Baada ya kuhakikisha kuwa kila mtu aliyestahili kufika kwenye
kikao amefika, na wale ambao hawajafika washatanguliza dharura zao, kikao kikaanza, na
kwa vile mimi ndiye niliyekiomba hicho kikao, nilitakiwa mimi nimkaribishe
mwenyekiti , lakini kwa heshima, nikamuomba mume wangu aifanye hiyo kazi, ya
kumkaribisha mwenyekiti ili kikao kianze.
Mume wangu akasimama kuwakaribisha wajumbe, na kumkaribisha
mwenyekiti wa kikao,ambaye ni baba yangu. Baba kaba haajasena neno aligeuka
kuniangalia mimi, nahisi kuna kitu alikiona sio kawaida, na, kabla hajasema neno
mara mlago ukagongwa.....
Watu wote wakageuka kuangalia mlangoni, kwani haikutarajiwa
kuja mtu mwingine, kwahiyo kila mmoja alikuwa na mawazo yake, kuhusu huyo
aliegonga mlango, wengine walihisi ni askari, wengine wakahisi huenda ni
wafanyakazi wa hapo wananihitajia mimi, ilimradi kwa muda mfupi kila mmoja alikuwa
na wazo lake. Mwenyekiti akanigeukia, kutaka kuniuliza, lakini kabla hajasema
neno, mlango ukafunguliwa na akaingia mtu akiwa bado na kofia la waendesha
pikipiki, kuonyesha kuwa ni mwendesha pikipiki, na mimi nikakumbuka yule mtu
aliyenipita, na kunipungia mkono, sikujua ni nani kwa muda ule.
Huyu mtu, alipofungua mlango, akiwa kavalia jaketi la kuzuia
upepo mwilini, na kumfanya aonekane bonge, alismama na kutuangalia akiwa na
kofia lake lile lile, inaonekana hakutaka kulivua huko nje, labda kwa vile
aliona keshachelewa, kama ni mjumbe wa kikao hiki, ambaye mimi sikuwa na habari
nay eye,au alifanya hivyo kwasababu zake nyingine. Kila mmoja ndani ya kikao
alimwangalia yeye, na yeye alipoona watu wote wanamtizama, akafanya mambo
mawili kwa haraka, kwanza akainama, kama
vile anasalimia au kutoa heshima na pili, akageuka kuangalia mlangoni, akalivua
lile kofia lake na kuvua koto , halafu taratibu akageukia watu, na kusema;
‘Samahani mwenyekiti, nimechelewa, nilikuwa naweka mambo
sawa...jamaa wananifuatilia kila kona...’ akasema huku akiangalia pale alipokaa
mwenyekiti, lakini alikuwa hamuangalii moja kwa moja usoni, na mwenyekiti
akasema;
‘Huyu amefuata nini kwenye hiki kikao...?’ mwenyekiti
akaniuliza na kabla sijamjibu akamgeukia huyo mtu na kusema;
‘Kikao hiki hakikuhusu, hiki ni kikao cha watu maalumu,
sizani kama wewe ni mmoja wa waalikwa, kama unavyoona hawa ni wanafamilia, na
watu maalumu...’akasema mwenyekiti.
‘Lakini mimi nimealikwa....’akajitetea huyo mtu.
‘Ni nani aliyekualika, majina yote ninayo hapa, sijaona jina
lako,..., kwanza wewe unatafutwa na polisi, ukionakena hapa tutaambiwa kuwa
tunakuficha, na tuna mipango na wewe, tafadhali, ondoka, usituharibie
mipangilio yetu, sisi sio wavunja sheria...’akasema baba, na mimi nikaona
niingilie kati nakusema;
‘Baba , oh mwenyekiti, mimi ndiye niliyemualika huyu mtu, nilimualika
wakati nimeshakupa hayo majina ya wajumbe, kwani sikuwa na uhakika naye, kwa
vile alikuwa haonekani, lakini ni mmoja wa watu muhimu kwenye hiki kikao, kuwepo
kwake kunahitajika ili aweze kutoa ushahidi, kutokana na mambo
tutakayoyaongelea leo hii hapa...’nikasema na mume wangu akadakia na kusema;
‘Unasema anakuja kutoa ushahidi, mdogo wangu, ana ushaidi
gani hapa, kwani kuna kesi ya nani, sijaelewa mke wangu, anyway, vyovyote
iwavyo, lakini kitu kinachomuhusu mdogo wangu nilitakiwa mimi nifahamu..’akasema
akikunja uso, kuonyesha kukerekwa.
‘Utayafahamu baadaye, kikao hiki nimekiitisha mimi, kuna
mambo mengi ambayo yatajitokeza, na yeye anayafahamu zaidi yako, kwa vile wewe
ulikuwa unaumwa,....’nikasema
‘Sio kweli, mdogo wangu hawezi kufahamu jambo, mimi nisiwe
nalifahamu, kuna kitu gani anakifahamu mimi nisikijue, kwanini unataka
kumuingiza mdogo wangu kwenye matatizo.. huyu ni mdogo wangu, mimi ndiye mwenye
dhamana naye, ...kama alivyosema mwenyekiti ni bora mdogo wangu uondoke, maana
polisi hawana dogo wakikuona hapa watakimbilia kukufunga, kabla hatujaweka
mambo sawa, nenda huko ulipokuwa tutakuja kuonana baadaye kwanza nakuhitaji
sana......’akasema mume wangu.
‘Subiri kwanza, hiki kikao nimekiitisha mimi, na ajenda zote
za kikao ninazo hapa kama katibu, na kwa bahati mbaya sikuwawagaia ajenda za
kikao hiki, kwasababu maalumu, mimi sijwahi kumuingiza mdogo wako kwenye
matatizo, ni wewe ndiye uliyemuingiza ndugu yako kwenye matatizo, kama
tutakavyokuja kuona huko mbele, ...kwahiyo yeye ni mjumbe wa hiki kikao, na
kuwepo kwake hapa ni kwa ajili ya kusema ukweli, ulitokana na wewe, yeye hawezi
kuondoka mpaka huo ukweli uthibitishe...’nikasema
‘Aje kusema ukweli upi mke wangu, usitake kikao kituelewe
vibaya, kuwa mimi sijui wajibu wangu, kila kitu hapa ni sahihi, na nathibitisha
hilo, kwani siongei kinyume na mkataba wetu,wa kifamilia, ....’akasema na kuushika
mkataba mkononi, utafikiri ndio mtetezi wake.
Mwenyekiti akaingilia kati na kusema; ‘Hebu tusikilizane kwanza..’akasema na sisi
tukatulia,
‘Kwanza , mimi kama mwenyekiti sijakubaliana na kuwepo kwa
huyu mtu hapa, kwani anatafutwa na polisi, mnafahamu kuwepo kwake hapa ni
kuvunja sheria,na mimi sio mvunjaji wa sheria, kama mwenyekiti ninaamuru huyu
mtu atoke kwenye hiki kikao...’akasema mwenyekiti.
‘Hata mimi nakuunga mkono mwenyekiti...’akasema mume wangu.
‘Mwenyekiti, naomba huyu mtu awepo, na kama ni swala la
uvunjifu wa sheria, hilo tutakuja kulimaza baadaye, kuwepo kwake, hapa
kutasaidia kuyaweka mambo yote sawa, na huenda tukaisaidia hata hiyo polisi kwa
hayo wanayoyatafuta..’nikasema na baba akaniangalia kwa makini, na akageuka
kumwangalia huyo mtu,
‘Mimi bado sijaafiki kwasababu muda uliopita niliongea na
mkuu wa upelelezi wa eneo lenu nikamkatalia kabisa kuwa huyu mtu sijawahi
kumuona, na nikimuona moja kwa moja nitamfikisha kwao, au nitawaita waje
wamchukue, na sasa hivi napiga simu waje wamchukue...’akasema
‘Usifanye hivyo baba, huyu ni mdogo wangu, na mimi ndiye
nabeba dhamana naye, kama polisi wanamuhitaji kwanza waje kuonana na
mimi,...mdogo wangu hana hatia, kama wanavyodai wao, wanamuhisi tu..mimi ndiye
niliyesababisha aonekane hivyo...’akasema.
‘Wewe ndiye uliyemtia hatiani,..basi polisi wakija
utawaambai hivyo, lakini kuwepo kwake hapa ni ukiukwaji wa sheria....’akasema
baba.
‘Baba usijali tuendelee na kikao, ...’nikasema na baba
akasema;
‘Sawa mimi naendelea na kikao, lakini msimamo wangu ni huo
huo, huyu mtu atoke nje, ...na kwa vile nimemuona, nitawapigia polisi waje
wamchukue..siwezi kwenda kinyume na sheria...’akasema
‘Kwanza mume wako kasema kuwa nyie katika familia yenu mna
katiba, na Katina hiyo ndiyo inayowaongoza,..naona katika ajenda zako katibu,
hilo swala la katiba umeliweka kuwa la kwanza, na mume wako keshalianza, naona
tuanze na hicho kipengele, cha katiba, kwanza nataka kufahamu kwanini mliamua
kuanzisha katiba, maana familia zipo, na sijawa kusikia mume na mke wakawa na
katiba? Akauliza mwenyekiti, na mume wangu akasimama;
‘Nafahamu kuwa swali hilo limemlenga mke wangu,kwa vile
ndiye mwenye hiki kikao, na diye alitakiwa aataje ajenda zake, na bahati mbaya
, kikao kimeanza juu kwa juu, kutokana na hili lilitokea, ...ni kweli ndugu
mwenyekiti, katika familia yangu, nikiwa na maana mimi na mke wangu na watoto,
tuna aktiba yetu inayotuongoza....’akatulia kidogo akiishika ile katiba.
‘Kwanini tuliamau kuwa na katiba, ni kwasababu kwanza
tulitaka familia yetu iongozwe kitaalamu zaidi, ...lakini sababu kubwa ya
kimsingi ni kuwa tulijiona kuwa na mambo mengi, mimi nikiwa nashughulika kwenye
kampuni yangu, na mke wangu kampuni yake,lakini vyote hivyo ni vyetu, japokuwa
kitaalamu kutokana na hisa kila mmoja alikuwa na mamlaka na kampuni yake...’akatulia
‘Kwa vyovyote iwavyo, mnapoona, hata kama mke alikuwa na
vitu vyake, kampuni yake, mali yake, lakini akishakuwa mke wa mtu, basi kila
kitu chake kinakuwa kwenye mikono ya mume....na hili tumelibainisha kwenye
katiba yetu....’akasema akitaka kufungua hiyo katiba.
‘Mhh, usifungue hiyo katiba kwanza, ninachotaka kufahamu ni
kwanini mliamua kuanzisha hiyo katiba, na kwa ufupi tumeelewa...swali langu la
pili, je katiba hiyo imesajiliwa kisheria au ni katiba yenu tu kwa ajili ya
mambo yenu ya ndani?’ akauliza
‘Sisi baba, ndug u mwenyekiti, kila kitu tumekipeleka
kitaalamu, katiba yetu imesajiliwa, na aliyeiandika ni mwanasheria, kwahiyo
katiba yetu ni kisheria, imetimiza matwakwa yote ya kisheria, ..hatuna matatizo
na hilo....’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema kila kitu chenu, taratibu zenu za
kila siku mumeziainisha kwenye hiyo katiba, na likitokea tatizo, mnahukumiana
kutokana na katiba yenu?’ akaulizwa
‘Ndio mwenyekiti, ndio maana nashangaa kikao hiki, kuitishwa
na mke wangu, nilitakiwa mimi ndiye nikiitishe, lakini kuna dharura kama hizo,
kama ikitokea dharura,basi mmojawapo anaweza kuitisha kikao, lakini ilitakiwa
mimi niambiwe kila kitu, kwanini kikao kiwepo, hilo
halikufanyika...nimeshitukiziwa tu, kuna kikao, cha nini na kwanini,
sijaambiwa, huo ni ukiukwaji wa katiba...’akasema
‘Ndugu mwenyekiti naomba niliongee kidogo kuhusu hii katiba,
samahani sana, kwani mimi ndio mwenye mamlaka, wa familia yangu, na kwahiyo
nina mamlaka ya kuona kila kitu kinaenda sawa...’akasema na mwenyekiti akageuka
kuniangalia, mimi nikamuashiria amuache mume wangu aendelee
‘Watu wanapofunga ndoa,
wanakuwa na taratibu zao, kama mke na mume, na wanakuwa wameshajitoa kwenye
mamlaka ya baba na mama zai, hawalindwi au kuchungwa tena na familia za baba na
mama zao, kikeni au kiumeni, wao ni watu huru, na wanakuwa na utaratibu wao
kama familia inayojitegemea, na ndivyo
tulivyofanya sisi, na kwa ajili ya kurahisisha mambo yetu tukaona tuwe na
katiba, ni wachache sana wanakuwa na utaratibu kama huo, ....’akasema mume
wangu.
‘Sisi tuna katiba inayokubalika kisheria, kwasababu
imeandikwa na mwanasheri a wa familia, yetu, na sote tukaweka sahihi zetu, mimi
na mke wangu, na wakili wetu..ikapitishwa na kusajiliwa kwa msajili wa mambo hayo,
sio katiba ya mitaani , ni Katiba iliyokubalika kisheria, ukiangalia hapa ina
kila sifa zote za kisheria, ...mimi kama kiongozi wa familia naitumia hii
katiba na ninaweza kumshitaki yoyote atakyeingilia mambo yetu ya ndani....’akasema.
‘Kwahiyo itakuwa ni ajabu kama mtu atakuja na kuingilia
familia yangu,wakati yeye ana familia yake, .....’akasema na mwenyekiti akauliza
‘Hiyo Katiba yenu iliandikwa lini?’ akauliza
‘Muda mrefu sana, kipindi wakati tuna mtoto mmoja,
imeshafanya kazi zaidi ya miaka mitano,
kwahiyo sio kitu kigeni ndani ya familia yangu...’akasema
‘Naomba niione hiyo katiba..’akasema mwenyekiti, na mume
wangu akasimama huku akiwa kashika ile katiba na kwa madaha, akaelekea pale
alipokaa mwenyekiti kumkabidhi hiyo katiba, na wakati huo shemeji yangu alikuwa
bado kasimama, alikuwa hajafahamu kuwa akae au aondoke, na mimi nikamuonyeshea
ishara kuwa akae kwenye kiti. Na mwenyekiti akamuona , na haraka akasimama na
kusema;
‘Mimi sijakuruhusu ukae, mimi bado sijakukubalia na uwepo wako
kwenye hiki kikao, kama mwenyekiti siwezi kukaa kwenye kikao kinachovunja
sheria, nimeshasema huyu mtu anatafutwa na polisi, kuwepo kwake hapa ni
uvunjifu wa sheria....’akasema mwenyekiti na mimi nikasema;
‘Mwenyekiti nakuomba uniamini, huyu mtu ni mtu muhimu sana
kwenye kikao hiki, nakuomba umruhusu awepo, na kama ni uvunjifu wa sheria mimi
nitalijibu hilo, ...’nikasema.
‘Mimi nakubaliana na mwenyekiti, ndugu yangu atoke nje,
kwanini mke wangu unamkaidi mwenyekiti,
mimi kaka yake nipo , nitawakilisha mawazo yake, kwanini ung’an’ganie awepo apa,
au unataka polisi waje wamkamate...’akasema na kuongeza kusema;
‘Mke wangu umekuwa ukimuandama sana mdogo wangu, sijui kwanini,kama
kuna lolote dhidi yangu niambie mimi, na sio kumtumia mdogo wangu
kinyemela,mimi sipendi, kama kaka yake ninaamuru atoke kwenye hiki kikao, mimi
nitawakilisha mawazo yake kama kuna umuhimu huo, ni kwa usalama wake kwa sasa, mengine
aniachie mimi ...’akasema mume wangu.
‘Hata mimi sioni umuhimu wake hapa, maana anatafutwa na
polisi akionekana hapa itaonekana kuwa tunamficha sisi, au nimuite mkuu wa
upelelezi aje amchukue,...’baba akasema huku akinua simu yake kumpigia huyo
mkuu wa upelelezi
‘Baba tafadhali utaharibu kila kitu, nilishakuomba kuwa
unipe nafasi nifanye nionavyo mimi , kama utamuita huyo mkuu wa polisi
utaharibu kila kitu, naomba tafadhali endelea na kikao chako, muda utafika ,
utaona ni kwanini nimeamua awepo hapa kwenye kikao hiki...’nikasema,
Shemeji yangu alipoona malumbano dhidi yake yanapamba moto,
akaona aingilie mwenyewe, akasema;
‘Tafadhali mzee na
wajumbe wote wa kikao hiki,mimi naomba mnipe muda, niongee kilichonileta hapa,
na baadaye kama unaona nimevunja sheria, basi utampigia huyo mkuu wenu, ...huyo
mpelelezi, simu aje kunichukua, mimi siogopi kukamatwa kwa hivi sasa, ..kwa vile
nimeshathibitisha kile nilichokuwa nikikichunguza, kumgundua muuaji wa
Makabrasha,...
Mimi kuja kwangu hapa,ni kusema ukweli, na hasa ni kumtetea
kaka yangu, kwani kuna mipango ilipangwa dhidi yake, yeye hafahamu, kuwa kuna
watu walioshirikiana kumuua Makabrasha, na kwa vile wanataka wasikamatwe,
wameona kosa hilo wambambikie kaka, bila ya yeye kufahamu, ...’akasema na kaka
yake akabakia kuduwaa,
‘Mimi nina ushaidi kuwa kaka hajamuua Makabrasha, na wala
hajui ni kitu gani kilitokea siku ile, yeye kwanza alikuwa mgonjwa, na pili,
aliyemuua, alikuja bila ya yeye kufahamu akafanya hayo mauaji na kukimbia,
kaka, hamjui na hajui kwanini ilitokea hivyo..’akasema na kaka mtu akataka
kumzuia mdogo wake asiendelee kuongea.
‘Kaka nakuomba utulie , nataka kuongea haya kwa masilahi
yako, na masilhi ya wote waliohusika, kwasababu nimeona huk o tunapokwenda ni
kubaya, na hayo yaliyopangwa dhidi yako, yatakutia matatani, wewe hujui
tu...’akasema na kaka yake akamsogelea na kumshika mkono na kusema;
‘Mdogo wangu hayo sio ya kuongea hapa, tutakuja kuyaongea
tukiwa wawili, wewe toka nje ya kikao,...’akasema huku akimshika mdogo wake
mkono, ili watoke naye nje...mwenyekiti alipooa hivyo akasema;
‘Naomba mtulie mimi ndiye mwenyekiti wa kikao,
nimeshamfahamisha mkuu wa upelelezi, amesema tuendelee na kikao, lakini kikao
kikisha, huyu mtu tunatakiwa tumkabidhi kwake, kwahiyo kuanzia sasa upo
mikononi mwa polisi mimi siwezi kuvunja sheria kwa ajili ya kumfurahisha mtu
yoyote, hata akiwa mwanangu, hili nitalifanya,mimi nafuata sheria na taratibu
zilikubalika ....’akasema
‘Kwahiyo mimi sina haja ya kusema ukweli ambao nilitarajia
kuusema?’ akauliza shemeji yangu.
‘Ukitaka kuusema sawa, sasa hivi upo huru kusema, maana
wenyewe wameshatambua kuwa upo hapa, na ukweli gani ulio nao ambao ni tofauti
na ukweli ninaoufahamu mimi, hayo unayotaka kuyasema , na jinsi ulivyoelezea
hapo, ni mbinu tu ya kuficha ukweli, ni kumtetea kaka yako kiujanja unjana, na
mimi sikubaliani na hilo....maana ushahidi wote ninao hapa...’akasema baba.
‘Baba labda tufuate
utaratibu wa kikao chetu, wewe endelea na kikao, ukifika muda wake wa kuongea
ataongea, na ukweli utajionyesha, labda tuanze na ajenda zetu kama
zilivyojiapanga, kama tulivyoanza awali, tulikuwa tukiongelea kuhusu katiba,,...’nikasema.
‘Utaratibu kama huu siutaki, ..lakini sawa tuanze
kikao...’akasema mwenyekiti kwa hasira.
‘Ninataak niliweke hili wazi, siku nyingine mkiniita kwenye
vikao vyenu, kwanza mumechelewa kufika, mimi kama mwenyekiti natoa onyo,
sipendi tabia hiyo itokee tena, mkiniita kwenye kikao chenu mjipange vyema,
pili sitaki mambo kama haya ya watu kujitokeza katikati ya kikao bila mipangilio,
na tatu kikao kama hiki mkinichagua mimi kama mwenyekiti, sitaki mtu kujiona
yeye yupo juu yangu, mimi ndiye mwenye mamlaka ya kikao hiki, mambo ya familia
mnayaweka pembeni...’akasema.
Pili kuna mambo nataka kuyaweka wazi, ndio nimesikia kuwa
mna katiba mna utaratibu wenu wa kimaisha, mimi sikatai, na nimefurahi kama
mlifikia hatua hiyo,lakini ninataka niwarejeshe nyuma kidogo, niwakumbushe kwa
muhutasari....
‘Kikao hiki kimeitishwa na binti yangu, na baadhi yetu tumealikwa
kuna mambo anataka kutuambia ambayo sisi kama wanafamilia, tumekuwa tukiona kuwa
yanakwenda kinyume cha maadili, ambayo sio tu yanaharibu sifa za kifamiia,
lakini pia yanaharibu biashara na maendeleo yetu. ..’akasema.
‘Kwa kawaida mimi nimekuwa kiongozi wa familia kuu, ...ni
kiongozi wetu hadi hapo nikapokufa, japokuwa nikiona sina muda, ninaliachia
hilo jukumu kwenu, ...ndio ninakubali kuwa kuna familia ndogo ndogo, za watoto,
maana kila mmoja ana familia yake, ya mke na mume, na watoto, wao, lakini kuna
familia kuu, na tangu awali, kila aliyekuja kuoa kwangu, nimekuwa nikimwambia
hilo, na akakubaliana nami..’akasema na kumwangalia mume wangu.
‘Nilishasema kwenye familia yetu hatutaki mambo ay kashifa,
ikiwemo kuvunja sheria, na kuvunja sheria ni swala pana zaidi, ni pamoja na
uwongo, kusalitiana, na kugushi, na mambo kama hayo, ..mambo ambayo
yanatuharibia jina letu,achilia mbali kuua, ambalo ni kosa la jinai ....hilo
niliwakanya tangu mapema, na nilisema hata kama ni mtoto wangu kafanya hayo,
sitasita kumfikisha kunakostahili..
‘Mnafahamu madharaya yote hayo, binti yangu alifungwa, na
nilipoona kafungwa, sikukimbilia kumtoa, nilifanya utafiti kwanza kuhakikisha kuwa
kweli hana hatia, na kama ingeligundulikana kuwa ana kosa, ana hatia, kafanya
makosa, mimi nisingelihangaika, ..lakini nilipofuatilia, niliona kuwa hana
kosa,hana hatia, yote ni visingizio juu yake kwa masilahi ya watu wachache
...
'Hayo ni madhara ya kutukuaminiana, hakuna uaminifu kati yenu, kila mmoja ana lengo lake binafsi na kufikia hata kuvunja
sheria, hayo ni madhara, ya kutokuwa waadilifu, ...hilo nilishawakanya toka
mwanzoni, silitaki katika familia yangu, iwe iwavyo, kama umeungana na mimi
sitakubali, na kuungana na mimi ni kama umeoa kwangu, una hisa na kampuni zangu
nk...’akasema baba.
‘Kwenye familia yetu maovu yamegawanywa kwenye vipengele,
kuna maovu ya bahati mbaya, yanajulikana na unaweza kusema hilo ni kwa ajili ya
kuhangaika, inatokea kama biandamu ukateleza, lakini kuna maovu ambayo kabisa
unayaona kuwa huyu kakusudia, ...
‘Sasa basi sisi kama familia kuu, tumaliona hilo, kuwa kuna
mambo yametendeka kinyume na sheria, na ni kwa makusudi kabisa, sio kwa bahati
mbaya, sisi tulitaka tuchukua maamuzi yetu wenyewe, lakini tukaona ni vyema
wahusika wenyewe waseme, waeleze ilivyokuwa, na nyie kama kikao mtaona je hiyo
inastahili adhabu gani,..japokuwa adhabu sisi tunaifahamu, na adhabu ya familia
yetu haina msamaha,..maana ukisamehe makosa kama hayo, ya makusidi, yenye nia
mbaya ya kuliharibu jina la familia hii, wengine wataiga, wataona wakifanya
hayo watasamehewa, hilo halipo, kwasababu sio bahati mbaya....’akatulia.
‘Sasa basi nakukaribishwa mwenyeji, au mtu ambaye umetuita
kwenye hiki kikao uelezee, ni kwanini sisi kama wanafamilia kuu tusichukue
maamuzi, tuliyoona ni sahihi, kwa masilahi ya familia na vizazi vijavyo, kwani nyie wenyewe mumeshindwa kutimiza wajibu wenu
ndani ya familia zenu, sitaki kusema yapi ni yapi mumeyakiuka, lakini kwa
ujumla wake, mumetia doa familia yetu, haijawahi kutokea hivyo kabla, je ni
kwanini, na kuna nini...’akasema na kuniangalia mimi, kabla sijasema kitu, mume
wangu akasimama;
‘Mimi kama mume wa familia inayoshutumiwa kwa kukiuka hayo
aliyosema baba, nataka kuelezea ni kwanini hayo yalitokea, naomba niongee mimi
kwanza kabla hajaanza kuongea mke wangu japokuwa ni yeye aliyeitisha hiki
kikao,....’akasema na baba, akataka kumkatiza lakini mimi nikasema;
‘Baba, muache aongee tu, akimaliza nitaongea...’nikasema
‘Kikao ni lazima kiwe na mpangilio, sio kwamba mimi sifahamu
hilo, kuwa wewe ni mume wako familia, lakini kikao hiki sio wewe uliyekiitisha,
tumeitwa na mke wako, ...na kama nilitaka wewe uongee, ningelikupa hiyo nafasi,
sipendi kabisa huo utaratibu, heshima ni muhimu sana, lakini kwa vile mke wako
kakuruhusu haya ongea kama ulivyotaka wewe, maana kila hatua mnazidi
kunionyesha jinsi gani mlivyo....’akasema baba na mume wangu bila kujali
akasema;
‘Nakubali kuwa kuna udhaifu ulitokea, na hilo linaweza
kutokea kwa yoyote yule, hasa mnapokuwa katika harakati za kutafuta maisha,
kuna changamoto za hapa na pale,..huenda katika kuyafanikisha hayo tulijaribu
njia ambayo sio stahiki, ...ni katika kujaribu, ndio tukajikuta
tumeteleza,..naomba tusamehewe kwa hilo...’akasema.
‘Lakini, pamoja na hayo, mimi nimeshaitoa katiba yetu,
ambayo inalinda haki za familia yangu , na nimewekaw azi kuwa hiyo katiba
inatambulika kisheria, sio katiba ya kutunga, na kuishia mitaani, mimi
sijafanya kitu kinyume na katiba, na kama nilifanya, basi ujue nilifanya kwa
nia njema, na kama nilitelekeza, kama mume, nina haki zangu, kisheria...na
nilifanya mengine kwa minajili ya msilahi ya familia...’akatulia
‘Katiba niliyokupa ni halali, na nisingelipenda watu
waingilie familia yangu, nina mamlaka yangu kama kiongozi wa familia. Ni sawa
nilipoona kwako mzee, ulitoa masharti yako, ni sawa, kama mzazi nilitakiwa
kufanya hivyo,lakini ukumbuke kuwa sisi sio watoto tena, sisi tuna mamlaka
yetu, ..tuna utaratibu wetu, kama mtaona tumekwenda kombo, ni swala la
kutushauri, na sio kutuingilia kiasi cha kutoa hata adhabu,...katiba yetu ipo
wazi, inatulinda, inanilinda mimi kama mume wa familia, naomba hilo liwekwe
bayana...’akasema.
‘Umemaliza...?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio mwenyekiti, nilitaka kuweka hilo wazi, maana nimeona
ukitoa vitisho kwenye utangulizi wako..’akasema
‘Sio vitisho, hayo niliyoongea ni kweli na yatafanyika ,
kama ulikubali kuona kwangu, ujue una wajibu wa kuunza heshima yangu, sio
kwamba nakuingilia, ...na sina haja ya kukuingilia, ila kama umevuka mpakana
sitasita kukuwajibisha,...’akasema mwenyekiti.
‘Katiba ya familia yangu inanilinda...’akasema mume wangu,
na mwenyekiti akaichukau ile katiba na kuinua juu na kuuliza
‘Hii ndio Katiba inayosema inakulinda?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio ...’akasema mume wangu.
‘Katika katiba yenu halali, mlikubaliana kuwa kila
kilichonadikwa kitasimamiwa, kitatekelezwa, na sheria itafuata mkondo wake,
kama mmoja akikosea, kutokana na mlivyokubalia atawajibishwa kisheria, hata
kama ni kuvunjika kwa ndoa..., au sio?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio tumekuliana, na kila mmoja analifahamu hilo, ndio
maana tukaisajili hiyo katiba, na mimi nipo tayari kuwajibka kwayo, hiyo hapo
isome,utaona kila kitu kipo wazi, hakuna nilichokosea hapo, lakini unaposema
kuvunjika kwa ndoa una maana gani maana ukisome vyema utaona kuwa mimi ndiye
mwenye usemi wa mwisho kuhusu ndoa, siwezi kukubali ndoa yangu ivunjike...’akasema
‘Nauliza tena, upo
tayari kuwajibika kutokana na katiba yenu halali,ambayo inatambulikana na
msajili wa katiba, ?’ akauliza mwenyekiti
‘Ndio nimeshakuambia hilo, yote yapo wazi kwenye hiyo
katiba, sioni kwanini uniulize swali hilo, wakati katiba unayo hapo, na mimi
nimekubali na sahihi yangu ipo na ya mke wangu ipo?’ akauliza mume wangu.
‘Una uhakika kuwa hii ndio katiba halali mliyokubaliana wewe
na mke wako,...?’ akauliza mwenyekiti na nilimuona mdogo wake akiinamisha
kichwa chini, na kujishika na mikono yake miwili, kuonyesha kukata tamaa....
NB: Mambo yamenza, ushaidi wa kwanza wa uaminifu kwenye
ndoa, ....ni uaminifu...
WAZO LA LEO:
Heshima ndiyo inayolinda utu wa mwanadamu, bila heshima, kutakuwa hakuna
utaratibu wa kimaisha, heshima ni pamoja na kutii amri, taratibu na sheria,zilikubalika
na jamii husika, zenye maadili mema, na
hili huanzia nyumbani, kwenye familia zetu, mkubwa kwa mdogo kila mmoja anatakiwa
kutambua nafasi yake. Mke na mume , kila mmoja anatambua nafasi yake, kwe wema
na hekima tukilifahamu hili, amani na upendo utakuwepo tu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment