Ni kipindi
nimesharudi hotelini kwangu, na kuanza kushangaa simu niliyopewa, mawani
nilishaiweka pembeni, hamu yangu kubwa ilikuwa hiyo simu, ambayo ilikuwa na
kila kitu kilichopo kwenye laptop.
‘Hii ni
zawadi yako kijana, kwa kuja kujiunga nasi, na humo tutaweza kuwasiliana
nawe...’niliambiwa na jamaa mmoja aliyeniletea hiyo simu, na mdada
akanionyeshea ishara kuwa nipokee.
‘Pamoja
nayo, tunakukabidhii hii saa, uhakikishe unavaa wakati wote, kwani muda ni
muhimu sana, bila kujua muda, huwezi kufanikiwa mambo yako...’akaniambia huyo
jamaa na kunivalisha hiyo saa mkononi.
Vitu vyote
hivi niliviona vya thamani sana, na niliogopa nisije kupewa gharama ambayo
sitaweza kuilipa, nikamwangalia mdada, na mdada akatabsamu na kusema;
‘Sasa
umekamilika,....kilichobakia ni wewe kutoa tamko...’akasema
‘Tamko la
kukubali kuwa upo tayari kujiunga na kundi, na hilo sio lazima utamke, ila
matendo yako, kazi zako, na majukumu utakayopea ndio yatawahakikishia wahusika
kuwa upo kwenye kundi...uwajibikaji, ni muhimu sana...unatakiwa kila mwezi
uonyeshe juhudi zako kwa kutoa kiasi fulani kwenye kundi....’akasema
‘Kiasi
fulani?’ nikauliza
‘Kundi
litaendelea vipi bila kuwa na mfuko,....hayo utayafahamu hatua kwa
hatua...’akasema
‘Lakini....’nikaanza
kuongea na mdada, akanionyeshea ishara kwenye vifaa nilivyopewa, akasema
‘Uwe na
kauli ya ujasiri, na kujiamini, usipinge au kulalamika...’akasema
Niliviangalia
vile vifaa, simu, saa na mawani, nikajua vyote hivyo ni sehemu ya mipango ya
kuniingiza kwenye kundi nisililolifahamu, na sijui kazi yao ni nini...nikatulia
nikisubiria, na mara sauti ikasikika,..
‘Kwenye
miwani yako hiyo, utasikia kila kitu...’akasema mdada, na kweli, nilisikia
sauti ikitoka, ni kitu kama hotuba, mtu alikuwa akiongea, kuwashukuru
waliohudhuria, na kupongeza juhudi za kundi, akasema;
‘Pamoja na
kupoteza mwenzetu mmoja, lakini usemi wetu ni kata mti panda mti, ....tuna
furaha kuwa tuna kizazi kipya, wapo wanachama wapya wamejiunga, ....na wengine
wapo kwenye mafunzo maalumu, ili waweze kujua wajibu wao,tuna wenzetu wengi
wameshaingia kwenye sehemu nyeti, kwahiyo tumeimarika kabisa...natumai baadaye hao
wote watakuwa watu muhimu kwenye kundi. Lakini pia tukumbuke uhai wa kundi ni
michango yenu...kila mahali unapokuwepo, ujue unachomeka mirija yetu....
‘Hupotezi
kitu hapo, kwani unachoiingiza ni kingi zaidi ya kinachotoka, lakini ni lazima
tuwe na akiba maalumu kwa shughuli za utawala,tuweze kuwekeza kila eneo,....miradi
yetu inaendelea, na huenda tukawa kundi la kwanza afrika katika
uwekezaji,..bado tunasifika kwa ufadhili, kila mwanachama wetu anafadhili mambo
makubwa kwenye taifa, na hilo ndilo lengo letu.
'Dunia yangu, ndio ndoto yetu, na hili litafanikiwa kama kila eneo kutakuwa na mtu wetu, kwahiyo hatutakuwa na kizuizi kila tunapotaka kufanya mambo yetu...hilo linakaribia kukamilika...
‘Pamoja na
hayo zipo changamoto,...wapo wasiotutakia mema,wanataka kuziba mirija na juhudi
zetu, wapo wasaliti, wapo ambao hawawajibiki, hilo ni lazima lifanyiwe kazi ili
iwe fundisho,...mwenzetu aliyeondoka, ni mmoja wa watu waliojaliwa, lakini
hakujali kundi, hakukumbuka wapi alipotoka, tukaondoa kinga yetu,....mnaona
yaliyomkuta..
‘Kumbukeni
kujiunga hapa ni huru tu, ila kutoka hakupo, ukitoka, tunakusindikiza kuzimu,
natumai hayo mnayaelewa...zaidi ya hayo ni kuwatakia sherehe njema, na
makaribisho mema kwa wanachama wapya, .....’mara kukawa kimiya,
Nilibakia
kimiya nikijiuliza huyo aliyekuwa akiongea ni nani, mbona haonekani, na kwanini
iwe siri kiasi hicho, nikageuka kumwangalia mdada, na niliona kama anaongea na
mtu, kwenye simu yake, alipomaliza akasema;
‘Nimeambiwa
nikuambie kuwa file la kesi yako lipo mikononi mwa wahusika, wanalifanyia
kazi,na huenda baada ya wiki hivi kesi hiyo itakuwa haipo, lakini kwanza ni
wewe uonyeshe kujali....’akasema
‘Nionyeshe
kujali kwa vipi?’ nikauliza
‘Kwenye simu
yako hiyo, kuna fomu ya kujaza, utaijaza na kuelelezea kila kitu
wanachokihitajia, ukimaliza unatuma kutokana na maelekezo, baada ya hapo
utakuwa ukipewa maelezo ni kitu gani ufanya, ukumbuke, hayo yote ni siri
yako.....’akasema mdada
‘Mhh....’nikaguna
‘Usigune
baba, ndio unaanza hapo, baada ya mwezi utakuwa unanukia
umwenzetu,.....’akasema na kusimama, akaangalia saa, na kusema;
‘Ni muda wa
kujichanganya, simama tutembee, kuna vitu vya kufahamu, usione hiki ni chumba,
upande wa pili kuna maonyesho mbali mbali, kama ulivyosikia kundi hili ni
wafadhili wakubwa, sio kuwa wanatania, ....’akasema
Tulitoka na
kuelekea upande wa pili
**********
‘Mbona tangu
jana nakutafuta hupatikani?’ ilikuwa sauti ya mchumba wangu aliyeniamusha toka
usingizini, simu yake ilikuwa imeita mara nyingi, nilipuuzia kuipokea lakini
ilipoita tena na tena, nikaona niipokee
‘Nilikuwa na
mawakili, na watu wanaosimamia kesi yangu...’nikasema
‘Asubuhi
hii, ?! Jana nimekupigia wee, hupatikiani, leo, asubuhi, nimepiga mara nyingi
tu, simu inaita hupokei, upo nanani hapo ulipo?’ akaniuliza
‘Nipo peke
yangu...nimeshakuambia, nilikuwa kwenye mkutano na mawakili, na nililala usiku
sana, mawazo na mambo mengi yalinifanya nichelewe kulala,...’nikasema
‘Kwahiyo upo
wapi, nyumbani kwako au umelala wapi?’ akauliza
‘Hapana...’nikasema
‘Hapana
nini, mbona sikuelewi, upo wapi sasa..?’ akauliza
‘Sikiliza
sio muhimu sana, kujua wapi nilipo, tutaonana kesho...’nikasema
‘Jana ulionekana
ukija kwenye hoteli, ...au sio, ndio huko mlipokutana na hao watu wako,
wanaokudanganya,..na kwanini ni lazima
mkutanie kwenye hoteli...?’ akauliza
‘Nani
kakuambia nilikuwa hoteli?’ nikauliza
‘Kwahiyo
unataka kunificha, basi nikuambie ukweli, jana wakati nilikuja pale polisi
uliposhikiliwa, na wakati nafika bahati mbaya mkawa mnaondoka, tukawafuatilia,
hadi mlipoingia kwenye hiyo hoteli kubwa...’akasema
‘Ulikuwa na
nanii?’ nikauliza
‘Nilikuwa na
shangazi, na sasa hivi nipo hapa hotelini....nilikuwa na baba...’akasema
‘Ulikuwa na
baba yako!? Baba yako amefuata nini huku?’ nikauliza
‘Alikuja
kwenye mkutano wao, na kwa vile nipo huku, alinitumia ujumbe kuwa
hatakuwananafasi ya kuja huko kwa shangazi, kwani ana wageni anaongea nao, akaniita
nije nionane naye mara moja, yeye sasa hivi anaondoka...’akasema
‘Mkutano...?’
nikauliza kwa mshangao
‘Ndivyo
alivyoniambia...’akasema
‘Ulifanyika wapi
na ilikuwa muda gani?’ nikauliza
‘Alisema
ulifanyika Usiku, mimi sijui saa ngapi lakinini muda wa usiku....’akasema
‘Oh,
..lakini hapa kwenye hoteli kuna kuwa na mikutano mingi..’nikasema
‘Mimi sijui
hayo....alisema ulikuwa mkutano muhimu sana kwao, walikuwa wanakaribisha
wanachama wapya, na kuomboleza kupoteza mwanachama wao mmoja, baba bwana
hapumziki, kila siku mikutano...’akasema
‘Oh,.....’nikajikuta
nikiguna
‘Mbona
unaguna,ninakusumbua, kwanza hebu
niambie wewe sasa hivi upo wapi, nataka kuonana na wewe.....’akasema
‘Leo
haitawezekana...’nikasema
‘Kwanini, na
mimi nina ujumbe wako muhimu...’akasema
‘Ujumbe gani
kutoka kwa nani?’ nikauliza
‘Kuhusu huyu
mwanamke unayetembea naye....’akasema
‘Mwanamke
gani huyo?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi
‘Tatizo lako
unafikiri mimi ni mtoto mdogo,unafikiri nimekuja hapa mjini kukaa tu, ni lazima
na mimi nihangaike,...’akasema
‘Kwanini
uhangaike..?’ akauliza
‘Niangalia
nitasaidia nini kwenye kesi yako....’akasema
‘Kwanini
ujisumbue, kesi yangu ni ngumu, inafanywa na mawakili, wewe huwezi kusaidia
kitu....’nikasema
‘Nani
kakuambia siwezi kusaidia kitu, ndio maana nataka kuja kukuona, nimegundua
jambo, japokuwa baba anasema halina uhakika, lakini ni kweli kabisa...’akasema
‘Umegundua
jambo gani?’ nikamuuliza
‘Kuhusu huyo
mwanamke wako mwenye mashetani ....’akasema
‘Mwanamke
gani, kafanya nini?’ nikamuuliza
‘Hata
nikikuambia sasa hivi huwezi kuamini, lakini ni kweli kabisa, huyu anahusika, ndio
yeye aliyemuua huyo jamaa, halafu
katumia mbinu ili ionekane ni wewe uliyefanya hivyo....’akasema
‘Wewe acha
maneno yako haya...utafungwa...una ushahidi gani ?’nikasema kwa kunong’ona, na
akanifanya nisimame, nilitaka hata kukata simu asiendelee kuongea, lakini
haikuwezekana.
‘Hahaha,
unaogopa eeh, kwa vile ni mpenzi wako,shangazi anafahamu kila kitu,sasa wewe
cheza na hii familia, tuone kama utafanikiwa...’akasema
‘Sikiliza...’nikataka
kuongea na yeye akasema
‘Mwanzoni
nilikuwa simuelewi baba, alivyokuwa akisema hakuamini, ....nilimkatalia kabisa,
lakini haya niliyosikia sasa, yananifanya nianze kuamini kuwa, wewe una
mwanamke huku mjini, na huyo mwanamke na huyo huyo....’akasema
‘Hayo ni
mawazo yako, ....’nikasema
‘Lakini yana
ukweli, nimeanza kumwamini baba, nimeshamwambia kuwa nina mashaka na wewe, yeye
kanipa tumaini kuwa, anakufuatilia, kasema sasa hivi upo mikononi mwake,
keshajua mambo yako yote, anasubiri muda muafaka, .....’akasema
‘Sikiliza....tutaongea
kesho, nakuomba tafadhali.....’nikasema
‘Baba wakati
anafuatilia kesi yako, amegundua kuwa, huyo mwanamke ameshakurubuni, na huwezi
kusema lolote juu yake, anakuperekesha kama garo bovu, ...lakini muda wako
unakaribia, angekuacha uoze jela, ila kakustahi kwa vile umezaa na
mimi...’akasema
‘Unasema
baba yako anafuatilia kesi yangu, nani kakuambia yeye anafuatilia kesi yangu?’
nikamuuliza kwa sauti.
‘Unafikiri
isingelikuwa baba, ungepata hiyo dhamana,...na hiyo kesi kwa vile ni ya kubambikiwa,
yeye anaweza kuhakikisha inakwisha juu kwa juu...’akasema
‘Tutaongea
kesho....’nikasema nikitaka kukata simu
‘Kesho
naondoka, lakini kabla sijaondoka nataka kuonana na huyo mwanamke wako,
nimueleze wazi kuwa wewe ni mchumba wa mtu…..,wewe ni muhini uliyeniharibia
maisha yangu, na kama anataka kukurubuni, kwa umalaya wake, ajue atakuangamiza,
mimi sitakubali...’akasema
‘Nakuomba
tafadhali....’nikasema
‘Huna haja
ya kuniomba...kesho nikiondoka, nataka uniambie utaratibu wetu wa ndoa ni
lini,.....’akasema
‘Tutaongea
kesho
‘Kesho
kwanza nataka kuonana na huyo hawara wako,sijui kama mpo naye hapo au yupo
nyumbani kwake, mimi sijali, nimeshafahamu nyumbani kwake, nitakwenda kuonana
na yeye....’akasema.
Wakati huo
huo, upande mwingine wa chumba, mdada akiwa na furaha, aliinua uso na kuangalia
saa ya kitandani, na alipoona ni muda wa kuamuka, akijinyosha akiwa bado kitandani,
na baadaye akatupa shuka pembeni, huku akilini akisema;
‘Mambo sasa
yameanza...hakuna kupoteza muda sasa...huyu mtu sasa ni wangu, iliyobakia ni
kuhakikisha anafanya kila ninachotaka,....’ akasema na kuelekea bafuni.
Huku kwenye
chumba kingine mazungumzo yalikuwa yakiendelea, mhasibu akiwa katika wakati
mgumu na mchumba wake, alitaka kukata simu, lakini aliogopa kuonekana anamzarau
mchumba wake, akasema;
‘Tafadhali
nakuomba usiende huko, utajitakia matatizo...’nikasema
‘Mimi
siogopi mashetani yake, nitapambana nayo, hata mimi nina mashetani zaidi yake..kwanza
niambie upo wapi, nije nikuone sasa hivi...’akasema na nikasikia kama sauti
inaongea karibu yake , nikauliza
‘Unaongea na
nani?’ nikauliza kwa hasira na wivu ukatanda moyoni
‘Naongea na
shangazi....’akasema
‘Ndiye huyo
anayekudanganya au sio....?’ nikasema
‘Nimwambie
hivyo...’akasema
‘Mimi
naongea na wewe, kwanini umwambie,..ina maaana mpo naye hapo, mlikuja naye,sikiliza....’nikasema
na yeye akasema
‘Ndio
nimekuja naye, alikuja kumsalimia kaka yake, na kumbe upo humu humu hotelini, ,
nimeshagundua, ina maana umelala humu humu na huyo hawara wako sio,...nakuja
huko huko nionane naye...’akasema
‘Nina
mkutano na wakili, sina muda wa kuongea na wewe kwa leo....’nikasema
‘Nimesema nakuja
huko huko,....’akasema na kukata simu.
Mara
nikasikia mlango wa chumba changu ukigongwa, nikashituka, maana sikutegemea
mgeni yoyote muda kama huo, nikajiweka sawa na nilipoona nipo tayari kukutana
na huyo mgeni, nikaelekea mlangoni, kabla sijashika kitasa cha mlango, mlangu
ukafunguliwa .....
NB: Oh, tuishie hapo kwa leo
WAZO LA LEO: Inapofikia hatua wapenzi, wanandoa
wanaanza kudanganyanya ujue hapo kuna tatizo, kwani uaminifu ni nguzo muhimu ya
upendo wa kweli...sasa hiyo nguzo muhimu inavunja , tutarajie nini hapo...
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment