Siku mbili ambazo niliachiwa ofisi zilikuwa za
mtihani mkubwa kwangu, kwani Mdada, alinikalia kooni, alitaka pesa nyingine
zaidi, na hata kufikia kunitishia kuwa anaweza kuniharibia maisha yangu kama
sitakubaliana na matakwa yake;
Baada ya kunioana nimekataa kata, kata,
akaamua kuniingia kwa njia nyingine, na kuanza kuongea;
‘Sikiliza mpendwa, hii ndio nafasi yako pekee,
ya kumaliza shida zangu na zako, na wenzako walikuwa wakifanya mambo yao wakati
bosi hayupo, kama alivyoondoka hivi sasa, ...’akasema na mimi nikawa sitaki
hata kumsikiliza kwani akilini mwangu nilikuwa nawaza jinsi gani bosi akigundua
hayo malipo, atakavyokasirika na ndio mwanzo wa kutokuaniamni tena.
‘Mpenzi, unajua mimi kila ninachokifanya
nakufikiria na wewe, usione kuwa nimefanya ile kwa dili kwa ajili yangu tu,
nikuambie ukweli, hilo gari likitoka bandarini, litakusaidia na wewe
hutatembelea tena ile pikipiki wewe ni mhasibu mwenye sifa zote za kuwa na
gari,...usione kwa vile hilo gari litakuwa limeandikishwa kwa jina langu ndio
uone kuwa ni langu,hapana, mimi ni mtu mwema sana, hili gari lina mkono wako,
kwahiyo kiundani mimi wewe ni mau
muhimu, hilo gari ni letu, hasa kama mambo yatakwenda vyema, na ukaweza
kuachana na huyo mshamba....’akaniambia.
‘Mdada, naomba hiyo kauli yako ya dharau, ya
kumuita mchumba wangu mshamba uachane nayo, ..humfahamu vyema, na sivyo kabisa
kama unavymfikiria wewe...mimi ndiye nilimuhadaa, tukashindwa kuvumilia,
ikatokea hilo lililotokea, hata mimi ninajuta sana kwa tendo hilo...’nikasema
‘Hahaha...wanaume bwana, ...haina haja ya
kuniambia hayo..nafahamu yote, ...na ukiwa sambamba na mimi,
tutayamaliza,...nafahamu kabisa moyoni unanipenda sana mimi, kama
ninavyokupenda wewe...cha muhimu, nisikilize, ....utaona matunda yake...kwanza
unaona hii dili ilivyopita kilaini, ulikuwa unaogopa nini..hivyo ndivyo
wanavyofanya wenzako....’akasema
‘Mdada, mimi sitaki kabisa unihusishwe na
mambo yako, sijui cha gari lako wala pesa hizo ulizochukua, hayo mambo ni yako,
kwangu mimi nafahamu kuwa pesa hizo zimetoka kwa bahati mbaya kwa wateja,
sikuwa makini kuangalia nyaraka zao, nikalipa nikujua kuwa ni wateja wa kila
siku, wa kusafirisha mizigo...kwahiyo hata bosi akiniuliza nitasema hivyo na
hivi sasa natayarisha ripoti yangu...’mimi nikasema
‘Unasema nini, kama unataka kufukuzwa kazi na
hata kufungwa wewe fanya hivyo,...andika huo ujinga wako kuwa ulikuwa hujui,
..eeh, umelipa kwa bahati mbaya, ...wewe kweli huna akili, kwa mtaji huo
utakufa masikini, nikuambie ukweli, hilo halitajulikana kabisa na likijulikana
wewe kama mhasibu utajua jinsi gani ya kulifunika, ..hivi wewe mbona upo
hivyo..’akaniambia
‘Huwa hatuendi hivyo, sio kwa vile unaitwa mhasibu,ndio
unafahamu jinsi gani ya kutafuta pesa kwa njia haramu, najuta kwanini
niliziandikia zile hundi, sitafanya hayo makosa tena, ....maana najiingiza
kwenye matatizo ambayo sina faida nayo...’nikasema
‘Nimeshakuambia gari hilo ni letu, na sasa
nataka kumalizia nyumba yangu,...nataka iwe yetu , mimi na wewe...nimekuja na
mpango mwingine, nikufundishe jinsi gani ya kutafuta maisha,....’akaniambia
‘Ina maana unajenga, na kujenga kwenyewe ni
kwa pesa za wizi..?’ nikamuuliza
‘Nani kaiba wewe..huu sio wizi, ni ujanja
kutumia elimu yako kwa faida, sio wizi, maana wenzetu wanatumia jasho letu,
nguvu zetu, wanatulipa mshahara mdogo, wanajijenga, na sisi tukipata mwanya wa
kuzirejesha nguvu zetu walizotunyonya inabidi tufaye hivyo, bila hivyo, hebu
niambie utajenga lini...’akawa kama ananiuliza.
‘Tutajenga tu....kuna njia nyingi halali, ...’nikasema.
‘Kama zipi, hebu niambia kwa huo mshahara wako
utajengaje,...sasa hivi ndio unatarajia kuitwa baba, ..ina maana majukumu
yanaongezeka, kwa hiyo gharama za maisha zinaongezeka, kipato chako kinapungua,
si ndio hivyo, mhasibu...’akawa kama ananiuliza
‘Kila kitu kina wakati wake, na mipangilio
yake, ikifika muda huo, nikiwa na familia, nitajipanga upya, lakini sio kwa
njia hiyo unayotaka wewe, hiyo sio haki,....’nikasema
‘Nisikilize kwa makini, mimi ninachotaka ni
kukusaidia wewe kwa kukupanua akili yako na mawazo, mimi nafahamu jinsi gani
wengi waliotajirika wanavyofanya, nimekaa nao nakuwauliza kwa undani, hasa nyie
mnaojiita wahasibu, wengi waliojaliwa nimejaribu kuwadadisi na kuwachunguza...’akasema
‘Hakuna mtu anayeweza kufanya uchafu huo
akakuambia, hilo nalipinga, hayo ni mawazo yako ...’nikamwambia.
‘Hahaha, uchafu huo....mimi ni mtoto wa mjini,
nikitaka jambo ni lazima nilipate, hiyo ndio siri ya maisha yangu,...’akaniambia
‘Unataka kusema nini?’ nikamuuliza
‘Nimekuja na mkakatai wa kukusaidia wewe, na
kukusaidia wewe ni pamoja na kujisaidia mwenyewe, hakuna kitu cha bure siku
hizi, asikudanganye mtu, ukiona unafanyiwa fadhila ujue kuna gharama zake...unisikilize
kwa makini....’akasema
‘Unataka nini tena, hebu subiri, tuangalia
hili janga ulilolifanya litaishaje, na sijui utalimazliza vipi, maana kiukweli
ni lazima bosi akiniuliza nimwambie ukweli...’nikasema
‘Utamwambia ukweli gani, hebu niambie, ..ukimwambia
utaonekana mjinga, hujui kazi yako, na utaonekana unafahamu mpango wote,
kwanini ulikimbilia kuzipitisha hizo nyaraka, kwanini uliandika hiyo hundi,
kwanini hukumwambia bosi wako...tumia akili, hilo cha kufanya ni kulinyamizisha
kiaina, lisahau, na katika mahesabu yako lifiche kinamna,...ukipiga gharama
zake, unaziweka kwenye sehemu isyogundulikana, mimi nafahamu yote hayo....’akasema
‘Oh...kweli una ndoto za ajabu,siaminu,
nilikuwa nakuona mtu mwema, na nilivutika sana kwako, nikijua una mapenzi ya
dhati, ...lakini sasa naanza kukuogopa, ...’nikasema na yeye akanisogelea na
kuanza kunipitisha mikono yake mgongoni, na kusema;
‘Sikiliza mpendwa, mimi nakupenda sana, ndio
nafanya haya yote, ...ili na wewe uwe mtu miongoni mwa watu, nakutafutia maisha
bora, usione wenzako wana maisha bora ukafikiri wamefanya kihalali, hakuna
hiyo, asikudanganye mtu......sasa nataka mimi na wewe tuwe kitu kimoja, na ....’akachukua
simu yake, iliyokuwa ikiita,;
‘Halloh mpenzi, niambie dear,.....umeshaupata
huo mzigo, ....?’ akauliza
‘Unasema nini, haiwezekani, kwani uliambiwa
nini ulipozipeleka benki?’ akauliza kwa mshangao, huku akiniangalia kwa macho
yaliyojaa mshangao, akasikiliza kwa muda halafu akageuka kama anataka kutoka
nje, halafu akasema;
‘Usijali, nitahakikisha nalifanyia kazi,
...naomba tafadhali, nisaidia, litoke hilo gari,....nipo chini ya miguu yako,
unaona livyojitahidi, ...fanay unavyoweza, mimi nitahakikisha unazipta hizo
pesa...ngoja nifanye uchunguzi, maana sijui kwanini wamezikataa....’akasema na
baadaye akakata simu na kuniangalia.
‘Ujinga gani umefanya wewe mtu...’akasema kwa
hasira huku kanitolea macho
‘Mimi sikuelewi, unaongea nini...’nikasema
huku sijui kwanini ananiambia hivyo
‘Zile hundi mbili, za hao wafadhili, ....ambao
ndio wananisaidia kutoa hilo gari zimekataliwa benki, zimezuiliwa....ni nani
anaweza kufanay hivyo kama sio wewe
mhasibu maana bosi hayupo...niambie kwanini umefanya hivyo?’ akaniuliza huku
akiwa kanitolea macho ya hasira.
‘Kama imekuwa hivyo, mbona nitashukuru sana,
..kweli wamezikataa,oh, ahsante mungu, ...’nikasema huku nikiangalia juu
‘Wewe mjinga, na utakufa kwa umasikini, na
sikiliza sasa hivi nampigia baba mkwe wako na namtumia mapicha ya uchafu wako,
si unajiona wewe ni mjanja, ngoja nikuonyeshe kuwa mimi ni nani...’akasema na
kuchukua simu akapiga, mimi nilijua kuwa anatania, akasema;
‘Shikamoo, baba, ni mimi, nilikuwa nakujulia
hali na kukupa taarifa ya kile ulichoniambia nikufanyie kazi...ndio baba,
nitakutumia taarifa zote, ....mmh, yupo ofisini kwake, kama unataka kuongea
naye....hebu subiri nimfuate....’akasema na kuiziba ile simu sehemu ya
kusikilizia akasema;
‘Ili kukuhakishia kuwa mimi sitanii, ongea na
baba mkwe wako...’akasema huku akinipa simu, na mimi nikiwa nimeduwaa,
nikaipokea hiyo simu, na sikujua niongee nini, nikawa nimeduwaa, nikaiweka
sikioni.
Sauti
ya baba mkwe wangu ikawa hewani, na mimi kwa heshima nikasema;
‘Shikamoo mzee, ...’nikasamilia
‘Nimesikia taarifa zako....’akaanza kuongea
‘Taarifa zangu,....hapo nikahisi mwili
ukiniisha nguvu, nikamwangalia Mdada, ambaye alikuwa akitafuta kitu kwenye
kabati langu, nilitaka kumzuia, lakini baba mkwe alikuwa hewani, na mara mdada
akatoa kitabu cha hundi akakifungua na nilimuona akitoa nakala moja ya zile
hundi alizosaini bosi, akaichana na kuanza kuondoka nayo...
‘Ndio taarifa zako...’akasema baba mkwe, na
hapo nikawa nataka kumkimbilia mdada kumzuia, na huku nataka kumsikiliza baba
mkwe anataka kuniambia nini kuhusu hizo taarifa zangu..
***********
Nikiwa nyumbani, bosi alinipigia simu,
akaniambia benki walimpigia simu, na kumpa taaarifa za hundi mbili zisizo
kamilika vigezo vya malipo, ..
‘Hundi gani hizo bosi....?’ nikamuuliza huku nikiwa
na mawenge kichwani, kichwa kilikuwa kinaniuma sana, na nilitaka kukipooza kwa
kinywaji.
‘Sijazijua vyema, na hata huyo mlipwaji
simtambui vyema, nikaona jambo jema ni kuzizuia, hadi hapo nitakaporudi, jaribu
kuzitafiti, umeshapitia nyaraka zote vyema?’ akaniuliza
‘Nilipitia wakati ule naandika, na kwa vile
nilikuwa naandika kwa haraka, huenda niliandika bila kuangalia vyema, ngoja
nipitie tena...’nikasema
‘Tafadhali fanya hivyo, na hakikisha kuwa hawo
wateja, unaangalia mikataba yao, kama kweli wapo kwenye kumbu kumbu zetu au
wametoka wapi, na ongea na mdada, yeye anawafahamu wateja wote, ni muhimu sana
na wewe ukawafahamu ....’akasema
‘Sawa bosi nitafanya hivyo, samahani sana,
maana imenijia kwa mshituko, sikuwa na wasiwasi, nilijua kuwa mdada,
kaambatisha kila kitu...’nikasema.
‘Katika kazi hasa hiyo yako, usimwamini mtu
yoyote, unachotakiwa kuamini ni nyaraka, ni kumbukumbu za malipo, sio
mtu,...inaweza mtu mwingine akatumia mwanya wa uzaifu wako kujipatia malipo
yasiyo sahihi....sitaki nikufundishe majukumu ya kazi zako, lakini ni muhimu
sana uwe makini...’akaniambia
‘Sawa bosi nitahakikisha kuwa hilo
halitarudiwa tena....’nikasema
‘Sijui, hilo ni jukumu lako, usije
ukaghilibiwa na uzuri, tamaa, udugu na kujuana, katika kazi yako, ukiwa katika
kazi yako, kumbuka, stakabadhi, kumbukumbu, mikataba, na nyaraka ndizo kigezo
cha malipo ....hakuna jingine, ....na hakikisha umepata taarifa za hawo watu
wawili, niliozuia hundi zao, nikirudi nipate maelezo....’akasema
‘Sawa bosi...nimekusikia, nitafanya hivyo ....’nikasema
huku nikikumbuka hiyo hundi nyingine aliyoichukua mdada, sijui kaanzika kiasi
gani, na kwa nani...
‘Je kuna malipo mengine umeyafanya kwa hivi
sasa?’ akaniuliza na hapo nikashikwa na kigugumizi, na hakusibiri jibu langu
akasema;
‘Nina salio kidogo hapa, ngoja nikusimulie
sehemu ya kisa changu, halafu kama kuna lolote utaniambia....’akasema na kuanza
kunisimulia sehemu hii ya kisa chake...
*********
Nikiwa nasubiri hiyo ndoa, akili yangu
ilishajenga mipango mingine, kuwa nikatae kabisa kuwa mimi sipo tayari kuolewa
na huyo mtu, kwani simpendi na ndoa hiyo ni kama ya kulazimishwa, na niliona
ndio njia pekee ya kuwakomoa hawa watu, lakini kwa upande mwingine, nilimuonea
huruma mama, ina maana lolote litakalolifanya hapo, madhara yake ni kwa mama
‘Hapana, siwezi kukubali, ni lazima
niwaonyeshe baba kuwa na mimi naweza kujiamulia mambo yangu mwenyewe, ...lakini
mama ataumia sana,..sasa nifanye nini...’nikasema kimoyo moyo.
‘Je umekubali kuolewa na ndugu fulani, kwa
mahari yake....’nikasikia nikiulizwa, ilikuwa kama sipo, na hata yule muulizaji
akashikwa na mshangao, kwani aliniona kabisa kama mimi sipo makini..yeye kabla
hajauliza tena, akamnong’oneza msaidizi wangu, na msaidizi wangu, akanisogelea
na kuniuliza
‘Vipi kuna tatizo mbona umekuwa hivyo, unaumwa,
nikawa kama mtu aliyeshituka toka kwenye usingizi, nikasema;
‘Hamna tatizo...oh, samahani, siumwi, nipo
tayari,....’nikasema na kukaa tayari, na huyo mtu wa kufungisha ndoa akaanza kuniuliza
maswali tena, na wakati huo nilishaamua ni nini la kufanya, lakini mdomo
haukufanya hivyo, nikajikuta nikikubali, sikuweza kupinga tena, nikakubali kuwa
nimekubali kuolewa na huyo mume, ndoa ikafungwa.....sehemu hiyo ikapita, na
kutangazwa kuwa mimi sasa ni mke halali wa mume wangu,....
Baada ya ndoa, kukawa na shamra shamra ndogo,
kama ilivyoandaliwa, ilikuwa kama sherehe ya kifamilia tu, japokuwa kulikuwa na
vigelegele vya hapa na pale, na washambenga wakibeza kwa kusema;
‘Hii ni harusi gani, ni harusi ya mkeka...’
Hata hivyo mimi nilishukuru, nikijua sasa mimi
ni mke wa mtu , sina ujanja tena kwani lile jukumu muhimu la harusi ambalo ni
kufunga ndoa limekamilika, mengine ni kushehesha tu, na hapo nikawasikia
wengine wakiimba huku wakiruka ruka;
‘Mlisema hayawi sasa yamefika, mke kapata
bwana, ....’kukawa na nyimbo za hapa na pale na nyingine za kupigana vijembe,
hata hivyo ukweli ulibakia kuwa harusi hiyo haikuwa kama zilivyokuwa harusi za
wengine, hata hivyo, sikuweza kumlaumu mtu au kuweka kinyongo dhidi ya yoyote
yule.
Ilipofika saa za usiku kukawa na chakula cha
usiku na walialikwa majirani baadhi tu kama ilivyo kuwa kwenye ndoa wakajumuika
kupata chakula rasimi cha usiku. Na baada ya chakula cha usiku mie na mume
wangu tukaenda kupumzika kama ilivyo kuwa kasumba ya ndoa.
Ukumbuke kuwa mume huyu sikuwa na mazoea naye,
na moyo wangu hakuwa umempenda, kwahiyo hapo sasa nilitakiwa kuyaondoa hayo, na
kujenga hisia nyingine kuwa sasa huyo ni mume wangu, ...nikajitutumua na
kutimiza yale niliyofundishwa, kuonyesha upendo wa dhati kwake, hasa siku hiyo
muhimu ya kwanza.
Kwenye maeneo yetu, na taratibu zetu, kuna
jambo linafanyika, unapoolewa, na usiku huo wa kwanza wa kukutana na mume wako
ni usiku muhimu sana, wa kupima uvumilivu wa mwanamke, je kweli aliweza
kujitunza, na ili usiku huo aweza kumpa mume wake zawadi muhimu,...
Ni mila na desturi, ambazo zilimlenga zaidi
mwanamke, kwa mwanaume, hana tatizo, yeye, ni kufanya kazi yake,na baada ya
akzi hiyo, ushahidi huo hutolewa asubuhi na mapema, bila kificho,
Kwahiyo kama ada, kesho yake baada ya kufunga
ndoa, na tendo la usiku wa kwanza kati ya mume na mke, watu hufika asubuhi kusubiria
kwa hamu matokeo ya tendo hilo la kwanza lililofanyiaka usiku kwa wanandoa hao,
hilo litampa sifa mama mzazi na muolewaji au kuwaumbua, na watu hawana dogo,
hata wale wasioalikwa hufika asubuhi na mpema, ili yasiwapite.
Na kweli, kama ilivyo ada, watu wakafika
wakiwa wana yao, kama ilivyokuwa nyuma, wengi walishanipaka matope kuwa mimi ni
muhuni wa siri, japokuwa sikuwa anjionyesha, na wengine wakasema nilifukuzwa
shule kwa sababu ya uhuni wangu, hata kutembea na walimu, na wengine wakawa
wananitetea, na kwa malumbano hayo kukajenga makundi mawili, yenye mtizamo
tofauti.
Bila kutarajia, watu wakawa wengi sana,
asubuhi, kuhakiki, vinywa vya watu,na waliyosikia juu yangu, na wengi
walishajiandaa kuniumbua, kuwa kweli mimi ni muhuni, na sikuwa nasingiziwa, na
hata wale wasio na simile, wakaanza kusema;
‘Hivi mumewahi kuja asubuhi hapa kusubiria
nini, huyu anawezaje kuwa bikira kwa jinsi ya tabia yake ilivyo, mnajisumbua
bure...,?.’wakasema wale walionipaka matope
‘Ni muhimu tufike tuhakikishe...’wengine
wakasema.
Ikafika muda muafaka,Matroni, akaingia chumbani, akalibeba shuka jeupe, ambalo lilikuwa
limetandikwa rasimu kwa kazi, hiyo, na kutoka nalo nje,huku akiwa kalifunua ili
kila mtu aone, na watu hapo wanasukumana, kuhakiki, kama unavyojua wafunua
vinywa, wasiotaka kupitwa na kitu.
Kinyume na matarajio ya wengi, kinyume na
matope waliyonipaka, kila mtu liyeliona hilo shuke, alibakia mdomo wazi, na
wengine, wakajifanya kama hawakuona, ilimradi kukazuka namna fulani ya gumzo la
chini kwa chini, ooh, unaona, eeh, ilikuwa hivi, aaa, wewe ndiye ulisema,....aibu,
wakashushuka, hasa wale waliojaribu kunipaka matope, wakiongozwa na mama wa
kambo.
‘Mumeona hamjaoana...?’ akauliza matroni kwa
kusheheneza
‘Tumeoana,...’wakasema watu na kupiga viegele
Watu wengi walishikwa na aibu na matron kwa kushabikia, akawa
anawapitishia watu kwa karibu ili waone, hizo ni mila na desturi zetu, na kwa
muda huo wazazi wanakuwa pale mbele, ili kupewa pongezi, au kinyume chake.
Wazazi wangu ambao hawakutaka hata kukaa pale
mbele wakijua ni aibu, waliposikia watu wanashangilia, wakajitokeza, na mama wa
kambo ambaye alihisi kuwa watu wanashngailia kiushabiki tu, kwa vile
nimeumbuka, akajitokeza kidogo, na alipoona ule ushahidi, akawa kashikwa na aibu,
baba ndiye aliyebakia mdomo wazi,akionyesha kama haamini, maana yeye ndio kabisa, alikuwa keshaamini maneno
ya watu wa nje, kuwa mimi ni muhuni, malaya, na mara nyingi alikuwa
akimsikiliza mke wake, bila kujali utetezi wangu.
Basi mume wangu akatoa zawadi kwa mama yangu
mzazi kwa malezi bora, na kushukuru kwa kumpa mke aliyekamilika, na harusi ikawa
imekamilika kihivyo, na kilichobakia kwa siku hiyo ni kupata chai maalumu ya
asubuhi ya kuagana, na sisi , yaani mimi na mume wangu na watu wake aliokuja
nao,tukajiandaa kwa safari ya kwenda huko kwa mume.
Hapo kikafuata kipindi cha majozi, maana mtu
unaagana na familia yako,wazazi wako unawaacha, ndugu zako unawaacha, unakwenda
kukutana na wazazi wengine, ambao hata kuwafahamu vyema, huwafahamu, na hujui
utakwenda kukutana na maisha gani huko mbele, zaidi ya mungu wako kukusaidia.
Nikaagana na ndugu zangu, na baba, na mama wa
kambo, ambaye aliona aibu hata ya kuongea na mimi, zaidi alisema, ; `haya,
nenda sasa ukayaone maisha halisi ya mume na mke, maisha ambayo wengi
walinilaumu, ...utajionea mwenyewe jinsi gani ya kuishi na watoto wa wenzako...’akasema
kwa kujitetea, na mimi sikumjibu kitu.
Nikaagana na mama, mama chozi lilimtoka,
akanikumbatia na alishindwa hata kuongea, na baada ya kunikumbatia kwa muda,
akasema;
‘Mwanangu kumbuka niliyokuhusia, huko
unakwenda kwa baba na mama mwingine, unatakiwa kuwaheshimu kama ulivyokuwa
ukituheshimu sisi, utakutana na mitihani mingi, lakini ipokee yote kama maisha
ya kawaida,mtii mume wako, kwani yeye ndiye kila kitu kwako..nakutakia
kila-laheri, tukijaliwa tutakuja kukuona...’akasema mama, na mimi nikashindwa
kuvumilia, nikajikuta nikilia...
‘Muda umefika mwache aondoke, ...’akasema
baba, na kweli, safari ikafika, na ikabidi niondoke kutoka mikono ya familia
yangu na kuingia kwenye familia ya mume.
Ilikuwa safari ndefu kidogo, ya kwenda mkoa
mwingine, na ili kufika huko ilibidi kwanza kupitia kwa shemeji yangu, ndugu wa
mume wangu, na hapo tukakaribishwa kidogo, na shamra shamra za hapa na pale,...
Niliona kuna sintofahamu inaendelea, kwani
mume wangu aliitwa, wakawa an kikao chao, baadaye akaja kuniona akaitwa tena,
nikahisi kuna jambo ambalo halipo sawa, baadaye, shemeji akasema;
‘Mama hamtaki shemeji....kama mlivyojua,hakutaka
hiyo ndoa, na kashikilia msimamo wake huo huo, kasema kabisa yeye haitambui
hiyo ndoa...’akasema shemeji, na kunifanya nibakie na mshangao, sikuelewa
kwanini huyo mama mke haitambui hiyo ndoa yangu na mtoto wake.
'Na kwanini hanitaki mimi..'nikajiuliza kwani sikumbuki kukutana naye kabla, na nilishindwa hata nimuulize nini mume wangu,
maana hata yeye alionekana hana raha kwa akuli hiyo, wakawa wanajadili na ndugu
wafanye nini, baadaye mume wanagu akafika, nikasubiri kusikia atasema nini...
NB: Ni kwanini, tutapata sehemu ijayao.
WAZO LA LEO: Ndoa ni kati ya mume na mke, na iliyotokana na ni kiapo cha ndoa,
cha kukubaliana, baada ya kiapo hicho, hiyo ni familia inayojitegemea, japokuwa
ina mfaungamano na wazazi wa pande zote. Cha muhimu kwa wanandoa ni mipangilio
ya jinsi gani ya kuishi. Wengine watahitajika tu kama washauri, lakini sio
kuingilia ndoa hiyo tena, labda kama kuna tatizo ambalo mnaona ni muhimu ili
kuiokoa hiyo ndoa. Kuna watu wanapenda kuingilia ndoa za watu, na hata kumkataa
mume au mke,...tusifanye hivyo, tunakiuka mikataba ya ndoa, na kuhini imani
zetu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment