YOTE NI MAPENZI YA MUNGU
(Duwa ya menye kudhulumiwa)
‘Mama sasa sisi tutakwenda kuishi wapi, nyumba yetu ndio
hiyo inauzwa,…kwanini lakini wanatufanyia hivyo…?’ ilikuwa ni sauti ya mtoto yatima
‘Nimeshawaambia, haya yote ni mapenzi ya mungu, iliyobakia tumuachie mungu mwenyewe, yeye
ndiye atajua tutaishi wapi…’akasema mama mjane kwa huzuni, …wakiwa wamekaa
wakisubiria nyumba ije kupigwa mnada,
kisa ni kutokana na deni , deni lilikopwa benki
Je watu hawa watakwenda kuishi wapi, mama mjane na watoto wake…, je hili deni lilitokea wapi,
maswali haya yalinifanya niingilie kujua undani zaidi wa kadhia hii na ndipo
nikagundua makubwa ualiyokuwa nyuma ya pazia. Ama kweli yale yote yanatotokea juu ya uwezo wetu , yote ni
mapenzi ya mungu…
Tukio hili na kauli hizo hapo juu ziliniandama sana kichwani
na ndio nikaamua nikiwekehiki kisa ili tuweze kupata fundisho sote, Inshallah…
*********
‘Mnada ,mnada ….kesho ndio kesho, kwa idhini tuliyopewa na mahakama, kesho tuna
mnada mkubwa wa hadhara, wa kuuza nyumba kubwa ya kisasa, ili kulipia deni la
benki… fika ujionee mwenyewe…., fika ununue nyumba ya kisasa yenye kila kitu,
ikiwa na uwanja mpana, na sehemu kubwa ya kuegesha magari…’ aliendelea kutoa
wasifa wa nyumba hiyo, huku kila mmoja wetu akijiuliza ni nyumba gani hiyo.
Nikasikia jamaa mmoja akisema;
‘Hiyo itakuwa ni ile nyumba ya Yule jamaa aliyekuwa ulaya,
…’akasema na niliposikia hivyo kuwa ni nyumba ya huyo jamaa aliyekuwa huko
Ulaya nikaikumbuka hiyo nyumba, kwani niliwahi kupita maeneo hayo siku za nyuma,
wakati huo ndio ilikuwa inamaliziwa ujenzi, na kila mtu aliyeiona aliisifia na
ukiuliza ni ya nani watu waliishia kusema ni ya jamaa kutoka ulaya, lakini
ilikuwa muda kidogo …
Tashwishwi ikaniingia kutaka kujua zaidi na nilijaribu
kuangalia huku na kule kama kuna mtu anayeweza kunipatia majibu hayo, lakini
sikumuona kwa muda ule, hamasa ikaniingia zaidi kila nikisikia jamaa wa
anayepiga hiyo mbiu kwenye gari akizidii kuipa sifa hiyo nyumba…hapo tena sikutaka
kumuuliza maswali mtu, nikaona niende nikajionee mwenyewe.
Nilifika eneo hilo, ilikuwa
eneo pembeni kidogo na maeneo yaliyojaa nyumba, ilijitenga kinamna, kutokana na
mwiinuko, nikapanda ule mwinuko na kupitia kwenye barabara inayoelekea kwenye hiyo nyumba.
Sikuwa na wasiwasi, kwasababu hiyo nyumba ilikuwa inapigwa mnada nilijua sitapata
kizuizi cha kuweza kuiona, na kweli nilipofika, niliwakuta watu wakiikagua ,
lakini wengi walikuwa nje ya geti, nikahisi huenda hawaruhusiwi kuingia ndani
ya geti, lakini sio hivyo, wao walishaingia na sasa walikuwa wakihakiki kwa
macho tu, na mimi nikaona niingie ndani nijionee jinsi ilivyo….
Nikakupumbuka kwa kipindi kile ndio ilikuwa kwenye ujenzi wa
mwisho mwisho, na sikuwahi kuingia ndani kuona jinsi ilivyokuwa, japokuwa
nilitamani sana niingie, kutazama ilivyo, kwani ilikuwa na muundo wa kipekee …sasa
ndio imezungushiwa geti kubwa la kisasa lenye nyaya za usalama, nahisi zina umeme.
Geti lilikuwa wazi, nikaingia ndani.
Mashallah, …kiukweli ilikuwa ni nyumba kubwa, na mjengo wake
kwa mbele tu, ulikuwa ni wa kipekee,
wanasema ramani hiyo jamaa alikuja nayo mwenyewe kutoka ulaya,…na mafundi wake
walikuwa wa kimataifa, na ilijengwa kwa gharama kubwa sana …na kile aliyeulizwa
alisema ni muundo wa ulaya
‘Huu ni muundo wa huko Ulaya, toka chini msingi ni wa mawe
matupu..inakuwa kama imewekezwa juu yam awe…!’akasema jamaa mmoha alipoona
naangaza macho kuangalia yale mawe yalivyopangwa, ni mawe makubwa,magumu…
Watu walikuwa wakiingia na kutoka, na kila mmoja aliongea
lake, lakini mimi kichwani nilijiuliza maswali mengi, yakihitajia majibu, hata
hivyo sikupenda kuwauliza kwanza, nikaona niwahi kuingia ndani ya nyumba
yenyewe kwanza
Nikawa nahesabuu hatua, huku nikijiuliza ni kwanini ilifikia hatua hiyo, …watu kukopa
pesa na kujenga nyumba ya gharama hivi, baadaye wanashindwa kulipa deni, na
hatimaye ndio hiyo inapigwa mnada….na je wao wenyewe watakuwa wapi, yawezekana labda wana nyumba nyingine wanaishi…au wapo
huko ulaya!
Nikawa natembea taratibu kama vile mnunuzi kwenye
zile njia za bustani sasa nikiwa
naelekea kwenye mlango mkuu wa nyumba yenyewe….maua mazuri ya kila namna
yalikuwa yamestawi, na kuzidisha nakshi ya hiyoo nyumba, na moyoni nikatamani ,
kama ningelikuwa na pesa, ….hahaha…itakuwa mwendo wa bilioni, ikawa ni ndoto za
Alinacha
Kiukweli kunapendeza, utafikiri upo wapi vile,….., sasa
nikawa naangaza huku na kule, kabla sijafikia mlango wenyewe, eneo la kuingilia
ndani …nikageuka kulia , nikaona eneo kubwa limependwa miti na migomba, na ..ndege
walipita huku na kule, ..nakataka kugeuka kushoto, mara nikasikia sauti,
mwanzoni nilijua ni watu waliokuja kuitizama hiyo nyumba lakini haikuwa hivyo…
Hiyo sauti ni masikitiko,…na kama kilio, kwikwi ya kilio,…nikasita
kutembea , nilipoona kumetanda ukimia, nikainua hatua moja , mbili , tatu, sasa nilishafika kwenye maru maru za
kupanda ngazi, nikaanza kupanda, ngazi ya kwanza, ya pili ya tatu, mara macho
yangu yakanasa kitu,…na moyoo wangu ukalipuka kwa mashaka.
Nikasimama, …kwanza sikuamini, maana nilijua humo kwenye
hiyo nyumba hakuna mtu tena,…mpaka inafikia kunadaiwa ina maana wenyewe
watakuwa sehemu nyingine lakini ….mhh kumbe bado kuna watu, ni akina nani hawa?
nikajiuliza
Pale kwenye mlango
mkubwa wa kuingilia kulikuwa na mama mmoja akiwa kakaa mkao wahuruma, ule mkao
wa mtu kukaa chini, miguu imejikunja na kichwa kinakuja kulala kwenye magoti…na
pembeni yake kulikuwa na watoto wawili,….
Mama Yule alikuwa analia, ….! Nina uhakika alikuwa analia….
Kwanini analia, nikawa najiuliza sasa….na cha ajabu watoto
wake walionekana kama wanambembeleza, itakuwa ni watoto wake!
Nikawa nimepigwa na butwaa,
Mtoto mkubwa alikuwa
upande wa kushoto kwake, akiwa naye kakaa chini na mkono wa mmoja wa huyo mtoto
upo kichwani kwa mama yake, na mtoto mwingine yeye alionekana sio mkubwa sana,
alikuwa naye kakaa akiwa kajiegemeza ubavuni kwa huyo mama, na alikuwa kainama kuficha uso,
huenda na yeye alikuwa analia
Hali ikanibadilikia…nikahisi mwili ukinisisimuka…
Ile hali ilinitia simanzi, japo sikuwa nafahamu kisa cha wao
kuwa vile ni kama vile kuna msiba …
Kwa muda wote huo walikuwa kama hawajaniona, au hata kama
walioniona hawakuwa na hamasa namimi….,huenda walishachoka na watu waliokuwa
wakiingia na kutoka, maana watu walikuwa wakija na kuondoka, kwahiyo kwa hivi sasa walikuwa hawana habari
na hao watu tena, swali likajijenga kichwani hawa ni akina nani , nijuavyo
waliokuwa wakiishi humo hawapo!
Haya maswali ya huenda , huenda sikuyapenda yajirudie
kichwani mwangu, nikaona niwasogelee wale watu ili nijue wao ni akina nani, na kwanini
wapo kwenye majonzi kiasi kile…., na nilipowakaribia ndio nikasikia kauli hiyo,
…kauli iliyonifanya niache ile kazi ya kuikagua hiyo nyumba na kuwaelekea wao …
‘Mama sasa sisi
tutakwenda kuishi wapi, nyumba yetu ndio hiyo inauzwa,baba mdogo haji, toka majuzi,
na mama …kwanini wanatufanyia hivyo…?’ ilikuwa sauti ya Yule mtoto mkubwa
‘Nimeshawaambia yote
tumuachie mungu, yeye ndiye atajua tutaishi wapi…’akasema mama huyo kwa sauti
ya huzuni
‘Tutamuachiaje mungu
mama….kama ni hivyo kila mtu angemuomba mungu apate kila akitakacho, na
akasubiria akipate, lakini kila mtu anahangaika kwanza…sasa tukikaa hapa tu,
watakuja kutufukuza…hata hivyo, mama mimi sitaondoka hapa, nitabakia hapa hapa,
hii ni nyumba yetu, baba alitujengea kwa pesa zake, kama ni kutuua watuue tu…’akasema
huyo mtoto
‘Hata mimi siondoki
hapa mama, ….’akasema Yule mdogo
Na alioongea huyo mdogo ndio huyo mama akainua uso, na
alipoinua uso ndio akaniona, nilikuwa sasa nimefika pale walipokaa, akanitizama,
nilichokiona usoni kwa Yule mama ni machozi,….mhh,
moyo wangu ukasononeka…nikajitahidi kusema;
‘Habari zenu….’nikasalimia na wote walibakia kimia, nahisi
walishachoka na hizo salamu
‘Samahanii jamani nilikuwa nauliza nyie ndio wenye hii
nyumba…?’ nikauliza sasa nikiwa mkabala na wao, na Yule mama akainua uso ,
halafu akageuka kumuangalia mtoto wake mdogo!
‘Nzuri,….. samahani tunaomba usizidi kutuongezea machungu
zaidi….’akasema
‘Hapana mimi sio lengo langu hilo…’nikasema
‘Wewe unasema wenye nyumba wakatii unasikia kuwa nyumba hii inapigwa mnada…sisi hapa hatuna chetu tena…wenye
nyumba sasa ni hao wenye uwezo wao, waje wanunue …kama ni wewe haya kagua uondoke
zako, mtuachie na majonzi yetu,….’akasema huyo mama
‘Mimi sijui kabisa kinachoendelea, nimesikia huyo mtu wa
mnada akinadi kuwa nyumba hii inauzwa, na inatokana kuwa mwenye nyumba alikopa
pesa benki akashindwa kurejesha…’nikasema
‘Kama umesikia hivyo yatosha….’akasema huyo mama na mtoto
wake akamkatisha na kusema kwa sauti kama ya ukali..
‘Mwenye nyumba hajakopa pesa yoyote, waongo hao…mwenye
alikuwa ni baba yangu sasa ni marehemu angekopaje hizo pesa….’alisema huyo
kijana mkubwa na hapo nikashikwa na mshituko, …mwenye ni marehemu ina maana
hawa ni yatima……!
‘Oh, ina maana mwenye hii nyumba sasa ni marehemu ndiye
alikuwa baba yenu…? Nikauliza na hapo hakuna aliyenijibu, na mama huyo baadaye
akasema
‘Ndio hivyo, ….’akasema hivyo tu kwa sauti ya huzuni.
‘Oh poleni sana, mimi sikujua siku nyingi zijapita maeneo ya
huku, nashangaa hata huo msiba sikuwahi kuusikia…’niliishiwa cha kuongea maana kiukweli
sikuwahi kusikia kuwa mwenye hiyo nyumba sasa ni marehemu,….sikumbuki kabisa
kusikia hata mtu mmoja akisema hivyo…watu walikuwa na hamasa tu ya kuiona, na
kuitamani, huenda wengine ni madalali, wanataka kukimbia kuwatafuta wanunuzi
wapate
cha juu…
‘Ina maana huyu…hata siamini, Yule jamaa sasa ni marehemu…’nikabakia
nimeduwaa.
‘Mbona ni muda mrefu sana mume wangu alishatangulia mbele ya
haki, na wengi walishasahau, ile mwenye kovu usizani kapoa, mimi nimekuwa nikiombeleza
miaka yote hiyo…na haya yanayotokea sasa yananizidisha machungu, na kuzidi
kunikumbusha marehemu mume wangu,….’akatulia na akavuta pumzi ya kutaka kulia.
‘Pole sana…’nikasema
‘Najua ndio basi tena,sitamuona tena… sasa sina jinsi
inabidi nikubali hali, inabidi nikateseke kama wanavyotaka wao, wanafikia
kusema si ulikuwa unaringa..jamani, lini nilifanya hivyo, ‘akatulia
‘Hiyo ni kawaida ya vinywa vya watu…’nikasema
‘Lakini nina uhakika kama angelikuwepo hai haya yote
yasingelitokea…’akasema huyo mama kwa uchungu,na hapo akaanza kulia.
Akilini nilikumbuka yale maneno ya mazito ya mtu wa imani
akisema; ‘mpende umpendaye ipo siku
mtaachana naye, kipende ukipendacho ipo siku utakiacha…itakayobakia kwako ni
amali yako njema…na wakati nawazia hayo Yule mama alikuwa bado analia, nikamsogelea
na kuanza kumliwaza kwa kusema;
‘Yote ni mapenzi ya mungu, poleni sana na mola aiweke mahali
pema peponi, ….shemeji cha muhimu sasa sio kulia zaidi, kwa kuonyesha mapenzi
yako kwake, wewe uzidi kumuombea marehemu maghafira na najua , nimjuavyo mimi,
mume wako alikuwa mtu mwema sana,…sasa hivi atakuwa sehemu njema…’nikasema
Ni kweli huyo jamaa alikuwa mtu mkarimu sana, pamoja na
kutokea hukoo alipokuwa ulaya hakuonyesha ile hali ya kuringa, hakuweza
kukupita njiani na gari lake kama anakufahamu ni lazima atasimama akuchukue, na
hata kukufikisha nyumbani kwako, lakini sasa ndio hivyo hatunaye tena…Yote
mapenzi ya mungu.
‘Ni kweli yote ni mapenzi ya mungu, lakini haya yanayotokea
sasa, yanatuzidishia machungu, maana kila alichokiacha sasa kinachukuliwa, hebu
fikiria hata haya makazi yetu ya hapa duniani, sehemu ya kusitiri aibu yetu
nayo ndio haiyo nayo inatakiwa kuchukuliwa, sisi tutakwenda kuishi wapi….’akasema
huyu mama akiangalia juu, kuiangalia hiyo nyumba!
‘Oh…’nikaguna hivyo na huyo mama akaendelea kuongea kwa
sauti yanye huzuni
‘Hawa watu sijui mwishowe wanataka nini kwetu, walianza kutunyang’anywa
kimoja baada ya kingine…mashamba yake aliyoyanunua mume wangu akiwa hai
yamegawanywa…’akatulia kidogo
‘Yamegawanywa kwa nani…?’ nikauliza
‘Kwa wanandugu kila mmoja akija na visingizio vyake, mara
hili shamba lilikuwa la familia, na mmoja akifa shamba linatakiwa kurudi kwa
familia,..mara hili eneo walinunua kwa umoja wa familia eti walichangiana ndugu
wakanunua kwa pamoja kwahiyo sasa
linakuwa mikononi mwa familia, nikajiuliza ina maana sisi sasa sio miongoni mwa
familia, jamani hata hawa mayatima hawana haki, waniache mimi mjane lakini hawa
ni haki yao….’akatulia akiwageukia watoto wake mmoja mmoja!
‘Ina maana wewe wakati mume wako ananunua hayo mashamba hukushirikishwa…?’
nikamuuliza
‘Hayo mashamba eti…wanawake hahaha,….. usijifanye hujui…kiukweli
yeye aliniambia ananunua hiki na kile na wakati mwingine tunakwenda naye,
lakini yeye kwa upendo aliokuwa nao kwa ndugu zake, kila kitu aliwaweka mbele
walikuwa kama sehemu ya maendeleo na
familia yao, yeye hakupenda ubinafsi, na ndugu zake walikuwa muhimu sana…’ akasema
‘Ikiwemo na wewe pia au sio..?’ nikauliza
‘Mimi si ndio yeye, alichofanya yeye kipindi hicho ni kama
nimefanya mimi, sikuwa na wasiwasi wowote…’akasema
‘Sasa kwahiyo wewe unauhakika kuwa mume wako ndiye alinunua
hayo mashamba, na kama alifanya hivyo si
kuna hati na kitu kama hicho, mume wako hakukuonyesha, au ilikuwaje hati hizo zikawa
mikononi mwa ndugu?’ nikamuuliza
‘Kipindi hicho sikuwa natilia maanani, sikujua haya yatakuja
kutokea, sikujua kuwa hawa ndugu watakuja kunibadilikia,….mimi sikuwa na wazo
hilo kuwa nichukue hati, au….niliwaona hawo shemeji zangu kama alivyo mume wangu…’akasema
kwa uchungu.
‘Sasa kwanini walikuja kubadilika….?’ Nikamuuliza
‘Hayo mimi sijui…na kiukweli tabia hiyo hawakuwa nayo kabisa….walianza
kubadilika pale walipooa…nakumbuka hata alipokuwepo mume wangu, ndugu zake hawa
waliishi kwa ushirikiano na kaka yao, lakini baadaye walianza mabadiliko
fulani,….walipooa, hata hivyo kwa muda huo walimuogopa kaka yao….walikuwa
wakimuheshimu sana kaka yao...’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema labda tabia hiyo ya ubinafsi
ilichangiwa na wake zao..?[ nikamuuliza kwa umbeya ili kutaka kujua hisia zake
‘Mimi siwezi kuwasingizia wake zao maana msimamo ni mtu
mwenyewe, kama mume unatakiwa uwe na msimamo wako ujue nini majukumu ya
familia, usiyumbushwe, lakini nii hisia zangu ziwezi kusema zaidi kuhusu hilo..’akatulia
‘Sasa hao wake wenza kwa shemeji zako, hawakuwa na
ushirikiano mwema kama walivyokuwa shemeji zako, maana mlitakiwa muwe pamoja au
sio, kwani haya yanaweza kuwakuta hata wao au sio..?’ nikamuuliza
‘Wewe hujui sisi wanawake, tuyaache hayo….’akasema na kutaka
kuacha kuongea lakini ghafala akasema
‘Klichonishangaza hata kushindwa kuamini ni pale tu mume
wangu alipokwisha kulazwa kaburini, …hao hao nilioishi nao kwa upendo akiwemo
kaka yao, walinibadilikia, ule upendo wa shemeji zangu haukuwepo tena…yaani
hata siwezi kuamini, hata wengine wananisingizia mabaya, hata siamini, niwezeje
kumuaa mume wangu…yaani inaniuma sana...’akatulia pale mtoto wake mkubwa
alipomshika akimuashiria asiendelee kuongea zaidi.
‘Mama akiongea hayo anazidi kulia..ni bora mama usiyaongee,
yameshapita, mungu atawalipa, kama ni haki yao waendelee kuwa nayo, lakini kama
ni haki yetu ipo siku mungu atatulipia…’akasema mtoto mkubwa, alikuwa na kama
umri wa miaka kumi na mbili hivi…
‘Ndio hata mwalimu wa dini alituambia dhuluma haidumu,ukidhulumiwa
ukimuomba mungu dua zinapokelewa moja kwa moja , tunamuomba mungu atatusaidia
mama,…’akasema yulemdogo, huyu anaweza kuwa ana miaka nane au tisa.
‘Mhhh…mimi bado hapo sijaelewa,…hati za mashamba na mali ya
mume wako walikuja kuchukua wao, au ilikuwaje,,,?’ akauliza
‘Nikuambie kitu, hawa shemeji zangu, wote walianzia maisha
yao humu, walikuwa wakiishi humu, lakini baadaye mume wangu akawasaidia kila
mtu akawa na nyumba yake, na ndio wakaoa mmoja mmoja, kwahiyo humu ndani
walipafahamu sana, kila kitu walijua kipo wapi,….nina uhakika wao walikuja
kuchukua kipindi mimi sijiwezi, kwani nilizitafuta hati sehemu zilipokuwa
sikuziona na nilipowauliza nikaambiwa hayanihusu, ….’akasema
‘Je kwa hali hiyo, mashamba kuchukuliwa, ….wewe ulikaa kimia
tu, hukutaka kudai haki zako….maana hiyoo ni haki yako wewe na watoto….?’
Nikamuuliza
‘Nikuambie ukweli hayo yote yalifanyika kipindi sijiwezi ,
ni miaka mingi sikuwa mnzima nilikuwa nusu mfu…itakuwa ni muda huo wao wakaja wakachukua
hizo hati, na mashamba wakagawana wakidai ni mali ya familia,…’akatulia
‘Na hilo nisingeligundua hadi pale nilipoanza kupata nafuu,….ni siku moja
nilianza kufuatilia, maana hali ilishaanza kuwa ngumu, angalau ikiwezekana
tuuze kipande cha shamba, ndio nikashangaa kukuta maeneo hayo mengine yamejengwa
nyumba za watu , nauliza naambiwa wameuziwa…’akasema
‘Mhh…basi yaonekana uliumwa sana, ilikuwaje kwani, ni
mshituko au…?’ nikamuuliza
‘Kifo cha mume wangu kilinichukua sana, nilipatwa na
mshtuko, nikawa nimeishiwa nguvu mwili mnzima, wanaita kiharusi,… nikawa mtu wa
kitandani, siwezi hata kuinua mkono,…nilibakia hivyo miaka nenda rudi kila kitu
kitandani…’akatulia
‘Mume wangu akiwa hai, nilikuwa na kazi yangu, kutokana na
mshutuko huo, kuumwa huko, hata kazi niliyokuwa nayo nikafukuzwa,…na pesa yote
iliyobakia ya mume wangu ilitumika kunitibia,..kiukweli mimi nilijua ni maiti
tu….’akatulia
‘Kilichokuwa kikinizuia ni hawa watoto…hebu fikiria sasa hivi
nipo hai wanafanya hivi, je kama ningelikuwa nimekufa ingelikuwaje, yaani hapo
ndio namshukuru mungu kuwa nipo hai, japokuwa siwezi kupambana nao, lakini …’akasema
na kuinua mikono juu
‘Kwahiyo kwa miaka mingi nilikuwa kitandani sijijui…ikafikia
watu wananiona kama mnzigo, walioweza kuja kunisaidia ni ndugu zangu wa
kuzaliwa nao, na wao ikafika muda na wao wamechoka, maana na wao wana familia
zao,…kuuguza mtu kama mimi ilikuwa ni
kazi kweli,…siwezi kuwalaumu..’akatulia
‘Na hao shemeji zako je…?’ nikamuuliza
‘Mhh, namshukuru sana huyu shemeji aliyekuwa amechaguliwa
kama msimamizi, kiukweli….sijui kwanini hili likatokea,….lakini alijitahidi
kuwa mwema kwangu.alinisaidia sana.’akatulia
‘Kwahiyo unataka kusema kuna mtu , yaani kati ya shemeji
zako yeye alichagiliwa kama msimamizi…au sio? Yeye akapewa mamlaka yote, ikiwemo hati za mali au
sio…..?’ akaulizwa
‘Ndio …..kutokana na hali yangu ilibidi ikafanyike hivyo, na
mimi hilo, japokuwa sikuwepo, japokuwa sikujua ni lini hayo yalifanyika, lakini
ilibidi…unaniona naongea hivi, sikuwa hivi, nilikuwa mfano wa maiti…kwahiyo walikubaliana
wakiwemo ndugu zangu kuwa awepo mtu wa kuchukua hatua, na huyo shemeji yangu ndio
akachaguliwa akayachukua majukumu yote, ya mali, ya watoto, matibabu….akajitahidi
alivyoweza…na ubinadamu tena, sijui ….’akatulia akitikisa kichwa.
‘Mhh….naona hapa bado kuna maswali mengi, lakini ngoja kwanza
nikuulize , sasa hii nyumba kwanini inapigwa mnada, na unasema,… mtoto kasema
baba yake hakuwahi kukopa hizo pesa ilikuwaje, ina maana ni deni lilikuja baada
ya mume wako kuondoka, au ilikuwaje?’ Nikamuuliza
‘Katika kitu ambacho mume wangu alikuwa hataki, ni kukopa,
hasa mikopo yenye riba, mume wangu alikuwa mcha mungu sana, na aliwahi kuniasa
kipindi nilipotaka kujiunga na vikoba, kuwa riba ni sumu ya mali halali, riba
inatafuta baraka yote kwahiyo niachane na maswala ya kukopa kwa riba,…ni kusema
kuwa mume wangu hakuwahi kukopa benki hilo nina uhakika, wakisema eti lilikuwa
deni la mume wangu ni uwongo…’akasema
‘Sasa ilikuwaje mkopo huu ukatokea maana ni mkopo mkubwa
sana, …?’ nikamuuliza na hapo mjane huyu akajaribu kujinyosha na kusema;
‘Ndio maana nikasema haya yote ni mbinu za kuhakikisha kila
kitu tunanyang’anywa…mkopo huu sikukopa mimi, na wala sijui ulivyokwenda hadi
ikafikia pesa nyingi kiasi hicho, hata mimi nashangaa, utakopaje, huku hujui
jinsi ya kulipa, hiyo si mbinu jamani…’akasema
‘Atakuwa ni baba mdogo…’akasema mtoto wake na mama yake
akamuashiria anyamaze..
‘Kama mtoto anavyosema, yawezekana kuwa shemeji au msimamizi
wenu ndio alikopa, na wewe wakati anafanya hivyo, ulikuwa bado hujawa na
ufahamu, au ulivyoambiwa hilo deni lilitokea wapi..?’ nikamuuliza
‘Lakini nikuulize unaniuliza haya maswali yote ili
iweje….sisi yote haya tumeshamuachia mungu, na nimekuambia hayo niliyoweza
kukuambia,…yatosha,…’akasema na kujikuanyata.
‘Samahani sana shemeji usione nakusumbua, nina nia njema,
huwezi jua msaada wangu kwako, mimi…’kabla sijamalizia akasema
‘Mimi sitaki tena kuja kuonekana mbaya, mungu yupo, nasema
haya kwani kuna kipindi tulikuja kukorofishana na huyu shemeji yangu, akaongea
maneno mengi mabaya sana,…kuwa yeye kajitokea, bila yeye ningekuwa wapi, kawa name
muda wote, akawa hahangaiki na familia yake ananihangaikia mimi tu, sasa
nimepona naanza kuleta kiburi….unaona, sasa mimi nashindwa kidai chochote…ndio
maana imefikia muda nimeona nimuachie mungu….inatosha’ Akasema sasa akiwa hataki kuongea tena.
NB: MAMBO ndio hayo, msinione nilikuwa kimia , nina mengi
nimeyapata kwa jamii….matatizo, visa vingi, lakini ndio hivyo nitafanyaje,bado
sijapata sehemu ya kujishikiza, lakini kwa uwezo wa muumba, ipo siku,
WAZO LA LEO:
USITENDE WEMA, ukiwa na malengo na kujinufaisha, wema
hulipwa na mwenyewe muumba, kama utataka unufaike na huo wema, basi huo sio
wema, hiyo ni biashara yenye kuhitajia malipo na malipo yake ukiyapata huo wema
haupo tena! Kumbuka wema hauuzwi, unajiuza wenyewe kutoka kwa muumba!
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Sawa ndugu wa mm tupo pamoja
Je tukio hili halijawahi kutokea maeneo ya kwenu, kwa jamaa zenu...watu kuwadhulumu yatima, wakala haki zao. Twashukuru sana kwa visa vyako
Post a Comment