Wakati tupo
tunaongea na huyo mshauri nasaha,mara mlango ukagongwa na akaingia jamaa , akiwa
na koti refu na mkono kauweka mfukoni kuonyesha kuna kitu kakishikilia,
akasimama mlangoni, kwa muonekano wake nilitambua kabisa huyo ni askari,….
Docta
akamwangalia kama anataka kumuuliza ana shida gani, nahisi hata yeye
alishagundua huyo mtu ni nani, au huenda anamfahamu, lakini alivyoingia sio kistaarabu, maana
aligonga mlango mara moja halafu akaingia, na dakitari akasema...
‘Samahani bado nina wahudumia hawa, unaweza
kusubiria kidogo.
‘Habari
zenu, na samahani, mimi ni mtu wa usalama,
,…’ haraka akatoa kitambulisho
chake hewani.
‘Nyie wawili
mnahitajika kituoni kuisaidia polisi,…’akasema na mshangao ukatawala kila mtu
akilini akiwaza lake..
‘Kwanini…?’
nikauliza
‘Hayo
mtaambiwa huko mkifika, simameni….’akasema
‘Huwezi kuja
kutuamrisha hivyo, tuna haki zetu kama raia, tuambie kwanza kosa letu ni nini,
…maana sisi tuna uhakika sio wahalifu…’mwenzangu akasema
‘Hii ni amri
halali…mnahitajika kituoni, simameni ….’akasema kwa ukali akiwa ametowa
karatasi nyingine yenye maelezo ya kuja kukamatwa kwetu, hakutupa muda wa
kuisoma, alionyesha tu.
Tulimwangalia
docta ushauri, naye alionekana kuwa na mashaka kidogo, baadaye akasema;.
‘Hawa ni wateja
wangu wamekuja na matatizo yao, unapokuja na kuwakata mbele yangu sio taratibu
nzuri, basi ungelisubiria wakitoka, kwa namna hii huoni unaniharibia biashara
…’akasema dakitari.
‘Haya
mtaongea huko mbele, na samahani dakitari kwa hilo, sisi tunatumiza wajibu
wetu….utaambiwa ni kwanini…’akasema
Tulibakia
kwanza kimia, hakuna aliyesimama.
‘Mnasikia
simameni twende,….mpo chini ya ulinzi na lolote litakalokwenda kinyume na
maagizo yangu litachukuliwa kama kukiuka amri halali ya serikali…’akasema na
mshauri nasaha akasema
‘Sawa nyie
fanyeni anavyotaka ni kawaida kutokana na hilo tukio, tutaongozana na mimi nitakwenda
kuwatetea huko kituoni…’akasema na sisi tukawa hatuna jinsi tukatoka nje, na
kuwakuta jamaa wengine wanne hawa walikuwa na silaha kabisa, nikaona sasa kuna
tatizo tukawa hatuna namna, tukaingizwa kwenye landrover na safari ya kwenda
kituoni ikaanza.
*********
Tulipofika
kituoni tukaandikisha majina na maswali machache ya kazi tunafanya na pale
hospitli tulifuata nini, tukawaambia tulifika kuulizia mgonjwa wetu…
‘Huyo
mgonjwa wenu ni nani….?’ Wakauliza
‘Ni jamaa
yetu tu…’tukasema
‘Jina lake
ni nani, kwani hana jina, si jmaa yenu mnamfahamu au sio…’akasema
‘Kwa ujumla
hatufahamu jina lake ila tunafahamu kuwa alikuja hapo kutibiwa, na bahati
tumeambiwa hayupo…’tukasema
‘Nyie watu
wa ajabu mlikwenda hospitali kumuona mgonjwa ambaye hamumfahamu hata jina lake,
tusipotezeane muda jina lake ni nani…?’ akauliza
‘Tumekuambia
kuwa hatufahamu jina lake…unataka tutunge jina la uwongo…’tukasema
‘Kwanini
sasa mliingia kwa huyo dakitari ushauri badala ya wodini..?’ akauliza
‘Kwasababu
huyo mgonjwa hatumkuta, ikabidi tufike kwa huyo mshauri tupate maelezo
yake…’tukasema
‘Ndugu,…hili
ni jambo nyeti, na msiposhirikiana nasi mnaweza kujikuta kwenye matatizo
makubwa sana…’akasema
‘Sasa sisi
tushirikiane nanyi kwa lipi…hatujui tumekamatwa kwa kosa gani, tunashindwa hata
kujitetea…’tukasema
Huyo askari
aliandika maelezo yake, tukaambiwa tuingie kwenye chumba kimoja wapo tukaambiwa
tusubirie humo. Dakitari nasaha yeye libakia nje akiongea na hao watu wa
usalama, baadaye sasa tukaanza kuitwa mmoja mmjoa na kukutana na jamaa
aliyejitambulisha kuwa ni mpelelezi wa makosa ya ujasusi.
‘Makosa ya
ujasusi….?’ Tukauliza
‘Ndio
muelewe hivyo, kuwa swala tunalolishughulikia ni nyeti, na kwahiyo mnahitajika
kutoa ushirikiano unaostahiki, …’akasema na akaanza kuuliza maswali, na kwa
jinsi alivyo alikuwa akifahamu vyema kumuingia mtu kirafiki mpaka unajikuta
unaongea yote anayoyahitajia
Baadaye
akasema
‘Mnajua
msione kama mnasumbuliwa, lakini kwa hali kama hii inabidi kila anayehusika kwa
namna moja au nyingine, iwe kwa mawasiliano,…au kwa njia yoyote,inabidi
ahojiwe, na ushirikiano wenu ndio utakaotufanya tuweze kuikamilisha kazi yetu
kwa haraka…’akasema
‘Kwahiyo
tunaweza kuondoka…?’ tukauliza
‘Mimi
nimemalizana nanyi, siwezi kuwaambia muondoke, subirini maagizo ya
waliowakamata, …’akasema na kuondoka.
Tulirudishwa
tena kwenye kile chumba, kulikuwa na joto, hewa nzito,lakini
tutafanyje….walikuwepo jamaa wengine wa
makosa mbali mbali. Na tulipooona muda unakwenda tu, hakuna
kinachoelezewa ikabidi tuanza kupaza sauti
‘Hawa watu
vipi jamani…’tukaulizana, na baadaye akaja dakitari ushauri nasaha akasema kuwa
mkuu wa kituo kasema hawezi kutuachia kwa leo kwani kuna uchunguzi unafanyika,
kwani inaonyesha tuna mahusiano ya mawasiliano na hao washukiwa…
‘Washukiwa gani…?’
tukauliza
‘Ni pamoja
na huyo mliyekuja kumuulizia, kwa hivi sasa kile aliyekuwa na mawasiliano naye
anakamatwa, ni taratibu zao…’akasema
‘Lakini
ushahidi unaonyesha kuwa huyo mdada alituandikia barua pepe tu, na alifanya
hivyo ili kuelezea matatizo yake, sasa sisi inakuwaje tuingizwe huko….?’
Tukahoji
‘Hii ni
kawaida ,…kutokana na sheria hizi za makosa hayo,…kwani huu ni uhalifu wa kimataifa,
hamuwezi kuachiwa mpaka wajirisizhe wenyewe..kuna mawasiliano yanafanyika
kuangalia nyendo zenu zote,…mitandao yenu yote itachunguzwa, …’akasema
‘Hiyo sio
haki…’tukalalamika
‘Ndio sheria
za ugaidi kwa hivi sasa….’akasema
‘Ugaidi…kwani
hilo linaingilianaje na ugaidi!!!?’ tukauliza kwa mshangao
‘Ndio imegundulikana
kuwa kundi hilo, linahusiana na majasusi wa kimataifa ambao wamewekwa kwenye
kundi la magaidi wa kimataifa…na huyo mliyemuuliza alikuwa akitumiwa na hao watu ama bila kujijua au anafahamu na
yupo kwenye kutekeleza majukumu aliyopangiwa….’akasema
‘Mhh, sasa
hapo inanitia mashaka, lakini huyo mtu alikuwa mgonjwa kweli, na alihitajia
huduma yenu, kweli si kweli, na mlihakikisha kuwa anaumwa,.. inakuwaje docta’
tukauliza
‘Msijali,
inabidi mvumilia tu kidogo, na subira huvuta heri…’akasema na tukawa hatuna
jinsi , jioni ikaingia, mara usiku….hakuna kinachoendelea,…ikabidi tulale hapo
kituoni, mbu, …na harufu mbaya, …usiombe, kweli hujafa hujaumbika sikutarajia
nitalazwa sehemu kama hiyo.
***********
Kukapambazuka
kwa shida…na asubuhi tukaambiwa tujisafi, kupiga mswali kama unao….tusibirie
kuitwa. Kiujumla, japokuwa nafanya kazi za kujitolea, na unatakiwa uwe tayari
kupata shida, …lakini siku hiyo nilikereka sana, sikupendelea jinsi walivyotufanyia,
lakini tukawa hatuna la kusema, kwani wao wamesimamia kwenye sheria hiyo ambayo
haina cha kuulizwa…
Baadaye
tukaitwa ofisini kwa mkuu wa kituo, na hapo tukakutana na maofisa watatu, kila
mmoja alikuwa akihoji mambo yanayomstahiki, kuna wa maswali ya mtandao, kuna wa
maswali ya uhalifu, kuna wa maswali ya
kisheria ,huyo wa kisheria alijifanya kama mtetezi fulani wa haki lakini ndani
ya kazi zao, anauma na kupulizia, ili tu isionakane tumeonewa.
Maswali yao
yalikuwa ni yale , …tulifika hapo hospitalini kumuona nani na kwanini..je huyo
mtu tunamfahamu, na tulianza kufahamiana lini…ni kwanini akatuandikia sisi..na
kwanini tukaamua kumfuatilia….tuna kibali gani cha kufanya hivyo, je
tulishawahi kufanya hivyo tena, na kwanani…yaani maswali chungu mbovu
Baadaye
tukaambiwa tusubiria, haikupita muda akaja jamaa mwingine ambaye naye ni askari
upelelezi,akawa anaongea nasi sasa kirafiki zaidi, na alikuja na dakitari wetu
wa ushauri,
‘Huyu ni
mwanausalama anayeshughulikia hilo tatizo la mdada na kundi hilo la
kijasusi..’akasema dakitari ushauri.
‘Nimeamua
nimtambulishe kwenu ili muweze kumuuliza yote mnayohitajia kumuhusu huyo mdada,
kama anastahiki kuwaambia, maana mimi sina kibali cha kuyaongea hayo, kama
nilivyowaambia sasa hivi hili jambo lipo mikononi mwao …’akasema, na jamaa
akasema
‘Ndugu
zanguni, kama mlivyoambiwa, hili tatizo ni kubwa, na ni la kimataifa..msione
kama mnasumbuliwa…dunia sasa ina mitihani mingi,na hili la ujasusi, sasa hivi
yatambulikana kama ni ugaidi limekuwa na sura nyingi sana, ..’akatulia
‘Nyie
mnafanya kazi za uandishi mnatakiwa muwe makini sana na mnachokiandika na watu
mnaowasiliana nao,…kwani hawa wahalifu wanatumia kila nyanja kupenyeza mambo
yao, wana wataalamu wa kila fani, na wengine mnaweza kujikuta mnatumiwa hata bila
kujitambua…hawa ni wachawi wa kisasa’akasema akitabasamu kidogo
‘Maana
wachawi wanaweza kumtumia mtu ambaye sio mchawi kutimiza malengo yao, wewe
usiku unachukuliwa hujijui, unaenda kuwanga kwa nguvu za kichawi lakini wewe
hujui na sio wewe mchawi…tunaambiwaga hivyo….’akasema
‘Kwahiyo,kwa
hili swala mlilokuwa mkilifuatilia, tafadhali, mliache kabisa…huko mnapokwenda
ni kubaya,…na bahati mbaya ni kuwa hata huyo mdada mwenyewe huenda alikuwa
akitumiwa tu hajui kitu masikini.
‘Sasa bado
tunalifuatilia, na tutahakikisha kuwa wote wanaohusika na kundi hilo,na lingiine
kama lipo tutawakamata wote, tunashirikiana na wenzetu wa ncho jirani…’akasema
‘Unajua sisi
hatuelewi afande, tumehusishwaje na mambo hayo, maana kazi yetu ni uandishi na
uandishi hauna mipaka, kuwa hili ni la hivi au vile, tunachotakiwa ni
kuielimisha jamii, pale linapotokea tukio, kwa mtindo huu hamuoni mtatufunga
pingu huku mnataka tuandike..kinyume nyume,…….’tukasema
‘Ni bora kwa
hivi sasa muelewe hivyo, kwani tupo kwenye mapambano na haya makundi
haramu,….na sisi ndio tunaofahamu ni kwa namna gani inaweza kuleta madhara kama
tutawapa uhuru huo wa kuandika kila kitu.
Nyanja hii
ya uandishi sasa hivi ni silaha kubwa inayotumiwa, na hawa watu, kwa
propaganda, potofu, kuhofisha, kupelekeana taarifa, na vitu kama hivyo, ndio ni
vigumu sana kuisimamia hii fani maana nayo ina sheria zake, lakini inapobidi ni
lazima tuingilie kati..’akasema
‘Kwahiyo kwa
hivi sisi ni bora msielewe zaidi, itawasaidia,…lakini hata hivyo, inabidi
niwaelezee yale yanayostahiki kuwaambia ili muwe na tahadhari,…’akasema
‘Kundi hilo
alilokuwa nalo huyo mdada lilikuwa ni wakala wa kundi la kimataifa la ujasusi,
ni magaidi kwa jina jingine, maana ugaidi ni mpana sana,tofauti na wengi
mnavyofahamu,…’akasema
Kundi hilo liliweka
tawi lake huko kijijini …na wapo sehemu mbali mbali wametawanya ki aina
kutegemeana na fani za jamii…wapo hadi huku , huku mjini nakadhalika, sasa hilo
la huko kijijini alipokuwa huyo mdada ni kundi lililopewa kazi ya kuuza madawa
ya kulevya, vingine vilitumika kama viini macho…
‘Kundi hilo
ili liweze kufanya kazi zao linahitajia pesa, na pesa zao mara nyingi
zinapatikana kwenye biashara haramu kama hizo, au kuiba, kutapeli…sasa kwa
upande wa hilo kundi huko kijijini alipotoka huyu mdada, wao walijitambulisha
kama waigizaji, watengenezaji filamu, na vitu kama hivyo…huku wanauza madawa,
wanaafnya biashara za ngono, wakitengeneza kanda za ngono…ni vitu nyie mtaviona
vya kawaida kwa hivi sasa lakini lengo lao ni pana zaidi huko mbele.
Kizazi
kinazoea….jamii inaharibika..jamii inakuja kujikuta ipo na vijana wasio na
nguvu, legevu, walevi, wamepandikiziwa sumu ya kuchukiana, …..maana madawa hayo
yana namna zake,yanaharibu mwili, ubongo, nguvu, kizazi……hilo hamlioni kwa sasa,
lakini siku zinavyozidi kwenda ni hatari kweli kweli….na hiyo ni mbinu nyingine
ya kumshinda adui…maana sisi wanatuona ni maadui zao kwa vile hatuwaruhusu
kufanya watakavyo, dawa ni kuharibu nguvu kazi…
‘Sasa hao
waliopelekwa huko kijijini walipewa hiyo kazi ya kutafuta pesa, na kuchunguza
mambo mbali mbali yanayoendelea huko kijijini,…mnafahamu kile kijiji kina nini,
ni kwanini wakilenga wao,…mnafahamu?’ akauliza na kwa kweli hatukuwa tunafahamu
chochote, tukasema hatufahamu
‘Kijiji kile
kinasadikiwa kuwa na madini, mali asili nyingi sana zinapatikana eneo hilo….,
serikali inafahamu hilo, ina mikakati yake, lakini hawa watu nao wana mikakati
yao, wanajua ni kwanini wanafanya hivyo, kujiandaa kwa ajili ya kuja kuwekeza hapo….ni
mambo ambayo ukiyaangalia juu juu huwezi kuyatambua athari zake baadaye…ni watu
wanaona mbali miaka mia,ambayo hata wao hawatakuwepo!
‘Hivi
niwaulize kama vijana pale, eneo hilo, …..na sio eneo hilo tu tuzungumzie nchi
kwa ujumla, nguvu kazi ikiathirika hivyo, haina nguvu, wagonjwa, hawana
elimu,..kazi yao ni kubwia madawa, kulewa, kuiga iga mambo ya starehe tu, wawekezaji
wakafika kuwekeza, ni nani atakuja kufanya kazi kwenye hayo makampuni, …..?’
akauliza
‘Ni wao …na
watu wao….’tukasema
‘Eeeh, ndio
hivyo,…maana vijana, watakuwa hakuna, hawana nguvu, hawana elimu, wameathirika,
wagonjwa watakuwa ni wengi,….na ukomo wa maisha yao utakuwa ni mfupi tu,… ni
lazima wao watakuja na nguvu kazi zao au waagize sehemu nyingine, na kwa maana
hiyo wageni watajaa makazini,
….tutamlalamikia nani…’akasema
‘Hili tunatakiwa
kuliangalia kwa mbali zaidi,…leo hii tunataka kuwekeza kwenye ardhi…unajua
kwenye hiyo ardhi kuna nini, hawa wajukuu na vitukuu watakuta nini,…ndio lengo
lao, huo ni mfano mdogo tu….lakini pia mali asili itachukuliwa bila ya kuwepo
msimamizi mwenye uchungu wa nchi, maana hakuna mzawa kwenye usimamizi wao
….hayo nyie hamyaoni kwasasa, sisi watu wa usalama tunayajua hayo, ndio maana tunafanya kazi yetu.
Haya nyie
kalieni starehe, kuandika story za ngono, mapicha ya ngono, wenzenu wanawekeza
kiakili…..baadaye mnakuja kulalamika…tuamuke jamani, mfumo huo umetengenezwa
kiakili, msiponaswa kwenye madawa, kwenye siasa, mtanaswa kwenye vinywaji,..au
kwenye vyakula,…hivi vyakula tunavyoagiza kutoka nje, tujiulize kwanini
hatulimi wenyewe, samaki wapo wengi tu, kwanini…humo humo kwenye makopo ya
vyakula nk wenzenu wamewekeza….sasa nyie kalieni kupiga makofi, kushangilia….’akasema
na sisi tukacheke kidogo.
‘Sasa kwa
hilo,…hapo kijijini, wao wakawa
wanapitisha madawa kwenye makasha ya kanda za video kitaalamu zaidi, huwezi
kujua wanavyopaki, hizo dawa kuna za kuelewesha kuna za kuharibu akili, kuna za
kupandikiza maradhi,….,
Vijana
wanalewa hawajijui, wanashawishiwa kufanya machafu, ….haya ndio wakawa kuendesha
biashara za ngono, na kuigiza video za ngono kisiri siri, maana akili sio zao
tena…hata humu mjini yapo haya, nadanganya, sasa jaribu kutumia nguvu kuzuia
mambo hayo usikie watu wakavyolalamika…utaambiwa haki za binadamu! Hivi kufanya
hivyo hukiuki haki za binadamu, niwaulize nyie…’akasema
‘Haya yote
ni mbinu, …na hatujui,….hakuna kitu kibaya kama kutawaliwa kifikira…elimu yetu
ni ya kuiga iga tu…hata kile tunachokifahamu ni kuiga tu, wazee wetu waliweza
kuwekeza na tungeliweza kuendeleza nguvu zao kitaalamu tungelikuwa
mbali…viwanda hakuna vimekufa, kwanini, ilipangwa iwe hivyo, waje
wawekezaji,….hayo yalifanyoka kitaalamu… , yote hayo kwa manufaa ya hao
majasusi….jamii haijui!
Majasusi
hawa wa kimataifa ni wakatili sana….wanaua bila huruma, na kuua kwao ndio hiyo
wanatumia madawa yasiyoweza kugundulikana, mnajiona mnalewa kumbe mumekunywa sumu….madawa
haya haya ya kutibia wanapandikiza sumu, ni ndogo lakini athari yake baadaye ni
kubwa….ni vitu vinafanyika kitaalamu sana!
Haya huko maofisini
kwenye makampuni hayo waliyowekeza wao wanatumia nguvu zenu kwa mshahara mdogo,
wananeemeka wao, wakijua ukomo wa maisha yenu ni mdogo, ukichoka unatafutiwa
mbinu unafukuzwa, wanaweka watu wao….huko siwezi kuenda zaidi, ila
…..nawaombeni muamuke, badilisheni mfumo wenu wa maisha, tujitegemee!
‘Hili
nawaambia nyie waandishi ili muwe
makini, saidieni jamii kuwaelimisha,
andikeni yenye tija, msiwe bendera tu kufuata upepo. Kila kitu cha nje mnaona
ndicho bora, yaani hata utamaduni, hata kula….hahaha…’akatikisa kichwa
Na kwa hili tukio la huyu mdada...mkijifanya
mnajua mkaanza kulifuatilia mjue mnaingia kwenye mdomo wa mamba, hayo waachieni
wataalamu wanaijua hiyo kazi…maana mtaingia kwenye anga za hao watu wasio na
ubinadamu…na zaidi mtaishia kueneza uchafu wao bila hata nyie kutambua….
‘Kama nyie
mnaandika stori za ngono, stori za kutumia madawa ya kuelevya kama vile ni
jambo la kawaida, mjue nyie mumeshakuwa wakala wao…mnaharibu jamii…mnakiua
kizazi kinachochipukia, na ndio lengo lao…kwahiyo mnatumiwa hata nyie wenyewe
kujijua..na wasomaji wa mambo hayo ni wengi,na wengi wao ni vijana…..
Vijana hivi
sasa wanaathirika kisaikolojia bila kujijua….badala ya kusoma vitu vya
kuelimisha vyenye tija,wakazalisha wakaleta maendeleo jamii ikaishi kwa
maelewano na amani, wao, wanaishia
kusoma vitu vya kuwaharibu kiakili, hii mitandao ni moja ya nyenzo zao, yapo
mazuri, lakini humo humo wameshaweka mambo yao,…muwe makini jamani…hiki
mnachokifanya mtakuja kuulizwa na muumba…’akasema
‘Lakini sisi lengo letu ilikuwa kuja kumuokoa
mdada…’tukajitetea
‘Kumuokoa
mdada!!!,….hahaha…nyie mnaweza kumuokoa mdada?….mnatania’akasema akitukazia
macho yenye mshangao huku akicheka kidogo
‘Kwa vipi
hebu niambieni….?’ akauliza
‘Sasa sisi
tungelifanya nini…?’ tukamuuliza
‘Huyo
msingeliweza kuja kumuokoa hamngeliweza, ….na hamuwezi…, kabisa msingeliweza
hilo nawaambia….’akasema
‘Una maana
gani kusema hivyo,kwani imekuwaje kwa mdada, samahani kwa hilo swali maana
tutaondoka bado tukiwa na maswali mengi , je imekuwaje kwake, maana sisi
hatukupoteza muda kufika hapa….?’ Tukauliza
‘Kwanza
jiulizeni hiyo barua pepe ilifika lini kwenu, hiyo ya kutoka kwa mdada…na leo
ni siku ya ngapi..sasa mnaokoa nini hapo..’akasema
‘Kwanini
unasema hivyo…maana sisi tuliipata hiyo barua pepe jana usiku…na asubuhi na
mapema, tukawahi kuja ili tuweze kuona kama tunaweza, kumuokoa…’tukasema
‘Tukio la
huyo mdada limetokea lini, ni wiki ya tatu sasa….au sio docta, …wiki ya tatu,
leo mnakuja kumuokoa mdada, hahaha…ili sasa muone wenzenu walivyo mbele
yenu,…’akasema na sisi tukabakia kuangaliana
‘Ina
maana….’tukataka kujiuliza
‘Mumechelewa
sana…., ndio maana nasema hamungeliweza kuja kumuokoa…mpaka lengo lao litimie,
huenda kweli mdada aliwaandikia akijua mtaweza kufanya hivyo, kwasababu hajui ,
na kama mungekutana naye leo, mkasema mumekuja kumuokoa ataona nyie ni wahuni
tu,… wenzenu wapo mbele yenu kwa kila jambo…’akasema
‘Lakini hiyo
barua pepe yaonyesha kabisa imetumwa muda huo na kufika kwetu muda
huo….tuliichunguza kabla hatujafika hapa sisi tuna utaalamu huo…’tukasema
‘Ndio maana
tunawaambia sisi watu wa usalama tunajua ni nini tunachokifanya,… mtaona
tunawaingilia kwenye kazi zenu lakini ni lazima tufanye hivyo,kwa masilahi ya
jamii, kwa masilahi ya vizazi vijavyo, hata kama leo mtatuona wabaya…’akasema
‘Oh, hii
ajabu kabisa….haiwezekani, kwahiyo afande unataka kusema nini, ina maana mdada
hakuweza, au imekuwaje kwa mdada….yupo wapi….?’ Tukajikuta tunauliza kile
ambacho tumeambiwa tusifuatilie. Afande alituangalia kwa makini halafu akasimama
na kutoa simu, akapiga namba halafu akasema;
‘Mleteni….’
WAZO LA LEO: Jamii zetu zinaharibiwa kwa mengi, ipo mitihani ya
kawaida na ipo mitihani ya ya kupangwa na watu kwa masilahi yao na hayo
yamepangwa kwa mbinu za hali ya juu kweli, inahitaji tafakuri la ziada….kuna umamboleo
unaoathiri tamaduni na fikira za watu nk…..nia ni, ili kuwanufaisha wenye tamaa
zao, watajirikie na wazidi kutawa! kwa kutumia
misemo kama ile ya ‘walionacho waendelee kuwa nacho, na wasio kuwa nacho wazidi
kukosa…’. Hayo yapo na yanendelea, tusipokuwa makini, tutaishia kusindikiza na
kuwapiga makofi wenzetu huku wakiendelea kuneemeka, na huku wengine wanasafiri
kwenda mwezini. Tuamuke, …
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment