'Mbona
unaniangalia kama umeona shetani....’ilikuwa sauti ya mdada akiwa kasimama
mlangoni akiwa amevalia sweta zito, kuonyesha kuwa alitokea kulala, na hakutaka
ubaridi umuingie, alionekana sio mtu wa kutoka, na mkononi alikuwa na mkoba
wake mkononi.
‘Mbona
umewahi hivi, mimi sijajiandaa....’nikasema nikijikagua
‘Nimekuja
tuongee kidogo kabla hujakutana na hao watu.....’akasema
‘Watu gani?’
nikauliza nikitoa macho ya mshangao, maana sikumbuki kuambiwa kuwa leo
nitakutana na watu
‘Leo
utakutana na watu muhimu sana,ambao pamoja na mengine, ni kukuweka sawa, na
huenda wakaja na taarifa nzuri kwako...’akasema
‘Taarifa
gani, kuwa kesi imefutwa au?’nikauliza nikiwa na hamasa
‘Watakuambia
wenyewe, cha muhimu ni kujiweka sawa kwa wageni wa heshima, sio wageni wa ovyo,
hao ndio wanaojua hali halisi yah ii nchi, wanaweza kukugeuza leo ukawa mtu
mwingine kabisa, au kukupoteza, usionekane tena hapa duniani..’akasema
‘Mhh,
sielewi...ina maana wao wanauwezo wa mungu? ’nikauliza kwa mshangao.
‘Usiulize
maswali kama sio msomi, swali gani hilo, nilichoongea hakimgusi mungu,
mwenyezimungu ana uwezo wake, mimi nazungumzia mamlaka ya hapa duniani, ya hapa
kwetu....’akasema na kuniangalia, mimi nilikuwa nina wasiwasi kuwa sasa hivi
kuna mtu atagonga mlango.
‘Kuna mtu
unatarajia kuonana naye mbona hutulii...nimekuambia nataka kuongea na wewe...’akasema
‘Mhh, hapana,sio
kitu ...ila mimi nataka kwenda nyumbani kwangu kuna mtu alinipigia simu
kuwa,kuna watu walifika kwangu, wanatoka kijijini wanataka kuonana na mimi...’nikasema
‘Walikuja nyumbani
kwako,...lakini siwanafahamu kuwa bado umeshikiliwa na polisi au?’akauliza kwa
mshangao
‘Ndio walikuja
nyumbani kwangu haponilipopanga..sina uhahika kama wanafahamu lolote, lakini..’nikasema
nikikwepa kuangalia naye nay eye akanikatisha kwa kusema;
‘Nakuomba
uachane na hao watu, na huko kwako upasahau kwa sasa, ulishaambiwa kuna watu
wanakuwinda, na nyumbani kwako ni lazima kutakuwa na watu wanakusubiria, upo
kwenye hatarani inabidi kuwa na tahadhari, kwa hivi sasa huwezi kujua ni nani
yupo nyuma yako..unalifahamu hilo,....’akasema
‘Hata hivyo
ni lazima niende huko mara moja, kwani hao wageni inaonekana kuwa wanafahamu
kuwa nimeshapata dhamana, ndio maana wakafika kuniona,nitachukua tahadhari
uasijali kwa hilo...’nikasema
‘Unataka
kuonana nao sasa hivi?’ akaniuliza akionyesha kukerwa na maelezo yangu hayo
‘Ndio...ni
muhimu sana’nikasema
‘Hapana,
huwezi kuondoka kwa hivi sasa, hata baadaye..., kwa leo haitawezekana, ....’akasema
‘Kwanini?’
nikauliza
‘Nimeshakuambia
kuwa leo ni siku muhimu sana kwako,unahitajika kukutana na hao watu, ukimalizana
nao, ukakubaliana nao, basi ukitoka hapo utakuwa huru kwenda unapotoka,
tutaangalia na muda...hata hivyo baada ya hapo utahitajika pia kwenda kuonana
na wakili , ukumbuke kuwa kesi bado haijafutwa, japokuwa jalada lako la kesi
lipo kwa waheshimiwa...’akasema
‘Lakini nina
mambo yangu binafsi...na ni muhimu kwangu mimi, sijafungwa, nipo huru au? ’nikasema
‘Ndio upo
huru, lakini uhuru wako kwa sasa una masharti, kwanza hebu niambie una mambo
gani muhimu kama ulivyosema binafsi unayoyahitajia...au ndio hao wageni unaosema
wamefika kutoka huko kijijini, ...au una jingine,?’ akaniuliza
‘Pamoja na
hayo...’nikasema nikionyesha kutokuwa na furaha
‘Sikiliza
kuanzia sasa, hadi hapo mambo yatakapokuwa sawa, unatakiwa uniweke wazi kwa
kila jambo unalotaka kulifanya, kumbuka kuwa mimi ndiye mdhamini wako,
...’akasema
‘Nafahamu hilo,
na sina nia mbaya,nitajitahidi kuchukua tahadhari, ni lazima nitoke humu ndani
haraka,...’nikasema nikijiandaa kuondoka huku nikiangalia mlangoni
‘Utoke humu
ndani haraka!? Wewe mtu vipi, kwanza unaonekana kuna mashaka-mashaka, unaogopa
nini, kuna hatari yoyote umeihisi au kuna jingine,hebu niambie ukweli?’
akaniuliza akiniangalia kwa makini
‘Sio jambo
la hatari, ni huo ugeni tu, ni muhimu kwangu....’nikasema
‘Huo ugeni
ni kuhusu huyo mchumba wako, au sio?’ akaniuliza na kunifanya nishituke,
nikamuuliza
‘Nani
kakuambia ni kuhusu mchumba wangu?’ nikamuuliza kwa mshangao na yeye akacheka
kwa dharau, na kusema;
‘Nakuomba
uwe muwazi kwangu, yaani muda wote unahangaika kumbe ni kuhusu huyo
mtu,...nikuambie ukweli, hakuna mtu anayeruhusiwa kuonana na wewe hadi hapo,hao
waheshimiwa watakapoondooka,...ni maswala ya usalama, hao watu ni watu muhimu,
...siwezi kukueleza kila kitu lakini huyo mtu wako hawezi kuonana na
wewe.......kwa sasa’akasema
‘Mhh, mbona
mnanikwaza...’nikasema
‘Ukumbuke
kuwa sasa hivi, kila unalolifanya linachunguzwa, ...wao wana utaalamu wao,
hawawezi kuja kuonana na wewe bila kujua usalama wao, ndio maana ukawekwa
hapa,...hata hivyo hata mimi ninayekudhamini, natakiwa nikuchunge kama
ninavyochunga mboni yangu ya jicho...’akasema na mimi nikamwangalia kwa macho
ya mshangao
‘Kwahiyo,
kama ni kuhusu yeye, huyo binti gani sijui, hawezi kuja kukuona kwa hivi sasa,
kama anavyotaka yeye...hataambiwa hivyo moja kwa moja...’akasema
‘Kwa vipi,
na na.....’nikaanza kuhisi wasiwasi
‘Tulizana,
usitake kuharibu mambo, tuna nusu saa ya kujiandaa, kabla waheshimiwa
hawajafika, ninachotaka kukuambia ni kuwa hao watu sio watu wa mchezo, wakija
unachotakiwa ni kukubaliana nao kila kitu, after
all, ni kwa faida yako, sioni kwanini ukatae...’akasema
‘Mimi
sielewi, kwanini yote hayo siambiwi, sifahamu , kila jambo naperekeshwa tu,
kwani kuna nini mnanitafuta mimi, hebu niambie ukweli mdada, yote haya ni ya
nini, na kwanini mimi?’ nikauliza
‘Ipo siku
utakuja kufahamu, na nahisi muda unakaribia,..usijali..subira huvuta heri, na
baada ya yote hayo, huenda ukafurahi, cha muhimu usiniangushe,...’akasema na
kuangalia saa yake, halafu akageuka kunitizama, akiwa na uso usio na tabasamu,
alionekana yupo kikazi zaidi, akaangalia kitandani na kuona vile vifaa, akasema;
‘Hivyo vifaa
ni muhimu sana kwako kwa hivi sasa, vina maana yake....usiviweke ovyo, na
ukijiandaa tunatakiwa tutoke hapa, kuna ofisi ipo chumba cha pili yake...’akasema
na mimi nikageuka kuangalia yale mawani, simu na saa, nilikuwa nimeviweka
kitandani
‘Unasema
hivyo vifaa ni muhimu sana, wa nini kwangu mimi, kama ni mtego,mimi...sivihitaji....’nikasema
kwa sauti ya kukata tamaa
‘Utavihitaji
tu,....usiwe na wasiwasi mwanaume wewe, mimi nakuhakikishia utavipenda,na
hakikisha unakuwa mchangamfu ukija kukutana na hao wageni,...wakifika utakaa
ongee nao, mimi sitakuwepo wakati mnaongea, kwahiyo unatakiwa
kujiamini,...unasikia wewe mwanaume?’ akasema
‘Sijui...’nikasema
na yeye akaniangalia kwa uso wa kushangaa, akanisogelea na kunishika kidevuni
‘Wewe mwanaume
vipi wewe, hebu amuka,usiniangushe bhana,...’akasema na huku akichezea kidevu
changu kwa vidole.
‘Unajua
mdada, sikuelewi...’nikasema
‘Mhasibu,tupo
kazini hapa, usitake nibadilike...haya yote yanafanyika kwa ajili yako, ujue
kesi yako haijafutwa, na hao watu ndio wanaoweza kuifuta hiyo kesi, kama
hutaonyesha ushirikiano nao, ujue,...utasahaulika...nakuonya kwa mara ya
mwisho...’akasema na alipotaja kuhusu kesi nikashituka, nikasema;
‘Baba mkwe
wangu anasema anashughulikia hii kesi, sielewi kwa vipi?’ nikauliza
‘Mimi
sijui,..na hata hivyo mimi sitaki kuongea maswala ya baba mkwe wako hapa, huyo
mtu kanipigia simu leo asubuhi, akaanza kunishutumu, eti naingilia ndoa ya
binti yake,...simuelewi huyo mzee, kwanza kanipa kazi nimfanyie, hajui naifanya
vipi, anakimbilia kusema nimeitumia nafasi hiyo kukurubuni, hivi kweli mzee
huyo ana akili, hanielewi kabisa...’akasema
‘Lakini
mengine naona kama yana ukweli,au sio..’nikasema
‘Hahaha...na
wewe upo upande wake,..sikiliza si baba mkwe wako au nani, wewe na mimi ni kitu
kimoja, huyo kwasasa achana naye, hana maisha ya maendeleo na wewe, mimi natakiwa
kukujenga ili ufanane na wanavyotaka hao watu, ..hata hivyo,...nilishakuambia
wewe ni wangu,hunielewi..’akasema
‘Huwezi
kulazimisha penzi,...’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho ya kuelegeza,
halafu akatabasamu, na kusema;
‘Una uhakika
na hilo, tukifungua moyo wako hapo, hakuna kingine zaidi yangu, tusitake
kupoteza muda na mambo hayo kwasasa, ila baba mkwe wako kanichafua, na hawezi
kunitishia mimi,...’akasema
‘Kakutishia
kasema nini...?’ nikauliza
‘Eti
nikiendelea kufanya hivyo,atahakikisha ananiharibia maisha yangu, kwani
anafahamu siri zangu zote,...yaani mzee huyu keshasahau fadhila zangu, hajui
bila mimi asingelijua mambo mengi, ...anapenda kunitumia tu akiwa na shida
zake, zikiisha keshanisahau...’akasema
‘Unakutumia
eeh, ndio maana akakutumia kunichunguza mimi ?’ nikamuuliza
‘Nilifanya
hivyo kwa vile nilihitajika pia kuendelea na mipango yangu mingine, inayokuhusu
wewe, la sivyo, nisingelifanya anavyotaka yeye...’akasema
‘Mipango
gani?’ nikauliza
‘Ndio hiyo
inafikia hatima yake leo..ukikutana na hao watu, utafahamu...utakuja
kunishukuru,...’akasema
‘Nikushukuru
kwa kuniharibia amani ya maisha yangu, wewe unafikiri nitaongea vipi na baba
mkwe, kama umemzuia binti yake asionane na mimi, na sijui umemfanya nini...’nikasema
‘Hajafanywa
kitu...yupo chumba fulani anakusubiri, lakini atakusubiri mpaka atachoka,na
mwisho wake ataondoka....’akasema
Mara simu
yangu ikalia, nilipoangalia nikaona ni namba ya bosi wangu, nikamwangalia
mdada, na mdada akaniangalia na kuuliza
‘Ni nani
huyo?’ akaniuliza
‘Ni bosi....’nikasema
‘Oh, bosi,
bosi wako wa kampuni, aah, achana naye, nikuambie ukweli, kuanzia sasa, huyo
utamsahau....’akasema.
‘Kwanini
unasema hivyo?’ nikauliza huku simu ikiendelea kuita, na yeye akaniashiria kwa
mkono kuwa niipokee hiyo simu. Nikasema
‘Samhani, ngoja
niongee naye....’nikasema
‘Ongea
naye...lakini hukutakiwa kuongea na yoyote kwa hivi sasa, ....ok, ongea
naye....’akasema akiangalia saa yake, na mimi nikaiweka hewani simu ya bosi, na
bosi alianza kwa kusema;
‘Hongera
sana..’akasema nikajua kuwa huenda ananipa hongera ya kupata dhamana, nikasema;
‘Lakini kesi
bado haijaisha....’nikasema
‘Sio hongera
ya kesi yako, kesi yako nasikia haina nguvu sana, mimi nakupa hongera ya kupata
kazi mpya, ...’akasema
‘Kazi mpya
kazi gani hiyo...?’ nikauliza na kumwangalia mdada, na mdada akawa anatabasamu
tu, inaonekana alikuwa anafahamu ni kitu gani kinachoendelea , bosi akasema;
‘Lakini uwe
na tahadhari, sio kila king’aacho ni dhahabu, na sio kila anayekuchekea ana nia njema na wewe....
NB: Hongera
mpendwa kwa kuwa nami, naishia hapa kwa leo je wewe unasemaje? Tumalize kisa, umechoka,?
WAZO LA LEO: Ni kweli kila mmoja anatafuta, ili
kupata riziki na maisha bora,lakini zipo njia ambazo sio sahihi, na zipo kazi
ambazo sio halali,na hizo wakati mwingine zina mvuto wa masilahi mazuri,kwani
kazi haramu haziishi hamu. Tahadhari tu, tusivutwe na tamaa za kupata na
kuchuma kwa haraka kwani mwisho wake ni mbaya.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
ilipofikia naona siielewi hata nimeshasahau kule maisha ya bosi imekuwa na mzunguko sana
Yaani ni kama vile nilikuwa nasoma kitabu na mara nikashtuka eti mwisho ..aahhh emu-thre..Mimi sijachoka kabisa. Je unaposema "tumalize kisa" unamaanisha kivipi?
Post a Comment