Nimeona leo tutete kidogo, huku kisa chetu cha 'Baada ya Dhiki ni Faraja', kikiendelea .
Ni muhimu tukaliongelea hili kama utangulizi,
kwani huenda kisa hiki kikiisha tunaweza kuanza kisa kingine chenye mtizamo
huo, japokuwa mengi mengine yatakuwepo. Ni swala zima la ndoa, mahusiano na
mitihani yake.
‘Kwanini mnapenda kuongelea maswala haya ya mapenzi, na ndoa,...hakuna mengine ya kuongelea?’ nikaulizwa hili swali, na jibu lake ni
rahisi tu kama tutakuwa na nia njema, na kuitizama asili ya jamii.
‘Je katika maisha yetu, swala la mapenzi na ndoa halipo?
Ukweli ni kuwa lipo, na pamoja na mengine utaona hili linachukua nusu ya mambo
yetu, kwani huko ndipo tulipotoka, na ndipo tunapoishi na ni maisha yetu ya
kila siku, upende usipende, na mungu akijalia, huko ndipo tunapopata matunda
yake.
‘Haya Matunda yake’ Ni muhimu sana katika jamii, katika
taifa na dunia kwa ujumla ...na haya matunda yake yanategemeana na nyie wawili
mlivyoweza kupata kizazi na kukilea vyema, nyie ndio mliosababisha au mtakaosababisha amani na upendo
katika hii dunia, na kinyume chake pia, ndio maana umuhimu wa hili swala
unapokuja.
‘Ulezi wa watoto’, ndio ngao , ndio nguo, ndio...swala
muhimu, kwa ajili ya kujenga jamii yenye upendo na amani wa hii dunia, lakini
ulezi huu utakuja vipi kama hakuna upendo kati ya wawili walioweza kupata hawa
watoto, utakuta unarudi kule kule, kwenye swala zima la kujadili mapenzi na
ndoa.
‘Ili taifa liendelee ‘linahitaj watendaji wazuri, wenye sifa
zote, kielimu, kimaadili na kiafya, hawa watendaji hawaji hivi hivi, ila
wanatokana na familia, wanatokana na baba na mama, wanatokana na familia
iliyojengwa kwa upendo na amani, je upendo na amani vinatoka wapi, kama sio kwenye
mahusiano mema...Mnapoishi wawili mlijue hili, kuwa kama hampendani, kama
mnanuniana, kama mnagombana, mnakuwa chanzo cha jamii mbaya.
Tusijidanganye kuwa hatuwezi kukaa bila kulijadili hili, ni
kweli yapo mambo mengi ya kujadili ambayo ni changamoto za kimaisha, lakini
haya mambo mengine, yawe ya kisiasa, kiuchumi, au kiutamaduni, ya kuleta
maendeleo, yasingelikuwa ni tatizo, kama tungeliangalia hili, la msingi wa
familia, wapi familia hii ilipotokea, inapotokea, na inatakiwa itokee, ili kujenga
jamii iliyo bora.
Ni kwamba kama tungekuwa na msingi mzuri, wa jinsi gani
kwanza ya kuchagua mume na mke bora, pili, watu hawa waishi vipi basi...na hapa
unaweza kuchungulia nyuma, walivyofanya wazee wetu, utaona kuwa haya mengine
yasingelikuwa ni tatizo...leo hii jamii, ambayo haijui misingi hii, inakaa na
kujadili haki za kuona jinsia moja,hivi hii kweli ni haki ya binadamu, huo sio
ugonjwa jamani, mbona tunamzihaki, bin-adamu...tunakwenda wapi. Haya
ndio matokea yake, wa kulaumiwa ni nani...
Hapa kwa wenye hekima wataona kosa limetoka wapi, ni kuwa,
nyanja hii ya chimbuko la familia kama msingi wa jamii, imeachwa kama ilivyo
ijiendeshe yenyewe tu, kwani kama wanavyosema wengi ambao hawalioni hilo kwa
mapana yake, eti ni swala la asili kwahiyo linajileta
lenyewe,... na kwa msimamo huo ndio maana tumefika hapa tulipo,...Hatuangalii
visa vya maadiko matakatifu, kuwa kwa hiyo kulitokea, gharika, hatujiuliza hii
gharika ilitokana na nini,...hayo sasa tunayaona kama visa vya kitabuni.
Tunajidanganya.
Mzazi bora ambaye
anafahamu wajibu wake atamuelimisha mtoto wake, kwa gharama yoyote ile, kwani gharama kubwa iliyo njema kwa mtoto ni kumsomesha.
Usipomgharamikia mtoto wako leo, ili aje kuwa na maisha bora ili aje kuwa
kiongozi bora, unategemea nini, na gharama ya kumsomesha huanzia ndani kwenu,
wewe na mwenzako, mnaishi vipi, vinginevyo, tuache iwe ya asili tu, ..ndio haya
yanayotokea hii leo katika dunia yetu, kuwa tumeona gharama kubwa kwa mtoto ni
kumnunulia gari, kumjenga jumba la kifahari,...kumnunulia laptop, sherehe za
kuzaliwa za anasa kwa kushindana..
Sawa kwa wenye uwezo hatuwakatazi, ila tufanye kwa tahadhari, kwani vyote hivyo vina mitihani yake, kama huyu
mtoto hajajengeka kielimu kimaadili, na kiitikadi, kwani mwisho wa siku hizo
gharama za hivyo vitu vya anasa, haitakuwa na manufaa kwake, huyo mtoto atavitumia
hivyo vitu kwa kuja kumuangamiza yeye mwenyewe huko baadaye na jamii haitakuwa
na amani tena.
Swala la kujiuliza ni hapa ni hili, huyu mzazi bora anatoka
wapi? Haya maadili mema yanatoka wapi, hiki kizazi bora kinatoka wapi,
utajikuta unarudi kule kule kule kwenye asili, kwenye msingi wa familia, ambao
unatokana na familia yenye upendo na amani. Na huo upendo na amani unatokana na
wazazi walioishi kwa mapenzi na mahusiano mema ambayo yametokana na mume na mke
mwema, waliolelewa na kuijua ndoa na
muhusiano yake.
Kwa wazo hili la leo, blog yenu inawapa pole wale wote walikumbwa
na mitihani ya kimaisha kama kuugua au kuuguliwa, kufiwa,kupoteza ajira, na
mengineyo, na wale wote waliopo kwenye mitihani ya kindoa, kuitafuta ndoa, na
kuipata lakini bado hakuna upendo ndani yake, na pia swala zima la miitihani ya
maisha magumu. Yote haya ni sehemu ya maisha yetu, tusikate tamaa, tuzidi
kuwajibika huku tukimuomba mungu, kwa kila mtu na imani yake,Imani ya dini ndio
sabuni ya kuzisafisha nyoyo zetu ili ziwe na huruma na upendo.
Ahsanteni sana
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment