Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, February 5, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-9




Kitu cha ajabu nilichogundua ni kuwa Mdada alikuwa kabadilika, sio kama alivyokuwa mwanzo, sasa hivi nilimuona katulia, na hakuwa akinisumbua kama ilivyokuwa awali, ni kama vile alishakipata kile alichokuwa akikitaka, nikajua labda mambo yamekwisha, nikawa nafanya kazi zangu na ikifika jioni namkuta keshaondoka, au kama yupo ananiambia niondoke tu,

Hata hivyo moyoni na akilini mwangu nilikuwa nimejenga chuki fulani dhidi yake kwa kile alichonifanyia, maana zile picha alizonionyesha ni za aibu tupu hazifai kuonekana kwa watu, na baya zaidi sijui kusudio lake ninini, kwahiyo nikawa naishi maisha ya mashaka, nikitarajia jambo, nikahisi kuna kitu kibaya kitakuaj kutokea.

Siku moja nikapokea barua kutoka kwa mchumba wangu akinisisitizia kuhusu ndoa yetu, na huyo mchumba wangu akasema hawezi kusubiri zaidi , kwahiyo likizo yangu ikifika niwe tayari kwa ajili ya kufunga ndoa, sikuwa bado nimejiandaa, lakini kwa jinsi alivyoandika, nikaona kweli kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Nikawa nawazia jinsi gani nitalifanikisha hilo, kwani ndoa siku hizi ni swala la kijamii, na ilitakiwa liwe na maandalsii yake, lakini hata hivyo sikutaka niwaambia wfanyakazi hapo ndani mpaka niwe na uhakika nalo, na hapo hapo nikajikuta nikiwaza mdada, je akisikia hivyo atachukua hata gani, sijui kwanini niliwaza hivyo.

Hapo hapo nikawa namuwaza mdada, sijui kwanini namuwaza sana yeye, kuliko hata huyo mchumba wangu,  ni kama mtu maalumu aliyekuja kuuharibu ubongo wangu,kwani pamoja na hilo alilonifanyia, lakini kila nikimuona nahisi moyo ukinienda mbio isivyo kawaida, na nlitamani aniongeleshe tu, au angalau nione lile tabasamu lake..

 Nilipomaliza kuisoma ile barua, nikawa nimetulia ofisini kwangu, na mara simu ikalia, nikaipokea, ilikuwa sauti ya mdada, akaniambia;

‘Leo nataka tuonane kama una nafasi..’akasema.

‘Tu-tu-onane wapi?’ nikamuuliza baada ya kutulia kidogo

‘Wewe unafikiri wapi, maana nina maongezi muhimu sana na wewe, au tufanye pale pale ninapopenda kupata kinywaji...ni muhimu sana...’akasema kwa suati ya utulivu kama sio yeye.

‘Mhh, ...’nikasita kuongea na yeye akasema
‘Kama haiwezekani leo, hakuna shida, ...’akasema.
‘Nitakuambia baadaye...’nikasema nay eye akakata simu, na mimi akilini nikawa na hamu ya kuonana naye, sijui ni kwa vile umepita muda sijawahi kuwa karibu nay eye, au kuna nini kinanitesa moyoni.

Nikajifanya hakuna tatizo na kujaribu kulipotezea, nikamaliza kazi zangu, na nilijua bosi leo anaweza kuniita ili tuendelee na kisa cha maisha yake, nikawa namsubiria, na kweli baadaye akaniita, nikaenda kwake, akaniangalia machoni, na kuniuliza;

‘Una tatizo gani?’ akaniuliza
‘Kwanini bosi unaniuliza hivyo, sina tatizo kabisa...’nikasema huku nikikwepa kuangaliana na yeye moja kwa moja usoni.

‘Kwanini unakunywa pombe kiasi hicho, nakumbuka mwanzoni uliniambia kuwa pombe ni adui yako, kama ukinywa, unakunywa kwa ulazima fulani, labda ni shughuli muhimu, vinginevyo hutaki kabisa kunywa pombe...’akasema.

‘Ni kweli bosi, nakunywa kunywa..., sijui kwanini imetokea hivi, unakumbuka niliwahi kukuambia kichwa kinaniuma sana, nikagundua kuwa nikinywa pombe kinatulia, sasa imekuwa kama kawaida, nikihisi maumivu ya kichwa nakunywa angalau kidogo nikamdanganya maana siku hizi nakunywa kweli,sio kidogo..

‘Sikiliza mpendwa, angalia sana maisha hayo uliyojiingiza nayo, usikubali kuwa mtumwa wa watu wengine, nimeshakuambia hilo, kwanini ukabli kurubuniwa, ...kila mtu ana akili yake, ana mipangilio yake ya kimaisha, na kila mtu ana mtizamo wake wa jinsi ya kuendeleza maisha yake..muhimu sana ni elimu, itumie elimu yako vyema, ili we msingi wa kila kitu, kama una elimu yako basi itumie kwa hekima, sasa kwanini unakubali kutekwa akili?’ akaniuliza

‘Bosi mbona sijakuelewa?’ nikamuuliza.

‘Usinione mimi mtoto mdogo, hapa ndani wote ni wafanyakazi wangu, nawafahamu kama watoto wangu, na kama kuna mabadiliko nafahamu, ..na nimekuhisi kuwa una tatizo kubwa linakusumbua, na nahisi huenda umeshatekwa na wajanja wa mjini, ..nakuonya, uwe makini sana, na hawo watu..’akaniambia.

‘Bosi mimi sijatekwa na mtu, hakuna mtu wa kuniteka akili yangu, mimi najiamini, bado nina msimamo wangu ule ule,...’nikasema kwa kujiamini.

‘Haya nakutakia kila-laheri, vipi kuhusu mchumba wako, mnatarajia kufunga ndoa lini ?’ akaniuliza.

‘Katikati ya mwaka,kwenye likizo yangu..’nikasema, japokuwa sina uhakika na hilo.

‘Mhh, ni vizuri, na vipi kuhusu mdada mumewekana vipi,maana niliwahi kumsikia akidai kuwa wewe ndiye chaguo lake?’ akaniuliza.

‘Huyo alikuwa anatania tu, yeye sio chaguo langu...sijawaku kumtamkia hivyo, na sijui kwanini akasema hivyo ...kwanini unaniuliza hivyo...maana...’nikasita kuendelea.

‘Maana nini, mbona unasita kuongea, nahisi unanidanganya na sio unanidanganya mimi, ila unajidanganya mwenyewe, kuna kitu ndani yako kumuhusu huyo binti, naona umeshavutika kwake, na hapo ulipo unapatataabu kumlinganisha na mchumba wako, nikuambie kitu, katika haya maisha, kuna mipangilio, na hiyo mipangilio inawekwa kwenye mizania kwa wenye hekima wanafanya hivyo.

Kila jambo lina nafasi yake na uzito wake, na halikadhalika, unapochagua mchumba kuna mambo mengi ya kuangalia, na hayo mambo unatakiwa kuyaweka katika mizania, kutokana na umuhimu wake...usije ukalogwa na mvuto, ukasahau mambo muhimu, ni kweli mdada ana mvuto, ni mrembo sana na kila mwanaume anavutika kwake, lakini je anaweza kutulia kama mke wa nyumbani,...’akawa kama ananiuliza.

‘Sijamchunguza sana, kwahiyo simjui na sina mazoea naye sana...’nikasema huku nikiangalia chini.

‘Mimi nakueleza tu, na sijasema upo naye karibu au hafai kuwa mke wako, anaweza kufaa, lakin ukiwa naye, kwa mtu kama huyo unatakiwa uwe mvumilivu sana,usiwe na wivu, kwani ataweza kukupa shinikizo la damu...’akasema.

‘Kwanini unaniambia hivyo?’ nikamuuliza

‘Nakuasa tu maana ya dunia huwezi kuyatathimini hadi litokee, nakutakia heri kama utafanikiwa kumuoa mchumba wako, lakini inaweza ikatokea, asiwe yeye, huwezi kujua, ama kuhusu Mdada, huyu binti ana matatizo yake binafsi ndiyo yanayomfanya anywe sana pombe, sasa akipata mume wa kumtuliza nahisi atabadilika,na kutulia...’akasema.

‘Akipata lakini sio mimi...’nikasema kwa sauti ya mashaka.

‘Unaweza ukawa wewe, usijiaminishe sana, bado hujafunga ndoa ya  huyo mchumba wako lolote linaweza kutokea, maana nimekuona upo karibu sana na Mdada, huwezi jue ni nini mwenzako anakiwaza, na kapangilia mbinu gani, na mtu kama wewe ni rahisi sana kurubuniwa, ndio maana tangu awali nimekuwa nikikunya kuwa uwe mwangalifu ukiwa na binti kama huyo,..’akasema.

‘Mhh, bosi mimi nina mchumba wangu, na wala sina mpango na huyo mdada...’akasema.

‘Ni kweli..una uhakika na kauli yako?’ akawa kama ananiuliza halafu akasema

‘Tuyaache hayo, ..ila nakuonya kama kweli huna mpango naye, hakikisha unakuwa na msimamo huo, pingana na nafsi yako jaribu kuishinda nafsi yako, kwani sio kila kinng’aacho ni dhahabu..na ili kulishinda tatizo, usilikimbie, pambana nalo, ili uwe na uhakika ...ujiamini na unachokifanya...’akaniambia.

‘Sawa bosi nimekuelewa, nitajiathidi sana ...niishinde nafsi yangu..’nikasema huku kichwa kikianza kuniuma,...nikawa natamani niondoke nikapate kinywaji, na mara simu yangu ikaingia ujumbe; nilipoangalia nikaona ni ujumbe wa mdada;

‘Leo usiniache, tutatoka pamoja...’nikahisi mwili mzima ukinisisimuka, uwoga, na hali isiyo ya kawaida ikaniteka akili yangu,kichwa kikawa kinauma sana nikamwangalia bosi nikitaka kuomba niondoke, na yeye akasema;

‘Haya ngoja tuendelee na kisa chetu...’akasema bosi, na nikashindwa kumpinga nikatulia kukisikiliza hicho kisa, lakini hapo kichwa kilikuwa kikiuma sana....


**********

Nilipomaliza kuzimeza zile printoni 30 kwa pamoja nilikwenda kulala nikijua ndio safari yangu mwisho sitaamuka tena,sitasumbuliwa tena, nitapumzika milele, nikalala nikikisubiria, huku nikimuwazia mama yangu jinsi gani atakavyohuzunika akisikia nimeshakufa kwa kujiua,...

Mwili ulianza kulegea, nikahisi usingizi mnzito ukininyemelea, na giza likatanda usoni, na kujikuta kwenye dunia nyingine, nikijua huko ndio ahera tena.

Nakumbuka kuna muda nilihisi watu wakiniinua, ni kama ndoto, au hisia kwenye kichwa, na mmojawapo niliyemuhisi alikuwa mfanyakazi wetu wa ndani, lakini yote hayo nilikuwa nikihisi tu au kuyaona kwenye njozi ya aina yake, kitu ninachokumbuka ni kuwa nilipoamuka nilijikuta nipo hospitalini nikiwa nimetundukiwa dripu

Walivyonihadithia ni kuwa mfanyakazi wetu wa ndani aliingia akinitafuta nikasaidie kazi, na alipoingia chumbani akanikuta nimelala, akaniita sana, lakini sikuitika, akanisogelea akijua namfanyia makusudi, na kuanza kunitikisa tikisa, lakini akanona nipo kimiya, ndipo akahisi sipo salama.

Kwa haraka akawaambia kaka zangu, kwani wazazi walikuwa kwenye shughuli zao, na kaka zangu kwanza walipuuzia, lakini walipoona huyo mfanyakazi anawasisitizia, na kuwaambia huenda mimi nimeshakufa, ndipo wakaingia na kunikuta nimelala fofofo..

‘Amekufa weli huyu, hebu angalia mapigo ya moyo...’akasema mmojawapo

‘Yanapiga kwa mbali....’akasema huyo aliyeniangalia na kila mmoja akafanya hivyo.

‘Huyu kazimia, huenda kazidiwa na njaa, au kashikwa na kizunguzungu akaanguka...’akasema mwingine.

‘Sasa tufanyeje, tuwaite wazazi...?’ wakaulizana.

‘Cha muhumi hapa ni kumpeleka hospitalini, maana nijuavyo mimi mpaka wazazi wafike hapa itachukua muda,...’akashauri kaka yangu ambaye tunazaliwa pamoja.

Basi wakakubaliana na ushaurii huo wakanipeleka hospitalini, na huko nlipofika cha kwanza tu ni kuniwekea dripu ya maji na dawa za kuongeza nguvu, na ilipoisha ya kwanza nikazindukana kutoka kwenye huo usingizi mnzito.

Kweli kama siku yako ya kufa haijafika hata ufanye nini, ndivyo ilivyotokea kwangu,sikufa, na docta akashauri niendelee na dripu nyingine huku wakinifanyia uchunguzi, nikalazwa hapo hospitalini, na wazazi walipofika kuniona sikuongea nao sana, wao walishafikiria kwingine, wakamuuliza docta kuwa huenda mimi ni mja mnzito,docta akawaambi vipimo bado vinafanyiwa uchunguzi.

‘Lakini sizani kama ni mja mnzito, inavyoonekana kuna kitu kikali amekinywa, lakini yote hayo tusubiri vipimo..’akasema

Baadaye nikapata nguvu, na hapo docta akajaribu kunihoji nina tatizo gani, au nimekula kitu gani, sikuweza kumwambia ukweli, nilisema mimi sijui, nilihisi tu mwili umechoka na kuisha nguvu, docta akasema;

‘Usijali, vipimo havionyeshi tatizo kubwa, lakini kuna dalili kuwa ulikunywa dawa, au kitu kikali, ...vipimo vyetu hapa havina uwezo wa kutambua zaidi, ni wewe ungetuambia ukweli tukajua jinsi gani ya kukusaidia,....’akasema.

‘Sijala au kunywa kitu kikali...’nikasema uwongo, sikutaka kuishi, niliona kama inawezekana hiyo dawa iendelee kuwepo huko tumboni huenda nikajifia, lakini docta akasema.

‘Hiyo dawa tuliyokuwekea, inasafisha sumu zote tumboni, kwahiyo kesho au kesho kutwa hali itakuwa nzuri kabisa..’akasema docta.

Baada ya siku tatu nikapata nafuu na kurejea nyumbani ila sikusema siri yangu hiyo kuwa nilitaka kujiua, nilitamani nirudi huko huko hospitalini, kwani nikikanyaga pale nyumbani, ni kazi, kusimangwa, matusi, kusingiziwa uwango, na hawakujali kuwa nilikuwa nimetokwa kulazwa hospitalini, ile nafika tu, nakutana na kazi,nikaendelea na maisha ya taabu na sijui ilitokea nini, kwani baba na mama walikaa, wakapanga niondoke hapo nyumbani.

‘Mimi huyu mtoto sitaweza kuishi naye tena, ...’akasema mama wa kambo

‘Lakini yeye ndiye anayekusaidia kazi nyingi za hapa nyumbani...’akasema baba

‘Kusaidia gani kazi, huoni kuwepo kwake hapa ni taabu kuliko huo msaada unaosema, vitu vinapotea, vyomvo vinavunjika, anafanya kazi kwa kujilazimisha tu, huoni sasa anajisingizia kuumwa, ...hapana huyu mtu hanifai tena hapa nyumbani....’akasema mama

‘Sawa kama unaona humuhitaji tena, atarudi kijijini akakae na mama yake, najua huyo wataivana...’akasema baba.

Kweli nikarudi kijijini na kukutana na mama yangu ambaye alijaribu kunihoji, kisa cha kurudishwa, kwani alijua kuwa huko mjini nilikuwa natafutiwa chuo, au sehemu ya kujiendeleza kama walivyodanganywa, mimi sikutaka kumuumiza mama kwa kumuhadithia mambo ya huko, nikasema;

‘Naona imeshindikana, na mimi sijui zaidi, labda uwaulize wao...’nikasema

Kutokana na hayo mateso ya muda mrefu, akili yangu ilikuwa kama imeganda, na sikutaka kusema sana kwa mama, kwahiyo nikajenga tabia ile ile ya kule mjini ya kutokuongea, nikawa kimiya kabisa, na hata mama aliponiuliza kuwa nina tatizo gani nikamwambia.

‘Mama sina tatizo, ndivyo nilivyo, nikiwa huko mjini, nilikuwa hivi hivi, nakuogopa kuongea kwani nikiongea nasingiziwa uwongo, ...kwahiyo niliona bora niwe nakaa kimiya, na nimezoea kuwa hivi...’nikamwambia mama.

‘Lakini hapa upo na mama yako, ongea, usione hofu..’akaniambia.

‘Sijui kama nitawza kuongea, ...nimeshazoea hivyo, usiwe na wasiwasi na mimi mama..’nikasema

Ikawa nimejijenga hiyo hiyo tabia, nikuamka saa kumi na moja alfajiri kuanda chai kwajili ya mama ,kisha mama akiamka anajianda kwenda kazini,huku mie nikiwa naanda chakula cha mchana na usiku nakula jikoni nafanya usafi na kwenda kulala, ikwa ndio ratiba yangu.

Mama akirudi huwa kachoka, hatuna mua mwingi wa kuongea, na mimi nikawa sijishughulishhi na shughuli zozote za kijamii, kwenda kusalimia ua kutembea, hata tv, iliyokuwepo humo ndani nikawa siangalii au hata kusikiliza redio nilikaa hivyo kwa muda wa kama miezi mitatu.

Siku moja tukajiwa na ugeni wa gafla alikuwa ni rafiki mkubwa wa mama yangu alikuja kumtembela kutoka mikoani, alipofika tukasalimiana, na kama kawaida yangu nikaingia chumbani kwangu na kujifungia, nikiwaacha mama wakiongea na huyo mgeni, lakini baada ya kufanya maandalizi yote ya mapishi.

Yule mgeni akahisi utofauti wangu, kwani alikuwa akinifahamu kabla, akamuliza mama nina tatizo gani, au nina uja uzito, kwani ananiona kama sie yule mtoto anayemfahamu kabla, na mama akamwambia sina tatizo ni athari ya maisha ya huko mjini.

‘Athari gani...alikuwa akiishi vipi huko mjini?’ akadadisi.

‘Hataki hata kuniambia, lakini nahisi mama yake wa kambo alikuwa akimnyanyasa sana, kwahiyo amekuwa akiogopa hata kuongea....’akasema mama

‘Inabidi umsaidia huyo mtoto hali anayoishi nayo sio sahihi, ataumia kisaikolojia...’akasema huyo mgeni.

‘Najitahidi kumsaidia, lakini kama unavyojua kazi zetu, nikirudi hapoa nyumbani nimechoka, nashukuru kuwa yeye sasa yupo hapa nyumbani ananisaidia kazi za nyumbani,...’akasema mama.

‘Mimi kwasababu nipo siku mbili tatu, nitakusaidia kuona tatizo ni nini...’akasema na mma akamwambia

‘Nitashukuru sana ukinisaidi kwa hilo,...maana sio kwamba haliniumizi kichwa linaniumiza sana, lakini nitafanya nini,...’akasema mama.

Siku ya pili yake mama akaenda kazini, mimi nikabakia na huyo mgeni na nikafanya kazi zangu kama kawaida na huyo mgeni akanisaidia zile kazi alizoziona na baadaye kazi zikaisha, mimi nikamwambia mgeni naenda kupumzika ndani, akaniambia sawa, yeye anaangalia tv, akichoka ataingia chumbani kwake kujipumziha kama mimi, kulikuwa hakuna kazi ya kufanya kwa muda huo.

Na baada ya muda, nilihisi kabisa kuwa hata huyo mgeni atakuwa na yeye kaenda kujipumzisha kwani nilihis ukimya na tv, ilikuwa imezimwa,....

Kama kawaida yangu huwa nikimaliza kazi, nachukua kitabu changu cha kumbukumbu, diary, na kuanza kuandika, kila kilichotokea, kilikuwa kina mambo yote niliyokuwa nikifanyiwa huko mjini, na nilianza kukindika siku nyingi sana, tangu nikiwa shuleni, kwahiyo kina kila kitu kinachonihusu mimi.

Nikiwa chumbani mara nikasikia mlango ukigongwa, nikashituka, maana humo tulikuwa mimi na huyo mgeni, mimi nilikuwa namuita Aunty, lakini yeye alishasema anaangalia tv, akichoka naye ataingia chumbani kwake kujipumzisha kwahiyo sikutegemea kuwa ni yeye aliyenigongea, nikaanza kuhisi wasiwasi, ..ni nani huyo!

Ndio hali yangu niliyokuwa nayo, nikikumbuka huko mjini, ilikuwa nikigongewa mlango kama nipo chumbani, ujue kuna tatizo, na kitakachofuata hapo kama si kipigo, ni lawama matusi, na masingizio ya kila namna, kwahiyo hiyo hali ikawa imeniathiri kisaikolojia, na hata hapo mlango ulipogongwa, nikajikuta nahisi hivyo hivyo..

Moyo ukaanza kunienda mbio, nikajawa na wasiwasi, nikitarajia mabaya, nikajisahau kuwa nipo nyumbani kwetu kwa mama mzazi, kwanza nikajaribu kuituliza ile hali, akili ikubali kuwa sipo huko mjini tena, lakini haikuwezekana, nikaona kwanini nijitese, nikauliza;

‘Wewe ni nani?’ nikauliza

NB: Tuishie hapa kwa leo, huyo ni nani aliyemgongea mpendwa mlango

WAZO LA LEO: Athari nyingi za watoto kisaikolojia huanzia wakiwa wadogo, na hali kama hiyo isipodhibitiwa mapema, mtoto huyo atakuwa hivyo hivyo, na ukubwani atakuwa na madhara fulani, ..

Kuna watoto wanaandamwa na mishituko ya moyo! kupiga kelele ovyo, uwoga na wasiwasi, misongo ya mawazo, kuishi maisha magumu, mateso ya hapa na pale,mabadiliko ya hisia za kimaumbile haya yote yanaanzia utotoni...na utakuta watoto wengine, huanza kupagawa wakishaanza shule, na watu hukimbilia kusema ni mashetani kumbe chanzo ni maisha ya utotoni.


Jamani ulezi sio lele mama, tuweni makini katika malezi ya watoto wetu, tusipende kuwatisha watoto, au kuwapeleka watoto kuishi na watu tusiokuwa na uhakika nao, au kuwalaza na wageni, hata kama ni ndugu mnaowafahamu, huwezi jua ni kitu gani kinatokea usiku na hata hawa wafanyakazi wa ndani wanaweza kuwa chanzo kibaya kwa watoto wetu kutegemea na jinsi wanavyoishi nao wakati wewe haupo,  tukumbuke athari za hayo yote hutaweza kuziona sasa hivi, athari zake zitajitokeza ukubwani.
Ni mimi: emu-three

3 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Inasisimua na kufundisha..Wazo la leo nimelipenda mno...nilikuwa nasikiliza kipindi fulani cha malezi ya watoto kinafanana na hiki..Ahsante

Serina said...

Nakubaliana na Da Yasinta kuhusu wazo la leo. Mwenyewe napitia makuu sasa hivi na kama sio wanangu ningeshakuwa chizi.Sitaki ninayopitia sasa yawadhuru zaidi. Uzazi jukumu kweli!

Anonymous said...

[url=http://buy-arimidex.xyz/]arimidex steroids[/url] [url=http://buy-albuterol.eu/]where can i buy albuterol online[/url] [url=http://buy-erythromycin.date/]buy erythromycin[/url] [url=http://doxycycline-hyclate.eu/]doxycycline hyclate 100mg price[/url] [url=http://tamoxifen.win/]tamoxifen[/url] [url=http://genericlevaquin.ru/]purchase levaquin[/url] [url=http://diclofenacsodium.webcam/]diclofenac[/url]