Mdada aliendesha gari kwa mwendo wa kasi, hadi hotelini kwangu, na haraka akatoka nje, na kama kawaida yake akakimbilia kunifungulia mlango, wakati huo mimi nimeshaufungua huo mlango wa gari nusu, akauvuta na ukafunguka kwa mapana yake, halafu akangalia saa yake na kusema;
‘Fanya haraka huyu mshenzi anakuja, tuna dakika kumi mbele yake, kama hatakutana na foleni...’akasema
‘Mshenzi gani huyo tena mdada,...?’ nikauliza kwa mshangao
‘Si huyo mtu wako, sijui anataka nini, lakini kwangu amefika, sikuanza hii kazi jana, kama yeye katumwa na hao mabwana zake mimi nimetumwa na wenye nchi....’akasema huku akianza kuondoka kuelekea hotelini na mimi nikamfuatia nyuma, tukaingia hotelini,
‘Unakwenda wapi huko, nani kakuambia tunaenda chumbani kwako, unielewe, sasa hivi tunaelekea moja kwa moja ofisini kwako,...’akasema
‘Oh, ....kwanini huko?’ nikauliza na yeye hakusema neno akawa anatembea ule mwendo wa kiaskari
‘Ina maana hukunielewa nilivyokuambia, au unanichezea shera, nataka zile nyaraka nilizokuambia, i am serious, ni muhimu sana kwako, ni muhimu sana katika mipango yetu, zitatusaidia sana kama tutasimamishwa kutoa ushahidi....’akasema
'Lakini hizo hazihusiani kabisa na kesi hiyo ya mauaji, labda kama unazihitajia kwa mambo yako mengine...'akasema
'Mambo yangu mengine yapi,...ujue sasa hivi tupo kwenye kesi kubwa sana, kama sio huyo mlinzi , ujue ni wewe au mimi tunaweza kutuhumiwa,....'akasema
'Polisi wamesema wana ushahidi wote kuhusu huyo mlinzi,mimi sioni kwanini tuwe na wasiwasi na ujiongezea matatizo....'akasema
'Kujiongezea matatizo gani wewe, mbone unakuwa muwoga wewe mwanaume,niamini mimi...'akasema akiongeza mwendo
'Hapa sio swala la kukuamini, hapa ni je hilo tunalootaka kulifanya linakubalika kisheria, kiutaratibu, je tukiulizwa tutasema nini...'nikasema
'Tukiulizwa wapi au na nani?' akaulizwa
'Na watu wa usalama, polisi au mahakamani' nikasema
'Kama watatuuliza mahakamani itakuwa bora, maana tutakuwa na ushahidi wa kujilinda, hizo nyaraka zitathibitisha mengi yaliyokuwa yakifanywa na huyo mtu, na kwahiyo kufika kwake kwangu, ilikuwa ni sehemu ya shughuli zake za kuhujumu mali ya nchi...unataka nikuambie kila kitu..'akasema
'Kama ni hivyo, kwanini tusingewafahamisha polisi wakalifanyia hilo kazi, au hata wakili wetu, ili tuwe na dhamana kisheria...'nikasema.
'Cha muhimu ni kuzipata hizo nyaraka kwanza...hayo mengine yatafuta baadaye...'akasema
‘Nyaraka zipo nyingi, wewe ulikuwa unataka nyaraka zipi, na ukumbuke kuwa mimi sistahili kuzitoa kwako, bado sijapewa mamlaka ya kuendesha hiyo ofisi, kwahiyo sijui unataka mimi nije kueleweka vipi, kwanini hizo nyaraka ni muhimu?’ nikauliza
‘Wewe usinifanye mimi mjinga, nijua nini ninachokifanya, wewe fuata ninayokuambia, mengine utayajua vyema baadaye, unakumbuka nilikuambia nataka nyaraka gani, usitake kunipoteze muda, au upo njama moja na huyo jamaa yako, huyo jamaa yako ni wale wale,, hapo alipo kavaa ngozi ya kondoo, lakini ukimfunua sana utamgundua kuwa ana masilahi yake,dunia hii kila mtu ni mjanga, hata mjinga ana ujanja wake, sasa wewe zubaa tu’ akasema
‘Lakini wewe unamzungumzia jamaa yupi huyo, mbona unamtaja kwa namna hiyo, hana jina, ni nani huyo?’ nikauliza na yeye akaniangalia kwa macho makali, akasema;
‘Twende ndani ...tatizo lako wewe unajifanya kama vile hujui, unafikiri mimi ni mtoto mdogo, hapo unachofanya ni kupoteza muda, nahisi umeshawasiliana na jamaa yako kakuambia upoteze muda ili afike....lakini kumbuka tulipotoa, huyo jamaa atakuhadaa, na mwisho wake atakuacha kwenye mataa...’akasema
‘Mdada,mimi sina lolote kwa yoyote, sana sana nawafuata nyie, na kwanini wakili wangu hayupo, maana haya yote ynahitajia wakili awepo ili afahamu jinsi gani ya kutushauri, tusije tukafanya mambo kwa utashi wetu tukaja kujijutia....’nikasema
‘Wewe mwanaume hebu, fanya haraka, najua huyo jamaa keshafika hapo chini, kwa muda tuliopteza hapa kwa uzembe wako, atakuwa ameshafika, ..hata hivyo mimi sio mjinga, watu wangu watamzuia mpaka nipate hizo nyaraka,tuna dakika nyingine kama tano mbele yake....’akasema na kuhakikisha mlango umejifunga kwa ndani, ina maana mtu wan je hawezi kufungua mpaka mtu wa ndani amfungulie
‘Lakini ufungua wa hizo kabati sina, ....’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho yaliyojaa chuki, na mara nikasikia mlango ukigongwa, ....mdada akachukua simu yake, akaangalia na kusema;
‘Oh, keshafika imekuwaje, hawa watu vipi nimewaambia wamzuiezuie huyu mtu asifike mapema lakini hawakunielewa sijui, au katumia nguvu nini....hata hivyo, ni lazima hizo nyaraka zipatikane haraka iwezekanavyo,....’akasema na huku akiniangalia mimi, akashika mkoba wake huku akiwa kaniangalia akaufungua huo mkoba wake akawa anatafuta kitu, na mara akatoa fungua na kunikabidhi, akasema;
‘Haya, ufunguo hizi hapa fungua hilo kabati nafahamu ufungua wako unao,lakini lengo lako ni kunipotezea muda, na hili linanionyesha kuwa umeanza kunisaliti, nakuonya sana mhasibu, kumbuka pamoja na haya, mimi ndiye mchumba wako, ....’akasema na mara mlango ukagongwa tena, na safari hii kwa nguvu, nikamwangalia mdada, na kusema;
‘Mdada huenda ni wakubwa hao...’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho yaliyojaa hasira akasema;
‘Huyu ni jamaa yako wewe fungua hilo kabati , wewe vipi, mbona hunielewi, hivi wewe unataka nikubebe mpaka lini...’akasema
Na mimi nikaelekea kwenye hilo kabati na kuanza kulifungua, ...kweli likafunguka, akilini nikawa najiuliza jinsi gani mdada alivyoweza kupata hizo ufunguo, zilikuwa zakuchongesha, na kabati likafunguka, na kujikuta nikishikwa na mshangao mkubwa, nikabakia nimeduwaa...
Kama sekunde chache nilibakia mdomo wazi, kwani kabati hilo lilikuwa na nyaraka nyingi na nilishaambiwa kuwa hizo ni nyaraka za siri, lakini kwa muda huo kulikuwa hakuna hata nyaraka moja, sehemu ile ya nyaraka za siri kulibakia jalada moja tu, na lenyewe lilionekana kuwa tupu, nikageuka kumuangalia mdada, na mdada akasema
‘Unaniangalia nini, toa zote nyaraka haraka, nipe mimi, nitaangalia mwenyewe hizo zinazohitajika...’akasema na mimi nikasogea pembeni na kusema;
‘Mdada mbona hakuna kitu, ina maana unanijaribu ....’nikasema na yeye akaniangalia halafu akaangalia pale kwenye hilo kabati, nilimuona akishikwa na mshangao, halafu akageuka kuangalia mlangoni na kusema;
‘Funga hilo kabati, wajanja wametuwahi,na huyu mtu nitamuonyesha kuwa ni nani hii leo, atakoma kunifuata-fuata, bahati yake sikuja na bastola yangu, simpendi huyu mtu....’akasema na kutembea kuelekea mlangoni, akashika kitasa kabla hajafungua huo mlango akageuka kuniangalia, akaniashiria nikakae kwenye kiti kikubwa, na baadaye akafungua mlango,...
NB: Leo ni jumamosi, nimeona niwape hiki kidogo,
WAZO LA LEO: Kuna watu wanaishi maisha ya ujanja ujanja, kazi yao ni kudanganya, kutapeli watu, hiyo kwao ni fani na wanajisifia kwa hilo, huu ni wizi, hata kama wewe utajiona ni mjanja, lakini kiukweli wewe sio mjanja wewe mhujumu, fisadi. Ujanja unaokubalika ni ujuzi wa elimu yenye manufaa kwako na kwa jamii, ujanja wa kugundua mambo kisayansi ,yenye tija, kuwa wabunifu katika fani mbali mbali kimaendeleo, na ujanja huo ukawa na faida kwako na kwa jamii, huo ndio ujanja.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment