Baada ya kumaliza
mazungmzo yangu na huyo mwenyeji wangu ambayo yalianza baada ya ubishi wangu
nikitaka kusikia nini Yule jamaa wa kijijini alitaka kusema, na hasa alipotamka
kuwa ni jambo linalomuhusu aliyekuwa mchumba wangu. Lakini hata hivyo mwenyeji
wangu alikataa kata kata na kuanza kutunga story nyingine za kunidanganya, ….
Nakiri kuwa
maongezi yangu na huyu mshauri, yalinipa faraja kubwa…na niliweza kukaa na
kuwazia kuishi maisha hayo ya matumaini…..lakini dhamira ilinikaa sana moyoni….labda
ni kutokana na tabia yangu, nikiamua jambo langu siambiliki,….na kwahiyo
nilichokuja kukifanya baadaye , msione ajabu!
***********
Katika
mazungumo yangu na Mwenyeji wangu yaliyochukua muda mwingi wa kumsikiliza yeye
zaidi, kuninasihi…yeye akitumia ujuzi wake wote wa ushauri nasaha, siwezi
kuyaandika yote aliyoniambia,…ila nakiri kuwa wakati mwingi alipokuwa akiongea
nilikuwa kama simsikilizi, akili yangu ilikuwa ikitekwa na dhamira yangu
Dhamira…..ni
lazima nitende nilichokusudia , hilo ndilo suluhisho…..
Mwishowe mshauri
huyu, pale alipohakikisha kuwa nimeiva akaona sasa aseme ukweli, na hapo
alianza kwa kuniuliza kama nipo tayari kuyapokea majibu ya vipimo vyangu;
‘Mimi nipo
tayari….nimeshajiandaa tokea jana, nipo tayari kuyapokea hayo majibu ya vipimo
vyangu, na kwa hali halisi,…na uhalisia, nilishayajua matokeo hayo yapoje kabla,
na zaidi nilishaoteshwa, na nina uhakika ndoto yangu haijakosea…’nikasema na
yeye akaniangalia kwa macho ya mshangao, lakini hakutaka kunidadisi zaidi
kuhusu hiyo ndoto, akaendelea kusema;
‘Sawa unajua
nikuambie kitu, sisi tunapotaka kutoa matokea ya vipimo kama hivi, hatuangalii
kuwa mtu huyu kaathirika au la,….nia kwanza ni kuelimishana, uwe na tatizo hilo
au la, kama nilivyokuambia awali,..kwani kama ulivyosikia maelezo yangu ya
awali ilikuwa kukujenga kukulinda na kuja kukusaidia, …uwe au usiwe na tatizo
hilo….’akasema
‘Na kwa
vyovyote vile, matokea hayana maana
yoyote, chenye maana kwa yoyote Yule ni juhudi zake binafasi za kujisaidia kwa
kula vyema,..kujilinda na maradhi, hasa maradhi ambukizi…., na ukumbuke wewe ni
mpiganaji wa kuendeleza kizazi chako, ukishindwa leo, ina maana kizazi chako
kimepotea, je upo tayari kukipoteza kizazi chako…?’ akaniuliza
‘Mungu
mwenyewe ndiye anajua jibu la hilo swali lako…’nikasema
‘Mungu
kakupa utashi wa kuamua hatima ya maisha yako,…ndio maana mpaka leo unapumua,
kakupa utashi wa kuamua uishije ndio maana leo unaishi hivi kesho vile,
..kwahiyo kujua kwa mungu utaishije ni wewe mwenyewe kwanza ulivyojielekeza…na
ndio maana kila mtu anatakiwa kuweka dhamira kuwa ataishije kwa vitendo na
dhamira ya kweli,…ama kufa hayo ni mamlaka yake mola huwezi kuzuia….’akasema
‘Mimi nipo
tayari, nilishasema awali,usiwe na shaka na hilo, maamuzi yanguniliyodhamiria hayatarudi nyuma…usiwe na shaka kabisa.’nikasema
‘Haya mimi
nakutolea majibu yako ambayo kama nilivyokuambia yanahitajia juhudi
zako,yanahitajia utashi wako, tukishirikiana mimi na wewe utaishi vyema
kabisa,…maana sasa umeshajifahamu mwenyewe ulivyo…’akasema
‘Sawa nambie
usizidi kunichelewesha nipo tayari…’nikasema
‘Ni kweli
kuwa katika vipimo vyako kuna viini hivyo vinavyoharibu kinga za mwili za
kupambana na maradhi, lakini pia wamegundua kuwa mwili wako una nguvu ya kuweza
kupambana navyo, kama utafuata ushauri utakaopewa wa lishe bora, na mengineyo
kutokakwa mtaalamu yaani walikuwa na maana mimi….’akasema
‘Kwahiyo kwa
kifupi mimi nimeathirika…au sio?’ nikauliza nikitaka uhakika zaidi
‘Wewe una
matatizo ya upungufu wa kinga mwilini, hujafikia kile kiwango cha kusema
umeathirika,…naomba unielewe hapo kidogo kuna namna ilivyo kwenye tatizo hili,
madaraja, hatua…….’akasema
‘Swali langu
hujanijibu, nimeathirika au sijaathirika, ninao au sina huo ugonjwa…?’
nikauliza na yeye akaniangalia kwa makini halafu akasema
‘Ndio unao..unalo
hilo tatizo, lakini…sio kwa kiwango hicho….unaweza ukapona…ukifuata masharti na
ukiishi kwa matumaini, zaidi ya hata Yule asiyekuwa na tatizo hili…’akasema
‘Hamna haja
ya kukwepesha ukweli…haina haja, ya kuogopa kuniambia ukweli, nilishakuelewa, ..’Nikasema.
‘Mimi
nilishayajua hayo mapema, ila swali langu jingine nataka uniambie wazi bila
kunificha,je hilo tatizo jingine ninalo….?’ Nikauliza
‘Tatizo
jingine lipi hilo tena..!!..Mmh, ni hilo
la kupungukiwa damu, mara kwa mara, unajua hujanielewa, haya matatizo mengine
yanatokea kwasababu ya huo upungufu wa kinga mwilini, kinga zikipungua mwilini
,kila ugonjwa utakushambulia,..kwahiyo hilo tatizo jingine lipo, lakini ni
kutokana na…’kabla hajamalizia nikasema
‘Mtaalamu wa
nasaha, mimi nimeshakuelewa, ninachotaka ni uhakika…nimekuuliza hivyo nikiwa na
maana yangu, je hili tatizo lipo au halipo, unatakiwa unijibu ndio au hapana, …samahani
kama ninakosea, ama kwa maelezo umeshaniambia si ndio hivyo…utakuwa unarudia
rudia tu,mimi nimeshasema nipo tayari…usijali’nikasema
‘Ndio hilo
tatizo jingine pia limeonekana, lakini kwa hivi sasa hatuwezi kuwa na uhakika
mpaka ukijifungua, kama alivyosema dakitari bingwa wa mambo hayo, amesema
ukijifungua itakuwa ni nafasi nzuri ya kulijua vyema, na kupamabana nalo na mengine
kama yatakuwepo, mara nyingi tatizo kama hilo kwa mama linaweza likatokea na mara mama
akijifungua linakwisha, na likabakia kwa mtoto…’akasema na nilijua anayasema
hayo kwa kunitia moyo.
‘Sawa
nimekuelewa docta mshauri, nafahamu hayo ni kunipa matumaini, au sio…kuishi kwa
matumaini au sio….nimekuelewa….’nikasema na yeye akanitupia jicho la mashaka,
halafu akasema
‘Kinachotakiwa
kwanza ujifungue, ..na kujifungua huko kutafaywa kwa upasuaji, natumai hilo
umeshaambiwa, haiwezekani kusubiria muda wa kujifungua kwa njia ya kawaida…sawa?’
akasema
‘Sawa,…’nikasema
‘Sasa ukashajifungua
itakuwa ni kazi rahisi ya kupambana na tatizo hilo, madakitari wote bingwa
wamesema wataweza kushirikiana kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kupambana na hayo
matatizo na wanasema hakuna shaka utafanikiwa…utapona, utakuwa kwenye hali
nzuri tu. Usiwe na shaka na tatizo hilo wewe upo kwenye nafasi nzuri ya kupona…utakuja
kutuambia,….walifika watu wana hali mbaya zaidi yako…lakini sasa hivi wapo
kwenye shughuli zako….’akasema
‘Sawa najua hayo
ulishaniambia…najua ni kunipa matumaini au sio…sawa tumuachie mungu..’nikasema
kwa sauti ya upole
‘Hebu
fikiria kwanza, madakitari wote mabingwa wa matatizo hayo, wameamua kujitolea
kuhakikisha wanalimaiza tatizo hilo kwako na kwa mtoto, …uone jinsi gani ulivyo
na bahati, mungu kawaelekeza watu hao watumie ujuzi wao wote kwako, ujuzi walijaliwa
na mola wao, nina uhakika mola wako hatakutupa,…’akasema
‘Na iwe
hivyo docta…’nikasema
‘Mimi nina
imani kuwa mungu kakupa mitihani hii, ili wewe uwe njia ya kuja kusaidi wengine,
uwe ushuhuda kwa wengine, sasa usije kuacha jukumu hilo, utakuwa umewasaliti
wale wote wanaokutegemea, pambana kwa kujipa moyo, utashinda…’akazidi kuongea
‘Sawa na iwe
hivyo…’nikasema
‘Muhimu na
la kushukuru ni kuwa hilo tatizo jingine linaponyeka, kama lilivyo tatizo hili
la upungufu wa kinga mwilini. Mwanzoni uliona watu wengi walipoteza maisha kwa
hali mbaya kabisa…kwasababu watu waliangalia ponyo la gonjwa hilo zaidi….badala
ya kinga, kitu ambacho hakikuwa sahihi, ilitakiwa kuangalia kinga, na kinga ni
masharti yake…kama nilivyokuambia.
Hapo
nikatikisa kichwa kukubali…
‘Ujue sote
tuna madhaifu ya kinga, kutegemeana na utofauti wa mwili, kutegemeana na tabia
za kuishi, lishe tunayokula…na hii ndio inaleta utofauti, kinachofanyika kwa
hivi mtu akionekana kaathirika ni kufuata masharti , hasa ya kula….mazoezi nk….kama
nilivyosema awali, na jingine ni kupambana na vile vitu vyenye kuleta maradhi
ambukizi,, na hilo ni kwa kila mtu, uwe umeathirika au la…na siku zinavyozidi
kwenda kinga nayo inaongezeka…’akatulia
‘Nimekuelewa….’nikasema
‘Kwahiyo
nakuomba sana, na muhimu kufuata masharti, sasa hivi kuna viini lishe, kuna
dawa mbadala zamiti shamba, …vyote hivi vimefanikiwa kupambana na maradhi hayo
na mafanikio yake ni makubwa…katika maisha ya yoyote Yule uwe unaumwa au
huumwi, ni kuishi kwa matumaini, kuwa
utaishi maisha marefu au sio…’akasema
‘Sawa kabisa…nashukuru
mtaalamu nasaha…’nikasema na yeye akaniangalia kwa makini, halafu akasema
‘MIMI
nimemaliza kama una maswali mengine naomba uniulize…’akasema na mimi nikakaaa
kimia kwa muda, nikizama kwenye mawazo …
‘Kwa ujumla
kutokana na nasaha zake, alishaniweka njia panda…nilianza kuyeyuka na kutaka
kulisahau dhamira yangu, lakini sikutaka kusema lolote zaidi kwa muda huo,
nikabakiwa na maswali yangu kichwani;…
Ndio labda watafanikiwa
nikazaa salama,…je maisha ya kawaida huko mbele yatakuwaje, je wataweza
kunisaidia maisha yangu yote maana matatizo hayo ni ya kudumu,…nikajijibu kwa
kusema sio rahisi, nikitoka hapa ni mimi na shida zangu.
Pili
nitaishije, sina kazi, sina mtu wa kumtegemea, je watu hawa wapo tayari
kuniapatia ajira, sizani na zaidi wanaweza kunifanya yaya wa nyumbani na mimi
inavyoonekana nina damu ya kunguni, nitaishia kusakamwa zaidi…sitaki tena
kunyanyaswa sasa nitaishije,…nitapata wapi pesa za kujikimu, na kumlea mwanangu…hakuna
jinsi, dunia hii sio yangu tena
Nilijua kuwa
kwa vyovyote iwavyo, mwisho wa siku watasema nitarudi kwa wazazi wangu, wazazi
ambao hawana mbele wala nyuma, wazazi ambao walishawekeza maisha yao kwangu, wakijua
mimi nitasoma , nitakuja kuwasadia, sasa kipo wapi, nitakuwa mzigo kwao, na
majonzi ya kila siku….hapana sitaki kuja kuwa mzigo kwa yoyote yule
Niliyawazia
hayo na mengine mengi, na mwishowe nikamuwazia mtoto ambaye kama angelizaliwa,
najua atakuwa wa kuumwa umwa tu…, kutokana na matatizo hayo ya pili, huenda hatafikisha
hata miaka miwili hili ni kutokana na maelezo ya wengi niliowaulizia, mtoto
kama huyo atakuwa akiumwa na kuandamwa na upungufu wa damu..hilo ni tatizo,
nitaishije kwenye hiyo hali, mtoto ataishije….dhamira ikaanza kuniteka akili
Sasa kwa
hali hiyo ni nani atamuweza, kama mimi nitatangulia, …itakuwa ni shida, atanyanyaswa,
atasimangwa na miaka yake hiyo mwili ya uhai itakuwa ni adha kwa watu….dhamira
ikaanza kuniingia akilini….
Kesho,itasema…kesho….kesho…
Hiyo...kesho
kila mtu atajua….
Kwahiyo hiyo
kesho nawaomba nyie watu msishangae, nitakachoamua….
Nilipobakia
peke yangu nilichukua mkoba wangu wa kike, humo nilikitafuta kile
nilichokitaka, BAHASHA NDOGO,..ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na tiketi yangu,
tiketi ya kutimiza dhamira yangu….nikaiona na moyo mwili ukanisisimuka,…oh,
sasa kesho itasema…
Niliifungua
ile bahasha…lakini nikahisi tofauti, sijawahi kuifungua hii bahasha tangia
nilipopewa, na nakumbuka ilifingwa vyema, sasa mbona ipo kama ilifunguliwa…labda
kwa vile ilikaa muda bila kufunguliwa, lakini nilichokitaka nilikiona,…vipo
sawa sawa, na hapo nikakumbuka ile sauti siku ile..
‘Hii ndio kinga yenu, kama ukishikwa
na polisi wakakutesa ili utaje siri la hili kundi, ili ututaje sisi kamwe usije
kugeuka nyuma ukafanya hivyo ukatusaliti…
Ukitusaliti, sisi tutakuandama wewe
na familia yako…tutaingamiza familia yako..kama huwapendi baba na mama yako
ufanye hivyo, utusaliti…
Sasa ili usipate taabu, kuliko kutoa siri ni bora ufe..,
hiki ni kiapo,..na ujue kundi hili lina nguvu, kuna viona mbali, kuna watu
wanatuona hadi sasa hivi kuwa tunafanya nini….sasa ili usije kuumia,
kuzalilika, wewe unachukua hiki kidonge kimoja tu, unakitia chini ya ulimi,
kikiyeyuka na wewe umeshayeyuka,….hutasumbuliwa tena, na hawatakuona tena….’
Nilipumua
kwa nguvu….nikasema moyoni, sasa muda umefika…sitaki kusumbuliwa tena..
***********
Kama
nilivyowaambia awali kundi hilo kwa pale kijijini lilijulikana kama kundi la
kuigiza, na wanakijiji wengi walikuwa wakilisifia, kwa jinsi walivyoweza
kuigiza kwenye majukwaa na zaidi pale tulipoweza kutoa kanda za video, lakini
miongoni mwao, wateule, walikuwa wakifanya zaidi ya hayo, kuna mengina hata
mimi nilikuwa siyajui.
Mimi
nilikuja kuingizwa kwenye baadhi ya mambo baada ya kugundua kanda za video
kwenye kabati la mchumba wangu…..ndio yeye akaniambia hicho nilichogundua ni siri
ambayo alisema natakiwa kuitunnza, nikiitoa sio tu nitaangamiza kundi, lakini
hata mimi nitakuwa hatarani n familia yangu , baba na mama wataangamizwa..na
mimi niliwapenda sana wazazi wangu licha ya yote yaliyotokea sikuwa tayari
wazazi wangu wapate shida, wateswe au kuuwawa kwasababu yangu…kwahiyo hilo
nikaliweka kuwa siri
‘Na
nikuambie kitu, wewe uliwahi kushirikishwa bila kujijua,..unakumbuka siku ile
ulipopoteza fahamu…ukila chakula, unafikiri ilikuwa nini, na ilitokea mara
zaidi ya nne, na zote hizo ulishiriki na watu tofauti..na tulipata faida kubwa
hukujua kilichoendelea…’akaniambia
‘Ina maana
nyie mlinifanyia nini…’nilikasirika sana siku hiyo , lakini mpenzi alijua namna
ya kunipooza, siku hiyo nilipewa pesa nyingi sana na zawadi nipeleke nyumbani…
‘Usiogope
mpenzi, haya ndio maisha…usione watu wametajirika, watu wana magari, wanajenga
mgorofa, ukazani ni mambo ya kihalali tu,..hapana kuna mambo mabaya
yanafanyika, kukwepa kodi, wengine wanaua watoto wao, wengine wanafanya vitu
kama hivi ambavyo kwa jamii ni vibaya lakini vina pesa nyingi ,…sisi hatu-ui
watu, ila tunafanya biashara hii, unaona tofauti yake, ila mtu akituingilia,
hatusiti kum-maliza…’akasema akipitisha kidole kooni halafu akainua moja ya
kanda ya video.
‘Sasa hivi
wewe ni malikia wa hapa kijijini, unaona unavyosifika, wewe ni muigizaji
mashuhuri, yote hiyo ni kwasababu ya haya, kuna gharama zahitajika, kufanikisha
haya yote, na hizo tunapata kwa kuuza
hizo kanda…hizo za hapa kijijini ni pesa ndogo tu, …pesa nyingi tunapata kwa
njia hii…’akaonyesha hiyo kanda hewani, nilichokiona pale mbele ya ganda lake
nilifunika macho.
‘Hahaha
unafunika macho….wakati wewe mwenyewe upo humu..’akasema
‘Eti
nini…’nikataka kuangalia akazuia…na kusema
‘Sasa
kuanzia leo wewe ni mwanachama halali….ungeliendelea kuwa mwanachama usiyejua
kinachoendelea, lakini kwa kimbelembele chako cha kuchunguza chunguza vitu
vyangu, sasa wewe ni mwanachama hai, na ole wako uje kulisema hili, wazazi wako
hutawaona tena, au watakuwa wakiteseka mpaka waombe kufa….’akaniambia sasa kwa
sauti ya vitisho.
Kweli
sikujua,…sikujua kuwa uchafu huo na sifa hizo ndizo zilizonipandisha kwenye
kilele cha ujeuri, …nikawa siwasikii wazazi wangu, sifa zilizonilemaa, nikawa
namsikiliza mchumba wangu tu,…oh…
Nilipofikia
kuyawaza hayo, niliinama na kuanza kulia….nilitubu dhambi zangu…nikamlilia mola
wangu, nikamuomba anisamehe……nikaomba kuwa hayo nilitenda kwa vile sikupenda
kabisa wazazi wangu waje kuteseka…nililia kwa muda halafu nikatulia
‘Hata
nikilia nitamlilia nani kwa hivi sasa, ..’nikajiuliza
‘Oh nakulilia
wewe mola wangu , wewe ndiye unaiona roho na nafasi yangu, je kweli niliyafanya
haya kwa utashi wangu….hapana sikujua kuwa walinifanyia ujanja, na kuniingiza
kwenye mambo machafu bila kufahamu na nilipofahamu waliniweka kwenye vitisho
ndio maana ilikuwa ni siri… mola wangu nisamahe…
‘Najua …...yote
sasa sio siri tena yameshajulikana, najua yote sasa itabakia ni historia …lakini
sitaki mtu aje kuninyoshea kidole tena kuwa ndiye huyu alifanya uchafu
huo….sitaki kiumbe hiki kije kunyoshewa kidole na kuambiwa mama yako ndiye
alifanya hivyo, sitaki yeye aje kuwa tunda la uchafu huo….hapana..hapana.. ama
kwa wazazi wangu najua sasa wanaweza kulindwa….sijui…mungu atawalinda.’nikasema
nikishika tumbo langu
‘Nilichokitaka
nimekipata, …japokuwa sikupenda iwe hivi…sikutaka , na sikujua ni kwa njia
hiyo, na sasa nimevikwa hii nishani,…..hapo nikakumbuka moja ya picha
niliyowahi kuigiza huko kijijini, nikiwa
kama muigizaji mkuu….niliipenda sana hiyo video ndiyo iliyonipandisha chati na
kuwa kama mrembo wa kijiji
Nakumbuka
walikuwa wakiniita, malikia wa kijijini , ni kutokana na kazi hiyo, kwenye kazi
hiyo niliigiza kama binti wa mkulima mmoja masikini, nikiwa shambani akapita
mwana mfalme akiwinda akaniona na kwa uzuri wangu akanipenda, na haraka
akamwambia baba yake kuwa hatimaye kampata mke, na ikatumwa watu kuja kwetu.
Watu hawa
walituma madaraka yao na pesa, hawakutambua kuwa mimi name nilikuwa na utashi
wangu, mimi nilikuwa na mchumba wangu,
niliyempenda sana kijana wa jirani yetu tuliyekulia naye..
Alikuja
mwana wa mfalme akataka kumposa yeye, lakini mimi sikumtaka, sikutaka ufahari
wa kuitwa malikia, kwani kulikuwa na mtu aliyekuwa mfalme wa moyo wangu,…lakini mfalme , kiongozi wa
utawala alikuwa na mamlaka, hakujali kitu alitaka kukidhi matakwa ya mwanae,
kwani ni nani atakataa kuolewa na mwana wa mfalme, aje kuwa malkia baadaye….lakini
mimi nilikataa
‘Niliigiza
vizuri sana, na ni moja ya kazi zangu iliyonipatia umaarufu pale
kijijii,…nakumbuka humo, ili kuonyesha dhamira yangu ya kweli kuwa sitaki
kuolewa na mwana wa mfalme tulipanga nibebe mimba ya huyo kijana… hapo kuna
kipindi kilipita cha malumbano, kuandamwa na mchumba wangu akisakamwa kwa hili
na lile, na wazazi nao wakishurutushwa.
Na katika
sehemu hizo ndipo nilionyesha ujuzi wangu wa hali ya juu, ni kipande hicho
ndicho kilinifanya niitwe malikia wa mapenzi….hahaha, kumbe ni ulimbukeni!
Ni kwel
mimba ikatunga, na siku ilipofikia kuwa natakiwa kwenda kufunga harusi na mtoto
wa mfalme nikamwambia huyo mtoto wa mfalme kuwa nina mimba ya mchumba wangu wa
zamani,…kijana Yule wa mfalme, akapandwa na hasira akamwendea baba yake, …na wakajadili
kuwa huyo mpenzi wangu auwawe..na hiyo mimba itolewe….
‘Kama
mkimuuamchumba wangu basi na wewe utaoa
maiti yangu…’nikamwambia na yeye hakunielewa, akasema nitalindwa na nitaolewa na
yeye nipende nisipende, na yeye ana uhakika huyo mchumba wangu akifa,
nitamsahau na mimi ipo nitajirudi kwa kuwa nitakuja kuwa malikia wa nchi hiyo..
Na kweli
mchumba wangu akachukuliwa kwenda kuuwawa…..na mimi huku nyuma nikatafuta sumu
ya kujiua….
Ni wakati
nawazo hayo ndio nikashituliwa na sauti ikisema ;
‘Wanasema
inabidi ufanyie upasuaji…’sauti ilinishtua, na kujitoa kwenye lile dimbwi la
mawazo, alikuwa sio mwingine ila Yule
mwenyeji wangu alikuwa kafika kunipa habari hiyo…
‘Watakavyoamua
kwangu yote ni sawa…ila nahitajia siku mbili za kujiandaa..’nikasema
‘Siku mbili
…kwanini siku mbili…kesho wanaona ndio siku muafaka,…na mimi nimewaambia sawa,
leo watakuwekea damu, na kesho upasuaji huo utafanyika, …hiyo ni kwa manufaa
yako na mtoto..’akazidi kusema
‘Kesho……sawa
kesho…’nikasema kama vile mtu yupo ndani ya ndoto
‘Ndio kesho,
ila wanachotaka ni wewe kutuliza kichwa ili kukwepa shinikizo la moyo…’akasema
‘Sina
shinikizo la moyo, nipo tayari kwa lolote lile..’nikasema na menyeji wangu
akaniangalia kwa macho yenye udadisi…halafu akasema
‘Nikuambie
kitu kuna wengi walikuwa kama wewe, na walifikia hata kutaka kujiua, lakini
baadaye waliamua, wakatuliza kichwa wakajitambua,..sasa wanaishi na watoto
wao..kwa matumaini…ni lazima na wewe ufanye hivyo..’akasema na nilishtuka
alipotamka neno kujiua..
‘Ni kweli,
lakini sizani kama walikuwa na tatizo kama hili langu, tatizo la kusubiria
miaka miwili, ukiombea miaka miwili ipite ndio uwe na uhakika wa maisha, na
utakuwa kila muda unaishi kwa kuongezewa damu, tatizo juu ya tatizo,…sizani
kama kati yao kulikuwa na mmoja, mwenye tatizo kama mimi….’nikasema
‘Walikuwepo
wenye matatizo mabaya zaidi ya hilo..lakini matatizo kama hayo yanatokea
kwasababu ya upungufu wa kinga kama nilivyokuambia, lakini dawa za kuongeza
nguvu za kinga hizo husaidia kupambana na hilo tatizo, na jingine kubwa ni
kutliza akili, ukalikabili lile tatizo kwa moyo mmoja,….’akasema
‘Nilimekuelewa…..’nikasema
nikihema.
‘Lakini
mbona ghafla umebadilika, sio hali ile uliyokuwa nayo mchana..’akasema
‘Hapana
usijali mimi nipo sawa,ni kuchoka tu…’nikasema na mara nikamuona akiangalia ule
mkoba wangu wa kike,nikajiuliza kwanini anauangalia, sikuwa na zaidi cha
kufikiria, labda ni kwa vile kauona upo karibu name.
‘Kwanini
unaweka mikoba kitandani, kuna kitu unakitafuta nikusaidie…?’ akauliza
‘Hapana..kuna
kitu nilikuwa nakitafuta, hamna shida,..nitauweka, usiwe na shaka…’nikasema na
yeye akaondoka akionyesha wasiwasi...
Na mimi
moyoni nikasema kesho itakuwa siku nyingine,..kesho watamkuta Yule mrembo wa
runinga aliyetakiwa kuolewa na mwana wa mfalme…na walipomuua, mpenzi wake, na
yeye akajiua, …na harusi ya mrembo na mwana wa masikini ikaja kufanyika
ahera..nilikumbuka hiyo picha huku michirizi ya machozi ikishuka shavuni
*******
Siku kabla
ya kufanyiwa upasuaji, ndipo niliazima simu yenye mtandao, nikakesha nikiandika
yote haya niliyowatumia, niliandika kwa kifupi kifupi, lakini nafaham mwandisha
atajua jinsi ya kuependesha…nilifanya hivyo kabla ya kutimiza dhamira yangu…,
nilichukua muda wa kulitafakari hilo na hatimaye niliona hakuna jinsi, ni
lazima nichague maoja kati ya mawili;
‘Nitimize
matakwa ya dhamira yangu …ili niweze kupumzika..na taabu hizi za dunia
‘Au niishi
kwa matumaini...huku nikiteseka na kudhalilika…’
Mpaka muda huo naanza kuandika haya ….nilikuwa
sijafikia muafaka….dhamira ilinisuta na nafsi ya matumaini ikawa inaniteka moyo
wangu…
Niliandika
nikijua mchumba wangu atakuja kuyasoma …..sikuwa na ufahamu zaidi ya kujua
anaumwa, lakini sikumuweka kwenye kundi la kufa..huwezi kumdhania mwenzako kufa
hata kama unamchukia.
Ila kule kunong’onezana
mshauri nasaha na jamaa wa huko kijijini kulinifanya nifikirie vinginevyo na
nilipowauliza ndio wakatafuta stori nyingine ya uwongo , nilijua ni ya uwongo..
Huyu mshauri
nasaha aliniambia eti, huyo mchumba wangu amekubali kujiunga na kundi la matumaini
na sasa anaendelea vyema, na mimi ni bora nitulie hata kama itaonekana nina
matatizo basi nijiunga na kundi hili nikiwa nimeshajifungua ili niweze
kuwaelimisha watu
Mimi
niliwajibu; ‘Sizani kama ni kweli…, na kama ni kweli mimi sihitaji kukutana
naye…na sizani kama anaweza kukutana nami tena….’nilisema hayo nikiwa sijali
lolote hata kama amekufa kwangu mimi haikuwa na maana tena.
‘Kwanini
unasema hivyo!..., huwezi jua mnaweza mkalewana vyema tena, mkaishi pamoja….’akasema
‘Sijui…’mimi
nikasema
‘Haya wewe
tuliza kichwa chako wala usiyawazie hayo, hata mimi nimeona hayana umuhimu kwako, muhimu
kwako ni wewe tu kujiandaa….’akasema na huyo jamaa kutoka kijijini akasema;
‘Ndio hivyo,
nilitaka kumwambia, ila sikupenda muonane mpaka wewe mwenyewe uridhie…akukute
ukiwa umeshabadilika na kuwa mtu mwingine moyo umuume….’akasema
Niliona
nisiendelee kuwang’anga’ania, kwani niliiona story hiyo kama ni ya uwongo, kwa
muda ule niliiona kama ni story ya
kutunga tu ili kunifanya nisiwaze zaidi, nikakubali yaishe.
Nilikubali
yaishe, japokuwa nilikuwa sijaelewa ni nini kimempata huyo aliyekuwa mpenzi
wangu, japo nilimuuliza huyu niliyekuwa nikiwasiliana naye kwenye mtandao,
lakini yeye anasema hajawahi kumuona huyo mchumba wangu ,
‘Sina habari
zaidi za kwake,…kwa mara ya mwisho nilisikia mke kamkimbia na yeye hali ni
mbaya, .. ngoja nifuatilie…’akaandikiwa hivyo na baadaye akapokea ujumbe
ukisema.
‘Huenda
keshafariki….ila haijathibitishwa…wanafamilia hawajaweka wazi sijui kwanini….’aliandika
maneno hayo baadaye na mimi moyoni nikasema
‘Kama
keshafariki ni heri tu, tutakutana huko mbele ya mola huko atakwenda kujibu mashitaka
…’ sikuwa na mshituko wowote….nikawa najiandaa kutimiza dhamira yangu.
*****
Kabla sijaamua
lipi nifanye kwanza, nilifumba macho na kuanza kumuomba mola wangu…. Aniongoze njia
nichukue uamuzi ulio sahihi, Na nilipomaliza kuomba nikaanza kuyaandika haya ya
mwishoni lakini kwa muda huo kidole kilishachoka kuandika, mnisamehe;
Nawaomba
nyote mnisamehe..hasa wazazi wangu, kwani wao ndio niliowakosea sana, sikuweza
kuwasikia, nawaomba wanielewe,ili nisiishie kwenye moto mkali wa jahanamu….lakini
wazazi wangu waelewe kuwa dunia ya sasa imemejaa mitihani ya shinikizo la
utandawazi, vishawishi sasa vipo vingi sana sio sawa na zama zao, nilipoingizwa
kwenye huo ushawishi, sikuwa na ufahamu zadi, nilijua ndivyo ilivyo, kama
walivyofanikiwa wengine…sikuelewa..
Nawashangaa
sana hawa washawishi kwani siri waliyosema tuifiche,mimi nilijitahidi sana
kufanya hivyo, hata maelezo yangu ya awali hakuna sehemu niliyowahi kuielezea
wote ni mashahidi zangu.. wao ndio wa
kwanza kuifichua….!
‘Unajua mimi
toka udogoni nilipendelea sana kuangalia kanda za video, na nilipowaona waigizaji
wazuri, warembo,wameinukia na kuwa matajiri, niliwazia na mimi niwe kama wao,na
ilipotokea nafasi hiyo nikajua huo ndio mwanzo,…oh, kumbe …kumbe, masikini,
kweli masikini haokoti, kweli….nimekuwa sikio la kufa… nikaingia kwenye mtego
wao, waliniambia hayo mengine hufanyika
kwa siri hata hao huwa wanafanya ila ni kwa siri..
Mungu wangu
nakuomba unisamehe …..’ nilitulia nikiwaza kuwa hayo ndio maneno ya mwishi
kabla ya uamuzi, lakini baadaye nikapata nguvu na kuanza kuyaandika haya;
**********
Nawaombeni
nyote mlione tukio hili kama fundisho kwenu,…msije kuhadaika kama mimi, kila
jambo mlionalo hapa duniani liangalieni kwa macho mawili, viapizo vya mambo
machafu havina maana ni uwongo, ushirikina nk, ni uwongo,…kutapeli, kuhadaa
wenzako ili ufanikiwe upate cheo, … utajiri wa namna hiyo ni wa muda mfupi tu
utaishi nao kwa mashaka tu , na mwisho wake utadhalilika, utakufa kwa aibu …..wao
wapo wapi sasa….walikuwepo kama hao, hivi sasa wapo wapi…
Labda mtaona
mimi ni fungu la kukosa lakini haya….ila ninachowamba nyote, mniombee mola
anisamehe, msiangalie machafu yangu tu mkanibeza, kuwa nimejitakia mwenyewe, kuwa
mimi nilikuwa sikiola kufa…sikuwa muangalifu, lakini oneni nilipotoka, haya
yanaweza kukuta hata wewe au kizazi chako, naombeni sana myaangalie haya kuweni
makini na huu utandawazi, labda mimi akili yangu ya kuona iliishia hapo, haya
na wewe ipambanue…
Nashukuru
pia, pamoja na utukutu wangu, lakini nilikuwa binti ninayependa kuwasaidia
watu, kuwasaidia watoto hasa mayatima, hasa wanyonge,nilikuwa najitolea kwenda
kusomesha shule za chekechea za mayatima, nilipenda pia kuwa mwalimu, japo nilitekwa sana kuwa muigizaji…pia nilikuwa
napenda sana kuwasaidia majirani,…sifa hizo na nyingine ziwe kwenye toba zenu mkiniombea…
Najua hata
mimi natakiwa kujiombea sana, basi mola kwa kutumia hayo machache ya wema
niliyofanya,unisaidie, ama kwa kufika huko mbele yako mapema, au ….vyovyote
uonavyo ni heri kwangu, ila hapa nilipo akili imechoka, sina jingine zaidi ,
zaidi ni kutimiza dhamira yangu,….
Oooh mola
wangu nakuomba usiniache nikateketea kabisa, nakuomba kutokana na mema hayo machache,
uniangalia kwa jicho la huruma unisaidie,…sijui
kama naweza kuishi tena,…ila wewe ndiye ujuaye zaidi….ila kama nitakuwa kwenye
mitihani zaidi , nikateseka na magonjwa haya naomba aichukue roho yangu haraha mimi
na mwanangu,…
Na kama mema
hayo yanaweza kunisaidia, yakanikwepesha na mitihani hiyo ya magonjwa , na
magonjwa hayo yakaponyeka, na kuondoka, basi naomba unipe njia sahihi, kwa
kadri upendavyo…
Ni kweli
kila mtu ana tamani kuishi sana, lakini kama uhai utakuwa kwenye mateso kama
haya mimi sitaweza kuvumilia tena….nimechoka mola wangu, nakuomba unisaidie
mola wangu, ,..Nifanikishe dhamira yangu na isiwe sababu ya kuniingiza kwenye
huo moto mkali,…bali iwe saabbu ya kunipumzisha na mateso haya,…najua ni kosa ,
lakini nifanyeje mola wangu….
‘Nifanyeje
mola wangu….! ‘ hapo nilitulia kwa muda kwani sikuweza kuvumilia, nililia sana…lakini
nikagundua muda umepita
Hapa
nashindwa hata kuandika zaidi, nimechoka, mwili umeanza kuchoka,… machozi
yanazidi kunimiminika, macho yamekuwa mazito sijui ni kwasababu ya usingizi….lakini
najua mengi mtaandikiwa, mimi naishia hapa….
Ila kabla
sijawaaga naomba msije kunifuatilia,…. hamtakuta kitu zaidi ya kaburi langu, naishia
hapa na kusema kwaherini wapendwa wangu, nawapenda sana….
Muda umefika
wa kutimiza dhamira yangu,… ninachukua kidonge hiki kwa uchungu japo dunia
naitamani…hata hivyo ni lazima nikimeze ili niweze kuyasahau haya mchungu yote…ngoja
nifanye haraka maana nasikia mtu anakuja, kwaherini…..
MWISHO
Hapo ndio
ilikuwa mwisho wa maelezo yake…
************
Sehemu hiyo
ya kwanza iliishia hapo, kutokana na melezo ya muhusika mwenyewe hivyo ndivyo yalivyotufikia,
sasa Maelezo mengine yatakayo fuata,ambayo yatakuwa kama hitimisho, yanatokana
na uchunguzi tuliokuja kuufanya baadaye
tulipojaribu kufuatilia tukio hilo.
Uchunguzi
wetu ulianzia hapo hospitalini alipokuwa amelazwa huyo mdada, japo hatukuwahi
kumkuta….
Swali je
ilikuwaje....je ilitokea nini….ni sehemu nyingine ya kisa hiki..
Tuzidi
kuombeana heri mola atufungulia njia za heri
WAZO LA LEO: MACHUNGU na RAHA, yote ni majaliwa
ya mola wetu! Ukipata RAHA leo usisahau kumshukuru mola wako, kwani yeye ndiye
mpaji wa yote na wala usijione kuwa wewe ni mjanja sana kuwazidi wasio nacho,
muhumu jitahidi kuwasidia wale waliopo chini yako, kwa hali na mali, kwani kwa
kufanya hivyo unajiongezea baraka, na wala usiwasimange na kuwaona wao ni
wajinga,….Kumbuka kuna kupata na kukosa.
Na
halikadhalika ukipata mitihani, shida zikakuandama usione kama umeonewa, huenda
kwa kuzipata hizo shida, mitihani hiyo ya maisha ni namna nyingine ya kukufanya
uvuke hatua, na kupanda daraja la juu zaidi, cha muhimu usikate tamaa, unachotakiwa ni kuzidi
kuwajibika, kujibidisha, huku ukimuomba mola wako, ipo siku utafanikiwa.
Tupo pamoja
Ahsanteni
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment