REJEA: Kisa hiki ni cha mjane na watoto wake, waliotakiwa
kudhulumiwa mali zao, ikiwemo nyumba, ikafikia nyumba kupigwa mnada ili kulipia
deni la nyumba…mama na watoto hawajui waende wapi, hawajui deni hili limetoka
wapi, ndugu wa kiumeni wanawapiga
vita…kisa ni nini….mama akiulizwa anasema yeye kamuachia mungu, maana yote hayo
ni mapenzi ya mungu…Je iwe hivyo tu…
Tuendelee na kisa hiki tuone ukweli nyuma ya pazia…
*********
‘Lakini nikuulize
unaniuliza haya maswali yote ili iweje….sisi yote hayo tumeshamuachia mungu, na
nimekuambia hayo niliyoweza kukuambia,…yatosha,…’akasema na kujikuanyata.
Kauli hii yake hiyo ilinifanya hata mimi nijiulize, je
ninavyomuuliza haya maswali nitawezaje kumsaidia huyu mama mjane na watoto
wake, akili yangu ilifanya kazi kwa
haraka nikamkumbuka rafiki yangu aliyebobea kwenye sheria na mara nyingi
hujitolea kuwasaidia watu kama hawa, nina uhakika akilisikia tatizo la huyu mama,
huruma itamuingia anaweza akamsaidia, ndipo nikamuambia huyo mjane;
‘Shemu unajua matukio huja, humtokea mtu kama mitihani, na mara
nyingi tunayaona kama matukio tu,…na pengine mtu kujiona yeye labda kaonewa na
mungu, lakini matukio mengine yanasababu, hayatokei hivi hivi tu, ….kuna
dhuluma zimetengezwa, ….mimi katika hayo maelezo machache uliyoniambia,
nimehisi kuna tatizo,…hapo kuna jambo halipo sawa, …’nikasema
‘Ndio kuna tatizo lakini, sioni sababu tena ya kuhangaika,
mimi nimeshaamua…., tuyaache kama yalivyo…wewe nenda kamtafute mnunuzi unayemuona,…..
kama sio wewe unayetaka kununua, nyumba ndio hii hapa inapigwa mnada, nyumba
mume wangu aliyoihangaikia kwa ajili ya watoto wake, sasa hayupo,…mimi
nimeshindwa, nitafanya nini masikini wa
mungu….’akasema kwa uchungu.
‘Shemu sio kwamba nataka kukukosanisha wewe na shemeji
zako,…hapana, ila nahisi kuna tatizo, linaloweza kusababishwa huenda na
wao,…hata hivyo bado siwezi kulihakiki hilo
tatizo mpaka nisikie maelezo yako yote…’nikasema
‘Ili iweje…?’ akauliza akiniangalia kwa jicho moja
‘Shemu wakati mwingine watakiwa kuipigania haki yako, na
katika kuipigania haki yako, unatakiwa umuweke mungu mbele kuwa akusaidie,
usiogope, usiwe mnyonge, pambana vinginevyo, watu wenye mioyo ya dhuluma,
watachukua kila kilicho chako na kamwe hawatosheki……’nikatulia nilipomuona
anataka kusema neno lakini hakufunua mdomo.
‘Unajua shemu, mungu
humsaidia zaidi Yule anayejihangaisha, na huwezi jua mimi naweza kuwa
mmoja wa msaada wako kwa kupitia…. , jiulize kwanini nimeweza kufika hadi hapa,
wakati sina uwezo wa kuinunua hiyo nyumba, mimi sio mnunuzi, sina uwezo huo,
lakini nikavutika kuja hapa na kuonana na wewe…kiukweli mungu mwenyewe anajua
ni kwanini, ….’nikatulia nilipomuona yanamuingia.
‘Mhhhhh’akaguna hivyo tu.
‘Sasa shemu mimi naona tufanye kila kinachostahiki, ….tuchukue
hatua , tujitahidi kuitafuta haki, ili mali ya hawa watoto, mali yenu
mliyoihangaikia wewe na mwenzako akiwa hai isiende mikononi mwa watu wasiostahiki, na
mengine tutamuachia mungu, lakini kwanza tufanye jitiihada…nina imani kwa
mapenzi yake mungu tutafanikiwa…’ nikasema na yeye akatikisa kichwa kama vile
kukataa…moyoni nikajiuliza ni kwanini
huyu mama anakataa kudai haki yake ni lazima kuna jambo!.
‘Labda mimi kwanza nijitambulishe kwako,….’nikasema na yeye
akanikatisha kwa kusema
‘Haina haja, wewe kama sio mnunuzi, mimi naona uondoke tu,
kwani oh, sijui nisemeje, ….ila
nikuambie kitu, kama unachotaka kusema ni kwenda mahakamani, ….hapana , mimi sitaki
tena kwenda huko mahakamani,….nikafanye nini tena huko, nimechoka..’akasema
akitikisa kichwa
‘Ina maana kumbe uliwahi kwenda mahakamani…!...?’
nikamuuliza na yeye kwanza akabakia kimia, baadaye akasema;
‘Ilibidi nifanye hivyo…..’akasema na kutulia, baadaye kabla
sijasema neno akasema
‘Ni baada ya kupewa barua ya notisi kuwa nyumba hii
inatakiwa kupigwa mnada,…nilishtuka sana siku hiyo, na siku hiyo shemeji
hakuwepo, ikabidi nianze kufuatilia ni deni gani hilo,…na nilikuwa bado sina
nguvu, lakini ….ikabidi nikajitetee, maana sasa tungeenda wapi, ..hawa watoto
watakwenda kuishi kwa nani, hata hivyo,
sikufanikiwa…’akasema
‘Shemeji mimi nina
mtandao wangu wa jamii, na moja ya kazi yake ni
kutetea wanyonge, tunajaribu kutetea haki za wanyonge kwa njia ya
kuandika visa na matukio yaliyowafika watu,mbali mbali kwa ridhaa yao, na kwa
njia hiyo taarifa zinafika kwa wengi,…’
‘Na kwenye wengi pana mengi, miongoni mwao kuna mungu kawajalia hekima , busara,
kawajalia utashi, kawajalia duwa zenye kujibiwa, na zaidi kuna ambao hujitolea
kwa ajili ya watu….. nimekuwa nikiwatetea akina mama, watoto..wazee, wanyonge,
waliodhulumiwa, …na imeleta mafanikio,..japokuwa ni kazi ya kujitolea tu!’nikatulia
pale aliponitupia jicho kama la kujiuliza.
‘Ina maana unayafanya hayo bure…?’ akaniuliza
‘Ni nani atakulipa,….ujue hapo unatetea wanyonge watu wasio
na kitu, unataka nini tena kwao…sisi anatulipa mungu….’nikasema
‘Lakini mimi sihitajii huo msaada wenu….na sitaki mambo haya
yajulikane, ….sitaki kabisa, naombeni tafadhali…’akasema akionyesha wasi wasi
mkubwa.
‘Usiogope,….kwani kwa jinsi sisi tunavyoandika hizo habari, inakuwa haipo wazi kihivyo, kuwa watu
watakufahamu waje kukusumbua, hapana…tunachofanya ni hivi baada ya kuupata
ukweli ulivyo, tunakahakikisha ukweli
wake, hatutaki kuzua, unaona, ….kwa njia zetu tunajua jinsi gani ya kuupata huo
ukweli…,
‘Tukishaupata ukweli, tunatafuta watu wanaoweza kulifuatilia
hilo jambo…na wakati kazi inaendelea ndipo sisi tunashika kalamu,…unajua kalamu
ina nguvu sana kwa wenye kuelewa, kalamu ni silaha, silaha yenye kuua au
kusaidia, silaha yenye kujenga au kubomoa,…’nikatulia kuona kama ameelewa
‘Hapo ndipo tunaanza
kuliandika hilo tukio, kutokana na ushahidi tulioupata, ukweli na uhalisia wake, na kuliweka hilo tukio hewani , kuna watu wenye mioyo yao safi wanalifuatilia
hilo jambo kwa kujitolea…najua dunia ya
sasa kila kitu ni biashara, lakini wema …..sio biashara. Na tunachotaka sio kumsaidia muhanga tu…,
tunapoliweka hilo tukio hewani, tunakuwa
tumesaidia jamii kubwa…., na haki inapatikana…’nikasema
‘Mimi nimekuelewa, lakini kwa hili langu, usijisumbue bure,
hujui ni kitu gani kipo hapa, huwajui hawa watu walionizunguka,….kifupi mimi sitaki
kuendelea ku-kukuelezea zaidi maana naogopa…’ akawa anasita kuniambia jambo.
‘Kwanini uogope shemu, kwani hii sio haki yako, nyumba
,mashamba si mali yenu, kwanini uogope…?’ nikamuuliza
‘Mimi naomba uniache,…sitaki tena kuongea zadi, japokuwa
nyumba, mashamba, ni mali halali ya watoto wangu, mali aliyoichuma baba yao kwa
shida, akajinyima….we acha tu, ni haki yao, lakini utafanyeje…., kwa hivi sasa Mungu
pekee, ndiye anayeweza kutoa haki, sitaki tena, kama ni mali wachukue tu,
waniache mimi na wanangu, sisi tumemuachia mungu kwa mapenzi yake najua haki
itapatikana….’akasema akiinua mikono juu, halafu akainama na kukaa mkao ule wa
huruma.
Nikaona ni muingie kwa njia nyingine, nikauliza…
‘Hebu kwanza,
nikuulize, huo mkopo ulijaribu kufuatilia ukajua ulitolewa kwa ajili gani, kufanyia biashara,
kujengea au kufanyia kazi gani, …?’ nikamuuliza, alikaa kimia kwanza bila
kunijibu nikajua labda hataki kuongea tena, na ghafla akasema
‘Mhh, huo mkopo …walisema ulichukuliwa kwa mambo mbali
mbali, ikiwemo biashara, kusaidia familia, na utarejeshwa kwa kupitia
biashara, na dhamana yake ikawa ndio hii
nyumba, na …hapo sielewi zaidi na pia walisema ni , kwa ajili ya matibabu yangu,
haya ya matibabu alianiambia shemeji ni hivyo
tu…’akasema
‘Shemeji…. ukiwa na maana huyu aliyechaguliwa kuwa msimamizi
wenu…?’ nikamuuliza kuwa na uhakika zaidi
‘Ndio, yeye ndiye angeliweza kufanya hilo…., huyo aliyechaguliwa kama msimamizi wa mali ya
marehemu mume wangu…’akasema kabla hajatulia nikauliza swali la haraka haraka
‘Ulisema yeye alichaguliwa kuwa msimamizi wa mali ya
marehemu mume wako wakati wewe hujitambui au sio na baadaye ulipoanza
kujitambua mkawa mnashirikiana naye au sio?’ nikamuuliza
‘Ndio kama nilivyosema awali, kipindi hicho, nilikuwa
sijiwezi, sikuwa na utambuzi mnzuri,
nilikuwa kama maiti tu,….wanasema nilikuwa kama nimechanganyikiwa siongei, nipo
nipo tu, …nimelala mwili haufanyi kazi, … ‘nimeparalize’.. kwahiyo asingeliweza
kushirikiana nami, yeye alifanya kile alichoweza yeye kufanya…’akatulia kama
kakumbuka jambo, lakini akasita kusema
‘Sasa kuhusu huo mkopo, ujuavyo wewe, au ulivyoanza
kufuatilia, ulitolewa lini, na ulikuwa umechukuliwaje, maana nauona utakuwa mkubwa sana …’nikasema.
‘Hilo ndilo lilinifanya ning’ake, kwanini wamesinginizie
mume wangu kuwa yeye ndiye aliyeanza kuchukua
huo mkopo benki kabla hajafariki, hilo sikubaliani nalo kabisa na denim
bona kubwa sana….’akasema
‘Hayo uliyajulia wapi, kuwa mume wako ndiye alianza kuchukua
huo mkopo….`alianza ..’ au sivyo?’ nikamuuliza
‘Siku nilipoamua kufuatilia, niliambiwa deni hilo ni la siku
nyingi, limeanzia kipindi mume wangu akiwa hai…’akasema
‘’Alianza, yeye ndio alianza….ok, sasa ni nani alikuambia hivyo..?’ nikamuuliza
‘Ni watu wa benk….’akasema
‘Hapo sasa tunakwenda sawa, watu wa benki ndio waliokuambia
au sio….’nikasema
‘Ndio hivyo….’akasema kama vile anajua nimemalizana naye,
nikamuuliza
‘Nirudi nyuma kidogo, …ulifanya yote hayo , kufuatilia, ni
baada ya kwenda mahakamani kufuatilia ili kuweka pingamizi si ndio hivyo?’ nikauliza
‘Ndio hivyo …..nilipopokea hiyo barua ya kuwa nyumba
itapigwa mnada deni lisipolipwa, …nilichanganyikiwa kabisa, sikujua ni deni
gani, na kipindi hicho shemeji alikuwa hayupo kasafiri sehemu ya mbali na
hatarajii kurudi karibuni, nikaonana na mtu ninayemfahamu, yeye ndio
akanisaidia, tukafungua pingamizi,…’akatulia.
‘Ok, ikawaje…?’ nikauliza
‘Pingamizi ina maana ili lipite natakiwa niende
mahakamani….mambo yao haya siyaelewi, mambo ya mahakama ningeyajulia wapi…..ndio
tukafika mahakamani kabla ya kesi, kuna kusikilizwa kwanza, nikaambiwa nipeleke vielelezo vya kusaidia
hilo….nikauliza vielelezo gani…?,
wakaniambia vya kuthibitisha madai yangu…sasa hapo…uone, mimi ningevipata
wapi hivyo vielelezo…’akatulia
‘Ndio nikarudi kwa huyo rafiki yangu akanishauri niende
benki, na ndio nikakutana na hiyo kauli, kuwa hilo ni deni ni la siku nyingi….halikuwahi
kulipwa kutokana na makubaliano,…kuna mkataba wa mkopaji na benki ulitaka deni hilo lilipwe kwa kiasai fulani
kila baada ya muda fulani, lakini haikuwahi kulipwa….,
‘Nikaomba tu nipewe hiyo statement,ili niweze kuipeleka mahakamani …hiyo wakanipatia haraka, lakini
nilipopeleka nikaambiwa hiyo haitoshi, natakiwa nakala ya mkataba, hati za
malipo na vitu kama vitatu hivi,……ilikuwa kazi kuvipata kwa watu benki, maana
ilibidi nirudi tena mahakamani wanipe barua, ndio nikarudi tena benk
wakanipatia…..’akasema
‘Kwahiyo hilo deni la siku nyingi au sio, kama ni la siku
nyingi ni kwa muda gani, tangia mumeo akiwa hai au sio, ina maana ni deni alilochukua mume wako bila yaw ewe kujua, au….’akanikatisha,
‘Mume wangu hajachukua mkopo…nimeshakuambia unielewe, mume
wangu hakuwahi kuchukua mkopo, huo ni uwongo….’akasema kwa hasira,
‘Lakini huwezi jua, yawezekana mume wako alichukua mkopo huo
kwasababu ya kupanua biashara, hakutaka kukuambia hilo, sizani kama benki
wanaweza kutoa kitu cha uwongo…, hebu nikuulize wewe una uhakika gani kuwa mume
wako hakuwahi kuchukua huo mkopo, ?’ nikamuuliza
‘Nina uhakika, kwa hilo na kamwe sitokubaliana nalo kabisa,
….hebu jiulize yeye kila siku alikuwa akinikanya nisije nikachukua mkopo wenye
riba, kwanini yeye anikanye hivyo halafu yeye achukue mkipo huo wa benki ambao
una riba kubwa tu…’akasema
‘Hebu nikuulize , huko benki walipokupatia hizo hati, hivyo
vielelezo, si vyote vinaonyesha sehemu
mume wako alipoweka sahihi yake…hata kwenye mikataba ya deni hilo,kuna sahihi
yake au sio, je nyaraka zote hizo uliwahi kuziangalia kwa
makini, hukuona sahihi ya mume wako,…?’ nikamuuliza
‘Ndio….walinionyesha vyoye hivyo,….’akasema
‘Na sahihi ya mume wako unaitambua vyema,….?’ Nikamuuliza
‘Ndio …naitambua vyema…’akasema
‘Na kwenye mikataba hiyo, uliona sahihi kuwa ni yake au
sio….?’ Nikauliza
‘Ndio ni sahihi yake…ndio hapo nikachanganyikiwa, lakini
haiwezekani, sio yeye, siamini kabisa….na kingine kwenye hilo deni jipya eti na
mimi nilihusika nikaweka sahihi yangu…sikumbuki kufanya hivyo, ila….’akasita
kidogo
‘Deni jipya, kwahiyo kuna madeni mawili, au zaidi ya hilo….?’nikamuuliza
‘Lipo zaidi ya moja, kuna hilo la zamani, wanalosema ni la mume
wangu, ndilo kubwa, kuna jingine kipindi baada ya kufariki na kuna jingine
jipya kabisa….’akasema
‘Na kwa hayo mawili mapya , ya baada ya mume wako kufariki
wewe unahusika,….?’ Nikamuuliza
‘Ndio…nahusika, wamenionyesha sahihi yangu…na kweli ni sahihi
yangu..’akasema
‘Kwahiyo wewe hukumbuki kuwa uliweka hizo sahihi..?’
nikamuuliza
‘Mara nyingi, shemeji
alikuwa akija kwangu japokuwa sijiwezi kujiinua, baada ya kuanza kujitambua na
ananiambia anataka kufanya hili na lile, mimi naitikia tu kwa kichwa…maana
japokuwa nilikuwa sijiwezi kihivyo, kichwa kilikuwa kinaweza kutikisika, kuona,
kusikia…..’akatulia kidogo
‘Na kwa vile nilimuamini, na yeye ndiye aliyechaguliwa kuwa msimamizi wa kila kitu sikuwa na shaka
naye, na nilikuja kujua hiloo kuwa yeye ndiye msimamizi nilipojitambua,
walifika shemeji na baadhi ya ndugu zangu wakaniambia , nikiwa kitandani,
nikawaitikia tu kwa kichwa.
‘Na ndio nakumbuka pia, kuna kipindi alikuwa akija huku analalamika
kuwa hali ngumu, lakini akasema nisiwe na wasiwasi atajitahidi kuweka mambo
sawa….ni hivyo ninavyokumbuka mimi….’akatulia
‘Lakini hakuwahi kukuambia anataka kuchukua mkopo benki….?’
Nikamuuliza
‘Kwa hilo, hakuwahi, sikumbuki kitu kama hicho, sizani,
labda kama aliniambia kipindi sijitambui…yawezekana, aliniambia kipindi hicho, na
huenda nikaitikia, lakini kusema kweli,
sikumbuki, na kwa vile alishapewa hayo mamlaka ya kufanya aonavyo ni sahihi,
labda alioona kuchukua mkopo ni sahihi…’akasema
‘Kwa vile hukumbuki, yawezekana pia alikuambia uweke sahihi
ya mkopo, ukaweka, na umesahau kuwa ulifanya hivyo au sio?’ nikamuuliza
‘Hapana, hilo haliwezekani kabisa….nimejaribu kukumbuka,
..haijatokea, …wasinifanye mimi mjinga, na kwanini kama ni hivyo, anifanye
niweke sahihi kitu kama hicho, wakati anajua sijitambui…hebu kumbuka kipindi
hicho mimi ni mtu wa kulala….alinifanyaje mpaka nikaweka sahihi….mhhh, sijui
ilikuwaje..’akasema
‘Je unahisi shemeji yako anaweza kufanya hivyo, yaani
kufanya ujanja ujanja kwa nia mbaya…?’ nikamuuliza
‘Kiukweli, shemeji huyo ni mtu mwema tu, sina sababu ya
kumuhisi vibaya, lakini sasa kwa haya nitafanyaje,… yeye ni mmoja wa watu
wanaoaminika sana, kutokana na shughuli zake, na kwa jinsi alivyojitolea kunisaidia, nashindwa
kumshuku vibaya…na ndio hapo naingiwa na
sintofahamu, na….na…sitaki kwenda mbele zaidi…’hapo akatulia pale kijana wake
alimuashiria kuwa sio kweli.
‘Kwani wewe unamjua vipi…’akasema huyo mama
‘Mama, baba mdogo angekuwa mtu mwema, asingelifanya haya…tatizo
la mama anapenda kumtetea sana baba mdogo kwa vile tu kajitolea kwake, …mama
anaogopa kwasababu ya mdogo wangu …., mimi mwenyewe niliwahi kumsikia baba
mdogo akiongea na ….’akasema mtoto na mama yake akamnyamazisha
‘Mwanangu, wewe hujui dunia ilivyo, haya yote nayafanya kwa
ajili yenu,…hujui ni nini kinachoendelea shukuru nyota yako ni kali, ungekuwa
kama mdogo wako, nyamaza na usiseme kitu …’akasema akimuangalia mwanae kwa
jicho la ukali.
‘Lakini muache aseme huenda ikasaidia…kwani mdogo wake ana
nini….?’nikasema na kuuliza
‘Sitaki wanangu kujiingiza kwenye haya mambo, kuna mabaya
yapo nyuma ya pazia, inabidi niwalinde kwa kila hali, hizi mali,
nyumba,mashamba haya maana kwao zaidi ya
afya na usalama wao,…’akasema halafu akamgeukia mtoto wake na kusema kwa upole.
‘Sikiliza mwanangu nielewe, usijaribu kuniingilia au kuongea
chochote bila ruhusa yangu, unasikia, wewe hujui lolote kuhusu dunia na watu
wake…’huyo mama akasema na mtoto akainamisha kichwa kwa heshima.
‘Sasa kama huyo shemeji yako alikuwa mwema kihivyo , kwanini
achukue mkopo , na kuweka dhamana ya nyumba
yenu bila ya wewe kujua, maana sasa ulishapata nafuu, akachukua mkopo
mwingine, na kumbe kuna jinsi ya kulipwa, lakini hakuwahi kukuambia, mpaka
uliposikia kuwa nyumba inatakiwa kupigwa mnada…?’ nikamuuliza
‘Hakuwahi kuniambia hayo ya mkopo….., ila kuna siku alikuja
akaniambia mambo hayaendi vizuri, anataka kufanya jambo, anakwenda benki,
lakini hakusema anakwenda kufanya nini…halafu akasema kumbe kaka alifanya
hivyo, kwanini hakuniambia…nikamuuliza kuna nini, kaka yako alifanya
nini…lakini hakusema kitu akasema tu, usijali, …nitamaliza nao…, nitahakikisha
mpo salama, halafu akaondoka…’akasema.
‘Hebu niambie kidogo kuhusu shughuli za mume wako zilikuwaje
kabla ya kifo chake….hakuna kipindi kilikuwa kigumu kwenu, huenda kipindi hicho
aliamua kufanya jambo kwa nia ya kujikwamua na angelirejesha hilo deni kabla
riba haijawa kubwa….?’ nikamuuliza
‘Hapana kwa mume wangu kuchukua huo mkopo sitakubaliana nalo
mpaka kesho….ndio mume wangu alifariki kipindi
hana kazi, pesa zote alizokuwa nazo tulishatumia, na kidogo alichobakiwa nacho
alikiwekeza kwenye mipango ya kujiajiri…pesa akaziwekeza kwenye biashara, lakini
alikuwa na msimamo wake, kufanya kutokana na kile alicho nacho…kidogo kidogo
akawa anainukia kibiashara….’akatulia
‘Akaanza biashara za kutoka , kwenda mikoani,..na biashara
hizo hakuzianza zamani kabla ya kifo chake, kwenda mikoani ilikuwa ni mara ya
pili, ….ndio ilikuwa ni mara ya tatu ndio akakutana na umauti…kwahiyo huo mkopo
haukutokana na mume wangu ni lazima ulikuwa baada ya yeye kuondoka..au kuna
namna…asingeliweza kunificha’hapo akatulia
‘Kabla sijakuuliza jinsi gani mume wako alivyofariki, hebu
kwanza niambie kuhusu mahakamani, ulipofuatilia na kuwaonyesha hivyo vidhibiti, ilikuwaje…?’ nikamuuliza na yeye akabakia
kimia kidogo kama anawaza jambo.
‘Unasema ulikwenda
mahakamani, ukaambiwa upeleke vielelezo, ukawapelekea,sasa.ni nini
mahakama iliamua…?’ nikamuuliza
‘Haya ya Mahakamani achana nayo kabisa nimeshasalimu amri,
….’akasema
‘Ni muhimu niyafahamu, tafadhali….’nikasema
‘Wao walipoona hivyo vielelezo vyote, walisema hilo deni
lipo kisheria, sio kwamba nasingiziwa, wakaniuliza kama ulivyoniuliza wewe kuhusu
sahihi ya mume wangu, kama ndio yenyewe, kama naifahamu….nikakubali, basi
wakasema hilo deni ni sahihi….’akatulia
‘Na wakili wao akadai hilo deni jipya, mimi niliweka sahihi,
lakini kutokana na hali yangu, bado nilikuwa na tatizo la kusahau, kwahiyo eti niliweka sahihi na nimesahau kuwa nilifanya
hivyo, …mimi hapo naona kuna kitu ….’akatulia
‘Kwahiyo unahisi kuna kitu ….kitu gani labda…?’ nikamuuliza
‘We acha tu, siwezi kuamini hayo yote, ilitokeaje, kwanini
..najiuliza tu bila majibu,…lakini nashindwa nifanyeje, maana kwa yote hayo
aliyekuwa ni karibu kumshuku ni shemeji , na yeye …aah, ni mtu wa watu
kanisaidia sana, sitaki mabaya naye tena, siwezi …’akasema
‘Je shemeji aliporudi na kwa hali kama hiyo hukuongea naye
kuwa unafuatilia kuhusu hilo deni la zamani linalomuhusu mume wako, na ya kuwa
wewe unahisi kuna kitu zaidi ya hilo deni kinachohitajika kufuatiliwa ili
ukweli ujulikane,…kama ana nia njema angekusaidia,…je alisema nini…?’
nikamuuliza
‘Nilimuamba, akasema….yeye alishafuatilia akachoka, ….kwani
hata yeye hakujua kuwa kuna deni kama hilo, …hata yeye hakuwahi kusikia kutoka
kwa kaka yake na yeye ndiye alikuwa mtu wake wa karibu na hamfichi
kitu….anasema alifuatilia akitutetea kuwa huyo mdaiwa keshafariki na…waliobakia
ni mjane na mtoto….sasa iweje deni hilo lirithiwe…akahangaika kutafuta njia za kisheria
kutusaidia lakini ikashindikana kutokana
na mkataba …’akasema
‘Kutokana na mkataba, unasemaje….?’ Nikauliza
‘Mkataba ulianza kuvunjwa kwa kutokulipa kama
ilivyokubaliwa, haikuwahi kulipwa hata kidogo,kuashiria kuwa mkopaji alifanya
makusudi…..na mambo mengi ya kisheria,
sitaki hata kuyakumbuka…..’akasema
‘Ikawaje sasa….?’ Nikauliza
‘Alisema…. ngoja aniache na mimi nijaribu bahati yangu, huenda
nikasaidiwa, kwa huruma wakiniona mimi mjane na watoto…kwahiyo hakutaka kwenda
na mimi, ila kila nikirudi alikuwa akiniuliza imekuwaje,mwishoni akaniambia,
unaona hata mimi niliambiwa hivyo hivyo…’akasema
‘Kwahiyo ikawaje?’ nikamuuliza
‘Niliamua kwenda polisi kufungua jarida la upelelezi,
wajaribu kunisaidia kuwa labda kuna
namna imefanyika kutubambikia deni, huenda kuna watu wametumia nyumba yetu kama dhamana bila ya mimi
kufahamu….’akasema
‘Ulienda polisi, kumshitaki nani sasa…?’ nikamuuliza
‘Rafiki yangu mume wake ni polisi, alishauriwa na mume wake
nifanye hivyo, kuwa kunaweza kufanyika upelelezi ukweli ukabainika, ninachotakiwa
nikwenda polisi kutoa hiyo taarifa, mimi nikafanya hivyo….upelelezi
ulipoendelea, siku moja akaja kukamatwa
shemji kuwa huenda anahusika kwa namna moja au nyingine…’akasema
‘Ikawaje…?’ nikamuuliza
‘Ndugu zake ndio wakaingilia kati wakanijia juu,…’akatulia
kama anaogopa jambo
‘Yaani shemeji zako wengine….?’ Nikauliza akaitikia kwa
kichwa halafu akasema;
‘Mimi katika kujibishana, japokuwa hata mimi sikupenda hiyp
hali ya kukamatwa shemeji, nikawaambia ni kwanini yeye aliamua kuchukua mkopo
kwa dhamana ya nyumba bila ya kuniambia…na, baada ya mimi kuwa na nafuu,
kwanini hakunifahamisha mapema kuhusu hilo deni ina maana alikuwa akinificha
kwa masilahi fulani….’akatulia kidogo
‘Kiukweli kauli hii lilimfanya shemeji akasirikie sana…kuwa baada ya hayo yote hizo
ndizo fadhila zangu, na ya kuwa yeye hataacha kuwasaidia watoto kwa vile ni
watoto wao..ila mimi naonekana nina roho mbaya, sina shukurani….na hata dada
zao walifikia kuniambia mimi ni mwanga, mchawi, eti huenda..nilichangia kaka ya
o kufa..ikawa ni vita sasa, kwanini wananiambia mimi ni mchawi, eti nimloge
mume wangu ili iweje….’akasema
‘Lakini hayo yote yalikuwa kwenye harakati za polisi
kufuatilia na kutafuta ukweli au sio, na
swala hilo la kutafua ni nani alifanya hujuma….lilikuwa bado halijafika
mahakamani au sio,…kuacha lile la mwanzo la kutafuta ukweli wa deni kama ni
halali au la?’ nikamuuliza
‘Ndio….’akasema
‘Ehe …ikawaje sasa?’ nikamuulza
‘Baadaye ndugu walikuja wakaanza kuniomba kuwa niachane na
mambo hayo ya polisi hilo swala turudi kuliongelea nyumbani, mimi nikawaambia
hata tukiliongelea nyumbani hilo deni atalipa nani, ni lazima tutafute ukweli
wa hilo deni, kwani huenda kuna mtu mwingine anatuchezea…, ‘akatulia
‘Sasa walipoona sikubaliani na hilo, kukaanza vitisho kutoka
kwa wanandugu huku wakiniambia kuwa mimi sina fadhila, sina shukurani…hawakujua
kuwa mimi nipo hivyo, basi kama ni hivyo na wao watafanya hicho
ninachokitaka….na watahakikisha,najuta, nitakiona cha mtema kuni…’akasema
‘Ni nani alikuwa akiongea hayo…?’
‘Ni hao ndugu zake shemeji na wake zao, na mawifi…’akasema
‘Na kweli haikupita muda mara mtoto wangu huyu mdogo akaanza
kuumwa, kweli kweli..kila ikifika muda wa kwenda mahakamani anazidiwa, maana
mimi niliamua hayo mambo yafikishwe mahakamani, kutokana na uchunguzi wa
polisi, sikukubali mume wangu asingiziwe hilo deni, nataka haki ipatikane,…wao
wakasema tutaona…’akatulia
‘Na muda huo mshitakiwa ni shemeji yako, kutokana na
uchunguzi wa polisi…?’ nikasema kwa kuuliza
‘Ndio…’akasema na kabla sijamuuliza swali jingine akasema
‘Kiukweli hata mimi sikutaka ifikie hapo…maana sasa
namshitaki shemeji , mtu aliyenisaidia sana, lakini sisi tutakwenda wapi, maana
ilikuwa nifanye hivyo, ili pingamizi liendelee kuwepo, au nyumba ipigwe mnada,
na polisi walisema kuna uwezekano shemeji yangu huyo anahusika kwa namna moja
au nyingine na mahakama ndiyo itaitafuta haki, na huko kunaweza kuliondoa hilo
swala la kupiga nyumba hii mnada,…’akasema na kutulia kidogo
‘Cha ajabu wao wanasema nyumba ina umuhimu gani, zaidi ya
ubinadamu, nasahau fadhila,…yote eti yalifanyika kwa ajili yangu na watoto..na
kama ni denii lipo kwanini nisiche tu nyumba ipigwe mnada ili lilipwe na pesa
itakayobakia tujenge nyumba nyingine ,eti kwa kufanya hivyo, kwenda mahakamani
namshitaki marehemu aliyekopa hilo deni,…..’akasema
‘Unasema mtoto akaanza kuumwa, … hilo la kuumwa kwa mtoto
wako linahusikanaje na hiyo kesi,
unahisije kuwa mtoto wako anaumwa kutokana na hilo tatizo, kwani wewe unaamini
mambo hayo ya kishirikina,…kuwa huenda wao walifanya ushirikina kwa huyo mtoto
wako..?’ nikmuuliza
‘Unajua nikiongea haya utadhani mimi naamini haya mambo ya
kishirikiana,…mimi siamini hayo kabisa, mimi namuamini sana mungu , nimelelewa
hivyo na ….moyoni mwangu, siamini sana mambo ya kulogwa, japokuwa yapo, siwezi
kukataa…. lakini hujui ni nini kimetokea, naishi maisha yasiyo salama, vitisho,
na mambo ya ajabu ajabu yanatokea kila siku, usiku hatulali, mapaka…sijui vitu
gani vinacheza kwenye bati juu..ni shida kweli, …., na sana wakaamua kuwalenga
watoto wangu, hawa wana makosa gani….’akasema kwa uchungu
‘Kwa vipi?’ nikamuuliza
‘Huyu mtoto mdogo, hakuwa na tatizo hilo kabisa, sasa kila
nikitaka kufuatilia hilo jambo..hiyo kesi, mtoto anashikwa na homa kali mpaka
anakuwa kama ana dege dege, anapoteza
fahamu…., hapo wamenigusa pabaya, siwezi kuvumilia….na utashangaa siku
hiyo ikipita anapona…’akasema
‘Siku gani ikipita…?’ nikamuuliza
‘Yaani siku ikiwa ni ya kwenda kulipeleka hilo shitaka mahakamani, au nikitaka niifuatilie jambo
kuhusu mali ya mume wangu, mtoto huyo anaanza kuchemka homa….ni homa kweli,
anachemka mpaka anakuwa kama anawehuka, ooh, ilipotokea zaidi ya mara tatu, nikaona
sasa basi, kama ni mali wanataka basi wachukue tu…mimi sina la kufanya,nawapenda
sana watoto wangu,…. yote sasa nimemuachia mungu..’akasema
‘Ulihakikishaje…sio kwamba nakupinga kwa hilo, lakini jinsi
gani ulihakikisha kuwa mtoto anaumwa kwa sababu hiyo…?’ nikamuuliza
‘Mtoto anaumwa jamani…akianza kuchemka homa namkimbiza
hospitalini, akipimwa hana malaria hana tatizo, …anaishia kupewa
panadol…..nikirudi na kusema niachane na huko kufuatilia mtoto ni mzima kabisa,
utasemaje hapo, …..sasa ulitaka nihakikisheje..’akasema
Ilipita muda kidogo nikiliwazia hili, je mama kama mama
atawezaje kupata haki zake kwa hali kama hii, kama alivyosema kila akitaka
kufanya jambo, mtoto wake anaumwa,na keshahaikisha hilo…kwa mapenzi ya mama kwa
mtoto wake itakuwa vigumu sana, hapo itakuwa vigumu, sasa …nitamsaidiaje,
nikaona ni lazima nifanye jambo, nikasema
‘Shemeji wewe si unamuamini mungu?’ nikamuuliza
‘Swali gani hilo, kama nisingelikuwa namuamini mungu kwa
hali kama hii ungelinikuta nimeenda kwa waganga kupambana na hayo, lakini mimi
namuamini sana mungu na kwa haya
sijawahi hata kwenda kwa waganga, au
hata kufikiria hivyo, zaidi ya kumuomba mungu..’akasema
‘Sasa kama unamuamini mungu huoni kuwa huo ni mtihani tu,
unajaribiwa tu , ili tu usitete haki zako, mimi nakushaurii sasa tuifufue hii kesi …mimi kuna watu
nitawasiliana nao wataweza kwenda mahakamani, ….wataweka pingamizi
…..tusipoteze muda, unaonaje kwa hili…..’nikasema
‘Hapana…’akasema
‘Kwanini…hii ni haki yako, au sio…’nikasema
‘Ni haki yangu ndio, lakini sitaki …..kwanza nitaanzia wapi
wakati nimeshakubaliana na hawa wana ndugu tukasema basi yaishe, kama ni nyumba
watauza , italipiwa deni na kiasi kilichobakia tutajengea kibanda nyumba nyingine
ya kawaida inatosha hata kama ni kibanda cha vyumba viwili inatosha…’akasema
‘Wewe niamini mimi, hapa kuna ujanja umechezwa, kuna mtu
anakuzunguka, ili aifisidi haki ya wanao,…nikubalie tuipiganie haki ya watoto,
kwani ukiacha hivi hata mume wako huko alipo atakulaumu, ina maana juhudi zote
alizofanya zinapotea bure na wewe upo hai….mimi kuna watu wangu watapigania
hili hadi haki yako itapatikana, niamini,….’nikasema na yeye akabakia kimia, halafu
akatikisa kichwa akasema lakini sitaki mimi nijulikane kuwa nimeifufua hiyo
kesi, sitaki nihusike, mfanye mjuavyo wenyewe, mnaweza kufanya hivyo…?’
akauliza
‘Ngoja niwasiliane na watu wangu, nitakuambia….’nikasema
nikapiga simu kwa watu wangu nikawaelezea kwa kifupi ni nini kinatakiwa
kifanyike, …kazi ikaanza mara moja!
Hutaamini, wakati anaanza kunionyeshea baadhi ya nyaraka
alizokuwa nazo…, mara Yule mtoto mdogo akaanza kutetemeka, joto likaanza
kupanda, mama akaanza kuhaka, na kusema
‘Unaona ndiyo haya siyataki, hawa wanajua kila ninachotaka
kukifanya, unaona …’ akawa anamshika mshika mtoto wake ambaye kwa muda huo
alikuwa na joto kali , nikaanza kazi ya kumsaidia, kumsiponji, na kumpa dawa ya
kutuliza..lakini wapi….mtoto akawa hajiwezi mpaka anapoteza fahamu
‘Tumpeleke hospitalini..’nikasema
‘Tunajisumbua , dawa ni kuachana na hayo madai,…’akasema
mama mtu
Nilimuchunguza Yule
mtoto, kweli joto lilikuwa juu kweli, wakati mwanzoni alikuwa hana dalili ya
kuumwa, na kwa hali kama hiyo nilionelea
tumpeleke hospitalini lakini mama mtu akasema huko tunapoteza muda, cha muhimu
ni tuachane na hilo tulilotaa kulifanya
‘Shemeji usiamini
mambo hayo, wewe usiogope shemeji hivi ni viini macho tu, muombe mungu,
tuendelee na hili hebu kwanza lete panadon….nikasema akaleta panadoni
nikaisomea kwa imani yangu, nikachukua maji nikayasomea, nikamwambia ampe mtoto
anywe….mara mlango ukagongwa, na aliyeingia alikuwa shemeji mtu….
NB: HAYA MAMBO
YAMEANZA, KAMA NI WEWE UNGELIFANYA NINI
WAZO LA LEO:
Mwenyezi mungu anaweza kutupima kwa mitihani mingi, ….magonjwa, kukosa
kazi, misiba na kila jambo lenye kutia
wasiwasi, na mashaka. Haya yakitokea, kamwe tusikimbilie kumshirikisha
Mungu…tukafikia kwenda kupiga ramli na
mambo kama hayo, tukifanya hayo tutakuwa tumekufuru! Muhimu ni kuvuta subira,
huku tukimuomba yeye, kutubu makosa yetu na hatimaye tutaishinda mitihani
hiyo,…Tumuombe mungu atunusuru ni mitihani yenye kuzishinda nafsi zetu.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
hongera mkuu
Post a Comment