‘Wewe
Mhasibu.....’nikasikia sauti ikiita jina langu, kwanza nikajifanya sikusikia,
lakini ile sauti ikaita tena , na safari hii kwa msisitizo.
‘Wewe
mhasibu ina maana hunisikii au unanizarau.....’ikasema hiyo sauti
Niligeuka
taratibu kwa kujihami na kumtafuta huyo aliyeniita jina langu, ilikuwa ni sauti
ya kike, na pale sauti ilipotokea kulikuwa na kina mama watatu na wanaume
wengine, wakiwa katika pilika pilika za biashara, na hao akina mama walikuwa
wakihudumia chakula, kuonyesha kuwa wanauza bashara ya mama Ntilie.
Nikajaribu
kukisia ni nani kati ya wale wawili aliyeniita , sikuweza kutambua, lakini
kabla sijachukua hatua nyingine mama mmojawapo akasema;
‘Nakuita
mara mbili unajifanya hujanisikia je unatokea wapi mwenzangu?’ akaniuliza huyo
mama, nikamwangalia kwa makini kama niliwahi kuonana naye kabla lakini sikuweza
kumkumbuka vyema nikaamua kumuuliza kabla sijamjibu swali lake;
‘Samhani kwani
wewe ni nani unayeniuliza hivyo?’ nikauliza nikiwa nimesimama nikimwangalia na
wale akina mama wengine walikuwa wakiendelea na shughuli zao, bila kujali
kinachoendelea kati yangu na huyo mama aliyeniita jina langu.
‘Ajabu
kabisa wewe unataka kumuoa binti yetu halafu hunifahamu, mhh, ni kweli kabisa
nilishawaambia wenzangu kuwa wewe humfai binti yetu, na hilo nimalisema baada
ya kufanya uchunguzi wangu mwenyewe, nikagundua kuwa kweli wewe hustahili kuoa
katika familia yetu...’akasema
‘Niliwaambia
kabisa wakufunge baada ya kumharibu binti yetu ili iwe fundisho, wakapinga
kabinti kakajifanya kanakupenda kipo wapi...na kaka naye akashinikiza kuwa
atakutumia kwa mambo yake,...hamna kitu
hapa....’akasema akinionyeshea kidole juu chini.
‘Sasa
unaonaeeh,a wanaanza kukumbuka ushauri wangu...’akasema sasa hivi akiwa
keshaondoka pale walipokuwa wenzake na kuja hadi pale niliposimama.
‘Sijakuelewa
mama, kwani wewe ni nani,.?’nikauliza sasa tukiwa tumeangaliana. Macho ya mama
huyo yalikuwa makali, hayaogopi aliniangalia moja kwa moja usoni bila kupepesa,
akasema;
‘Mhh
unajifanya hunifahamu eti,...basi kwa taarifa yako mimi ndiye shangazi wa
mchumba wako..’akasema na kunifanya niiname chini kwa aibu nikanyosha mkono
kumsalimia, lakini akanipuuzia, hakunyosha mkono kabisa akawa kaangalia pembeni
na mimi nikasema;
‘Oh, samanahani
shangazi, mimi nilikuwa sikufahamu, hatujawahi kuonana kabla, unisamehe sana....’nikasema
nikijibaragua lakini yeye akakunja uso kwa hasira na kusema;
‘Hebu
niambie ina maana binti yetu hakuwahi kukuambia kuwa hapa mjini yupo shangazi
yake, na ulipoambaiwa hivyo, kama kweli ulikuwa na nia njema ya kumuua, natumai
ungenitafuta....’akasema
‘Kwakweli
Binti, hakuwahi kabla kuniambia hivyo, sikumbuki kabisa kusema kuwa kuna
shangazi yake huku mjini....’nikasema
‘Haya
alipokuja hapa mjini, hakuwahi kukuambia kuwa yupo hapa na anaishi kwa shangazi
yake?’ akaniuliza
‘Ni kweli
safari hii aliniambia hivyo lakini..’nikasema nayeye akanikatisha na kusema
‘Na
uliposikia hivyo ukawa kimiya, hukutaka hata kuja kunisalimia, kwasababu
unanifahamu kuwa nakutambua kwa tabia zako chafu, pinga kama huna tabia chafu
za ulevi na uhuni...’akasema.
‘Shangazi,
nilipolijua hilo, nilitaka kuja kuonana na wewe lakini ndio kipindi nilikuwa
kwenye matatizo, ’nikasema.
‘Matatizo ya
kujitakia mwenyewe, ...unajua nyie
vijana mnauingia mji kwa pupa mnatuhribia amani, mnakuja na tabia zenu chafu na
kuanza kuiga hata yale yasiyofaa,...nikupe ushauri wa bure, ukiingia mji hebu
jaribu kuulizia wenzako waliotangulia jinsi gani maisha hapo yalivyo ....’akasema
na mimi nikatulia kimiya , alipoona hivyo akasema;
‘Hivi wewe
katika wasichana wote, .....mdada, ndio uliona anakufaa, kuondoa tamaa zao za
kimwili...?’akaniuliza na mimi nikashituka kidogo na kusema
‘Kwanini
unasema hivyo shangazi, huyo unayemtaka ni mfanyakazi mwenzangu tu...’nikasema.
‘Haloooh,
mfanyakazi mwenzako eeh,, ...sawa anaweza akawa mfanyakazi mwenzako, kazi na
dawa sio, hahahaeeh , mimi hunidanganyi kitu, jinsi mlivyokuwa mnachukuana
mnaingia hapo hotelini, mankunywa, mpaka mnapitiliza na siku nyingine kulala
humo humo nilikuwa nawaona....’akasema.
‘Mhh hapana
sio hivyo shangazi, tulikuwa tunafika kwa maongezi, na wakati mwingine kuna kazi
tunafanya...’nikasema
‘Kazi za
usiku eeh, mumekuwa umiani, eeh, hahaha, hivi unaniona mimi mtoto mdogo eeh, haya hebu niambie una mpango gani na binti
yetu?’ akaniuliza kinigusa kwa kidole kifuani, na kunifanya nirudi nyuma
kidogo, nikasema;
‘Mbona kila
kitu kipo wazi shangazi, ....’nikasema nikiwa sasa nanyenyekea
‘Unafahamu taratibu
na mila za kabilazetu, na sio kabila letu tu, ni karibu mila nyingi za
Kiafrika, shangazi na mjomba ndio watu muhimu katika maswala ya kifamilia hasa
ya ndoa,..mimi usinione napika mama Ntilia hapa, ukanizarau nina biashara
nyingi tu, leo nipo hapa kesho nipo kwenye shughuli nyingine, nina watu
nimewaajiri, lakini hata hivyo, siwezi kukaa na kukunja nne, bila
kujishugulisha, nafanya kwa vitendo ili kuwaonyesha wafanyakazi wangu kuwa kila
kazi naifahamu, kwahiyo usinizarau kabisaaah...’akasema
‘Sijakuzarau
shangazi....’nikasema
‘Nimekuwa
nikikufuatilia nyendo zako hatua kwa hatua, na ndio maana niliwaonya ndugu
zangu kuwa tunampotezea binti yetu muda wake, na hata leo wakiniuliza kuwa wewe
unafaa kuwa mume mwema wa binti yetu, nitasema hufai, niulize kwanini’akasema
‘Kwanini
shangazi?’ nikauliza
‘Kwanza huna
msimamo, mnafiki mkubwa wewe, ....wewe ni wale wanaume wasiojua kusimamia
familia zao, na ni rahisi kurubuniwa... na kwa kuthibitisha hilo, angalia ni
janga gani uliloliingiza kwenye familia yetu,....’akasema
‘Shangazi
mbona mimi sijakuelewa....’nikasema kujitetea
‘Hujanielewa,
si ndio maana nikasema wewe ni wale wanaume bwege, wasio na msimamo, unajua
wewe sasa hivi umechangia sana kuiharibia familia yetu na maisha yetu, pamoja na kaka yangu kujitolea
kwa hali na mali kukusaidia wewe kukutafutia kazi, hebu angalia malipo yake,
hivi wewe unataka ubebwe vipi....’akasema
‘Mimi
nimefanya nini kibaya shangazi ...’nikasema nikiangalia saa yangu
‘Kaka yangu
sasa hivi anaumwa, yupo mahututi, kapatwa na gonywa la kiajabu ajabu, ghafla
kadondoka chini, kapoteza fahamu, mara
mwili mzima hauna nguvu kabisa , niliwaambia wewe ni muumiani umekuja kunywa
damu zetu , utatumaliza mmoja baada ya mwingine
, sasa wanaanza kuona,...chanzo ni wewe na kundi lako..’akasema
‘Shangazi
mbona mimi sina habari na hilo...’nikasema
‘Huna habari
na nini?’ akaniuliza
‘Kuwa baba
mkwe anaumwa...’nikasema
‘Uwe na
habari usiwe na habari, kwani kinakuuma nini , wewe siuonaona umepata, wajinga
ndio waliwao, au sio...?’ akawa kama anauliza
‘Sasa
sikiliza kama mumeamua kufanya hivyo, ujue na sisi hatujalala, tutapambana
chini na juu, siunafahamu kabila letu lilivyo eeh, ...sisi hatuogopi,
tunapambana ana kwa ana, mimi mwenyewe, sitalala mpaka nihakikishe na nyie
mnakumbana na shughuli nzito, na utanifuta ..wewe siunajifanya kijogoo, tutaona
kama bakora yako itaweza kazi , tupo....’akasema na kugeuka kurudi kwa wenzake.
Mimi
nilibaki nimeduwaa kwa muda halafu nikaangalia saa nikaona nimezidi kuchelewa,
nikageuka kumwangalia yule mama, lakini hakuwepo tena kwenye lile kundi,
nikaona nisizidi kupoteza muda nikageuka na kuanza mwendo wa kurudi hotelini.
Nilitumia
njia ile ile ya kificho na kuingia ndani huku nikijiuliza maswali mengi
kichwani, na sikujua kabisa nifanye nini,...
‘Huu sasa
msala , naona nikifika ndani cha kwanza ni kumpigia simu mchumba wangu nijue ni
kitu gani kinachoendelea...’nikasema nikiharakisha kuelekea kwenye chumba chang
***********
‘Niambie
unatoka wapi?’ sauti ikanishitua pale nilipofungua mlango wangu na kuingia kwenye
chumbani ninapoishi hapo hotelini, ni chumba kikubwa chenye kila kitu, kwa
kipato changu nisingeliweza kumudu vyumba vya hadhi hiyo.
Niliposikia
hiyo sauti, nilishituka karibu nidondoshe ufunguo, nikageuka na kumuona mdada
akiwa kakaa kwenye sofa kakunja nne, akiwa kabadili muonekano wa nywe zake, na
alikuwa akifanya kitu kwenye simu yake.
‘Oh, umeingiaje
humu ndani na .....?’ nikauliza nikiwa nimeshikilia ufungua wa hicho chumba, na
yeye akabetua mdomo bila kuniangalia, alikuwa akiandika kitu kwenye simu yake,
na alipoamaliza akasema;
‘Hilo sio
swali la kuniuliza, unafahamu fika mimi ndio mdhamini wako mkubwa, na zaidi ya
hapo mimi ndiye mtarajiwa wako.....hahaha, nikitaja hivyo, mtarajiwa,
unajifanya kushituka, usijifanye hulitaki hilo, kama moyo wako uneglifungulia
ni wazi kabisa ungenionyesha mimi, kuwa ndiye chaguo lako, nasema uongo...?’
akaniuliza akiniangalia kwa uso unaoonyesha kuwa hataki mchezo.
‘Hayo
unasema wewe...hata kama ni hivyo, lakini ujue mimi nina mchumba wangu, ambaye
ni mama wa mtoto wangu , unafikiri mimi hapo nitafanya nini...’nikasema
‘Kwa
minajili hiyo, ujue kabisa kuwa mimi ninaweza kuingia humu ndani wakati wowote
nitakavyo,...’akasema akiwa anacheza miguu yake na safari hii akiniangalia moja
kwa moja usoni. Na nikawa kimiya, nikiwa nacheza na ufungua mkononi akauliza
‘Haya
niambie umetoka wapi, toka muda wote huo?’
‘Nilitoka
kidogo..kupoteza mawazo...’nikasema
‘Kwanini
hukuniambia unataka kutoka..ki-do-go
kupoteza mawazo, kwani ningekukataza, lakini ni muhimu nifahamu ili nijue
jinsi gani ya kuhakiki usalama wako...’akasema huku akiyatamka maneno hayo kwa
mzaha
‘Hamna
shida, mimi nilijiamini kuwa hakutakuwwa na baya lolote, nimechukua tahadhari
zote...’nikasema
‘Niambie
ulikwenda kuonana na nani?’ akaniuliza akibadili sauti na kuongea kwa sauti ya
ukakamavu.
‘Nimesema
nilitoka kwenda kupoteza mawazo, sio kwenda kuonana na mtu, sikuwa na lengo la
kuonana na mtu...’nikasema
‘Sikiliza,
....mimi sio mjinga, nafahamu kabisa kuwa ulitoka hapa kwa minajili ya kuonana
na mtu, niambia ni nani huyo uliyekwenda kuonana naye, na kwanini hukutokea
mlangoni,ukatoka kwa kujificha?’ akauliza
‘Sikutaka
mtu afahamu kuwa nimetoka, ni kwa usalama tu, nilifanya hivyo kwa ajili ya
kuchukua tahadhari...’nikasema
‘Ninataka
kumfahamu huyo mtu uliyekwenda kuonana naye ni nani.....’akasema
‘Nimesema
sijatoka kuonana na mtu, ...’nikasema
‘Usitake
kunichanganya.....unasikia, unafahamu kwanini ninayafanya haya yote, ....,mimi
najitolea kwa ajili yako, bado unafanya mambo kinyume na makubaliano yetu,
...kama usiponiambia huyo mtu, nitahakikisha nayaweka machafu yako hadharani,
na unafahamu ni kitu gani kitafuata baada ya hapo..’akasema
‘Kwanini
unalazimisha kuwa kuna mtu nilikwenda kuonana naye, kwanini huniamini, au kuna
jambo jingine una wasiwasi nalo....’nikasema na yeye akatembea hatua mbili
kunikaribia na kama vile kasahau jambo akageuka na kunipa mgongo, akasema;
‘Ni
kwasababu nina uhakika kuwa kuna mtu alikuita mkaonane naye, ....ila
sijamfahamu ni nani, katumia namba ya kibandani, nitamfahamu tu, lakini kwanini
usiniambie ukweli, kwanini wewe unakuwa mgumu kuelewa....’akasema na mara simu
yake ikaita..’akaipokea na kusikiliza kwa muda, halafu akageuka na kuniuliza
‘Huyo
mwanamke uliyekuwa ukiongea naye ni nani?’ akaniuliza
‘Ni shangazi
ya mchumba wangu....’nikasema
‘Mlikuwa
mkiongea nini na yeye huyo mwanamke mwanga?’ akaniuliza
‘Alikuwa
kiniuliza msitakabali wa ndoa yangu na mchumba wangu....’nikasema
‘Wau
wau..mstakabali wako na mchumba wako, bado neno mchumba wako lipo moyoni, bado
hujanielewa, anyway, haina haja kwa
sasa maana familia hiyo sizani kama inakuhitajia tena baada ya hayo
yaliyotokea, sizani kama watakupokea kwa mikono miwili....’akasema
‘Kwanini
unasema hivyo?’ nikauliza
‘Kwa taarifa
yako tu, wenzako hao wameshakutenga...sasa hivi wewe kwao ni adui namba
moja....’akasema
‘Wenzangu
akina nani?’ nikauliza
‘Usijifanye
kuwa hufahamu, baba mkwe wako yupo taabani, hali yake ni mbaya sana, na kauli
yake ya mwisho kabla hajapoteza fahamu ni kuwa wewe umemsaliti....umekuwa
upande wa maadui zake,...na hayo aliyaongea mbele ya binti yake,na binti yake
akaapa kulipiza kisasi kwa lolote litakalotokea kwa baba yake, na sasa hivi
wameitana kikao, ....’akasema
‘Kwanini ,
kwani mimi nimefanya nini?’ nikauliza
‘Ndio maana nataka
nifahamu nyendo zako, ulipotoka hapa zaidi ya huyo shangazi uliongea na nani
mwingine?’ akaniuliza
‘Hakuna mtu
mwingine niliyeongea naye....sikuwa na haja ya kuongea na mtu, nilikuwa na
mambo yangu kichwani ya kutafakari...’nikasema
‘Nitakuja
kulifahamu hilo...ila kwasasa, nahisi cheo ulichoahidiwa kimeota mbawa,na
huenda ukajikuta ukikamtwa tena kwa kosa lile lile...japokuwa kuna utata
mwingine umejitokeza, ...’akasema
‘Utata
gani?’ nikauliza nikifikicha macho yako maana akili ilikuwa sio yangu mambo
yanatokea mengi wa wakati mmoja mpaka kichwa kinashindwa kuhimili, mdada
akaniangalia kwa makini akiwa katulia , akaangalia simu yake baada ya ujumbe
kuingia, akausoma, halafu akasema;
‘Mlinzi
wangu kapotea siku ya pili sijamuona,...na polisi wanamtafuta, inavyosadikika ni kuwa, kumbe ndio yeye aliyeingia ndani na huenda ndiyo yeye aliyefanya hayo yote,
akishikirikiana na mtu mwingine, huyo mtu mwingine alikuwa kabakia getini, sasa huyo mtu
mwingine ndiye kitendawili...’akasema
‘Ni nani
huyo mtu mwingine,na huyo mlinzi kaenda wapi?’ nikauliza
NB: Mengi
yanaanza kujitokeza, na mwisho wa yote ni ukweli kujulikana,kwani kile chenye
mwanzo hakikosi kuwa na mwisho tupo pamoja
WAZO LA LEO: Utajiri na mali sio kila kitu,
utaji na mali ulivyovichuma kwa dhuluma vinaweza kugeuka kuwa silaha ya
kulipiza kisasi kutokana na dhuluma zako. Vilio vya wale uliowadhulumu, vinasikiwa
na kisasi kinakuja kutoka kwenye mali yako mwenyewe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment