Inspecta Moto, alipotoka
mahakamani moja kwa moja alielekea huko hospitalini alipokuwa kalazwa mkuu wake
wa kazi,..akilini akitaka kujua jinsi gani huyo mtu aliweza kutoroka hapo
hospitalini,
Iliitwa kutoroka
kwasababu taarifa iliwafikia walinzi wa hapo, na wao hawakuona akitoka, na mkuu
huyo hakutoa taarifa kuwa anatoka, kwahiyo moja kwa moja ikachukuliwa kuwa
ametoroka…ni kwanini alitoroka, ikabakia swali kwa watu.
Inspecta Moto, akaanza
kuunganisha matukio, akaanza kumshuku mkuu huyo, lakini bado alikuwa hana
uhakika na hicho anachokiwaza, kwahiyo alipofika hospitalini pamoja na kutaka
kujua jinsi gani huyo mkuu alitoroka, lakini pia alitaka kumfahamu vyema mkuu
wake kutokana na kupenda kuja kutibiwa hapo ambapo kuna shahidi muhimu ambaye
anahusika na kundi haramu
Swali, ni wapi mtu huyo
amekimbilia,….
Inspecta Moto alipozidi
kumbana huyo nesi, akajikuta anaanza kupata fununu, kuwa huyo nesi anaweza
kujua mengi zaidi ya hayo aliyokuwa akiyawazia yeye, kwahiyo akaona amtumie
huyo huyo nesi, na huenda akawa ni njia ya kumpata mkuu huyo;
‘Kwanini mkuu wake
akatoroka hospitalini, kwanini alipenda kutibiwa hapo, na kama alipenda
kutibiwa hapo, basi watu wa humo wanamfahamu vyema, je kuna nini kati ya mkuu
huyo na kundi haramu,…’
Akazidi kumchimba yule
nesi, kwa kumuuliza maswali
Endelea na kisa chetu.
************
‘Kwani wewe
unanishuku nini mimi, mpaka unifanyie hayo yote, yaonekana kama unanishuku mimi
kitu fulani, nimekosa nini, naomba uniweke wazi , ili kama ni kumtafuta wakili
wangu nifanye hivyo, unanitia mashaka, nina kosa gani….?’
‘Nesi, kwenye kumbukumbu
za matukio, inaonekana wewe uliingia kwenye chumba cha vifaa vya kunasia
matukio, hebu niambie ulifuta nini huko?’ Inspecta hakujali hayo malalamika
akamuuliza huyo nesi hilo swali, na nesi akashtuka, na kusema;
‘Mimi, nani kasema....?’
akauliza akimuangalia Inspecta kwa macho makubwa
‘Sio nani kasema,
mitambo inaonyesha hivyo, ulionekana ukiingia kwenye chumba cha mawasiliano,
na kutoka kwa haraka, je ulifuata nini?’ akauliza inspecta Moto kwa mtego,
moyoni akisema uwongo mwingine unaweza kusaidia,
Aliwaza hivyo, akijua
kule kwenye kumbukumbu, hakuona tukio hilo la huyo nesi kuingia huko, lakini
moyoni alishahisi kuwa huenda ni yeye aliyeingia huko au docta msaidizi kwani
wao ndio wenye nafasi ya kuingia huko.
Alipomuona huyo nesi
akishituka, akajua keshampata. Huyo nesi akamuangalia Moto, kwa macho makubwa,
akionyesha kushitushwa na swali hilo, halafu kwa haraka akajibadili kuonyesha
hakuna kitu, akasema;
‘Nilikwenda mara moja
kumuangalia mlinzi, nikitaka kumuambia awe makini maana mgonjwa anaweza kuleta
matatizo...’akasema
‘Kwahiyo uliingia chumba
hicho, ….?’ Akaulizwa inspecta akijua sasa keshampata huyo nesi
‘Wewe si umesema
uliniona…wewe…..kwanini unanitega?’ akauliza kwa kubabaika.
‘Unasema wewe ulikwenda
kumona huyo mlinzi, au sio, ili kumuambia mlinzi awe makini, ni kawaida yenu
kufanya hivyo ikitokea jambo kama hilo….?’ Akauliza huku moyoni akisema `
'Nilitaka kuwa na
uhakika kuwa kweli uliingia humo, na sasa nimekupata’.
‘Ndio...ni kawaida,
....mmh unafahamu mimi ni nesi mkuu, mmoja wa viongozi, na moja ya wajibu wangu
ni kushirikiana na viongozi wote, na siku hiyo, kiongozi aliyekuwepo, kuachia msaidizi
wa docta, ambaye kwa muda huo alikwenda kumuona mgonjwa, nikabakia mimi
kuhakikisha hali ipo shwari, kwahiyo ilibidi niwajibike kwa jinsi
nilivyoweza….’akajitetea
‘Kwahiyo ikitokea tatizo
cha kwanza kufanya ni kuwsiliana na walinzi wa mawasiliano, ..?’ akauliza tena
Moto na nesi akaonekana kukerwa na swali hilo, kwanza alikaa kimia na alipoona
Moto anasubiri jibu akasema;
‘Sijui hunielewi, au
huniamini….unaweza kufanya hivyo kutegemeana a tukio, siwezi kusema kuna sheria
kama hiyo, inatokea mtu kuaona ni kitu gani ufanye kwa wakati gani, ni hivyo
tu.....’akasema
‘Ok, ..au nikuulize
hivi, siku hiyo kulikuwa na walinzi wengine nje….ambao wanalinda usalama , na
kulikuwa na mlinzi pale karibu na mkuu alipokuwa akihudumiwa, kwanini
hukuwaambia wao kwanza, wewe ukakimbilia kuongea na huyu mtu wa mitambo?’
akauliza moto
‘Nilitaka kuongea na
huyo wa mawasiliano maana yeye angeliweza kuona kila mahali… labda nisema
hivyo, hata hivyo, sikuwa nimetarajia kutokea kitu kama hicho, ndio maana
sikuona umuhimu wa kuwaambia polisi’akasema nesi kwa kujiamini.
‘Lakini maelezo yako
awali umesema ulikwenda kumuona huyu mtu wa mawasiliano, kuwa mgonjwa,
anasumbua, huenda akaleta matatizo, hapo umehisi tatizo, na watu wazuri wa
kusaidia kwa muda huo, mimi niliona ni polisi, ambao walikuwa hapo kwa ajili ya
mkuu wao, au sio…nimelewa hivyo,….’akasema moto.
‘Sawa elewa unavyopenda
na mimi nilifanya kilichoinjia akilini kwa muda, kama ilitakiwa iwe hivyo, basi
imeshafanyika nifanyeje tena..’akasema
‘Ulipofika ulimkuta huyo
mlinzi?’ akaulizwa
‘Hakuwepo...alikuwa
katoka....’akasema
‘Ulijuaje kuwa katoka,
yaani uligonga mlango kwanza, au uliingia ndani kwanza?’ akaulizwa
‘Yote mawili
yalifanyika..niligonga , nilipoona kimia nikafungua, mimi naweza kufungua na
kuingia, nilitaka kuhakikisha kuwa kweli hayupo, maana mtu unaweza kupitiwa na
usingizi,…’akasema
‘Ulipoingia, hukukuta
mtu, ulifanya nini?’ akauliza
‘Nilitizama mitambo,
kuona usalama, ….na, nilishangaa kuona mitambo haifanyi kazi,….’akasema
‘Ulikuta mitambo
haifanyi kazi, au ilizimika hu mtambo?’ akauliza
‘Nilikuta haufanyi kazi,
umezimika kabisa….’akasema akionyesha wasiwasi
‘Ukachukua hata gani?’
akaulizwa
‘Mhh, unajua
nilihitajika kujua kinachoendelea huko kwa mgonjwa, kwahiyo nikakimbilia huko,
nikijua wenyewe wakifika, watajua cha kufanya, mara nyingi inatokea hivyo, unajizima,na
wao wenyewe wanajua jinsi ya kufanya, nilijua katoka kwasababu hiyo ya
kuhangaikia, uwake, inatokea ni kawaida
tu ….’akasema
‘Hukuulizwa kama
uliingia humo, na walinzi baadaye?’ akaulizwa
‘Mhh, kama
nilivyokuambia kulikuwa na mambo mengi yametokea muda huo kwa wakati mfupi,
nakumbuka kama niliulizwa kitu kama hicho, na sijui niliwajibu vipi, nilikuwa
nimezongwa na mambo mengi, maana kwa kipindi hicho ndio nimegundua mgonjwa
hayupo, na msaidizi wa docta ana hali mbaya ….unaonaeeeh, kwahiyo huenda
niliwajibu sivyo ndivyo, hata siwezi kukumbuka,….’akasema.
‘Hebu kumbuka vizuri, Wakati
unaingia hukugusa waya, …inaonekana kuna waya ulikuwa umechomolewa, na wewe
ndiye uliyeingia, na mlinzi anasema alitoka na kuacha kila kitu kipo sawa, je
hukuchomoa, au kugusa waya?’ akaulizwa.
‘Waya gani , mbona
sikuelewi....?’ akasema nesi kwa sauti ya kushangaa huku akiwa katoa jicho,
kama kukasirikika au kutishia.
‘Unaniuliza mimi waya
gani, unafahamu vyema huo waya ni waya gani, nesi,….unajua tusizunguke, kwenye
huo mitambo kunaonyesha kila kitu,..hata kama waya ulitolewa, lakini kuna jinsi
nyingine ya kuonyesha matukio,…kuna waya wa akiba unaofanyakazi kukitokea
hitilafu, unalifahamu hilo…?’ akauliza.
‘Waya wa akiba! Waya
gani huo wa akiba mbona mimi sijawahi kuuona, lakini mimi sijui zaidi mambo ya
huko, waulize wenyewe….’akasema akiwa na mashaka.
‘Kuna waya wa akiba,
unaoweza kufanya kazi hata kama waya mkuu umechomolewa, na tukaufanyia kazi,
tukaona wewe, ukifuta kumbukumbu za siku, halafu ukichomoa huo waya na komputa
ikazima,ungekuwa mjanja wewe ungefuta tu, na kuzuia, kumbukumbu zisipokelewe,
sasa ujanja mwingi umekuumbua, unajua hilo ulilofanya ni kosa kubwa
sana…..’akasema Moto akitaka kumaliza malumbano.
‘Mimi sijui
lolote,na sikuelewi unachoongea, ina maana umekuja hapa kunishutumu,
kunisingizia mambo ambayo siyajui, mbona sijasikia walinzi wakisema kuna
waya ulichomoka,...na kwanini nichomoe huo waya, kwanza waya gani
unaozungumzia,ujue mimi ni kiongozi, siwezi kufanya kitu kama hicho….’akasema
lakini sauti ilionyesha kushindwa.
‘Utaona kila kitu mahakamani,...tutaonyesha
kama ushahidi, na wewe utashitakiwa kwa kumsaidia mhalifu, kwa
kufanya mgonjwa atoroke, na hujui ni kitu gani kimempata huko
alipokwenda…’akasema Moto, na nesi macho yakaanza kulenga lenga machozi.
‘Nesi wewe ni mrembo,
hebu fikiria uingie jela, wakuone hivyo, hebu mateso ya jela, na ukumbuke kama
utaficha ukweli, kuna mteso makubwa utakumbana nayo ili useme ukweli wote,
unaweza kuteswa kwa waya wa umeme, au ufungiwe kwenye chumba chenye nyoka, upo
tayari kuzalilika, ni bora uongee na mimi nijua jinsi gani ya
kukusaidia….’akasema Moto.
‘Chumba cha nyoka, mungu
wangu, hapana, hamuwezi kufanya hivyo, nyoka, hapana, ninavyogopa
nyoka…..’akasema sasa akionyesha woga
‘Ndio hivyo, mimi sitaki
hayo yakukute, lakini nikishindwa, na kwa vile ukweli mimi ninao, nitawaachia
wahusika wakushughulikie,…wakichka utarudishwa kwangu, najua hapo utasema kila
kitu…’akasema Moto
‘Kwanini unanisingizia
kitu ambacho sijafanya, mimi nimechoka, nahitaji kwenda kupumzika, kwanza
umeshaniharibia kabisa siku yangu, kwani kuna nini kikubwa kimetokea, na kama
unanishutumu kwa hilo, nitatafuta wakili wangu, naona sasa siongei tena….!’
Akasema akikunja uso kwa hasira.
‘Mpendwa, mitambo
inaonyesha kila kitu au unataka nikuonyesha,…’akasema Moto, kama
vile anatafuta kwenye simu yake ili amuonyeshe jinsi ilivyokuwa na nesi akawa
anamuangalia kwa mashaka.
‘Kwani hiyo simu yako
inaonyesha matukio yaliyotokea kwenye Mitambo yetu...?’ akauliza
‘Hii mitambo yenu
pia ina mawasiliano na vituo vyetu vya usalama, kila tukio likitokea huku,
inanakiliwa kwenye kituo chetu cha usalama kikubwa, kwahiyo moja kwa
moja, kila kinachotokea humu kinaonekana huko kwetu, tumekuona jinsi ulivyotoka
wodini, ukaingia ndani ya hicho chumba.....ukafanya jambo kwenye komputa, ukachomoa
waya , halafu ukarudi chumba chako cha mapumziko…kila kitu kipo wazi,….’akasema
Moto, akijua hapo anaweza kumpata.
‘Mimi nakubali kuwa kweli
nilikwenda hicho chumba, ….lakini ….sikuchomoa waya....hilo
unanisingizia....kwanza waya gani, ni ule uliokuwa na matatizo, kama ni ule
huwa uanachomoka wenyewe, huenda wakati naingia ulichomoka kwa bahati
mbaya....’akatulia.
‘Swali ni kwanini
ulichomoa huo waya…nijibu vyema mpendwa, maana umeonekana kwenye hiyo
mitambo…haikuwa Bahati mbaya, ulifanya makusudi,sasa swali ni kwanini ulichomoa
huo waya?’ akaulizwa.
‘Nani kasema nilichomoa
huo waya, kwanza waya gani?’ akasema akionyesha kama kuchanganyikiwa.
‘Tatizo lako unasahau
kuwa japokuwa ulichomoa huo waya, lakini tukio la mwisho hapa kwenye mitambo
yenu, achilia huko kwetu ambapo tuliona kila kitu, hapa kwenu inaonyesha
wewe uliingia kwenye hicho chumba, ukakuta mlinzi hayupo, na mlinzi aliporudi akakuta
waya umechomolewa, na mtu aliyeingia humo ndani wakati yeye hayupo ni wewe,
hakuna mwingine zaidi yako, sasa utakataa vipi kitu ambacho kipo
wazi....’akaambiwa na hapo nesi akatulia na Moto akajua sasa
keshamfikisha kwenyewe, na nesi sasa machozi yakaanza kumlenga
lenga, akasema;
‘Sijasema mimi
sijaingia, ....niliingia, lakini....’akasita.
‘Sasa nakupa nafasi ya
mwisho,....usiposema ukweli, mimi na wewe mguu kwa mguu hadi kituo cha polisi, unashitakiwa
kwa kuvuruga mitambao ya usalama, utashikiliwa kama mtuhumiwa, uliyesaidia
mhalifu kutoroka,na ukumbuke mateso, kuingizwa chumba cha nyoka uchi,
...’akaambiwa, nesi hapo akaonekana kuogopa, akasema;
‘Kwani huyo mgonjwa ni
mhalafu,....mimi huyo mgonjwa aliniomba nimsaidie, sikujua kuwa ni mhalifu,,…
alisema yeye anataka kutoka hapo hospitalini kuna kitu chake anafuatilia,
lakini anaogopa akitoka ataonekana,...akaniomba nimsaidie akimaliza
atarudi, na atanilipa pesa nyingi, na mimi nikakubali, sikujua kuwa ni
mhalifu...’akasema na Inspecta moyoni, akasema `bado hujafunguka vyema,
umetunga tunga habari, mimi sikuachilii…’
‘Na inavyoonyesha kule
hiyo sio mara yako ya kwanza kumfanyia hivyo, tulikuwa tukijiuliza kwanini
unamfanya hivyo huyo mgonjwa,…ni kweli au si kweli?’ akaulizwa na nesi
akatikisa kichwa kukubali.
‘Kwahiyo hilo la
kuhangaika na kujipiga piga, mlitunga uwongo, wewe na yeye?’ akaulizwa.
‘Hapana hiyo inamtokea
ana matatizo kama hayo kweli anaumwa,hata ungelikuwepo wewe ungejua kabisa
anaumwa,ndio maana mimi nikamuonea huruma ....’akasema
‘Hebu niambie , huyo
mgonjwa aliwezaje kutoka na alitokea mlango gani?’ akaulizwa
‘Alivaa nguo zangu za
unesi..kwahiyo walinzi walijua ni mimi natoka,,..ndio maana hakuna
aliyemshitukia....huwa mimi nikitoka, navaa mawani meusi,..na naendesha
pikipiki, na yeye alifanya hivyo hivyo....alichukua pikipiki yangu...’akasema
na Inspecta moyoni akajipongeza, akisema ;`sasa kazi imekwisha, kumbe ni
mshirika wa kweli…’
‘Alielekea wapi?’
akaulizwa
‘Hapo sijui, ila alisema
atarudi...’akasema
‘Wewe na yeye ni
marafiki wa muda mrefu au sio?’ akaulizwa
‘Hapana nimejuana naye
humu humu hospitalini...’akasema na inspecta akatoka simu yake, na kumuonyesha
picha, picha hiyo ilionyesha nesi huyo akiwa kwenye hoteli wakila chakula na
huyo mkuu
‘Hapa inaonyesha wazi
kuwa wewe na mkuu mna mafungamano , au urafiki wa karibu, sio kweli kuwa
mlijuana humu humu hospitalini, sisi tunafahamu, tuanwafahamu, hapa nakupima tu
ili useme ukweli, ikibidi nijue jinsi gani ya kukusaidia, lakini naona hubebeki,
..’akasema Moto.
‘Sasa nimekuamia ukweli,
naomba unisaidie, tafadhali….naogopa nyoka, naogopa kufungwa, nisaidie,
nitakuambia kila kitu…..’akasema sasa akipiga magoti.
‘Nesi niambie ukweli,….
unapoteza muda wangu, na huyu mtu akipotea, wewe ndiye tutakushika, na kumbuka
nyoka, ukiwa uchi, sema kila kitu huyo mtu apatikane na wewe uwe salama
....’akasema moto kwa ukali..
‘Atakuwa kaenda hoteli
ya Paradise...’akasema
‘Kwanini unasema kaenda
huko?’ akauliza Moto kwa ukali zaidi huku akianza kutafuta namba kwenye simu
yake, na kutuma ujumbe
‘Aliniambia tutakutana
huko...’akasema Nesi sasa akitaka kulia
‘Chumba gani…. ?’
akaulizwa Moto, akiwa keshaweka imu sikioni, akili sasa ikianza kuwazia jambo
jingine, akijua hapo kazi imekwisha sasa anaingia kwenye mapambano ya mwisho.
NB: Tuendelee…..hapana
tusubirie sehemu muhimu, ambao inaweza ikawa hitimisho
WAZO LA LEO: Kuficha muhalifu uliye na uhakika naye, ni
sawa na kuficha nyoka mwenye sumu ambaye ipo siku atakugeukia. Mtu mwenye tabia
ya uhalifu, ni mgonjwa, anahitajia kutibiwa, na kuna watu wanajua jinsi gani ya
kuwasaidia hao watu, tusiwafiche, tukawatetea wakitenda uhalifu kama kweli
tunahitajia wapone.
Na mara nyingi uhalifu
tunautengeneza sisi wenyewe, kwa jinsi gani tunavyowalea watoto wetu, hatuwi
karibu na watoto wetu, tukajua shida zao, elimu inakuwa ni gharama, na tunaona
ujinga ni bora, watoto hawa wanaanza kuiga,kuingia kwenye makundi ,
wanaharibiwa, na mwisho wake wanakuwa wahalifu kweli. Tuwajibike kwa watoto
wetu, tukiweka kipaumbele cha elimu, gharama nzuri kwa mtoto ni elimu.
No comments :
Post a Comment