Mdada alipoingia
alipiitiliza hadi kwenye kiti kirefu, anapokaa bosi wa hiyo ofisi, akakaa na kuanza
kujizungusha kwenye kile kiti, utafikiri yupo ofisini kwake, alifanya hivyo
mara tatu, na wote tukawa tunamwangalia yeye, na alipoona wote tunamwangalia
yeye, akatulia na kusema;
‘Jamani
ubosi mnzuri, au vipi mhasibu, kwanza nikupe hongera zako mhasibu,unaona mambo
yalivyo eeh, sasa usahahu fadhila ....’akasema
‘Tuanzeni muda
ni mchache sana....’akasema yule wakili waliyeingia naye huku akifungua
makabrasha yake na huku akimtizama mchumba wangu kwa mashaka, na mdada alipoona
hivyo naye akamtupia jicho huyo mchumba wangu, halafu akachukua mkoba wake.
Kwenye ule
mkoba wake, alitoa simu yake, na akapiga namba akawa anaisikilizia, ilionekana haijibiwi au ana maana yake kufanya hivyo, alisikiliza hivyo kwa muda, huku
akiwa kaangalia pembeni muelekeo wa dirisha huku akiwa kaweka miguu yake mmoja
juu ya mwingine.
‘Ok, tupo
tayari...’akasema baada ya kusikiliza
hiyo simu kwa muda bila kusema neno, halafu akaizima ile simu na kutugeukia
huku akibenua mdomo, na kusema kwa sauti ndogo;
‘Mambo
yameiva....mzee mzima anaumbuka kiutu uzima, hakuna jinsi, ok, mimi nipo
tayari...’akagauka na kutuangalia mmoja baada ya mwingine, halafu akageuka
kumwangalia mchumba wangu, na kusema;
‘Kwanza
kabla hatujaanza, natumai, huyu mwanamke hastahili kuwemo humu ndani...’akasema
akiniangalia mimi huku akionyesha kidole kwa mchumba wangu.
‘Ndio
anaondoka hamna shida, ...’nikasema nikimuangalia mdada kwa mashaka, maana ile
sura aliyoionyesha sio ya kawaida, alikuwa kama askari akiwa kwenye mapambano, na
mchumba wangu aliposikia hivyo, akasema;
‘Kwanini!!
kwani mimi sistahili kuwemo humu,kuna ubaya gani ....?’ akauliza mchumba wangu.
‘Niambie
sababu za kuwepo kwako humu ndani,...’akasema mdada
‘Kwani wewe
hujui...’akasema mchumba wangu akiweka mguu mmoja juu ya mwingine,na kushika
kidevu kwa zarau.
‘Mimi sijui,
ndio maana nakuuliza je, una sababu gani za msingi za kuwemo humu ndani, je
unafahamu ni kitu gani tunataka kukiongelea...?’akasema mdada kama anauliza.
‘Yanayoongelewa
humu yanamhusu mchumba wangu, nina haki ya kuyafahamu....’akasema na mdada,
akamwangalia huku akitabasamu, halafu akaniangalia mimi, halafu akageuka
kumwangalia mchumba wangu, na kusema;
‘Hayo ya
uchumba wako, ni huko nje, sio hapa,hapa tuna mambo muhimu sana na nyeti, ...nakuomba
usipoteze muda, kazi huko imeanza, usitake tukaharibu....tafadhali toka, ili tupate
nafasi ya kuongea mambo nyeti....’akasema
‘Mambo gani
nyeti ambayo yanamuhusu mchumba wangu, na mimi sistahili kuyasikia, au una lako
jambo....’akasema mchumba wangu.
‘Mchumba
mchumba.....hahaaaae, kweli masikini akipata matako hulia mbwata,...unajiona
ukitamka hivyo,..ok, ngoja sisi tuongee, tukimaliza kama bado unahitajia
kuongea na mtu wako, basi mtaongea tu, lakini kwa sasa haya tunayotaka kuongea
hayakuhusu, tafadhali, naomba nakuomba utoke kwa amani, nakuomba ten asana, unielewe
hivyo,au sio wakili, ninafanya makosa kumtoa huyu mtu, niambie...?’akasema
mdada kwa sauti ya utulivu, na kumgeukiwa wakili, na wakili akasema;
‘Ni kweli
kwenye ajenda zetu hatuna mtu mwingine, mimi naona ajabu yeye kuwepo, sijui
labda tumuulize mhasibu, kwanini ameongeza mtu bila ya kutufahamisha, kwani
hiki kikao ni rasmi, kina wajumbe wameorodheshwa hapa, hatuwezi kuongeza mtu
bila utaratibu, ....’akasema na kuniangalia mimi.
‘Anaondoka
jamani, .....’nikasema nikimuashiria mchumba wangu asimame , aondoke, lakini
hakutaka haat kuniangalia, macho yake yalikuwa kwa mdada
‘Kwanini
mnifukuze, na huyu mwanamke ananifukuza mimi, yeye ni kama nani?’ akauliza
mchumba wangu
‘Siwezi
kukueleza mimi ni kama nani, haina haja,na hata nikikuambia hutanielewa, maana inavyoonekana
umeshajenga hisia fulani kichwani mwako,ambazo hazina maana kwa sasa, cha
muomuni ni wewe kutii sheria, kama alivyosema wakili, au sio jamani ..?’ akawa kaam anatuuliza na mimi
nikamwangalia mchumba wangu lakini yeye hakutaka hata kuniangalia mimi.
‘Msipoteze
muda wenu, endeleeni, kama hataki kuwa mshiriki wa kuongea, basi mimi
nitasikiliza tu...’akasema
‘Mbona
huelewi....wewe mtu ni wa wapi,tunakuomba tafadhali utoke nje, tuna mambo
makubwa ya kujadili hapa, ...’akasema na mchumba wangu akakaa vyema, na kuweka
mikono kifuani kama vile hasikii. Mdada akaniangalia kwa macho ya kushangaa na
kusema;
‘Hivi ni
nani alimleta huyu mwanamke humu ndani, mhasibu umemuokotea wapi huyu mtu,
mbona mkaidi hivi, tutafika hivi kweli, tufanye mambo kienyeji enyeji tu...?’
akauliza mdada akiniangalia mimi.
‘Aliruhusiwa
na waheshimiwa aje anione,...na tumeshaongea, na alikuwa mbioni kuondoka
....’nikasema
‘Waheshimiwa,
waheshimiwa, ....ok, sasa...?’ akawa kama ananiuliza
‘Ndio
tulikuwa tunaagana na nyie mkaingia...’nikasema
‘Basi kama
ni hivyo,natumai mumemalizana au sio..., anaweza kuondoka, au kama bado mnataka
kuagana rasmi, basi inuka, muagane kimahaba,
labda ndivyo anavyotaka, na kama bado mna mazungumzo yenu sisi tuondoke, mkimaliza
mtatuita...’akasema mdada akitaka kusimama na kumwangalia wakili.
‘Tumeshamaliza
kuongea, anaondoka....’nikasema nikimuangalia mchumba wangu ambaye alionyesha
kama hatusikilizi. Nikasema;
‘Tafadhali,
Binti, nakuomba uondoke, tutaongea zaidi baadaye...’ nikasema na mdada
akaniangalia halafu akamuangalia Binti, na binti akamuangalia mdada kwa macho
yaliyojaa hasira, zarau na chuki ya wazi, na kusema;
‘Mnapoteza
muda wenu bure, nimeshasema humu ndani sondoki,....kwani nikisikiliza hayo mnayoyaongea
kuna ubaya gani?’ akauliza akimuangalia wakili na wakili akawa kimiya tu.
‘Kwasababu
tunayotaka kuongea yameshapitishwa kuwa waongeaji ni kadhaa, na wameandikwa
tayari kwenye ajenda za hiki kikao, ni mambo ya kisheria, sio ya kienyeji
enyeji, sio tunajitungia, ....kwa kifupi hayakuhusu, tafadhali ondoka...’akasema
mdada, sasa kipandisha sauti na kuniangalia mimi
‘Hebu
mwambie huyu mtu wako atoke nje...’akasema mdada
‘Wewe
mwanamke, usianze kunichefua, sio mtuu-
waake, mimi ni mchumba wake..unasikia, kama ulikuwa hufahamu vyema, elewa
hivyo, mimi ni mchumba wake wa halali, na ni mama wa mtoto wake...’akasema na
wakili akasema;
‘Ni muhimu
ukaelewa taratibu za vikao kama hivi, kuna wahusika wameshaainishwa kwenye
makatasi yetu haya ya ajenda ya hiki kikao, kuwa mimi kama wakili nitaongea na
nani, ....sasa wewe haupo kwenye muhutasari wetu, sio kwamba unafukuzwa tu,
bali ni taratibu, na unapoakaidi, unavunja sheria, utakuwa unaleta vurugu za
kikao halali...’akasema wakili kwa sauti ya busara.
‘Lakini wewe
kama wakili unaweza kuja kuandika baadaye kuwa na mimi mchumba wake,
nilikuwepo, hakiharibiki kitu hapo, maana kuna mambo nimeona yanayokwenda
kinyume, kuna mbinu zinatumika kumuingiza mchumba wangu kwenye matatizo, na
mimi nimeshazifahamu hizo mbinu, ni
lazima niwepo nisikie kila kitu...’akasema
‘Sawa
tumekusikia kuwa wewe ni mchumba wake, haijalishi, chema hujiuza na kibaya
hujitembeza su sio...lakini hata hivyo hata kama ungelikuwa ni mke wake hapa huna
maana kwetu, kuna taratibu zimeandaliwa, kama ungelihitajika ungeliambiwa,
nikuambie ukweli, ..waliochumbiwa au
wake za watu hawahitaji kusema...’akasema mdada na kumfanya mchumba wangu
amuangalie kwa jich baya na kusema;
‘Nyie ndio
wezi wa waume za watu, badala ya kuhangaika kutafuta wanaume wenu mnakimbilia
kuiba waume za watu, unaonyesha kabisa jinsi ulivyo, aongee huyu wakili
nitamsikiliza lakini sio mwanamke kama wewe, asiye na haya kabisa.....’akasema
mchumba wangu akimwangalia mdada juu chini kwa macho yaliyojaa hasira.
‘Kwanza kwanini
hujiulizi, kwanini uibiwe eti mume wako..hujiulizi hilo swali, ni kwanini
itokee hivyo, ...’akasema mdada.
‘Si
umemlaghai kwa uhuni wako, na madawa ya kumpumbaza....’akasema mchumba wangu .
‘Nikuambie
ukweli,...ni kwasababu hujui wajibu wako,nyie ndio mkipata wanaume, mnaona
mumefika, mnashindwa kuonyesha ni nini mwanamke afanye kwa mwanaume wake, mume anakuchoka
mapema, na basi akimuona mwanamke wa nje anayejua wajibu wa mke kwa mume,
anakuona wewe tena huna maana,matokeo yake nini, na huko,kuishia kulalamika, naibiwa
naibiwa..., mtaibiwa sana, nikuambie ukweli,kama ungelikuwa unajua wajibu wako
usingelizungumza hayo, ...’akasema mdada
‘Unaongea
nini hapo wewe, wajibu, wajibu, wajibu gani ambao mimi siujui, ..na wewe utajuaje
huo wajibu wa mume wakati hujaolewa,....hujui hata adabu za kuwa na mchumba au
mume, wewe unachojua ni uhuni tu, hebu jiulize,umri kama huo hujaolewa,
unasubiri nini, ni kwa vile una tabia mbaya...’akasema mchumba wangu na mdada
akamwangalia wakili , halafu akaniangalia mimi
‘Jamani huyu
mtu anatoka au sisi tutoke...maana sasa anataka kuharibu hali ya hewa’akasema mdada
akiniangalia mimi, na mimi nikamshika mkono mchumba wangu, lakini mchumba wangu
akaupachua na kusema;
‘Unaona
anaanza kunitukana, mimi nimeharibu hali ya hewa, ...unaona wewe wakili, hizo
ni kauli gani, sasa sitoki, naona anataka tuanze kupashana, .kwanza huyu
mwanamke ni malaya, ni mlaghai, pili anavunja ndoa za watu, na tatu, ni muuaji,
mwanga mkubwa...kazi yake kuua watu na kuwapakazia wengine...hiyo ndio tabia
yako wewe mwanamke, unisikie sana, ikuogopi, na nipo tayari kwa lolote lile...’akasema
akiwa sasa kasimama.
‘Umemaliza
eeh, kama umemaliza nakuomba uondoke...’akasema mdada mdada sasa akiwa kamkazia
macho mchumba wangu
‘Bisha kama
sio wewe uliyemuua huyo mtoza ushuru, ukatumia mbinu ionekane huyu mhasibu
ndiye kafanya hivyo, unabisha...wewe ni mwanga ukishirikiana na mashetani
yako...unabisha kama huna shetani linalokusaidia kuwahadaa wanaume, kuvunja
ndoa za watu, kila mara linahitaji damu za watu, sijui mpaka sasa umeua watu
wangapi,...unatumia hadaa za kujiremba remba uonekane mrembo , una urembo gani
wewe, kujichubua tu, ili kuwalaghai waume za watu....bisha kama sio kweli’akasema
‘Huna
unalolijua wewe, nenda kijijini kalime....’akasema mdada, sasa akijaribu
kutuliza hasira zake.
‘Sawa kilimo
ni jadi yetu siwezi kukataa, huko ni kwetu ndipo nilipokulia, hamna shida
nitakwenda kwa waati wangu, lakini na wewe uhuni ndio kazi yako, kuiba wanaume
za watu ndo jadi yako,...ikishindikana unaua, ili shetani lako lipate
kufurahia, mwanga mkubwa wewe,mimi
nikuambie ukweli,utaua lakini mwisho wa siku na wewe utakufa tu...’akasema
mchumba wangu akiwa kasimama, alionyesha kukasirika, na nilihisi kama hali
isipotulizwa lolote linaweza kutokea.
‘Hahaha, sasa
naona unakwenda mbali....wakili, hebu, niambie nikichukua sheria mikononi mwangu
hapa nitalaumiwa,....’akasema akimwangalia wakili, na wakili akageuka
kuniangalia mimi, na mimi nikamwangalia mchumba wangu kwa hamaki, na mdada
alipoona hakuna linalofanyia, akavuta kiti nyuma, na kusimama, akasema
‘Hivi wewe
mwanamke unanifahamu mimi, ...nimekuvumilia sana...’akasema mdada, akiinuka
kwenye kiti...na mimi nikaona sasa hapo linazuka balaa jingine, nikamshika
mchumba wangu mkono, na kuanza kumvuta kumtoa nje, ilikuwa kama kuvutana hadi
akasalimu amri. Namfahamu sana huyu binti, huwa hakubali kirahisi kushindwa.
‘Niache aje,
tupambane, haniwezi kabisa huyu malaya wako...kwanini unanishika...kamshike
huyo malaya wako, ...’akasema na mimi
nikatumia nguvu mpaka nikamtoa nje, na tulipofika nje, nikaanza kumuongelesha
‘Sikiliza
unachofanya wewe hapa ni vurugu, ni kuniharibia jina langu, na kwa hali kama
hii, mimi sitakubali, siwezi kuambiwa nimeoa mke asiye na tabia
nzuri...’nikamwambia
‘Kwahiyo
unataka kusema nini, kuwa mimi sina tabia nzuri, nafanya haya kukusaidia mtu
kama huyo hatakiwi kubembelezwa, namfahamu sana, nimemuota sana, huyo mwanamke
ni mwanga, atakuangamiza...sasa wewe unataka kusema nini, unamtetea?’
akaniuliza akiniangalia kwa wasiwasi
‘Ondoka
nenda nyumbani, rudi kijijini tutawasiliana...’nikasema
‘Hivi kweli
wewe unanijali mimi, badala ya kuwa upande wangu, unanifukuza, kwanza umepata
cheo, unatakiwa uwe na mimi wakati unasimikwa,unalifahamu hilo,....au hulijui kuwa
wakati unapewa majukumu na mimi nahitajika kuwepo kama msaidizi wako,ndivyo
wanavyofanya wenzako, ni lazima uonyeshe uungwana kuwa una mtu wako,
....’akasema
‘Lakini kwanini
unafanya hivyo, na hata kama ni hivyo, wewe ni mchumba wangu tu, hatujafunga
ndoa bado...’nikasema na kauli hiyo inaonyesha ilimkera, akaniangalia kwa jicho
baya na kusema;
‘Hatujafunga
ndoa eeh, lakini umenizalisha, hiyo ina maana gani, nakushangaa sana, kusema
maneno kama hayo,...badala ya kuniunga mkono, tukamkomesha huyo mwanga, unanifukuza
eti nirudi kijijini, kumbe ni kweli eeh, .....’akasema
‘Ni kweli
kuhusu nini?’ nikamuuliza
‘Kuwa huyo
mwanamke anakuendesha kama gari bovu,..keshakufukiza madawa, hujielewi kabisa,
hapo ulipo, kila anachosema yeye wewe huna ujanja unakubali tu, angalia kafikia
hadi kukuweka jela, na kesi haijaisha bado unazidi kuwa mtumwa wake...hiyo kesi
haijaisha kabisa wameifunika tu, ili upate hiyo kazi, wasema ndicho ulichokuwa
ukikitaka, umuue, ili upate hiyo nafasi....’akasema
‘Sikiliza
hayo ni maneno ya watu hayana msingi, mimi nakuomba urudi kijijini utulie huko
huko,nitakuja huko tutaweka haya mambo sawa,...ukiwa hapa mjini, nahisi
mtagombana sana na huyo mdada, na sipendi kashifa kama hizo...’nikasema
‘Umeoanaeeh,
kuwa tutagombana na huyo mdada, ni kweli tutagombana kiukweli, mpaka umuambie
mbele yangu kuwa hana lolote, mimi ndiye mchumba wako wa halali, ....kwanza
jiulize kwanini tugombane naye kwa vile ni mke mwenzangu au sio?’akaniuliza
huku akiwa kashika kiuno
‘Nani kasema
mambo ya mweka mwenzako hapa, mbona hunielewi,....sikiliza sasa naongea kwa
mara ya mwisho, ondoka rudi kijijini,...’nikasema na kuanza kutembea nikimuacha
akiwa kakasirika, na yeye akasema;
‘Mimi
kijijini sirudi, nimeshaongea na baba, kuwa niwepo kipindi ukisimikwa hicho
cheo, ni lazima niwepo kama mtarajiwa wako...’akasema akionyesha kutaka kurudi
huko ofisini.
‘Sawa muda
ukifika nitakuita uje, hilo mbona halina tatizo....sioni ni kwanini tuanze
malumbano yasiyo na tija, wewe rudi huko kijijini, tumalizane na haya yaliyopo
mbele yetu,nakuomba sana usilete ubishi
usio na maana, utaharibu kila kitu, achana kugombana na mdada, ....’nikasema
‘Kwa mtaji
huo bora niharibu, na nakuambia kiukweli, nitaharibu kweli kweli usiponijali
mimi, kwanza ngoja nikutane na huyo mwanamke wako, ameshanionyesha dharau na
kiburi, sasa ni vyema tupambane naye anifahamu kuwa mimi ni nani....’akasema
‘Halafu
utapata faia gani kwa kufanya hivyo?’ nikamuuliza
‘Mimi
sipendi shari, ni mvumilivu sana, nimevumilia mangapi huko
kijijini,....nimeambiwa mangapi huko kijijini, nikayavumilia,...lakini hizi
zarau za huyu mwanamke, sitaweza kuzivumilia keshanipandisha hasira, atanijua
kabila langu ni nani...’akasema akichezesha chezesha miguu.
‘Nisikilize
ninachokuambia, usiponisikiliza mimi, nitayaachia yende yawavyo, na wewe
utakuja kuumia, na kukosa kila kitu...’nikasema
‘Ni bora
nikose, lakini tukose wote, mimi sijali, lakini kwanza ni lazima nimkomeshe
huyo mwanamke wako...unanisikia, nenda mkaongee, lakini ujue kuwa mimi
namsubiri huyo mwanamke wako hapa nje,, kwasababu hajui ulichonifanyia mimi,
wewe si umeniharibia maisha yangu, umesahahu kwasababu ya hicho kinyago,...nimevumilia
vya kutosha, sasa basi....’akasema na kuegemea ukuta kuonyesha kuwa haondoki
hapo.
‘Kwahiyo unataka
kusema nini, hutaki kuondoka sio, ....?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia na
kusema;
‘Namsubiri
huyo mwanamke wako hapa nje...wewe nenda mkaongee,lakini mimi hapa
sitoki.....’akasema na mimi nikaona napoteza muda nikachukua simu na kumpigia
baba yake.
‘Mzee, Binti
yupo hapa analeta vurugu, ...’nikamwambia
‘Analeta
vurugu....., analeta vurugu gani, hebu nipe simu niongee naye...’akasema na
mimi nikampa simu huyo mchumba wangu, kwanza akaniangalia kama vile hataki
kupokea, akauliza;
‘Simu ya
nini, hata kama ni polisi mimi sitoki hapa....’akasema
‘Ongea na
baba yako...’nikasema na aliposikia baba yake, akaipokea kwa haraka na akaanza
kuongea naye, kwanza alimsikiliza baba yake akionega kwenye simu baadaye akasema;
‘Baba huyo
hawara yake yupo naye, na kwa kauli yake mwenyewe, huyo mwanamke,inaonyesha
kuwa wana mahusiano na huyu mchumba wangu, sasa huoni nikiondoka hapa nitakosa
muda wa kuongea naye, ni lazima nipambane naye....’akasema
‘Wapi,....kwani
wewe upo wapi,?’ akauliza akionyesha mshangao.
‘Lakini ulisema
umerudi nyumbani kijijini,....’akasema kwa mshangao
‘Oh,
kwanini, kuna nini kimetokea?’ akauliza na sasa akawa ananiangalia mimi kwa
mashaka
‘Baba
....una uhakika na hilo ...wamekugeuka,...akina nani?’ akauliza huku
akisikiliza kwa muda halafu akaniangalia wa jicho baya, akasema;
‘Msaliti mkubwa
wewe..utaona.....’akanipa simu yangu na kuondoka kwa hasira
NB: Kuna
nini hapa tena:
WAZO LA LEO:Hasira kwa binadamu wakati mwingine hazikwepeki, inatokea hali kama hiyo ukakutana nayo. Unapoona hali hiyo inakujia, jaribu kutafuta njia za kuituliza, ni muhimu kuwa makini sana kwa hali ilivyo sasa,, kwani
unaweza kufanya jambo ambalo utakuja kujijutia baadaye au hata kushinikiza
mapigo ya moyo, na kuleta athari mwilini.
Cha muhimu, tuliza kichwa chako
kwanza, fikiria kwa makini unachotaka kukifanya, kabla hujachukua maamuzi, ikiwezekana ni bora ukalikwepa eneo la tukio,
ukaenda sehemu nyingine ukatulia kwa muda, kumbuka hasira ni hasara.
Ni Mimi: emu-tatu
No comments :
Post a Comment