Wakati hayo yanaendelea, familia ya baba mkwe ilikutana, wao kama
familia waliamua kufanya kikao maalumu cha wanafamilia cha dharura chenye
ajenda moja ya jinsi gani ya kumsaidia mgonjwa wao, kwani penye wengi kuna
mengi, lengo ni kama kuna njia nyingine zaidi ya hiyo ya kutibiwa hospitalini,
je kuna nini kilichomfanya ndugu huyo afikie mahali hapo, na kama wanandugu wao
wachukue hatua gani..
Ndani ya kikao hicho, walihudhuria
ndugu wa baba mkwe akiwemo shangazi, mtoto wa baba mkwe ambaye ndiye mchumba
wangu, na jamaa wengine wanashibana na familia, pia alikuwemo wakili wa baba
mkwe na akaalikwa jamaa mmoja mgeni kabisa katika familia hiyo…...
Kati ya hao
ndugu wanaoshibanana hiyo familia mmojawapo alikuwa ni rafiki yangu, ndiye
aliyekuja kuniambia jinsi kikao kilivyofanyika;
‘Nakuambia haya
kama rafiki yangu uwe na tahadhari kwani hali ya hatari imetangazwa, wewe na
mdada, mumewekwa kama maadui wakubwa wa familia hiyo..’akaniambia
‘Usijali,
yote yatakwisha na ukweli utadhihiri, na ikifikia hapo wote watarudi nyuma na kugundua
kuwa, haki na ukweli wakati wote una
nguvu zaidi ya dhuluma…hebu niambie waliyoyaongea huko kwenye kikao chao ni yapi, au ni
siri yenu?’ nikamuuliza.
‘Nitakuambia
walichoongea, lakini halahala, usije kumwambia mtu yoyote kuwa mimi ndiye
niliyekuambia haya ninakuambia unasikia, wao wananiamini sana kama mwanafamilia, sasa usije ukanivurugia uaminifu wangu, tupo pamaja…’akasema.
‘Siwezi
kukusaliti rafiki yangu, …tupo pamoja kama kawaida yetu wewe lete maneno...’nikasema na yeye ndio akaanza kuniambia jinsi kikao
kilivyofanyika na yaliyoongelewa;
‘Kikao
kilianza kwa kiongozi wa familia ambaye ni mdogo wake baba yako mkwe, yeye
alianza kutoa taarifa ya kusudio la kukutana kwao…’akawa anajaribu kuiga sauti
ya huyo mtu kwani rafiki yangu huyu anapenda sana kuchekesha;
Alipomaliza
kuongea akadakia shangazi yako maana huyo ni mama mdomo, visinipite,akaanza
kuongea hata kabla mwenyekiti hajamruhusu kuonyesha yeye anajua zaidi…
‘Jamani hali
ya ndugu yetu ni kama mlivyoisikia, ni mbaya sana,kwa maelezo ya mtaalamu ni
kuwa kakumbwa na shetani, na bahati nzuri niliposikia hivyo kuwa kaka kadondoka
na kupoteza fahamu, nilimpigia simu jamaa yangu huyu hapa, kwa utambulisho huyu
ni mtaalamu anaifahamu sana kazi yake, na habahatishi, uliza watu watakuambia…’
akasema shangazi akimtambulisha huyo mtu mgeni
‘Yeye
anafahamu, na nilipomuambia akawa keshafahamu tatizo ni nini, na alisisitizia
tusimuwahishe kaka hospitalini kwanza, nikawaambia watu wa karibu wa kaka,
unajua tena watu wanaojiona ni wa kisasa,hawakunisikia, na mtaalamu akafika kwa
haraka, ili tumuwahi kaka kabla
hajapelekwa hospitalini…..’akasema shangazi.
‘Watu
wabishi bwana, tunafika wameshamchukua kaka kumkimbiza hospitalini na magari
yao,..lakini hata hivyo hakikuharibika kitu, kwani tulikimbilia huko huko
hospitalini, na mtaalamu akanipa dawa za kuwahi kumpaka kabla hawajamuwekea
madude yao..kazi ikawa kwa madocta,eti keshaingizwa eisiyuuu….’akasema shangazi
‘Jamani sio
kila ugonjwa ni ugonjwa wa kukimbilia hospitalini, mtuulizege kwanza, ilitakiwa
lifanyike jambo jingine kabla, na huenda yangeliishia hapo hapo nyumbani na
asingelifikishwa huko kabisa, wengi waliniona mtu wa ajabu sana, lakini mimi
nafahamu mengi, maana nawasiliana sana na hawa watu wanaoitwa wataalamu, na
wazee wa zamani....’akasema shangazi
‘Ni hiyo
dawa niliyompaka,japokuwa nilimkuta wameshamuwekea madude yao ilisaidia kidogo,
na mtaalamu aansema kama tungelimuwahi kabla hajafikishwa hapo, angelimaliza
kazi, kwani hilo tatizo sio kama wanavyosema wao, alikumbwa na pepo mbaya,
…..ule mshituko, mapigoya moyo yakapanda, ...’akatulia akimwangalia jamaa yake
huyo aliyetambulikana kama mtaalamu,.
Jamaa huyo kwa muda wote alikuwa kainama tu, akitikisa
kichwa kama kukubali hivi, kavaa kofia lenye manyoya ya kila aina ya
ndege…anatisha usoni.
Kiongozi wa
familia akaona amkatishe shangazi kwanza, kwani akimuachia kikao chote kitakuwa chake, akasema;
'Samahani kidogo dada, ni vyema tukamsikiliza kwanza wakili nahisi ana ujumbe muhimu kwetu, akimaliza utaendelea na maongezi yako, maana ni muhimu sana...'akasema huyo kiongozi wa kikao, na shangazi akatulia, na wakili aliyekuwa katulia akiwa kashika kichwa na kuonyesha kuwa na mawazo na kuangalia makabrasha yake, akainua kichwa na kusema;
'Tuendelee kuna kitu nakimalizia kwanza,...'akasema na kiongozi wa familia akasema;
‘Hali ya
mzee wetu bado sio nzuri, japokuwa keshaanza kuonyesha matumaini, ila kwa hivi
sasa ni vyema, akaachwa na kutulia, sisi tuchukue majukumu yake yale tunayoyaweza, kwa hali kama
ile hatakiwi kujua chochote kinachoendelea, japokuwa madakitari wanasema
alipozindukana tu kidogo alitaka kuongea na wakili wake,...’akasema kiongozi wa
familia akimwangalia wakili, na wakili alipotajwa mara ya pili akasema;
‘Ni kweli
nilikwenda kuonana naye, na mengi aliyoweza kuniambia ni maswala yetu mimi na
yeye, ni ya kikazi zaidi, sitaweza kuyaongea hapa,tuongee mengine tu, hayo niachieni mimi na mzee ...’akasema, na kiongozi wa familia akasema;
‘Sasa, haya tumuache wakili ana mambo mengi ya kufikiria, ila kama
mlivyosikia, ndugu yetu huyu japo anaumwa, lakini kazi kwake wakati wote ipo mbele, hajali hata afya yake, hajli hata umri wake,...hili
linazidi kummaliza siku hata siku,...sasa kama wanandugu tunahitajika kumsaidia...’akasema
‘Ni kitu
gani kilitokea hadi hali hiyo ikamkuta baba yangu, maana nijuavyo mimi, baba
hana matatizo ya shinikizo la damu, mimi sijawahi kusikia, yeye ni mkakamavu mtu wa mazoezi ....?’ akauliza Binti,mchumba wako.
‘Hiyo hali
inaweza kutokea kwa yeyote hata kama hana shinikizo la damu, hata kaam ni mtu wa mazoezi, inaweza kutokea tu, pale unapojikuta umesongwa na mawazo, au ukapata mshituko fulani,....akili nayo hufika sehemu ikagoma kufanya kazi, mapigo ya moyo yakashinikizwa, ni tatizo tu, hutokea tu, na huwezi
jua huenda baba yako alikuwa na matatizo hayo kabla, lakini hakuwahi
kuwaelezea...’akasema wakili wa baba mkwe.
‘Sio
shinikizo la damu hilo, mimi namfahamu sana ndugu yangu, nyie mkitaka kujua zaidi, muulizeni huyu mtaalamu niliyekuja naye, atawaambia kila kitu....'akasema shangazi akimuangalia huyu mtu anayeitwa mtaalamu
'Lile ni shetani,
alikumbana na pepo mchafu, aliyetumwa, kwa ajili ya kumuangamiza...’akasema
shangazi,alipoona huyu mtu katulia haongei kitu na wakati huo wakili alikuwa akitabasamu , na kabla shangazi hajaendelea mwanafamilia mmoja akaingilia na kuuliza;
‘Madakitari wao
wanasemaje, baada ya kupelekwa huko?’ akauliza huyo mwanafamilia mwingine
ambaye alikaa karibu na wakili.
‘Wanasema
ile hali mbaya imeshaondoka, sasa hivi wanacheza na kushusha shinikizo la damu
ambali wanasema lilipanda sana...dakitari anasema kuna kitu kilitokea, ambacho kilimshitua
sana mzee, au kuna shinikizo fulani...'akasema huyo jamaa na wakili naye akaongezea kwa kusema;
'Ni kweli, hata dakiatari aliniulizia kuna kitu gani kilitokea kwa huyo mgonjwa , kwani hali kama ile, ina sababu zake, je wakati hali hiyo
inatokea kulikuwa na maongezi gani, ni nani alikuwepo, sikuweza kumjibu, maana
tukio hilo limetokea mimi sipo naye....’akasema wakili
'Unaona mnazunguka tu mkikwepa ukweli niliowaambia...'akasema shangazi na mwanafamilia mwingine akauliza
‘Unahisi
kuna jambo baya alilisikia, au kuna kitu kilimpandisha hasira, na ni nani
alikuwa naye wakati hali hiyo inatokea ....?’ akauliza mwanandugu huyo,
akimuangalia wakili.
‘Unajua mzee
ana shughuli nyingi, nilishamshauri kuwa aachane na majukumu mengine, lakini kama umjuavyo mzee, kila kitu anataka akifanye yeye, au akifuatilie yeye mwenyewe,, kiukweli kwa umri wake alitakiwa awaachie majukumu watu
wengine lakini mzee ni mtu asiyependa kupumzika,...hilo ndio tatizo lake, japokuwa kwa namna nyingine inamsaidia kwani anaweka mwili na akili yake iwe inafanya kazi...’akasema
wakili.
‘Lakini
nahisi kuna jambo limetokea ambalo limemshitua mzee, sio bure, baba sio mtu dhaifu
kihivyo...’aksema mchumba wako.
‘Hivyo nyie
hamumuamini hayo ninayowaambia huyu mtaalamu, amesema kaka kakumbwa na shetani mbaya, pepo
mbaya...nyie mtakuwa mnajidanganya na madakitari wenu, eti shinikiza la damu,
hivi mambo kama haya yalipokuwa yakitokea kwa mababu zetu kulikuwa na vipimo
kama hivyo...mambo kama hayo yalitokea, na wao walijua ni sababu gani, na watu
wakatibiwa, siku hizi mnakimbilia mahosipitalini, mnawekewa madude gani sijui...mnaona
yanayowakuta....’akasema shangazi.
‘Lakini
shangazi hilo ni tatizo linalojulikana ni shinikizo la damu,linafahamika kitaalamu, na lina taartibu zake za kiutibabu....’akasema wakili.
‘Jidanganyeni
tu na mambo yenu hayo, ...hilo sio shinikizo la damu, kama asingelikuja
mtaalamu akaliondoa hilo pepo kabla hajafikishwa huko, tungelimpoteza
kaka kabisaa,....’akasema shangazi.
‘Mimi najiuliza
wakati hali hiyo inatokea alikuwa na nani, alikuwa akifanya nini, huyo mtu ndiye muhimu wa kutuambia, iwe ni pepo au shinikizo la damu, lakini mimi naona kuna umuhimu wa kujua chanzo kilianzia wapi,
...ni lazima kuna jambo...’akasema jamaa mwingine.
‘Hayo
hatuwezi kuyafahamu kwa sasa, ni mpaka mwenyewe aje kuyazungumza kama atapenda
kufanya hivyo....’akasema wakili
‘Sasa sisi
tufanye nini kama wanafamilia....?’ akauliza mtu mwingine
‘Tulipize
kisasi kwa yoyote aliye nyuma ya hili, bila kufanya hivyo hawa watu watazidi kutuchezea, kumbuka enzi za kaka, hakuna mtu aliweza kumchezea, walikuwa wakimuogopa, sasa sijui hiki kidudu mtu kimetokea wapi..’akasema shangazi
‘Kwanini kisasi
, kwani kuna kitu gani cha kulipiza kisasi?’ akauliza wakili akionyesha
mshangao.
‘Mimi
nafahamu kuwa kaka ana shughuli zake nyingi tu, na alikuwa na watu anawaamini,
akawapa majukumu, sasa hawa watu wamekuwa wakimgeuka, na kufanya mambo yao
mabaya huku wakimsingizia kaka yangu, lakini hili tukio la yeye kudondoka na
kupoteza fahamu ni la ghafla, na huenda hakuwa na mtu...’akasema shangazi.
‘Hayo ni
yakusikia, naomba hayo tusiyazungumze, na wala tusijitie kwenye matatizo ya
kulipiza kisasi kwa jambo ambalo halina uhakika, hata yeye kasema tusifanye
lolote kwa sasa mpaka hapo atakapotoka hospitalini...’akasema wakili
‘Mimi nasema
hayo nikiwa na uhakika,kuna watu wapo nyuma ya haya, ambao sasa wanatumia mbinu
hizo za kuwatupia wenzao mashetani, wameona njia nyingine hazifanikiwi...’akasema
shangazi
‘Uhakika
gani ulio nao shangazi kwa hayo unayoyasema.....shangazi mimi nilikuwa na ombi
kuwa kama kuna mambo unayohisi yamefanyika ni vyema ukamwambia wakili ili ayafahamu,
na aangalai jinsi gani ya kufanya, lakini hayo mambo ya mashetani, mimi
siyaelewi,...’akasema mchumba wako na shangazi akamgeukia wakili na kusema;
‘Kwanza yupo
mdada, huyu anajifanya kujua sana, kuna mambo kayatengeneza kwa kaka yangu ili
kaka aonekana ana fanya biashara haramu, hilo ni muhimu ulichunguze na uangalia
jinsi gani ya kumshitaki huyu mtu, kama ndivyo mnavyotaka, hili niliwahi
kuongea na kaka, lakini kama mnavyomfahamu kaka, hajali, na anasema hakuna
anayeweza kumfanya lolote,sasa unaona matokeo ya dharau zake....’akasema
‘Hayo
naombeni tuyaache, tusiende mbali kiasi hicho, mimi nitaongea na mzee, nitajua
ni jinsi gani ya kufanya...’akasema wakili
‘Wewe fanya
kazi yako, na sisi kama wanafamilia ni lazima tufanye kazi yetu, ni lazima hawa
watu, mdada, na huyo mkwe wa uwongo, huyo mchumba wako, ambaye anajifanya
ndumila kuwili, hawa watu wawili na wakili wao...ni lazima tupambane nao...’akasema
‘Kwa vipi,
mimi sioni kwamba wana ubaya kihivyo, ...’akasema mchumba wako
‘Wote hao
lao moja, nia na madhumuni yao ni kumuangamiza ndugu yangu, na wanafanya hayo
wakidhania sisi tumelala, hatujui wanachokifanya, sasa ni muda wa kuwaonyesha
kuwa na sisi tupo macho, ni lazima tuwashughulikie....’akasema shangazi
‘Ina maana hata
mhasibu anahusika?’ akauliza mchumba wangu
‘Saana, tena
huyo ndiye mbaya zaidi maana ni ndumila kuwili, yeye ndiye mtoa taarifa kutoka ndani ya
familia yetu, na kuwapelekea hao watu wake, hebu niambie siku ya tukio la
kumuua mtoza ushuru, huyu mhasibu alikuwa wapi, si alikuwa kwa mdada, wakifanya ufusuka wao na
kupanga mipango yao,...’akasema
‘Shangazi
una uhakika?’ akauliza mchumba wako.
‘Kama
unabisha nenda kawaulize polisi, wao kwa mdomo wao wanasema mhasibu alikuwa
kalala kwa mdada usiku wa tukio, na asubuhi akataka kukimbia wakamdaka, hata
yeye ukimuuliza hawezi kukataa, atakachosema kujitetea ni kuwa mdada,
alipandisha, na nijuavyo mimi hilo shetani la mdada likipanda, linachukiwa wanaume,
sasa hebu niambie kwanini yeye aliweza kubakia humo asidhurike...’akasema
shangazi
‘Shangazi
una uhakiika na hayo?’ akauliza mchumba wangu
‘Unataka
uhakika gani wewe binti, hivi mimi unaniona mtoto wa juzi,...kabla ya kukuambia
haya, nikuambie ukweli, nilishafanya utafiti, wa kisasa, na huu wetu wa
kumtumia mtaalamu, huo wenu wa kisasa, nimeongea na maaskari wanaohusika,
wakaniambia yote...’akasema
‘Polisi
wanaweza kukuambia mambo kwa nia ya kuficha ukweli, ukweli wote wanaufahamu wao
wanasubiri kuuelezea kwenye mahakama...’akasema mjumbe mwingine, na wakati huo
wakili alikuwa akiongea na simu na watu wake, hakutaka hata kusikiliza hayo
maongezi, lakini hakuondoka.
‘Tangu
tatizo hilo lianze, niwaambie ukweli, sijakaa chini, nimehangaika hadi kwa hawa
wataalamu, ndio maana nikamlete huyu mtaalamu awathibitishie
mwenyewe....’akasema kwa kujiamini.
‘Shangazi
haya yanayoendelea hapa hayahusiani na imani zako za giza, wenzako wanatumia
mbinu za kisasa...’akasema mchumba wako.
‘Tatizo lenu
nyie mnajifanya mumesoma, na ujinga wenu huo ndio unaofanya muumie na kujikuta
mnahangaika, wakati matatizo mengine hayahitaji mambo yenu ya kisasa,..sikiliza
mimi nimeshatembea kwa wataaalmu zaidi ya mmoja, na wote wameniambia
hayohayo...’akasema
‘Hayo hayo
yapi...?’ akaulizwa na mjumbe aliyeonekana kuyaamini sana hayo anayooongea
shangazi.
‘Wote
wameniambia...mhasibu anatembea na mdada kwasababu shetani lake linamkubali,
vinginevyo, angeshaangamizwa, kwani shetani la mdada halina urafiki na wanaume...’akasema
shangazi.
‘Na hao
wengine, wakili wao, na wengine, wengi tu, nia yao kubwa ni kuhakikisha ndugu
yangu hawezi kufanya kazi anazozifanya, wanasema anaweka kiwungu, keshastaafu
bado anang’ang’ania madaraka...kwahiyo wanataka wamuondoe kwa nguvu...’akasema
‘Makubwa
hayo, ....sasa ukaambiwa tufanye nini, au huyu mtaalamu ndio kaja kuyamaliza,
maana hapo tunatakiwa kujifunga au?’ akauliza huyo mjumbe.
‘Kazi za
kisheria tumuachie mwanasheria, na kazi za kifamilia na mambo yetu tunatakiwa
tufanye wenyewe, hawa watu tuwashughulikie
kwa kila njia, ni lazima waokote makopo, na kuzalilika, kama huyo mchumba wako
anajiona kidume cha kutembea na kila mwanamke, basi tuhakikishe, bakora yake
haifanyi kazi, hilo niachieni mimi....’akasema shangazi akimwangalia huyo jamaa
aliyembulishwa kama mtaalamu, na huyo jamaa akatingisha kichwa kukubaliana.
‘Shangazi,
mbona umekwenda mbali hivyo, ...’akalalamika mchumba wako
‘Kuna njia
nyingine ya kibabe zaidi,...mimi nawafahamu wahuni wote wa mjini, wengi ni
marafiki zangu kutokana na kazi zangu za hapa na pale,hawa watu ukiwalipa pesa
ndogo tu, wanahakikisha hawa watu wanazibwa mdomo...na sio kuzibwa mdomo tu, ni
kuhakikisha wanasahaulika kabisa....’akasema shangazi
‘Kwanini
tufikie huko shangazi, kwanza hatuna uhakika na hilo, na ukumbuke mhasibu ni baba wa mtoto
wangu...’akalalamika mchumba wako.
‘Sikiliza
wewe mtoto ni nani bora kati ya huyo mhasibu aliyekubaka, na baba yako?’
akaulizwa
‘Baba yangu ni
bora...lakini...’akasema
‘Lakini nini
tena...hakuna zaidi ya wazazi wako, baba yako katamka waziwazi, mhasibu mdada,
na kundi lake wamemsaliti...sasa unataka uelewi vipi tena, hapo, nikuulize je upo
tayari baba yako aangamizwe na watu wenye roho mbaya hata kama ni mchumba wako?’
akauliza
‘Kwakweli
sipo tayari hata kama ni nani,..lakini cha muhimu ni uhakika wa hilo, je ni wao
kweli, je yeye anahusika, au wanamsingizia tu, nakumbuka shangazi mwanzoni
ulisema mhasibu anasingiziwa mambo mengine, ...’akasema binti
‘Unataka uhakika
wako hile eehe, basi nenda chumba cha wagonjwa mahututi ukamuone baba yako
akipumulia mashine, kama kweli una huruma na baba yako pambana na hao
waliomfanya awe hivyo,hata kama anasingiziwa, lakini yupo na hao watu, wote
watawajibika, mimi kwa hivi sasa sijali...’akasema kwa hasira na Binti
alipotaka kusema akamnyoshea mkono kumnyamazisha na kuendelea kusema;
‘Kama
mapenzi yamekughilibu akili yako, kiasi hicho, basi ujue mimi sitakuwa na wewe,
tutakosana kabisakabisa, kwanza mtu mwenyewe ameshakuonyesha moja kwa moja kuwa
ana hawara, unataka nini tena, achana naye, wanaume wapo wengi wazuri, pia sisi
tutataifisha mali yote, keshaiandikisha kwa mtoto na wewe, ana nini tena, mjini
shule, kama hujui rudi kijijini ukajipange ...’akasema
‘Shangazi,
mimi sijakataa, ila ni vyema tukawa na uhakika, kwasababu wao wana mawakili,na
wanafuata sheria, au wanafanya huku wakijua jinsi gani ya kujikinga kisheria,
kwahiyo na isis tuwe makini kwa hilo....’akasema
‘Uhakika
gani unaoutaka wewe, ina maana huniamini mimi, ....huyu hapa ndiye mtaalamu
anayeaminika, anaitwa kila mahali kuwadhibiti watu kama hao, hakimshindi kitu,
...kama mnabisha anaweza kuwathibitishia mwenyewe hapa ...’akasema
akimuonyeshea yule jamaa ambaye kwa muda mwingi alikuwa kimiya,akitikisa kichwa
kukubali au kukataa, utafikiri hawezi kuongea, na alipotajwa akainua kichwa na
kukitikisa mara nyingi.
Watu wote
waligeuka kumwangali, na yeye akawa ametoa macho kama mtu aliyeoona kitu cha
kutisha, akatikisa kichwa chake tena mara nyingi, na kuhema kwa haraka haraka,
alikuwa kama anaona kitu cha kutisha, nay eye anajaribu kukikwepa, halafu kwa
sauti ya juu akasema;
‘Mdada, ana
shetani lenye nguvu sana, haingiliki kirahisi, ...mdada ana nyota kali sana,
mdada, ana nyota na nguvu ya utawala, huyu mwanamke sio mchezo,sivyo kama
mnavyomuona, kajivika ngozi ya kondooo, ..huyu atawaangamiza....haaaaah...na
kundi lake lote linamtegemea yeye,....haaaah, ’akasema
‘Sasa
tufanye nini?’ akaulizwa
‘Kwanza ni
kumuondoa huyu mtu haraka iwezekanavyo, japokuwa ni kazi ngumu sana, kama
nilivyowaambi huyu mtu ana nyota kali ya utawala na nguvu, sasa kama kuna njia
nyingine mnaifahamu nyie ifanyeni kwa haraka, mimi siwezi kuwaambia ni njia
gani, sina mamlaka na mambo hayo na nionavyo naona kama mumeshachelewa, lakini
jaribuni…., mkichelewa na …mumeshachelewa,….jaribuni,...’akasema akiwa kama
anaangalia hewani
‘Tusaidie mtaalamu,
tufanye nini....?’akauliza shangazi
‘Fanyeni
mfanyalo,...uwezo wa kumfanya lolote upo mikononi mwenu, sio kwetu, ila kwa
tahadhari, huyu mtu mkimuachia mtamalizwa nyie, keshaanza kazi, mmoja baada ya
mwingine atadondoka, mtapotezana, mtafungwa, mbele yenu kunaonekana mtando wa giza,gizaaa....’akasema
na kutulia kimiya huku jasho likimtoka kwa wingi .
Kilipita
kitambo, na yule mtu akatulia na kuangalia huku na kule, akainuka akijaribu
kutikisa kichwa kama kuondoa vitu kichwani mwake,halafu akahema, na alipotulia,
vyema, akainua kichwa na kumuangalia shangazi akasema;
‘Mimi
naondoka, kama mumesikia mliyoambia fuateni, mimi naondoka nina safari leo hii
hii, hata hivi sasa nimeshachelewa kuna mteja nahitaiika kumuona, ...’akasema
‘Lakini mtaalamu
umetuacha njia panda, tufanye nini…?’ akauliza shangazi
‘Kazi
iliyobakia ni ya kwenu wenyewe,siwezi kuwadanganya..mnahitajika kuhangaika
kweli kweli, kunaonekana kuna jambo limejificha ndani ya familia yenu gumu sana
kulitatua, linahusiana na mambo mabaya….’akasema
‘Mambo
mabaya, kama yapi?’ akauliza shangazi
‘Hayo siwezi
kuyataja, ila inaonekana sheria inawaandama,kuna ukiukwaji wa sheria na
mlifanya hivyo awali wakati nyota yenu
inang’ara lakini sasa imeshafifia, …mna wakati mgumu sana wa kujisahihisha,..inabidi
muhangaike kwelikweli,sio mchezo hapo, kwangu mimi sina cha kufanya…’akasema
‘Kwahiyo
huwezi kutusaidia kwa hili?’ akauliza jamaa mwingine
‘Mhh,kiukweli,
siwezi kuingilia huko, kila kazi ina mipaka yake, mipaka yangu inaishia hapo,
huko kwenye sheria, uvunjasji wa sheria, na ….hapana, huko mimi siruhusiwi
kabisa kupagusa, nina mafungamano na masharti makali ya kazi yangu,...fanyeni
mlichoambiwa kabla hamjachelewa...mimi naondoka, sina muda tena hapa…’akasema
na kuanza kuondoka
Wanafamilia
walibakia wakiangaliana, na shangazi akasema;
‘Mnaona, kazi
iliyopo mbele yetu ni kubwa na tunatakiwa tufanye jambo kwa haraka, mimi
namfahamu sana huyu mtu, hasemi uwongo,na kama jambo halina muafaka, atawaambia
..’akasema shangazi
‘Kwa mtizamo
swala hili la ndugu yetu halina ujanja, ni swala la kisheria, basi mimi naona
tumuachie mwanasheria.....’akasema ndugu mwingine
‘Yeye afanye
kazi yake kisheria na sisi tuhangaike kivyetu, ….niliwaambia toka wali,sio
swala la kisheria tu, mumesikia wenyewe, ..., kazi imeshaanza, na
tusipojitahidi tutampoteza ndugu yetu hivi hivi, hatujui ni nani atafuata, ila
mimi sikubali,mimi nitahangaika juu chini...’akajipiga kifua kama kutamba.
‘Shangazi,...mbona
haya mambo ni ya kutisha,...mmh, ....’akasema mchumba wako.
‘Ni ya kutisha
kwa vile nyie vijana mnayapuuzia, ..., lakini nina uhakika haya yote ni mambo
ya mdada, na shetani lake, kama alivyosema mtaalamu kuwa nyota yake kwa sasa
ina nguvu, lakini kuna namna ya kuivunja
nguvu, nitakwenda kwa mtu mwingine….’akasema shangazi
‘Lakini
nilivyomsikia vyema huyu mtaalamu tatizo hapo ni uvunjaji wa sheria, ..mimi
naona muhimu ni kumuachia wakili apambane nalo sizani kama ni mambo ya
kishirikiana….’akasema mtu mwingine akimuangalia wakili, wakili yeye muda
mwingi alikuwa akisoma makabrasha yake.
‘Yeye afanye
kazi yake kisheria,na sisi……tutafanya yetu…’akasema shangazi
‘Mhh hapo
sielewi kitu, wewe shangazi unataka tufanye nini?’ akauliza mchumba wako
‘Kulipiza
kisasi kwa hawa watu, maana nila wao hili tatizo lisingelikuwepo, huyu mchumba
wako na mdada ni lazima tuwafanyizie…, lakini adui mkubwa ni huyo anayetaka
kukunyang’anya mchumba wako…’akasema
‘Mhh,mimi
naona mambo haya ni kuyatisha,hata mimi sasa naanza kuogopa, nina wasiwasi na
baba, sijui kafanya kitu gani kibaya, lakini baba ni mchapakazi, hataki utani,
sizani kama anaweza kuvunja sheria, …..’akasema.
‘Unaonaeeh,
mimi ndio hapa nasema ni lazima tufanye kazi..sasa nakuuliza kwa mara ya mwiho
je upo tayari kukosa yote, mchumba na wazazi wako, maana haitaishia kwa ndugu
yetu, itakuja na sisi sote wanafamilia, hebu niambie upo tayari kukosa yote...’akasema
shangazi na binti akainuka kama anataka kuondoka.
‘Unataka
kwenda wapi, tulia hapa, usitake kuharibu mambo…kama unapanga kwenda kuongea na
huyo mchumba wako, kuanzia sasa ni marufuku kuonana naye, hutakiwi kuongea na
huyo mtu kabisa, mpaka tumalize kazi yetu, unanisikia, huyo ni mbaya wako, ni
adui wa hii familia,tunatakiwa tupambanae naye na washirika wake,...’akasema
shangazi
‘Sasa
tufanye nini?’ akauliza jamaa mwingine
‘Kwasasa
niachieni hiyo kazi mimi…kazi ya kisheria ipo mikononi mwa mwanasheria,wakili
wa kaka atafuatilia, mengine yapo mikononi mwetu, kuna msaada nahitaji kutoka
kwanu, hasa wa kifedha, ikishindikana sina budi kuongea na kaka japokuwa sio
wakatii muafaka wa kuongea naye, ni azima niongee naye kinamna, nahitajia
msaada wake, ...’akasema
‘Msaada wa
kitu gani?’ akauliza mwanasheria akiwa kasimama akitaka kuondoka huku
akiangalia saa yake.
‘Ninachohitajia
kwa sasa ni pesa, pesa nyingi, kuna watu natakiwa kuwapa hii kazi, na hao watu
hawawezi kuifanya hii kazi kwa pesa ndogo, nataka pesa nyingi sana....’akasema
shangazi.
‘Unataka
wafanye kazi gani?’ akauliza wakili akimwangalia kwa mashaka…
NB: Haya
vita imeanza, kesi imeanza, je haya yataishia wapi
WAZO LA LEO:Ukweli unauma,hasa unapogusa masilahi
yetu,hakuna atakyekubali kuwa mali aliyo nayo ni ya ufisadi, hata kama ni kweli
kaipata kwa ufisadi au kwa njia ambazo sio za halalimtu kama huyu atatafuta
kila namna ya kuhalalisha ufisadi wake huo hata kama ni kwa kubadili mikataba
na kugeuza vifungu vya sheria vilivyopo, hata kama ni kwa kunukuu maandishi
matakatifu kwa namna ya kuhalalisha ufisadi wake huo, ...mara nyingi dhuluma hujaribiwa
kulindwa kwa dhuluma, lakini hala hala, dhuluma ikidumu sana, kinachofuata ni
maasi, amani inakuwa haipo tena, kwani
dhuluma haidumu ikidumu inadumirisha.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment