Nilifika sehemu ambayo huwa tunafanyia vikao vyetu, ni
kazini kwangu , lakini kuna sehemu maalumu imejengwa kwa ajili ya vikao, na
siku hiyo ilipangwa kabisa kuwa kutakuwepo na kikao changu na familia yangu, ndio
maana msaidizi wangu alikuja nyumbani kunikumbusha.
Nilipofika kwenye chumba cha mkutano nilimkuta baba
keshafika, kama kawaida yake, huwa ni mtu wa kujali muda, alikuwa tayari kakaa
kwenye kiti huku akifungua makabrasha yake, na lapotop yake ikiwa pembeni, na
wakati nafika, alikuwa akiongea na simu. Alionyesha kuwa kafika muda mrefu, na
aliponiona naingia akafunga makabrasha yake na kuhakikisha kayaweka vyema,
halafu akasimama kunisamilia, halafu akaangalia saa yake na kusema;
‘Nilitarajia watu watafika kwa muda, lakini naona dakika
tano zimepita, siwaoni watu, ..’akaanza kulalamika
‘Foleni na hulka zetu baba, lakini nina uhakika wote
watafika,....’nikasema
‘Sawa hebu kaa kwenye
kiti tuanze kuongea yetu, ya baba na binti yake, unaona hata mama yako hajafika, nay eye ni muhimu sana kwenye
kikao hiki, alisema anapita dukani kununulia vifaa vyake na binti yake...’akasema
‘Na binti yake, binti gani huyu?’ nikamuuliza.
‘Utamuona tu , na yeye atakuwepo kwenye kikao, ....’akasema
na sikutaka kumuuliza zaidi, maana inawezekana ndio mtindo wa wanaume kuwa na
watoto nje, lakini siwezi kuamini kuwa baba yangu ana mtoto nje, ni mtu
anayejali sana sheria, na itikadi na ni mcha mungu wa aina yake, yeye kila mara
anasema uongozi bora, kiongozi bora huanzia nyumbani kwake.
Nilipotulia kwenye kiti, aliniangalia kwa makini kama
anaitizama ndani ya ubongo wangu kuna nini, halafu akasema;
‘Nilitaka kufahamu maamuzi yako, nataka nijue ni nini
msimamo wako baada ya haya yote, nataka nikushauri kama baba yako, kama mzazi
wako, japokuwa mimi na mama yako tumeshaongea na kufikia uamuzi wetu, ambao sio
tofauti na ule wa mwanzoni,....’akasema
‘Baba maamuzi yangu yatatolewa mbele ya wahusika,
ninawahitajia wenyewe waje wathibitishe waliyoyafanya, nina kuwa kama watakuwa
wakweli wakajitakasa , yote yaliyotokea tutayamaliza kwa amani na saama,
vinginevyo, kama ndivyo walivyo, na watang’ang’ania kuwa waongo, ......basi
sheria itachukua mkono wake, mimi nina imani kuwa kwenye wengi hapataharibika
jambo,....’nikasema na baba akaniangalia kwa makini bila kusema neno kwa muda,
na nilipotaka kufungua mdomo wangu akasema;
‘Hayo unayozungumza kuwa kwenye wengi hapaharibi neno, ni
kama vile upo kwenye kikao cha wazee wenye busara na hekima zao, ambao wanaweza
kususluhisha mambo kihekima, lakini ukumbuke kuwa kikao hiki, ni cha sisi
wazazi wako, ambao ndio wazee, wengine ni mume wako, rafiki zako na wahusika wa
kazia nzima, ambao wengi wao ni wahasimu wako, wanaojali masilahi yao , unatarajia
wao watakushauri jambo jema?’ akaniuliza
‘Lakini nyie si mpo, nyie mnawakilisha wazee, mtaongea
mawazo yenu nitawasikiliza, na wahusika watawasikia, watajitetea, wewe ni
mwenyekiti wa kikao hiki, unatakiwa uwe kati na kati, usionyeshe upendeelo,
ukawakandamiza watu, tuwape nafasi wajitetea, huenda kuna ukosaji wa bahati
mbaya, huenda hata sisi tuna makosa....’nikasema nikitabasamu huku nikionyesha
adabu, maana mbele ya baba unatakiwa ujiheshimu kweli.
‘Huwezi kunifundisha nini cha kufanya, naifahamu sana kazi
hiyo kama mwenyekiti, nimeifanya kazi hiyo karibu nusu ya umri wangu, kwahiyo
hilo nalifahamu sana, ndio maana nataka nikuweke sawa, ili nisije nikajikuta
nakusuta mbele za watu, nisije nikawa naegemea upande wangu, na sitakubali
uniangushe....’akasema na kuinama kama vile ananikaribia, na isingeikuwa meza,
angefikisha kichwa chake karibu yangu, akasema;
‘Hebu niambie wewe ulishafikia wapi, maana uliniambia kuwa
unafanya uchunguzi, na utakuja kutoa maamuzi yako mbele ya kikao, ..nataka
kuona mtoto wangu anaongea kama mimi, au zaidi ya mimi, unanielewa, nataka
niione kazi yangu kwako, kama huwezi uniambie, nitajua ni nini cha kufanya...’akasema
‘Hivi baba hujaniamini, baada ya yote hayo niliyoyafanya,
baba mimi sio mtoto tena, ni mtu mzima nafahamu ni nini ninachokifanya,
nimeweza kuisimamia kampuni yangu bia kutetereka, na ikawa kubwa, kama
unavvyoiona, nimetulia kidogo baada ya matatizo na mume wangu, lakini kuna
msaidizi wangu ambaye anaifanya hiyo kazi vizuri tu, japokuwa sasa naona mume
wangu kaamua kuingilia kote, akini ni kwa muda tu, kwanza anaumwa hawezi
kupigika itakiwavyo, baada ya hiki kikao nitarejea tena kwenye ulingo wangu..’nikasema
‘Binti yangu, sio kwamba nakushusha chini katika utendaji
wako wa kazi, hapana, kiukweli unajitahidi sana, hata mimi najisifia mbele ya
wenzangu, lakini hili lililotokea, ....mmh, limekushusa, haya yaliyotokea kati yako
na mumeo wako, imeharibu kila kitu. Unafahamu kupanda juu, kunachukua muda,
akini kushuka, ni mara moja tu...’akarudisha kichwa na kuegemea kiti, haafu
akasema;
‘Mimi sitaki ushuke kihivyo, nataka uendelee kuwa juu, hilo
lililotokea, nataka lisafishwe, maana watu wameshakushusha sana, wewe huwezi
jua, kwani kuna usemi kuwa kama mzazi, kama baba na mama unashindwa kuihudumia
familia yako, ukashindwa kuiongoza basi hutaweza kabisa kuongoza jamii,
kuongoza kampuni,..na hili linaonekana wazi kwa jamii, sasa kama wewe na mume
wako mumeshindwa kukaa pamoja, na hili tulilijua ndio maana tukakushauri kuwa
huyo sio mume mwema....’akasema
‘Baba mimi sijashindwa kabisa kuiongoza familia yangu, na
unapozungumza hivyo, unasahahu kuwa mimi ni mke wa mtu, ambaye nina mipaka
yangu, ...lakini hata hivyo, sio kwamba nimeshindwa kuiongoza familia yangu
kama mke...nimejitahidi kufanya yale ya mpaka wangu, kwa kadri ya uwezo wangu,
yaliyotokea yamekuwa changamoto kwangu..na sizani kwamba nitafanya hayo makosa
tena,..kamwe, baba niamini, ....’nikasema
‘Kama unayosema ni kweli, kama ni hivyo, nataka nimuone binti
yangu, akionyesha ukomavu wake, nataak nijione mimi, japokuwa watu wanasema
nimezaa binti, akini nina imani kuwa wewe ni binti, lakini umewajihi umimi, kia
nikikuangalia usoni, najiona mimi, naomba, na sio naomba, nataka ufanye kweli,
nataka uwaonyeshe watu kuwa familia yetu haiyumbushwi na watu wasio jua
maadili,...’akasema
‘Baba usiseme hivyo, ukazizarau familia nyingine, ukachukua
azaifu wa mtu mmoja, ukauchanganya na familia zao, mimi nina uhakika kuwa tabia
kweli zinaweza kujengwa kutokana na familia husika, kurithiana nk, lakini
ukumbuke sasa jamii zimechanganyikana, tabia za kifamilia zinajichanganya na
kuleta tabia nyingine tofauti, mtu akishapevuka
akachanganyika na jamii nyingine, anajichuja, anakuwa na tabia yake nyingine,
kwahiyo baba ngoja tuone kama kwei kuna mabadiliko tutayachukuliwa kihekima
zaidi, kitaalamu zaidi, ...’nikasema
‘Binti yangu, Usije ukaharibu, maana mimi nilijua utafanya
maamuzi ya msingi kwa masilahi ya familia, lakini unavyoongea inaonyesha kuwa
upo tayari kukubali yote yaishe hivi hivi..mimi hilo sitakubali, kwasababu
tabia ya kizalia haina dawa, hayo waliyokufanyia ni mwanzo tu, ujue chini kwa
chini kuna dhambi za damu ya mtu, unafikiri hiyo damu itafukiwa kwa mchanga tu
hivi hivi, hata kama tutayamaliza kienyeji, lakini sio sahihi, kuna mtu
kauwawa, hakuna haki iliyotendeka, hata kama alikuwa na madhambi yake, watu
wanasema aheri kafa, lakini ni wapi sheria ilisema auiwe,hilo uliangalie kwa
makini..’akasema
‘Baba mimi naomba unipe nafasi hiyo, kama nitakuwa nimekosea
mtanisahihisha, lakini nina imani kila mmoja atajihukumu mwenyewe muda ukifika,
uwongo na hadaa una mwisho wake, ...wewe subiria, tu, tusichukue maamuzi kabla
wenyewe hawajajitetea tukaona ukweli upo wapi..’nikasema
‘Ukweli wote ninao hapa, unayaona hayo makabrasha , huo ndio
ukweli wa kila mtu, vijana wangu wamefanya uchunguzi wa kina, na mimi kutokana
na uzoefu wangu, nimeyakinisha kuwa ni kweli. Sio kwamba wameniletea hiyo
taarifa nikapokea kama ilivyo na kuikubali tu, la hasha, ....nilifuatilia kwa
namna yangu nikagundua kuwa ni kweli,.....’akasema na mimi nilipotaka kuongea
akanikatisha na kusema;
‘Na muda mfupi uliopita nilikuwa nawasiliana na mkuu wa
upelelezi wa kituo chenu, na yule aliyefuatilia kesi ya mauaji ya Makabrasha,
wameniambia mengi ambayo wameyagundua wao kama wao, japokuwa yana uwalakini,ukilinganisha
na uchunguzi wangu lakini ukweli upo pale pale, kuwa mume wako sio mwaminifu,
mume wako ana ajena za siri dhidi yako, na akilenga sana mali zako, hafanyi
hivyo kwa upendo kutoka moyoni, na hayo ukitaak nitakuonyesha,...mimi imeniuam
sana, lakini sio ajabu, kwani asili yao ninaifahamu fika...’akasema huku
akifungua makabrasha yake, lakini baadaye akayafunga na kusema;
‘Mume wako hajui , hakumbuki wapi alipotoka, yeye anafikiria
kuwa mali aliyo nayo, ilipatika kwa dhuluma, anashindwa kufahamu chimbuko za
hizo mali zimetoka wapi, sisi tulihangaika, tukifuata sheria, babu , baba,
walikwua wachakazi, na mimi nikarithi hivyo, na kiichotusaidia ni ukweli,
uwazi, sheria, na itikadi,...kwanini usifanikiwe, kama unajituma kwa uadiifu,
tatizo watu wanataka kupata kwa kupitia kwenye migongo ya wenzao, dhuluma,
ndiyo sera yao, unapata kutoka kwa mlalahoi, ambaye kula kwake ni kwa shida,
wewe unalimbikiza, unajiona ni mjanja, hatuendi namna hiyo...’akasema
‘Baba mimi nimekuelewa, ndio maana nataka mume wangu aje aongea
mwenyewe ukweli wake,muda ukifika,kama kweli ana itikado hiyo ya dhuluma, kama
kweli nia yake ni kuchuma kutoka kwenye migongo ya wenzake, tutamsikia, ...’nikasema
‘Hivi wewe unawafahamu hawo watu, aje aongee ukweli, ili
akafungwe, aongee ili akose kila kitu, ina maana gani kufanya mipango yote
hiyo, unafahamu mipango hiyo ilianzia wapi, ina maana walikuwa wakiigiza, ii
baadaye waseme mchezo umekwisha, sasa basi, ..nikuambia mwanangu watu kama hawo
hawakubali kirahisi...mwanangu binadamu sivyo walivyo, inapofikia kwenye
masilahi ukweli unasahaulika...’akasema baba.
‘Baba hayo tutayaona, akishindwa kusema ukweli, ushahidi
utaongea, ...wahusika wote watakuwepo, watasema na vielelezo tunavyo
vitaoonyesha kila kitu....’nikasema
‘Halafu unatarajia wao wakubali,...mwanangu, hatua iliyofikia
ni ya uamuzi,....kwasababu wao wanataka kuishi kwa dhuluma, basi, tuwaachie
waende wakaishi kwenye uwanja wao ambao sio hapa kwenye hii familia yetu,,
familia yetu sio sehemu yao,...unasikia, hayo ndio maisha yangu, ndivyo baba ,
babu na kizazi chetu kilivyoishi, haki na ukweli. Na ili kuhakikisha kuwa hayo yanafanyika,
inabidi wakati mwingine uchukue maamuzi magumu, hata kama ni ndugu yako kafanya
hivyo, anatengwa, anawajibishwa, bia hivyo hatutafika, ...’akasema
‘Nimekuelewa baba, nikuulize kitu, huyo mkuu wa upelelezi
kaamua kufanya nini, baada ya ugunduzi wao huo?’ nikamuuliza baba ii kupoteza
lengo, kwani sikutaka kutumia sera za baba, nilikuwa na njia zangu mwenyewe, na
baba akaniangalia akatabasamu, na kusema;
‘Nimemuaomba anipe muda, baada ya kikao hiki, nitajua ni
nini cha kufanya, na kwa vile bado sijafahamu uamuzi wako ni nini,
ningelishamuamuru afanye kazi yake, afuate sheria, awakamate wahusika, na
watajua wenyewe a kufanya, lakini kama ningeliachia iende hivyo, ina maana
inakugusa na wewe, na hatima yake ni nini, na sisi tutaingia, na hapo ni
kashifa inajijenga...’akasema.
‘Ni kweli baba ndio maana hata mimi nikalichukulia kisiasa
zaidi, kwasababu mume wangu yupo ndani ya familia, maamuzi yoyote tutakayotoa
yataweza kuathiri familia yangu, kuna watoto, ....unahisi watajisikiaje, na
huenda na nyie mkaingilia kati, kitu ambacho sikukitaka, nilitaka haya
niyatatue wmenyewe, lakini kila nilivyojitahidi, naona nyie mnaingilia kati,
ndio maana nikaona leo niwahusishe rasmi,...sasa kwangu mimi sitaki kusema lolote mpaka wote waseme ukweli
wao, ...’nikasema.
‘Niwajuavyo hawo watu, sizani kama ukwel utasemwa,...na hata
kama hautasemwa, mimi nimeshaufahamu ukweli wote na umauzi nimeshaupitisha....’akasema
baba na mara mlango ukagongwa, wajumbe wa kikao wakaanza kuingia:
***********
Mjumbe wa kwanza: alikuwa ni mama, akiwa kavalia kitaifa
zaidi, muda wote utamkuta hivyo, akiwa na nywele zake za asili, hajawahi
kuziweka dawa, ngozi ya asili hajawai kuichubua, san asana ni machoni kaweka
kanta, akatabasamu, kama kawaida yake, huwa hataki kukunja uso, yeye ana kauli
yake kuwa mwanamke hatakiwi kukunja uso, akikunja uso anaharibu ngozi ya sura
yake, mwanamke muda wote unatakiwa kutabsamu,kujenga uzuri wa uso, kama uwa
inavyojichanua ...
Kwanza alipoingia alisimama, nilijuwa kwanini kafanya hivyo,
mimi nikasimama na kumkimbilia, tukakumbatiana, na akanishikilia kwa muda, hadi
nikaona nijtoe maana ilizidi, baadaye mama akasema;
‘Mwanangu, pole sana na majanga, hiyo ndio mitihani ya ndoa,
tulijua, hayo yatatokea, wakati mwingine mnatuzarau sie wazee, mnatuona sisi
tumepitwa na wakati, na wakati wenu hamkanyiki, mnasema mna haki zenu, sasa
ndio hayo yanayowakuta, lakini sasa umejifunza, na umejionea mwenyewe,
...’akasema na mimi nikakaa kimiya, na mama akaendelea kusema;
‘Nimeona sehemu mbambali wazee wakishukiwa eti ni wachawi,
chuki za watu , matatizo yao binafsi yanaelekezwa kwa wazee, badaa ya kuangalia
kiini cha tatizo, ambacho ni hai ngumu, ambayo haisababishwi na wazee,...watu
wanafikia kuwasingiziwa wazee uchawi, hivi
watu kama hawo wanatarajia nini mbele ya mungu, tuchukulie kama sio kweli,
halafu wanakwenda kumuua huyo mzee, halafu mnatarajia neema katika hii dunia,hakuna
neema tena....ni laana tu’akasema
‘Mimi namshukuru mungu nimebahatika, kwetu tunajiweza,
nimeolewa kwenye familia inayojiweza yenye tabia sawa na familia yetu,...
sijaweza kuishi maisha ya shida,lakini wazee wengi wa kijijini, wamepitia
maisha ya shida, kula yao ya shida, mazingira wanayoishi ni ya shida,...ndio
maana ngozi, miili yao macho yao yanakuwa hivyo,nyie vijana mnasema hizo ni dalili
za mchawi, hebu elimikeni , mumuona adui yenu ni nani,..adui yenu ni
ujinga,kwanini watu hawalifahamu hilo ....’akasema mama.
Mimi ni kiongozi wa akina mama, na ni mmoja anayetetea haki
za akina mama na haki za wazee, kwahiyo akiongea hivyo sikuona ni ajabu,
anajisahau na kujiona yupo kwenye uwanja wake,..nikampa nafasi, aongee.
‘Mwanangu, wakati mwingine mtu unaogopa kuwa mzee, maana
uzee imekuwa ni balaa,uzee umekuwa ni mtihani, ukikaribia uzee, unaanza kuwaza,
huna mbele wala nyuma, matajiri wameshakunyonya vya kutosha, sasa wanakutupa,
ukafe, nyumbani watoto ndio hawo tena, walikuwa wakikuangalia, sasa wanakuona
ni mzigo,...majirani wanaanza kukuzushia majanga,.... wazee hawapendwi, angalia
nchi za wenzetu, wazee wanatunzwa, wanaheshimika, huku kwetu Afrika ni kinyume
chake,jamani tunataka nini katika hii dunia,...’akasema mama.
‘Mama lakini mimi sijawatupa wazazi wangu....’nikasema
‘Unaweza usitutupe kwa kauli lakini kwa matendo ukafanya
hivyo, kama hutusikii yale tunayokuambia ina maana gani, unatuzarau,unatuona
tumepitwa na wakati,...maana tunafahamu umechanganya damu na watu gani,
....ambao mwisho wa siku, watatuona hatuna maana,....sisi tunahangaika usiku na
mchana kuona unaishi kwa amani, upat familia bora yenye maadili mema, tunakushauri
yale tunayofahamu yatakusaidia katika maisha yako hutusikii, hiyo ni moja ya
sababu kuwa hatuna maana kwako, unatuona sisi ni kikwazo kwa mambo yako, lakini
sisi tuichokuwa tukikiangaia ni matunda yenu, kizazi chenu,kitakuwa vipi, sio
hapo tu, kwenye starehe zenu, upendo wenu, lakini ni nini matunda ya hayo yote....’akasema
mama, na baba katikisa kichwa kumkubalia mama yangu, nikajua wao walishajipanga
na ajenda yao, nikakaa kimiya.
Kwa ufahamu wangu, mama hajawahi kumpinga baba waziwazi, hilo
kama lilifanyika ni basi kalifanya kipindi nimeshaolewa, lakini nilipokuwa
mdogo, kama kuna jambo mama haliafiki, atatafauta njia ya kumuita baba pembeni,
wataongea mpaka wakubaliane, ...na wakianzisha mazungumzo hayo, wanaongea jambo
walilokubaliana. Kuna wakati nilikuwa najiuliza iweje baba na mama wawe na
kauli moja, ina maana wote wanafikiria jambo moja, kwakweli nilipenda sana
maisha yao, na nikatamani niwe kama wao, lakini naona hiyo kwa sasa
imeshindikana.
Watu wanasema mimi nimerithi sana tabia ya baba yangu, baba
pamoja na kuwa kila anachokiongea mama anakiunga mkono kama vile wamefikiria
pamoja, lakini kwa namna nyingine, baba alikuwa na mkali, na akitaka jambo lake
lifanyike, litafanyika, lakini sio kwa nia mbayam ni kwa ushawishi, wanaweza
wakakaa na mama, wakilijadili hadi wanafikia muafaka.
Tabia ambayo nimeijenga hadi leo ni tabia ya kukunja sura, baba
alipenda sana kukunja sura kama hakupenda jambo, na tabia hiyo ndiyo niliyo
nayo mimi, tofauti na mama, mama muda wote anatabasamu, kwake yeye anasema
tabasamu ni asili ya mwanamke, ukikunja uso unaharibu sura ya uso wako, na
unaulazimisha uzee kabla ya muda wako. Tabia hiyo ya kukunja sura, ilikuwa inamkera
sana mama, na alipenda kusema, kwanini nakunja uso kama mwanaume...kama baba
yako.
Nilimwangaia mama, mama haonyeshi kuzeeka sana, watu
wanasema sura yake haifanani kabisa na umri wake, ukimuona utafikiri ni
msichana, kinachomfanya aonekane ni mtu mzima ni uvaaji wake, anavaa nguo za
kiutu uzima, vitenge, na sana sana anapenda kuvaa mabera, na nguo pana
pana,....na kichwani huwezi kumuona kajiachia, yeye na kilemba, au kitambaa.
Tuliachaiana na mama,
huku akiendelea kuniangalia usoni, kama vile ananikagua kama nina kovu, au nin
tatizo lolote, akatikisa kichwa, kama kunisikitikia, na aliporizika akageuka,
kuangalia kule aliposimama baba, baba alikuwa keshasimama alipomuona mama
kaingia, ni tabia ya baba, kumuheshimu yoyote. Yeye kama kaja mtu,na aikuwa
kakaa, atasimama, bia kujali kuwa ni mdogo au mkubwa, atasimama, kabla
hajasalimiana naye.
Nilijaribu kuangalia nje, maana nilimuona mama wakati
anakuja alikuwa kaongozana na mtu, lakini wakati anaingia ukumbini, aliingia
peke yake, huyo aliyekuja naye, kamuacha nje,nikataka kumuuliza huyo aliyekuwa
naye ni nani, lakini nikaona nisubiri, huenda huyo aliyekuja naye ataingia
baadaye, nikamwangalia mama, ambaye kwa muda huo, alikuwa kamgeukia baba , baba
naye alikuwa akituangalia kwa makini, huku akijaribu kutabasamu na alipomuona
mama anamwangalia akasema;
‘Maisha jamani, sikujua kuwa itafika muda, utakaa mbali na
watoto wako, natamani sana siku zirudi nyuma, kipindi kile nipo pamoja na
familia nzima, upo karibu na watoto na mama yao kama hivyo...lakini ndio basi
tena, kila siku zinavyokwenda ndio unazidi kukimbiwa,...na naona kama ndio
safari ya kuwaacha ..’akasema baba akitusogelea, tukawa tumeshikana, na mara
mlango ukagongwa ,akaingia mjumbe mwingine.
************
Huyu alikuwa wakili wa familia ya baba, mimi niliamua kuwa
na wakili wangu, kwahiyo huyo wakii wao akawa anawashughulikia wazazi wangu, mimi
nilitafuta wakili wangu, amabye pia natarajia kuwa atafika, nikasalimiana na
wakili huyo baada ya kusaliamiana na wazazi wangu, alipomaliza kusalimiana na
mimi akasogea kukaa na baba wakawa wanaongea mambo yao, na mimi nikapata muda
wa kukaa pembeni na mama, tukawa tunaongea yetu.
‘Vipi wajukuu wangu wanaendeleaje?’ akaniuliza
‘Hawajambo, wanaendelea na masomo yao...’nikasema
‘Na nyie mnapenda kuwapeleka watoto shule wakiwa wadogo,
...mtoto akimaliza shule anakuwa hajapevuka kiutu uzima, wakati wetu ukimaliza
shule, unakuwa unajitambua, akili imeshapevuka, hata ikitokea bahati ukaolewa,
unafahamu majukumu yako ni nini....siku hizi wanamaliza shule wadogo, lakini
cha ajabu wanafahamu mambo makubwa kuliko umri wao, lakini zaidi ni yale mabaya...’akasema
huku akicheka.
‘Ndio maendeleo mama, ili tupate muda wa kusoma zaidi, ili
mtoto afike elimu ya juu, sio kuishia sekondari tu...’nikasema.
‘Ni kweli kama kweli watafanya hivyo, tatizo ni kuwa
wanajifunza mambo ya kuwaharbu, kuliko mambo ya kuwajenga, muda mwingi wapo
kwenye mitandao, na wanachoongea ni mambo yaliyo juu ya umri wao, na ni wepesi
kuhadaiwa, ninawasikitikia sana, kwa vile mambo ya mitandao kwetu hayana
vizuizi, wenzetu wameweka vizuizi, huwezi kuingia sehemu zote, wenztu huko
ukiingia kwenye aina fuani ya mitandao, unaulizwa umri wako, na kwa vile
wanavitambulisho, wana stakabadhi za kusafiria, ambazo zinathibitisha umri wao,
zinawasaidia..’akasema
‘Ni kweli,...huenda na sisi wakianzisha vitambulisho vya
taifa wakakuja kuvitumia kwa njia hizo, kuwa huwezi kuingia mitandao ya kikubwa,
kama umri hakuruhusu, ukitaka kuingia mpaka utaje namba ya kitambulisho
chako,.....’nikasema
‘Mhh, lakini kwa Wabongo, itawezekana hiyo kweli, tatizo
linaanzia kwenye hawo wanaodhibiti, watakaosimamia hayo mambo, uadilifu wao una
walakini,haya ikishafikia kwa watumiaji ooh,....wataiba hizo namba na kuzitumia
wapendavyo, labda kuwe na namna nyingine ya zaida....tuombe mungu maana kizazi
chenu kina changamoto sana, tena sana, elimu, imekuwa ghali,lakini sio elimu ya
kuelimika ni elimu ya kusoma tu, ili upate kazi ....na hata hivyo,bado vichwa vyenu
ni vigumu sana, kwa vile mambo yamekuwa mengi sana, .....haya niambie maisha
yako na mume wako yakoje, maana yanayotokea kwako yananitoa doa, umeniabisha
mwanangu?’ akaniuliza
‘Mama maisha yangu na mume wangu ni kama ulivyosikia, na
nimeona kikao hiki kiwe ni muhimu ya kuliongelea hilo,nawashukuru sana kwa
yote, na wakati mwingine najilaumu kuwa huenda ningelifuata maneno yenu haya
yaliyotokea yasingelitokea, lakini yote ni sehemu ya maisha, hayo yalitakiwa
yatokee ili iwe ni changamoto, kwangu mimi na kwa wengine, utajifunzaje bila
kupitia changamoto kama hizo....’nikasema.
‘Kwahiyo wewe uwe ni sehemu ya kujifunzia, upate shida,
uumie, ili wengine wajifunze, au wewe ujifunze, huoni kuwa nu kuumizana,
kupoteza muda, na ni hatari, ...watu wanauana, watu wanateseka, ndivyo
mnavyotaka hivyo....mimi hilo siliafiki,..kwasababu kulikuwa na njia ya
kuepukana nalo,ukakaidi umekuponza uking’ang’ania kitu mpaka ukipate, ndivyo
alivyo baba yako...’akasema.
‘Mama, usijali leo yote tutayaweka sawa, wewe subiria
tu,....’nikasema, na tuikatishwa, kwani mlango uligongwa.
Wakaanza kuingia wajumbe wengine, akaingia wakili wangu,
akafika rafiki ya mume wangu akiwa na mkewe, na baaaye akaingia mume wangu, alipofika
akajibaragua, kama ujuavyo, waliokuwepo wapo hapo ni wazazi wangu, ni wakwe
zake, kwahiyo alionyesha ile adabu ya ukwe...hata hivyo nilipomuangalai usoni,
nilimuona hana raha, japokuwa alijitahidi kujionyesha kuwa yupo sawa, na akaanza
kuwajibika kwani yeye ndiye mwenyeji wa kikao, japokuwa mimi ndiye
niliyekiitisha, baadaye ainisogelea na kuniambia;
‘Ni lazime niwajibike, japokuwa wewe ndiye umeitisha hiki
kikao, kama mume wako ninawajibika hivyo, unakumbuka kwenye mkataba wetu
unasemaje, mume anatakiwa kuwajibika kwa ajili ya familia, au sio?’ akawa
naniuliza, mimi nikatabsamu, na kusema;
‘Mkataba upi unaouzungumzia, wa zamani au mpya?’ nikamuuliza
huku nikitabasamu,hapo akasita na baadaye akasema;
‘Hakuna mkataba mpya na wa zamani, hiyo kauli unaiotoa...’akasema
na hapo nikajua hajafahamu kuwa nimeshaupata ule mkataba wenu wa asili.
‘Tutaona..muda ukifika hilo litasahihishwa, ...nenda
kafungue kikao,’nikasema nay eye bila kusita akaenda mbele na kusalimia watu
akafungua kikao, na kumkaribisha mwenyekiti wa kikao, ambaye ni baba, kikawaida
kwenye familia yetu, kukiwepo na kikao kama hicho mwenyekiti ni baba, japokuwa
mara kwa mara, anasema hilo jukumu sasa litakuwa ni letu.
Baba hakuenda mbele , alikaa pale pale, kwanza alianza
kufungua makabrsha yake, na kabla hajasema neno, mlango ukagongwa, na kwa vile wote
tulijua kuwa tumekamilika, hatukutarajia mtu mpya, kujitokeza tena, kwahiyo
hiyo hali ikatufanya, sote tugeuke na kuangalia mlangoni, kuona ni nani huyo
anayeingilia, na kikao hiki hakimuhusu, mlango ukafungulia, akaingia mtu akiwa amevalia
kofia la waendesha pikipiki, na alipoingia akalivua kofia lake....
NB: Haya mambo yanaendelea tuwe pamoja.
WAZO LA LEO: Nakumbuka
babu yangu alisema; ‘Uongozi ni wito, uongozi ni kubeba dhamana za watu, na
ukiwa kiongozi mwadilifu, watu wako ni
kwanza, na wewe unakuja baadaye, kwahiyo kimasilahi, utahakikisha kuwa watu
wako wametosheka kwanza, kabla ya kujali tumbo lako, huo ndio uongozi bora. Je
kiongozi kama huyo yupo katika hii dunia ya sasa,...Ndio maana tunasema Mandela
alikuwa kiongozi wa kweli, kwani yeye alijaribu kulifanya hilo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment