Ilikuwa kama
ndoto, sikuwa na uhakika, ila nakumbuka siku ile nilipozindukana walikuja
madakitari wale wawili , kwanza walipofika walisimama wakiangalia ile mashine
ya ukutani inayoonyesha mapigo yangu ya moyo, hawakuwa na haraka, wakawa wameinama
kwenye meza wakiongea jambo karibu na kitanda changu,…
Mimi nikawa
sasa nimezindukana vyema, na wao sasa kwa haraka wakanisogelea na kuanza
shughuli zao za kuondoa vifaa walivyokuwa wameniwekea mwilini
Sina uhakika
sana kama ni wao walikuwa wakiongea au niliyaona hayo kwenye njozi, lakini kuna
maongezi ya watu, walikuwa wajibishana au kuelezana, nikijaribu kuyakumbuka
hayo maongezi lakini kwa muda ule ilikuwa vigumu kuyakumbuka
Akili yangu
iliingiwa na hamasa ya kuyakumbuka hayo maongezi, na hadi nikataka kuwauliza hao
madakitari kama ni wao walikuwa wakiongea au ilikuwa ni ndoto tu lakini kwa
muda ule sikuwa na sauti, koo lilikauka, na wao walikuwa wakiongea mambo yao
mengine,
‘Huenda
nilikuwa naota tu..’nikasema kimoyo moyo,
Kama ni
kweli, nilikuwa naota au ni mazingumzo niliyoyasikia, lakini moyoni nilishajipa
uhakika kuwa na mimi nimeathirika, na pamoja na hayo nina tatizo jingine kubwa
, tatizo ambalo linanifanya nisiwe na uhakika wa kuishi tena mimi na mtoto
wangu, ni swala muda tu.
‘Nitajua
tu..’nikajipa moyo, na kiukweli kwa hivi sasa nilitaka kujua kila kitu,
nilikuwa tayari kwa lolote lile.
‘Ni lazima
waniambie, sitaki kufichwa tena….’nikasema
Wale
madakitari waliendelea kuondoa vifaa na kuniweka sawa, huku wakiongea
‘Sasa naona yupo
safi keshazindukana vyema…hana tatizo lolote….’akasema mwenzake akinikagua
machoni.
‘Ok,….
natumai tunaweza kumtoa huku chumba cha wagonjwa mahututi , …’akasema mwenzake.
‘Ni kweli
haina haja ya yeye kuendelea kukaa chumba hikiwakati hali yake imeshatengamaa,
na mimi nimechoka nataka nikajipumzishe kidogo,…ila bado anahitajia uangalizi
wa karibu…inabidi kuwaagiza manesi wafanye jazi hiyo…’akasema mwenzake
‘Lakini hili
tatizo la kupungukiwa damu linahitajia uchunguzi wa kina..’akasema
‘Hilo jukumu
sasa tutamuachia docta wa mambo hayo….na yule mwenyeji wake yupo wapi, maana
nilimuona…ni muhimu aruhusiwe kuongea na mgonjwa wake…..’akasema na wakawa
wameshamaliza kuniondoa vile vifaa wakaniuliza najisikiaje nikawaambia
‘Mimi hata sijielewi,ila
najiona nipo salama….’nikasema
‘Upo salama
usijali,….ni hali ya kawaida, tu, sasa tunakutoa humu unakwenda wodini kwenye
vyumba vya kawaida, usijali …’akasema huyo dakitari
‘Kwani
kulitokea nini….?’ Nikawauliza japokuwa akili ilishakaa vyema lakini nilikuwa
sikumbuki vyema
‘Ulipoteza
fahamu kidogo…,nahisi kuna mshituko ulikupata,….’akasema
‘Kwanini
inatokea hivyo, ….?’ Nikauliza
‘Ni
kawaida,….itaisha tu, kwani tatizo kama hili huko nyuma huwa linakutokea mara
kwa mara..?’ akaniuliza
‘Lilianza
kipindi hiki nikiwa mjamnzito, sijui ni kwanini….’nikasema
‘Mhh…inatokea,
ila kwa vile imechanganyika na matatizo mengine….lakini itaisha tu,pamoja na
hayo naona bado unaendelea kusumbuliwa na tatizo la upungufu wa damu, …na hili
tatizo inabidi tulichunguze vyema tuone ni kwanini inatokea hivyo…..tukifanya
uchunguzi wake itakuwa rashisi kupata matibabu stahiki…’akasema
‘Ina maana
damu yangu imepungua tena…?’ nikauliza
kwa mshangao
‘Ndio lakini
kwanza tunajaribu kuangalia ni sababu gani inayosababisha hilo..’akasema docta,
na hapo nikakumbuka yale niliyoyasikia,…. niliyasikia kama ndoto…au watu
wakiongea wakiulizana.. huenda ni wao walikuwa wakiongea,….lakini bado nilikuwa
sina uhakika.
‘Vipimo vyake vinaonyesha una
upungufu wa damu tana…inashangaza sana maana karibuni tulimuongezea damu,
japokuwa haikuwa nyingi, lakini tulijua kiasi hicho kitaongezewa na
vyakula…’nilisikia sauti hiyo
‘Kama nilivyokuambia, huyu ana tatizo
la seli ….’hilo neno sikulisikia vyema, ila neno cell, nililisikia, …
‘Kwa umri kama huu,
haiwezekani..’sauti nyingine ikasema
‘Inawezekana…kutokana na tatizo alilo
nalo la upungufu wa kinga mwilini…’sauti nyingine ikasema
‘Mhh, yawezekana, na uwezekano mkubwa
tatizo hilo litakuwa na kwa mtoto pia…’sauti ikasema
‘Uwezekano huo ni mkubwa,…. na kwa
vile hali hii imegundulikana kipindi hiki , sijui kama tunaweza
kumsaidia,….ilitakiwa pale ilipojulikana ana ujauzito, ndio tungeliweza
kuidhibiti hii hali japokuwa kwa mtoto, …sijui…’sauti ikasema
‘Mimi nahisi alikuwa na tatizo hilo udogoni,
…. lakini haikuwa na nguvu, au…yawezekana ameambukizwa,au….inashangaza
kidogo,..hili tutamwambia docta anayehusika na mambo haya atupatie
ufafanuzi…kwa hivi sasa tupambane na hili …’sauti ikasema
‘Muhimu tuangalia uwezekano wa yeye
kujifungua,….maana kama ataendelea hivi, hataweza kujifungua kwa njia ya
kawaida..na atazidi kuteseka,..’sauti ikasema
‘Lakini..hata hivyo kwa hali hii ya
upunfu wa damu hatuwezi kumfanyia upasuaji,..mpaka damu iwe sawa sawa…mimi
naona tumuongezee damu ili upasuaji huo uwezekane….’sauti ikasema
‘Ni bora tuangalie kwa leo kwanza,
kwa kiasi hiki tulichomuongezea, na dakitarii huyo akija anaweza kutupa ushauri
zaidii,…wasi wasi wangu hata tukimfanyia na mtoto akitoka salama, bado nina
mashaka na huyo mtoto,…kwa tatizo kama hili, kama litakuwa kwa mtoto,sizani
kama mtoto atakuwa na maisha marefu..’sauti ikasema
‘Ngoja tuone kwa leo…hayo tusubirie
huyo mtaalamu wa fani hii….tusiumize kichwa, …...’sauti ikasema …
Nahisi ni
watu walikuwa wakiongea kipindi nikiwa sijazindukana vyema….
***********
Nilihamishiwa
kwenye wodi za kawaida, na muda huo niliambiwa mwenyeji wangu anakuja
kuniona,..nikawa namsubiria, lakini kabla mwenyeji wangu hajatokea mara
akaingia Yule jamaa wa kule kijijini,…alionekana hana raha, sijui ni kutokana
na haya yaliyotokea kwangu au alikuwa na jambo jingine.
‘Vipi
unaendeleaje,…samahani sana kwa ..uzembe wangu,
kiukweli sikujua na…oh,nilishituka sana, ulipopoteza fahamu..nilijilaumu
kwanini nilikuambia mambo mengi ambayo yamekushtua hivyo, sikuwa
nimefahamu …’akaanza kujitetea
‘Hapana
usijali, nashukuru hata hivyo, kwani nimeweza kujua kinachoendelea , na kwa kwa hilo nimepata ujasiri sasa, na kwa
hivi sasa nipo tayari kusikia lolote lile…’nikasema
‘Hapana kwa
hali yako hiyo unahitajika kupumzika,..usiwe na mawazo mengine…unahitajia muda
kurejesha afya yako, mimi nimepita mara moja, nilikuwa namtafuta Yule mwenyeji
wako…’akasema
‘Ndiye
namsubiria, anakuja….usijali mimi kwa hivi sasa mimi nipo tayari kusikia lolote,
na akija huyo mwenyeji wangu nataka awaambie hao madakitari wanipe vipimo
vyangu nijitambue kabisa, najue yeye atataka kunificha, lakini sitaki tena
kusubiria….’nikasema
‘Ningekushauri
usibirie kwanza…hata hivyo mbona huna tatizo kubwa, kama lingekuwepo
wasingekusubirisha hivyo, wewe yuliza kichwa chako kwanza….’akasema
‘Hia haja…mimi
mwenyewe nimeshajijua, ….nahisi kama niliota,..lakini nahisi nimeathirika….ninao
huo ugonjwa,…na zaidi ya hayo nina hilo tatizo jingine..uhakika huo ninao kwa
sasa….’nikasema
‘Hujaathirika
dada …kwasaabbu nijuavyo mimi akina mama wajawazito wanapimwa mapema, na wewe
ungelishajijua …wangelishakuambia hilo mapema ili uchukue tahadhari na
wangetakiw akukupa dawa za kukusaidia, na kama hawakukuambia mapema ina maana
huna tatizo…’akasema
‘Nahisi
waliechelea kuniambia, wakiogopa hali yangu, kwani tangu awali nimekuwa ni mtu
wa kushituka na kupoteza fahamu..na hili la kuniambia mtoto kakaa vibaya nahisi
ilikuwa ni mbinu ya kunificha jambo…ili niweze kufika sehemu ya wataalamu
zaidi, tatizo ikawa hali ya uchumi…..nauli na….sijui kwanini walinichelewesha
hivyo, labda walijua sitaishi ….’nikasema
‘Hapana wala
usiwaze hivyo, mimi ningekushauri sana uwasikilize madakitari wanachokushauri,
wao wanajua zaidi…na ukijiwazia mabaya, unazidi kujiumiza zaidi, ..jipe moyo kuwa huna ili mungu akujalie ujifungue salama,
…maana hapo ulipo unapambana na mawili, wewe na mtoto..’akasema
‘Mtoto
mwenyewe ataishi basi…..’nikasema nikijaribu kuangalia tumboni,…nikajitahidi
kuondoa mawazo ya huzuni ili nisijiweke kwenye hali tete tena.
‘Kwanini
unasema hivyo…?’ akauliza
‘Kama
ulivyosema awali kuwa…., ndugu yako alikwua na tatizo akizaa mtoto hadumu,
anafariki kabla hata hajafikia miaka miwili wakasema ana tatizo la cell, …na
mimi nahisi kaniumbukiza…’nikasema
‘Lakini huna
uhakika na hilo..na sio lazima,…..mimi naona usiyawazie hayo kabisa, …ngoja
niende nikaonane na huyo mwenyeji wako, ninachokuomba kwa hivi sasa ni kuweka
mawazo ya kwa mungu,…mungu ndiye atakuwa msaada wako mkubwa, na ujue kabisa
magonjwa, shida ni sehemu ya mitihani, yakubali na na kubali kuwa yana mwisho ,
utapona, …na kupona kwako ni udhabiti wako wa nafsi, usijinyongeshe…na kwa hivi
sasa ni bora upumzike kwanza….’akasema akitaka kuondoka.
‘Usiwe na
haraka…mwenyeji wangu atakuja hapa kaa tuongee, haiwezi kutokea tena,..hilo
nakuhakikishia, ikitokea ujue ndio safari yangu, na safari yangu nimeshaiona
kwenye ndoto…sina muda wa kuishi tena, nimeshachoka,..haya hivyo nataka kujua
kila kitu…kwanza nimeshajua kuwa nimeathirika, ….na zaidi nina hilo tatizo
jingine ambalo linanifanya nijue kuwa mimi sina maana tena hapa duniani….’nikasema
‘Hapana,
huwezi kujua hilo mpaka mtoto azaliwe na mara nyingi anayekuwa na matatizo hayo
anakuwa ni mtoto sio mama…huenda ukahisi hiyo hali, …lakini ni ya kupita tu
,ukijifungua hali itakuwa vyema…na hata mtoto akibahatika akavuka miaka zaidi ya miwili anakuwa keshaepukana na ugonjwa huo,
mbona imetokea,..na utaalamu siku hizi upo muhimu kama nilivyokuambia ni
kufuata masharti….’akasema
‘Mimi
nimeathirika hilo sina shaka nalo…waniambie wasiniambie nimeshajifahamu na ni
lazima waniambie… kama mchumba wangu alikuwa nao, na huyo kaka yako mshenzi …..japokuwa
keshafariki lakini ….tutakutana huko ahera, ana kesi ya kujibu…..’nikatulia na
mdogo mtu akawa kainama akionyesha machungu.
‘Wote hao,
na hata huyo mchumba wangu ndiye kabisa, sijui kama nitamsamehe kwa hili…najua
ni vyema kusameheana, lakini …..kwanini wakanifanya hivi….unajua niikuwa
najiuliza ni nini kilitokea hadi nikatembea na hao wanaume wote, nimekumbuka….’nikasema
‘Achana na
hayo shemeji , usiyaongee hayo tena…’akasema
‘Haina haja…nakuambia wewe kwani wastahili kufahamu na hata
ukikutana na huyo mchumba wangu mwambie kabisa aliyonifanyia,….kuniingiza
kwenye madhambi nisiyostahiki nayo ana dhmabi kubwa mbele ya mungu….’nikasema
‘Msamehe,….anastahiki
msamaha wako,ili…’akatulia
‘Msamaha
wangu ataupata, sawa, mimi nimeshamsamehe, lakini hiki kiumbe je,…kina makosa
gani,..yeye ni nani atamuhurumia, …kaingizwa kwenye shida kutokana na tamaa za
watu wengine,…walitaka mali,haya walipata sasa wamefika wapi….’nikasema
‘Mimi najua
tatizo hilo sikuwa nalo, sijawahi kusikia kwenye familia yetu wakiliongelea
hilo, nina uhakika limetokana na huyo kaka yako…siku waliponiwekea madawa, na
kuigiza mapicha yao, bila ufahamu wangu…najua hakuna atayenielewa hilo…’nikatulia
‘Hayo
yamepita shemeji mimi naona usiyawazie hayo tena…’akasema
‘Ni lazima
niwaze maana nilitaka kujua ni kwanini niweze kutemeba na hao wanaume wte,
wakati mchumba wangu alikuwepo…ni yeye aliniruhusu…yawezekana ni yeye aliniruhusu
kwa tamaa zake, au wenzake walimzunguka, ila nina uhakika nilitembea nao…niliwahi
kuiona hiyo video, sikuwa nimelazimishwa inaonekana kabisa niki….kwa hiari
yangu kabisa..’nikasema
‘Hayo madawa
hukutoa akili kabisa…nafahamu,lakini usiyawazia sana….achana nayo, mbona huyo
mwenyeji wako anachelewa kuja….’akasema
‘Mimi
nimeshajifahamu …sitaishi muda mrefu, maana hayo madhara ya ugonjwa huo mwingine, yamehamia
kwangu kutokana na upungufu wa kinga mwilini, sina kinga za kuzuia, mimi na
mtoto sote tupo hatarini, nahisi hivyo….na hio la kusema tatizo hilo litaondoka
pale nitakapojifungua ni kudanganya tu, kwani wanawake waliowahi kuzaa na huyo
kaka yako waliishi ,si walikufa wote,..’akasema
‘Nani
kakuambia hayo…shemeji achana na hayo, usiyawazie hayo zaidi, huyo mwenyeji
wako yupo wapi?’ akauliza akionyesha wasiwasi.
‘Nimeyasikia…hahaha,
nani asiye yajaua, yeye alidanganya kuwa walipata ajali,mwingine alifariki
kwakuumwa tu, akijifungua….ila ufunuo huo nimeupata kwenye njozi, mimi sina
muda mrafu wa kuishi....na namuomba mungu hicho kiumbe chake kisitoke hai
kisije kupata haya mateso ya dunia…ndio maana naimeingiwa na shauku moja,….’nikasema
‘Shauku gani….?’
Akaniuliza akionyesha mashaka
‘Nakumbuka
wakati tunapeana viapo…tuliambizana kuwa ikitokea kushikwa na askari ikabidi
kutajana ni bora unwe ile sumu…ili uachana na mateso ya polisi,…’nikasema
‘Wewe unawaza
nini tena….’akasema sasa akionyesha wasiwasi wa dhahiri
‘Nakuambia
wewe kama mtu uliyenifunulia ukweli nataka hii iwe siri kwako,….nakusudia
kufanya hivyo,….’nikasema
‘Hapana,
hapana, usifanya hivyo, tafadhali….’akasema
‘Yote
yategemea jambo moja….’nikasema
‘Jambo gani….?’
Akaniuliza
‘Ukweli
halisi wa vipimo….’nikasema
‘Lakini huna
matatizo….’akasema
‘Kama
wataendelea kunificha hivyo, ndio sitachukua muda kutimiza maamuzi yangu…ni
bora waniambie ukweli haraka, ili nisiendelee kuwapa shida….’nikasema
‘Umevunja
mungu, nilitaka wewe uwe mmoja wa watu tutakaoungana pamoja kupambana na haya
matatizo tuwaelimishe wanajamii…kwa nini ukate tamaa huoni mimi nipo pouwa
kabisa….’akasema
‘Wewe upo
pouwa,..wewe ni mwanaume, wewe hutaraji kushika mimba….wewe…lakini mimi hapa
nilipo nimekalia kuti kavu, nina mimba, natarajia kuzaa kusicho riziki, maana hata
nikijifungua salama, mtoto huyo hatadumu,…namuona mtoto huyo kama marehemu,
hata mimi mwenyewe sio wa kuishi muda mrafu kwanini niwapatishe watu shida…..’nikatulia
‘Lakini
kwanini uwe na mawazo hayo mafupi,..?’ akauliza
‘Mimi kama
mama nampenda sana mwanangu, miezi tisa
ya mateso, ni ushahidi tosha, wa mapenzi ya mama kwa mtoto, nilitarajia nimbebe
mwanangu anyonye ziwa, alie, nimbembeleze, lakini fursa hiyo sitaipata tena,
yatakuwa maisha gani ya huzuni na kulia, maisha ya mateso, siwezi kuiona hiyo
hali tena,…nimeshachoka, na pia sitaki pia watu waje kusumbuka na huyo mtoto….’nikasema
nikitamani kulia…lakini nikaizuia hiyo hali ya unyonge.
‘Lakini…mbona
wataalamu wamesema hilo lawezekana, kupata mtoto, na asiwe na hayo matatizo na
hata kama atakuwa nayo kuna njia siku hizi za kuidhibiti, na kwanini unakata tamaa hivyo, hujajua lolote….hujaambiwa kuwa…?’
Akauliza na akakatiza kuendelea
‘Mimi
nilitaka nimpate huyo mtoto, japokuwa kiukweli atakuwa ni kumbukumbu yenye
majonzi ya maisha yangu ya taabu na mashaka, lakini hapo hapo angelikuwa ni faraja
kwangu,…..lakini nimesikia hata akizaliwa huyo mtoto atakuwa ni mtoto wa kuumwa
umwa tu, na hataweza kufikia miaka mitatu, ….mimi sielewi , ila njozi na maono
yameniambia hivyo nd ndio ukweli wenyewe…’nikasema
‘Ni nani
kakuambia hayo, umeyasikia wapi…?’ akauliza na mara mlango ukafunguliwa, na
akaingia Yule mwenyeji wangu akiwa na dakitari mgeni machoni mwangu.
Tulisalimiana
na mwenyeji wangu akasema;
‘Waonekana
leo mchanamfu na mwenye nguvu ya ajabu, hii ni dalili njema…’akasema
‘Ni kweli
kama ukiwa na mgonjwa, akiwa kazidiwa, na siku moja ukaja ukamuona tofauti ana
nguvu…ujue ni dalili njema, kuwa aliyemuumba anamuhitajia, au sio….’nikasema
nikicheka kama utani na wao wakacheka kuashiria ni utani, hawakuja nafsi yangu ….
‘Hapana,
hiyo ni dalili njema kuwa mgonjwa anapona…na utapona tu kwa uwezo wamungu na
kwa madawa, ….siku hizi utaalamu umeongezeka…’akasema mwenyeji wangu na
kumgeukia Yule dakitari aliyekuja naye
‘Huyu hapa
ni dakitari bingwa wa maswala ya mambo ya damu…na mambo yanahusiana na hayo,
amekuja maalumu kuangalia tatizo lako hilo la kupungukiwa damu, …..na atakuwa
na maswali ya kukuuliza kidogo…., ila kwa hivi sasa nataka kuongea na wewe,
yeye ataonana na wewe baadaye….’akasema mwenyeji wangu na dakitari akanisalimia,
‘Basi
baadaye nitakuja tuongee, nasubiria matokea ya vipimo vyako vya damu, yakitoka
nitajua tatizo ni nini, ila kuna maswala muhimu nitakuuliza baadaye ukimalizana
kuongea na mwenyeji wako, matatizo kama hayo yapo na yana tiba usiwe na shaka
kabisa….’akasema na kuondoka.
Alipoondoka
huyo docta, mwenyeji wangu akageuka kumuangalia yule jamaa kutoka huko
kijijini, akasema;
‘Vipi wewe bado
upo mbona wenzako wameshaondoka…?’ akaulizwa
‘Ndio
sitaongozana nao kwenye hiyo safari,
nilitaka tuonane kwanza na wewe…’akasema
‘Sasa
kwanini umekuja huku, nilikuambia usije
kumuongelesha huyu mdada tena, hujasikia una nini na huyu mgonjwa unataka
kumuondoa duniani kabla ya siku zake…ina maana, hukunielewa…’akasema kwa sauti
ya ukali
‘Nilipitia
kumuaga tu….’akasema
‘Unajua
sisemi haya kwa ubaya nayazungumzia haya kwa nia njema, kitaalamu, na kwa hayo
yaliyotokea, ungeliweza hata kuchukuliwa hatua za kisheria, hukutakiwa kuongea
naye kabisa, kumwambia hayo uliyomwambia na kwa jinsi ilivyotokea umewapa shida
sana madakitari….’akasema
‘Kiukweli….nilijua
….ana…ufahamu huo..sikuwa nime…’akazidi kujitetea na mwenyeji wangu akamkatiza
na kusema;
‘Wewe huoni
kuwa unaweza kumdhuru huyu mgonjwa bila kujua, na sijui kwanini walikuruhusu
kuongea naye…nesi mnafanya nini...’akasema akigeuka kumwangalia nesi aliyefika
akiwa na dawa
‘Hatukumruhusu
sisi…walikuwa kwenye semina zao, na sijui walianza kuongea muda gani, na huyu
mgonjwa….’akasema nesi
‘Samahani
sana sikujua….’akajitetea
‘Hukujua eeh…!
Wewe hujui kuwa wagonjwa kama hawa wanahitajia namna yao ya kuongea, hapa alipo
ana mzigo mkubwa, huyu hapa ni mja mnzito, utaharibu uja uzito wake, unaweza
hata kumleta tatizo kubwa zaidi hili…hili unalielewa, kwa vile wewe upo kwenye kundi la kuhamasisha
watu, si mlielekezwa haya …...?’ akasema na kuuliza
‘Mimi
nilikuja kumuaga tu, natakiwa kurudi huko kijijini haraka….sikuwa na nia ya
kumwambia lolote baya kwa hivi sasa, nafahamu kabisa hali aliyo nayo na
uangalifu anaotakiwa kuwa nao,…kosa la mwanzo ni kuwa sikuelewa ana matatizo
gani, lakini hata hivyo….’akasema na mwenyeji wangu akamkatisha na kwa kusema;
‘Tafadhali
nakuomba uondoke…huyu hana matatizo makubwa kihivyo, wewe umemfanya ahisi hivyo
kumbe tatizo lake ni dogo tu, na atapona bila shaka…’akasema huyo mwenyeji
wangu
‘Kuna jambo
muhimu nilitaka tuongee mimi na wewe, ….’akasema jamaa wa huko kijijini
‘Hilo jambo kwa
hivi sasa litasubiria,…utaniambia baadaye , …ama kwa huyu mgonjwa wangu sitaki
umwambia tatizo jingine lolote kwa hivi sasa, umenielewa, sitaki kosa lijirudia
tena kwa hali aliyo nayo haitakiwi hiyo hali ijirudie tena, …’akasema mwenyeji
wangu kwa sauti ya ya chini kama anamnongeneza ili nisisikie, wakati huo nesi
alikuwa akinipa dawa.
Walisogea pembeni kidogo, nikasikia akimuuliza
‘Kwani kuna
nini……wataka kuniambia… ni kuhusu huyu mgonjwa au kuna jambo linamhusu.?’ Akamuuliza
na mimi nikasema kwa sauti
‘Ni tatizo
gani hilo na mimi nataka kulisikia kama linanihusu mimi…., mwacheni aniambie ,
mimi nipo tayari kwa lolote, na kwanini mpaka umwambie yeye, yote
nimeshayafahamu, kumebakia nini tena, na hata hivyo, sasa nipo tayari kwa
lolote, haiwezi kutokea tena mshtuko…’nikasema na mwenyeji wangu akatikisa
kichwa kukataa, na mimi nikasisitiza kuwa aniambie
‘Ni bora
asema ni jambo gani maana asiponiambia nitabakia na mashaka nikiwazia ni jambo
gani na najua litakuwa linanihusu, asema tu…’nikasema
‘Wewe
usijali, nitamalizana naye…tutaongea naye ofisini kwangu ni maswala yao ya
kampeni za kuhamasishana hakuna zaidi au sio
’ akasema na kumuuliza na akijaribu kumsogeza mbali kidogo jamaa ili
nisiweze kusikia, na jamaa akamwambia kwa sauti ya chini chini lakini mimi
niliweza kusikia hayo maneno machache
‘Ni kuhusu aliyekuwa
mchumba wake….’alianza kusema na mwenyeji wangu akamzuia asiendelee , akisema;
‘Tutaongea
ofisini kwangu, sasa hivi nina taka kuongea na mgonjwa ili aendelee na matibabu
mengine…nimeshakuelewa, sawa..tangulia nakuja…’akasema akimsukuma aondoke, na
mimi nikasema.
‘NI lazima aseme
na mimi nisikie, huyo aliyekuwa mchumba
wangu kafanyaje…..aseme tu ….’nikasema nikijiinua kitandani. Na mwenyeji wangu
akawa akimuashiria jamaa aondoke, lakini sikukubali……
NB: Kunani..
WAZO LA LEO: Ubaya umtendee mwenzako, na mabaya
yampate mwenzako, ..ni rahisi kutamka pole, au yote mapenzi ya mungu. Ila kwa wale
yaliyowakuta watajua ni nini adha na maumivu yake. Hii inatupa fundisho kuwa
sote ni wanadamu na sote yanaweza yakatukuta mabaya na mazuri, kwahiyo
tunahitajika kusaidiana, kuoeneana huruma tuwe kama mwili mmoja, ambao sehemu
moja ikipata jereha mwili mnzima unahisi maumivu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment