Tuliamua kulifuatilia hili tatizo, kama tunaweza kuwahi, kwahiyo tukafunga safari ya kwenda hospitali aliyokuwa kalazwa huyo mdada, haikuwa vigumu kuipata kutokana
na vyanzo vyetu vya uchunguzi, na kinyume cha tulichotarajia, tulijikuta kwenye
matatizo makubwa, mpaka ilifikia kujuta kwanini tulifuatilia,lakini hayo ni
moja ya majukumu yetu ya kusaidia jamii.
Hebu tuone
mwanzo wa hitimisho hili, …ni nini kilitokea kwa mdada, ukumbuke hapa sio mdada
anajieleza , haya ni mambo tuliyokutana nayo tulipoamua kujua ukweli…kweli
dunia ina mambo….Tuendelee na kisa chetu
*********
Tulifika
hospitali ambayo alikuwa kalazwa mdada, tukajitambulisha kuwa tuna mgonjwa wetu
kalazwa hapo, na sisi ni marafiki wake, lakini marafiki wa mtandao….hatukutaka
kuficha jambo, kwani tulijua tunachofuatilia ni muhimu hata wao wanaweza
kutushukuru.
‘Mgonjwa
huyo ni rafiki wa mtandao, kiukweli hatujawahi kuonana naye uso kwa uso, ila
sisi tunatokea kwenye mtandao wa `diary yangu,..’ mtandao wa mambo ya kijamii na visaha vyenye kunasihi, ….sijui
kama uliwahi kuusikia…’tukasema
‘Mhh,
nausikia …sikia,unajua tena kazi zetu wengine hatuna muda wa kusoma soma visa,
ila mke wangu ni mpenzi wa mtandao huo, ehe sasa niwasaidie nini…’akasema
‘Sisi
hatutaki kukuficha,hapa kuna mgonjwa mmoja ambaye alilizwa akiwa mjamnzito, na
yasadikiwa kaathirika, na alikuwa kwenye mipango ya ushauri nasaha…ila kwa taarifa
zake alizotutumia ni kuwa alikusudia kujiua, na kwahiyo tumekuja tusaidiane
kumuokoa…’tukasema
‘Kujiua…?’
akauliza huyo dakitari msemaji mwenye dhamana hiyo, maana ilibidi kumtafuta mtu
ambaye ataweza kutuamini na mwenye mamlaka ya kutoa taarifa!
‘Ndio
tulipokea ujumbe wake kwa barua pepe, na maelezo yake kwa ujumla yaliashiria
hivyo, kutaka kujiua…’
‘Kwanini
atake kujiua…lakini hayo mbona yapo sana hapa, wanakuja watu kihivyo na baadaye
wanabadilika, sioni kama jambo la ajabu hapa kwetu ajabu yake ni kuwa nyie
mumekuja kufuatilia…’akasema
‘Kwa maelezo
yake haoni haja ya kuishi kwa matumaini kwani anajua baada ya yote ni lazima
atajikuta kwenye maisha magumu, yeye na mtoto wake, sisi tunaomba tuonane naye
kama hilo halijatekelezeka, maana tumefika hapa kwa haraka, ni swala la muda,…je
hakuna mgonjwa yoyote aliyetaka kujiua…mkagundua?’’tukauliza
‘Hapana….wapo
wanakuja wakijieleza hivyo,…lakini haijawahi kutokea akafikia hatua sasa anataka
kujiua mpaka kwenda kumuokoa,…anakuja kihivyo kachanganyikiwa baadaye anaeleweshwa
mapema na anakubaliana na ushauri lakini
kwa kipindi cha karibuni hakuna mgonjwa kama huyo,…labda ni taarifa za uwongo
za mitandao…’akasema
‘Hapana hizo
taarifa sio za uwongo, sisi huwa tunafuatilia taarifa yoyote inayokuja, tunajua
hiyo ni uwongo wa kutunga au huo ni ukweli…tuna uhakika hiyo ni taarifa ya
kweli na ni swala la kufuatilia kwa haraka, na hivi inawezekana tunapoteza muda…’nikasema
‘Je jina la
mgonjwa huyo ni nani…?’ akauliza
‘Mhh…ndio
tatizo hapo, yeye alijitambulisha kama mdada…mrembo, aka, malikia wa
kijijini…’nikasema na dakitari akacheka kidogo na kusema
‘Mnaona…hilo
jina tu linaonyesha dhahiri kuwa ni story za mitandao za kutunga, wayu kama hao
ni matapeli wanatafuta misaada kwa njia hiyo…’akasema
‘Docta, hili
ni swala la kumuokoa mtu, kama hijatokea basi kakusudia kufanya hivyo, inabidi
mufanye juhudi za kumuokoa…tusaidiane tumpate , yuna uhakika yupo hapa kwenye
hospitali yako…’nikasema na mwenzangu akaonyesha hamasa hiyo kwani hadi hapo
tuna uhakika hakuna dalili ya tatizo , huenda hajajiua.
‘Kiukweli
hakuna mtu kama huyo aliyewahi kufanya jambo kama hilo, na hakuna mwenye dalili
za kufanya hivyo, hebu niambieni yupoje kwa maelezo yake, maana atakuwa
kajieleza vya kutosha….’akasema na sisi tukamuelezea jinsi alivyo na yakuwa
alitokea kijijini akiwa mja mnzito akafikishwa hapo kwa ushauri nasaha…
Na hata
baada ya maelezo hayo dakitari huyo akasema;
‘Hatuna mtu
kama huyo hivi karibuni,…’akasema akiangalia saa yake kuonyesha tunampotezea
muda
‘Docta sisi
tuna uhakika na hilo….na nia yetu ni kuokoa, na hatungeliweza kuja hadi hapa
bila sababu ya msingi, na tunaogopa, inaweza kutokea jambo,na nyie mkawa
lawamani, kwani hamkutaka kushirikiana nasi…’tukasema na yeye hapo akawa kama
kaingiwa na shaka akasema
‘Mimi sina
zaidi cha kuwasaidia, labda kwa sasa mkajaribu kuongea na mshauri nasaha, kama
yeye atakuwa na kumbukumbu hiyo, lakini kwa utendaji wako na kwa taarifa nilizo
nazo hakuna jambo kama hilo ..mnasema ni lini mlipokea hiyo taarifa….’akasema
‘Jana
….usiku……’nikasema
‘Basi hakuna
kitu kama hicho, na hakuna mgonjwa mwanamama wa aina hiyo kwa hivi
sasa…’akasema
‘Hakuna
mgonjwa kama huyo mliyetakiwa kumfanyia upasuaji akiwa na matatizo hayo, jana
…au leo asubuhi,..?’ tukauliza
‘Hakuna…nina
hakika huo, kwa maelezo zaidi basi nendeni mkaongee na mhsauri nasaha yeye
atawathibitishia hilo, si mnasema huyo mgonjwa alitumwa kwake…si ndio hivyo,
nendeni ofisini kwake…’akasema
Basi ilibidi
tuombe kibali cha kuonana na mshauri
nasaha huyo, ila tukaambiwa kwa muda huo hayupo,…tukawa hatuna jinsi ila
kumsubiria, tukiombea mungu huyo mgonjwa asije akafanya hilo jambo..kama kweli
hajalifanyika
Baadaye
kidogo mshauri nasaha alifika, …
**********
‘Kwani nyie huyo
mgonjwa mnayemuulizia kama kweli yupo ni nani kwanu, maana mambo yote
yanayowahusu wagonjwa hapa ni ya siri ya wagonjwa na labda na familia zao
husika, na sisi kama watendaji wao, tunalinda haki na usiri wa wagonjwa..?’
akauliza
‘Sisi ni
rafiki zake wa mtandao, tuliwasiliana naye kwa njia hiyo, alituelezea kadhia ya
maisha yake na hatua ya mwisho ndio akaandika hivyo kuwa anataka
kujiua…’tukasema
‘Unajua watu
kama hao wanaofikia kusema wanataka kujiua wanakuwepo hapa, wanakuja kwa
dhamira hiyo, lakini mwishoni baada ya kukaa nao, tukawapa ushauri nasaha wanakuja
kubadilika, sasa sijui ni yupo kati ya hao wengi,na hatujapata kadhia kama hiyo
hivi karibuni mimi, sikumbuki…?’ akauliza
‘Mdada huyo
alitokea kijijini na aliletwa kwako na ndugu yako…’tukasema na hapo akaonyesha
kama kushituka kidogo lakini akaificha hiyo hali, na kwa macho ya kama kudharau
hayo maneno akasema
‘Aliletwa na
ndugu yangu, hivi karibuni, jana,juzi ….mmh, sikumbuki….’akasema
‘Sio kwamba
alimleta yeye, ila ndugu yako huyo alimuagiza kwako, na wewe ukaenda kumpokea
kituoni na wakati mnakuja naye kuelekea kwako, ukahisi hali yake sio nzuri, ikabidi
mpitie kwanza hapa hospitalini, akaonekana ana upungufu wa damu….’tukasema na
hapo akaonyesha kama kukumbuka jambo akasema
‘Mnasema yeye
huyo alitokea kijijini alikuwa mjamnzito, alifika hapa kwa maelekezo ya ndugu
yangu, akawa na tatizo la upungufu wa damu…au sio, mhhh… aliyemuagiza kuja
kwangu ni ndugu yako, sijui kama ni huy…lakini hapana sio yeye…’akasema sasa
akiwa kautulizana, akitafakari
‘Lakini kwa
kumbukumbu zako yupi mtu kama huyo..?’ tukauliza
‘Ok…sijui
kama ndio huyo…ila kama ndio huyo mimi siwezi kusema lolote kumhusu yeye kwa hivi
sasa…’akasema kwa sauti ya huzuni, akitikisa kichwa
‘Kwanini
mshauri nasaha, kwanza tukuambie kuwa tumekuja hapa kwa haraka ili ikiwezekana
muweze kumuokoa kwa tatizo hilo la kupanga kujiua, na kama haijatokea mtu kujiua,
au kukusudia kujiua,…basi ina maana bado yupo, na jinsi alivyotuelezea kama
hakufanikiwa kunywa hiyo sumu basi mtakuwa mumeshamfanyia huo upasuaji, lakini
ni vyema mkachukua tahadhari, na kama inawezekana tunaomba tuonane naye.’ Tukasema
‘Ndivyo
alivyowaambia kuwa mje kuonana naye…au nyie mnapenda kufanya hivyo?,….lakini
mimi bado sijakubaliana na nyie, hakuna mtu kama huyo…’ akauliza na kusema
‘Hajasema
tuje kuonana naye..ila ni muhimu kama yupo tuonane naye kuna maswali ya kijamii,
kama wasamaria wema tungelipenda kumuuliza na vile katuamini hadi kutuandikia sisi
hayo yote tuna imani atatupokea kama ndugu zake….’tukasema
‘Sio
kweli…’akasema
‘Kwanini
unasema hivyo….?’ Tukauliza
‘Kama ndio
huyo mnayemzungumzia, …sio kweli, kuwa atawapokea nyie kama ndugu zake,…kwasababu
asingelipendakabisa hilo litokee, ..la kuonana na watu…sio kweli, na hata hivyo
kamani huyo hamuwezi kumuona tena….’akasema
‘Hatuwezi
kumuona tena! Ina maana tumechelewa au una maana gani, kwahiyo alijiua kweli, keshashakufa…au …?’
tukauliza kwa mashaka.
**********
‘Kama
nilivyowaambia mimi kama mshauri nasaha siruhusiwi kutoa taarifa zozote za
mgonjwa wa hapa,..japokuwa utawala umesema nishirikiane nanyi kwani nyie
mnaonekana hamna nia mbaya…’akasema
‘Ni kweli
nia yetu ni kusaidiana kwa hilo, kusaidia jamii kwa ushauri, hasa kwa njia ya
mtandao lakini ikibidi tunawatembelea watu kwa nia hiyo hiyo, …ikitokea jambo
la kufanya hivyo, kama ni uhalifu, tunashirikiana na polisi, na kama jambo kama
hili , tunawahi kuokoa kabla halijafikia kubaya,…’nikatulia kidogo
‘Tungelikimbilia
polisi, lakini tuliona haina haja,ngoja kwanza tumuokoe ..ndio maana
tukaimbilia huku kwa nia njema, kama hajafanikiwa kufanya hivyo basi tuongee naye
tu, kumnasihi tunavyoweza…’tukasema.
‘Ndio
nimeshawafahamu…. hata mimi nafuatilia visa vyenu vyenya mafunzo, msione kuwa
madakitari tupo tu, tunasoma mambo mengi sana hasa yenye manufaa kwa jamii,
hasa kwenye hii kazi yangu ya nasaha, ninajitahidi sana kuwa karibu na jamii,
na kikweli nimependa sana mnavyoisaidia jamii kwenye mtandao kwa njia ya visa
mbali mbali,….lakini hili swala kwa hivi sasa lipo nje ya uwezo wangu, kwa
jinsi lilivyo…’akasema.
‘Labda
utujibu kwa mkato, maana tusipoteze muda wako, …na sisi tulikuja kwa haraka
kama zima moto wameitwa kuzima moto,kama tumewahi au la,..je kuna tatizo au
hakujatokea tatizo, kama hilo, ?’ tukauliza
‘Kwahiyo
nyie mlikuja kufanya nini hasa, kutoa taarifa kuwa tufuatilie au kuja kusaidia
kuokoa,…kwanini nauliza hivi, maana kama ni huyo mnayemzungumzia mbona mumechelewa
, …..?’ akauliza
‘Sisi
tulipoisoma tu hiyo barua pepe, tuliamua kuchukua hatua za haraka iwezekanavyo
ndio maana tumekuja hapa hata bila ya kupoteza muda baada ya kuhakikisha kuwa
barua pepe hiyo sio ya uwongo ni kweli,…’tukasema
‘Basi
mumechelewa….’akasema
‘Kwa vipi…?’
tukauliza kwa mashaka
‘Kama ni
huyo ambaye ninajua taarifa zake, aliyetumwa kwangu na ndugu yangu mbona ni
tukio la muda, ni kiasi cha wiki mbili sasa na siku kama tano zimeshapita, ndio maana nahisi tunaongelea
watu wawili tofauti, na mimi huwa nahudimia watu wengi…sasa sijui kama ndio
huyo…’akasema
‘Atakuwa
ndio huyo…alikuwa mja mnzito kutoka kijijini na kaelekezwa na dada yako kuja
kwako, kwa ajili ya matibabu na ushauri nasaha, lakini tukio hilo ni la jana,
sio wiki mbili…’tukamfafanulia vyema, akatulia akiwaza halafu akasema
‘Kuna mmoja
alifika hapa akiwa na mja mnzito kweli , alifika kwa kuelekezwa na dada yangu kweli,
tukampokea na kujitahidi kumsaidia kadri tulivyoweza, tulimpa ushauri nasaha,
akakubaliana nasi, lakini katika hatua za kwenda kufanya upasuaji kukatokea
jambo ambolo haturuhusiwi kuliongelea kwa hivi sasa kwani lipo juu ya uwezo
wetu….’akatulia
‘Sawa
inawezakana kumetokea matatizo au sio… na polisi wamehusishwa au sio….sisi
tunachotaka ni kuwa na uhakika je tumemuwahi, je kuna baya limetokea,…au vipi
kama hakuna tuweze kuonana naye tu….’akasema mwenzangu.
‘Lakini sio
huyo kutokana na muda mliosema…’akasema
‘Yawezekana
ndio huyo,kama tunaweza kumuona itakuwa ni vyema zaidi…tukaongea naye sisi
wenyewe..’nikaongezea kusema na yeye akabakia kimia kwa muda, mimi nikauliza
‘Je aliwahi
kunywa hiyo sumu…..kumeza hicho kidonge kwa nia ya kujiua au la…?’ nikauliza
‘Mimi
ninachoweza kuwaambia kwa hivi sasa, kama ni huyo hamuwezi kumuona…’akasema
‘Kwanini
docta, tunaomba sana basi utupe maelezo ya kujitosheleza ili tukiondoka hapa na
sisi tujue la kufanya, …’tukasema
‘Nina maana
yangu kubwa kusema hivyo, kama ingekuwa yupo hapa hospitalini kwanini
nisiwaruhusu kwanza nyie mnafanya kazi ambayo na mimi naifanya, kusaidia jamii,
japokuwa mimi ni mtaalamu zaidi yenu, na sihitaji msaada, lakini nafahamu
juhudi zenu…’akasema
‘Sawa kabisa…wengi
wanaotufahamu tunashirikiana kwa wema kabisa…japo kuwa tunajitolea tu…ni kazi
kubwa, lakini wema hauozi…..’tukasema
‘Ni
kweli…wema hauozi,…Lakini mnielewe hamuwezi kumuona huyo mtu,kwani
hayupo…’akasema na kukatiza na mimi nikatafsiri moyoni kuwa alitaka kumalizia,
`duniani’ kuwa keshafariki..lakini sikupenda kutumia neno hilo na mwenzangu
naye akauliza kwa haraka
‘Ina maana
keshaondoka…?’ akauliza
‘Siwezi
kusema….’akatulia kama akiwanza na mimi nikazidi kumuuliza
‘Kwahiyo kwa
kifupi, mlifanikiwa kumfanyia upasuaji salama na keshaondoka, ni bora
utuelekeze wapi tunaweza kumpata ili tuongee naye asije akabakia na wazo hilo
tena, ina maana hakukubali kubakia kwenye mamlaka yako tena, maana alikuwa
akihitaji msaada wa kijamii wa hali na mali?’ tukauliza
‘Mnajua
nasita kuwaeleza zaidi ya hapo kutokana na hali ilivyokuwa, ni nyeti na hatari,
mnaelewa, ni swala la kiusalama….’akasema
‘Basi kwa
msaada wako tunaomba utuamini, hebu tuambie japo kwa ufupi, Ilikuwaje, labda
utufafanulie japokuwa unasema ni siri lakini tuambie yale unayoweza kuelezea
ambayo hata sisi yatatusaidi ili turidhike, ilikuwaje , tusipoze muda au hilo
nail huwezi kutusaidia?’ nikauliza
Mshauri
nasaha huyu alitulia kwa muda,…baadaye aliamua kutuambia ukweli, tuliohitajia…
****************
‘Unajua
aliyekuja kuniambia na kutusaidia kwa hilo ni huyo jamaa kutoka kijijini, na
aliniambia hilo wakati tunaongea naye kuhusu aliyekuwa mchumba wa huyo mdada
akaniambia kuna jambo jingine muhimu sana anataka kuniambia na kwa muda huo
nilikuwa na miadi mingine kwahiyo nilimuambia
‘Sikiliza
kama ni mambo hayo hayo, wewe achana nayo mimi mwenyewe nitajua jinsi gani ya
kuongea naye…’nikamwambia
‘Hapana sio kuhusu huyo mchumba wake tena, hilo linamhusu
huyo mgonjwa wako mwenyewe ina maana mdada, malikia wa kijiji…..yeye anakusudia
kujiua….’akasema
‘Kujiua!!
..ndivyo alivyokuambia hivyo, lini..?’ nikamuuliza kwa mshangao, japokuwa
kiukweli sikuona ajabu , maana kuna wengi wanakuja na msimamo huo, lakini
tunapokutana nao tunawashauri na wanakuja kubadili nia yao, nikahisi huenda
alisema hayo awali kabla hajapata ushauri nasaha
‘Lakini
naomba usije kumwambia ni mimi nimekuambia hilo, …kwani ni hatari zaidi akijua nimekuambia
na ni hatai zaidi pia akijua mumemfahamu dhamira yake yake hiyo….’akasema
‘Kwanini, na
alikuambia hayo muda gani…?’ nikamuuliza
‘Muda ule
ule uliponikuta naongea naye,…na nahisi kapanga kufanya hilo kabla ya upasuaji,
na nijuavyo mimi watu wa kundi hilo wakidhamiria hivyo kutokana na kiapo chao,
hawarudi nyuma kwani yawezekana ni kutokana na shinikizo la kundi…sina uhakika
zaidi, ila yeye kaniambia ni kutoka na kujua kuwa huko mbele hatakuwa na maisha mazuri, yeye ni mtu wa
kufa tu.. ’akasema na mimi hapo nikahisi kuna jambo, nikatulia kidogo na yeye
akaniuliza swali kwa haraka
‘Ni lini
mnatarajia kumfanyia upasuaji,…?’ akauliza
‘Kesho , leo
au keshokutwa hiyo ni kazi ya madakitari….’nikamwambia
‘Basi
ningewashari upasuaji huo muufanye haraka iwezekanavyo,na pia mumuwahi
kuhakikisha hazitumii hizo dawa, ikibidi mziondoe kwenye himaya yake, kwani
anaweza kuzitumia muda wowote ule kutegemeana na shinikizo la kundi hilo,...na
pindi akizimeza, hamuwezi tena kumuokoa….fanyeni hivyo haraka iwezekanavyo…’akasema
kwa msisitizo
‘Dawa gani
hizo, zipoje….?’ Nikamuuliza
‘Wewe
fuatilia hilo ni muhimu sana, ..siwezi kusema ni dawa gani hizo , ila
ninachojua ni vidonge akivimeza tu vitamuua hapo hapo…..na hamtukuja kujua ni
sumu….’akasema na mimi hapo nikaanza kuingiwa na wasiwasi. Kiukweli mwanzoni
sikutilia maanani lakini alipotaja sifa za hiyo sumu, nikaanza kuingiwa na
mashaka.
‘Niliongea
naye mwenyewe akakubaliana nami kuwa kaelewa kwanini atake kufanya hivyo tena,
kuna yoyote aliyokuambia ya kubadili nia yake , maana tulikubaliana naye
akasema yupo tayari kufuatilia ushauri wangu...?’ Nikamuuliza
‘Mshauri
nasaha, dakitari….usije kujutia kwa hili…wahini, tafuteni mbinu haraka ili
muweze kulizuia hilo, kabla hamjachelewa, ..mimi nimetimiza wajibu wangu, japokuwa
kwa kufanya hivyo najiweka kwenye maisha hatarishi zaidi…’akasema
‘Lakini
haiwezekani , hata kama anazo hawezi kuzitumia…lakini kama unavyosema basi
itakuwa ni vyema kuziondoa kwenye miliki yake….,kwani kweli huko mbele, anaweza
kubadili nia….’nikasema
‘Naomba
unielewe mshauri hayo ninayokuambia sio swala la kukisia, huyo anatarajia
kujiua, mimi nina uhakika,…wanachama wengi wa hilo kundi walivyoapishwa kwa
vitisho, na sio vitisho ni kweli wanafanya hivyo,…kwahiyo hapo japo hakuniambia
hivyo, anaogopa asipofanya hivyo, wazazi wake watateswa au kuuwawa…hata hivyo
yeye akijiua hatapoteza kitu kutokana na hali aliyo nayo kuwa hatapona…’akasema
‘Unasema
wanachama wa kundi hilo, ni kundi gani hilo...?’ nikamuuliza
‘Mimi
nawaombeni wala msipoteze muda, nendeni kwenye mkoba wake wa kike,…ni lazima
zitakuwepo hizo dawa humo, sizani kama anaweza kuzificha sehemu nyingine…ziondokeni
mikononi mwake…mtakuwa mumefanya jambo muhimu sana kuliko kuhangaika kujua ni
kundi gani,…’akasema
Kwa kusikia
hivyo, niliona nimeshindwa jukumu langu kama mshauri na haijatokea, wengi
nawasaidia,na wakikubali, haitokea kinyume chake, na kama huyo mdada atajiua
mimi nitakuwa matatani,…na hata kama nitaweza kujinasua kwa hilo, lakini nafsi
yangu itaumia sana, kwahiyo niliposikia hivyo, ikabidi niwasiliane na utawala
wa hospitalini, na ilikuwa ni swala la muda. Je huyo mdada atazitumia hizo dawa
au la na akipanga kuzitumia ni muda gani…haikujulikana .
Ikabidi
tuharakishe hata upasuaji wake, ili kutokuweza kumpatia muda mwingine, lakini
pia lazima juhudi za haraka zifanyike kumuokoa huyo mdada, kama alivyosema huyo
jamaa kutoka kijijini kuwa mdada kwa hivi sasa kama hatafanikwia kulifanya hilo
atakuwa akiwindwa, kwani wenzake watakuwa hawamuamini tena ,……
Ikabidi
juhudi za haraka zifanywe kuupata huo mkoba wake ambao alikuwa habanduki nao,
na ilitakiwa kufanyika hivyo bila hata ya yeye kufahamu, kitu ambacho kilikuwa
kigumu sana, mdada habandukani na huo mkoba wake…
‘Je
tumwambie?,….ilikuwa jambo la mwisho kufanya kutokana na alivyotuonya huyo
jamaa…
*********
Tukaanza mikakati ya haraka na kuhakikisha
kila mara kuna mtu anakuwa karibu yake, japo kujifanya kama anahudumia wagonjwa
wengine lakini ahakikishe hachezi mbali na huyo mdada….ujue hayo yamefanyika
kwa muda mfupi sana. Kuna nesi wetu tunamuamini sana, tukamtumia ili tuweze
kumfanya awe mbali na huo mkoba wake.
Nesi akafanya
hilo, alitumwa ili amwambie huyo mdada kuna maandalizi yanatakiwa kufanywa kabla ya kufanyiwa huo upasuaji, nesi
huyo akaelekezwa cha kufanya ili watoke naye hadi huko bafuni na ajitahidi
kumchelewesha ili tuzipate hizo dawa, na ikibidi tuwexe kuzibadili hizo dawa za
sumu na dawa nyingine ili asije kugundua hilo.
Kama nilivyosema nesi anayemuhudumia mara kwa
mara huyo mdada, anasema Mdada huwa haachi mkoba wake hata akienda bafuni au
chooni, lakini tulimwambia huyo nesi ajitahidi, awezavyo ili mdada aweza kuucha
huo mkoba wake, haikuwahi kutokea tangia afike hapo kuachana na huo mkoba wake.
Nesi
alifanya kazi yake na kweli huo mkoba ukapatikana, na kwa muda huo na sisi
tulishatafuta dawa tunazohisi zinazofanana na hizo..kwa kukusia,.kama
alivyotuelezea huyo jamaa kutoka kijijini
Lakini tulipoziona
hizo dawa tukakuta haziendani na hizo tulizozipata,…, ikabidi zitafutwe
nyingine kwa haraka ili kuzibadili …nia ni kuhakikisha huyo mdada haligundui hilo
kuwa tumezibadilisha, lakini cha muhimu ni kuwa tulishaupata ule mkoba na zile
dawa zilishakuwa mikononi mwetu….
‘Hizo dawa
zipoje…?’ nikauliza
‘Ni vidonge
vidogo sana, vyeupe….sisi tulipovipata mtaalamu wa dawa akaitwa na kwenda
kuvichunguza, ilikuwa ni swala la muda…ziligundulakana kuwa ni sumu inayoweza
kumuua mtu kwa haraka sana, na ikipita saa moja huwezi kugundua kuwa mtu huyo
kauwawa kwa sumu na huwezi kugundua mtu
huyo kauwawa na aina gani ya sumu, utakachogundua ni kuwa mtu huyo kapatwa na
shinikizo la damu.
Sumu au aina
hiyo ya dawa hutumiwa sana na majasusi wa kimataifa…kuwaua watu wao au kujiua
pale anapokuwa kwenye hatari kama hataki kusema au kutoa siri!
‘Majususi wa
kimtaifa …?’ tukauliza kwa mshangao
‘Ndio hivyo,
ndio maana hatukutakiwa kuwaambia hili, ila kwa vile mumeonyesha uaminifu na
mpo tayari kuliweka hili kama siri hadi hapo polisi watakapofanya uchunguzi wao,
nimeona niwaambie tu…ili muwe na tahadhari hiyo na muache kupekenya
pekenyua..ni hatari…’akasema.
‘Sasa
ikawaje ….maana mpaka hapo angalau umetupa ahueni kuwa mdada hakuwahi kumeza
hizo dawa…au sio…?.’tukasema
‘Hilo
halikusaidia bado…kwani hatukuwa na uhakika…kuwa humo kwenye bahasha kulkuwa na
dawa ngapi kabla, kwani huenda kuna moja alikuwa keshaichukua tayari kwa ajili
ya kuitumia na kwa jinsi ilivyo ndogo anaweza hata kuiweka kwenye kucha zake
ndefu, na ndivyo alivyofanya…..’akasema na sisi hapo tukaingiwa na wasi wasi
tena…
‘ Tulipogundua
hilo, kuwa hapo tunashughulika na mtandao wa kijasusi wa kimataifa, mimi pamoja
na utawala, haraka tuliwasiliana na
polisi ,…kwani ilikuwa sio swala la kusubiria tena hata kama ni mgonjwa wetu
lakini kwa hali hiyo ni muhimu kuchukua tahadhari zote, lolote laweza kutokea…
Polisi
walipokuja cha kwanza ilikuwa kumkamata huyo jamaa kutoka kijijini ili kuisaida
polisi , wao wanajua namna yao ya kulifuatilia swala kama hilo, tunachoshukuru
jamaa aliweza kushirikiana na polisi vizuri sana, sasa hatujui ni kwa nia njema
au ni moja ya mbinu zao..’akasema
‘Kwanini
tena, kama aliamua kumuokoa mdada, na tena akakubali kushirikiana na polisi..?’
tukauliza
‘Hawa watu
ni wajanja sana…anaweza kufanya hivyo kwa lengo maalumu, ndio maana polisi
walihakikisha yupo nao hadi hapo uchunguzi wao ukamilike, anasema kundi hilo
lina watu mpaka madakitari….’akasema
Wakati polis
wanaendelea na uchunguzi wao kwa tahadhari , maana mdada hakutakiwa afahamu
lolote hadi hapo ili kutokumuongezea shinikizo lolote la moyo, sisi tukawa na mdada, sasa kwa tahadhari
kubwa…
Huko polisi
jamaa wa kijijini akawa anashirikiana na polisi,
Yeye alikiri
kabisa kuwa hata yeye alikuwa mmoja wa kundi hilo, na kama angekuwa nia mbaya
angeacha mdada ameze hicho kidonge lakini alishaamua nafsini mwake kujitoa
kabia kwenye hilo kundi na kujitakasa na toba kwa mungu, na alikuwa tayari kufa
kwa ajili ya kusaidia jamii, kwani kama alivyosema anajua uhai wake ni mfupi tu.
Kwahiyo
ndugu zanguni maswala yote kwa hivi sasa yapo mikononi mwa polisi….’akamalizia
hivyo
Sasa ikawaje
kwa mdada…?’ tukamuuliza tukiwa na hamu ya kujua zaidi na kabla hajasema neno
mara mlango ukagongwa na jamaa akaingia , kwa kumuangalia tu niligundua ni mtu
usalama,
Je kuna nini
kinandelea
….je mdada
amekufa, au yupo hai, na nini kinachoendelea …
WAZO LA LEO ;
Msaidie mwenzako wakati wa shida, hasa
akiumwa, jibidishe kumsaidia kwa hali na mali kwani kwa kufanya hivyo unaweza
kumuokoa na kifo…japokuwa kifo hakikimbiwi siku ikifika…Tusipende kusubiria mtu
kafa ndio tunajazana msibani na kuchanga mapesa mengi tukijifanya tulikuwa
tunampenda, hiyo haisaidii tena kwa marehemu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment