Bosi aliporudi, kwanza alituita mimi na mdada
kutaka kujua maelezo ya hizo hundi na majina ya hao wateja ambalo walilipwa hizo hundi bila vielelezo vya kutambulikana , na mimi nikatakiwa kuleta kumbukumbu zote, za hawo wateja, viambatishi vyake, ikiwemo
ankara ya kuomba malipo na mkataba na hati nyinginezo.
Nilikwenda kwenye file la kuhifadhia
stakabadhi za malipo, nikazitafuta hizo nyaraka lakini hazikuwepo, nihakikisha
tena na tena, sikuziona na nilikuwa na uhakika kuwa niliziweka kwenye hilo
file,...baada ya kutafuta tena na tena, nikakata tamaa, nikarudi kwa bosi na
kumwambia;
‘Hizo kumbukumbu hazipo, stakabadhi za malipo
na nyaraka zake...kwenye file, ...’nikasema nikiwa na wasiwasi.
‘Una maana gani kusema hazipo, ina maana
zimechukulia na mtu, anazitumia labda, au ..mbona sikuelewi, kwanini hazipo
kwenye file lake?’ akauliza bosi
akiwa kanitolea macho ya mshangao.
‘Mimi nia uhakika niliziweka zote kweye file
la malipo na jana tu, niliziona wakati uliponiambia nijaribu kuangalia ni watu
gani hao tuliowalipa malipo bila ukamilifu wa viambatishi vyake..., lakini hivi
sasa zisizioni, ina maana kuna mtu kazitoa kwenye file,....’nikasema
‘Anayehusika na hilo file ni nani?’ akaniuliza
kama vile hajui, kwana anafahamu fika kuwa mimi ndiye mwenye dhamana na hilo
file.
‘Ni mimi, ila watu wakihitajia rejea, huja
kulichukua,na mara nyingi wanaangalia hapo hapo na kulirudisha hilo file,
hawachukui nyaraka, na sana sana anayelitumia
mara nyingi ni Mdada...’nikasema nikikwepa kumuangalia. Mdada akakohoa kama
kunipa onyo.
‘Kwa maana hiyo wenye mamlaka na hilo file, ni
wewe kama mwenye lilihifadhi, hata hivyo mdada, anaweza kulitumia na kuchukua
nyaraka hata bila yaw ewe kufahamu, na akazitumia na kuzirejesha, kama ilivyo
mimi, mimi pia naweza kulichukua hilo file, kama nalihitaji, lakini ni lazima
nikupe taarifa....kwahiyo mnaowajibika kwa hilo ni wewe na mdada?’ akauliza
tena kama vile hafahamu huo utaratibu.
‘Ndio bosi....’nikasema lakini mdada alikaa
kimiya.
‘Basi nyie wawili nitafutieni hizo kumbukumbu,
nazihitajia haraka iwezakavyo...’akasema bosi na mimi nikamwangalia mdada,
ambaye alikuwa kimiya, nikamuuliza;
‘Mdada umezichukua hizo nyaraka kwenye file?’
nikamuuliza na yeye akaniangalia kwa macho makali na kusema.
‘Kama ningezichukua ningelisema, na toka lini
nikachukua file lako bila kukuambia,...’akasema na kuniangalia kwa macho
makali, na mimi nikasema;
‘Bosi, mimi naona ajabu kabisa, maana jana tu
zilikuwepo, na nilihakikisha kuwa zipo, kabla sijalirudisha hilo file sehemu
yake, ...ni lazima kuna mtu kazichukua,...’nikasema.
‘Sasa ni nani....mtafuteni, mniletee hizo
kumbukumbu, ni muhimu sana, maana kama wenyewe wakija kudai malipo yao,
tutasemaje, kuwa tumezipoteza, na wakati hundi zilishakwenda kwao, wakazipeleka
benki, lakini kukapatikana na hitilafu...’akasema bosi.
Sikujua
kabisa nikamuulize nani, maana haijatokea mtu kuchukua file, bila kuniarifu, na
kama mtu anahitaji kitu kwenye hilo file, ananiambia mimi nakitoa na kumtolea
nakala, huwezi kuchukua nyaraka yoyote humo...sasa ni nani kachukua hizo
nyaraka za malipo, ....nikawa najiuliza kichwani bila kupata jibu.
Tukatoka kwenye ofisi ya bosi na kurudi
ofisini kwangu na mdada, na mdada, akawa kimiya akiniangalia kwa makini,
aliponiona nahangaika kuzitafuta akasema;
‘Hivi unaweza kutafuta shilingi iliyozama
chooni...’akasema kama ananiuliza, nikageuka kumuangalia na yeye akageuka na
kuanza kuondoka.
‘Mdada hebu niambie ukweli, umezichukua hizo
nyaraka?’ nikamuuliza
‘Jibu unalo mwenyewe, na haina haja ya kuumiza kichwa,
tumia akili yako, ...wewe ni mhasibu bwana, au ?’ akaniuliza akiniangalia kwa dharau.
‘Sijakuelewa...’nikasema na kumwangalia kwa
macho yaliyojaa hasira.
‘Jamani, ...mhasibu unatia huruma....’akasema huku kashika shavu, na mwingina kama anashika kichwa, kama vile ananionea huruma, na aliponiona namwangalia wa hasira akaondoka, nikabakia nimeduwaa,
Nilibaki peke yangu nikitafakari, nikijaribu kujiuliza ni nani kachukua hizo nyaraka, inawezekana kweli mdada, sasa sijui kwa madhumuni gani, na wakati natafakari huku nikiendelea kutafuta, mara bosi
akatokea,..akaniangalia kwa
makini halafu akasema;
‘Una uhakika hizo nyaraka zipo huko unapozitafuta?’
akaniuliza
‘Kwakweli hapa nimechanganyikiwa , kwasababu
mimi mwenyewe niliziweka, na nina uhakika zilikuwepo, ukiangalia katika
mfululizo wa namba wa mpangilio, inaonekana kabisa kuna mtu kaja kazitoa, na hakutoa kwa utaratibu,
alivuta, unaona mabaki ya karatasi, ya
kuonyesha kuwa wakati anavuta zilichanika...’nikasema na bosi akaangalia na
kugeuka, akasema;
‘Hilo ndilo lililofanya nikawafukuza wahasibu
waliopita, sitaki lirudie tena, nimesimamisha malipo yoyote yanayokwenda benki
ambayo hayana uhakiki wangu, ina maana kila hundi ikienda huko ni lazima
wanipigie simu nihakiki, kuwa kweli anayelipwa ndiye mlengwa, na jana tu,
nimepigiwa simu, kuwa kuna hundi imekwenda huko....’akatulia kidogo.
‘Hundi gani tena hiyo...?’ nikauliza kwa
mshangao.
‘Je zile hundi nilizosaini zikiwa hazina
mlipwaji kwa ajili ay dharura, ulizitumia?’ akaniuliza na kunifanya nishituke,
maana ile hundi aliyochukua mdada, hakunirudishia, nikasema;
‘Hapana..ila, kuna hundi alichukua
mdada,alisema kuna malipo ya haraka yanatakiwa, nikamwambia kabla ya kulipa, ni
lazima nipate hizo kumbukumbu zake, ...sizani kama kaipeleka benki...’nikasema
‘Sikuelewi hapo, ina maana alichukua hiyo
hundi, ikiwa haijaandikiwa mlipwaji, nay eye ndiye aliyeandika ni nani
anatakiwa kulipwa, au sio...nifafanulie vyema, ...?’ akauliza.
‘Ndio hivyo, kwani huyu muhusika, sikuwa
namtambua, yeye ndiye anayemfahamu..’nikasema.
‘Hapana, hapo unaniambia kitu ambacho
hakiingii akilini, toka lini mdada akaandika hundi yeye, ....je akiandika
gharama ambazo sio kweli, je akiandika mtu ambaye hahusiki,...hilo ni kosa
kubwa, sitaki kuliangalia kwa nia mbaya, lakini nataka wewe mwenyewe ulihakiki,
na uniambie ukweli kwanini haya yametokea, kwani nahisi yana maingiliano na
kupotea kwa hizo kumbukumbu, sina uhakika na hao watu waliotakiwa kulipwa...ila
nahisi kuna kitu kisocho cha kawaida kimefanyika...’akasema akiniangalia kwa
makini.
‘Bosi kwani mdada hatumuamini?’ nikamuuliza na
yeye akaniangalia kwa makini na kusema.
‘Sitaki nikufundishe uwajibikaji wa kazi
yako,...nafahamu unafahamu taratibu na kanuni za kazi zako, je hilo
lililofanyika ndio utaratibu wa kazi zako?’ akaniuliza.
‘Kwakweli, hilo limetokea bila kutarajia,
niseme ukweli bosi, mdada alikuja na mambo mengi yaliyonichanganya kichwa, na
hata sijui aliichukua vipi hiyo hundi, nilikuja kugundua haipo, na
nilipomuuliza ndio akanipa maelezo hayo....’nikasema na bosi akaniangalia kwa
mshangao.
‘Mhasibu, upo makini na kazi yako kweli, je
kama nikiondoka ndivyo utakavyokuwa unafanya kazi hivyo, huoni utaleta hasara
kubwa kwenye kampuni, sitaki nichukue hatua yoyote kabla sijalifanyia hili
swala uchunguzi....’akasema huku akiniangalia machoni.
‘Sitaki hayo yaliyotokea huko nyuma yajirudie
tena, ....sasa nakuambia hivi nataka wewe mwenyewe, ufanye utafiti, kama kweli
hujui ukweli wa hayo yote, ni nani hao watu waliotakiwa kulipwa, pili hizo
kumbukumbu zimeenda wapi, na hiyo hundi iliyokwenda hivi karibuni alitakiwa
kulipwa nani, na uje na maelezo yanayojitosheleza kama mhasibu wa kampuni,
maana mimi nafanya uchunguzi wangu pia..kesho wewe na mdada tutakuwa na kikao.’akasema.
‘Sawa bosi....’nikasema huku nikihisi kichwa
kikianza kuuma, hadi nikakishika, nikainama kwenye meza na kutulia kwa muda, sikujua
kuwa bosi bado yupo mlangoni ananitizama, nilipoinua kichwa nikamuona
ananiangalia, yeye hakusema kitu akaondoka.
*********
‘Nimekuita
tuendelee na kisa chetu, natumai unalifanyia kazi hilo swala la malipo na hizo
kumbukumbu zilizopotea...hilo ni jukumu lako na ni dhamana yako, ukumbuke kuwa
dhamana ni deni, ...’akasema na mimi nikawa kimiya
‘Ama kama kuna kitu kinachoendelea hapa, na
unahitajia msaada wangu, nieleze, ili isije nikagundua mwenyewe, halafu ndio
ukaanza kujitetea, sitakusikiliza, na sitasita kuchukua hatua za kisheria,
...sasa hivi nataka kampuni hii ilewe vyema taratibu za kazi, na kanuni za
kazi, na kila mmoja awajibike kwenye nafasi yake....’akasema.
‘Wewe ni mhasibu, hutakiwi mtu akuingilie
kwenye kazi yako, unaona hata mimi sipendi kukuingilia kwenye mamlaka yako,
japokuwa mimi ni bosi wako, sijawahi kuja kukushurutisha jambo ulifanye, huwa
nakuuliza na tunashauriana, sasa iweje, mtu mwingine aje akushurutishe, au
achukua majukumu yako, bila ya rizaa yako, ni nani huyo yupo juu ya sheria na
kanuni za kampuni,....’akawa ananiuliza.
‘Wewe na mdada, mna lenu jambo, na usipokuwa
makini na huyo msichana, utajikuta, unaingia matatizoni, ...nakuona sasa hivi
unahangaika na maumivu ya kichwa, je ulishafanay utafiti ni kwanini sasa hivi
unaumwa sana na kichwa...huoni kuwa hayo maumivi ni kutokana na msongo wa
mawazo, je hayo mawazo yanasababishwa na nini hasa..’akasema kama ananiuliza.
‘Sikiliza mhasibu, usipende kabisa mtu
akakuingilia katika maisha yako,na hasa hasa aktika fani yako, akawa ndiye
usukani wa maisha yako, na fani yako, maana kila mtu anafanya jambo kwa
masilahi yake, na wengina wanachojali ni masilahi bila kujali atahari zake kwa
upande wako, ...’akasema
‘Usiwe kama bendera fuata upepo, utajikuta
mwenzako ananeemeka wewe unaumia, usikubali kabisa kuwa hivyo...’akazidi
kunisisitizia kama vila anafahamu kuwa mdada ndiye nyuma ya hayo yote.
‘Nina muda kidogo, ngoja nikusimulie kisa cha
maisha yangu, ili upate muda wa kuendelea na kazi yako, kwani kesho ni muhimu
sana, nipate taarifa kamili ya hilo tukio , na nataka uniambie ukweli...ukweli na
kutenda haki, ndio njia pekee itakayokusaidia katika maisha yako...’akasema.
******
Katika kisa cha maisha
yangu tuliishia pale tulipofika kwa shemeji, ndugu wa mume wangu, na hapo
tukapata taarifa kuwa mama mkwe hanitaki, na haitambui ndoa yangu na mtoto wake,.....
je kiliendelea nini, hebu tuanzie hapo...
‘Kwani kuna nini kinachoendelea kwanini mama
hanitaki mimi?’ niamuuliza mume wangu na mume wangu alionekana hataki kunieleza
ukweli akasema;
‘Usiwe na wasiwasi ni maswala madogo tu
tutayamaliza...’akasema, lakini kwa tetezi nilizozisikia, wakiongea, ni kuwa
mama mkwe alikuwa hanitaki, eti yeye hakutaka mimi niolewe kabisa na mtoto
wake,sikuelewa ni kwanini!
Niliposikia wakiongea watu humo ndani japokuwa
haikuwa rasimi nilihisi kama vile damu yangu ina mkosi. Moyoni niliumia sana,
pale nilipokuwa peke yangu, niliinama na bila kujijua nikaona machozi
yakinitoka kwa mfulululizo. Nilijuta kwanini sikutilia mkazo ule msimamo wangu
wa kukataa kuolewa, lakini hilo lilishapita siwezi kujilaumu tena.
Nikajikuta nawaza huku nalia, kwanini mimi
maisha yangu yawe hivi, na hata siku muhimu ya ndoa naianza kwa mkosi, ina
maana mimi nina makosa gani, katika hii dunia, ina maana hata huko nilipokuwa
nikiona ndio matumaini yangu mapya, haitakuwa hivyo tena, kama mama mkwe
hanitaki mimi nitakuwa mgeni wa nani.
‘Mume wangu ina maana tunakwenda kuishi na
mama huyo ambaye hanitaki?’ nikamuuliza.
‘Tunaenda kuishi huko, huko, ..usijali...ngoja
tuongee na wanandugu tuone tutaklifanya vipi hili jambo..’akasema. Na mimi
niligundua jambo, mume wangu sio muongeaji sana kama alivyo ndugu yake, na
anaonyesha kuwa hataweza kuwa na msimamo wake kama alivyo ndugu yake. Ndugu
yake, alionekana muongeaji na mwenye msimamo.
‘Kama ni hivi nitakwenda kuishije huko?’
nikajiuliza bila kupata jibu.
Baadaye wanandugu wakaitana tena, kwani muda
ulikuwa unakwenda na taarifa kutoka huko nyumbani kwako, zinasema mama mkwe
hataki kabisa kusikia lolote , kashikilia msiamamo wake. Kwa vile tulitakiwa
kuondoka hapo siku hiyo, wanandugu wakaona wakutane walijadili ili kutafutwe
njia ya kulimaliza, kwani mume wangu, anaishi na familia yao, akiwemo huyo mama
mkwe asiyenitaka.
Wakati wanaongea, japokuwa sikuwemo kwenye
hicho kikao, lakini niliweza kusikia sauti zao, wakijadiliana, kuna mmoja akatoa
hoja, kuwa kwa vile mama mkwe hanitaki, basi kwa muda, nitafutiwe sehemu
nyingine ya kukaa, hadi hapo watakapolimaliza hilo tatizo,
‘Mhh, haiwezekani....’nikajikuta naguna na
kulikata hilo wazo kimoyo moyo.
‘Ina maana kweli mtu ndio umeolewa, unatengana
naye, kila mmoja akikaa sehemu tofauti, kwasababu ya mama mkwe...’nikajiuliza
Wazo la huyo likajadiliwa kukawa na wengi
wanalipinga, na muwakilishi wangu akaingia ndani pale nilipo, kwani kuna mtu
alinisindikiza ambaye atarudia hapo na kunifahamisha jinsi kikao
kinavyoendelea, akasema anawasiliana na wazazi wangu, kama inawezekan nirudi na
yeye
‘Kweli hilo ni wazo zuri, kama hawa watu
hawajajipanga nikakae nyumbani, wakiwa tayari ndio waje kunichukua...’nikasema
‘Sawa ngoja niongee na wazazi wako...’akasema
na kuwapigia simu wazazi wangulakini
Wazazi wangu wakalipinga hilo wazo, wakasema,
mimi sasa sio mtu wao, nahitajika kuwa pamoja na familia ya mume wangu, na hilo
la kusema mimi nikaishi sehemu nyingine, wao hawaliafiki, hata hivyo, wao
hawawezi kuingilia mambo ya huko, hayo ni mambo yangu na mume wangu, yule
muwakilishi wangu akasema;
‘Mimi niliona wazo jema, mimi nirudi na bibi
harusi huko nyumbani, tuwaache hawa watu wakamalizane na mama yao, wakiwa
tayari ndio wamchukue mke wao...’ akasema
‘Haiwezekani hilo halipo, na usije ukalitoa
hilo wazo kwenye kikao chao, wao wanajua ni jinsi gani ya kulitatua,
hawajatuomba msaada, huyo ni mtu wao....’wakasema wazazi wangu.
‘Hamuoni kuwa mtoto wetu ataenda kuishi maisha
mugumu huko anapokwenda?’ akauliza huyo msindikizaji wangu.
‘Hayo ni kawaida tu, na ni maswala ya muda,
yatakwishi, yeye anatakiwa kumtii mume wake, na familia hiyo....’wakasema
wazazi wangu, na huyo msindikizaji akawa ahana jinsi,akaniambia jinsi wazazi
wangu walivyosema, na mimi nikasema;
‘Ina maana kweli wazazi wangu hawanitaki tena,
ni kama walinitupa, wameniozesha kwa nguvu kwa mume ambaye sikuwa na mapenzi ya
yeye, na haya yanatokea, bado ahwataki kunisaidia...’nikasema kumueleza huyo
jamaa yetu aliyenisindikiza.
‘Sio hivyo, sio kwamba hawakutaki, hayo ni
maswala ya ndoa, yana taratibu zake ukishaolewa, unakuwa sio mtu wa familia
yenu tena, wewe ni mtu wa familia ya mume wako,...wazazi wako hawatakiwi
kuingilia mambo yenu,mpaka waombwe kufanya hivyo...’akasema.
‘Sasa mimi wananiweka katika hali gani?’
nikauliza
‘Cha muhimu wewe ni kusubiria tu, watakubaliano
jinsi gani ya kufanya na wewe huna hiari, watakavyosema wao, ndivyo
utakavyofuata...’akaniambia.
Kwa hali kama hiyo mimi nikajiona sina raha,
nikajiona mpweke, wazazi wangu hawataki kunipokea, huku kwa mume mama mkwe
hanitaki. Nikawa sina jinsi ila kusubiria yatakavyoamuliwa. Baada ya
majadiliano marefu wakamua kuwa twende huko huko kwa mama mkwe.
‘Atakubali tu, maana ndoa imeshafanyika, hana
uwezo wa kuivunja...’akasema shemeji.
‘Je kama akikataa kabisa tutafanya nini,...?’
akauliza mume wangu.
‘Hawezi kukataa, ni hasira tu, mama ni mama
tu, atafikia muda atakubaliana tu, unachotakiwa wewe ni kuwa na msimamo na ndoa
yako...’akasema shemeji.
Mimi
nikiwa ndani, nikawa namkabidhi mungu, maana sikuwa na la kufanya, kama nyumbani
hawanitaki nitakwenda wapi, na kama huko kwa mume sitakiwi, ina maana mimi ni
mtu wa kusubiria tu, ni kama mkiwa sina la kufanya,...nikatulia, na mara mume
wangu akaja, na kuniambia;
‘Tunaondoka usiku wa leo, jiandae...’akasema
‘Na mama mkwe keshakubali....?’ nikauliza.
‘Atakubali tu, ni hasira za muda, ....mambo
yote tutayajua huko tukifika...’akasema.
‘Kama hanitaki kwanini ulikimbilia kunioa?’
nikamuuliza na yeye akaniangalia kwa muda baadaye akasema;
‘Kwani yeye ndiye aliyekuoa au ni
mimi...unachotakiwa kunisikiliza ni mimi, ....’akasema.
‘Sawa lakini mama ni mama, unatakiwa
umsikilize mama yako...’nikasema
‘Kwahiyo nikuache, ndivyo unavyotaka...?’
akaniuliza
‘Mimi ninachojiuliza ni kwanini, kama mama
yako alikuwa hanitaki ukakimbila kuja kushinikiza unioe?’ nikamuuliza
‘Nimeshakuambia kuwa mama sio anayekuoa, mimi
ndiye niliyekuoa, hilo linatosha mengina tuachie sisi wenyewe, tutajua jinsi
gani ya kuongea na mama...’akasema na kuonyesha kukerwa na kauli yangu hiyo.
Tukajiandaa kwa safari hiyo ambayo ilifanyika
usiku, na ilipofika usiku tukaondoka kwenda kukutana na mama mkwe asiyenitaka.
WAZO LA LEO: Tusikate tamaa na maisha pale tunapokutana na mitihani mbali
mbali, cha muhimu ni kuangalia kuwa tumesimamia kwenye ukweli na haki.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Outcomes will certainly differ depending upon the individual.
Lots of see results within the very first week, and most will find their garments fitting better by the end of the first month.
Also visit my website: garcinia cambogia extract (imobileface.com)
Post a Comment