‘Kweli ilikuwa ni surprise kama alivyosema mdada, kwani nilikuta maandalizi makubwa sana, chumba alichokodi au kukodiwa kwa shughuli hiyo kilikuwa kimepambwa konamna yake. Na ilionekana ilikuwa tofauti na nilivyotarajia mimi. Mimi nilijua ni shughuli ndogo ya kwangu,kumbe....
‘Usione ajabu, ndio maana nikakuambia ni surprise...’akaninong’oneza mdada
Ndani ya hicho chumba maalumu kulikuwa na watu mbalimbali wa rangi zote, na wote walikuwa na suti nyeusi, na kwenye mfuko wa koti la juu kulikuwa na ua la waridi mfukoni, na kila mmoja ana mawani makubwa, meusi, ....nikajiuliza kwanini...maana humo ni ndani, hakuhitajiki mawani kama hayo,...
‘Mhh, hayo mawani...ya nini...?’ nikajiuliza, huku nikihangaika kuangalia huku na kule, na mimi nilikuwa na yangu, sikuwa na tofauti na wao, lakini akilini najiuliza kwanini,....
‘Surpriseeeeee’ akasema mdada, nikasikia sauti sikioni mwangu, nikageuka kumwangalia, alikuwa mbali na mimi, sikujali sana, nilijua kanisogelea , akaninong’oneza na kusogea pembeni
‘Mhh,kweli surprise, na haya mawani ya ajabu, nilijua ni ya juani, kumbe yanaona vyema kabisa....’nikasema huku nikishangaa shangaa
‘Karibu kwenye kundi.....’akasema mdada, nilitaka kumuuliza kundi gani, lakini nikatulia kimiya, akanielekeza kwenye kiti, nikakaa na kutulia, nikiwa naangalia mbele, kuwaangalia watu waliokuwepo, hakuna hata mmoja niliyemfahamu.
Niliendelea kuwachunguza na kugundua kuwa kila mmoja alikuwa na hamsini zake, wengine walikuwa wakinywa, wengine wanaongea kwa sauti ya chini chini , wengine wameshikilia ipod zao, wakiwasiliana na jamaa zao.
Kwa jinsi walivyovalia na hayo mawani ya kiaina huwezi kumgundua mtu sura, labda uwe unafahamiana naye...hata mdada alikuwa kavalia hivyo hivyo, na hiyo suti aliyovaa, huwezi hata kujua ni mwanamke, labda kichwani...
Kukapita kitambo, nikageuza kichwa kuangalia kulia na kushoto kwangu, watu sasa walikuwa wamekaa wametulia ilionekana ni watu wazito, kwa jinsi walivyovalia,...na nahisi walikuwa wakisubiri jambo fulani...
*********
Awali nilipoingia kwenye hiyo hoteli, tukitokea mahabusu, nilipokuwa nimeshikilia, mdada alinielekeza kwenye chumba ambacho ndicho nilichoandaliwa, na nikaambiwa nioge na nijiweke sawa kwa ajili ya sherehe hiyo maalumu, ambayo hata sikujua ni ya nini, japo mdada,aliniambia ni sherehe ya ushindi, ...
‘Sherehe ya ushindi gani, mbona hata kesi haijafanyika...’nikasema
‘Una wasiwasi gani, kwani umeua,..hujaua au sio, kama hujafanya kosa hustahili kuwa na wasiwasi, pili hiyo kazi tumeshampa wakili, ni kazi yake kuumiza kichwa, sio wewe tena, ndio maana analipwa kwa kazi hiyo,...’akasema.
‘Ni lazima niumize kichwa, kwasababu sijui kinachoendelea, ni kweli sijaua, ni kweli sina kosa, lakini kwanini niingizwe kwenye haya yote, nahisi kama kuna jambo lipo nyuma ya haya yote, akili inahangaika kulitafuta....’nikasema
‘Sikiliza, wewe jione ni mtu mwenye bahati sana, kwani hicho kilicho nyuma ya haya yote ni kwa ajili ya maisha bora kwako na familia yako ijayo...ndio maana nikakuambia uachane kabisa na ndoto zako za nyuma, sasa hivi lenga mambo makubwa,...
'Unanisikia,uachane kabisa na yale uliyokuwa umepanga awali...sasa hivi unatakiwa uwe unawaza utajiri,...lakini sio kuuwaza tu, pia uwe na mawazo ya jinsi ya kuupata, ...ndio sera ya hapa, utajiri-na-jinsi-ya-kuupata,...achana na swala la ndoa na huyu binti, atakupotezea muda wako, unaona watu waliopo humu, kila mtu ana mali, wapo wanawake na wanaume, na wote hawa wanaifahamu dunia, sasa nikuambie moja, achana na mawazo finyu..’akasema.
‘Mhh, hapo sizani kama tutaelewana,...hasa katika swala la ndoa na maisha yangu binafsi, siwezi kukubaliana na mambo yenu, nisiyoyafahamu,....’nikasema na yeye akatabasamu tu.
‘Utakubaliana tu, hilo halina shaka....’akasema
‘Nasema hivyo, kwasababu hujui yaliyotokea katika maisha yangu hadi kufikia hapo, ....siwezi kamwe kumuacha huyo mchumba wangu, na maisha yangu ndivyo yalivyo...’nikaamua kumwambia ukweli.
‘Hebu nikuulie una sababu gani ya msingi ya kukimbilia kumuoa huyo binti....hata hivyo,.. hujaambiwa umuache, ila kwasasa, swala la ndoa itakayofanyika ni baina yangu na mimi, kwasababu maalumu, huyo atakuwepo tu, mtapigana kalenda hadi atachoka mwenyewe, ikibidi utamuoa, ....usiulize kwanini..’ akasema.
‘Huyo ni mama watoto wangu, ukisema nimuache ina maana niitelekeze familia yangu, hivi kweli hata kama ingelikuwa ni wewe ungelifanyiwa hivyo ungelikubali...?’ nikamuuliza
‘Kuna wakati unahitajika kuchukue maamuzi magumu, ...kwa ajili ya maisha bora ya baadaye,....ni kwa ajili ya faida yako, na maendeleo pia, hivi wewe unafurahia kuishi na kufa masikini?’ akaniuliza
‘Ndio maana nafanya kazi, ili nipate kipato changu cha halali, nina imani kuwa kutokana na kipato hicho sitakuwa masikini, japokuwa .....’hapo nikatulia na yeye akaniangalia, huku akitabasamu, na kusema;
‘Japokuwa huwezi kutajirika....malizia hivyo, na kwanini usitajirike eeh, hebu niambie, elimu unayo, akili unayo....kwanini...?’ akawa kama ananiuliza
‘Kila kitu huenda kwa wakati, kidogo kidogo naweza kufikia huko...’nikamwambia
‘Ina maana unakubali kabisa kuwa, huwezi kuishi maisha bora kama wanayoishi wenzako, kuwa na nyumba nzuri, yenye kila kitu, kuwa na usafiri wa kwako mwenyewe,....uwe na miradi yako mwenyewe, itakayokuwezesha, usiwe na wasiwasi tena, hata kama,ukiwa huna kazi...unakubali kutokana na mshahara unaopata, kuwa hautakuwezesha kuyapata hayo kwa haraka, au sio, mpaka ufanye kazi ya ziada, au sio?’akatulia na kuniangalia
‘Lakini hata kwa mshahara huohuo unaweza pia kupata maisha bora, ....tena kwa njia halali tu,....’nikasema
‘Ni nani kakuambia mimi nakufundisha njia isiyohalali,kwenye kutafuta maisha hakuna njio isiyo halali, kama ukitumia akili yako vyema, kipaji chako, na hata madhaifu yako, huwezi amini, wenzako wana-akili ya kuwazia hata udhaifu wako wakautumia, ....’akasema na kutulia kidogo halafu akasema kwa sauti ya upole
‘Hebu nikuulize swali, kwa mfano, umefika mahali ukaona watu wana utajiri, na utajiri huo unatokana na kukusanya mali ya wanyonge, wao wakawa wanaiba na kujitajirisha wao wenyewe, wananeemeka wao wenyewe, wakiwa wanafanya hivyo kwa kutokana na nyadhifa zao, elimu yao, akili yao ....’akatulia kidogo.
‘Watu hao wana nguvu, wana heshimika kwa nje, ....wakiongea wanasikiwa, ....lakini kwa ndani mmh, ..ndio hivyo kutumia akili, kutumia mbinu zao zisizo na mashaka,...maana hata hao wanaoibiwa ukiwaambia kuwa wanaibiwa hawawezi kukuelewa,...kwanza wanawaogopa hao watu, sio kwa vile wana wadhifa, lakini pia ni kutokana na mali, mali ambayo inatokana na hao watu, ..lakini masikini hawajui....’akatulia kidogo.
‘Na hata ufenye ufanyalo, hutaweza kuurejesha huo utajiri kwa wahusika,....na sana sana ukijifanya kujua sana, ukachonga mdomo wako, watakuua, kwasababu mbali mbali,...mara umepotea , mara umeingiliwa na majambazi, mara...ilimradi itatafutwa visa uondoke kwenye hii dunia, kisa ni nini, unaingilia yasiyokuhusu..hebu niambie hapo utafanyaje?’ akaniuliza
‘Kama ni kwa nchi kama hii yetu yenye amani na ulivu, na utawala bora,nitawaambia watu wa usalama, wao watajua jinsi gani ya kufanya...’nikasema huku nikitabasamu nikijua nimetoa jibu sahiho.
‘Hahahaha, unasema nini, watu gani,...usinitanie, unasema watu wa usalama, ok, najua unamaanisha polisi, au sio....nikuulize swali jingine. hivi, serikali, ni nani?’ akauliza
‘Ni mimi na wewe..’nikasema nikirejesha akili yangu shuleni.
‘Tatizo lako unakuwa mwanasiasa wa kishule..., sema ukweli serikali ni wale watendaji walioajiriwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi...na mapato yao au mishahara yao inatokana na kodi yako wewe mwananchi, kwahiyo huyo serikali ni muwakilishi wa kutoa huduma kwako, ...lakini wewe ndiye uliyemuajiri,....huo ndio ukweli wenyewe....’akasema
‘Mhh, huo ni mtizamo wako,.....’nikasema
‘Usiogope kusema ukweli, ....kiukweli, mwajiri wa serikali na watu wake, ni ni raia wa hiyo serikali,...ndio maana, kishule-shule unasema serikali ni mimi na wewe, au sio?’ akaniuliza
‘Mhh, ndio nasema hivi huo ni mtizamo wako....’nikasema
‘Huo ndio ukweli kivitendo,...vinginevyo ni nadharia zinazopambwa na lugha za kupambia walaji tu, hakuna kingine...’akasema na mimi nikawa kimiya.
‘Umenielewa hukunielewa ila hilo nilikuambia ndio ukweli wenyewe unaposema kumwajiri, ina maana ni ule uwezo wa kumlipa huyo mtu, jiulize mshahara wa watenaji wa serikali unatoka wapi, ...ukiangalia kwa mtizamo wa mtu mmoja mmoja, ni kweli kipato chako wewe binafsi huwezi kukilipa maana kuna watu wanalipwa sio mchezo, lakini angalia watendaji wa kawaida tu...ina maana uwezo wa serikali unatokana na mimi na wewe...sijui unanielewa hapo.....’akasema
‘Huo ni mtizamo wako.....’nikarudio usemi wangu akaniangalia na kukunja uso kuonyesha kukerwa, lakini hakuacha kuongea, akasema;
‘Ndio ukweli ulivyo, serikali haiwezi kuwepo bila kodi yako wewe,..kwahiyo wewe ndiye uliyemuajiri huyu mtu mtendaji..., ndio kuna baadhi ya miradi ya serikali inayotambulikana, kama kweli ipo,mmh, mfano mbuga za wanyama kwa mfano...ushuru, nk, lakini zote hizo zinatokana na nguvu yako wewe mwananchi unayetumika,...’akatulia kidogo
‘Wewe leo hii ukinunua chochote kile unakuwa umelipa kodi, ukipata huduma mbali mbali, ukatoa pesa yako, ujue hmo kuna kodi yako, hapo ndipo serikali inapata mapato yake,....sasa nilitaka kukuambia nini....?’ akawa kama anauliza, mimi nikabaki kimiya, akatikisa kichwa na kusema;
‘Serikali ina idara zake nyingi tu, katika utendaji wake, na ukiangalia kwa makini,....kiukweli, hata hivyo, pato lake sio kubwa sana.....ndio maana hata hao watendaji wake, ambao, wamejitolea kutoa huduma kwa wananchi...hawapati mishahara mikubwa kihivyo, labda kwa wajanja wajanja....’ akaangalia saa yake.
‘Mimi najiuliza kama ni hivyo, huyu mtu umemuajiri wewe, lakini wewe ni masikini, huna mbele wala nyuma, kila siku unakamuliwa kodi yako, ....kuna huyu mjanja mjanja, iweje huyu mtu wako uliyemuajiri,apate kipato kikubwa kuliko wewe uliyemuajiri...okey well and good, ....kwa vile kuna ujumla wa mapato yake, bla, bla...ndio maana inatokea hivyo,....lakini vyovyote iwavyo, kipato chao kinajulikana bhana.....’akasema
‘Sasa unataka kusema nini....?’ nikamuuliza
‘Tuchukulie tu mfano, wa huu mjadala wetu, ulisema kuwa ukiona watu hawo wanachuma na kutajirika, kutoka kwa mali ya uma, wewe utakwenda kwa watu wa usalama, au sio...,wewe unafahamu kipato cha hao watu au sio?’ akaniuliza
‘Sifahamu....’nikasema
‘Kinafahamika bhana, sio mshahara mkubwa...tunaishi nao wanatuambia ....wanalipwa kidogo sana,.....huoni kwenye bajeti...mimi nakushangaa sana mhasibu wewe, acheni ujinga wa kukaa maofisini, fungueni macho, fungueni masikio....watu hawa wanastaafu wakiwa wamechoka, hawana mbele wala nyuma, wanaishia kupatwa magonjwa yasiyotibika, mashinikizo....hakuna zaidi....’akasema
‘Lakini wapo hao wajanja wajanja.....wakitoka huku, labda wamestaafu, wanapelekwa huku...hao eeh, walishafikia ngazi fulani,hawawezi kutupwa,...wenzetu
‘Nikuonyeshee kidole kwa hawa waliopo hapa jirani kwetu, unawafahamu au sio....wanamiliki mahoteli, magari ya abiria na kadhalika, hivi kweli kipato chao kinaweza kufanya hivyo?’ akaniuliza
‘Ndio, ...inawezekana huenda waliwekeza, wakachukua mikopo, wakaweka miradi wakatajirika...’nikasema
‘Hahahaah, hivi nyie watu mna akili kweli, kwa huo mshahara wa serikali, wanaopata, wafanye hivyo, na kwa muda mfupi tu, waweze kuwa matajiri kiasi hicho, tusidanganyane, ndio maana nataka nikufungue macho, na nimetoa mfano kwa idara moja tu ya serikali...'akatulia kidogo
'Lakini mambo hayo hayapo tu serikalini hata sekta za watu binafasi kuna watu kama hao, wanatumia nembo za makazi yao, nembo za ajira zao,hata imani za dini zao, na kupatia nafasi ya kujitajirisha, hayo yapo, tunayaona na kushangaa wewe unajifanya huyaoni, sasa ni wakati wa wewe kufungua macho na masikio yako, uone.. ...’akasema
‘Kwa vipi?’ nikauliza na yeye akanisogelea na kunigusa na kidole chake kwenye paji langu la uso akawa ananigusa gusa na kile kidole huku akiniangalia machoni kwa makini bila kusema neno kwa muda
NB: Naishia hapa kwa leo,bado afya ina migogoro...hata hivyo tupo pamoja
WAZO LA LEO: Dunia hii kuna mambo mengi ya ajabu, kuna matendo mengi ya ajabu, kama hujakutana nayo huwezi kuamini, lisemwalo lipo.... Cha muhimu ni kuwa makini, kwani maisha ni kuhangaika, na katika kuhangaika uwe tayari kwa lolote, ila uwe makini, usikubali kurubuniwa, au kuwa bendera fuata upepo.
Ni mimi: emu-three
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Pole kaka miram3 mungu atakusaidia. Name story tamu sema ndo hvo hauko poa
Pole kaka miram3 mungu atakusaidia. Name story tamu sema ndo hvo hauko poa
Post a Comment