‘Mlinzi wa
mdada ameshakamatwa , yupo mikononi mwa polisi....’akasema mpelelezi,
nilipokutana naye tena, safari hii alikuja rasmi akiwa na kibali cha kuonana na
mimi.
‘Mhh,kakamatwa!
Alikuwa wapi?’ nikauliza
‘Amewaambia
polisi kuwa alipatwa na dharura ,alitumiwa ujumbe kuwa mtoto wake aliyekuwa
kijijini anaumwa, na bahati mbaya simu yake ikaibiwa, kwahiyo hakuweza
kuwasiliana na bosi wake, ...inawezekana alikuja na hadithi ya kutunga au ni kweli ilitokea hivyo,
polisi hawakutaka zaidi, nia yao ilikuwa ni kumkamata tu kwani wao kama wanavyodai,walishakuwa na ushahidi kuwa ndiye
aliyehusika na hayo mauaji ya mtoza ushuru.
'Na mlinzi huyo hakuwa na jinsi, akakamatwa na kumweka mahabusu, na baadaye kwa
haraka wakamfikisha gerezani sehemu yenye ulinzi mkali...’akasema
‘Oh, mbona
wamemfanyia haraka hivyo, inaonekana kweli wana ushahidi wa kutosha na hawataki
kupoteza muda, ...au kufanya makosa...’nikasema
‘Ndivyo
walivyosema, na hakutakiwa kuonana na mtu yoyote, hata wakili wake alizuiwa kwa
muda, na wakili huyo alikuja kuonana na mteja wake baadaye kabisa...’akasema
‘Hiyo sio
haki.....au sio?’ nikauliza huku nikishindwa kuficha furaha yangu moyoni kuwa hatimaye kesi yangu itakuwa imeshafutika kabisa.
‘Wakati
mwingine inabidi ifanyike hivyo, ili kupata taarifa nyeti,..kabla
hazijachaachuliwa, japokuwa kwa huyo mlinzi, walishachelewa, ....’akasema
‘Kwa
vipi,...wamechelewa kwasababu gani?’ nikauliza
‘Jamaa
alishajipanga, anafahamu aseme nini, na alishajua ni kitu gani polisi
watamuuliza, sizani kama wanajambo jipya dhidi yake, ....’akasema.
‘Kama ni
hivyo, kwanini sasa waseme kuwa wana uhakika kuwa ndiye aliyefanya hayo mauaji?’
nikauliza
‘Polisi ndivyo
wanavyosema, na wamesema safari hii hawataki utani tena ni lazima haki
itendeke,kwani wana ushahidi kamili wa kumbana huyo mlinzi,kuwa yeye ndiye
aliyemuua mtoza ushuru, na hawataki kumchelewesha, watamfikisha huyo jamaa
mahakamani haraka iwezekanavyo....’akasema
‘Hebu niambie
kwa uchunguzi wako wewe, je ni kweli huyo mlinzi ndiye aliyafanya hayo mauaji,
kwa uchunguzi wako wewe uligundua nini, hebu niambie ulivyoona wewe ilikuwaje
siku ile....?’ nikamuuliza
‘Jinsi
ilivyotokea, ukichunguza kwa makini ni tukio lililopangwa kwa utadi wa hali ya
juu, sio kwa bahati mbaya,.....huyu jamaa aliyekuja kumuona huyo mlinzi wa
mdada, alifika na kutoa amri, na mlinzi akatii bila kupoteza muda, ...kama
angeluwa hawajawasiliana au hawajuani, au ni swala la kupewa chochote,
kungelikuwa na maongezi ya kubishana ....lakini haikuwa hivyo,...’akasema
‘Pili huyu
mlinzi alipotoka pale getini, hakuingia ndani moja kwa moja, alichofanya yeye
ni kuelekea kwenye gari la mdada, na humo alijua kuna kitu gani ambacho
angeliweza kukitumia, japokuwa kulikuwa na vyombo vingine, lakini yeye
alichagua nyundo. Hii nyundo ina maana gani, ....’akatulia kidgo.
‘Siwezi
nikathibitisha hilo, kuwa huenda nyundo ilikuwa na maana fulani, lakini kwa
haya makundi kila jambo lina ishara zake, na baada ya tukio hilo, hiyo nyundo
ilitoweka, huyo mlinzi hakuwahi kuirudisha hapo, au kuonekana sehemu yoyote....Hapo
utaona kama ni kitu kilichokuwa kimepangiliwa, kwa namna fulani....’akasema
‘Unavyosema
alikuja huku kwenye maegesho magari, kauli yako inanifanya niwazie mengine, ni
kama vile upo kwenye hayo maegesho na huyo mlinzi akafika eneo hilo ulipokuwepo
wewe,hebu nifafanulie vyema hapo?’ nikauliza
‘Alipofika kwenye eneo la magari, akaingia
kwenye gari la mdada, ...akitumia ufungua bandia, akafungua mlango na kuingia
ndani ya hilo gari, alikaa kidogo, na kutoka akiwa kashikilia hiyo nyundo,
akaichomeka kwa nyuma, kama wanavyofanya watumia bastola...
‘Haraka
akasogea kwenye madirisha na kuanza kuchungulia ndani,...nahisi alikuwa
akihakiki usalama, na baadaye akatoa pisipisi,.....unaona kwenye ule mfuko,
alichukua na pisipisi, ambayo ndiyo aliyoitumia kupachulia kiyoo cha lile
dirisha, akasogeza kiyoo, nahisi hilo dirisha, lilikuwa halifungi vyema au
alishalilegeza kabla...’akasema
‘Akaingia
kwa kuruka dirishani,i...’akasema
‘Halafu
ikawaje?’ nikamuuliza
‘Sijui
yaliyotokea huko ndani...’akasema na mimi nikamwangalia kwa mashaka, nikauliza
‘Hebu
niambie ukweli, ...unavyoongea ni kama vile ulikuwepo kwenye tukio,...’nikasema
‘Ni
kweli...mimi nilikuwepo kwenye eneo hilo.....’akasema na kunifanya nibakie
mdomo wazi
‘Kweli, ina
maana ulikuwepo!!!....’nikamaka
‘Ndio maana
nikawa nakusisitiza useme ukweli,...kwani ukweli mwingi naufahamu, ...’akasema
‘Kama ni
hivyo, kwanini hukuwaambia polisi?’ nikauliza
‘Mimi
nafanyakazi kivyangu, ...lakini mwisho wa siku ni lazima yote hayo wayafahamu
polisi, kwa hivi sasa sijamaliza kazi yangu, bado nakusanya ushahidi wangu, kwa
kazi yangu maalumu.....’akasema
‘Wewe
unamfanyia nani hiyo kazi?’ nikamuuliza
‘Nchi
yangu....’akasema
‘Hata polisi
wanafanya kazi kwa ajili ya ncho yao au sio?’ nikauliza
‘Halikadhalika,.....
lakini kila mmoja ana malengo yake...’akasema
‘Hebu
niambai zaidi kuhusu huyu mlinzi, kwa jinsi alivyoipata hiyo silaha, ....hiyo nyundo?’
nikamuuliza.
‘Ni kama
nilivyokuelezea, aliipata kutoka kwenye gari la mdada....’akasema
‘Ehe....’nikasema
‘Japokuwa
mimi baadaye mimi nilipata nafasi ya kuingia kwenye gari la mdada na kuangalia
vyema, ndipo nikagundua mkoba uliokuwa na vifaa vya ujenzi, humo kulikuwa na msumeno,
misumari, na vifaa mbali mbali vya ujenzi, ina maana mdada, alikuwa kaviweka
hivyo vifaa kwa ajili ya kumpelekea fundi, ....’akasema.
‘Kwanini Polisi hawakuligundua hilo?’ nikauliza
‘Polisi wana
malengo yao na mimi nina malengo yangu totauti,...sio kila kitu ni muhimu kwao,
mimi nafanya kazi kwa undani zaidi kuhakikisha napata kiini cha haya matatizo,
ili ning’oe mti na mizizi yake, ...kwahiyo kazi yangu ni polepole na kwa
umakini zaidi,na kila kitu kilichotokea kwangu ni muhimu, ....’akasema
‘Lakini
huoni kwamba kama ungeshirikiana na polisi ungeliwarahishia kazi yao..’nikasema
‘Yah..ni
kweli, lakini kwa hali ilivyo, ni bora iwe hivi,...’akasema
‘Kwahiyo
uliona kabisa huyo mlinzi akiingia kwenye hilo gari na kutoka, akaingia kwenye
hiyo nyumba kwa kupitia dirishani na kutoka lakini hufahamu ni kitu gani
kilitokea huko ndani?’ nikauliza
‘Yah...huko
ndani nisingeliweza kufahamu maana mimi nilikuwa nje, na nilikuwa sehemu ya
kujificha, nisingeliweza kutoka na kuangalia huku na kule,...na ukumbuke baada
ya muda, polisi nao walishafika kwenye hilo eneo, kwahiyo mimi nilitakiwa
nitafuta mwanya wa kutoka hapo kwa haraka, sikupenda kukutana na hao watu, ...’akasema
‘Lakini ni
watu wa idara yako...’nikasema
‘Yah,
...hata kama ni watu wa idara yangu, lakini malengo yetu ni tofauti....’akasema
‘Kwahiyo wewe
ulimuona mlinzi wakati anatoka kutoka ndani ?’ nikauliza
‘Nilimuona
wakati anatoka, ..alitoka kwa njia hiyo hiyo aliyoingilia, akiwa na mfuko mkononi
kuonyesha kuwa kabeba kitu fulani, ....’akasema
‘Kitu cha
namna gani,..kwa mtizamo wako?’ nikauliza
‘Kitakuwa
sio kitu kikubwa,....nahisi inawezakana ikawa CD’s, au hivi vifaa vidogo vya
komputa vinaweza kubebe kumbukumbu nyingi..’ akasema
‘Kwahiyo
kumbe alijua ni kitu gani anakitafuta, ....kwani angelijuaje hicho kifaa?’ nikauliza
‘Huyo mlinzi
ameenda shule,...na anafahamu sana maswala ya komputa, ni fundi wa mambo mengi
sana, akiwa jeshini, alikuwa fundi mzuri, lakini kwa matatizo ya kiafya aliacha
kazi, akaenda kutibiwa, na aliporudi hakutaka kuendelea tena na kazi hiyo ya
jeshi, akawa mlinzi wa watu binafsi,....amefanya hiyo kazi sehemu mbali mbali,
na hakuwahi kufanya jambo lolote baya.....’akasema
‘Mhh,....nahisi
sio kazi hiyo ya ulinzi peke yake, nahisi ana kazi za siri...’nikasema na
mpelelezi akaniangalia kwa haraka na kusema
‘Seehemu
niliyokuwepo, ilinifanya nisione mengi, nilijaribu sana kuchunguza, lakini
sikuweza kupita kwa mbele ya nyumba, kwani kama ningelifanya hivyo, huyo mtu
aliyeachwa getini, angeliniona...’akasema
‘Mimi
najiuliza, wewe uliwezaje kuingia na kutoka
bila kuonekana ...?’ nikamuuliza
‘Kwa muda
mwingi,mimi nilikuwa nje...., na nilikuwa upande wa nyuma, niliingia kipindi
kile kile wakati mlinzi anaongea na huyo jamaa mwingine. Huyo jamaa alivyokuwa
amevaa usingeliweza kumtambua ni nani,...alikuwa kavaa kofia pana,
alilolishusha na kuficha uso,....na akavaa koti refu utafikiri anajikinga na mvua...’akasema
‘Unasema kwa muda mwingi ulikuwa nje ya hilo jengo,...kwahiyo
ulimuona huyo mtu akifika,...huyo mtu aliyeongea na mlinzi na wakafanya
waliyoyafanya, je huyo mtu alifika kwa
usafiri gani, kwa mguu au kwa pikipiki?’ nikauliza
‘Ndio
nilikuwepo hapo nje, nikijaribu kuchunguza mambo yanayoendelea humo, na nilishasikia
kuwa mdada ni mgonjwa,...na wewe umo humo ndani, ....’akasema
‘Kwahiyo
ulifika hapo kutaka kufanya nini?’ niamuuliza
‘Nilishagundua
kuwa kuna jambo linaloendelea hapo,...nilifika hapo nikimfuatilia mtoza
ushuru,...nilitoka naye mbali, akiwa anafuatiliwa na vijana wangu, na hadi
alipofika hapo...’akatulia na ilionyesha alikuwa akificha baadhi ya maelezo.
‘Wakati nipo
hapo nje, ndio akatokea huyo mtu, ambaye alifika bila usafiri wowote, alifika
akitembea kwa kujiamini tu, akafika kwenye hilo geti na kugonga mlango, na mimi
nikavutiwa naye, wka jinsi alivyokuwa amevaa, nikasogea, karibu, japokuwa
hawakuniona, nikawa napiga mahesabu ya kuweza kuingia humo ndani....’akasema
‘Ukawa unapiga
mahesabu ya kuingia humo ndani, ili ufanye nini, kwani ulishajua ni kitu gani
kinaweza kutokea,?’ nikauliza
‘Sikuwa
ninajua kuwa hayo yote yanaweza kutokea, ila mimi nilikuwa namfuatilia mtoza
ushuru, kujua ni kitu gani kilichomleta kwa mdada, ....na sasa akaja huyu mtu
asiyefahamika, nikahisi kuna kitu...’akasema
‘Sasa
uliingiaje humo ndani...?’ nikauliza
‘Yule mlinzi
alipofunguliwa mlango, yule jamaa akawa kasimama kwa muda kidogo, halafu
aaingia kwa ndani,wakawa wanaongea kwa muda mfupi tu, ni kiasi cha kutoa
maelekezo..mimi kwa haraka, nilisogea hadi pale mlangoni na kuwachungulia kwa
nje...
‘Yule jamaa
alipoingia, alisimama ndani, akiwa kanipa mgongo, na mlinzi akawa kasimama huku
kaangalia jengo, mlengo wa nyumba yam dada, ilivyoonyesha huyo jamaa ni mtu
muhimu sana kwa mlinzi, kwani mlinzi alionyesha kunyenyekea, kwa jinsi
nilivyomuona, kwahiyo hata ile akili ya kuangalia huku mlangoni haikuwepo kwa
muda huo...’akasema
‘Ok, kwahiyo
huenda ni bosi wake, au aliwahi kuwa bosi wake...’nikasema
‘Yawezekana...’akasema
‘Wakati
wanaongea, yule mlinzi kwa haraka akakimbilia kuelekea kwenye jengo, na mimi
nikasukuma mlango taratibu, na kupata upenyo wa kupita...nilimuona huyo jamaa
akiongea na simu, na muda huo alikuwa
akiangalia yule mlinzi anavyotembea kwa haraka kuelekea eneo la jengo, hapo
hapo sikupoteza muda, nikapita pale mlango kwa haraka, nikawa naambaa ambaa upenuni mwa michongoma,..
‘Kama huyo
jamaa angeligeuka nyuma, angelioniona, lakini nilicheza na bahati nasibu kuwa
hatageuka kwa haraka, na kweli ikawa hivyo, nikatembea hadi kwenye maegesho ya
magari nikajificha huko...na ndipo nikamuona yule mlinzi akifungua mlango wa
gari la mdada...
*******
Mlinzi
alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, na kusomewa mashitaka yake, na yeye
akayakana yote kuwa yeye hajamuua mtoza ushuru, kwa hiyo ikapangwa siku ya
kesi.
‘Sisi
tumeshakamilisha ushahidi wetu, hatuna shaka..’alisema muendesha mahitaka
alipoulizwa, na alipoulizwa mshitakiwa
kuwa ana wakili , yule mlinzi akasema
‘Ndiye
ninaye wakili wangu, lakini nashangaa kwa jinsi wanavymzuia kuonana na mimi,
...’akasema na hakimu akasema huyo mshitakiwa ana haki ya kuonana na wakili
wake, na muendesha hayo mashitaka akasema hilo linafanyika....
Kwahiyo
tarahe ya kesi ikapangwa,...
******
Wakati hayo
yanaendelea ndani ya familia ya baba mkwe, kulikuwa na kikao maalumu cha
wanafamilia, kwenye kikao hicho alikuwepo shangazi, mchumba wangu, na ndugu
wengine, na wakili wa baba mkwe na ndugu mmoja aliyetambulikana kama mtaalamu.
NB:Naona kama tunaingia kwenye hitimisho la kisa chetu, ...mahakamani, je haki itatendeka?
WAZO LA LEO: Mara nyingi madhalimu wanaogopa ukweli na haki, kwani katika ukweli na
haki madhambi ya ufisadi hayana nafasi, na ndio maana mara nyingi madhalimu,hutumia
nguvu nyingi, na uwongo na poropoganda potofu ndio sera zao. Lakini kwa
vyovyote iwavyo, miali ya nuru ya ukweli na haki itapenya kwenye giza nene la
dhuluma zao, na mwanga wa haki na ukweli utaleta matumaini kwa wanyonge.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment