‘Kile kisu kilipopokelewa na yule mtoto, mwili
wote ulianza kusisimukwa,..’ alianza kunisimulia mpelelezi kuhusu chimbuko la
dunia yangu.
‘Na hadi kufikia kumpa huyo mtoto hicho kisu ilikuwa
ni baada ya juhudi kubwa sana ya kwani ilikuwa kama kuna mtu anamzuia yule baba
asiweze kufanya hivyo, na ilikuwa ni lazima huyo baba afanikishe hilo, kwani
kuna mambo ya utangulizi alishayafanya, na hapo ilikuwa ni hitimisho.
‘Baba huyo alitakiwa kukabidhi majukumu na
utaratibu mzima kwa huyo mtoto, kutokana na ile hali ya ugumu wa kulifanya
hilo, yule mzee alihisihuenda mtoto wake huyo alikuwa akikiogopa kukishika kile
kisu.
‘Japokuwa mtoto huyo alijengwa, alifundishwa na
kulelewa kijasiri, ikitambulikana kuwa ndiye atakayeshika hatamu za familia
hiyo, kwahiyo hakuwa muoga, na asingeliweza kuogopa kitu kama hicho, sasa
kwanini hali ile itokee, mzee akawa anajiuliza, kwanini kitu kidogo, kisu tu
kimuogopeshe yule mtoto(kijana)
Hata hivyo yule mzee ambaye kwa muda huo
alikuwa kalala kitandani, sio kulala kwa moja kwa moja, hapana, alikuwa kalala
huku kaegemea mtu, kwahiyo alilala nusu na nusu huku mto aliolalia ukiwa
umeweka sehemu ya mgongo na kumfanya awe kakaa nusu na nusu kalala...
Baba yule pale hakuweza kusema kitu,
alichofanya ni kujitahidi kumuashiria yule mtoto asogee ili aweze kumkabidhi
hicho kisu mkononi, hapo hakukutakiwa kutamkwa neno zaidi ya yale maneno ya
kukabidhi majukumu, kauli hapo sio muhimu, cha muhimu ni vitendo, ndio maana ya
kutokuongea hapo.
Baba yule alikuwa ameanza kuumwa, na ilifikia
hatua hakuweza kutoka nje, akawa mtu wa kitandani, na ndipo siku moja akaota
kuwa muda umefika kukikabidhi hicho kisu kwa mrithi wake, na mara ya kwanza
alipuuzia, lakini alipoona hali inazidi kuwamba mbaya, ndipo akamuambia mkewe,
kuwa wakati umefika way eye kutoa majukumu yake kwa mrithi wake.
‘Kwahiyo unataka kumpa nani hayo majukumu?’
akauliza mkewe
‘Hilo swali la kuniuliza mke wangu, mwenyewe
uliona juhudi zangu kwa mtoto wetu huyu tunayeishi naye, wengine wamekuwa mbali
na mimi, huyu ndiye ninayeona anafaa kushika hatamu za kifamilia...’mzee
akasema na yule mama akatabasamu na kusema
‘Mambo si hayo, nahisi muda sas amefika, haki
ichukue mkondo wake, na mimi roho yangu itulizwe,..nilikuwa naliombea sana hilo
lija kutokea, lakini nilikuwa naona linachelewa...’akasema mkewe na mume mtu
akamuangalia mkewe akijiuliza ana maana gani, lakini hakuweza kupata muda wa
kumdadisi maana dakitari alishafika, na kuendelea na matibabu ya kumpima na
kumfanyia mazoezi ya viuongo, baada ya hapo, mze yule akamuita mtoto wake.
Mtoto wake alipofika, alionyesha adabu zote,
halafu, akawa kama ana jambo anataka kumuambia baba yake, lakini baba yake
akamuashiria kuwa huo sio muda wa kuongea.
Mzee akajitutumua na kuweka mto vyema, na akawa
sasa kalala mtindo wa kukaa, ili aweze kumuona mtoto wake vyema, wakaangalia
kwa muda, halafu baba akachukua ala ya kisu iliyokuwa pembeni mwake, ala hiyo
huwa haachani nayo,..
Mzee akaifungua ile ala, na kukichomoa kile
kisi kwenye ala yake, akakishikilia mkononi, kilikuwa kisu cha kawaida,
ukikiona juu juu, lakini kiimani zao ni zaidi ya kisu, kilikuwa kinameta meta
kwa weupe na makali yake yalikuwa sawia,...mzee akakitembeza mkononi, halafu
akakishikia mfano wa mtu anayetaka kumchoma mtu mwingine, akakiashiria mara tatu,
kama vile anachoma kitu..
‘Baadaye yule mzee, akashika kwenye makali, na
kule kwenye mpini akaelekeza kwa mtoto wake, akitaka, mtoto huyo akishike..pale
ndipo mambo yalipoanza..
‘Baba mtu mkono ukawa unatetemeka, kukawa na ni
kitu kinamrudisha mkono wake nyuma,...lakini baba mtu akihisi labda ni kutokana
na kuumwa, yeye akaendelea na taratibu za kutamka yake maneno ya kujitoa kwenye
majukumu na kumkabidhi mtoto wake majukumu hayo, ni maneni ambayo mzee hakuweza
kuyasahau hadi muda huo toka alipokabidhiwa kisu hicho akiwa mdogo hadi umri
huo wa uzee...
Ilitokea nguvu ya ajabu ikawa inautetemesha
mkono wa yule baba, na mkono ukawa kama unavutwa nyuma, kwa muda ule hakutakiwa
kusema neno jingine, ni yale yale maneno ya kukabidhi kisu kwa mtoto, lakini
mtoto alikuwa mbali kidogo na uwezo wa mkono wake ulikuwa umeshindwa, mkono
ulikuwa mnzito kusogea na ulikuwa kama unavutwa kurudi nyuma, na mzee akawa
anajitahidi kumuashiria mtoto asogee karibu akipokee kile kisu, lakini mtoto
alikuwa akimuangalia baba yake kwa uso wa mshangao.
Mtoto yule alikuwa kama yupo mbali kabisa,
mawazo yake hayakuwepo hapo, kitu ambacho kilimfanya baba atake kutamka neno la
ukali, au kumuashiria asogee karibu,lakini hakutakiwa kusema neno, angeliharibu
taratibu za hilo zoezi, na yule mtoto hakuweza kuiona ile hali kwa mtoto wake,
mtoto alikuwa amekaa pale pale, uso wake ukiwa umejaa kitu kama mshangao, kama
vile anaona kitu kingine cha ajabu kutoka kwa baba yake!
‘Hata hivyo yule baab hakukata tamaa, akajitahidi,akijua
huenda ni moja ya changamoto, za hayo makabidhiano, na huenda alitakiwa kufanya
juhudi kuonyesha dhamira ya kweli, ya kuyatoa hayo mamlaka kwa mtoto huyo.
Juhudi zake baadaye zikazaa matunda, yule mtoto
naye aliona kile kisu kikiwa mkononi mwa baba yake kwa muda mrefu, na baba
anahangaika, akataka kuinua mkono wake, ili akipokee, na hapo napo ikawa ni
maajabu mengine, maana ule mkono wa yule mtoto ukawa kama unatetemeka, na mtoto
alionekana kupambana na kitu kilichokuwa kikimvuta mkono wa yule mtoto ili
asifikie kile kisu, lakini mtoto naye akawa anajitutumua, akikumbuka mazoezi ya
baba yake ya kutokukubali kushindwa, akajitahidi
kunyosha mkono kukipokea kile kisu....
Yule mtoto hatimaye mkono wake ukaweza kushika
eneo la mpini wa kile kisu, ghafla sura ya yule mtoto ilibadilika..hili mzee
aliliona akilini, sio kwamba kweli sura ya yule mtoto ilibadilika, hapana, ni
kama hali ya kumbukumbu ya taswira ikaonyesha hivyo, ni kama akili kufunguka na
kukumbuka sura ambayo licha alizoea kuiona lakini sura ile ikawa inamkumbusha
jambo, mzee akahisi labda ni kuchanganyikiwa kwa akili
Na muda ule ule wakati kisi kimeshashikwa na
mtoto,kwenye mpini na baba kashika kwenye makali, mzee aliona kisu kile kama
kinabadilika rangi, kutoka kwenye weupe wake, na kuanza kutapakaa rangi
nyekundu, rangi ya damu, kilianza kidogo kidogo kutoka kule aliposhikilia mtoto
na kuja hadi kwenye ncha ambayo baba alikuwa bado kaishikilia, na hapo
akakumbuka kauli ya babu yake...
‘Kisu
hiki ni kisafi, na usafi wake ni ishara ya utakatifu, na kinatakiwa muda wote
kiwe hivyo, na hali ikiwa shwari, haki ikitendeka, na kukawa hakuna uvunjifu
mkubwa wa amani, kisu hiki kitabakia hivi hivi, kitaashiria, upendo na amani kuendelea
kuwepo, na ilivyo kinatakiwa kiwe hivyo wakati wote, kisibadilike rangi yake,
hakikisha unakitunza, na kutunza mila na desturi zetu....’ilikuwa sauti ya
babu
‘Kisu hiki kinaweza kubadilika rangi, kiabdilike
rangi chenyewe...?’ nikauliza kwa udadisi.
‘Ndio
lakini ni pale ukikosea masharti, na kawaida dalili hizo huanzia mwanzoni pale
mrithi anayechukua hayo mamlaka anapokuwa anamkabidhi mtu mwingine asiyefaa, au
huyo aliyekichukua akawa anafanya mabaya,...ndio maana mtawala wa kipindi hicho
anatakiwa kuwa makini, awe na uadilifu, amlee huyo anayehisi ni mrithi wake
katika maadili mema, kwani kiongozi mwema huanzia utotoni ...’akasema babu
Yule mzee alianza kuwaza pale pale, kwa
kujiuliza nimekosea nini, maana kiukweli mtoto huyo nilimlea vyema kabisa na
kuonyesha dalili zote za mtoto mwema, hakuwahi kufanya mabaya ya kuiaibisha
familia, na kama alikosea ni makosa madogo madogo ya kiutoto na sasa kafikia
ujana, na kuwa kijana jasiri....sasa hili linalotokea hapa lina maana gani
Wakati anajiuliza hayo kichwa chake kikawa kama
kimefunguka, na hisia fulani zikamjia akilini mwakeu, yule mtoto ambaye sasa
alikuwa kashikilia kile kisu, akiwa anahangaika nacho kukishika vyema na wakati
huo mkono wa yule mtoto ukawa unaonyesha maajabu mengine,ule mkono ukatuna kama
le mikono ya wainua vyuma, kuashiria kuwa kashika kitu kizito sana, asichoweza
kukihimili, lakini akawa akijitahidi kukishikilia
Na muda ule mzee aliona kisu chote kikiwa
chekundu, ...damu, ishara ya damu, ishara mbaya...
Yule mtoto kwa juhudi kubwa akawa kakishikilia
vyema sasa kile kisu mikononi mwake, na kwa zile juhudi.Baba mkono wake
ukabakia mtupu, lakini baba alikuwa akimuangalia yule mtoto kwa uso wa
mshangao, kwanza kijana yule hakuwa na mwili bado wa kuwa na misuli yenye nguvu
kiasi hicho, maana mkono ulituna na misuli ukaonekana imejipanga
mkononi,...mzee akajipa moyo kuwa huenda ndivyo ilitakiwa iwe, japokuwa kwake
haikuwahi kutokea hivyo.
Mzee yule aliendelea kumuangalia yule mtoto
wake usoni, na wakati huo akili ilikuwa kama imemfunguka kumuelezea jambo...na
sasa sura aliyoiona sio sura ile aliyoizoe,japokuwa ni sura ile ile, alihisi
kama kaona sura ambayo hakuwa ameifikiria kabla,na sura hiyo ikamkumbusha jambo...
‘Sura ya mtoto huyu mbona sasa naiona inafanana
kama mtu niliyewahi kumjua, ni sura ya...’hapo akahisi kitu kikichoma kwenye
moyo wake, na kuhisi mwili ukiwa kama umekufa ganzi upande wote wa kushoto,
lakini akili ilikuwa vile vile ikiwaza, na kujikumbusha
Ilikuwa ni sura ya mtu mzima, sura ya mtu
aliyewahi kumfahamu, japokuwa sasa ni marehemu..., sura ya aliyekuwa mpinzani
wake, mpinzani wake toka utotoni hadi pale alipomshinda na kuweza kumpata mama
wa mtoto huyu...
‘Mhh mbona hili sikuwahi kuliona kabla, mbona
sura hii naiona sasa kama ngeni kwangu, mbona mtoto huyu nimekuwa naye wakati
wote lakini sikuwa kufikiria hivyo...’yule baba mtu akawa akiwaza, na hapo
akasikia sauti ikisema akilini mwake, ni sauti ya aliyekuwa babu yake, pale
alipogundua sura ya mtoto wake, na kumfananisha na huyo marehemu, sauti ile ya
babu ilisema;
‘Kisu hiki
ni cha urithi wa kimila, na anayestahili kukipokea ni mmoja wa damu ya familia,
na ilivyo ni kuwa baba anatakiwa kumkabidhi mtoto wake anayestahiki,mtoto huyo
awe ni damu yake,na awe amemzaa huyo mtoto ndani ya ndoa halali kwani kisu hiki
kinajulikana kama kisu kitakatifu cha kimila...’sauti ya babu yake ikasikika ikisema akilini mwa huyo
baba mtu.
‘Oh, sasa itakuwaje, maana ishara niliyoiona
hapa ni kuwa huyu mtoto sio damu yangu,..lakini haiwezekani, maana nimeishi na
mtoto huyu tangia akiwa mchanga, sikuwahi kuhisi sura hii kabla, sikuwahi
kumafananisha na huyo aliyekuwa adui yangu, sikuwahi kusikia mtu akisema mtoto
huyu anafanana na huyo marehemu, sasa leo imekuwaje, na hapo sauti ya babu
ikaendelea kusema;
‘Kama
ukimkabidhi mtu ambaye sio damu ya familia hii, mtu ambaye hastahiki, ujue ni
lazima kuna baya litatokea, na baya hilo litaanzia kwako, na hali hiyo
isipozuiwa na mtu wa familia haraka iwezekanavyo, basi kutazuka balaa, na balaa
hilo litakwenda mbali zaidi...uwe makini kwani tumekuwa makini kizazi hadi
kizazi,...’akakumbuka alivyoambiwa
Baba mtu
alipoiona ile ishara, ishara ya sura ya mtoto wake, akifanana kabisa na
mpinzani wake, kitu ambacho katika maisha yake, katika malezi yake, hakuwa
amekigundua hicho, mwili wote ukawa hauna nguvu, aheri mkewe angelikuwepo hapo
akamuuliza, lakini mkewe hakutakiwa awepo hapo akifanya hilo jambo, ni jambo
kati ya baba au babu na anayestahiki kukabidhiwa jukumu hilo...
Baba mtu akamtupia mtoto wake jicho jingine,
sasa likuwa jicho la uwoga, wasiwasi, mashaka, na kweli sasa aliweza kuiona sura ya yule
mtoto, ni kweli sura ile ilikuwa ikifanana na aliyekuwa mpinzani wake, hakuna
shaka hapo huyo mtoto, ambaye sasa kafikia ujana sio damu yake,..
‘Sasa nifanye nini...?’ akajiuliza, huku
akihisi shinikizo la damu likiongezeka, kichwa kikawa kinamuuma sana, na mara
akahisi kitu kikimtafuta upande wa kushoto,na alipojaribu kuinua mkono wake upande
wa kushito, akashindwa, ilikuwa kama sehemu hiyo haipo, haiinuki, hii
iliashiria kuwa upande huo umeshapooza, hawezi kuuinua tena...hapo moyo ukazidi
kumuenda mbio, na alitaka kutamka jambo, kumuambia yule mtoto amuite dakitari,
lakini sauti haikuweza kutoka.
Kisu sasa kilikuwa mkononi mwa yule mtoto,
akiwa kakidhibiti vyema, ile hali ya kutetemeka kwa yule mtoto ilikuwa
imekwisha, lakini sura ilikuwa ni ile ile, ni sura yake ya kawaida, lakini sura
ile ilikuwa ikifanana na huyo marehemu, baba mtu hakuwahi kuligundua hilo
akilini mwake kabla
‘Ina maana kweli huyu mtoto sio damu
yangu.....’akajiuliza akilini
‘Sasa nitafanya nini..?’ akazidi kujiuliza,
lakini sasa kisu kilishafika mikononi mwa mtoto ambaye kumbe sio damu yake, na
taratibu za awali zilishapita, na ina maana sasa hapo mzee hana mamlaka, hana
nguvu za asili alizokuwa akitamba nazo, sasa atafanya nini.
‘Ni lazima nimnyang’anye huyu mtoto hiki kisu
haraka, halafu nikaulize taratibu gani nifanye, ili kulisafisha hili
kosa,lakini nitafanyaje na mimi siwezi kuinuka, na mimi siwezi hata
kuongea...’akawa anajiuliza akilini
‘Lakini kwanini, kwanini mke wangu akanifanyia
hivyo, na kwanini akili yangu muda wote huo haikuwa imeligundua hili...’akawa
akijilaumu...
Hapo akamtizama yule mtoto tena, mtoto ambaye sasa
alikuwa kakishikilia kile kisu, na sasa akianza kutabsamu, lakini tabasamu lile
halikuwa la furaha, lilionyesha chuki fulani,...na hapo mzee huyu akakumbuka
chuki aliyokuwa nayo huyo mpinzani wake, hasa siku ile alipomtamkia kuwa sasa
keshamuoa mama wa mtoto huyo, ambaye kabla ya hapo, alikuwa mchumba wa huyo
adui yake.
Wakati anawaza hayo, mara kitu cha ajabu
kikatokea, yule mtoto akiwa kakishikilia kile kisu mara sauti nzito, ikaanza kutoka
mdomoni mwa yule mtoto, sauti nzito kweli, na sauti ile ilimtetemesha yule
mtoto, na kumfanya yule kijana, atoe macho, kama anatishika, na ni dhahiri
ilikuwa kama kitu kimemuingia yule kijana, kwani alikuwa akitetemeshwa huku jasho
likianza kumtoka, yule kijana sasa akawa akinguruma,na ghafla akasimama kutoka
pale pembeni ya kitanda alipokuwa amekaa.
Baba mtu akamuangalia yule kijana, kwake yeye
ni mtoto tu, alimuangalia kwa hali ya kuogopa sasa, ..akiwa amelala pale
kitandani, akiwa bado anaugulia , akajua
sasa siku zake za kuishi zinahesabika,,na alitakiwa kulifanya hilo, kumkabidhi huyo
mtoto wake kisu cha urithi, sasa kumbe kavuruga, sasa kumbe huyo mtoto sio damu
yake, na kwa kufanya hivyo kakiuka mila, na balaa linaweza kuanzia kwake...lakini
kwa upande mwingine mapenzi ya baba kwa mtoto huyo yalikuwa hayajaondoka, kwani
alimlea na kumpenda, ....kosa ni kutoka kwa mke wake.
‘Oh, mungu, nimefanya kosa gani...?’ akawa
anajilaumu
‘Mke
mwema,...mwanangu hakikisha kabla hujaoa uwe umefanya uchunguzi wa kina,
hakikisha kuwa kweli unayetaka kumuoa ni mke mwema, maswala ya ndoa sio ya
kukimbilia tu, ni maswala yanayohitaji umakini, ...mchunguze mwenza wako, uliza
wakubwa zako, watakuambia, watakuelekeza mke mwema ni yupi,..’hii ilikuwa
kauli ya baba yake siku alipotaka kuoa, baba yake kipndi hicho alikuwa anaumwa,
na kifo chake kikatokea hata kabla baba huyu hajamuoa mama wa mtoto huyu
aliyekabidhiwa kisu leo.
‘Baba
huyo mchumba wangu nimempenda sana, sitaweza kuachana naye, nina uhakika kuwa yeye
ni mke mwema kwangu, kwani mimi ndiye ninayemuoa, sihitaji kuuliza watu, ..baba
usiwe na shaka, huyo atakuwa mkwe wako mwema...’akasema huyo baba mtu.
Baba yake huyu hakutaka kubishana na huyo mtoto
wake, kwani yeye kwa muda huo alikuwa kwenye wakati mgumu, akigua, maradhi
ambayo yalimtesa sana, hadi akafariki dunia bila kujua hatima ya mtoto wake
huyo, na mtoto wake huyo akawa akimtegemea babu yake, babu ambaye baadaye
alikuja kumkabidhi kisu , kwani hakukuwa na mrithi mwingine kwa wakati huo,
wengine walikuwa mbali, wakihangaika na maisha yao.
Yule mtoto aliendelea kunguruma kama simba, na sasa
alikuwa kasimama, na kusogea mbele, pembeni ya baba yake, wakawa wanatizamana
baba na mtoto, baba akishindwa kufanya lolote, hawezi hata kutamka neno,
machozi sasa yakawa yanamtoka akijuta kutokumsikiliza baba yake, alipenda kupitiliza,
na hakuwa akiwasikiliza hata ndugu zake walipomshauri kipindi hicho, akaona na
baadaye akaja kumzalia huyo mtoto anayepewa kisu leo..hakuwahi kuhisi kuwa mke
wake anaweza kumsaliti,...alimpenda na kumuamini.
Yule mtoto sasa akiwa kakishikilia kile kisu
vyema, akiwa ananguruma, akiwa katoa macho ya hasira, akitikisa kichwa kama
kukataa, alikuwa akikataa nini, baba mtu akawa anamuangalia tu na kujiuliza,
akiwa hana la kufanya
Baba mtu akaanza kuona wasiwasi, kinyume na
alivyotegemea, alitegemea leo ingekuwa siku ya furaha kwa familia, siku ya
kumhakikishia mwanae kuwa yote aliyokuwa akimfanyia mtoto huyo ya kumjenga
kiujasiri,sasa matunda yake ndio hayo, ya kukabidhiwa jukumu la kifamilia.
Alikumbuka jinsi alivyokuwa akimfundisha mtoto
huyo, ambaye mara nyingi alionekana kutokutimiza mambo mengi aliyokuwa
akimuelekeza, tofauti na alivyokuwa yeye, babu yake aliwahi kumuambia kuwa yeye
alikuwa mtiifu sana, na kila alichofundishwa alikifuata sawasawa tofauti na
alipokuwa akimfundisha huyu mtoto wake, ilikuwa vigumu kumfanya ajue jambo, na
kulifuata, ilichukua muda, japokuwa baadaye alikuwa kuweza na kuwa na muelekeo
japo sio sana.
Mara nyingi mama wa mtoto alimtetea sana mtoto
wake huyo, na baba ili kuonyesha ubaba wake, akawa anamchapa sana huyo mtoto
ili aelekee anavyotaka yeye, lakini yota hayo yakiwa na lengo moja, vyote
vilifanyika makusudi, ili mwisho wa siku mtoto huyo aweze kujengeka vyema ili aweze
kulipokea jukumu kubwa la kuilea famlia, lakini kumbe alikuwa akimlea mtoto asiyekuwa
damu yake bila kujua, ilikuwa siri ya mama wa huyo mtoto.
Baba akiwa na mapenzi, akamuomba mungu angalau aweze kumsaidia
mtoto wake, maana aliona mabadiliko kwa mtoto wake yasiyo ya kawaida, na kweli
dua zake zikapokelewa, mara sauti yake ikatoka;
`Vipi mwanangu unaumwa, nimuite dakitari’ Baba
mtu ghfala akaweza kuongea, na kumuuliza mtoto yule kwani hakuwahi kuiona hali
hii kabla kwa mwane, na japokuwa yeye ndiye aliyekuwa akiumwa zaidi , lakini
sasa akawa anahisi mtoto wake ndiye anayeumwa zaidi, mapenzi ya mzazi kwa mtoto....
Baba mtu hali ile ilimtisha,akaona ni vyema
amuite dakitari, akitumia mono wake wa kulia ambao ulikuwa sasa una nguvu
tofauti na upande ule wa kushoto, akajitutumua na kuweza kujisogeza, huku mtoto
akimuangalia, ...mtoto alikuwa akimuangalia huku macho yamemtoka, mdomo upo
wazi, ukihema, kama anavyohema simba....
Baba mtu akajitahidi hadi mkono ukaweza
kukifikia kitufe cha dharura cha kumuita dakitari...
Wakati baba mtu anataka kubonyeza kile kitufe
cha kuomba msaada wa dakitari akizani mwanawe amepatwa na mshituko wa ghafla, mara
akahisi kitu kikali kikichoma kifuani kwake, sasa sio kile cha awali, mchomo
huo ulikuwa tofauti, kwani sasa alihisi maumivu makali yakipenya kifuani
katikati ya moyo, na wakati macho yake hayaamini nini kinatokea, alisikia kisu kikivutwa
toka mwilini na kikatua tena mwilini kikapenya moja kwa moja na safari hii
hakikukosea kilimaliza maisha ya bwana tajiri, bwana Mapesa! ..gizaaaaaa....
NB: Karibuni kwenye kisa hiki kipya, chenye
vionjo mbali mbali, mikasa , mapenzi, usaliti, mauaji..na huo hapo juu ni
utangulizi tu...hebu tuone hii ndoto ya dunia yangu ilianzaanzaje...
WAZO LA LEO: Makosa
makubwa huanzia kwenye chaguzi zetu za kumpata mke au mume mwema, tumekuwa
tukipuuza sana haya maagizo na maelekezo ya wakubwa zetu, na hasa mafundisho
tunayoyapata kutoka kwa viongozi wetu wa dini, na kuyazarau kabisa maandiko
matakatifu, kuwa ili uwe na familia bora, unahitajika kumpata mwenza mwenye
muelekeo, usikimbilie tu kwa ushahiwishi wa kimwili, ukaona sura, na mwili ni
kivutio pekee,...amani , upendo, furaha huanzia hapa penye kumpata mke au mume
mwema.
Ndugu wapendwa mnaotaka kuoa au kuolewa, kabla
humjachukua maamuzi ya kuoa, au kuolewa, muombeni sana mwenyezimungu, pia ulizeni
kwa wakubwa kumjua mwenza wako vyema, chunguza kwa makini kabla ya kutekwa na
ushawishi wa kimwili, tukumbuke kuwa mke au mume mwema hutoka kwa
mwenyezimungu, na hili ni kutokana na maombi yako kwa mwenyezimungu.
Soma sehemu ya kwanza
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Hey! Do you knoա if thеƴ make any plugins to aѕsist with SEO?
I'm trying to get my blߋg to rаnk for some tɑrgeted keywords but I'm not seeing very good results.
If you know of any please shɑre. Cheers!
my ԝebpage temp2
Post a Comment