akasema
‘Nitakuja kukuonyesha kuwa kweli mimi nimesoma wewe subiria
tu, ila kwanza nataka uelewe kuwa hata huko benk kunaendeshwa na watu, na watu
wote sio sawa, na kuna ushahidi huo, nitakuja kukuonyesha hilo, ila kwasasa
nakuambia hivi,…nina mashaka kabisa hilo deni halikuchukuliwa na kaka
yako….’nikasema
‘Hilo sasa ni jipya, …hahaha…wewe mtu wa ajabu kweli, nyie
ndio mnaopenda kuzusha mambo…, hata wapelelezi wa polisi hawakuwahi kusema
hivyo,….’akasema
‘Wao walisema nini…?’ nikamuuliza
‘Wao walihisi kuwa mimi nilikuwa najua hilo deni , maana
deni lilishathibitishwa kuwa lipo…ya kuwa kaka kweli kachukua, wao wakahisi kuwa huenda mimi nafanya mbinu labda, ili hilo deni
lifutwe….sasa wewe unasema kaka hakuchukua, hizo hati alizosaini, kila kitu kipo
wazi, mimi nimeona sahihi yake….’akasema
‘Sahihi inaweza kuchezewa na wajanja….’nikasema
‘Kwa vipi, sahihi, dole gumba je…mimi sikuelewi ukisema
hivyo, …sasa hebu niambie alichukua nani, hebu niambia wewe, kama benk wameleta
vithibitisho, hebu na wewe leta vya kwako, ili tuone kama kweli sio deni
halali…tusaidie kwa hilo, tutashukuru sana, na ujue hapa tunapambana na muda,
kesho, mnada..kesho ni mnada, hata shemeji anajua…na jingine tunamtesa mtoto…’akasema
‘Huo mnada hautafanyika…’nikasema
‘Eti nini, hautafanyika, nani kakuambia, wakati kila kitu
kipo tayari, unajua mimi sijakuelewa wewe mtu, ni nani na unataka nini, una
ushahidi gani kuwa hilo deni sio la kaka, kwa vipi, wewe unanipotezea muda
wangu hapa bure, huo ushahidi upo wapi….?’ Akauliza kwa mshituko
‘Kwanza tunachotaka kujue ni ukweli wa hilo deni, hilo deni
lina mashaka,…na ukweli huo tunataka kujua kuanzia kwako, kwasababu wewe ndiye
uliyepewa dhamana,…., kwahiyo ili kusaidia hilo, ili tujue huo ukweli, tunataka
wewe ujibu maswali yetu ya msingi, na baada ya hapo nitakuonyesha hivyo vidhiti
unavyotaka wewe, na hivyo tutavipeleka mahakamani…’nikasema
‘Sasa wewe….unataka kuleta matatizo mengine kabisa…’akasema
akimuangalia shemeji yake, na ilionyesha keshaingiwa na wasiwasi, mimi
nikamtizama anavyobadilika,…hawa watu wanaoishi kwa ujanja ujanja kuna namba ya
kuwapatia,….ukweli tu…na hapo nikawa na uhakika na shuku yangu.
‘Nataka unijibu maswali yangu ya msingi…..upo tayari
muheshimiwa..?’ nikamuuliza
‘Wewe uliza hayo maswali yako, na… nataka unionyeshe hivyo
vidhiti, tusipotezeane muda hapa lakini, unaona hali ya huyo mtoto , mimi
sitaki tena hiyo hali imrudie, ujue hiyo
hali ikimrudia tena mimi sina uwezo wa kufanya lolote, ndivyo mtaalamu
alivyosema, hata angekuwa nani, hawezi kumsaidia tena..tutampoteza mtoto kwa
uzembe wenu, mimi sipo ….’ Akageuka kumuangalia shemeji yake
‘Shemeji unaona hawa watu, wanataka tumpoteze mtoto,..upo
tayari kwa hilo,yale mambo ya kesi ambayo tulishaambiwa hayatakiwi mpaka deni
lilipwe, hawa wanataka kuyarudisha tena, jamani, hivi…mali, nyumba, ina
tahamani gani mbele ya mtoto, haya, shemeji mwambie, usije kunilaumu mimi, ..’ akasema akimuangalia shemeji yake, na shemeji yake alikuwa kainama
chini tu. Mimi nilikaa kimia nikimuangalia tu.
‘Shemeji hawa watu hawajui tunavyoteseka na huyo mtoto, na hiyo
hali ikijirudia titafanya nini, mimi nanawa mikono yangu, mimi ni baba yake lakini kutokana na
mtaalamu, sitaweza kufanya lolote tena…unakumbuka ulivyoambiwa,….?’ Akamuuliza
shemeji yake na shemeji yake akahema kwa nguvu, lakini hakusema neno.
‘Ingelikuwa nimekwenda mwenye ungesema labda, lakini ndugu yako mwenyewe ambaye alisikia maneno
kutoka kwa huyo mtaalamu, alikuambia hilo na kukusitizia,…usije kukiuka hiyo
miiko,…mwisho ni mara tatu, basi….sasa jiulize ni hii ni mara ya ngapi….’akasema na simu yake
ikatoa mlio wa ujumbe wa maneno, akaitizama
‘Sasa ….., unaona eeh,….’akawa anasoma huo ujumbe, na akatikisa
kichwa kama anakubali kitu.
‘Shemu, unaona sasa mtoto joto likipanda anafikia kupoteza
fahamu, jamani hebu tusaidiane kwa hilo….tafadhali ndugu zanguni, mimi inaniuma
sana, mimi sasa ndiye baba yake, ni lazima niwe kama kaka,….mnielewe jamani, shemeji hebu mwambie huyu ndugu yako ohoo,
hayeni...’akasema akimwangalia shemeji yake
‘Sasa kwani tatizo lipo wapi hapa, kwanini unaogopa hayo maswalii yangu, mbona unakuja juu kama unajihami, una wasiwasi
gani, mimi kwa kuulizana hayo maswali tutakuwa tumekiuka hiyo miiko…ina maana
hiyo miiko inasema tusiulizane maswali, tusitake kujua ukweli, kama ni hivyo basi
kuna kitu…au unaniogopa, …?’nikasema
‘Nakuogoa….hahaha, nikuogope nini wewe…., kwanini
nikuogope…kwani wewe nani, utanifanya nini mimi eeh, …eti nakuogopa,
uliza…..’akatulia kwanza
‘Hivi,….unafikiri mimi ….hiyo kauli yako sijaipenda, sasa,
nasema, uliza hayo maswali yako yote na mimi nitayajibu moja baada ya jingine,
uliza….hivi unanionaje mimi, ’akakaa vyema. Na mara nikamuona shemeji akimshika
Yule mtoto shavuni, na akaonekana anakunja uso, kuashiria kuna tatizo…..
NB: Nisiwachoshe kwa leo tutaendelea sehemu ijayo,ni mwendo
wa maswali na maswali yalikuja kubaini ukweli,lakini mtoto je……tuwemo kwenye
sehemu ijayo.
WAZO LA LEO: Mbinu za mnafiki ni fupii tu….ni kumwambia
ukweli!
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Kiss niko hot kinasisimua
Miram usichoke Baba tupe kiss kinafundisha Sana Kuna watu wanatamaa Sana.Mungu msaidie mjane Wako maana WW ndo mume
Post a Comment