Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, May 9, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-54


‘Mshitakiwa anataka asimamishwe kizimbani aongee mwenyewe....’akaniambia mpelelezi

‘Kwanini?’ nikauliza nikiinua kikombe cha maziwa, tulikuwa kwenye mgahawa tukiongea kipindi cha mapumzio baada ya kusikiliza kesi kipindi cha asubuhi, na ukatolewa muda wa mapumziko.

`Anahisi kuwa ukweli unapotoshwa, na haoni kwanini muda mwingi upotee kwa maelezo ambayo mengine anasema sio ya kweli na mengine yeye mwenyewe anaweza kuyatolea ufafanuzi...’akasema mpelelezi.

‘Unahisi hiyo itasaidia ?’ nikauliza

‘Inaweza kusaidia...’akasema

‘Lakini mbona hajasimamishwa...?’ nikauliza

‘Kinachosubiriwa ni kauli ya wakili mtetezi, ...nahisi kuna itu kimetokea, na huenda akacheleweshwa kusimamishwa...’akasema

‘Hujajua ni kwanini, au unahisi ni kitu gani kimetokea?’ nikamuuliza

‘Sijajua...lakini vyovyote iwavyo, atasimama kutoa maelezo yake, na huo ndio muda muafaka...’akasema

‘Muda muafaka wa nini?’ nikauliza na yeye akaangalia saa yake na ugeuka kuangalia upande wa kulia kwetu, ambapo mdada alikuwa akiongea na wakili wake, ilionyesha kama wanabishana jambo fulani na mdada alionekana kama hakubaliani nalo. Nikasema;

‘Naona mdada ana jambo’ nikasema, nikakumbuka kikao changu mimi na yeye aliponiita hotelini wa haraka, na nilipofika akaniambia alitaka kuhakikisha kuwa siendi kuonana na watu asiowaamini,...nikashangaa

‘Hata bosi humuamini?’ nikamuuliza

‘Kwa kipindi kama hiki hata yeye siwezi kumuamini, ila kuna jambo muhimu sana nataka kukuambia, kuna nyaraka za siri alizokuwa nazo marehemu kuhusu kazi zake za ziada, zipo kwenye hiyo ofisi yake, uliwahi kuziona?’ akaniuliza

‘Zipo nyaraka nyingi tu, sijui zipi unazoongelea wewe..?’ nikamuuliza

‘Kuna mizigo ya wakubwa inayoingia, ambayo ina misamaha ya kodi,...nataka kufahamu ni nani na nani...na kuna mengi tu, nahitaji tuzipitie kwa pamoja...’akasema

‘Lakini mdada huoni huo sio uataratibu, mimi bado sijakabidhiwa ofisi,...’nikasema

‘Huo ndio muda muafaka...kabla hawajapitia kila kitu...’akasema
Kabla hatujamaliza maongezi mara mlango ukagongwa na mdada akaniangalia, na mimi nikawa nimetulia nikionyesha kushangaa, akaniuliza;

‘Ni nani huyo?’ akaniuliza

‘Sijui,...’nikasema na yeye akachukua simu yake na kuandia ujumbe kwa haraka na mara akajibiwa akageuka na kuniuliza

‘Mpelelezi amekuja hapa kufuata nini?’ akaniuliza

‘Mimi sijui....’nikasema na yeye akasimama wa hasira na kuchukua mkoba wake, akasema;

‘Nitakuja tena, ni lazima hilo zoezi lifanyike....’akasema na kuondoka, alipofika mlangoni, akageuka kuniangalia, na uso alionionyesha ulikuwa umekunjamana kwa hasira, na akafungua mlango mpelelezi akaingia...

********

Wakati nakumbuka hayo, kule kwa mdada na wakili wake, bado kulikuwa hakuna makubaliano, niliona kama mdada anataka kuongea na mawakili wake wanamsihi, alikuwa wakili wake na wakili wangu.

‘Yah, ndio hivyo mambo yanaanza kupamba moto, joto linazidi kupanda, ...’akasema

‘kwahiyo huyo mtuhumiwa akismama, nahisi kesi ndio ianfikia ukingoni kitakachobakia ni hukumu au? nikauliza

‘Ngoja tuone..., kama atasimamia maelezo ya polisi, bado kibarua kitakuwa kigumu, lakini kama ataamua kusema ukweli, itasaidia sana....inaweza ikawa mwisho wa hii kesi, hata mimi nitakuwa tayari kutoa ushahidi wangu...’akasema

‘Oh, kwahiyo unataka kwenda kinyume na wakubwa zako?’ nikamuuliza

‘Sio kwenda kinyuma na wakubwa zangu, hata wao wanasubiri muda muafaka, wanachotaka wao ni kutokuleta mtafaruku,...ni mambo ya kisiasa tu, ...na ilivyo hata wao wenyewe wameshagawanyika,...unajua siasa hizi bwana, sijui zinataka nini, lakini tutafika tu...’akasema

‘Kwani hao wanasiasa wanataka nini?’ nikauliza

‘Ni zile zile sera za kulindana, huyu ni mwenzetu , ni lazima asaidiwe, kwa masilahi ya chama, ndio kauli zao hizo, hawataki kusema kwa masilahi ya matajiri ambao ndio mafisadi wakubwa, ambao wana utajiri wa kukufuru, wana account huko nje,kama hao matajiri wangeliamua kuwasaidia masikini, wakawasaidia mikopo ya kuwekeza, mbona umasikini ungelipungua kwa kiasi kikubwa, lakini wapiii ...hawa watu sijui kama wataweza kuuona ufalme wa mbingu...’akasema

‘Naona sasa unakiuka kanuni za kazi zako...’nikasema na yeye akacheka, na kuangalia kule walipokuwa mdada, na wakati huo, walikuwa wakisoma makabrasha, na mara kwa mara mdada, alikuwa akiinua mikono juu, kama kupinga jambo, mimi nikasema;

‘Lakini kwanini watu kama hao walindwe, hata kama wanafanya ubaya, kwanini wasiwajibishwe, mimi ndio maana hata hii kazi yao, sitaki kuifanya....wewe mwenyewe hapo ulipo, unajuta kwanini ulikubali kufanya kazi kama hiyo..’nikasema

‘Ipo siku na wewe utajionea mwenyewe, wanakuandaa, wewe mwenyewe utakuja kuniambia, ...inauma sana, hasa nikiona wazee wangu, wazee wa kijijini wanavyoteseka, wanaishi maisha duni, lakini kodi yao imechukuliwa toka wakiwa wadogo...'akasema

'Kodi ya wazee hiyo ndiyo imewaneemesha mafisadi, wanakula kodi ya wanyonge bila huruma, na bado wazee hao wanazidi kukamuliwa, hakuna hata sera moja ya kuwasaidia wazee, hebu niambie ni chama gani chenye sera za kuwasiaidia wazee, wao wanapigiwa debe, mafao ya mazishi yao...’akasema

‘Nikuulize wewe unapenda kuwa mwanasiasa, ili ukagombee ubunge, ili uweze kutetea hayo bungeni, maana watu kama nyie mkikaa bungeni mtaweza kutetea haki za wanyonge, unafaa sana au sio?’ nikamuuliza

‘Sipendi kabisa siasa?’ akasema

‘Kwanini?’ nikamuuliza

‘Kwasababu sijui maneo ya uwongo,,...na nyanja hiyo ili uweze kushinda na kueleweka vyema hasa ukiwa jukwaani ,kwenye hadhara unatakiwa ujue kuongea saana, na mengi ya maneno yako yatakuwa ni ahadi za uwongo, ...mimi hiyo siwezi, nitaongea ukweli na wananchi walivyo, hawatanichagua, kwani wamezoea kudanganywa ...’akasema

‘Oh, mimi nilijua ukweli una nguvu, ukiongea ukweli unakuwa na sauti,na watu watakuamini sasa mbona unapinga kauli yako ya awali?’ nikamuuliza

‘Ukweli una nguvu sana,...ila kwa muda huo, wakati unatafuta ubunge, ukweli utapuuzwa, kwa wakati huo wananchi wameshapandikizwa fitina, propaganda potofu zimeshajaa kichwani mwao, na wewe ukija na ukweli wako,watakuona wewe huna sera, ...’akasema na kutulia kidogo

‘Lakini wa vile ukweli una nguvu,baadaye wanakuja kujuta, na kuanza kuku-kumbuka, kuwa yale uliyoyasema siku ile jukwwani ni kweli tupu, lakini wakatu huo wameshapigika na sera za uwongo walizoziona awali kuwa ndizo zinazofaa, zinaanza kuwatafuna...ndio maana sipendi kabisa mchezo huo....’akasema na tukabakia kimiya kwa muda, halafu mimi nikauliza;

‘Sasa huyu mtuhumiwa, amakubaliwa na mawakili zake?’ nikamuuliza

‘Mawakili zake ndio wametoa hilo ombi kwa hakimu,...japokuwa haliufikishwa kwa ahkimu kwa mpangilio,..ilitokea juzi wakati wewe ulipoondoka na mdada...’akasema

‘Ilikuwaje, mbona nilikosa sehemu muhimu sana?’ nikamuuliza

******

‘Ndugu hakimu mimi nina ombi japokuwa mimi sio mtetezi, lakini kwa bahati nzuri, mimi ni mtu ninayependa haki na ukweli, niliongea na mshitakiwa akaniomba mimi niruhusu yeye aweze kusimama na kutoa maelezo yake, sikuwa na pingamizi na hilo, kwahiyo muheshimiwa hakimu kama muda unaruhusu basi ni heri huyu mshitakiwa akasimama ..’akasema muendesha mashitaa na hakimu akaonyesha uso wa kushangaa na kuangalia upande wa utetezi

‘Ndugu hakimu sisi upande wa utetezi tunaona ajabu sana, kwanini muendesha mashitaka anaingilia kazi zetu, kama wameishiwa waseme....’akasema wakili mtetezi, na kukatokea malumbano ya kisheria kati ya mawakili hawa, hadi hakimu akaingilia kati, na baadaye hakimu akampa nafasi wakili mtetezi, kwa kumuuliza

‘Je nyie hamkubaliani na hilo ombi la mteja wenu kutaka kusimama na kutoa maelezo yake mwenyewe?’ akaulizwa wakili mtetezi

‘Ni kweli mteja wangu anataka kusimama na kutoa maelezo yake mwenyewe muheshimiwa hakimu, lakini hilo nilitakiwa mimi ndio niliwakilishe kwako muheshimiwa,kwa mpangilio wetu, hii inaonyesha jinsi gani wenzetu wanavyoingilia kazi ambayo sio ya kwao,na hapa inaonyesha kuwa wanajaribu kumshinikiza mteja wangu afanya kile ambacho sio sahihi...’akasema wakili mtetezi.

‘Je huoni kuwa wewe na mteja wako mnaonekana hampo sambaba?’ akaulizwa

‘Sio kweli,tupo sambamba kabisa, lakini kauli hiyo ya muendesha mashitaka inaingilia kazi zetu, na sisi hatukufurahishwa nayo, sio utaratibu huo, ilitakiwa niiseme mimi kwa wakati wangu...’akasema wakili mtetezi

‘Utaratibu au sio utaratibu ni kazi yangu hakimu, nakuuliza swali, je kwa mpangilio wako unataka mteja wako asimamishwe lini, leo au kesho?’ akaulizwa

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, mteja wangu yupo tayari kuongea hata leo, lakini mimi nionavyo kwa leo, sio vyema, kutokana na mambo mengi yaliyotokea leo, naomba hilo lifanyike siku itakayopangwa esi hii tena, ili na mimi niweze kuongea na mteja wangu vizuri...’akasema

‘Sawa, kumbe bado mlikuwa hamjakubaliana, nab ado unasema mpo sambamba, ... hata hivyo muda uliobakia ni mchache, ...kwahiyo tunaahirisha hii kesi hadi kesho kutwa, na mkija hapa muwe mumejiandaa vyema...’akasema hakimu, na kesi ikaahirishwa

Nikakumbuka siku ile nilitoka mapema kutokana na muito wa mdada,ambaye alitaka tuondoke,nikampe baadhi ya stakabadhi alizouwa akizihitajia, nikamuuliza

‘Kwani hizo stakabadhi ni muhimu sana kuliko hii kesi?’ nikamuuliza

‘Kesi hii ikiisha unatakiwa uwe na maandalizi ya kesi ijayo, niliyoyasikia hapa leo, yananituma kuwa muda wowote mimi na wewe tutasimamishwa kutoa ushahidi, sasa ni lazima tujiandae, wewe hulifikirii hilo, lakini mimi naona mbali...’akasema

‘Oh, mimi nilijua akiongea na ukweli ukadhiri, haina haja ya sisi kuongea tena...’nikasema

‘Kauli yake peke yake haitoshi, na je unajua ni kitu gani ataiongea, je akisema wewe au mimi ndiye tuliyemuua mtoza ushuru, utajitetea vipi, ni lazima ufikiria zaidi,na ujipange jinsi gani ya kujitetea...’akasema

‘Wakili kashauri hivyo?’ niamuuliza

‘Vitu vingine unatakiwa ufiirie wewe, na wakili atakuja kukushauri tu...mimi naifahamu sana sheria, japokuwa sio wakili, kwahiyo nafahamu ni kitu gani kitahitajika, twende uanipe hizo stakabadhi, .....’akasema

‘Lakini mimi siruhusiwi kutoa hizo stakabadhi,..sijakabidhiwa ofisi rasimi...’nikajitetea

‘Kwahiyo upo tayari kufungwa kwa mauaji ya mtoza ushuru, upo tayari kushikiliwa tena, hebu tumia akili yako,...ni kweli nafahamu kwa kufanya hivyo ni kosa, lakini wakati mwingine inabidi ufanye kosa kwa kujihami,na hilo kosa litakuja kusahihishwa na ukweli utakaokuja kubainika baadaye...’akasema

‘Kumbe na wewe umeajiriwa idara aliyokuwa akifanya mtoza ushuru?’ nikamuuliza na yeye akanitupia jicho la haraka na kusema;

‘Kakuambia nani, ...ni bosi huyo karopoka, nilijua tu...kwahiyo unataka kusema nini, kuwa wewe ni bosi wangu, kwahiyo sistahili kukutuma kitu, haya, fanya upendavyo, lakini ujue kuwa hili ninalolifanya ni kwa masilahi yako...’akasema

‘Sijasema hivyo..hayo unasema wewe....’nikasema

‘Kwahiyo tunakwenda huko hotelini ukanipe hizo stakabadhi au ndio bosi hutaki kutumwa na mfanyakazii wako wa chini?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho makali

‘Mimi sio bosi wako, ...na hata hicho cheo mimi sikitaki, nimemwambia bosi kama inawezekana, mimi nirudi kazini kwake, lakini kasema hilo litakuwa gumu, sijui kwanini wamefanya hivyo...’nikasema

‘Ukisikia ulofa, ujue huo ndio ulofa, wewe unapewa ulaji, halafu unaukataa, sasa unataka nini katika hii dunia, hivi wewe unafurahia kupiga mguu, kuendesha pikipiki, ....ina maana kweli hutaki maisha bora,...gari nyumba,...utajiri...’akasema huku akiangalia hewani kama mtu anayeota jambo.

‘Napenda sana, lakini kwa amani....hicho cheo ninachopewa hakina amani, nahisi kina mtego, nahisi kuna jambo nyuma yake...’nikasema

‘Ni wasiwasi wako tu....cha muhimu ni kujipanga, ..usijali tupo pamoja..’akasema na kunishika mkono kunivuta tuondoke, sikuwa na hiyari, tukaondoka pamoja, na wakati tunaingia kwenye gari, mpelelezi akanipigia simu,..nilisita kuipokea, lakini baadaye nikaipokea;

‘Mbona umetoka bila kuniaga?’ akauliza

‘Ni dharura tu mkuu..’nikasema

‘Sasa sikiliza kuna nyaraka muhimu, nazihitajia, zile nilizokuambia,...hakikisha kuwa hazitoki, ni muhimu sana kwa mustakabadli wa hii kesi, nimeshawakilisha hilo kwa wakubwa zangu, kwahiyo hizo nyaraka ni moja ya ushahidi....’akasema

‘Oh, mbona sielewi...’nikasema na mdada akanishika pajani, nikageuka kumuangalia nikamuona akitabasamu, na kwenye simu nikasikia mpelelezi akiuliza

‘Kwani upo na mdada?’ nikamuuliza

‘Ndio’ nikasema

‘Mnakwenda wapi?’ akauliza

‘Hotelini kwangu...’nikasema

‘Ok, nakuja huko huko..usifanye lolote hadi nifike...’akasema na kukata simu, nikageuka kumuangalia mdada, nilimuona akisoma ujumbe kwenye simu yake, na akiwa kakunja uso kwa hasira halafu akasema;

‘Shhhit, huyu mtu mbona ananifuata fuata,....'akasema akiniangalia kwa hasira

NB: Vipi tena, kuna nini hapa


WAZO LA LEO:Kila unapotenda jambo baya, lisilo la wema kwa mwenzako au kwa jamii, ukafanikiwa, usione kuwa umeshinda...hiyo ni sawa na kukalia kuti kavu, na ubaya hutafuna hilo kuti kavu ulilolikalia, ipo siku utadondoka nalo. Cha muhimu ukitenda ubaya kwa bahati au kwa makusudi ukaja kujirudi, basi jitahidi kutenda mema, ili hayo mema yaje kuufuta huo ubaya.
Ni mimi: emu-three

No comments :