‘Sio hongera
ya kesi, bali ni hongera ya kazi nimesikia kuwa umepata kazi mpya...’
‘Bosi kazi
gani umenipandisha cheo, .....?’ nikauliza nikiwa na hamasa ya kujua,
‘Nimekupigia
simu kukupa ushauri tu, sio kwamba sikupendezewa na taarifa hiyo, nimefurahi
sana, maana hayo ni maendeleo,...’akasema
‘Bosi mbona
mimi sijaelewa, sijui lolote....’nikasema
‘Basi kumbe
nimekuwa mmbea,...huenda sikutakiwa nikuambie mapema, ila ninachotaka kukuambia
ni maswala ya kukushauri tu...’akasema
‘Bosi ina
maana kazi hiyo sio hapo kwako?’ nikauliza
‘Hayo
tuyaache, ninachotaka kukuambia ni kuwa, uwe makini kwani dunia sasa
imebadilika, usione mtu anakujali, ukaona huyo ni mtu mwema sana
kwako,...inawezekana ikawa hivyo, lakini ni mmoja kwa mia...’akasema
‘Wapo
wanadamu watakuchekea, ukaona ni wema sana kwako, lakini moyoni kwake ana
inda,...’akasema
‘Bosi ...’nikataka
kumkatiza
‘Nisikize,
wewe tumekaa pamoja, nakufahamu sana,..nimekuona kama mdogo wangu, kwahiyo
inabidi nikushauri huko unapokwenda,...ni kwema, kuna masilahi mazuri, lakini
....’akatulia
‘Bosi kwani
ninakwenda wapi...?’ nikamuuliza
‘Watakuambia
wenyewe,....nahisi sikutakiwa nikuambie,..muda utafika utaambiwa....’akasema.
‘Hapana
bosi, nimuhimu niambiwe, kwanini ..’nikaanza kulalamika, na mara nikasikia mlio
wa simu kukatika...
‘Sio hongera ya kesi, bali ni hongera
ya kazi nimesikia kuwa umepata kazi mpya...’
******
‘Sio hongera ya kesi, bali ni hongera
ya kazi nimesikia kuwa umepata kazi mpya...’
Haya maneno ya
bosi wangu yaliendelea kujirudia kichwani kwangu, yalikuwa maneno yenya ujumbe
fulani, na niliona ajabu simu yake kukatika ghfal, na hata nilipojaribu
kumpigia tena ikawa haipatikani, na mdada akaniangalia na kusema;
‘Mambo ya
digitali hayo, nimeshakuambia hutakiwi kuongea na mtu yoyote wa nje kwa hivi
sasa, nahisi hao ni watu wa usalama wanafanya vitu vyao, kwani wenyewe
wameshafika....’akasema mdada akiangalia saa yake.
‘Ili
iweje,hawajui kuwa huyo ninayeongea naye ni bosi wangu,....’nikasema
‘Kwao wao
hawawezi kuwa na uhakika wa kila mtu, hawawezi kubahatisha, na ni nani
atamfahamu huyo bosi kuwa hana lolote dhidi ya hao watu, ni maswala ya
kiusalama, wao wanafahamu zaidi, ...’akasema
‘Lakini hata
hivyo, mimi naingiwa na wasiwasi, bosi anasema nimepata kazi mpya ni kazi gani
hiyo ambayo hata mimi siifahamu?’ nikauliza na kabla hajatamka kitu mlango
ukagongwa na mdada akasema
‘Subiri,
nahisi ndio hao wameshafika, natumai wao wenyewe watakupa jibu la swali lako,
kazi nyingine hazitangazwi ovyo...’akasema na kuelekea mlangoni, akawa anaongea
na mtu aliyekuwa nje, yeye akiwa kasimama mlangoni, baadaye akaniambia;
‘Unahitajika
kwenye chumba cha mkutano, ....’akasema na kwa muda huo nilikuwa nimeshavaa
nguo rasmi, ambazo aliniletea mdada, nikasimama
bila kuleta ubishi nikafanya kama alivyoniagiza mdada nikaelekea huko
kwenye chumba walichokiita ni cha mkutano.
Nilipofika
mlangoni mdada, akanishika begani, akaniangalia kwa jicho ambalo nilihisi kama vile
anaona keshanipata, na kwahiyo mipango yake imakamilika, lakini sikumuelewa,
lile jicho lina ujumbe fulani, ...akageuka kuangalia pembeni akasema
‘Kila-laheri...’akaondoka
kwa mwendo wa kasi kama anawahi jambo, hakugeuka nyuma na mimi nikafungua ule
mlango na kuingia ndani...
‘Ilikuwa ni
ofisi iliyokamilika, na inaonyesha inatumika, maana humo ndani kulikuwa na kila
kitu cha kiofisi, na humo nilimkuta mtu mmoja akiwa anapanga vitu mezani, na
aliponiona akaacha na kunisogelea akanyosha mkono kunisalimia;
‘Karibu
muheshimiwa...’akaniambia na kunifanya nishituke, toka lini mimi nikawa
muheshimiwa, name nikanyosha mkono tukasalimiana, halafu nikasogea hadi kwenye
kiti alichonielekeza, akasema;
‘Wakuu
wameshafika, wanakuja muda wowote , cha muhimu wanachotaka kufanya ni taratibu
za kupata mfanyakazi mpya kutokana na nafasi iliyoachwa wazi na
marehemu...’akasema
‘Marehemu!
Marehemu yupi huyo?’ nikauliza nikishituka maana kupewa kazi ya marehemu
inashitua kidogo, sikuwa nimehisi lolote kwa wakati huo
‘Huyu
aliyefariki hivi karibuni humkumbuki wa kitengo cha ushuru...’akasema
‘Oh, sikujua
hilo, lakini mimi badi nipo kwenye kesi, na kesi yenyewe wananishuku kuwa mimi
huenda nahusika...sasa iweje tena niwe katika watahiniwa wa hiyo
nafasi,...isije ikawa ni mtego...., hata hivyo, mimi nimesomea mambo ya
uhasibu....’nikasema
‘Kazi ni
hizo hizo bwana, ni bahati imekuangukia, usije ukaijutia,..cha muhimu ni sifa
wanazozitaka wao, ...swala la kesi hilo wanalifahamu sana, na kama ungekuwa
katika kashifa yoyote wasingelikuchukua, watakuwa wamegundua kuwa huhusiki, na
nahisi katika kuchunguza kwao, kuhusu hiyo kesi, ndio wakagundua kuwa wewe
unastahili, vinginevyo watakuambia wao wenyewe,....’akasema na kunikabidhi
makabrasha
‘Soma hayo
maelezo yatakusaidia kwenye usaili wao,...mimi sina zaidi nimemaliza kazi
yangu, kama kuna kitu unahitajia kwa sasa, au swali loloye niulize,..’akasema
na mimi sikujua nimuulize nini, nikabakia kimiya na yeye akasema;
‘Mimi nakutakia
kila la heri...’akasema na kuendelea kupanga panga vitu mezani, halafu
akaondoka, na haikupita hata dakika moja mlango ukafunguliwa, wakaingia watu
wawili waliokuwa wamevalia suti za bei mbaya, waliangalia huku na kule, kama
kuhakikisha kuwa mambo yapo sawa, na mmojawapo akasema;
‘Oh,
umeshafika mhasibu..’ilikuwa sauti nzito, na mimi kwa muda huo nilikuwa nimesimama
nikijua ndio waheshimiwa wenyewe, na mmojawapo akanisogelea akiwa na chombo
fulani, akanipitishia halafu akasema;
‘Ok, upo
salama,..naomba hiyo simu yako...’akasema na akaichukua ile simu yangu
akaikagua, na baadaye akamwambia mwenzake;
‘Ni ile ile,
haina kitu...’akasema na mwenzake, akaipokea na kikagua, halafu akasema
‘Ok, labda
ni maingiliano,..tutaona huko mbele, lakini hakuna lolote baya, waache waingie
tu...’akasema na haikuchukua muda wakatoka, na mara wakaingia jamaa wengine
wawili, hawa walikuja na makabrasha yao mikononi, wakaniangalia na kusema;
‘Oh,
umeshafika mkuu,.....?’ akauliza mmojawapo na mimi nikasema
‘Nimeshafika
mkuu.....’nikasema na wote wawili wakanisogelea na tukasalimiana na wao
wakajitambusliha kuwa ni maofisa uajiri, na kazi yao kubwa ni kunifanyia
usaili, ili kukamlisha taratibu za kumpata mfanyakazi wa nafasi iliyobakia
wazi,
‘Kama
unavyojua kuna nafasi iliyoachwa wazi kwenye idara zetu za ushuru, na kwa
utaratibu nafsi hii inatakiwa itangazwe, na hilo limeshafanyika, na wengi
wameomba nafasi hiyo ukiwemo wewe mwenyewe...’akasema na mimi nilitaka kusema
sijawahi kuomba hiyo nafsi lakini nikabakia kimiya
‘Sisi kama
wataalamu wa kumpata huyo mtu tumeshafanya uchunguzi wetu unaostahiki, na
tumerizishwa na wewe kuwa unafaa kuziba hilo pengo, na kilichotuleta hapa ni
kukamlisha taratibu zetu tu..baadaye huenda ukaonana na wakuu kwa utambulisho
zaidi...’wakasema
‘Nashukuru....’nikasema
nikijiuliza hao wakuu ni akina nani, na haya mambo mambo yanakwenda hata mimi
mwenyewe kufahamu, lakini niliona nivute subira tu.
‘Wakati
uchunguzi wa kesi ya hayo mauaji, ndipo tulipogundua kuwa wewe unafaa sana kuziba pengo la marehemu,...na
kiukweli, kesi yako inahakikiwa, umeshikiliwa kwasababu ya kukutwa kwenye
tukio, ...hilo linafanyiwa kazi na wahusika..usiwe na shaka nalo...’akasema
‘Cha muhimu
ni kuwasikiliza watu wako, kwani kufanikiwa kwako kumetokana na juhudi za hao
watu wanaokudhamini,...na zaidi ni kutoka kwako, kwani utakuwa na miezi mitatu
ya majaribio,....ni matarajio yetu kuwa wewe utafanya kazi kama alivyofanya
marehemu, ujue kuwa nafasi hiyo nyeti sana, sio rahisi kupatikana na sio rahisi
kupewa watu ovyo ovyo....’akasema
‘Nitajitahidi
kutimiza wajibu wangu kama inavyostahili....’nikasema huku moyoni nikijipa
moyo,japokuwa sikuwa na uhakika, ni kazi gani hasa nastahiki kuifanya.
‘Sasa
unatakiwa kujaza hizi fomu hapa, ukimaliza, tutakuwa tumekamilisha kazi
yetu....’wakasema na mimi nikakabidhiwa hizo fomu, nikazisoma kwa makini, ni
mkataba wa ajira, una maelezo mengi sana,...niliyapitia kwa haraka, na kule
kwenye nafasi za maelezo binafsi,....nikajaza kila kitu baadaye nikawakabidhi ,
wakaniuliza maswali mbalimbali, ya kiutendaji, nami nikawajibu kadri niwezavyo,
na mwisho akaniambia
‘Haya ndugu
kazi yetu tumemaliza, ....nimeambiwa kuwa kuna mtu anakuja muonane naye mara
moja, muongee naye kwa haraka kidogo, kutokana na muda, kwani baada ya hapo
unatakiwa kuonana na wakili wako, kwahiyo usubiri hapa....’akasema na
wakaondoka,
Nilibakia peke yangu kwa muda, baadaye mlango ukafunguliwa, na
aliyeingia alikuwa ni mchumba wangu
‘Hivi Wewe
unanifanya nini...’akaanza kulalamika
‘Kwanini
unasema hivyo,?’ nikamuuliza na aliponiona nilivyovalia na chumba chenyewe
akaduwaa, na kusema
‘Oh, kumbe
ni kweli...’akasema
‘Ni kweli
kuhusu nini?’ nikauliza
‘Baba
kaniambia kuwa umepata kazi mpya na sasa hutakuwa na kisingizio tena kuwa
huwezi kunioa mpaka ujenge, ufanye nini, ...kwani wamesema utapewa nyumba ,
gari,....oho, tumshukuru mungu...’akasema akionyesha furaha ya hali ya juu, na
moyoni nikawa namuona mdada kasimama nyuma yake, akionyesha huzuni
‘Usianze
kufurahi , wakati hata sijajua kuwa hiyo kazi ipoje, je nikikataa, maana siwezi
kupewa kazi yenye mitego na masharti, hawa watu siwaelewi..’nikasema
‘Utakuwa mtu
wa ajabu sana, wenzako nafasi kama hizo wanazitafuta, wewe unasema utaikataa,
sikuelewi....’akasema
‘Kwanza
nikuulize baba yako mumeongea naye saa ngapi, kakupigia simu?’ nikamuuliza
‘Ndio
kanipigia simu....’akasema akianiangalia kwa makini
‘Kwanini
unaniuliza hivyo?’ akauliza
‘Naona kila
kitu anakifahamu yeye mapema tu,hata sijui anahusika vipi na haya yote.....’nikasema
‘Baba huwa
anafahamu mambo mengi ya nchi hii, anakwenda na wakati, ni mtu wa serikali, ana
majukumu yake hata mimi siyajui...’akasema
‘Mhh, haya
...niambie ulisema unataka kuongea na mimi, naomba mambo mengine tuyaongee
tukiwa huko nje, hapa sio mahali pazuri pa kuongea chochote, na nimepewa muda
mchache wa kuongea na wewe....’nikasema
‘Ni kuhusu
huyo mdada, ...ni muhimu sana umuelewe mapema, haaminiki huyo mwanamke,kama
usipokuwa makini utajiingiza kwenye matatizo....’akasema
‘Usijali,
huyo ni mfanyakazi mwenzamgu, hana matatizo kabisa....hilo lisikuumize
kichwa...’nikasema kwa kujiamini
‘Na huko
unapokwenda kufanya kazi mtakuwa naye?’ akaniuliza
‘Wapi,
...sijajua wapi,...lakini sijui, ,...yeye ana kazi yake, .....’nikasema huku na
mimi nikiwaza kuwa ina maana kweli nitakuwa mbali na mdada, nitakosa uchakaramu
wake, nikamwangalia mchumba wangu ambaye kwa muda huo naye alikuwa akiniangalia
kwa makini
‘Umebadilika
kweli siku hizi...’akasema
‘Nimekuwaje?’
nikamuuliza huku nikiangalia saa yangu, nikijua sina muda wa kuongea naye, na
nilikuwa na mambo mengi ya kuongea na huyu mtu, ili asije akaharibu.
‘Umekuwa
mweupe, unazidi kupendeza, ..halafu, hueleweki,.....’akasema
‘Naona huna
la muhimu kwa sasa, nimeambiwa kuna watu wanakuja kuonana na mimi, ni vyema
ukaondoka, ...’nikasema
‘Unanifukuza..’akasema
akiniangalia kwa mshangao
‘Huoni nipo
kwenye ofisi za watu, na kuna wakubwa wanakuja kuongea na mimi, nisingelipenda
wakaja kukuta humu.....’nikasema
‘Ndio vizuri
wajue kuwa mimi ndiye mchumba wako wa halali, sio huyo mwanamke wako,
anayekuzuzua...hivi kwanini mwanamke kama huyo anakusumbua kichwa
chako....’akasema na mara mlango ukagongwa
Nikageuka
kuangalia mlangoni, na mchumba wangu akanisogelea kusimama karibu yangu, akasema
‘Nataka
wakija unitambulishe kuwa mimi ni mchumba wako....’akasema
Na mara mlango ukafunguliwa, akaingia wakili akiwa pamoja na mdada,....
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment