‘Ninahitaji milioni kumi na tano....’Mdada
akaanza kuongea na kunifanya nishikwe na kikohozi, hata kile kinywaji
nilichokuwa ninakunywa kikamwagika, na aliponiona jinsi nilivyoshituka,
akacheka na kusema;
‘Kwanini umeshituka hivyo, ....kutaja hizo
pesa ndio umeshituka?’ akaniuliza
‘Milioni kumi na tano! Mbona pesa nyingi
hivyo, za nini na zitapatikana wapi?’ nikamuuliza.
‘Kwani kwenye biashara pale ofisini, nyaraka
moja ya biashara, kutoka kwa ,mteja inafikia shilingi ngapi?’ akaniuliza
‘Nyaraka za kutaka malipo ? una maana invoice, oh, ni kweli kuna hata za
milioni hadi hamsini ,....lakini hizo ni za kiofisini, sio za mtu binafsi, na
hizo zimetokana na kazi maalumu, ...kwanini unaniulizia nyaraka za ofisini..?’
nikamuuliza kwa mashaka.
‘Sikiliza nikuambie kitu, usione wenzako
wanajenga, usione wenzako wanatembelea magari ya kifahari, ukafikiri ni pesa za
mshahara, mshahara ni kitu kidogo sana, ni pesa ya kukuweka mjini, kuwa upate
angalau kitu cha kula, ...wanaolipwa mshahara ni wenzetu wazungu, lakini sio
sisi waswahili,...unanielewa?’
‘Kwahiyo ili uishi maisha ya kisasa inabidi
utumie akili yako, uchangamshe bongo lako, ndio maana jina la bongo
likapatikana, bila kutumia ubongo wako, utaishia kusindikiza wenzako kwa
kibwagizo cha kusema yule nilisoma naye...’akawa
anaangalia nje, nimi nikaangalia huko anapoangalia, ilikuwa gari moja la
kifahari lilikuwa linaingia na jamaa aliyevaliwa kinadhiufu na mpenzi wake
akatoka kwenye hilo gari.
‘Unaona, hayo ndio maisha, unamfahamu huyo
jamaa na anafanya kazi wapi?’ akaniuliza
‘Simfahamu...’nikamwambia
‘Unaona ulivyo, wewe muda wote upo ofisini,
ukitoka upo nyumbani, akili yako haijui ni kitu gani kinachoendelea huko nje,
hubadilishi mawazo na wenzako, ndio maana upo pale pale, na ukiendelea hivyo
utazeeka vibaya na kuishia kufa kwa msongo wa mawazo, ukiwazia hizo bahati
ulizozichezea...’akasema.
‘Mimi sijakuelewa, kwanini unaniambia hivyo na
hayo yote ya nini, kila mtu ana mpangilio wa maisha yake, na jinsi gania
atakavyojijenga, na wengi tunategemea malipo ya uzeeni, ukiangalia kwenye
mshahara kila mwezi unakatwa pesa, ili ndio akiba yako ya baaadaye..hata hivyo,
kwanini tuingiliane kwenye mpangilio wa maisha..?’nikamwambia.
‘Hahaha, unazungumzia hiyo mnayoiita nini,
malimbizo ya uzeeni,akiba ya nini sijui ....hahaha, nikuulize niambie ni nani
aliweza kujijenga kwa hiyo pesa, maana kila muda unavyokwenda ile pesa inashuka
thamani yake, ...ule ni ujanja wa wenzako kuwawezesha wawekeza kwa mgongo wako,
ilivyo, pesa yako ya leo sio sawa na utakavyolipwa uzeeni, wao wanaichukua leo
ikiwa na tahamani, wanaiwekeza, na ikifika muda wa kukulipa wewe haina thamani
tena,ndio maana wanakutangazia, kuwa itakufaa kwa ajili ya maziko yako...hivi kwanini
nyie hamuelewi, nini maana ya shule zenu...?’ akaniuliza kwa mshangao.
‘Hayo ni mawazo yako wewe mwenye tamaa ya
utajiri wa haraka haraka...na kwanini unaniambia hayo yote..huo ni mtizamo
wako, ....’nikamwambia.
‘Angalia utakavyosumbuliwa wakati wa kulipwa,
unafikiri kwanini wanafanya hivyo, ili waendelee kuzizalishia,..ili uendelee
kupata msongo wa mawazo, ili ufe haraka...kwanini wasibuni njia mbadala,
ukaweza kuwa na hisa huko walipowekeza ili hata ukiwa mzee ujue zinafanya kazi,
kwanini wasikupe mkopo wa nafuu ili ujenge,...kwanini....habu fungukeni akili
nyie watu mliolala....’akasema.
‘Watu kama nyie hamfai kuwepo makazini, nyie
ndio mnaleta vurugu kwenye jamii...nimekuuliza kwanini unaniambia hayo yote?’nikamuuliza.
‘Kwasababu nyie mpo kwenye nafasi ambazo
tunazitafuta, lakini hatuwezi kuzipata kwa vile nyie mumezishikilia, na hamjui jinsi
gani ya kuzitumia...’akaniambia
‘Mhh, kumbe na wewe unatakami uwe mhasibu,
nakuhakikishia kama ungeusomea huo uhasibu, hizo fikira zako chafu zingeondoka,
maana ungelijua kanuni za uhasibu, ...lakini hujachelewa kwanini usiende ukausomea
kama unaona ni rahisi hivyo...’nikamwambia
‘Sikiliza nikuambie kitu, mimi nataka hizo
pesa, na nazihitaji mwisho wa mwezi huu nizipate..’akasema
‘Kwa vipi, mimi sijui jinsi gani ya kuzipata
pesa nyingi hivyo kwa muda huo mfupi, kama ningelikuwa nafahamu jinsi ya
kuzipata hizo pesa, ningelishajenga nyumba....’akasema.
‘Hahahaha, hujui jinsi gani ya kuizipata hizo
pesa, hizo pesa kidogo tu hujui jinsi gani ya kuzipata halafu unajiita
mwanaume...unajiita mhasibu, unanichekesha kweli kweli, ama kweli kwenye miti
hapana wajenzi, nikuulize huo uhasibu wako ulisomea nini?’ akaniuliza.
‘Kutunza mahesabu ya pesa kwa utaratibu
unaotakiwa....’nikasema
‘Kuwatunzia wenzako, ...huku unapiga miayo ya
njaa, hebu amuka, ulizia wenzako waliokuwa kwenye hiyo idara wamefanya
nini...’akasema.
‘Mimi ninavyojua , walifukuzwa kwa sababu ya
udanganyifu na wizi , wakafukuzwa...’nikasema
‘Unafahamu sasa hivi wapo wapi,.....ulishawahi
kufuatilia nyendo zao ukafahamu hawa watu wapo wapi?’ akaniuliza.
‘Mimi sijui, kwanini nifuatilie nyendo
zao,zinanihusu nini mimi, mimi natimiza wajibu wangu, na sitaki kufanya kama
walivyofanya wao, maana sio taratibu za kiuhasibu, ...’akasema
‘Sasa nikufungue akili yako, mmojawapo ndio
huyu uliyemuona hapo nje, akiwa na hilo gari la kifahari...’akasema.
‘Kwahiyo unataka kusema huo utajiri kaupata
kwa kuuiba, kwa kutumia ujuzi wake wa kiuhasibu na kuzipata hizo pesa au?’
nikamuuliza
‘Akili kichwani mwako,...soma ujue, halafu
pambanua akili yako uone mbali, ..kila elimu ina njia nyingine mbadala, ukiwa
docta, una njia nyingine ya kupata pato, ukiwa mwalimu, halikadhalika, sasa
wewe upo kwenye idara nyeti ya pesa, kwanini ushinde kubuni njia mbadala ya
kukuza kipatao chako..mshahara hautakujenga hata siku moja...hebu niambie wewe
unatarajia kuoa, ukioa utaweza kuishi vipi na mke wako, mke ambaye hajasoma,
....utawezaje kuwasomesha watoto, utaendelea kukaa kwenye nyumba ya kupanga
mpaka lini...?’ akaniuliza.
‘Mhh, mimi sikuelewi na sitakuelewa, maana
huko unaponipeleka ni kubaya, nawafahamu sana watu wa namna yako, mna tamaa
sana, watu wa namna yenu, mnafkiri ukiwa mhasibu basi utakuwa na mwanya wa
kupata pesa, hamjui jinsi gani tunavyotakiwa kufanya ...uhasibu una utaratibu
wake, na sheria zake na kanuni zake...’nikasema.
‘Unatakiwa ufanye nini,...yaani wewe
uchungulie makataratasi ukiangalia jinsi gani wenzako wanavyotumia, au uangalie
jinsi gani wenzako wanavyotafuta pesa, hebu amuka kidogo, hebu fikiria kidogo,
usije ukaja kujuta wakati huna kazi, wakati upo mzee, wakati hujiwezi..’akasema.
‘Ok, kwa kuongea, hebu niambie jinsi gani hizo
pesa zinavyopatikana, bila uzifanyia kazi, bila gharama?’ nikamuuliza huku
nikimwangalia kwa makini.
‘Nataka wewe ndiye unitafutie hizo pesa,
milioni kumi na tano, mwisho wa mwezi huu nizipate..’akasema na kunifanya
nishituke na kumtolea macho ya kutoamini hiyo kauli yake.
‘Ina maana .....oh, mimi ndiye nikutafutie,
kwa vipi, mimi nitazipata wapi hizo pesa, na kwanini mimi, una deni gani na
mimi , mpaka mimi ndiye nikutafutie, mimi ni mzazi wako, mimi ni ...sisi ni
marafiki tu, lakini sina shinikizo na wewe...sikuelewi, kwanini mimi..?’
nikamuuliza baada ya kuduwaa kwa muda.
‘Kwanini wewe eeh, unafahamu thamani ya
mapenzi wewe....hujui mapenzi yana gharama, ok, tuseme mimi ndiye
nimekushnikiza unipende, wewe hunipendi, ulikuwa unatumia mwili wangu tu, kwa
tamaa zako..tuseme hivyo,...Nasikia unataka kuoa kwenye likizo yako?’
akaniuliza na kunifanya nishangae, maana sijawahi kumwambia mtu kuhusu mpango
wangu huo.
‘Ni nani kakuambia hivyo, ...?’ nikamuuliza
kwa mshangao.
‘Mimi sitaki kukuharibia mipangilio yako ya
ndoa, japokuwa moyo unauma sana, kwani nilishakueleza lengo langu kuwa wewe
ndiye unayenifaa kuwa mwenza wa maisha yangu. Nilishakata tamaa kabisa, ya
kuolewa, lakini nilipokuona wewe nikajua wewe ndiye chaguo langu, lakini
....naona kuna vikwazao, sio mbaya sana, kama ukinipatia hizo pesa, nikagomboa
gari langu, ambalo lipo bandarani, ...sitakusumbua tena...’akasema.
‘Mhh, mimi sikuelewi, kama uliweza kununua
gari huko nje, kwanini ushindwe kuligomboa huko bandarani, uliwezaje kulinunua
na sasa unashindwa kuligomboa....?’ nikamuuliza.
‘Kila kitu na mpangilio wake, hatua ya kwanza
ilikuwa kulinunua, wakapatikana wafadhili, na hatua liyobakia ni kuligomboa, na
hiyo ni kazi yako wewe....’akasema na kuangalia saa.
‘Kazi yangu mimi! Mbona ....hivi wewe
unanionaje mimi, yaani gari lako, mimi niingie kwenye kazi chafu kwa ajili yako
wewe, mimi siwezi hiyo mipango yako, na sizani kama tutakuja
kuelewana.....’nikasema.
‘Basi nikuambie ukweli, mimi ndiye utakuja kunielewa
kuliko mtu mwingine, kwani nikiliachia hili swala kwa wadau wengine,
utazitafuta hizo pesa huku unalia, huku unahaha..aheri mimi nimekuambia kisiasa
kwa vile nakupenda...’akasema na nilimwangalia kwa mashaha, akili ilikuwa
imeshaanza kutekwa na pombe.
‘Sikiliza wewe mwanamke,sio kila mwanaume,
yupo kama unavyotaka wewe...sina akili hiyo, akili niliyo nayo ni ya kufanya
kazi yangu kwa mujibu wa kanuni za uhasibu, ...na moja ya kanuni hiyo ni
uaminifu, ...usipokuwa mwaminifu hujawa muhasibu,laba uwe mhasimu..’nikamwambia.
‘Hahahahaha..sheria na kanuni za
uhasibu,....unatamba unajiona kuwa kweli wewe ni mhasibu, unasema huku unajiamini
kabisaaa, ....pole sana...’akaniangalia kwa makini huku akitabasamu na mimi
nikawa nimekunja uso, halafu akakunja uso kidogo na kusema kwa sauti ya
kuonyesha umakini fulani.
‘Kuna siku niliweza kuongea na baba mkwe wako,
nakumbuka mara ya kwanza aliongea na mimi akikupigia debe ili upate kazi hapa,
sasa safari hii akawa na shauku ya kujua tabia na mwenendo wako hapa kazini...’akatulia
kidogo huku akiangalia pembeni.
‘Nilihamasika sana alipotaja mambo hayo,
nikajiuliza kwanini anataka kujua maisha yako ya ndani, unaishije hapa, je una
....tabia ya kihuni, una mpenzi, unalewa...hayo maswali yalinivutia sana,
nikataka kujua kunani...’akageuka kuniangalia.
‘Nilipomchimba kiujanja, maana mimi nikitaka
kujua undani wako nitakupata tu, huwezi kunificha, mzee, mwanzoni alijifanya
mwanasiasia baadaye nikamuingiza kwenye anga zangu, nikafahamu ni kitu gani
anakitafuta....’akaniangalia huku akitabasamu.
‘Ndio hapo nikafahamu kuwa una mipango ya kuoa
kati ya mwaka huu, na inaonyesha huyo mzee hajakuamini , ...bado anakuchunguza,
na huenda anatafuta mwanya wa kulipiza kisasi kwa hayo uliyoyafanya kwa binti
yake, sasa akigundua kuwa una tabia chafu, na una nia ya kumpotezea binti yake
muda, huku umeshamuaharibia utaratibu wake wa maisha nia imani kuwa
litakalotokea huko mbele ni baya sana, hatasita kukuweka ndani ...’akageuka na
kuangalia pembeni, halafu akasema.
‘Kumbe na ujanja wote huo, ...wewe ni mbakaji,
unajifaya mtakatifu, kumbe, ulikuwa unavizia vitoto vya shule, mwisho wake ukambandika
mtoto wa watu mimba akiwa shule, tena shule ya msingi, ua hatari wewe, sasa
umekalia kuti kavu, uwe mwagalifu...’akasema na kunifanya pombe zote zilizokuwa
kichwani ziishe.
‘Kwanini uliongea na huyo mzee....ni nani
kakuambia yote hayo, kwanini unanifuatilia mambo yangu , yanakuhusu nini’
nikamuuliza nikiwa na hasira.
‘Kila simu inayoingia hapo ofisini ni lazima kwanza
ipitie kwangu, na hapo ndipo ninapoweza kuwajua watu wangu, mimi sio mjinga
kama unavyofikiria, usione yote hayo yanayofanyika ukaniona mimi ni malaya, ..mimi
sio muhuni nina akili yangu timamu...wewe sasa upo hapa kiganjani, ....na
nimekueleza hilo makusudi, ili unielewe vyema, na nimefanya hivyo kwasababu
nakupenda, kama ingelikuwa watu wengine, ningefanya kama tunavyofanya, kificho
na kwa siri, aanaumia mtu, ...’akatulia kidogo.
‘Ina maana unajifanya kuwa unanipenda kumbe
una kundi ....’nikataka kusema akanikatisha
‘Siwezi kupinga ukweli kuwa kweli nimetokea
kukupenda, hiyo sio kawaida, na sijawahi kupenda katiika maisha yangu, kwangu
mimi wanaume wote ni sawa, huwa nyote nyie sio waaminifu, mnachojua ni kutamani
miili ya wanawake, mkipata mnachokitaka, mnasahau, mnatutenda, ..ndio maana
nawafanyia hivyo,...ila wewe kama utashirikiana nami vyema, itakuwa zimwi
likujualo...’akatulia
‘Mimi sikuelewi, ni kwani ufanye hivyo, ni
nini lengo lako hasa...?’ nikaonyesha kuchanganyikiwa kwa kushika kichwa
changu.
‘Nimekubali moyoni kuwa nakupenda...sijui
kwanini...’akatulia kidogo.
‘Sasa kwanini unanifanyia hivyo?’ nikamuuliza
‘Nimegundua kuwa wewe kama walivyo wanaume
wengine,umevutika na mimi, moyo wako hapo ulipo unatamani mimi niwe mke wako,
sio wewe tu, wapo wengi...sikushangai sana, hata hivyo, hata mimi nataka sasa
nitulie, nipate mume, nami nizae niwe mama watoto, sijui itakavyokuwa huko
mbele, maana maisha ya ndoa nayaona kama ni utumwa fulani, hata hivyo muda
umefika na mimi niwe hivyo, niwe mtumwa,.....’akatulia kidogo.
‘Sasa niliposikia kauli ya baba mkwe wako na
hayo uliyoyafanya, moyo wangu umevunjika, nimeumia sana, kwani nishakuchagua
wewe uwe mwenza wa maisha....hivi ni nani atafurahi kunyang’anywa tonge
mdomoni...kwakweli nimeumia sana, na ulivyoona nimetulai kimiya nikawa kama sio
mimi, nilikuwa natafakari sana, nikufanye nini, ...sitakubali hilo
kirahisi...’akasimama, na akawa kama anajikagua, akageuka na kuniuliza.
‘Hivi mimi na huyo mchumba wako nani zaidi?’
akaniangalia kwa macho yaliyojaa taswiswi fulani.
‘Usiniulize hilo swali, hayo ni maswala yangu
binafsi, na sikuwa na mpango wa mahusiano na wewe, yote hayo umeyasababisha
wewe, sikuwahi kukutaka, ni wewe umekuwa ukinilazimishia kwako...hata kama unavutia,
hata kama wewe ni mrembo, lakini swala kubwa ni je unafaa kuwa mke wa nyumbani,
wewe,.....’nikasita kidogo.
‘Hahaha, mke mwema, ...lakini je wewe ni mume
mwema, hujichuji na kujikagua, je hayo uliyotenda huko kwenu, yanaonyesha nini,
...kwanini uangalie upande mmoja wa shilingi wakati wewe upo upande huo
huo....hata ugeuze vipi shiligi ni hiyo hiyo, ..sote tupo sawa, sote ni
wakosaji, wema wa mtu ni hapo mtakapokaa na kukubaliana na kukubali ukweli...’akageuka
na kuniangalai kwa makini.
‘Anyway,
sawa nimekuelewa, ....kama ni hivyo, ninaweza kukubali yaaishe, kwa
sharti,...kuwa ni kwanza ni kuhakikisha nampata mpenzi wangu wa kweli..nikishampata
huyo haaah, sijui , maana namtamani namuota, huyo sina wasiwasi naye,yupo kwa
ajili yangu, atanipenda kama nitakavyompenda mimi...vinginevyo, kutachimbika...’akasema
huku akikunja ngumi.
‘Mpenzi gani huyo,....kumbe unaye mwingine,
unataka kunighilibu mimi....’nikasema kwa kung’aka, na nilihisi wivu moyoni,
sijui ni kwanini, badala ya kushukuru kuwa hilo limepata ufumbuzi, nikajikuta
nakasirika, na kujiona nakosa kitu fulani, hasa niliposikia kuwa ana mpenzi
mwingine.
‘Hahaha, unataka kumfahamu huyo mpenzi wangu,
una uhakika na hilo, ..hata kama hua uhakika lakini ndio ukweli, ni lazima
nimpate,....hata kama utaingiwa na wivu, kama unavyojionyesha, lakini ni lazima
nimpate....’akatulia na akawa kama anawaza mbali.
‘Ni nani huyo mpenzo wako,....?’ nikauliza kwa
hasira.
‘Unataka kumfahamu ehe? ...mimi mpenzi wangu
sio kama wako, sio kama unavyofikiria wewe, mpenzi wangu anatokea ng’ambo, kaja
kwa meli, sasa hivi yupo huko bandaraini, ukinitafutia hizo milioni kumi a tano
tu, ....nakuachia uende ukakutane na huyo mshamba wako, lakini nakuhakikishia
kuwa utamuoa, lakini wakati wote utakuwa ukuniwaza mimi,a ndoa yako haitakuwa
na raha, maana huyo mshamba wako hataweza kukupa pendo halisi, ....’akasema
huku akinishika shika mkono.
‘Mimi sikuelewi, ...ina maana mpenzi wako ni
hilo gari..hahahaha...?’ akaniuliza
‘Sasa kwa ukusaidia tu, ninakupa dondoo,
mengine unafahamu wewe jinsi gani ya kufanya. Maana wewe ni mhasibu, au sio,...’akainama
na kuniangalia moja kwa moja usoni.
‘Kuna mzigo unaingia pale kazini hivi karibuni,
mzigo huo ni wa pesa nyingi, unafahamu hilo, kinachotakiwa ni kugushi
nyaraka,...unatengeneza nyaraka kuwa wewe ni wakala wa usafiri, zile nyaraka
hazikaguliwi sana, kwa uzoefu wangu, ...mimi nitakupa akaunti ya benki, na
kampuni ya usafisrishaji, ambayo itahitajika kulipwa hizo pesa, na hizo
nyaraka, wewe kama mhasibu, kazi yako ni kuzikagua kuwa ni sahihi, sio ndio
unavyofanya zikifika kwako, ...?’ akaniuliza.
‘Wewe mbona unachukulia mambo kirahisi hivyo,
kila nyaraka ya malipo ni lazima bosi aipitie, na ili ilipwe kuna taratibu
zake...sio kwamba tunalipa ilimradi nyaraka hiyo ipo, kuna uhakiki wa ankara ya
deni, je lipo sahihi, je huyo mtu kafanya hiyo kazi, na kabla ya hapo kuna
vitangulizi vyake, maombi, na mikataba, sasa wewe unataka ulete ankara ya deni
juu kwa juu, hatuendi hivyo...’nikamwambia.
‘Mimi sio mjinga, hilo halijafanyika mara
moja, na nyaraka hizo mimi ndiye ninayezifuatilia, na wakati mwingine bosi
ananituma nizitafute ili mambo yawe safi kuhakikisha tunabaa matumzi,...wewe
umeingia kichwa kichwa, huulizi wenzako wanaponea wapi,...sikiliza nikuambia...’nikaona
nimkatishe kwa kusema.
‘Mimi siwezi kufanya hayo hata siku
moja,...sio fani yangu hiyo, mimi ni mwaminifu na naifahamu akzi yangu vyema...’nikasema.
‘Usinichefue,...ungelikuwa muaminifu
ungelibaka kitoto cha shule...hujui ni nini maana y aumanifu, uaminifu hujengwa
pia kutokana na matendo yako katika jamii...usijidanganye, subiri nikuelezee
jinsi ya kumeki money, mjinga mkubwa
wewe...’akasema huku akibenua mdomo .
‘Mimi ndiye nineyepeleka hundi za malipo benki,
hata kabla hujafika, watu wa huko wapo hapa...’akaonyesha kiganja cha mkono,
‘Usicheze na sure nzuru, ukiwa mrembo na
ukajua jinsi ya kuutumia, hufi njaa, kila mahali ina watu wangu, dunia ipo
hapa, tumeijenga dunia yetu,...kwahiyo, kuwa nami, nisikilize uwe ndani ya
chama chetu, kinaitwa dunia yangu....’akasema na kutulia kidogo.
‘Chama ...mna chama ..ohooo, kumbe, wewe ni
wakala wao, nimeshakuelewa, hapa hadanganyiki mtu,...’nikwamambia.
‘Mimi nakupa dondoo tu jinsi ya kufanya, kama
nilivyokueleza ni mimi ndiye ninayezipeleka hizo hundi kwa wahusika, na wengi
wao ni watu wetu,...nakufundisha njia moja wapo, nyingine, ni kugushi hundi,
unaandika namba chache, huku nyuma unaacha nafasi, ambayo nitakuja kumalizia,
..kwenye maneno unaacha hivyo hivyo, nafasi ya kuongeza maneno...ikifika benki
inakutana na watu wangu, wao wanajua jinsi gani ya kufanya,...hiyo ni kazi
rahisi, tatizo wewe umeingia sehemu ambayo hujui kuitumia, ..’akasema.
‘Mimi sikuelewi,...na sizani kama hilo
litafanikiwa, ...sijui na wala sijawahi kufikiria hivyo, na nashindwa hata
kukuelewa, ina maana hiyo ndio tabia yako, hapana...naanza kukuogopa...’nikasema
na yeye akasimama, safari hii akaniangalia kwa macho makali, na kusema;
‘Kuna kazi alinipa baba mkwe wako
kukuchunguza...sitaki kukuharibia maisha yako, sitaki umkose mchumba wako,
japokuwa umeshamharibia mstakabali wa maisha yake, lakini naona unanilizimisha, na nikianza
kukuharibia maisha yako nitahakikisha yanaharibika kweli...umeanza kwa ulevi wa
pombe, nitahakikisha unakwenda kuokota makopo..na mwisho wake utafia
jela....chagua moja kufanya nilivyokuambia au ....’akasimama na kuanza
kuondoka.
Nilibakia pale meza ni nikiwa nimeduwaa,
kichwa kikawa kinaniuma kweli kweli, nikatamni niagize pombe, lakini, mfukoni
nilikuwa mkavu, mdada ndiye alikuwa mfadhili kwa siku hiyo, nikasimama kuondoka,....na
wakati nasimama macho yangu yakaona kitu mezani, nikajua ni mdada kasahau mzigo
wake,nikakichukua, ilikuwa ni bahasha, na juu yake kuna jina...oh, ni jina la
mchumba wangu, ..
‘Ni barua , ni ...nikafungua na ndani yake
nikakuta picha mbili, ni zile picha chafu,zikionyesha nikiwa a mdada, ni picha
ambayo sikutaka hata kuiangalai mara mbili, nikaichana na kuitafuna kuhakikisha
hakibaki hata kipande kimoja, ndani ya bahasha kulikuwa na karatasi ndogo
imeandikwa;
‘Hii ndio kazi ya mchumba wako...’
Nikasimama nikiwa na hasira nikamkimbilia mdada,
sikumkuta nje,na pikipiki langu lilikuwa halipo....
*********
Asubuhi nilipofika ofisini na nikiwa
nimechanganyikiwa kwani pikipiki sikuliona na sikujua I nani kalichukua hata
ilipowauliza walinzi , wao walisema hawajui, kwani sikuwakabidhi, ni kweli nilipofika
jana kwasababu ya maongezi na mdada, sikuweza hata kuwakabidhi walinzi hilo
pikipiki, nilisimamisha na kuigia ndani, kichwa kilikuwa kikiuma na nilichokuwa
nikitamani ilikuwa ni kinywaji.
Nilishapanga kwenda kutoa maelezo polisi, kwani
mdada nilimpigia simu, akasema yeye hajui, aliondoka na taksi ...
Nilifika ofisini nikiwa nimechanganyikiwa,
nitamwambia nini bosi, ....lakini cha ajabu nilipofika ofisini nikalikuta
pikipiki langu, nikaangalia kuhakiki ni nani kalileta, sikuweza hata kuwauliza
walinzi, nikajua huenda mdada ananichezea akili, nikaingia ndani kuhakikisha
kuwa mdada ameshafika, alikuwa hajafika, na nijuavyo, yeye hajui kuendesha,
sasa ni nani alifanya hiyo kazi, ..nikalikagua lile pikipiki na kuliona halina
tatizo, nikaingia ofisini nikijua nitamkuta mdada, lakini alikuwa hajafika.
‘Ni nani huyu ananichezea akili yangu?’
nikajiuliza, nikaona bora sasa niwe makini hasa na huyu mdada, lakini kwanini
kila nikimuwaza napata shida,...hapana .....
Siku nzima hiyo nilikuwa nimetawaliwa nay ale aliyonieleza
mdada, na hata kazi ikawa haiendi vyema, nikjaribu kuangalia nyaraka mbali
mbali za malipo kuhakiki ukweli wa mdada, lakini ilikuwa sio rahisi kuligundua
hilo...hata bosi alipofika aliikuta nikiwa kwenye lindi la mawazo, hakunidadisi
sana.
Kama kawaida ilipofika muda wa mapumziko, bosi
akaniita, na hakutaka kunidadisi sana, japokuwa alianza na maneno yake ya
hekima kwa kuniambia;
‘Katika maswala ya kazi, ni muhimu sana
ukachunga sheria za taratibu za hiyo fani, na mkufunzi mzuri ni yule
asiyeghilibiwa na hamasa za watu, maana kila mtu ana mtizamo wake kutokana na
jinsi yaye anavyofanya...’akaniambia
‘Kwa mfano mkulima, anajua kulima na mambo
yake ya shamba, akisikia mtu yupo ofisini ataona huyo mtu kazi yake ni kukaa
tu, na kucheza na makaratsi, atakuona huna kazi, hata ukisema umechoka
atakushangaa sana, na kukuuliza unachokeshwa na kitu gani,i wakati wewe upo
ofisini, umekaa tu...ni kwanini anasema hivyo, ni kwasababu yeye kazingatia fani
yake tu, hajaupanua ubongo wake kinamna nyingine...’akasema bosi.
‘Sasa wewe ukiwa kwenye fani yako, mfano hiyo
ya pesa, wengi watafikiria wewe huna shida, wewe unajua jinsi gani ya
kutengeneza maisha, maana unachezea pesa, lakii hawajui fani yako ina masharti
na taratibu gani...wengi wanaingia kwenye hizi fani wakiwa na tamaa zao, hawaingii
kwa wito, bali ni kutamani kupata pesa, wanakuwa na ndoto zisizo za kweli,
ukiwa haupo makini na fani yako, watu watakuchota akili yako, na kukuharibia
maisha yako....’akaniambia na kujikuta nashangaa, amejuaje yale aliyokuwa
akiniambia mdada.
‘Sitaki nikuchoshe leo, kwani nataka nikupe
mambo muhimu yaliyotokea katika sehemu hii, ni kama hitimisho la sehemu ya
kwanza ya kisa hiki,. ..nitaanza moja kwa moja na kisa cha maisha yangu kutoka
pale tulipoishia.....;’
*********
Mama alipokwenda kazini nilibakia na yule
rafiki yake, mgeni aliyekuja kututembelea, na baada ya kazi za mchana kutwa,
ikafika muda wa mapumziko, kama kawaida yangu sikuwa na muda wa kukaa kuangalia
tv, nikamwambia mgeni wetu kuwa mimi nakwenda kujipimuzisha ndani, na yeye
akasema;
‘Sawa hata mimi nitajipumzisha, ngoja
niangalia tv kidogo...’akasema.
‘Sawa basi mimi nipo chumbani
kwangu...’nikasema
‘Haya ...’akaitikia huku akiwa kavutiwa na
kitu kwente tv, na mimi nikaingia chumbani kwangu.
Imekuwa ni kawaida yangu, kila siku naandika
jambo kwenye diary yangu, na hasa muda kama huo wa mapumziko, nimejijengea hiyo
tabia tangu nikiwa shuleni, kwahiyo karibu kila kitu kilichotokea katika maisha
yangu kilikuwa ndani ya diary yangu hiyo.
Nilipoingia chumbani,nikachukua ile diary
yangu na kuanza kuandika yaliyotokea siku hiyo, na nilipomaliza, nikajilaza
kitandani na haikuchukua muda nikashikwa na usingizi, na ghafla nilikuja
kushituka mtu akigonga mlango,..
Nilijua kuwa huyo mgeni yupo anaangalia tv, au
kama haangalii tv, atakuwa chumbani kwake kalala, sasa ni nani huyo alikuwa
akinigongea mlango, nikaingiwa na shaka, na shaka hiyo ilizidi kutokana na hula
niliyokuwa nimejengeka nayo nikiwa huko mjini, mara nyingi mlango ukigingwa hivyo, ninajua nimefuatwa
kwa kosa fulani, japokuwa sikulifanya, na hapo kitakachofuata ni kipigo, matusi
au kusimangwa.
Kwasababu nilitoka usingizini, akili yote
ilikuwa haijawa sawa, na akili yangu ilinituma kuwa bado nipo mjini, kwahiyo
nikawa na wasiwasi, hadi pae akili yangu ilipotulia na kujipa moyo kuwa sipo
mjini , na huyo anayegonga huenda hana nia mbaya na mimi, ndipo nikauliza
‘Wewe ni nani?’ nikauliza
‘Fungua mlango mimi ni Aunty wako, nataka
tuongee...’akasema
Nikajiuliza huyu mgeni anataka kuongea nini na
mimi, na nafahamu kaja kwa ajili ya mama, je mimi anahitajia nini kutoka kwangu,
sikuwa napendelea kuongea na mtu, hasa yule ambaye atataka kujua maisha yangu
ya nyuma, maisha ambayo nilyaona kama mwiba uliochomekwa kwenya moyo wangu.
Nikainuka na kwenda kufungua mlango, na yule
mgeni akaingia na moja kwa moja akaenda kukaa kwenye kitanda changu, na
kunisubiri nije nikae, na mimi nikaenda na kukaa pembeni, mbali kidogo nay eye,
huku nikiwa na wasiwasi, huyu mtu anahitaji nini kwangu.
‘Aunty, una kitu unahitaji ...?’ nikamuuliza.
‘Hapana nataka kuongea na wewe tu...’akasema
‘Kuhusu nini?’ nikamuuliza kwa mashaka.
‘Nakuona siku hizi umebadilika sana,...sio
kama ulivyokuwa kipindi kile nilipokuja kabla hamjaenda mjini, kuna nini
kimetokea?’ akaniuliza
‘Hakuna kitu Aunty, ni maisha tu, sasa
nimekuwa mkubwa, naona nijitulize tu..’nikasema.
‘Sio kweli, niamini mimi, nipo tayari
kukusaidia, kama kuna tatizo limetokea au kuna jambo linakukera wewe niambie
mimi nitatafuta jinsi ya kukusaidia..’akasema
‘Hamna tatizo nimeamua kwa hivi
tu...’nikamwambia na ilionekana wazi kuwa hakutosheka na maneno yangu hayo,
akaniambia.
‘Mbona nilisikia ulifukuzwa shule kwa tabia
mbaya ya uhuni, na umeshindwa kukaa na mama yako wa kambo kwa vile umejiingiza
kwenye mambo ya kihuni?’ akaniuliza
‘Ndivyo mama alivyokuambia?’ akaniuliza
‘Mama yako kasema ndivyo alivyoambiwa na mama
yako mdogo, japokuwa yeye haamini kabisa hayo aliyoambiwa, na wakakusingizia
kuwa umetoa mimba kuwa sio kweli...sasa mimi ni rafiki mkubwa wa mama yako,
huenda kuna mambo ambayo yanakukera, naomba uniambie ili tuweze kukusaidia,
mimi nipo tayari kukusaidia..’akasema.
‘Hebu niambie nakuona unaandika andika kwenye
hicho kitabu, unaandika nini?’ akaniuliza
‘Mambo yangu tu...’nikasema kwani sikutaka
ajue nini ninacho andika na sikutaka kumuonyesha,na alikaa na mimi kwa muda
akitaka kunichota ili niweze kumuelezea lolote, lakini hakupata lolote
alilohitajia, na baadaye akatoka na kuniacha nikiwa peke yangu chumbani.
Baadaye sana, akaniita na kunituma dukani,
kwenda kumnunulia kitu, kitu ambacho, sikuwa nakipenda, mara nyingi, hata
dukani sikuwa napendelea kwenda, yeye akaniambia niwe natoka toka.
‘Hapana Aunty, mimi huwa sitoki nje ...’nikasema
‘Kwanini?’ akaniuliza
‘Nimezoea hivyo,...’nikasema kwa kifupi, na
yeye akasema akionyesha mshangao.
‘Kwanini hutoki nje, wewe ni msichana mkubwa,
unatakiwa kujichanganya, sio kwa nia mbaya, lakini ni vyema ukaangalai dunia
inavyokwenda, sasa sikiliza ukiwa na mimi, kazi zikisha utakuwa unatoka ukawatembelee
rafiki zako ina maana huna hata rafiki mmoja?’ akaniuliza
‘Wapo, wanakuja siku moja moja, lakini mimi
sina mazoea ya kwenda kwako..’nikasema.
‘Sasa utakuwa unakwenda kuwatembelea, maana
mimi nipo, kazi zilizopo haap sio nyingi, tukimaliza kazi wewe unakwenda
kuwaona wenzako, mimi nitamwambia mama yako hivyo...’akasema.
Kweli ikawa hivyo, nikawa natoka kila
tukimaliza kazi, kutoka kwangu nje,
ilikuwa kama ngomba aliyekuwa kafungiwa kwa muda mrefau sasa kaachiliwa,
nilikwua kama mgeni wa dunia, kila sehemu nikawa nashangaa shangaa, kama vile
nilikuwa mgeni kabisa hapo kijijini.
Sikuwa nimefahamu huyo Aunty alikuwa na
malengo gani, lakini hata hivyo na mimi niliona ni muhimu nitoke toke, huenda
nikajifunza jambo, kuliko kukaa kaa ndani, kwahiyo nikaanza kujenga mazoea ya
kutembea na nikirudi nachukua diay yangu naandika kile nilichoona na kujifunza.
Siku hiyo mama hakuwa amekwenda kazini, mimi
nkatoka kama kawaida yangu niliwaaga, na niliporudi, mama akaniita na wakati
huo huyo mgeni alikuwa nje, na mama akaniuliza;
‘Mwanangu hebu niambie ukweli, ulipokuwa huko
mjini kulitokea nini?’ akaniuliza nikashangaa kwani swali kama hilo alishawahi
kuniuliza na sikumwambai lolote nilimficha.
‘Mama nilishakuambia kuwa hakuan kitu,
niliishi na wenzangu na nikafukuzwa shule...’nikasema
‘Hujanaimbia ukweli, ilivyokuwa, naona
umenificha mambo mengi sana, leo nataak uniambie kila kitu..’akasema mama
‘Kwanini mama unataka nikuambai kila kitu ,
tumeshakaa wote muda mrefu ghafla tena unafufua mazungumzo yaliyopita..’nikamwambia.
‘Tumegundua kuwa kuna mambo mengi ulitendewa
huko mjini , lakini hukutaka kuniambia, kwanini unanificha mimi mama yako?’
akaniuliza
‘Mumegundua na nani?’ akaniuliza na mara Aunty
akajitokeza na kusema;
‘Mimi ndiye nimemwambia ukweli wako, samaahni
sana, wakati ulipokuwa unatokaa, niliingiwa na hamu sana ya kutaka kujua ni
kitu gani kila siku ulikuwa ukiandika, ndip nikasoma na kugundua yote
yaliyotokea ukiwa huko mjini, na ndio nikamwambai mama yako...’akasema na mimi
nikashikwa na butwaa, maana sikutaka kabisa mama yangu ayafahamu hayo, na kuja
kukosana na mume wake, au mama yangu wa kambo.
‘Huyu ni mama yako mzazi aastahili kufahamu
kila kitu kuhusu yeye, yeye anaumia moyoi akikuona hivyo ulivyo, wewe unaona ni
kawaida, lakini yeye anaumia, anajaribu kutafuta jinsi ya kukusaidai
anashindwa, sasa mimi nimemuelezea kwa kifupi, ni wakati wako kumuelezea mama
yako kila kitu kilichotokea huko mjini..’akasema.
Hapo sasa nikaanza kuongea kila kitu
kichotokea huko mjini bila uwoga, na hapo sasa kwa mara ya kwanza ndipo mama
akaelewa yote yaliyonitokea mimi toka awali, lakini ilikuwa nimechelewa, maana
shule gani ningeenda tena, mama aliumia sana.
‘Kwani mwanangu hukuniambia hayo yote mapema,
ningehakikisha unakwenda shule, mimi nilishaanza kuamini badhi ya meneno yao,
ndio maana nikaona ni bora ukae nyumbani tu...’akasema mama
‘Kesho ni lazima nimuita baba yako niongee
naye, siwezi kukubali, haya aliyokufanyia sio sahihi, atamtesaje mwanae
mwenyewe wa kumzaa, kwa kusikiliza pande moja tu.
‘Mama ndio maana sikutaka kukuambia,
nilichelea hili kuwa mtakosana na baba..’nikasema.
‘Wewe hujui kuwa ulichofanya ni kosa kubwa
sana, maana hapo unajiangamiza mwenyewe, ukweli ni muhimu sana, hilo niachie
mimi....’akasema mama, na kweli kesho yake akamuita baba ae haraka huku
kijijini, na baba alifika kesho yake akiwa na wasiwasi kumteokea nini tena.
‘Huyu mtoto kaanzisha balaa gani tena huku?’
akauliza baba akijua kuwa kuna kitu nimekifanya, na mama hakumpa muda
akamuelezea yote yaliyotokea huko mjini, na baba akawa kama haamini.
Baada ya maelezo hayo baba akasema atayafanyia
uchunguzi, ili ajue ukweli upo wapi, akarudi mjini, na kukaa kimiya mama
akamuita tena baba kutaka kujua hatima ya maisha yangu hasa kielimu, baada ya mvutano
mrefu baba akakubali kuwa mimi niende Dar- es salaam kusoma, sikuamini.
Nilisafiri hadi Dar, nikapata chuo, nikaanza
masomo, akilini mwangu nilikuwa na mengi ya kujifunza, na kila ambaloi sikuwahi
kulifanya nikawa na hamu ya kulifanya, na kwa vile nilikutana na marafiki zangu
wengi wa zamani, wakawa wananifundisha mengi, ilikuwa kama mtoto wa getini
kutoka nje...
Nikaanza kujiingiza kwenye makundi mabaya,
huku nasoma, nikaanza kujifunza hata kuvuta sigara, ili eti kuondoa mawazo ya
zamani, niliona ndio maisha, niliona nipo huru sasa naweza kufaya kila
nikitakacho, na wakati ndio huu,..na tabia ya kuvuta sigara ikawa imejijenga
sana kwangu...hata hivyo, sikuacha kusoma, nilikuwa nafuatilia sana kusome,sikutaka
kufeli katika masomo, nilijitahidi hadi nikamaliza chuo, nikafauli vyema tu, na kupata sehemu ya kuanza kazi.
Tabia yangu hiyo na mabadiliko hayo niliyoyaonyesha
yakaja kugunduliwa na dada yangu , mtoto wa mama wa kambo, na yeye kwa haraka akaipeleka
hiyo taarifa kwa wazazi wangu. Baba aliposikia hivyo, kwa haraka, akasema
nirudi huko mkoani, akaagiza nirudi nyumbani haraka, mwanzoni sikujua naitiwa
nini, nikahisi kuna mtu anaumwa au msiba, kwahiyo nikarudi nyumbani.
Nilipofika nikaambiwa yote niliyokuwa
nikiyafanya huko, na kuambiwa na baba sasa kazi hakuna na hakuna kurudi Dar
tena, kwani nimevunja ahadi yake, nimemuabisha, kwahiyo nitaka huko huko
nyumbani , kwa kipindi hicho, akili yangu ilishapevuka, sikuwa na wasiwasi
tena, ....
Nilikaa huko mikoani, na wazazi wangu, kwa
umri kama huo nisingeliweza kuteswa tena, nikawa nafanya kazi ile inayostahili
kwa kujituma mwenyewe, lakini sio kama ilivyokuwa awali kufanywa kama mtumwa na
kunyanyaswa, na baada kama ya miezi mitano nikapata mchumba, taarifa za mchumba
huyo zilikuja juu kwa juu...
‘Binti yangu kuna posa imefika hapa, sasa
tunataka kukusikia kauli yako’ akasema baba akioyesha furaha. Na mimi ilikuwa
kama mshituko, sikutarajia taarifa kama hizo;
‘Baba ni nani huyo mbona sijakubaliana na mtu yoyote
kuhusu kuoana?’ nikauliza nikiwa na mashaka , kwani nkumbuka kuna watu zaidi ya
wawili waliniambia kuwa wanataka kunioa lakini ilikuwa kama ni utani, sizani
kama wanaweza kuwa ni mmojawapo. Baba akaniambia kwa hasira;
‘Kwahiyo wewe unataka ukae hapa nyumbani hadi
uzalie hapa, huoni kuwa hiyo ni bahati yako umeipata, ...wenzako wanaitafuta
hiyo bahati hawaipati...sisi tumemuoana huyo huyo anakufaa inatosha..’akasema
baba.
‘Lakini baba ni haki yangu kuolewa na mtu ninayempenda,
na awe ni mtu ninayemfahamu, huyo mtu simjui na wala sijakubaliana
naye...’nikasema
‘Sasa nakupa siku tatu, unipe jibu kama
unataka kuolewa au hutaki, na kama humtaki huyo mtu uniambie, na kama una mtu
wako mwingina utuambia ni nani, maana wewe mtoto umekuwa ni tatizo katika
watoto wangu, nakukaya tena, safari hii sitaki upuuzi, wewe unapata bahati hiyo
unaikataa, una lengo gani....’akasema baba kwa ukali, akamwambia mama;
‘Kaa na mtoto wako huyo muongee, mnipe jibu
haraka...’akasema
Mwanzoni
sikukubaliana kabisa, lakini nilipokaa na mama akanikumbushia maisha ya nyuma
ya mateso, na kuniambia kuwa sasa ni wakati wa kuanza maisha yangu mwenyewe na
mume wangu, sitakuwa na na mtu wa kunitesa tena...
‘Lakini mama huyo mtu ni nani mbona sijamfahamu?’
nikamuuliza na kabla mama hajanijibu kuwa ni mtu gani, akaanza kunikumbusha
maisha yangu ya nyuma;
‘Mwanangu hebu kumbuka ulipotoka, umekuwa ni
mtu wa mitihani, sasa angalau umempata huyo mtu, yupo tayari kukuoa, na mimi
sioni kama ni mtu mbaya, kama baba yako keshamkubali, wewe kubali yaishe,
mengine utayajua wewe na mume wako..’akaniambia.
‘Sawa mama lakini ni nani, ...ndilo swali
langu la muhimu...?’ nikamuuliza mama, na mama alionekana kutokumjua vyema,
zaidi ya baba, ...hata hivyo, nikawaliwazia sana hilo swala kabla sijaweza
kutoa jibu, nilitaka angalau ionane na huyo mtu ili nimfahamu vyema
‘Basi mama naomba angalau nimfahamu huyo mtu,
hata kwa kumuona wa mbali, ili nijue naenda kwa nani,..’nikasema.
‘Baba yako kasema siku ya kutoa jibu ndio
utamuona...’akaniambia mama na nilitakiwa kutoa kauli ya kukubali au kukataa
kwa baba,kabla ya siku hizo hizo tatu
NB: JE ILIKUWAJE? Nawashukuru wote kwa dua na
maombi yenu, kwani nilikuwa na mtihani wa kuumwa,sasa nahisi sijambo,
namshukuru mungu.
WAZO LA LEO: Kila fani ina utaratibu wake na masharti yake, ni vyema
ukazingatia elimu yako kutokana na jinsi ulivyoisomea hiyo fani, na sio kwa
jinsi watu wanavyosema au jinsi watu wanavyotaka kwa utashi wao...
Mara nyingi fikira za wengi ni kupata, hata
kama sio halali, hata kama ni kukiuka taratibu za hiyo fani. Wizi sio lazima
uvunje duka, hata kugushi, kudanganya na kupata mali isivyo halali kiujanja
ujanja ni wizi,..utapeli, ufisadi, ni wizi wa hali ya juu, tukumbuke kuwa katika maisha, ukweli-uamnifu, na haki
ndio njia ya heri na baraka.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment