Inspecta Moto aliwasiliana na watu wake tayari, na
kutaka kuhakiki kama kweli huyo binti anachosema ni kweli, aliwaambia watu wake
wafuatilie kama huyo mtu aliwahi kufika hapo, lakini isijulikane, na ulinzi mkali ufanyike kuzunguka
hilo jengo, kuhakikisha kuwa huyo mtu hatoki hapo. Kwa taarifa za haraka
zilisema hajafika hapo, akamgeukia nesi na kumuuliza.
‘Una uhakika huyo mgonjwa alikuambia atakuwepo huko?’
‘Ndivyo alivyoniambia, kama huniamini basi….’akasema kwa
hasira
‘Tunachotaka ni kuwa na uhakika, maana muda kwetu ni
muhimu sana, mimi nakuamini, na tutakwenda huko,cha muhimu ujua kuwa huyo mtu
sio mtu mwema, kama kuna alichokuwa amekuahidi ujue ni mbinu za kujinufaisha, …’akasema
Moto
Nesi ambaye sasa alikuwa hana raha, akionekana kukata
tamaa, akamwambia;
‘Mimi hata sijui, hata sijielewi, …’akasema
‘Kila jambo lina mwisho wake, na mwisho wa hawa watu ni
huu, ninachokuomba ni kutoa ushirikiano ili tumnase huyu mtu, na haki itendeke,
hatujasema kuwa ni mhalifu, uhalifu wa mtu ni mpaka afikishwe mahakamani na
ndicho tunachokitafuta ...’akasema
‘Mimi sikujua kabisa kama huyo mtu ni mhalifu, na
niliamua kumsaiida kwa nia njema, hata mnavyoniambia nashindwa kuelewa, mtu
tajiri, ana mapesa yake, kwanini tena awe mhalifu, ndio maana nasema mimi
sielewi, nitafanya mtakvyo tu,...’akasema
‘Nimekuelewa, ila kukuamini kwetu kuwa kweli upo na sisi
ni wewe kufanya hayo tutakayokuambia…sawa, haya hebu geuka kidogo…’akasema inspecta akawa anamvalisha kitu kwenye nguo ya
huyo nesi kwenye ukosi, ni kitu kidogo tu ambacho hata nesi hakuhisi kuna kitu
kimewekewa na kingine akakiweka kwenye nywele kinamna tu, kinafanana na ywele
huwezi kuhisi kuna itu kimewekwa
‘Unaniweka nini?’ akauliza
‘Ni lazima ufike pale ukiwa mtanasahati, kola ya koti
lako ilijikunja….’akasema Inspecta
‘Hata sijali tena, siku yangu yote umeiharibu, hata
sitamini kwenda huko tena…’akasema
‘Kwenda ni lazima uende huko utakutana na watu wangu
watakulinda, usiwe na sahaka….’akasema Moto
‘Kuna watu wako nitakutana nao…!, kwani wewe
utafanya nini, utaniacha niende peke yangu, ....mimi nimeshaanza kuogopa, najua
akifahamu kuwa nimemsaliti anaweza kunifanya kitu kibaya...’akasema
‘Ndio maana nataka uwe makini kwa kila hatua, hatutaki
kabisa afahamu hilo,....wewe ukifika hakikisha unakuwa kama unavyofanya siku
zote, na usijishuku, uchunge kauli zako, na akikuuliza lolote kuhusu mimi au kama kuna
kitu chochote, utasema uliongea na mimi, ukaniambia hujui lolote basi....’akasema
‘Wewe humfahamu huyo mtu anashuku kama
mchawi....’akasema nesi
‘Kwahiyo unamfahamu vyema, inaonekana mnafahamiana sana, ...ok tusipoteze muda, wasiliana naye
kuwa unakwenda kwake, usikie atasemaje….’akasema, na nesi akachukua simu yake
na kutuma ujumbe wa maneno, na ikachukua muda, ujumbe ukajibiwa, na Inspecta
akachunguza ile namba, ni namba ngeni, haikuwepo kwenye zile orodha za namba
alizokuwa nazo mwanzoni
‘Hii namba aliwahi kuitumia kabla?’ akaulizwa
‘Hapana yeye huwa anabadili namba za simu kila mara, hii
namba sijawahi kuiona kabla...’akasema nesi
‘Soma huo ujumbe unasema nini...’akasema Inspecta
‘Kama
tulivyopanga, uwe na makini....’akasema Nesi
‘Mlipanga nini?’ akaulizwa
‘Nifike huko, tuongee, tustarehe kwa kunywa na kula,
kupoteza muda, ikifika usiku mimi narudi zangu ni yeye anarudi hospitalini
kuendelea kuwa mgonjwa ni hivyo tulivyopanga, sasa sijui kama itakuwa hivyo..,
.....’akasema
‘Sasa nikuelekeza jinsi gani utakavyofanya, ukifika
huko, fika kama kawaida, usiwe na wasiwasi, mengine wewe utuachie, utatumia
usafiri wako kama kawaida, hutakwenda na mtu,..ila hakikisha humwambia chochote
zaidi ya kuwa umeongea na mimi....natumai umenielewa....’akasema
‘Eti nisiwe na wasiwasi, hivi kwa hali hiyo utakuwa huna
wasiwasi, hilo siwezi kukuficha,…hata sijui kuigiza..’akasema
‘Jitahidi….’akasema Moto
Yule nesi alitangulia kuondoka, na Inspecta akakutana na
mmoja wa watu aliyemuagiza vifaa mbali mbali ikiwemo bastola yake. Akachukua
kifaa maalumu, akakiweka kwenye simu yake,, sasa akawa anamuona nesi hatua kwa
hatua kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Alipohakikisha kuwa kila kitu kipo shwari na ameshabadili nguo zake na kuvaa
nguo za kikazi na fulana maalumu ya kuzuia risasi zisipenye, akaanza kuondoka.
Alipofika mlangoni akakumbuka kitu, akarudi hadi ofisini
kwa msaidizi wa doctai ambaye kwa muda huo alikuwa akihudumia wagonjwa, japouwa
alionekana hayupo kwenye hali nzuri, akamsalimia tu,
‘Naona mlikuwa manaongea na nesi wangu ....’akasema huyo
docta msaidizi kwa sauti ya kilevi levi
‘Ni kawaida tu, je umewasiliana na docta wenu mkuu......’
akauliza
‘Ndio kaniambia kila kitu, na nakuhakikishia tutashirikia
nanyi hadi mwisho, hata mimi natamani hali hiyo iishe, ili tufanye kazi kwa
uhuru, nilikuwa naishi maisha yasiyo na amani.
Nilipokuja kugundua kuna kitu
kisicho cha kawaida kinachoendelea hapa kwenye hii hospitali..’akasema
‘Kuna lolote ambalo unaweza kuniambia kwa hivi
linaloweza kusaidia, maana sina muda wa kupoteza kwa hivi sasa?’ akaulizwa
‘Kwa ujumla mimi sijui mengi, aliyekuwa karibu na huyo mgonjwa
ni docta mkuu...kwakweli sikuamini jinsi huyo mgonjwa livyonifanyia, mimi
nilijua anaumwa kweli nilivyoitwa kumuona na nesi, ....nilipofika kitandani
kwake nikijua kuna mtu, kumbe kaweka mito mithili ya mtu kalala, nilipoinama
kufunua, mara nikahisi mtu anakuja kwa nyuma kabla sijageuka, akanipiga sindano
hiyo ya usingizi...’akasema
‘Ok, tutajua zaidi baadaye, na ujue utasimama mahakamani kutoa
ushahidi...’akaambiwa
‘Hamna shida, nipo tayari kwa hilo, nitaeleza kila
ninachokifahamu..’akasema
Inspecta
akaondoka, huku akiendelea kuwasiliana na watu wake kujua wamefikia wapi, na
nesi keshafika wapi, katika simu yake ambayo ina mitandao alikuwa akimuona nesi
hatua kwa hatua, huku pia akiwasiliana na watu wake , akachukua pikipiki yake
na kuendesha kuelekea huko Hoteli ya Paradise.
Alipofika maeneo hayo, akakutana na watu wake, akapewa taarifa
nini kinachoendeelea, yeye akawaambia mengine anayafahmu, yeye anaingia ndani
ya jengo, na wakati huo, alishamuona nesi akiwa keshafika orofa ya juu, akawa
sasa anatembea kuelekea chumba alichoelekezwa, kabla hajakifika moja ya chumba
kingine kikafunguliwa, na mtu aliyevaa sweta lenye kuficha uso,akatokeza na
kumshika nesi mkono, akamvutia ndani ya hicho chumba
Inspecta akawasilianna na mtu wake aliyekuwa karibu na
eneo hilo, na huyo mtu akasema keshaliona hilo tendo, je achukua hatua gani
‘Subiri kwanza....’akasema Inspecta na muda huo
alishafika eneo la rosheni hiyo, na akawa anaangalia simu yake, akamuona nesi
akiongea na huyo mtu.
‘Una uhakika hakuna mtu aliyekufuatilia...?’ huyo jamaa
akauliza
‘Hakuna..nina uhakika, akasema nesi, na huyo mtu
akachukua kifaa fulani akawa anamkagua nesi, kuhakikisha kuwa hana kinasa
matukio, na Inspecta alikuwa na mashaka kuwa kile kifaa alichomwekea nesi
kitaonekana, na ndicho kinachomsaidia kujua ni nini kinachoendelea, lakini yule
mtu kabla hajamaliza, akapigiwa simu, akamuacha nesi na akawa anaongea na simu.
‘Ameshafika…’akasema
‘Sawa nitamuambia…’akasema halafu akamgeukia nesi na
kusema;
‘Sasa mkuu yupo chumba kingine sio kile alichokuagiza,
kafanya hivyo kwa tahadhari, toka hapa nenda chumba namba 285, gonga mara
tatu...tulia gonga tena mara tatu, atakufungulia...’akasema huyo mtu.
‘Kwanini anafanya hivyo, ana wasiwasi gani,mbona siku
zote tunakutana bila tahadhari za namna hiyo...’akasema nesi
‘Wewe huoni katoroka huko hospitalini, ni lazima atakuwa
anafuatiliwa, na nahisi kama kuna kitu umevalishwa, sikioni, lakini sio hoja,
wewe nenda tu..’akasema huyo mtu akimkagua nesi kwa macho
‘Kitu gani, na nani anivalishe, nyie watu bwana, kwanini
mnaniweka roho juu, na mbona siku nyingine alikuwa anatoka na kurud kwanini sasa
atoroke, hamuoni kuwa mimi mnaniwekwa kubaya,...’akasema
‘Usijali yeye anajua ni ni cha kufanya...mtaongea naye,
mimi nimemaliza kazi yangu, …..’akasema huyo mtu na akawa anaongea na simu, na
baadaye nesi akatoka, na kuelekea chumba alichoelekezwa, akagonga kama
alivyoambiwa, na chumba kikafunguliwa, na nesi akawa yupo ndani ya chumba
Hakukuonekana kuwepo na mtu yoyote ndani ya hicho chumba,
lakini mlango ulijifungua, na nesi alipoingia ndani ukajifunga wenyewe, na kulipita
muda, mara sauti ikitokea kwa juu kwenye kitufe, ikasema;
‘Nitakuwa na wewe dakika chache nahakikisha usalama
kwanza, mitambo yangu yote imezima ghafla, nahisi kuna tatizo,na kama ni tatizo
n bora wewe uondoke bila ya kuonana na mimi…’sauti ikasema
‘Hata mimi sina muda wa kukaa zaidi, nitakuwa natafutwa
huko nilipotoka, ujue kuondoka kwako kumeleta matatizo, unatafutwa haujulikani
wapi ulipo..’akasema nesi.
‘Nafahamu hayo, nimefanya hivyo makusudi, waache
wanitafute tu,....ni nani mwingine zaidi ya Moto mliyeongea naye….maana mitambo
yangu haifanyi kazi siwezi kujua kinachoendelea…’akasema
‘Hakuna mwingine, ….na mtu mmoja niliekutana naye
akanielekeza nije hapa, basi, hakuna mwingine…’akasema
‘Huyo ni mtu wangu ndiye aliyebakia wa kumuamini…..’akasema
‘Lakini sasa, mimi unaniweka katika mahali gani, huoni
kuwa umeniingiza kwenye matatizo….?’ akauliza nesi
‘Usiwe na wasiwasi, ...nitakulinda ikishindikana utakuwa
kama hao wengine, hawatakuona tena, na watakusahau basi tutafanyaje....’akasema
‘Watanisahau una maana gani?’ akauliza nesi
‘Utakuja kujua nina maana gani baadaye ikibidi
, sasa hivi nipo vitani, na kwenye vita hatuangalii mtu
machoni yoyote atakeyekuja mbele yako, ukamuhisi ni adui, unatakiwa kummaliza
mara moja...’akasema
‘Sijakuelewa,..upo vitani na nani?’ akauliza nesi
‘Sio muda wa kuulizana maswali, unakumbuka nilikuambia
ukija nitakuagiza kitu...’sauti ikasema
‘Kitu gani, mimi nikitoka hapa narudi nyumbani kwangu
siwezi kuja hapa tena, naogopa kbisa na sasa hata sikuelewi, naoana kama
ulikuwa ukinitaka ili tu nikusaidie mambo yako, kumbe wewe ni mhalifu...’akasema
‘Achana na upotofu huo,….sikiliza kuna kifaa, kuna mtu
kapewa kifaa na Inspecta Moto, kifaa hicho ni muhimu sana kwangu, nakihitaji,
kuna mambo yangu mengi humo, ...sasa wewe unatakiwa uende na pesa nyingi tu
umshawishi huyo mtu akupe hicho kifaa, yule kijana akipewa pesa nyingi hatakuwa
na maneno, namfahamu sana..’akasema
‘Kifaa gani hicho....?’ akauliza nesi, akajikuna kichwa
akahisi kitu kigumu, akataka kukivuta lakini akasita akatulia akimsikiliza
‘Ni kifaa cha komputa, kina kumbukumbu zangu za nyuma,
....nakihitajia sana, hicho kikifika mikononi mwa hao watu,
...basi...nimeumbuka,..unasikia, ni muhimu sana kwetu, alikuwa nacho mama,
nikajua kimeshaharibika,..lakini kumbe..bado kipo, unajua mimi nakupenda sana,
na ndoto zangu kiukweli ni mimi na wewe, wewe uwe malikia wangu wewe huoni sina
mke mke mke wangu mtarajiwa ni wewe, lakini sasa...oh , hicho kitaharibu kila
kitu...’akasema
‘Umejuaje kuwa hicho kifaa bado kipo...ulisema kila kitu
kipo shwari, hakuna kikwazo, sasa kwanini unasema hivyo?’ akauliza nesi
‘Kuna mitambo niliyokuwa nikiitumia, nilikuwa naona kila
kitu, lakini sasa haifanyi kazi na mtu wangu wa mitambo na mitandao ameshakamatwa, ndio maana hawa
watu sikutaka waendelee kuwepo,...nilijua kila kitu naweza kukifanya mwenyewe
baadaye, lakini naona bado nawahitaji, sasa....lakini…., sijui ilitokeaje, wakapona, wangetoweka kabisa
ningejua jinsi gani ya kutoka tena, kutoka tena kama mtu mwingine, lakini
haiwezekani bila hicho kitu,....’ akasema.
‘Mimi hata sikuelewi,...mambo yako unayongea ni kama
muota ndoto isiyowezekana, sasa niambie moja, ndoto yetu ya kuwa pamoja, ya
kunisomesha niwe docta mkubwa, yote ilikuwa ni mashairi ya kuniteka akili, au….?’
akauliza nesi
‘Sijui....natamani ingelikuwa hivyo, lakini
sijui...muhimu, ni hicho kifaa, unaona hapa nipo gizani, wala sijui
kinachoendelea, Moto, huyu mtu anayeitwa Moto, kaharibu kila kitu, nataka huyu
mtu afe, lakini kila mbinu zakumaliza zimeshindikana,......angekubalia akawa
kama Maneno, isingelikuwa ni taabu...mmh, hawa watu bwana, wanataka niniI
katika hii dunia, ….wanataka kishi maisha ya taabu, mimi utajiri ninao,
nilitaka na wao wawe matajiri, lakini hawanielewi, ....aah, unaona hapa, hata
siwezi kabisa kuwasiliana na yoyote...’akasema
‘Kwa hiyo unataka mim nifanye nini....? akauliza nesi
‘Unajua, nilimuona Inspecta Moto akiwa nacho, sikujua
kipo wapi kabla, maana hakikutakiwa kuwepo kabisa, kiltakiwa kiharibiwe mapema
mama,…akakificha,….ajabu nakiona anacho huyu mtu anayeitwa Moto, akampelekea
huyokijana, unakumbuka kuna siku nilikuambai unisaidia nitoke, lakini
ikashindika..?’ sauti ikasema
‘Yah, ...unajua isingeliwezekana siku ile...ilikuwa ni
hatari, bosi alikuwepo, alikuja bila kutarajia,.....unajua kila kitu, chako ni
cha kuficha ficha ningelijua ni nini kinachoendelea ningelijua cha
kufanya...’akasema nesi
‘Basi siku hiyo nilipanga kwenda kumvamia huyo kijana
kwani alikuwa akifanya juhudi ya kukifungua, kila kina namna ya kukifungua,
nahisi atakuwa keshagundua, yule kijana ni mtundu sana, ningelijua nikamchukua
huyo kijana kwenye anga zangu, sasa hata
sijui nifanyeje,...na kwa utundu wake, najua sasa hivi atakuwa ameweza
kukifungua....kwahiyo nataka uende kuonana naye. Mapema iwezekanavyo,
vinginevyo ndoto yetu itakuwa kweli ya kufikirika...’sauti ikasema
‘Kwani wewe sasa hivi upo wapi., nimeambiwa tutaona hapa..?’
akauliza
‘Nipo wapi hilo sio muhimu, nipo duniani tu,....huwezi
kuniona, hakuna anayeweza kuniona kwa hivi sasa….nilishakufa na ….na sijui kama
nitarudi tena….’akasema
‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza nesi
‘Hapa nilipo huwezi kuniona, na …oh, unaona mitambo yote
haifanyi kazi,hapa naweza kuwasiliana na wewe tu, kweli hawa watu wameniweza,
nimejaribu kila njia, lakini ....mmh, naona sasa muda umefika, nahisi, namuona
ooh mama yule, baba yule…..kuzimu kuleee…hahahaha, nenda, kamalize hiyo kazi...’sauti
ikasema na kukawa na kucheka kwa mda mrefu
‘Unajua mimi nashindwa kukuelewa, kila siku unakuja na
mambo mapya, hebu niambie ukweli, kwani wewe ni nani hasa na hapa kwenye hili
jengo umekuja kufanya nini, kwanini uweze kufika hapa na kufanya kila
ukitakacho kama vile hapa ni kwako,..au kweli wewe ni mhalifu...?’ akauliza
‘Mhalifu,...hahaha, watasema hivyo, lakini kwenye dunia
hii kila mtu ni mhalifu, maana hakuna wema, kama kungelikuwa na wema, aah, basi
sote tungelikwua watakatifu, lakini, wema,..nani mwema hapa duniani hakuna,…..
ubaya ubaya tu,....kila mtu anashindania tumbo lake,au sio, nipate , ni change .....’akasema
‘Hata sikuelewi...’akasema nesi
‘Kama huamini, kwanini kila mtu anataka kupata zaidi ya
mwingine, kungekuwa na wema, mtu akipata kitu, angelipenda kugawana na
mwenzake,..nani anaweza kufanya hivyo, hakuna, kila mtu hatosheki na anataka
kupata zaidi ya mwingine...wema ni ndoto, hakuna kitu kama wema, asikudanganye
mtu,.....unanielewa...’sauti ikasema
‘Kwahiyo unataka kusema nini?’ akauliza
‘Ndio maana na mimi niliona njia ya kupata zaidi...ni,
ni....kujiunga na dunia yangu, kama walivyowenzangu, kila mmoja ana ndoto yake,
ana dunia yake, na mimi dunia yangu ndio hiyo, imeshaundwa na mimi nikajiunga
nayo, na sasa natakiwa niwe nayo, na kama ni kufa basi nife na dunia yangu, kila
mtu akafa na dunia yangu, nimekabidhiwa na mimi ikifika mwisho wangu nitakufa
nayo..’sauti ikasema
‘Umesema mama alikuwa nacho, mama yako ni nani, mbona
sijawahi kumuona, na mbona ulisema aliyeunda hilo wazo la dunia yangu
alishakufa, kwani wewe ndiye mrithi wake, au..?’ akauliza nesi.
‘Mama,mama,...oh usinikumbushe mbali,...mama yangu umeshawahi
kumuona mara nyingi tu...ila ..inasikitisha sana, sijui kwanini ilitokea hivyo,
sijui, ..sasa sikiliza angalia ujumbe kwenye simu yako, pitia hapo kwa muhasibu
atakupa kiasi cha pesa nilichomuagiza, utaondoka nazo hadi sehemu
niliyokuandikia kwenye huo ujumbe, hapo utakutana na huyo kijana....najua
ukimuonyesha pesa tu, atabadilika, pesa, inambadili kila mtu, ana njaa kali, na
tamaa, wewe mwenyewe utamuona,....fanya hilo kwa ajili yetu.’sauti ikasema
‘Lakini mimi sirudi tena huku,....’nesi akasema
‘Hutaki tuonane tena sio..hutaki pesa zako sio, hutaki noto yetu ikamilika sio, unajua nataka
tuwe pamoja hata kama ni huko kwenye dunia isiyojulikana, twende pamoja, kama
kweli unanipenda urudi hapa,tutaondoka pamoja, na dunia itabakia kutukumbuka
tu,....kama hutaki pesa zak o, utajiri, au ndoto yetu itimie, basi, ..mimi
nitajua la kufanya, ,...’sauti ikasema
‘Sasa hata nikija hapa nitakuona wapi , kwani i wewe sasa
hivi upo wapi, hayo makao yako yapo wapi ....?’ akauliza nesi
‘Nenda huko nilipokuagiza, sikuhitaji hapa kwa hivi sasa
nahisi kuna hatari inakuja,..nahisi dunia yangu imevamiwa, ....umesema ulimuacha
wapi Moto,...huyo ni adui yangu,...kwaheri, ila lolote litakalotokea ujua mimi
nakupenda na wewe ulikuwa mtu pekee yake aliyebakia ...sasa nahisi hata wewe
huenda, umeniacha, wewe ondoka,....ondoka haraka, nataka kumaliza kazi,,....’sauti
ikasema na kukawa kimiya
‘Yule nesi akatoka, mle kwenye kile chumba, na akawa
anatembea kwenye corido, kueleekea
kwenye ngazi, na alipokaribia kwenye ngazi, akakutana na Inspecta Moto.
‘Oh, umeshafika,...mimi narudi nyumbani, sitaki tena
kuwepo hapa, naogopa...nakwenda zangu, wala sitaki mambo yenu, naona naingia
hataraini bure, sitaki hata kumsikia huyo mtu tena, basi imetosha.....’akawa
anaongea huku akitembea kwa haraka, na Moto akasema;
‘Wewe fanya kama alivyokuagiza , mengine tuachie sisi,
usijali tupo pamoja....’akasema Inspecta na nesi hakujibu kitu akaingia kwenye lifti
kushuka chini.
Inspecta moto akawasiliana na watu wake, ambao walikuwa
wanafuatilia tukio hilo kwa karibu, na
kila mtu alikuwa tayari kwa lolote lile, alipomaliza kuongea nao, akawapigia
watu wa idara ya mawasiliano, ambao walikuwa wakitafiti simu zote zinatoka na
kuingia kwa huyo nesi , na Inspecta Moto alipouliza;
‘Mumempata huyo mtu yupo eneo gani kwenye hili jengo,
...?’ akauliza
‘Hayupo kwenye vyumba vya hapo chini....’akaambiwa
‘Atakuwa wapi sasai?’ akauliza
‘Yupo juu kabisa summit, alama inaonyesha hivyo....kuna sehemu imejengwa kama chumba kwa kwenda juu,
mawasiliano ya hapo ni magumu, ila kifaa chetu kimenasa sehemu hiyo, inaonekana kumewekewa vifaa vya kuzuia mtu
asigundue, miale ya mawasiliano haipenyi hapo ....’akaambiwa
Inspecta moto, akapiga simu sehem nyingine na kuongea na
watu wake wengine
‘Hao mashahidi hali zao zipoje?’ akauliza, na akaambiwa
kidogo wana nafuu
‘Mwambie huyo mtu wa mawasiliano, huyo shahidi aliyekuwa
mtaalamu wa mawasiliano wa hao watu, ajitahidi aingie kwenye mtandao,
tunamuhitajia sana, hatujui huyo mwendawazimu anafanya nini kwa hivi sasa,
ajitahidi mpaka aweza kuingie kwenye mitandao yake, kwa vile yeye ndio kaibuni
, ni lazima atajua jinsi gani ya kuweza kuiingia huko ...’akasema
‘Ina maana aje huko?’ akauliza huyo mtu
‘Hapana sio lazima yeye kuja huku, akiwa hapo, akipata
vifaa vyake ataweza kuwa sambamba na huyo mwendawazimu, atadhibiti mawasiliano
yake yote na kujua kitu gani anachokifanya, hatujui kwa hivi sasa huyu mtu ana
lengo gani....’akasema Moto.
‘Sawa, ngoja niongee naye , vifaa vyake tumeshavileta,
sasa hatujui kama akili yake itaweza kufikiria vyema maana bado wapo kama
walevi-walevi, docta kasema hali hiyo itachukua muda, sijui kama na y eye
anafanya hivyo kuchelewesha au ni kweli...’akasema
‘Muiteni yule mzee wa tiba mbadala,..yule aliyenitibia
mimi, ataweza kulimaliza hilo tatizo, ....’akasema Moto.
‘Sawa ngoja tumtafute, nasikia alikuwa hapa mjini, ngoja
tuone yupo wapi....’akasema huyo mtu wake.
Inspecta moto alipomaliza kuwasilana na watu wake, akawageukia
makomandoo wake aliokuwa nao, akawaambia;
‘Sasa mimi na askari wawili, tutatangulia kwenda juu,
wengine msubiri, maagizo,...’akasema
‘Mkuu hiyo kazi ungetuachia sisi...’akasema mojawapo
‘Hapana, ni lazima nionane na huyo mtu ana kwa ana,
nataka kuwa na uhakika kama ni
yeye, ni mjanja sana huyu mtu,....’akasema Moto
‘Ina maana tunaweza tukamkuta mtu ambaye sio yeye....?’
akauliza mwingine.
‘Yote yawezekana kwa hawa watu yote yawezkena, maana
hata mimi hapa sijamelewa vyema, kauli yake alipokuwa akiongea na nesi
inanichanganya, ngoja tutaona, huona hisia zangu za awli ni kweli,..twendeni....’akasema
na wakaanza kazi ya kwenda juu na askari wawili
‘Tupo pamoja mkuu...’akasema mmoja wa askari wake,
waliokuwa wakisubiria amri.
‘Hata hivyo muwe makini, japokuwa hakuna mawasiliano
yake na watu wengine, lakini hatuwezi kujua, huenda bado kuna watu wake wapo
kwenye jengo wanamsaidia...kuna huyo aliyemchukua nesi na kumuelekeza wapi pa
kwenda, mkamateni,, na hakikisheni hana mawasiliano na huyo mtu tena, vyumba
vyote vikagueni, kuona kama kuna watu wake, na hakikisheni hakuna mawasiliano
tena kutoka juu....’akasema Moto
Moto akatoka na kuelekea huko juu summit, akiwa na hao askari wawili anaowaamini- makomandoo.
WAZO LA LEO: Amani, upendo, hujengwa kuanzia utotoni, malezi bora ya watoto wetu, elimu safi, na huduma bora kwa watoto wetu, ndio chanzo kizuri cha jamii yenye muelekeo mwema, jamii yenye mendeleo na amani. Tusipoangalia chanzo hiki muhimu, tukaangalia ubinafsi wa kuendeleza wangu tu, tukapuuzia watoto wengine, tukiwa tumepewa majukumu hayo, tujue kuwa tunajenga jamii itakayokuja kuishi kwa shida,...hata kama tumejizungushia uzio wa umeme, .... ghasi na amani itakuwa ni kitendawili. Tukumbuke hili, Jamii njema inategemea malezi mema ya watoto wetu, elimu na huduma safi kwa watoto wote.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment