‘Katika
maisha yangu naogopa sana silaha hasa bunduki, na bastola, na sikutarajia kabisa
ipo siku moja na mimi nitakutana nayo, na mbaya zaidi, ikielekezwa
kwangu,...moyoni nikawa najenga taswira ya kuwa nimeshapigwa risasi nipo
sakafuni natapa tapa...hasa niliposikia milio karibu mitatu ikitokea humo
ndani...’
Tuendelee na kisa chetu...
‘Yupo chumba gani?’ sauti ikanishitua nikiwa
nimezamatulipofika ndani na mimi hapo nikajifanya sijui wapi alipo, nikasema
‘Sina uhakika, mimi sijui yupo chumba gani....’
nikasema na nikakatishwa na kipigo cha kitako cha ile bastola, jamaa alikuwa
akipiga kweli...nikahisi maumivu na haraka nikanyosha kidole kuelekea chumba
alipo mdada,
‘Haya tangulia twende huko huko...’akasema
akinisukuma kwa mguu wake, na mimi nikatembea kwa kupepesuka, nikielekea huko ndani
huku nikiwa na wasiwasi nikijua sasa naenda kukutana na simba aliyejeruhiwa,
kwani nimjuavyo mdada kama atakuwa kapandisha ikianza mambo yake ni bora
ukutane na huyo simba aliyejeruhiwa....
Nikakifikia kitasa cha mlango na kwa mkono
unaotetemeka, nikakishika hicho kitasa cha mlango na kukinyonga, na huyo jamaa
alipoona nachukua muda kukizingusha akakishika mwenye na kuufungua ule mlango
halafu kwa nguvu akanisukumia ndani na yeye akawa nyumba yangu bastola ikigusa
kichwa changu.
Na mimi nikiwa bado na wasiwasi nikatizama
kitandani ambalo nilijua kuwa mdada kalala,...na ilionyesha hivyo, kuna mtu
kalala, kajifunika gubi gubi,
‘Haya mwamushe wewe mwenyewe....’akasema na
mimi nikasogelea kitanda, na kujaribu kutikisa tikisa, lakini kimya...
‘Una uhakika kuna mtu kalala hapo?’ akaniuliza
‘Ndio, yeye anaumwa, kwahiyo nahisi kapitiwa na
usingizi kutokana na madawa anayokunywa...’nikasema na jamaa akanisukuma
pembeni, akasogelea kitandani huku kashikilia bastola tayari kwa lolote akalivuta
lile shuka kwa nguvu....
Ilikuwa kama mlipuko, ilikuwa kama
kishindo...na kilichofuata hapo ni vurugu, haikuchukua dakika, nikasikia sauti
mbili za risasi zikilia, nikajua kuna mtu kafa, nikajihakiki kama sio mimi,
nilipoona naweza kugeuza shingo, nikajua nipo salama,...nilimuona yule jamaa
akiwa sakafuni, huku kajaa damu usoni, nikageuka kuangalia,...mdada alikuwa na
damu zinamtoka begani....
‘Toa hii maiti humu ndani....’sauti ikasema
nikageuka kuangalia pale alipolala jamaa, kweli alionekana kama maiti, uso
umeharibika, umekuwa kama umekwaruzwa na chombo maalumu, na asilimia kubwa ya
ngozi ya usoni haipo.
Huku natetemeka, nikamshika yule jamaa, na
kuanza kumuinua, na mdada akaona ninachelewa akamshika kama mtu anayeshika kitu
kidogo, akamrusha kwa kupitia mlangoni, na nikasikia kishindo cha mtu
akidondoka kama gunia. Sikuamini, ..
Unajua kama unamfahamu mdada, na hicho
kilichotokea ni vitu viwili tofauti, kwani alichofanya ni kama mtu kuchukua
kilo chache kwenye kiroba uinue na kurusha kutoka chombo hiki hicho kigunia
kidondokee sehemu nyingine, varandani...
Nikageuka kumuangalia mdada, nikamuona akitembea
kuelekea mlangoni na mimi kwa haraka nikaindea bastola iliyokuwa sakafuni, ile
naishika tu, nikahisi kitu kikigonga kichwani mwangu, ..nikapoteza fahamu kwa
muda.
Sijui ulipita muda gani, ....ninachokumbuka ni
kuwa nilifungua macho yangu kwa shida na kumuona mdada, akiendea ile bastola
aliyokuwa sakafuni, na kuishika mkononi, hapo nikajua umauti ni wangu sasa,
mdada atatumaliza wote, nikageuka kuangalia mlango, nikauona mlango upo
mbali,...lakini nikasema kimoyo moyo, ni bora nikimbie hata nikifa nijue
nilikuwa na jitetea,...
Nilihesabu moja mbili tatu...nikatoka mbio,
...nilipofika sebuleni pale alipodondokea jamaa nikamuona anajiinua kumbe bado
yupo hai, mimi nikamwambia
‘Kimbia hapa hakukaliki tena....’nikasema
‘Nimeshakufa, imebakia nini, lakini ni lazima
nife na mtu,...’akasema huku akijitahidi kuinuka, na mimi sikusubiria,
nikachomoka mbio kuelekea nje....
Wakati nipo nje, ndio hapo nikasikia tena sauti
ya mlio wa risasi,...na ukelele wa mtu akilia maumivu,...nikahisi kuwa huyo
analia maumivu ya risasi, keshakufa, sijui ni nani, mdada au huyo jamaa, mimi
hapo sikusubiria mbio..kuelekea kwenye pikipiki langu, nilipolifikia, nikasikia
sauti ikisema nyuma yangu
‘Simama hapo hapo ulipo...’nikasinyaa.
*********
Sehemu hii nilisimuliwa nikiwa nimeshikiliwa
kituo cha polisi, alipokuja kunitembelea bosi, na alianza kwa kusema;
‘Pole sana na majanga,... atakuja wakili wa
kampuni kuona jinsi gani ya kukusaidia, unahitajika kumuelezea kila kitu, ukumbuke,
niliyowahi kukuambia kabla kuwa kama kuna tatizo la kisheria, tunahitajika
kuwatumia watu wenye ujuzi nayo,lakini hukutaka kuwa muwazi, ..’akasema bosi akiniangali jinsi nilivyonyong’onyea,
nilikuwa kama mtu aliyenyeshewa, na hajala kwa muda mrefu, nikatulia huku
nimeinamisha kichwa chini.
‘Haya majanga haya yanakukuta, sijui utafanya
nini kukabiliana nayo, lakini hujachelewa wakili wetu atakuja kukusikiliza, na
atatupa ushauri wake, vinginevyo, mimi sijui nikusaidieje, kama wewe mwenyewe
hukutaka kujisaidia, ...’akasema huku
anaangalia saa yake.
‘Umesikia nilivyokuambia lakini...?’ akaniuliza
alipoona bado nipo kimiya
‘Mhh, nimekusikia bosi, nitamwambia kila kitu....lakini bosi,mdada
anaendeleaje ?’ nikauliza
‘Hata sijui ...kama yupo hai au vipi, nimewauliza
watu wa usalama, lakini hakuna aliyetaka kuniambia ukweli mpaka sasa, wanasema
bado wapo kwenye uchunguzi wataongea wakishamalisha uchunguzi wao, ....mpaka sasa
sijui ni nini hasa kilitokea na kuna nini kinaendelea..’akasema bosi
‘Kwahiyo hufahamu kabisa habari za mdada....?’nikamuuliza
na yeye akasema.
‘Kwa hivi huhitajiki kupaniki...kifupi sifahamu
bado, lakini nitafahamu muda sio mfupi,., cha muhimu, ni kujaribu kukumbuka
kila kitu kilichotokea hapo, na pili, kukumbuka mambo muhimu ambayo huenda
yanahusiana na hilo,...ila kwa sasa kwa kukuweka sawa ili kichwa chako kitulie,
kidogo, nataka nikumalizie sehemu hii mwisho ya simulizi langu, ..’akasema
‘Mhh, bosi unafikiri kichwa changu kipo
hapa...sijui kama nitaweza kusikiliza, maana haya yaliyopo mbele yangu ni
makubwa, naona kama nimebebeshwa mzigo nisiouweza...’nikasema
‘Hilo sio shida, akili inahitajika
kutulia,...na ukumbuke matatizo yanapotokea, cha muhimu, ni kuhakikisha kuwa
akili na mawazo yako hayafikirii matokea mabaya, yawe yanalenga matokeo mazuri,
kwa kujipa moyo, ....ili mwili na akili zisianze kuchoka na kukata tamaa...’akasema
bosi
‘Nia na lengo langu ni kukupa ujasiri kuwa
katika maisha ya taaabu, ukavumlia, ukajitahidi, mwisho wa siku
utafanikiwa,....ndio maana nataka kukumalizia sehemu hi muhimu ili nawe uwe na
ujasri fulani akilini mwako....’akasema bosi
‘Kama unana hivyo, sawa...’nikasema
‘Unakumbuka nilikuwambia kisa cha maisha yangu
ni kirefu, na sehemu tuliyokuwa tukienda nayo ni sehemu ya kwanza, na sasa ndio
naimalizia...nitakusimilia hitimisho la sehemu hii ya kwanza ambayo ni mwanzo
wa sehemu ya pili, huku tukimsubiria huyo wakili wetu...ili tuone atakusaidia
vipi...’akasema
‘Lakini bosi mimi sionu umuhimu wa wakili, kwani
mimi nina kosa gani,maana mimi....mhh, ...sijui kilichotokea nilipoona mdada
kabadilika, nilikimbia, huko nyuma sijui kulitokea nini....’nikasema.
‘Hayo utamwelezea wakili sio mimi, au hutaki
nikumalizie kisa changu, maana huenda hutapata muda wa kukisikia tena,
....’akasema na mimi nikamwangalia kwa mashaka.
‘Kwanini unasema hivyo bosi...?’ nikamuuliza
nikianza kuogopa.
‘Kwa jinsi kesi yenyewe ilivyo, nahisi hutakuwa
na muda wa kutulia na kusikiliza mpaka kesi yanyewe iishe, sasa hatujui
itachukua muda gani,....kesi yenyewe imeshagubikwa na mauji...sio kesi ya
mchezo...’akasema bosi
‘Mauji! Unasema mauaji,, ..ni nani kafa...?’
nikauliza kwa mashaka huku nikitoa macho ya uwoga, na yeye akaniangalia na
kusema;
‘Ngoja nikumalizie kisa changu kwanza....akija
wakili atakuelezea yeye mwenyewe kile unachohitajika kukijua na wewe utamsimulia
hayo yaliyotokea ....usimfiche kitu, kama kweli ulifanya hivyo, au ....’akasema
na mimi nikamkatisha na kusema;
‘Kufanya nini bosi, mimi sijui,...sijafanya
kitu bosi....’nikasema sasa nikianza kuogopa.
‘Usiwe na shaka, wakili akija
atasikiliza,...ninachotaka kwa sasa ni kukutuliza kichwa chako, usipotulia na
kuweza kutafakari vyema, unaweza ukajikuta kwenye wakati mgumu,...’akasema bosi
Nikawa sina jinsi ila kutulia na kumsikiliza bosi
akimalizia kisa chake....
*******
‘Siku zikawa zinakwenda na maisha yakawa
yanaendelea na juhudi zangu, zikaleta matunda nikawa na maendeleo mazuri maduka
yangu yakawa yamesheheni viti, na wateja wakawa wanajazana, kwani nilikuwa
nafahamu ni kitu gani mteja anahitajia, jinsi gani ya kumvuta mteja, hayo
niliyasomea na niliweza kuyatekeeleza katika biashara zangu.
Wakati hayo yanaendelea pia maisha ya ndani
nyumba yalikuwa yakiendelea kwani nilijikuta nina mimba nyingine, na hii
nilikuwa nimejiandaa nayo, kwahiyo sikuwa na shaka nayo, kwahiyo niliweza
kujipangia taratibu zangu za kikazi bila kujichosha na bila kusimangwa na mtu
Ukumbuke kuwa nilishapeleka maombi ya kazi, na
kuwa muda niliona kama vile sitaweza kuipata hiyo kazi kwani muda ulishapita,
lakini nilishangaa siku moja naletewa barua ya kuita kwenye usailikwani, kule
nilipopeleka maombi ya kazi, nikajibiwa kuwa nahitajika kufika kwa ajili ya
kufanyiwa usahili.
Kwa vile nilishaanza kazi za biashara, na
nilishajenga uzoefu wa kukutana na watu mbali mbali, kwenda huku na kule, kwa
ajili ya kufanikisha maswala ya biashara, hali hiyo ilinijenga kuwa na ujairi
wa kuongea na kila mtu, kwahiyo hilo la kuitwa kwa usahili halikunipa mashaka.
Kuna kitu nilijifunza katika maisha, ambacho
kinanisaidia mpaka leo ni tabia kujiamini. Ukiwa unajiamini katika jambo lolote
ni rahisi sana kufanikiwa, na kujiamini kunatokana na kuwa na uhakika na kile
unachotaka kukifanya, na ili uwe na uhakika nacho ni lazima uwe unakifahamu,kama
hukifahamu uione soo kuuliza, au kama ni kitu cha kusomea nenda kasome.
Kitu kingine nilichojifunza ni kujituma,
unapokusudia jambo, kujituma kunakupa mori, usifanye kitu kama umelazimishwa,
fanya kwa uhakika, kwahiyo nilipoamua kutafuta kazi, nilikuwa nimejihakikishia
kuwa ninaweza, na sio natafuta kwa ajili ya kupata pesa tu, lakini pia ni
kwa vile nilijua kuwa ninaweza kuifanya
hiyo kazi.
Pamoja na kuwa maiha yangu yalipitia kwenye mitihani
hiyo,ambayo ingeweza kuharibu hata utashi wa kufikiri na kusimamia mambo yako
itakiwavyo, lakini kwangu mimi haikuwa
hivyo, nilijua kabisa kusoma ni nguzo muhimu katika mafanikio yenye tija,kila
muda nilipokuwa napata nafasi, sikuacha kusoma, nilikuwa najikumbusha yale
niliyowahi kujifunza shuleni na vyuoni, kwahiyo sikuwa nimejisahahau sana.
Kitu kingine kilichoweza kunisaidia ni lugha,
shuleni nilikuwa nimejitahidi sana kujua lugha, nah ii ilikuja kunisaidia sana
katika hughuli za kibiahara, maana ukiwa mfanyabiashara unatagemea kukutana na
watu tofauti, na lugha ya kimataifa ni kiingereza, na hilo nililijua nikawa
nimejiandaa nalo,...na ukikumbuka, kama nilivyoelezea awali, darasani nilikuwa
nafanya vizuri sana, kwahiyo pamoja na changamoto hizo za kimaisha uwezo wangu
wa kitaaluma ulikuwa pale pale.
Nikajiandaa kwa taratibu hizo, nilishauliza
natakiwa nijiandae vipi kwa waliobahatika kuajiriwa, na pia kupitia makabrasha
mbali mbali kwenye mitandao, na vitabu, na kwa jinsi walivyonielezea wenzangu niliona
ni kazi rahisi, kwani hayo ya kuongea na wateja, jinsi gani ya kumfanya mteja avutike
na kujiona ni mtu muhimu ndiyo ilikuwa kazi yangu, kwahiyo hayo sikuwa na
mashaka nayo, mimi nilikuwa nayafahamu vyema.
Basi siku hiyo nikajiandaa na kwenda huko
kwenye kampuni yenyewe, nilitarajia kuwa nitakuta watu wengi, wakiwania hiyo
nafasi lakini ikawa kinyume chake,ilikuwa kama walishanifahamu kabla, wakanihoji
maswali yao, na walivutika sana na mimi, na walisema wameshaniona ninafaa,
lakini kwa vile kuna wengine wanatahiniwa, nisubiri nyumbani wataniita.
Siku moja nikapigiwa simu na mtu maarufu wa
kampuni niliyowahi kufanyiwa usahili, kwajili ya kazi ,nilifika haraka bila
kuchelewa na nikapewa barua ya kukubaliwa kufanya kazi kwenye kampuni hiyo,
ilikuwa moja ya kampuni kubwa zya tiketi za ndege na nilianza tu baada ya
kujifungua na kumaliza arobaini kama kawaida yetu.
Sasa naamini kuwa pamoja na shida, pamoja na
dhuluma za dunia, ma madhaidi yetu, tunatakiwa tusikate tamaa, na usiangalia
kuwa wewe ni jinsia gani, kuwa kwa vile wewe ni mwanamke hutaweza, hiyo sio
kweli, ukiwa na ukamlifu wa mwili, hata kama huna ukamlifu huo, lakini una akili
za kufikiri vyema, utafanikiwa tu, cha muhimu na kujibidisha, na akilini jenga
hoja, kama wenzangu wanaweza kwanini mimi nishindwe.
Hutaamini, mimi saa ni mmoja wa wanawake
wanaoweza kujiendesha wenyewe, nina maduka, nina miradi na kampuni ambayo nitakuja
kuelezea kwenye sehemu ijayo jinni gani nilivyofanikiwa kufikia hapo, nayo
ilikuwa na changamoto zake.
Mimi kama binadamu, huwa pia nina mapungufu
yangu, kwahiyo hayo ni lazima nije kuyaelezee pia, kwani mimi sio malaika, nilipofanikiwa
kuna muda na mimi nilianza kujiona, nikaanza hata kumzarau mume wangu nikamuona
mtu wa chini...’akasema na kutabasamu.
‘Inatokea kibinadamu, kwasababu mimi nina uwezo
nina pesa, yeye kidogo, sio sawa na mimi japokuwa na yeye alikuja kujiwekeza
kidogo, kukawa na changamoto zake...yote hayo ni mapungufu ya mwanadamu, na
tutakuja kuyaona kwenye sehemu ya pili ya simulizi letu, kama mambo yako
yakienda vyema ...’akasema bosi na mara akaja mtu na kusimama karibu yetu
Bosi akaniangalia halafu akamgeukia yule mtu,
na baadaye akanianglia mimi na kusema;
‘Huyo ndio wakili wetu, ...’akaniambia na mimi
nikainua kichwa kumuangalia, huku mwili ukianza kuhisi joto...damu ikianza kwenda
mbio, nikijiuliza ina maana sasa natakiwa kusema kila kitu, hata siri zangu..
WAZO LA LEO: Ukweli na
haki ndio msimamo sahihi, ili uweze kafanikiwa, ili uweze kuyashinda majaribu,
ili uweze kufanikiwa, simamia kwenye msimamo huo, sema kweli, na tenda yaliyo
haki.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment