Nikiwa kwenye pikipiki yangu nikielekea sehemu
ambayo nafahamu Mdada bado yupo hapo, mara nikakutana na gari dogo, hilo gari likakatisha
mbele yangu na kunifanya nisimame kwa ghafla, nikaanza kulalamika, kwa hasira
‘Wewe vipi unataka kuniua ni udereve gani
huo...’nikasema huku nikiwa tayari kuteremka kwenye pikipiki yangu niende
kuzozana na huyu dereva, na huyu mwendeshaji wa hilo gari, bila wasiwasi, akafungua mlango wa gari lake, na
taratibu akanifuata pale niliposimama, alikuwa kavaa mawani
makubwa,akanisogelea, akayavua yale mawani yake.
‘Oh, ni wewe afande, samahani, lakini ulivyofanya sio sahihi,wewe ndiye unayesimamia uendeshaji sahihi wa magari na leo unanifanyia mimi hivi, ..huoni ungesababisha ajali...’nikasema na yeye akawa ananiangalia kwa dharau, halafu akasema;
‘Nataka kukuonyesha kuwa unachokifanya,
kitakuja kukuharibu, ujue kuna watu na watu, sasa angalia sana...’akasema huku
akiwa kashikilia usukani wa pikipiki yangu.
‘Afande mimi sijakuelewa...’nikasema
‘Unanielewa sana, ...kwanza nikuulize Mdada
yupo wapi?’ akaniuliza na hapo nikajua kumbe mwanzangu anaongelea kuhusu
aliyekuwa mchumba wake.
‘Anaumwa, kwa taarifa nilizozipata
anaumwa...’nikasema
‘Anaumwa au, kasakamia mipombe, ndio maana haweze
kuja ofisini, nakuonya tena achana na huyo mwanamke, huyo mwanamke tunamfahamu
sisi tuliomkaribisha huu mji,...’akaniambia.
‘Lakini mbona mimi sina mahusiano na yeye, mahusiano
yangu mimi ni yeye ni kikazi zaidi...’nikamwambia.
‘Na iwe hivyo, ila yeye anasema kuna kidudu
mtu hapo ofisini kwake,ana kamba mguuni, huyo kuku mshamba, ndiye anayetaka awe
mchumba wake, sasa sijui kama ni wewe au ni nani mwingine, yoyote yule ajue
kuwa huyo mtoto nimemgharamia mimi, hadi akapendeza, na sasa anajiuona kafika,hajafika....’akaniambia
na akawa kama anakagua pikipiki yangu.
‘Afande mimi sijakuelewa, ...kwasababu nasikia
wewe na huyo binti mumeshaachana, na wewe umesema huna habari naye tena,
ulilitamka hilo mbele ya watu wenye heshimza zo, sasa iweje bado unadai ni mtu
wako?’ nikamuuliza
‘Kwahiyo unataka kushindana na mimi?’
akaniuliza
‘Aaah, kwanini nishindane na wewe afande,
...sijasema mimi namtaka huyo mwanamke, mimi mbona nina mchumba wangu,
...’nikasema.
‘Mchumba wako, ungelikuwa na mchumba wako,
ungelikesha na huyo mwanamke kwenye nyumba ya wageni...unafikiri mimi sijui
kinachoendelea kati yako na yeye, nakushauri kwa nia njema, achana naye,
....vinginevyo, huyo mchumba wako atajua kila kitu, na hiyo kazi inayokuweka
hapa mjini utaikosa, ....sio hivyo tu, unaweza ukaozea jela..huyo mwanamke ukamkosa
na maisha yako ya baadaye yakaishia jela, huyo mwanamke hakufai,...’akaniambia.
‘Sawa afande mimi nimekuelewa,na
nimeshakuambia mimi sina mahusiano ya kimapenzi na huyo binti....’nikasema.
‘Sawa tutaona ukweli wa kauli yao, ila mimi nakupa siku tatu, nikikuona upo na
huyo binti, utalifahamu kabila langu, huwa sisi hatutushii, nitakupiga, tunapiga
kwanza , kwaheri....’akasema akinipiga begani kwa ngumi, ni kipigo kidogo,
lakini nilihisi kama bega linataka kuachana na mwili,....yeye akaingia kwenye
gari lake akaondoka, na mimi nikawa najiuliza nifanye nini...mara simu yangu
ikaita..
‘Unakuja ....nimeambiwa na bosi unakuja, upo
wapi?’ ilikuwa sauti ya mdada.
‘Ninakuja, umeshajiandaa , maana sitaki
kupoteza muda?’ nikamuuliza
‘Unataka nijiandae vipi, hapa nilipo nina
khanga moja tu, nataka tumalizie pale tulipoishia jana...’akasema.
‘Ina maana huumwi?’ nikamuuliza nikitaka
kugeuza pikipiki nirudi kazini/
‘Ninaumwa sana, na docta wangu ni wewe,ndio
maana bosi akakutuma uje kwangu, ...’nikasema.
‘Wewe huna maana kweli, ina maana huumwi,
unamdanganay bosi...’nikasema.
‘Hivi wewe kwanini hutaki kunielewa, yaani
huoni kuwa yote haya nayafanya kwa ajili yako, hivi wewe ni mwanaume kweli,
angalia wanaume wenzako wanavyofanya,ujilinganishe na wewe. Ua wewe sio riziki.....’akasema
kwa sauti kama ya mgonjwa.
‘Sikiliza Mdada, huko unapokwenda ni kubaya,
hayo matusi yako siyapendi, nakuo,mba tuheshimiane, ...’nikasema kwa hasira, na
kauli yake ilinikera, na moyni nikawa naingiwa na jaziba, ya kumuonyesha mimi
sivyo hivyo anavyonifikiria.
‘’Kama umekasirika, onyesha hasira zako kwa
vitendo, wanaume hawabembelezwi kihivyo, mimi nina mashaka na wewe...’akazidi
kunikera.
‘Mdada, naomba tuheshimiane, wewe hujui
unaniweka katika hali gani, ...’nikasema.
‘Nakuweka katika katika hali gani!...,
sikiliza usijione wewe ni wa maana sana, wapo wanaume wananitafuta usiku na
mchana, hivi wewe una nini cha kuringia, ndio huyo mchumba wako wa
kijijini,mshamba kama wewe...nakuambia hivi , usipofanya nitakavyo mimi
nitakatumia hako kashamba kako huu upuuzi wako, nasikia baba mkwe wako
mtarajiwa ni mkali sana, .....’akasema.
‘Hayo yamefika wapi, na umeyapata wapi mambo
ya mchumba wangu, nakuomba usinichafue, nitukane mimi upendavyo, lakini sio
hawo,...usitake kumchokoza nyoka shimoni...’ nikasema kwa hasira.
‘Hahaha, eti nisimchokeze nyoka shimoni, hivi
na wewe unaweza ukajiona una nguvu sana, au una uwezo gani,...wala usitamke
maneno kama hayo, huna lolote, kama umenishindwa mimi, ujue huna lolote,...sasa
unakuja au unapoteza muda tu hapo...?’ akauliza kwa hasira.
‘Nakuuliza kwanza huyo baba mkwe wangu
umemjuaje, nakuona unanichimba?’ nikamuuliza, maana sijawahi kuongea na yoyote
kuhusu mchumba wangu, au baba makwe wangu, yupo vipi. Ni kweli baba mkwe wangu
ni mkali sana, na hadi kufikia kunikubalia niwe mchumba wa binti yake nilipata
shida sana, na akanikubalia kwa masharti makubwa sana na mpja ya masharti ni
kuwa nisije kumpotezea muda binti wake, nisije nikaonekana nina mahusiano na
wanawake wangine.
‘Mzee mimi naahidi mbele yako, sitakuwa na
mahusiano na wanawake wengine, binti yako nampenda sana, hakuna mwingine,
atakayeweza kunibadili akili yangu, ...ngoja nijiweke sawa, tutafunga naye ndoa
hivi karibuni...’nikamwambia.
‘Mimi nakuchunguza, popote utakapokuwa ujue
kuna watu wangu wanakuchunguza nyendo zako, sasa ujifanye mjanja,...binti yangu
nimemlea katika maadili mema, na atakusubiri, hadi hapo ytakapokuwa tayari, ole
wako, itokee vinginevyo, ...’akaniambia na kweli mzee huyo anaogopewa sana,
kutokana na wadhifa wake serikalini.
Sasa
kusikia huyo Mdada anamtaja, akashangaa, kamjuaje huyo mzee, huenda huyo mzee,
keshatuma watu wake huku alipo, na akakutana na huyo mdada, wakati anawaza hayo
mdada akasema;
‘Mimi nakufahamu sana, kuliko unavyofikiria
wewe, ....jana nimepata kitu muhimu sana, ambacho akikiona baba mkwe wako, ...ohoo. sisemi mengi, akiziona
hizi picha, sijui kama huyo mchumba utampata tena, na jela inakungoja, ...’akawa
kama anauliza.
‘Sikiliza mdada, mimi narudi ofisini,
nitamwambia bosi kuwa wewe huuwmi,...’nikasema huku nikigeuza pikipikii yangu
kurudi ofisini.
‘Unasema nini, hivi wewe una akili kweli,
yaani sasa umevimba mapembe unapinga amri ya bosi wako, kakuambia uje unipeleke
hospitalini, wewe bado upo njiani, umazubaa, unataka nini, hutaki kazi
eeh...nakupa dakika kumi kama hujafika hapa, nampigia bosi wako simu na picha
ya upuuzi wako juu....’akasema.
‘Ili iweje, nifukuzwe kazi, ndivyo unavyotaka,
na maswala ya mchumba wangu hapa yanakujaje, kwanini husemi kuhusu mchumba
wako, ambaye muda mchache aliopita alikuwa nami hapa, akinionya kuhusu
wewe...’nikasema.
‘Tatizo lako wewe bado mshamba, unatishwa na
mwanaume mwenzako unakubali, ina maana yeye ana nini ambacho wewe huna, wewe
mwanaume gani, utaerevuka lini, ina maana mimi mwanamke ndiye ninayekuelekeza
njia, kweli wewe sasa unanitia aibu, nimeshajiandaa, nakusubiri, tena fanya
haraka, nisije nikapoteza fahamu, ....’akasema na kukata simu.
Nilikuwa bado nimesimama nikiwa nashindwa
nifanye nini, nirudi ofisini au nienda kwa Mdada, na akilini sauti ya aliyekuwa
mchumba wake, ilikuwa ikinitisha,;
‘...vinginevyo, huyo
mchumba wako atajua kila kitu, na hiyo kazi inayokuweka hapa mjini utaikosa,
....sio hivyo tu, unaweza ukaozea jela..huyo mwanamke ukamkosa na maisha yako
ya baadaye yakaishia jela, huyo mwanamke hakufai,....
Niliamua kutii mari ya bosi wangu, nikaenda
moja kwa moja hadi kwenye ile nyumba ya wageni, kwani nilijua huyo Mdada bado
yupo hapo, na nilitakiwa kwenda kulipa pesa za watu, kama nilivyoahidi
Nilipofika, sikupanda juu, nikampigia Mdada
kuwa nimeshafika, nipo chini, nalipa pesa za watu, yeye akaniambia anahitaji
mtu wa kumshika mkono, maana hawezi
kutembea.
‘Madada, hebu ...’nikataka kujitetea, na yeye
akasema.
‘Unapoteza muda, panda huku juu, kwanini
hunielewi...’akasema na mimi kwa hasira nikapanda huko juu, nikagnga chumba
chake, hakuitikia, nikagonga tena, kukawa kimiya, nikafungua mlango, nilimkuta
amelala kitandani.
‘Ina maana hujajiandaa?’ nikamuuliza
‘Unataka nijiandae vipi,..nilikuambiaje kwanza
tumalize ile kazi tuliyoianza jana,...’akasema huku akiondoa shuka alilokuwa
kajifunika,..sikuamini, na mara mlango ukagongwa.
‘Oh, nani huyo tena, a..’akauliza mdada, na
mimi nikageuka, kuangalia mlangoni, mlango ukafunguliwa, na aliyekuwa kasimama
mlangoni ni afande.
‘Hongera ....sikujua kuwa umejificha hapa, na
ndio mipango yenu, badala ya kuwa kazini, mnakuwa kwenye nyumba za wageni, muda
kama huu,...’akasema huku akiwa kashika kiuono.
‘Hivi wewe mwanaume unanitafuta nini,....’akasema
mdada
‘Umesahaueeh, ni nani aliyekuingiza hapa
mjini, umesahau eeh, ni nani aliyekufanya upendeze, na kuonekana mrembo, lao
hii, ndio unatembea ni huyo bwege....sikiliza mimi sikuja hapa kuzozana na
wewe,ninachotaka ni gharama zangu, nataka kesho uondoke kwenye nyumba yangu,
unasikia,.....na mengine yatafuata baadaye...’akasema
‘Usinitishe wewe, nyumba gani yako kwako, hebu
nenda ardhi udai kuwa hiyo nyumba ni ya kwako, ina jina lako....hivi wewe
unaniona mjinga sana, au...ulipotoa vipesa vyako, nilikuomba, siulikwua
unanishaua mwenyewe tu, na ni pesa gani uliyonipa ambayo ingeweza kujenga
nyumba kama ile...nina hati ya mkopo wa benki, ambayo inathibitisha hilo,
....’akasema na yule afande akageuka kuniangalia, na kusema;
‘Unasikia..huyo ndiye mdada, kuna kitu
anatafuta kutoka kwako, mimi nakiri kuwa nimekuwa mjinga wake, lakini
sitakubali yaishe hivi hivi....yoyote atakyetumbukiza mguu kwake, atalipa hizo
gharama,....upo tayari?’ akaniuliza
‘Mimi hayanihusu...’nikasema na kuanza
kuondoka.
‘Wewe unakwenda wapi, bosi kakutuma nini,
unataka kuniacha hapa, ni nani atanipeleka nyumbani?’ akaniuliza na mimi
nikamwangalia huyo afande, na huyo afande akaanza kuondoka.
Nikageuka kumwangalia mdada, ambaye bila
kujali alinuka pale kitndani akiwa uchi, na kuelekea bafuni, ....
*********
Ilikuwa asubuhi, wakati bosi alipoingia
alinikuta nipo kwenye meza yangu nikiwa kwenye dimbwi la mawazo, nikiwazia
picha aliyonitumia mdada, ikionyesha siku ile alipotaka kunifanyia ujanja wake,
na ilikuwa ni bahati sana , kwani ilishafika hatua ambayo nilishaamua kufanya
atakavyo, aliyekuja kuniokoa ni muhudumu, alifika na akiniambia pikipiki yangu
ipo sehemu isiyoruhusiwa.
Nikazindukana kiakili, na haraka nikajiruudi,
na kumshukuru sana huyo muhudumu kimoyoni, kwani kama isingelikuwa yeye, huenda
ningeliingia kwenye mtego wa huyo Mdada, lakini hata hivyo, kumbe mdada,
alishachukua picha za tukio hilo, na picha hizo zipo wazi, hauwezi kukataa,
zinaonyesha wazi, nikiwa na dhamira ya zati ya kutenda tendo hilo ....
‘Huyu mwanamke ananitaka nini, ana nini anakihitaji
dhii yangu, sizani kwamba ni mapenzi tu, sizani kama ananipenda kama anavyodai
yeye, nahisi kuna jambo jingine analitafuta kwangu, ..’nikawa nawaza.
Nikaangalia hiyo picha na kukumbuka sauti ya
maneno yake aliponipigia simu baada ya kunitumia hizo picha, alisema;
‘Hii ni moja ya picha ambayo natarajia
kumtumia baba mkwe wako, unaona jinsi ilivyotoka vizuri, je akiiona unafikiri
atasema nini...ole wako, nakupa siku tatu, utimize lile nililokuambia, kuanzia
sasa mimi ni mpenzi wako, ukitaka niwe wa siri, fanya nitakavyo, lakini kama
unataka nidhirishe wazi kwa watu, endelea kunikaidi...’akamaliza.
‘Lakini kwanini unanifanyia hivyo?’
nikamuuliza
‘Kwasababu na kupenda, na moyo wangu
hautatulia mpaka uwe mpenzi wangu...’akasema
‘Lakini mimi nina mchumba tayari,
nimeshakuambia hilo...’nikasema na yeye akacheka na kusema.
‘Mimi na yeye ni nani zaidi, hebu angalia sura
yangu na yeye, ...huyo ni mchumba tu, unaweza ukaachana naye, ...’akasema.
‘Siwezi kufanya hivyo,...’nikasema.
‘Utaweza tu, hilo nakuahidi, labda nisiwe
hai...’akatamka na kukata simu.
Bosi alinisalimia na kuingia ofisini kwake
baadaye akaniita, na kuniuliza habari za jana, kwani jana niliporudi sikumkuta,
alikuwa katoka na hakurudi kazini,
‘Nilipofika alisema anajisikia vizuri,
hahitaji kwenda hospitalini, alishakunywa dawa...’nikamwambia.
‘Nilijua tu huenda ni ulevi, ...ok, sasa ngoja
nikusimulia kisa changu kidogo, maana baadaye natoka nina kikao na wenzangu ,
kama nitawahi kurudi tutaendelea...’akasema
‘Sawa bosi..’
‘Unakumbuka tulipoishia, siku ile nilipopigwa
na ndugu zangu ....’akaanza kusimulia
******
Waliponiona nimepoteza fahamu huku damu
zikinitoka kwenye tundu za puani mdomoni, ...wakashituka, wakajua wameshaniua,..wakaniachia
na kumwita dada yangu wa kambo kuniangalia;
‘Nyie mbona mumeua...’akasema huyo dada,
lakini wakati huo sikimsikia, nilihadithiwa hivyo.
‘Hajafa huyo anajifanya kama kafa ili
tusiendelee kumpiga..’akasema mwingine.
‘Hebu muangalie, kama kafa, tunalo, ...’akasema
mwingine.
‘Tukamwagie maji, ili hizi damu zisionakena...’akasema
mwingine.
‘Na haya majeraha je?’ akauliza mwingine.
‘Atajua mwenyewe, si kajitakia, ...tutaishije
na mwanamke malaya humu ndani..’akasema mwingine.
Wakati huo kwa mbali nilishaanza kupata
fahamu, hata wakati wananiinua kunipeleka bafuni, nilikuwa nimeshazindukana,
lakini mwili mzima ulikuwa ukiuma, na damu bado zilikuwa zinatoka, na wakamuita
mfanyakazi wa ndani ili amsaidia dada huyo wa kambo kuniosha hayo majeraha.
Waliponimwagia maji nikasikia nguvu ikinireja
japokuwa bado, nilikua na maumivu makali sana mwilini kutokana na majeraha, walipohakikisha
damu zimesita kutoka, wakanichukua hadi chumbani, na huko wakanifungia, bila
hata ya kujali kunipeleka hospitalini, yule mfanyakazi alinipa dawa za kutuliza
maumivu. Nikawa najiuliza ni kwanini nipigwe kiasi hicho, kuna kosa gani
nimelifanya hadi kupata kipigo kama hicho, sikuweza kupata jibu.
Nilikaa mle ndani chumbani huku nikishindwa
hata kulia, ila nilikuwa naumia ndani kwa ndani,nikiwaza na kuwazua, hicho
kipigo cha masaa yote hayo, kama wanapiga mwizi kilikuwa cha sababu gani,
baadaye mlango ukafunguliwa, na yule mfanyakazi wa ndani akaniambia ninaitwa na
baba na mama, nikajikongoja hadi hapo varandani, niliwakuta baba na mama
wamekaa wanaongea, hawakuniuliza kwanini
natemeba hivyo, wakaanza moja kwa moja na aliyeanza kuongea ni baba ;
‘Sisi tumeona uondoke hapa nyumbani, tumeona
urudi ukakae na mama yako mzazi huko kijijini...’akasema
‘Mimi nimekushindwa kuishi na wewe, sitaki
kuja kulaumiwa kwasababu ya tabia yako chafu....’akasema mama wa kambo.
Na kweli nikatafutiwa usafiri wa siku hiyo, na
kwa haraka nikasafiri kwenda huko kijijini kwa mama huku mawazo yakiwa pale
pale kuhusu sababu gani hasa iliyofanywa nipate kile kipigo cha masaa yote
yale, nilifanya kosa gani kubwa , kiasi cha kupigwa kama mwizi,, tena
wanaonipiga ni kaka zangu, je walitaka kuniua, na kwanini mara kwa mara
walikuwa wakinipiga mateke ya tumboni,....
Nilipofika kwa mama kijijini, ile kumuona tu,
nikaanza kulia, nililia sana, na mama akajaribu kinisihi nisilie kwani yote ni
maisha, na maisha yana mitihani mingi.
‘Mwaanngu usilie, kama wamekukatisha shule,
ipo siku utasoma, shule zipo tu,...’akasema mama akijua kuwa kilio changu ni
kwasababu ya kukatishwa shule.
‘Mama naona heri nikae huku huku tu,maana
nikirudi huko wanaweza kuniua’nikasema.
‘Usijali tupo pamoja,...japokuwa sina uwezo wa
kukusomesha lakini ipo siku utasoma, kwani kuna nini cha zaidi mbona upo hivi,
uso kama umevimba, ulikuwa unapigana?’ akaniuliza.
‘We mama acha tu, sitaki hata kukusimulia
nisije kukuumiza moyo wako, namuachia mungu...’nikasema, na kweli sikutaka
kumuhadithia mama, kwani niliogopa nitazidi kumuumiza, wakati yeye ana matatizo
mengi ya kimaisha, niliona hayo mateso yawe mimi na hawo walionifanyia na mungu
peke yake ndiye atawalipa, nikakaa kimiya.
Siku
iliyofuata nikashangaa ugeni ukifika nyumbani, walikuwa baba na mama wa kambo, na
walipofika tu, wakaitisha kikao, na mimi nikaitwa;
‘Nimeamua kuitisha hiki kikao maalumu, ili
kuliongelea swala la huyo mtoto wako, nafikiri keshakuelezea mengi, na anaweza
akakudanganya kutokana na tabia yake chafu,...’akasema baba.
‘Mhh, mbona mnanitosha, hajanieleza jambo
baya, zaidi ya kukatishwa shule, na hilo limeniuma sana, kwanini mumkatishe
mtoto shule, tena ikiwa imebakia muda mchache tu, amalize...’akalalamika mama.
‘Ina maana yeye hajakuambia sababu ya
kukatishwa shule, ...hawezi kusema maana ana madhambi mengi sana...’akasema
mama.
‘Mtoto wako ni muhuni, akienda shuleni hasomi,
kazi ni kufanya umalaya, ndio maana nikaamua kumsimamisha shule..’akasema baba,
na mama akaniangalia kwa mashaka, hakuamini maneno hayo , akaniangalia kwa
macho yaliyojaa mshangao.
‘Jana tu, ndio tulipata madhambi yake kwa
undani, na ni makubwa zaidi ya tulivyofikiria,na ndio maana tukaamua kumleta
huku haraka iwezekanavyo,...’akasema baba.
‘Jana kuna mtu katupigia simu, kutuelezea yote
anayoyafanya huyu binti, hata mimi mwanzon I sikuamini, lakini huyo mtu
aliyetupigia simu ni mtu mwenye heshima zake, akasema kuwa huyu binti ana mahusiano na kijana mmoja wa kutoka huko
moshi, anayeishi maeneo ya huko tulipo....’akasema baba
‘Hivi hayo mnayoniambia ni kweli,...ina maana
huyu mtoto wangu kabadilika kiasi hicho?’ akauliza mama kwa mshangao.
Mimi pale nilipokuwa nimekaa, nilishikwa na
butwa, sikuamini, kwakweli nilishtuka sana , maana huyo mvulana, sikuwa na mawasiliano
naye tena, baada ya kufukuzwa shule, muda mwingi nilikuwa nyumbani, hayo
wanayosema yametoka wapi...
‘Na isitoshe, katika umalaya wao huo,
alifikiwa akapewa mimba, na kuitoa...’akasema mama wa kambo, na kauli hiyo
ilimfanya mama ashituke hadi kuangusha kikombe alichokuwa kakishika mkononi,
mama akaniangalai kwa macho yaliyojaa uchungu, woga, na kukata tamaa, na mimi
nilipomuona mama alivyoshituka na jinsi slivyokuwa akiniangalia, nikaona
nijitetee, na kusema;
‘Mama sio kweli, wananisingizia sijawahi
kufanya hivyo....’nikasema na mama akaninyamazisha kwa mikono , na kusema;
‘Mimi siwezi hata kuamini, ina maana mtoto
wangu ndiye kabadilika kisai hicho, ...sio mtoto wangu ninayemfahamu ....hapana,..hapana...’akasema
mama huku akiniangalia kwa macho yaliyojaa huzuni, alionekana kubadilika usoni,
na nilihisi anaweza akadondoska kwa shinikizo la damu, ndio maana sikupenda
kabisa kumwambia mambo hayo.
‘Kama mnabisha, ushahidi upo, mimi nimeona ni
heri ukamkague mwanao mwenyewe,nendeni na mke mwenzako mkakague, ili uhakikishe
mwenyewe, maana nafahamu utasema tunamsingizia..’akasema baba.
‘Mimi naona hilo litakuwa jambo sahihi...’akasema
mama wa kambo akijiamini, nahisi alikuwa na uhakika kuwa kweli nimeitoa hiyo
mimba, na mimi ni mlaya, lakini kwa upande mwingine,nikakumbuka hicho kipigo,
walichkuwa wakinipiga, kililenga nini, huenda walifanya vile ili
niumizwe,lakini yote nikamuachia mungu.
‘Lakini mimi naona hilo sio jambo jema, hata
kama imetokea huyo ni mtoto wetu cha muhimu ni kukaa naye tumkanye tumelekeze...’akasema
mama, huenda na yeye alishanihisi vibaya, kuwa huenda ni kweli ni yeye
ataadhirika kuwa mimi ni muhuni, mimi nikasema;
‘Wazazi wangu mimi sijawahi kufanya hivyo...’nikasema.
‘Mwanangu una uhakika..?’ akaniuliza mama.
‘Mama mimi sijafanya kama wanavyodai wao...’nikajitetea
nikiwa nalia kwa huzuni
‘Unasikia alivyomuongo, ..sasa ili uthibitishe
uwongo wake,kama hujawahi kufanya hivyo, itaonekana, mchukueni huko ndani
mkamkague, mimi nina uhakika na hilo....namfahamu sana huyu mtoto wako, ni
malaya, ananitia aibu mimi...’akasema baba
.
Kwakweli, kauli hiyo ya baba iliniuma sana,alipoonyesha
kuwa ni kweli kuwa mimi ni muhuni, malaya, na nimetoa mimba, na zaidi anataka
nikaguliwe,chuki dhidi ya baba ikanijaa, lakini moyoni nikamuonea huruma, kuwa
baba anashinikizwa katika mambo ambayo hayajui, ipo siku atafahamu
ukweli,..nafahamu kabisa kwa hivi sasa sio yeye, yote hayo ni kwasababu ya mama
wa kambo.
Basi wazazi wangu hawo mama na mama wa kambo
wakanichukua hadi chumbani, wakaniambia nijiandae, nikaenda bafuni nikaoga, na
baadaye niakrudi hapo chumbani, nikawekwa mkao wa mama mja mzito anayetaka
kujifungua, ili eti nikaguliwe..
Nilikubali kuzalilishwa hivyo, ili moyo wao
urizike, nilifanyiwa huo uchunguzi na mama yangu mzazi na mama wa kambo....baba
akiwa anasubiri taarifa...
NB: Je kuligundulikana nini, je ni kweli mpendwa
alikuwa katoa mimba
WAZO LA LEO: Tukwepe kutoa kauli za kashifa kwa wenzetu bila kuwa na
ushahidi nazo, hasa kauli za umalaya, uchawi, wiz ink, kauli kama hizi ni nzito
sana, ni nyepesi kuzitamka mdomoni lakini ni kauli zinaziumiza sana hasa kwa
mtu ambaye hajawahi kuzitenda.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Hello there! This is my 1st comment here so I just wanted to give a quick shout out and tell you
I truly enjoy reading through your articles.
Can you recommend any other blogs/websites/forums that go over the same subjects?
Thanks!
My homepage ; myanmar airways
Post a Comment